

Siku moja Hamisi na babake walienda sokoni kununua sare ya shule.

Hamisi akamwona kijana mwingine amevalia shati la kijani kibichi. 

"Anaonekana nadhifu sana," Hamisi aliwaza.

"Shati lile lapendeza sana," Hamisi alimwambia babake.

Hamisi aliendelea kusema, "Tafadhali baba, ninunulie shati la kijani kibichi kama hilo."

"Hamisi, leo nitaweza kununua sare ya shule pekee." Baba alisema.

"Sina pesa za ziada za kukununulia shati kama hilo." Baba akaeleza.

Baada ya kulipia sare, baba alitambua kuwa alikuwa na pesa zilizobaki. 

Angeweza kumnunulia Hamisi shati la kijani kibichi!

Hamisi alifurahi sana. 

Alikimbia kwenda kujichagulia shati la kijani kibichi.

------------------------------------------------------------



Kijiji changu kina mbuzi.

Kiko mbali na miji mikubwa.

Mama aliniambia, "Tunakupa zawadi unaposherehekea miaka sita ya kuzaliwa."

Mimi, mama na shangazi tulisubiri basi kufika.

Mama alinipakata miguuni.

Nililala wakati wote tuliosafiri.

Tulifika sokoni.

Niliiona helikopta maridadi ya bluu.

Kibanda kimoja kilikuwa na matunda.

Nilimwuliza mama, "Haya yanaitwaje?"

Mama alijibu, "Haya ni matofaa."

"Tafadhali, ninunulie moja," nilisema.

Niliusahau mkona wa mama.

Nilizingatia tu lile tofaa langu.

Nilipomaliza kula tofaa, nilijikuta nikiwa peke yangu.

Nilianza kulia.

Mwanamke mmoja alinichukua. 

Alinipeleka walikokuwa watoto wengine.

Niliwaza kuwa labda watoto waliuzwa sokoni.

Nililia zaidi.

Mwanamume aliuliza, "Elly yuko wapi?"

Nilijificha ili asinione.

Sauti ya mama niliyoijua, iliita, "Elly!"

Nilifurahi sana.

Shangazi yangu aliitoa helikopta maridadi.

"Ni yako!" alisema.

------------------------------------------------------------



Kuliishi msichana mdogo katika kijiji kimoja karibu na ziwa.

Aliitwa Atieno.

Babake Atieno alikuwa mvuvi mashuhuri. Alikuwa na mtumbwi wake wa kuvua samaki.

Atieno alifurahi kwenda kuvua samaki na babake.

Atieno aliwatazama wavulana wakicheza mpira wa miguu.

"Hebu nicheze nanyi," aliwashihi siku moja.

Wavulana wale walimcheka, "Nenda ukacheze kidalipo na wasichana wenzako."

Wasichana nao walimwambia Atieno, "Miguu yako ni mirefu mno." Atieno alihuzunika.

Atieno alianza kulichezea jua kila asubuhi.

Jua likawa rafiki yake.

Siku moja, jua halikuchomoza. Jogoo hawakuwika, ndege hawakuimba na watoto hawakwenda shuleni. Hata babake hakwenda kuvua samaki.

Atieno alihuzunika. "Wapi rafiki yangu jua? Kwa nini leo kuna giza?"

Atieno alienda kuwaambia watoto wengine namna alivyohuzunika. Lakini, walimcheka, "Labda jua limefariki. Au pengine limekutoroka."

Atieno aliwajibu, "Jua ni rafiki yangu. Haliwezi kufa."

Atieno alihuzunika sana hata akakimbia kwenda nyumbani. Aliugonga mpira wa kakake kwa makosa nao ulikigonga kibuyu cha mafuta.

Atieno aliwaza, "Nitaucheza mpira huu hadi rafiki yangu jua litakaporudi."

Aliuchukua mpira na kukimbia nao nje.

Atieno alipofika nje, aliuweka mpira chini akawaza, "Ninaweza kucheza kama wao wanavyocheza."

Aliugonga mpira kwa nguvu ukaruka juu angani.

Kila mmoja akitazama juu, mpira ulitokomea kwenye mawingu mazito.

Kulikuwa na kimya kikubwa.

Ghafla, mawingu yaliyokuwa mazito yalipungua na jua likatokezea. Kijiji hicho kikawa hai tena.

Kila mmoja akajitayarisha kufanya kazi aliyozoea kufanya.

Atieno hakuweza kuamini kwamba alikuwa amelirejesha jua kijijini. Lakini zaidi ya yote, jua lilikuwa limerudi maishani mwake.

Aliwaeleza watoto, "Jua ni rafiki yangu na limerudi."

------------------------------------------------------------



Siku moja, mvua kubwa ilikuwa imenyesha. Imani alitazama angani na kwa mara ya kwanza, aliona rangi.

Rangi zile zilipendeza sana. Alidhani kuwa mtu fulani alikuwa amefanya kazi kubwa ya kuipaka anga rangi kama vile babake alivyozipaka nyumba.

Alikimbia kumweleza dadake. "Sarah, tazama! Mtu fulani ametupakia anga rangi na kuirembesha."

Lakini Sarah alisema, "Usiwe mshenzi! Huo ni upinde. Wewe ni mdogo nami ni mkubwa. Ninajua kwa nini upinde uko angani. Hebu nikuonyeshe."

Alimpeleka Imani katika bustani ya wanyama akasema, "Upinde hautokezei kwa sababu simba wananguruma kwa mara ya kwanza. Wala hautokezei kwa sababu tembo wanazaliwa."

Sarah alimpeleka tena Imani kwenye bustani ya maua akasema, "Upinde hautokezei eti kwa sababu vipepeo wameipoteza rangi yao mawinguni."

Sarah alimwonyesha Imani kitabu akasema, "Vilevile, upinde hautokezei eti kwa sababu vifaru wanakimbia na kuzitisha rangi."

"Ninajua kwa nini pinde hutokezea. Mama alinieleza, nami sasa ninakueleza!" Sarah alimwelekeza Imani kwenye uwanja wa michezo.

"Pinde hutokezea angani kwa ajili ya watoto kama mimi na wewe. Siku moja, rangi zilitazama chini kutoka juu na zikafurahia kile zilizoweza kuona."

"Ziliwaona watoto wenye rangi ya maji ya kunde, rangi nyeusi na rangi iliyo katikati. Ziliwaza, 'Ni ajabu ilioje kupendeza kama watoto hawa wanavyopendeza.'"

"Rangi hizo zilikuja pamoja angani zikajadiliana ambavyo zingefanya. Ziliamua, 'Tutaweza tu kupendeza tukiwa kikundi.'"

"Sasa, huwa zinaungana pamoja na kung'ara namna zinavyoweza. Zina matumaini ya kupendeza kama watoto zinazoona, watoto kama mimi na wewe."

------------------------------------------------------------



Twafahamu kuwa Tembo ana mkonga mrefu.

Zamani, pua la Tembo lilikuwa fupi na nono. 

Pua hilo lilionekana kama kiatu kilichopachikwa katikati ya uso wake.

Siku moja, Tembo alizaa mtoto aliyekuwa mdadisi sana. 

Alimwuliza swali kila mnyama aliyemuona.

Mtoto wa Tembo alimdadisi Twiga, "Kwa nini shingo yako ni ndefu?"

Pia alimdadisi Kifaru, "Kwa nini pembe yako ina ncha iliyochongoka sana?"

Mtoto wa Tembo pia alimdadisi Kiboko, "Kwa nini una macho mekundu?"

Alipomwona Mamba, alimdadisi, "Wewe hula nini?"

Mamake alimwonya, "Mwanangu, usiwaulize wanyama maswali kama hayo?" 

Mtoto wa Tembo alinuna akaenda kucheza.

Kunguru mwerevu akamwambia Mtoto wa Tembo,  "Nifuate twende mtoni nikuonyeshe wanachokula mamba."

Mtoto wa Tembo akamfuata Kunguru hadi mtoni.

Alijipenyeza katikati ya mianzi kwenye ukingo wa mto. 

Akatazama majini kisha akauliza, "Mamba mwenyewe yuko wapi?"

Jiwe lililokuwa karibu na mto lilisema, "Hujambo?"  

"Sijambo. Unaweza kunieleza mamba hula nini jioni?" alijibu Mtoto wa Tembo.

Jiwe lilimjibu, "Hebu inama kidogo nikwambie wanachokula mamba." 

Mtoto wa Tembo aliinama chini karibu kabisa na lile jiwe.

Wakati huo huo pua la Mtoto wa Tembo lilikuwa kinywani mwa mamba. 

"Mamba ataila nyama yako leo," Kunguru mjanja akasema.

Mtoto wa Tembo akakita chini miguu yake yenye nguvu, akasimama imara akaanza kujivuta. 

Mamba hakuliachilia pua la Mtoto wa Tembo.

Pua la Mtoto wa Tembo likarefuka zaidi, kisha, puu! 

Mtoto wa Tembo akaanguka kichalichali.

Baada ya kukikosa chakula chake, mamba alizamia majini na kutokomea.

Mtoto wa Tembo alilitazama pua lake. 

Lilikuwa refu kama mkonga na hakuweza kuona lilipoishia.

Mkonga wake mrefu ulimwezesha kuchuma matunda yaliyokuwa kwenye matawi ya juu.

Pia, aliweza kuoga wakati wa joto kuutumia mkonga ule.

Hadi leo, tembo wote huwa na mikonga mirefu inayowafaidi.

------------------------------------------------------------



Sungura alikuwa amelala chini ya mti.

Tofaa likaanguka kutoka mti ule.

Sungura akasikia sauti ikisema, "Kimbia Sungura, kimbia!"

Sungura akasema, "Kitu kilianguka nikasikia, 'Kimbia Sungura kimbia!'"

Kuku alianza kukimbia aliposikia alivyosema Sungura.

Wakamwambia Mbwa, "Sungura alisikia kitu kikianguka naye akakimbia."

Mbwa akaanza kukimbia pamoja na Sungura na Kuku.

Mbwa akamwambia Farasi, "Sungura alisikia kitu kikianguka naye akakimbia."

Farasi akaanza kukimbia pamoja nao.

Punda akawauliza, "Mbona mnakimbia?" 

Farasi akamjibu, "Sijui."

Punda pia akaanza kukimbia pamoja nao.

Punda akamwambia Ng'ombe, "Sungura alisikia kitu kikianguka akakimbia."

Ng'ombe alikuwa na wasiwasi. 

Akaanza pia kukimbia pamoja nao.

Ng'ombe akamwambia Paka, "Sungura alisikia kitu kikianguka naye akakimbia."

Paka akaanza kukimbia na wanyama wengine.

Walimkuta mvulana akawauliza, "Kwani hamjui kilichotendeka?"

"Ni mimi niliyesema, "Kimbia Sungura kimbia!" 

Mvulana alicheka.

------------------------------------------------------------



Edi na marafiki zake wanapenda kuweka Lala Land safi.

Kila asubuhi huwa Monkey  anatandika kitanda.

Huwa Edi anakunja nguo na kuziweka kwenye kabati, ili azivae siku nyingine.

Baada ya kuoga, huwa Rabbit anapiga deki. Anapenda chumba cha kuogea kikauke vizuri.

Baada ya kucheza, Rabbit na marafiki zake wanavipanga vitu vya kuchezea na vitabu vyote.

Huwa Monkey akimwaga chakula anazoa moja kwa moja.

Tiger hachori au kuandika ukutani. Huwa anachora kwenye karatasi ili ukuta ubaki safi.

Huwa Rabbit anavua viatu akiingia ndani. Hapendi kuchafua nyumbani.

Edi na marafiki zake wanaweka takataka kwenye ndoo. Wanapenda kuweka mitaa safi.

Wao wanapenda kuviweka mtaa na bustani safi kwa kufagia majani.

Asante Monkey.
Asante Rabbit. 
Asante Tiger. 
Asante Edi. 
Ninyi nyote mnasaidia kuweka Lala Land safi.

Na wewe je? 
Unaweza kufanya nini kuweka nyumbani kwako safi?

------------------------------------------------------------



Wao wako shuleni. Wao ni nani?

Wao ni wanafunzi. Wanajifunza kusoma na kuandika.

Yeye yuko hospitalini. Yeye ni nani?

Yeye ni daktari. Anawasaidia wagonjwa.

Wao wamo jikoni. Wao ni nani?

Wao ni wapishi. Wapishi hupika.

Yuko shambani. Yeye ni nani?

Yeye ni mkulima. Anapanda vyakula.

Wao ni nani? Wamesimama pamoja.

Wao ni watu wa familia moja. Wanapendana.

------------------------------------------------------------



Tarik na familia yake waliishi mbali na mji mkuu.

Tarik alikuwa na mbwa aliyeitwa Buchi. 

Walikuwa marafiki wakubwa.

Siku moja, Tarik na rafiki yake Bedilu waliwapeleka mifugo malishoni.

Bedilu alipenda wacheze, lakini Tarik alitaka kusoma.

Mwishowe, Bedilu na Tarik waliamua kucheza.

Walipokuwa wakicheza, kondoo walitoweka.  

Waliwatafuta kila mahali.

Mbwa mwitu aliua kondoo wa Tarik. 

Tarik aliogopa kuadhibiwa na baba yake.

Tarik aliamua kulala juu ya mti. 

Buchi alilala karibu na mti huo.

Usiku, fisi walipiga kelele Tarik akaogopa.

Tarik alianguka kutoka mtini.  

Alisikia kelele karibu naye.

Wakati huo, radi ilimlika anga.

Tarik alimwona Buchi akiwa anamlinda!

Tarik na Buchi waliketi juu ya mti hadi asubuhi.

------------------------------------------------------------



Tulikuwa tukiishi na Bibi yangu na mama yangu.

Binamu zangu, Kristina, Tandi na Junior na Shangazi waliishi nasi.

Bibi yangu angetufundisha michezo.

Ulikuwa wakati mzuri sana.

Halafu Junior akaenda Malawi, naye Bibi pia akaenda Malawi.

Shangazi na Kristina pia wakaenda Malawi.

Halafu Tandi vilevile, akaenda Malawi.

Ilisikitisha kweli.

Hakuna aliyeishi nasi.

Lakini, si mbaya sana, kwa sababu mama yangu bado yuko hapa nami.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani katika kijiji cha Lunyiko, kuliishi mwanamme aliyeitwa Ndong'a.

Ndong'a na mkewe Namukaywa walikuwa na binti sita.

Namukaywa alipokuwa na mimba ya saba, Ndong'a alimwonya, "Ukimzaa msichana tena, nitakuua. Lakini ukinipa mtoto mvulana, nitakuandalia karamu kubwa!"

Wakati wa kujifungua ulipowadia, Namukaywa alienda kwa mkunga wa kienyeji. 

Je, mtoto atakuwa msichana au mvulana?

Walikuwa mapacha! Mvulana alimwita Mukhwana, na msichana akamwita Mulongo. 

Alimtazama Mukhwana kwa furaha. Alipomtazama Mulongo, alihuzunika mno. 

Ni jambo moja tu angelifanya.

Namukaywa alimwacha Mulongo chini ya ulezi wa mkunga.

 Akampeleka Mukhwana nyumbani kwa mumewe.

Kwa fahari, alimwonyesha Ndong'a mtoto mvulana. 

Alifurahi sana na kuwaita wanakijiji kusherehekea kuzaliwa kwa mtoto wake mvulana.

Mukhwana alikua na kuwa kijana mwanamume wa kupendeza. 

Na Mulongo naye, akawa mwanamke mrembo mno.

Siku moja wakati alikuwa akichunga mifugo wa babake, Mukhwana alimwona msichana mrembo sana. 

"Huyu ndiye msichana ningependa kuoa," alijiambia.

Lakini alipomwuliza kumuoa, aliimba hivi: 

Mukhwana wetu, Mukhwana 
Mama alionywa na baba
Akijifungua mvulana
Ampeleke nyumbani
Akiwa msichana, atauawa.

Hii ilifanyika tena na tena. Mukhwana hakujua la kufanya. 

Alimwendea mamake, Namukaywa, akasema, "Nimempata msichana mrembo ambaye ningependa kumuoa. Lakini kila ninapomwuliza,  anaimba wimbo ule ule."

La kushangaza, Namukaywa alisema, "Anachoimba msichana yule ni kweli. Yeye ni dadako. Mlizaliwa mapacha. Babako alimtaka mtoto mvulana na wala si msichana. Nilimwacha dadako kwa mkunga nikakuleta wewe nyumbani."

Wakati Mukhwana alimwambia babake kisa hicho,  babake aliona kwamba alikuwa amefanya kosa. 

Alimwita Namukaywa, na pamoja walienda kwa mkunga kumleta Mulongo.

Mulongo alipofika nyumbani, babake na wazee wa kijiji walimchinja mbuzi.

Walitekeleza kimila cha kumwunganisha Mulongo na ndugu zake saba.

Mwaka mmoja baadaye, Mulongo aliolewa kwa mwana wa tajiri kutoka kijijini. 

Aliiletea familia yake furaha na mali mengi.

Wote waliishi maisha ya furaha.

------------------------------------------------------------



Jina langu ni Ndalo.

Baba yangu anamfuga ng'ombe.

Anaitwa Pendo.

Pendo hupenda kula nyasi siku nzima.

Wakati mwingine baba humpa Pendo nafaka.

Pendo pia hunywa maji mengi.

Mimi ninampenda Pendo.

Baba humkama Pendo. 

Sisi humtunza Pendo naye hutusaidia.

Pendo hutupa maziwa mengi.

Mimi hunywa maziwa mengi.

Baba huuza maziwa.

Hutumia pesa hizo kuninunulia vitabu vya hadithi.

Mimi hupenda kusoma hadithi.

Umefahamu kwa nini ninampenda ng'ombe wetu Pendo?

------------------------------------------------------------



Mod alikuwa amechoka kuishi majini.

"Jihadhari. Ngozi yako itanyauka," Kasa alimwonya.

Lakini, Mod alitaka kujua. 

Aliruka akaenda zake.

Alitazama kila mahali.

Alikuta kinyonga wa kizambarau.

Alikuwa kando ya dimbwi la maji.

Kinyonga aligeuka rangi ya waridi! 

Mod aliruka mbali naye.

Alimwona fisi akikoka moto.

Moto ulienea karibu na Mod. 

Aliogopa.

Moto uliichoma ngozi yake. 

Aliruka ndani ya dimbwi la maji.

Lakini ngozi yake ilikuwa tayari na malengelenge.

Mod alipata ngozi kavu na mbaya. 

Alianza kuishi miambani.

Vyura wachache wana ngozi nyororo. 

Wanaishi majini.

------------------------------------------------------------



Sokwe alimkuta Mamba kando ya mto mkubwa.

Mamba akasema, "Nina maumivu. Tafadhali nisaidie."

Sokwe akamwuliza, "Unahitaji nini?"

Mamba akamjibu, "Usiponipatia moyo wako, sitapona."

Sokwe akasema, "Kwanza nibebe hadi upande wa pili wa mto."

Mamba akambeba Sokwe mgongoni wakavuka mto.

Sokwe akasema, "Ninahitaji kisu ili niukate moyo wangu."

Wakati huo huo, upepo mkali ukaanza kuvuma.

Mamba akainuliwa juu karibu amuangushe Sokwe.

Sokwe alipoiona nchi kavu, akamwambia Mamba aharakishe.

Ghafla, Sokwe akaurukia mti.

Mamba akakasirika akasema, "Ulinidanganya! Utajuta!"

------------------------------------------------------------



Sisanda ni msichana wa umri wa miaka minane. Kila siku anapotoka shule, anavua sare, anakula chakula cha mchana kisha yeye na babu yake wanacheza mchezo waupendao. 

Wanafurahia sana kucheza hadi Sisanda hataki kuacha. 

Babu anamkumbusha kuwa angependa kuwa meneja wa benki atakapokuwa mkubwa.

Babu anamwuliza kwa utani, "Utawezaje kuwa meneja wa benki usipokwenda shule ya upili?"

Sisanda anacheka tu. "Nitamaliza masomo ya shule ya upili na hata niende chuo kikuu. Hiyo ndiyo sababu ninatia bidii sana masomoni!"

Sisanda ni mrefu kwa umri wake. Anafuata  urefu wa babake. Anamfanana mamake kwa uso wake ulio mfiringo na kwa tabasamu yake. 

Kila siku wazazi wake huamka mapema na kwenda kwenye hifadhi ya wanyama iliyo karibu wanakofanya kaz. 

Wakati Sisanda na rafiki zake wanapoanza kwenda shule, mabasi huwa tayari yamewafikisha watalii kwenye hifadhi hiyo ya wanyama.

Maadhimisho ya kuzaliwa kwake iliyopita, Sisanda aliandaliwa sherehe maalum. Wazazi walipata ruhusa ya kuandaa sherehe hiyo katika hifadhi ya wanyama. 

Twiga walivutiwa sana na watu waliofika kwenye sherehe hiyo. Waliyanyoosha mashingo yao marefu wakaiona sherehe vizuri na kutaka kuptata sehemu ya keki! 

Sisanda aliwapenda twiga zaidi ya wanyama wote kwa ajili ya upole na utulivu wao. Angewatazama kwa siku nzima.

Ijumaa moja, babake Sisanda alikuja nyumbani mapema kutoka kazini. Alionekana kuwa mwenye hasira. Sisanda alimwuliza, "Baba, kuna nini kibaya?" 

Babake alieleza, "Leo, kundi la nyuki lilimuuma mama twiga. Kichwa chake kilivimba hadi macho yake ya kupendeza yakazibwa. Tulijaribu kumwokoa, lakini ilikuwa bure. Alikufa. Kinachohuzunisha zaidi ni kwamba alikuwa na ndama mchanga ambaye bado anamhitaji."

"Ah, la!" Sisanda alianza kulia. "Heri ningeweza kumsaidia. Labda yule ndama vilevile analia kama mimi." 

Sisanda alilia kwa muda mrefu. Mamake alijaribu kumfariji. Alimsomea hadithi moja zaidi wakati wa kulala ili aweze kusahau angalau kidogo uchungu aliokuwa nao kumhusu yule ndama. 

Hatimaye, Sisanda alipatwa na usingizi huku akisikiliza sauti ya mamake.

Asubuhi iliyofuata Sisanda alikuwa na wazo! Alimwuliza babake, "Ninaweza kwenda kufanya kazi nawe leo? Ningependa kumpelekea mtoto twiga zawadi." 

Wazazi wake walitazamana kisha wakatabasamu, "Ndiyo, bila shaka, unaweza kuja nasi."

Siku hiyo ilikuwa yenye joto na mawingu. Kila kitu katika hifadhi ya wanyama kilitulia. Sisanda alisema, "Nadhani hakuna jua leo kwa sababu ya huzuni wa mtoto twiga." 

Tembo mkubwa aliitazama familia hiyo ikipita. Mamake Sisanda alisema, "Labda anashangaa kwa nini msichana mdogo anaenda kufanya kazi na wazazi wake." 

Sisanda aliitkia kwa kichwa. "Atashangaa atakapogundua sababu hasa," Sisanda aliwaza.

Walimpata mtoto twiga akiwa peke yake. Alilegeza shingo lake refu na kuinama. Macho yake makubwa yalipumbaa. 

Sisanda aliufungua mkoba wake akatoa kitabu. Wazazi wake walishangaa alipoanza kumsomea mtoto twiga. Mtoto twiga aligeuza kichwa chake akatazama kulikotoka sauti ya Sisanda akasikiliza kama aliyelewa kila neno. 

Mwanzoni, wazazi walidhani kumsomea twiga ni jambo la ajabu, lakini walibadili mawazo yao walipomwona mtoto twiga akitulia.

"Hadithi yangu ilimfariji," Sisanda alimwambia babu yake alipofika nyumbani. Sisanda alienda kumtembelea mtoto twiga kila alasiri na wakati wa wikendi. 

Kila alipoenda, alibeba hadithi tofauti kumsomea. Marafiki hao wawili walionekana vizuri pamoja hata watalii waliopita waliwapiga picha.

Polepole, mtoto twiga alianza kupata nguvu. Watu waliofanya kazi katika hafidhi hiyo walimlinda vizuri. Upendo kutoka kwa rafiki yake Sisanda, ulifanya miujiza. 

Siku moja meneja wa hifadhi alimwuliza Sisanda ampatie rafiki yake mpya jina. "Furaha ni jina nzuri," Sisanda alisema.

Siku iliyofuata, meneja wa hifadhi alimpigia simu mwalimu wa Sisanda. Aliwaalika wanafunzi wa darasa la Sisanda kumtembelea Furaha. 

Mtoto twiga alikuwa amekua mrefu na mwenye nguvu katika muda wa miezi mitatu tangu Sisanda alipomtembelea mara ya kwanza.

Siku ya matembezi, wanafunzi 40 wa darasa la 3 walisubiri kwa hamu kufunguliwa kwa lango la hifadhi. 

Sisanda aliwaongoza wote wakaenda kumwona Furaha. Wengine walimtazama yule twiga mrefu kwa mshangao. Wengine walicheka kwa woga. 

Bi Keziah, mwalimu wao, alitabasamu tu.

"Sisanda, rafiki yako ni mrembo. Umemsaidia sana," mwalimu alisema. 

"Anaitwaje?" Mvulana mmoja aliuliza. 

"Anaitwa Furaha," Sisanda alimjibu. 

Bi Keziah alisema, "Bila shaka anafurahi."

Watoto waliketi chini wakamsikiliza Sisanda akisoma hadithi aliyomsomea Furaha siku aliyomtembelea mara ya kwanza. 

Meneja wa hifadhi alipiga picha. Baadhi ya watalii waliopita pia walipiga picha. 

Mpiga picha kutoka gazeti moja vilevile alipiga picha. Aliwaahidi kuwa picha yao ingechapishwa katika gazeti la mtaa wao hivi karibuni. Kila mmoja alishangilia.

Ilikuwa zawadi ya kipekee! 

Sisanda kusoma hadithi ili kumponya rafiki.

------------------------------------------------------------



Mimi ninapenda kucheza na rafiki yangu Chuma.

Mimi na Chuma tunapendana sana. 

Tukitumwa, tunaenda pamoja.

Siku moja nilitumwa na bibi dukani nikanunue chumvi na mafuta. 

Nilienda na Chuma.

Tukiwa njiani, tuliwaona watoto wenzetu wakicheza mpira wa miguu.

Mimi nilitamani sana kucheza mpira huo. 

Nilisema, "Ah! Mpira!"

Nilimwambia Chuma, "Twende tuwaombe kucheza nao mpira. Mimi hupenda mpira wa miguu."

Chuma alinijibu, "Twende kwanza dukani, halafu turudi kucheza."

Lakini, nilimwambia Chuma, "Tucheze kwanza wewe! Tukienda nyumbani bibi hataturuhusu."

Tulikubaliwa na wenzetu tukacheza mpira. 

Nilikuwa golikipa.

Nilijitahidi kudaka mpira. 

Wenzangu hawakuweza kufunga goli hata moja.

Uwanja tuliochezea ulikuwa na mchanga mwingi. 

Magoli yake yalikuwa mawe makubwa.

Baada ya mchezo, tuliondoka kwenda dukani, lakini, hatukuwa na pesa. Nilianza kulia. 

Chuma alinikemea, "Acha kulia. Ni wewe ulitaka tucheze kabla ya kwenda dukani."

Tulirudi nyumbani bila chumvi wala mafuta. 

Pia, tulikuwa tumechafuka kweli kweli.

Tulimkuta bibi amekasirika mno. 

Alituuliza, "Mmekuwa wapi muda huu wote?"

Alipogundua kuwa tulipoteza hela, alisema,  "Nawasamehe leo, lakini, msirudie tena kucheza bila ruhusa."

Tulipoona tumesamehewa, tulienda haraka kuwalisha kuku na bata. 

Baadaye, tulioga na kuwa wasafi.

------------------------------------------------------------



Tembo Mdogo alikuwa akitembea porini na mamake na dadake mkubwa. Walikuwa wakiimba kwa sauti na kurusha vumbi.

Kwa bahati mbaya, Tembo Mdogo akajikwaa kwenye jiwe na hakuweza kutembea tena. Alibaki nyuma.

Mama na dada waliendelea bila kujua kama Tembo Mdogo alikuwa amebaki nyuma.

Tembo Mdogo hakujua pa kuenda. Alianza kulia kwa uoga.

Kwa bahati nzuri Panda alikuwa ndani ya majani karibu na mahali ambako Tembo Mdogo alikuwa ameketi chini.

Panda alimsongea akamwambia, "Nifuate. Mahali hapa kuna wanyama wengine ambao wanaweza kukuumiza."  

Tembo Mdogo hakusita kukubali kwa sababu hakuwa na mahali pengine pa kuenda. Vilevile kijiji chake kilikuwa mbali.

Walipofika katika kijiji cha Panda, kila mnyama alionyesha uso tofauti. Baadhi ya wanyama walimpenda Tembo Mdogo.  Wengine walikasirika na wengine wakaogopa. Hawakujua jinsi mfalme wao Simba angeamua.

Kwa kweli Simba hakukubali Tembo Mdogo abaki katika Kijiji kile. Alisema, "Atakayepinga uamuzi wangu, atafukuzwa pomoja na Tembo Mdogo. Ufalme wangu si wa watu wa nje ila ni wa vizazi vya hapa.

Simba alimwambia Tembo Mdogo, "Nenda mbali au niivunje mifupa yako mara mia."

Tembo Mdogo alishtuka akakosa la kusema. Akaamua kuenda. Lakini, rafiki yake Panda akaona hawezi kumuacha aende peke yake.

Kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwa Tembo Mdogo, Panda aliacha kila kitu na kumrudisha nyumbani.

Tembo Mdogo alifurahi sana hata akambeba mgongoni.

------------------------------------------------------------



Graca alizaliwa Msumbiji. Nchi yake ilikuwa maskini sana na hawakuwa wamepata uhuru. 

Watoto hawakuwa na shule nzuri za kwenda. 

Mamake alikuwa na ndoto ya kuwapa wanawe maisha mazuri. Bila masomo haingewezekana.

Mtoto Graca angekuwa mzaliwa wa sita. Licha ya furaha hii yote kulikuwa na huzuni kwani babake Graca alikuwa karibu kufa. 

Aliota kuwa mtoto wake mdogo angeenda shule nzuri. Alijua elimu ndiyo ingemsaidia mwanawe. 

Jamii yake iliapa kutimiza ndoto yake.

Wiki chache baada ya kifo cha babake, mtoto alipewa jina kuambatana na urembo wake. Aliitwa Graca. 

Kadri miaka ilipozidi kuyoyoma ndivyo Graca alizidi kuleta furaha kwao. 

Familia iliamua kumpa Graca masomo mazuri.

Graca alitia bidii sana shuleni. Alipata tuzo ambalo lilibadilisha maisha yake. Alipata ufadhili wa kumwezesha kusomea shule nzuri kijijni. 

Ndoto yake ilikuwa awe mwalimu. Alitamani watoto wa Msumbiji wajue kusoma na kuandika. Alitamani wakati ambapo watoto wote wangeenda shuleni.

Graca alitia bidii yake yote kwenye masomo. Baadaye kidogo alipata tuzo nyingine la kuhudhuria chuo kikuu huko Ureno. 

Alipata marafiki wengi, akajifunza lugha nyingi geni na akasoma vitabu vingi vipya. Akaona ndoto yake ya kuwa mwalimu ikitimia. 

Hii ilimpa furaha kubwa lakini bado alikuwa na huzuni.

Watu kule nyumbani kwao, hawakuwa na uhuru. 

Lakini sasa Graca alikuwa na elimu, ujuzi na matumaini. Pia, alikuwa na marafiki ambao walikuwa na mawazo kama yake kuhusu haki ya watoto kupata elimu. 

Alitaka kutumia ujuzi wake na marafiki zake kuleta mabadiliko kwao Msumbiji.

Kupitia usaidizi wa marafiki zake, hatimaye Msumbiji ilikuwa huru!

Rais aliyechaguliwa kuiongoza nchi ya Msumbiji alikuwa rafiki yake Samora. 

Walipendana na wakaona.

Graca alipewa kazi ya kuhakikisha kuwa watoto wote wamepata elimu nzuri. 

Ilikuwa kazi ngumu kwani watoto wengi wa nchini Msumbiji hawakujua kusoma na kuandika. 

Alianza kwa kuwapeleka watoto wote shuleni.

Graca na Samora walijaliwa kupata watoto wawili. 

Walikuwa na ndoto ya kuwapa watoto wao na watu wa Msumbiji maisha mazuri. 

Kwa bahati mbaya, Samora alikufa kwenye ajali ya ndege.

Graca aliomboleza kifo cha Samora kwa miaka mingi. 

Baadaye Graca alipendana na Nelson Mandela. Walifunga ndoa, wakafanya kazi pamoja kuwasaidia watoto wa Afrika.



------------------------------------------------------------



Hebu nikueleze kuhusu mtende.

Mtende ni mmea wa kudumu. 

Unasitawi mimea mingine inapokauka.

Kivuli cha mtende kina upepo mzuri.

Tunakula matunda ya mtende.

Tunatumia majani yake kuezeka nyumba zetu.

Tunatengeneza fagio kutumia majani ya mtende.

 Tunasuka mikeka pia.

Tunatumia nafaka zake kupika.

Sasa umefahamu kwa nini mtende ni muhimu sana?

------------------------------------------------------------



Paka na Panya waliishi katika kisiwa kimoja. Walipendana sana. Paka alichoka kuishi kisiwani na kumwambia Panya kuwa angetaka kuenda ng'ambo. 

Panya alifurahishwa na wazo hilo akaamua kumfuata. Papo hapo wakaamua kutengeneza mtumbwi.

Wakachukua gogo kubwa na kuchimba ndani. 

Gogo likawa kama mashua kisha wakalitia majini likaelea.

Siku iliyofuata, walianza safari yao asubuhi na mapema. Waliabiri kwenye gogo walilotengeza. 

Ilipofika jioni, Paka alihisi njaa na kumwambia Panya kuwa atamla. 

"Tazama nilivyokonda. Hutashiba ukinila," Panya akasema.

Panya alianza kutafuna gogo lao walilokuwa wakisafiria. 

Paka alipoamka alishangaa kumuona Panya akila. Paka akamwuliza, "Unakula nini?"

Panya akamjibu rafikiye Paka, "Tutakufa njaa. Tule mashua yetu!" 

Paka alijaribu kula gogo lakini hakupenda ladha yake. 

Panya aliendelea kulila gogo mpaka mtubwi wao ukatoboka.

Wakaanza kuzama. Panya aliruka majini akaogelea vizuri lakini Paka alipata shida kubwa majini. 

Baada ya Panya kumsaidia, alitoka salama salimini na kwa bahati, wakafika ng'ambo.

Paka alikuwa na njaa sana. Akamwambia Panya, "Sasa nitakukula maana umenona sana. Sikuachi!"

Panya alishangaa kwa muda kisha akasema, "Sawa, nimekubali utanila lakini nina matope mikononi. Subiri ninawe kwanza."

Panya aliingia kwenye shimo chini ya mti. Paka alimngoja nje lakini Panya hakutokea tena. 

Hadi leo, Paka anapoliona shimo popote, hungojea pale ili amle Panya.

------------------------------------------------------------



Katika mtaa wa Mfalele, kulikuwa na mvulana aliyeitwa Bobo. Aliishi na wazazi wake.

Bobo aliwaheshimu wazazi wake na watu wote mtaani kwao.

Jumatatu ni siku inayokuwa na shughuli nyingi pale mtaani. Watoto hujitayarisha kurudi shuleni baada ya wikendi. 

Siku moja Bobo alipokuwa njiani kwenda shule, alikutana na rafikiye, Jeuri.

Jeuri alipenda kupigana na kuwachokoza wengine. Mara nyingi alikosa kuhudhuria shule. Alikuwa mvulana mtundu aliyecheza Kamari na kuandamana na watu wengine waovu. 

Jeuri alimshawishi Bobo. Bobo hakupenda kuachwa na wavulana wengine. Polepole, alianza kuwa na tabia mbaya kama Jeuri.

Bobo alianza kuwachokoza watu. Pia, hakuwaheshimu wazazi wake na watu wengine. 

Alianza kulewa akashindwa kujitunza.

Bobo hakuyajali maisha yake. Aliambukizwa ugonjwa wa zinaa. Alipoanza kukonda, Jeuri alimfanya mzaha na kuukatiza urafiki wao. 

Wazazi wa Bobo walimhimiza aitembelea kliniki iliyokuwa karibu apate matibabu. Alitibiwa na akapata nafuu.

Bobo alitafakari juu ya maisha yake akaamua kubadilika. Aligundua kwamba alikuwa amefanya urafiki na adui. 

Alianza kutia bidii masomoni na kuwaomba msamaha wazazi wake na walimu.

Mwanzoni, Jeuri alikasirika alipomwana Bobo akibadilika na kuwa mwema. 

Baadaye, alianza kujutia tabia zake mbaya.

------------------------------------------------------------



Katiti alipenda kuuliza maswali. Aliyapata mazoea haya kutoka kwa wazazi wake. 

Waliokuwa wakimwambia, "Usipouliza maswali ukiwa mdogo, utakapokua mtu mzima, utakuwa mjinga!"

Siku moja, Katiti alimwuliza mwalimu wake, "Kwa nini wazazi wetu wanatueleza kila wakati tuwe tukinawa mikono yetu kabla ya kula, hata kama mikono yetu huonekana kuwa misafi?" 

Wenzake darasani walilipenda swali lake. Wao pia hawakupenda kuambiwa kunawa mikono yao.

Mwalimu alijibu, "Hilo ni swali nzuri, Katiti. Mikono yetu hata inapoonekana kuwa misafi, inaweza kuwa na viini." 

Mwalimu aliwaeleza wote, "Viini husababisha maradhi. Hatuwezi kuviona viini hivyo kwa macho yetu. Tunahitaji kifaa kilicho na nguvu zaidi ili tuvione."

Mwalimu aliichukua darubini kutoka kabatini. "Darubini ni kifaa tunachotumia kuviona vitu vilivyo vidogo sana ambavyo hatuwezi kuviona kwa macho yetu," alisema. 

Kwa utaratibu, mwalimu aliifuta mikono ya Kariza kwa kijiti. Halafu, akakifutia kile kijiti kwenye kioo cha darubini.

Mwalimu alikiweka kile kioo juu ya darubini. 

Hiki ndicho walichoona walipotazama. Hata kama mikono ya Katiti haikuonekana kuwa michafu, ilikuwa na viini chungu nzima juu yake.

"Kuna viini kila mahali. Vinapatikana kwenye vitu tunavyogusa, darasani kwetu, uwanjani na hata nyumbani. Viini hivi vinaweza kutufanya tuwe wagonjwa," mwalimu aliwaonya.

Mwalimu aliendelea, "Ili kuviangamiza viini hivi, lazima tuioshe mikono yetu kwa maji safi na sabuni, hasa kabla ya kula. Pia, tunapokuwa wagonjwa, lazima tuioshe ili tusivieneze viini."

Katiti alipofika nyumbani, alimkuta babake akiwa anatengeneza kiti cha aina ya pekee. 

Akamwuliza, "Baba, unatengeneza nini?" Babake alimjibu, "Hiki kinaitwa 'chukua hatua unawe'. Unakitumia kunawa mikono yako baada ya kukitumia choo na kabla ya kula."

Katiti alishangaa akasema, "Ndiyo! Mwalimu wetu ametuambia kuhusu kifaa hiki, lakini wengi wetu hatujui jinsi ya kukitumia. Kinatumikaje?" 

Babake alicheka halafu akamwambia, "Hebu njoo binti yangu nikuonyesha."

"Kwanza kabisa, kikanyage kipande hiki cha mti kilichoko sakafuni," baba akasema.

"Unapofanya hivyo, mtungi wa maji utainama na kuyamwaga maji mikononi kwako. Kumbuka kuitumia sabuni kunawa," baba akamwambia Katiti.

Katiti alifurahi akasema, "Ningejuaje jambo hili nisingeuliza maswali? Ni kweli kwamba maswali humwelekeza mtu kupata maarifa."

------------------------------------------------------------



Zamani, wanyama waliishi pamoja.

Walikutana kumchagua mfalme.

Jimbi alitaka kuwa mfalme.

Alidanganya kuwa alikuwa na moto kichwani.

Wanyama wengine walimwamini Jimbi.

Walimchagua kuwa mfalme.

Msimu wa mvua ulifika.

Kila kitu kilikuwa maji na baridi.

Sungura aliuliza, "Tutaupata moto wapi tujipashe joto?"

Kima alisema, "Tutaupata kwenye kichwa cha Jimbi."

Wanyama walimtuma Mbwa Mwitu kuleta moto kutoka kwa mfalme wao.

Mbwa Mwitu alienda kuuchukua moto bila kumuamsha Jimbi.

Mbwa Mwitu aliweka nyasi kavu kichwani.

Hazikushika moto.

"Mwamshe mfalme Jimbi! Tunahitaji moto sasa," Mbwa Mwitu alisema.

Jimbi hakuwa na moto wa kumpatia Mbwa Mwitu.

Kutoka siku hiyo, mbwa mwitu hula jimbi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, paliishi mzee aliyeitwa Lodipo. 

Aliishi na wakeze wawili, Akila na Akitela.

Mamake Lodipo alikuwa kipofu. 

Akitela pekee ndiye aliyekuwa akimsadia.

Siku moja, Akila alimwambia Lodipo, "Tuondoke kijijini humu twende kuliko na amani." 

Kijijini mwao kulikuwa na uvamizi wa mara kwa mara.

Lodipo akamwambia Akila kuwa hawangeweza kumuacha mama yake pekee. Akila alisisitiza waondoke na wamuache ajuza huyo. 

"Kama wewe hutaki kuondoka hapa, mimi nitarudi kwa wazazi wangu," Akila alimfokea Lodipo.

Lodipo alimpenda sana Akila. Hivyo, alikubaliana naye na kupanga watakavyotoroka. 

Akitela alishangazwa na haya yote.

Siku moja, mamake Lodipo alikuwa ameketi chini ya mti. Hakufahamu kilichokuwa kikiendelea. 

Huku akimwangalia na kumhurumia, Akitela alitafakari, "Itakuwaje tukimwacha peke yake?"

Lodipo na wakeze wawili walipakia mizigo yao kwenye ngamia wao wawili. Wakaondoka kimya kimya bila kumuaga yule ajuza. 

Akitela alikuwa akilia kwa huzuni ya kumuacha mama mkwe. Aliwaza, "Nitajificha nirudi kuwa naye."

Ajuza huyo alipoachwa peke yake nyumbani, alilia na kuimba wimbo huku akimtaja Lodipo.

Punde, Lodipo na wakeze wawili walipoondoka, wezi wa mifugo walivamia kijiji.

Wezi hao walimwambia ajuza awaeleze alikokwenda mwanawe. 

Majambazi hao walimwambia kuwa wangemtafuta Lodipo wamuadhibu. 

Ajuza aliwaomba majambazi wasimdhuru Akitela.

Pia aliwaambia wamrudishie kondoo dume aliyekuwa amechukuliwa na Lodipo.

Majambazi walimtafuta Lodipo na kumpata katika kijiji kipya. 

Walimshambulia Lodipo na Akila, mkewe wa pili.

Akitela alirudi kijijini pamoja na yule kondoo dume wakaishi kwa furaha.

------------------------------------------------------------



Hadithi hii inanihusu mimi na Makao ya Watu Wazee.

Makao hayo ni jumba kubwa lililoko mtaani Bertrams, Johannesburg.

Nyuta zake ni za rangi rangi. Ni jumba safi lakini ndani kuna kimya. Watu wanaoishi humo ni wakongwe mno.

Siku moja mamangu alitutembeza huko.

Makao haya ya Watu Wazee ni pahali pangu pa furaha!

Ninafurahi niwaonapo watu wazee na kuweza kuwasaidia.

Siku moja nilitembelea pahali hapo na kuziosha nywele za baadhi ya wale wazee.

Pia, niliwaandalia chakula.

Baadhi ya wazee wale waliogofya, hata hivyo, nilifurahia kuwa pale.

Kulikuwa na bi kizee mmoja ambaye hakutaka kusaidiwa na yeyote. 

Alianza kupiga mayowe.

Vilevile, kulikuwa na bi kizee mwingine aliyenikatalia nilipomshika. Mikono yake ilikuwa laini na joto.

Aliitwa Aisha, kama dadangu.

Watu wazee hunifurahisha. 

Wana hadithi za kale ambazo sitawahi kujua.

------------------------------------------------------------



Kuku na Jongoo walikuwa marafiki.

Walienda kucheza mpira wa miguu.

Kuku alikuwa golikipa.

Jongoo alilifunga bao.

Kuku alikasirika sana.

Kuku aliamua kummeza Jongoo.

Kuku alipoondoka uwanjani, alikutana na Mama ya Jongoo.

Jongoo aliyemezwa alilia, "Mama nisaidie. Nimemezwa."

Jongoo alikuwa na ladha mbaya sana. Kuku alihisi kichefuchefu.

Kuku alikohoa na kumtema Jongoo.

Jongoo alipotemwa, alitoroka na kwenda zake.

Kuku na Jongoo walikuwa maadui tangu siku hiyo.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, wasichana watatu walienda kutafuta kuni.

Ilikuwa siku yenye joto kwa hivyo walienda mtoni kuogelea. 

Walicheza wakirushiania maji na kuogelea.

Ghafla, waligundua kuwa saa zilikuwa zimeenda. 

Walifanya haraka kurudi kijijini.

Walipokuwa karibu nyumbani, Nozibele aliweka mkono wake shingoni. 

Alikuwa amesahau mkufu wake! "Tafadhali rudini nami!" aliwasihi marafiki zake.

Lakini, marafiki zake walisema kwamba saa zilikuwa zimeenda sana.

Kwa hivyo Nozibele alirudi mtoni peke yake.  Aliupata mkufu wake na kuanza kurudi nyumbani kwa haraka. 

Kwa bahati mbaya, alipotea gizani.

Kwa umbali aliona mwangaza ukitokezea chumbani. 

Alikikaribia chumba hicho na kubisha hodi mlangoni.

Alishangaa mbwa alipoufungua mlango na kumwuliza, "Unataka nini?" 

"Nimepotea, nahitaji mahali pa kulala," Nozibele alisema. 

"Ingia ndani, au nikuume!" mbwa akajibu. Nozibele aliingia.

Kisha mbwa akasema, "Nipikie chakula!" 

"Lakini sijawahi kumpikia mbwa chakula," Nozibele aljibu. 

"Pika, au nikuume!" mbwa akasema. Nozibele alimpikia mbwa chakula.

Tena mbwa akasema, "Nitayarishie kitanda." 

Nozibele akajibu, "Sijawahi kumtayarishia mbwa kitanda." 

"Tayarisha au nikuume!" mbwa alisema. Nozibele alitayarisha kitanda.

Alitakiwa kumpikia, kumfagilia na kumwoshea mbwa kila siku. 

Siku moja mbwa alisema, "Nozibele, nimelazimika kuwatembelea marafiki zangu. Fagia nyumba, pika chakula na uoshe vitu vyangu kabla sijarudi."

Mbwa alipoenda tu, Nozibele alichukua nywele tatu kutoka kichwani kwake. 

Aliweka mmoja mvunguni mwa kitanda, mwingine nyuma ya mlango, na mwingine kwenye zizi la ng'ombe. 

Kisha alikimbia kwenda nyumbani haraka alivyoweza.

Mbwa aliporudi, alimwita Nozibele kwa sauti, "Uko wapi?" 

"Niko mvunguni mwa kitanda," unywele wa kwanza ulisema. 

"Niko nyuma ya mlango," unywele wa pili ukasema. 

"Niko kwenye zizi la ng'ombe," ukasema unywele wa tatu.

Papo hapo mbwa alifahamu kuwa Nozibele alikuwa amemdanganya. Kwa hivyo, alikimbia moja kwa moja hadi kijijini. 

Lakini, ndugu zake Nozibele walikuwa wamemsubiri kwa fimbo kubwa. 

Mbwa aligeuka na kukimbia na hadi leo, hajawahi kuonekana tena.

------------------------------------------------------------



Miaka mingi iliyopita, Jua na Maji walikuwa marafiki. 

Wote waliishi duniani.

Jua alipenda kumtembelea Maji mara kwa mara. 

Lakini, Maji hakuwahi kwenda kumtembelea Jua.

Mwishowe, Jua alimwuliza Maji kwa nini hakuenda kumtembelea. 

Maji alijibu kwamba Jua ana nyumba ndogo sana. Alisema, "Nikija na familia yangu, tutakutupa nje."

Maji alisema, "Ukitaka nikutembelee, jenga uwanja mkubwa. Watu wangu ni wengi mno. Wao huchukuwa nafasi kubwa."

Jua alirudi nyumbani kwa mkewe, Mwezi. Mwezi alimsalimu kwa tabasamu kubwa. 

Kisha Jua akamwambia Mwezi kuhusu ahadi aliyompa Maji.

Siku iliyofuata, Jua alianza kuandaa uwanja mkubwa ambamo angemtumbuiza rafiki yake, Maji.

Uwanja ulipokuwa tayari, alimwalika Maji awatembelee.

Maji alipofika, alimwuliza Jua iwapo ingekuwa salama yeye kuingia ndani. 

Jua alijibu, "Ndiyo, ingia rafiki yangu."

Maji akaanza kutiririka ndani ya nyumba! 

Aliambatana na mamba, samaki, vyura, nyoka, konokono, na wanyama wote wa majini.

Muda mfupi baadaye, Maji alifika magotini. Alimwuliza Jua iwapo bado ilikuwa salama. 
"Ndiyo," Jua alijibu tena. 

Jamaa wengine wengi wa Maji wakaendelea kuingia.

Maji alifika kiwango cha upeo wa kichwa cha mtu. Alimwambia Jua, "Je, watu wangu zaidi wanaweza kuja?" Jua na Mwezi walijibu, "Ndiyo." 

Maji alitiririka ndani zaidi hadi Jua na Mwezi wakalazimika kuning'inia kwenye paa.

Watu wa Maji waliendelea kuingia hadi wakafika juu ya paa la nyumba. Jua na Mwezi walilazimika kwenda juu angani.

Tangu wakati huo, Jua na Mwezi huishi angani.

------------------------------------------------------------



Kijiji chetu kilikuwa na shida nyingi. Tulikuwa na mfereji mmoja.

Tulitegemea chakula cha msaada.

Tuliogopa kuvamiwa na wezi.

Wazazi wengine hawakuweza kulipa karo.

Wasichana wadogo waliacha shule.

Wavulana wadogo walirandaranda kijijini.

Uchafu ulikuwa kila mahali.

Watu walikatwa na vipande vya chupa.

Siku moja,  mfereji ulikosa maji.

Babangu aliwaita watu waende mkutano.

Watu walikusanyika wakajadiliana.

Babangu alisema,  "Lazima tuyabadilishe maisha yetu."

Mimi nilisema,  "Nitasafisha uwanja wa nyumba yetu."

Mamake Dama alisema,  "Wanawake wataungana wapande chakula."

Babake Mumo alisema,  "Wanaume watachimba kisima cha maji."

Kwa sauti moja tulisema,  "Tuyabadilishe maisha yetu."

------------------------------------------------------------



Chungu yuko wapi?

Konokono yuko wapi?

Panya yuko wapi?

Ndege yuko wapi?

Mjusi yuko wapi?

Paka yuko wapi?

Kuku yuko wapi?

Mbwa yuko wapi?

Nguruwe yuko wapi?

Mbuzi yuko wapi?



------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na Mfalme kwa jina Kayanja. Yeye, mkewe malkia na Apenyo binti yao,  waliishi katika kasri kubwa. 

Apenyo alikuwa msichana mrembo. Kila mwanamume alitaka kumwoa, lakini mfalme Kayanja alitaka mahari ya juu sana.

Karibu na kasri la mfalme Kayanja, aliishi Chifu Aludah Mkuu. Aliitwa 'Mkuu' kwa sababu kila aliyeishi pale kijijini, alimtii. 

Chifu Aludah alikuwa amempoteza mkewe kutokana na ugonjwa wa malaria. Alitaka kuoa mke mwingine.

Chifu Aludah alikuwa mzee mfupi mwenye upara. Aliamua kupeleka mahari kwa Mfalme Kayanja ili amwoe bintiye. 

Walipokuwa wakijadili mahari, Kakembo, kijakazi wa Mfalme, aliyasikia mazungumzo yao. 

Kakembo alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Apenyo.

Chifu Aludah alikubali kumpa Mfalme Kayanja nusu ya mali yake. Pia, alileta sindano ambayo ilikuwa sehemu ya mahari aliyoleta. 

Matayarisho ya harusi yalifanywa kisirisiri baina ya Mfalme Kayanja na Chifu Aludah. Mfalme Kayanja alijua kwamba bintiye hangefurahia uamuzi huo.

Juma moja kabla ya siku ya harusi hiyo ya kifalme,  Kakembo alimjulisha Apenyo.

"Mpendwa binti-mfalme, babako amepanga kukuoza kwa Chifu Aludah. Harusi itafanyika katika muda wa juma moja."

Apenyo alishtuka asijue la kufanya. Aliwaza, "Kamwe sitaolewa na yule mzee mwenye upara. Kamwe! Lazima nimwone Trevor, mpenzi wangu. Lazima achukue hatua bila kupoteza muda."

Usiku huo Apenyo alitoroka. Babake angegundua alikokuwa akienda angekasirika sana. 

Alipitia kwenye msitu wa giza wenye mawe. Mwishowe, akafika kwa Trevor. Aliwasili kwa Trevor akiwa mchovu, mwenye njaa na kiu.

Trevor alimkaribisha. "Mpenzi wangu, mbona ukakimbia umbali huu peke yako usiku?" Trevor aliuliza. 

Alimletea maji ya kunywa kisha akatulia kumsubiri Apenyo aongee.

Apenyo alikunywa maji, akashusha pumzi na kusema, "Babangu anataka kunioza kwa chifu Aludah Mkuu. Lakini, siwezi kuolewa na yule mzee mwovu. Trevor, ningependa kuolewa nawe hata kama wewe ni maskini. Ninakupenda."

"Lakini sina chochote cha kulipia mahari." Trevor alilalama. 

Apenyo alijibu, "Naelewa, lakini nataka kuolewa nawe tu." 

Apenyo alisema, "Hebu twende kwa Kategga, mwenye mashua, atuvushe hadi upande mwingine wa mto tumuepuke babangu."

Mfalme Kayanja alipogundua kuwa bintiye ametoweka, aliamuru msako ufanywe kijijini. Walinzi na askari walimtafuta Apenyo kila mahali, lakini, hawakumpata. 

Walirudi na kumwambia Mfalme kwamba Apenyo hakuonekana popote. "Basi tafuteni pia vichakani," Mfalme Kayanja aliamrisha kwa hasira.

Trevor na Apenyo walifanya haraka kwenda mtoni. 

Wakati huo, mawingu meusi yalianza kukusanyika angani. Dhoruba kubwa ilikuwa inakaribia.

Kategga, mwenye mashua, alikuwa anafunga mashua yake Trevor na Apenyo walipofika. Trevor alimwmomba Kategga awavukishe hadi ng'ambo ya pili ya mto. 

Kategga alikataa akawaelezea kwamba dhoruba kali ilikuwa inakaribia na ingekuwa hatari kuvuka.

Trevor alisizitiza huku akimwelezea kwa nini itawalazimu kuvuka  wakati huo. Alitia mkono mfukoni na kutoa kete yenye thamani na kumpa Kategga. 

Kategga aliwaonea huruma akakubali kuwavusha haraka kabla ya dhoruba.

Kategga aliivuta mashua ukingoni. Wakaabiri na kuanza safari. 

Mfalme Kayanja na Chifu Aludah walipofika ufukweni, waliwaona watu watatu mashuani wakivuka. 

Wakatambua kwamba Apenyo alikuwa anatoroka.

Dhoruba kali ilisababisha mawimbi makubwa. Kategga alishindwa kudhibiti mashua. 

Mfalme alilia, "Tafadhali rudini! Nawasamehe." Mayowe yake yalikuwa ya bure. Mashua ilipinduka wote wakazama. 

Tangu siku hiyo, walioishi katika ufalme wa Kayanja, walimwoa waliyemtaka, tajiri au maskini.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na wafanya biashara waliokwenda kila mahali. Walisafiri wakati wa musimu wa baridi na musimu wa joto. 

Walivuka milima, majangwa na misitu wakiuza na kununua bidhaa. 

Wafanya biashara hao waliwaogopa majambazi, kwa hivyo walisafiri wakiwa katika vikundi.

Ilitokea kuwa mfanya biashara mmoja hakuweza kupata kikundi cha kusafiri nacho, kwa hivyo, alisafiri peke yake. Alikutana na jambazi akawa na hofu. 

Jambazi huyo alimwuliza, "Wewe ni nani?" 

Alijibu, "Mimi ni mfanya biashara."

"Uko peke yako?" 

"La! Marafiki zangu wako nyuma ingawa sasa niko peke yangu," alijibu.

Wakati huo, mfanya biashara mwingine alikuja kutoka nyuma yao. Alijificha akatazama kwa hofu jambazi yule akimwua mfanya biashara wa kwanza na kumzika. 

Aliwaza, "Nitaendeleaje na safari yangu? Yaliyompata mwenzangu yatanipata mimi pia." Aliogopa kuvuka akabaki mahali hapo kwa muda. 

Baadaye, aliwaza, "Siwezi kukaa hapa milele. Lazima niendelee na safari yangu."

Alipita mahali ambapo jambazi alikuwa amemwua mfanya biashara wa kwanza. Alifika kijijini akiwa amehuzunika sana. Hakuweza kutabasamu wala kuzungumza na watu. 

Watu walimwuliza, "Ulikuwa mchangamfu, lakini sasa umehuzunika. Kwa nini?" 

"Nimechoka na ninahisi kiu," alisema.

Alikaa hapo kijijini usiku wote. Siku iliyofuata,  aliendelea na safari yake. 

Watu walizidi kumwuliza, "Unasumbuliwa na nini?" 

Mfanya biashara alijiuliza, "Je, niwaambie au la?" Mwishowe, aliamua kuwaambia yaliyompata mfanya biashara mwenzake.

Alipomaliza kuwasimulia, wanakijiji walijua kuwa jambazi alikuwa ametoka kijijini kwao. 

Walisema, "Ni vibaya sana kitendo kama hiki kutendeka hapa. Tutajaribu kujua aliyeuawa ni nani." 

Lakini, hawakusema jambo lolote kuhusu jambazi aliyemwua mfanya biashara huyo.

Mfanya biashara yule aliwaambia wanakijiji, "Nilimuona mtu akizika maiti ya mtu mwengine. Sikujua aliyezikwa alikuwa nani wala jambazi alikuwa nani. Sitawahi kurudi mahali hapa tena."

Mfalme wa kijiji alisikia jinsi wafanya biashara walikuwa wakiuawa na kuzikwa na majambazi. 

Alihuzunika. "Je, majambazi wanawezaje kuwafanyia wafanya biashara hivi katika milki yangu?" 

Alitafuta njia ya kusuluhisha tatizo hilo. "Nitawaalika watu wote katika sherehe kisha nijaribu kuwashika majambazi hao."

Mfalme alipendwa sana na watu wake. Aliwaandalia sherehe wakulima, makasisi na kila mtu kijijini. Wote walikula, wakanywa na kujiburudisha. 

Mfalme akasema, "Binti yangu ni mgonjwa. Dawa pekee inayoweza kumponya ni ndimu inayomea karibu na maji baridi yaliyo mbali na wanapoishi binadamu. Kuna yeyote anayeweza kuniletea ndimu hiyo?"

Kila mtu aliwaza, "Je, nitaipata wapi ndimu aina hiyo?" 

Hawakusema chochote ila jambazi alisimama haraka akasema, "Mheshimiwa, nitakuletea ndimu hiyo, lakini nipe muda wa wiki mbili."

Jambazi alikwenda moja kwa moja mpaka mahali alipomzika mfanya biashara aliyemwua kwa sababu ndimu aliyotaka mfalme ilimea hapo. 

Alikimbilia kuipata kabla mtu mwingine kufanya hivyo. Aliziweka ndimu mfukoni halafu akakimbia kumpelekea mfalme.

Baada ya kusubiri langoni kwa siku kadhaa, alikubaliwa kumwona mfalme. 

Alisema, "Niko tayari kutimiza mahitaji yako. Nimekuletea ulichokitaka. Tafadhali kipokee." 

Mfalme alisema, "Nimefurahi umekileta nilichotaka. Ningependa unipe tukiwa mbele ya watu wengi."

Mfalme aliwaita watu wote kutoka kijijini kwenda katika ikulu. 

Walipokuwa wanakula na kunywa, alisema, "Mtu huyu ametimiza ahadi yake kama mlivyosikia. Alisema ataleta tunda nililohitaji na amelileta. Ningependa kupokea zawadi hii kubwa mbele yenu nyote."

Watu walifikiri kuwa jambazi angepata zawadi ya pesa. Walimwonea wivu. Walishangaa jinsi alipata matunda hayo ya pekee. 

Jambazi aliufungua mfuko wake ili kumpatia mfalme ndimu mbili. 

Alipozitoa mfukoni, zilikuwa ndimu mbili, lakini alipomkabidhi mfalme, ziligeuka na kuwa mafuvu mawili ya binadamu.

Hili lilipofanyika, watu wote walikasirika, naye jambazi akapigwa na butwaa. 

Mfalme alitabasamu. 

Kwa muda mrefu, alikuwa akitamani kukomesha ujambazi katika ufalme wake. Alitaka vitendo vyao viovu kujulikana kwa kila mtu. Alikuwa akiomba Mola amwonyeshe nani aliyekuwa jambazi.

Siku hiyo, maombi yake yalijibiwa. 

Alijua mtu huyo ndiye aliyekuwa muuaji. 

Alitoa amri atiwe gerezani.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Mhogo na Mtende waliishi kijijini Koowa. Kama marafiki, walitembeleana kila siku. 

Walikuwa wakulima waliofanya kazi kwa bidii katika mashamba yao.

Katika mwaka mmoja, kulikuwa na ukosefu wa mvua. Mimea yote ilikauka. Watu wakakosa chakula.

Mhogo na Mtende waliamua kwenda kutafuta kazi katika kijiji tofauti.

Wlimkuta mwanamke mmoja wakamsalimu, "Hujambo?" Aliitikia kisha akwauliza, "Mnakwenda wapi?" 

Mtende alimjibu, "Tunakwenda kutafuta kazi katika kijiji jirani."

"Kazi gani mnayofanya?" Mwanamke yule aliuliza. Walijibu, "Tunaweza kuipa chakula familia yako na mifugo wako.

Mwanamke alwauliza tena, "Mtahitaji nini kutupatia chakula hicho?" Walimjibu, "Tupe ardhi, maji na huduma nzuri."

Mwanamke yule aliwapeleka nyumbani kwake.

Alasiri moja, Mtende na Mhogo walibishana vikali. Mhogo alisema kuwa yeye alikuwa muhimu zaidi kuliko Mtende.

Mtende naye akasema kuwa yeye alikuwa muhimu kuliko Mhogo.

Mwanamke yule aliwasikia kutoka chumbani kwake. 

Alitoka nje na kwauliza, "Mbona mnabishana?"

Mhogo alikuwa wa kwanza kuzungumza. "Mimi ni muhimu zaidi kuliko Mtende. Ninazaa mihogo mnayotumia kutengeneza fufu na unga wa mihogo."

"Watu hupanda mashina yangu. Mifugo wenu hula majani na maganda yangu. Je, Mtende hufanya nini?" Mhogo aliuliza.

Mtende alicheka, akatikisa kichwa chake kisha akasema, "Mwanamke wee, unaikumbuka supu ya tende unayofurahia sana? Hutoka kwa nani?"

"Mimi hutoa mafuta yanayotumiwa kukaanga samaki na nyama. Je, utawezaje kutayarisha kitoweo na mchuzi bila mafuta?"

"Zaidi ya hayo, matawi yangu huezeka paa za vyumba vyenu na vibanda vya kupumzikia. Mnaburudika baada ya kazi kwa kuinywa kosha ninayotoa."

"Isitoshe, fagio zinazotumiwa kufagia vyumba na uwanja wa nyumba zenu zinatoka kwangu," Mtende alimaliza kusema.

"Hmmm!" Mwanamke alizusha pumzi. "Ni sawa marafiki, nimewasikia. Nitaitatua shida hii."

"Ninyi nyote ni viumbe muhimu sana kwangu. Pamoja, mnatengeneza mlo mtamu wa fufu na supu ya tende!" mwanamke akasema.

Mwanamke yule alitayarisha supu ya tende pamoja na fufu kutoka kwenye mihogo. Aliwaalika marafiki zake kula naye. Walifurahia chakula hicho sana.

Tangu wakati huo, Mhogo na Mtende wamekuwa marafiki wakubwa.

------------------------------------------------------------



Kumuua nyani, lazima uwe na macho makavu.

Mbwa anayebweka, haumi.

Wakati viboko wanapigana, ni nyasi ndizo huteseka.

Kifaranga huchafua kiota kwa sababu hivyo ndivyo anaona mamake akifanya.

Usiseme kwamba kuna tembo unapokuwa pale juu ya mabega yangu.

Chura wote huzaliwa kwa njia ile ile.

Kidole kimoja hakiwezi kuua chawa.

Simba asiyekuwa na nyama, hula nyasi.

Ni mbuzi mdogo aliye nyuma ya kundi ndiye hupatwa na fimbo.

Unaogopa giza wakati ambapo hata fisi hawapo.

Kinyonga hufa kwa ajili ya aibu.

Ili uweze kuyaona macho ya konokono, lazima usubiri.

Mchekelee tu kasa, lakini ni yeye ndiye ana maji.

Mgeni ndiye humuua nyoka.

Fisi anayelilia mashambani hali wimbi.

Simba anayekula binadamu haendi nje usiku.

------------------------------------------------------------



Wiki iliyopita nilipokea barua nyingi.

Siku ya Jumatatu, daktari alimwandikia mwalimu wangu barua.

Tabisile ni mgonjwa. 

Ni lazima akae nyumbani.

Siku ya Jumanne, nilipokea barua.

Ilitoka kwa wanafunzi wa darasa langu.

Tabisile, tunakutakia nafuu haraka!

Siku ya Jumatano, nilipokea barua nyingine.

Ilitoka kwa rafiki yangu.

Nimekuchorea picha hii. 

Nakupenda sana.

Wako, Dudu.

Siku ya Alhamisi, nilipokea barua.

Nayo ilitoka kwa mamangu.

Nilifurahi.

------------------------------------------------------------



Nilisikia, "Hodi! Hodi!"

"Ni nani, jamani?" niliuliza huku nikisinzia.

"Ni mimi." Sauti inayokwaruza sikio ilinijibu.

"Nani ndiye 'Mimi'?" niliuliza.

"Nilikwambia kuwa, ni-mi-mi tu," sauti ile ile ilisema.

Nilijibu, "Mimi sijui mtu yeyote anayeitwa, 'ni-mi-mi tu.'" 

Nilitazama ikiwa chandarua changu kilikuwa kimenikinga vizuri.

"Jina langu ni Amosi," sauti iliyokwaruza zaidi kuliko awali ilisema. 

Ilisikika ikiwa karibu sana na sikio langu.

"Amosi nani?" niliuliza huku nikitazama ndani ya chandarua.

"Amosi Kuito." Hatimaye, sauti ilisema. 

Wakati huo huo niliumwa sikioni.

"Uui!" Niliruka juu na kuondoka kitandani. 

"Utalipia kitendo hiki!" nilipiga kelele.

Kwa hasira, niliiasha taa kumtafuta adui wangu.

Nilitangaza vita dhidi ya Amosi Kuito msumbufu!

------------------------------------------------------------



Hapo zama za kale, paliishi bwana mmoja aliyekuwa mwenye bidii sana. Yeye na mkewe walikuwa wenye umoja na ushirikiano.

Bwana huyo kwa jina Bidii, alikuwa mkulima hodari kijijini mwao, japo familia hii ilikuwa masikini.

Kila siku Bidii pamoja na mkewe, Subira waliamuka asubui na mapema na kwenda shambani.

Bidii alikuwa na shamba kubwa aliloachiwa kama urithi na wazazi wake. Bidii na Subira hawakujaliwa kapata mtoto.

Japo jambo hili liliwasikitisha, hawakufa moyo. Bidii alikuwa mtu mwenye subira na mvumilivu. Alijua kuwa subira huvata heri na mvumilivu hula mbivu.

Alijipiga moyo konde na kujua Maulana ndiye mpaji wa vyote.

Kila kulipokucha, Bidii alianza safari yake ya kwenda shambani. Ilipofika adhuhuri  mkewe Subira alimpelekea mmewe chamcha, kidogo alichokipata. 

Bidii alishukuru kwani alijua kuwa mtaka vyote hukosa vyote. Alipomaliza kupata chamcha alimshukuru mkewe na kuendelea na kazi.

Siku moja Bidii aliamka asubui na mapema kama ilivyokuwa kawaida yake na kwenda shambani. Alipofika alianza kazi yake.

Mkewe alimletea ujumbe kwamba bwana wawili walitaka kununua mazao yake yote.

Bidii alifurahi sana. Baada ya mauzo hayo alijiendeleza kimaisha.

Hapo ndipo alipojua kuwa bidii hulipa.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, palikuwa na Mbweha.

Alikuwa mvivu pia mjinga. 

Yeye na babake mzee waliishi jangwani Kalahari.

Asubuhi moja, Mbweha mzee aliamka na kumpata mwanawe amelala juani. 

Kifungua kinywa hakikuwa tayari na mbuzi walikuwa bado zizini! 

"Wewe kijana mvivu sana! Nenda ukamtafute mke. Nimezeeka na siwezi kukukimu tena," babake alisema. 

Mbweha kijana aliruka juu na kuwapeleka mbuzi malishoni.

Kichakani, aliona kitu kilichoangaza juu ya mwamba. 

Alipoukaribia mwamba ndipo mwangaza ulipozidi kupendeza. 

Labda huyu ndiye aliyekuwa mke wake!

"Wewe ni mzuri mno," Mbweha kijana aliueleza mng'aro. "Lakini, wewe ni nani? Mbona uko peke yako?" 

"Mimi ni Jua," mng'aro ulijibu. "Familia yangu iliniacha hapa ilipohama. Haikutaka kunibeba maanake mimi ni moto sana."

Mbweha alisema, "Lakini, wewe u mzuri sana! Mimi nitakubeba. Nitakupeleka nyumbani nikujulishe kwa babangu." 

"Ni sawa, unaweza kunibeba, lakini, usilalamike nikizidi kutoa joto usiloweza kuhimili," Jua lilisema.

Mbweha kijana alienda nyumbani bila ngozi, manyoya mgongoni, wala mke.

Babake Mbweha aliuuguza mgongo wa mwanawe kwa kutumia mafuta.

Polepole, manyoya yaliota tena.

Manyoya hayo mapya yalikuwa rangi tofauti na yale aliyozaliwa nayo. 

Rangi hizo tofauti zilimkumbusha Mbweha kila mara kutokuwa mjinga tena.

Maelezo kuhusu hadithi:

Katika mwaka wa 2005, mwanahadithi wa Naro kwa jina la Bega Cgaze kutoka Jangwa la Kalahari nchini Botswana alimsimulia Marlene Winberg hadithi hii ambaye anaielezea hapa. Hadithi inapatikana katika mitindo tofauti katika jamii nyingi za kiSan za Afrika ya Kusini. Inawaonya vijana wengi wa kiume dhidi ya kudanganywa na urembo wa kimwili wa wasichana, na inawaelezea wazazi kutowalazimisha watoto wao kuoa kwa ajili ya kupata msaada wa nyumbani. Vilevile inaonyesha nguvu za jua jangwani. Michoro imefanywa na Marlene na kufafanuliwa na Satsiri Winberg kupitia weledi wa kikundi cha Manyeka cha Kisanaa.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na mwanamume aliyeitwa Kijogoo. 

Kijogoo alikuwa mrefu sana.

Watu walizoea kusema, "Huyu ni binadamu wa ajabu!"

Alipokuwa mdogo, mama yake na baba yake walimpeleka kwa mganga.

Mganga aliwaambia, "Mtoto huyu amepewa laana. Baada ya kumzaa hamkumpa baraka zake. Kwa hivyo atakuwa na miguu mirefu. Na atakapofikia jua, atakufa!"

Mama na baba walishangaa. 

Baba akamlaumu mama akisema, "Wewe ndiye umesababisha maafa haya. Hukumpa baraka Kijogoo kwa kutoa sadaka ya ng'ombe dume na jike."

Kijogoo aliteseka. 

Alipofikia jua, alifariki.

------------------------------------------------------------



Buibui Anansi, na Sungura, walikuwa marafiki. Waliishi kwa amani kijijini milimani. Sungura alimiliki shamba kubwa lililojaa mboga na matunda. 

Ingawa Sungura alimgawia rafikiye Anansi kwa ukarimu, Anansi hakufurahia na alimwonea wivu.

Buibui Anansi aliwaza jinsi angelinyakua shamba la Sungura na kulifanya kuwa lake. Alifaulu na kumwacha Sungura katika hali ya umaskini na bila makao. 

Buibui Anansi sasa alijivunia kuwa mmiliki wa shamba lote la Sungura pamoja na mboga na matunda.

Siku moja, Buibui Anansi alienda sokoni kuuza matunda na mboga. Alizipata hela nyingi akakijaza kikapu! 

Alizitumia baadhi ya hela hizo kuinunulia familia yake nafaka. Aliweka nafaka hiyo juu ya hela zilizokuwa kikapuni.

Buibui Anansi alikibeba kikapu chake kichwani akaelekea nyumbani huku akiimba. 

Wakati wote huo, alikuwa akiwaza juu ya vitu vyote ambavyo angetumia hela hizo zote kununa.

Alipokuwa njiani, kulikuwa na manyunyu ya mvua. Punde tu manyunyu yaligeuka na kuwa mvua kubwa iliyomwagika. 

Buibui Anansi alikiacha kikapu chake pembeni mwa barabara naye akaenda chini ya mti kujikinga. Lakini alikichunga kikapu hicho cha thamani kutoka pale alikokuwa.

Mvua ilinyesha kwa wingi zaidi hadi Anansi akalowa na kuhisi baridi. 

Aliamua kukimbilia shimoni. "Nitaketi hapa shimoni hadi mvua itakapoisha," alijiambia. "Bora hela zangu zimekingwa na nafaka niliyoweka juu yake."

Muda mfupi baadaye, Tai aliruka pahali pale na kukiona kikapu kando ya barabara. Aliona pia kwamba kulikuwa na fedha na nafaka. 

Tai alikifunika kikapu hicho kwa mabawa yake na kusubiri mvua iishe.

Buibui Anansi alimwona Tai akiwa amekalia kikapu chake. "Ah asante rafiki yangu kwa kukilinda kikapu changu," alimwambia Tai. 

"Samahani, Anansi, nilikusikia vyema?" Tai aliuliza. "Eti kikapu chako? Kikapu hiki ni changu! Nilikipata hapo pembeni mwa barabara!" 

Buibui Anansi hakuweza kuamini masikio yake! "Ni changu, nakwambia!"

Buibui Anansi alienda kushtaki kwa Chifu. Tai aliwaambia Chifu na wazee, "Inawezekanaje kukiacha kikapu kilichojaa fedha na nafaka barabarani bila ulinzi wowote?" 

"Nilikuwa nikikichunga kikapu changu. Fedha ni zangu na nafaka ni yangu!" Buibui Anansi alisema. 

"Nilikuwa nimekikinga kikapu hiki kwa mabawa yangu ulipotokezea na kudai kwamba kilikuwa chako!" Tai alijibu.

Baada ya Chifu na wazee wake kusikiliza kwa makini pande zote mbili, waliwataka Buibui Anansi na Tai watoke hapo na kwenda mbali kidogo. 

Walijadili kisa hicho kwa muda mrefu. Hatimaye, walifikia uamuzi.

Waliwaita tena Buibui Anansi na Tai. "Tunamwamini Tai," walisema. "Yeye si mwizi. Wewe Anansi, ulikuwa ukijitakia kitu kisichokuwa chako." 

Buibui Anansi hakuweza kuamini masikio yake. Aliangua kilio.

Ujumbe ulisambaa kwamba uamuzi ulimwendea vibaya Buibui Anansi. Buibui Anansi alipoondoka, alimsikia Sungura akicheka kwa nguvu. 

Sungura alirudi shambani kwake akaendelea kupanda matunda na mboga. 

Buibui Anansi aliwapoteza marafiki wote. Alirejelea hali yake ya umaskini.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani kuliondokea mvulana mmoja aliyeitwa Demane. Alikuwa na pacha mwenzake aliyeitwa Demazane.

Wazazi wao walipofariki, Demane na Demazane walienda kuishi na mjomba wao. Mjomba aliwachapa na kuwalisha uji mwepesi.

Walitorokea pangoni wakaishi kwa hofu nyingi. Majitu yaliishi karibu na pango hilo.

Waliunda mlango wenye mashimo mawili ya kupitisha hewa na mwangaza. Demane akamwambia dadake, "Baki humu pangoni nikatafute chakula. Kamwe usipike nyama. Majitu hupenda sana harufu ya nyama."

Kila jioni Demane alirudi na nyama na kuimba:

Demazane, Demazane
nimefika kwenye pango
nimewinda korongo
ufungue kwa mpango
asiingie muongo 

Demazane alichoka kukaa pangoni peke yake. Siku moja alitembea na kupanda miti. Alifurahia akawaza, "Labda hakuna majitu."

Keshoye, alipata ukakamavu. Aliuwasha moto pangoni ili kuondoa baridi. Kwa kuogopa majitu, aliufunga mlango kabisa. 

"Nina hakika hakuna hatari nikichoma nyama kwa moto huu. Chakula cha kuchomwa ni kitamu." Demazane aliwaza.

Demane aliimba:

Demazane, Demazane 
nimefika kwenye pango 
nimewinda korongo 
ufungue kwa mpango 
asiingie muongo.

Demazane alimwambia, "Nilichoma nyama hii kwenye jua nje ya pango." Kwa vile Demane alikuwa amechoka, hakuuliza maswali zaidi.

Siku iliyofuata, Demazane alichoma nyama tena. Alpomaliza, alisikia wimbo: 

Demazane, Demazane 
nimefika kwenye pango 
nimewinda korongo 
ufungue kwa mpango 
asiingie muongo.

Demazane akasema, "Wewe si kakangu. Hiyo sio sauti yake."

Baada ya muda mfupi, aliskikia sauti tena ikiimba:

Demazane, Demazane 
nimefika kwenye pango 
nimewinda korongo 
ufungue kwa mpango 
asiingie muongo.

Sauti hiyo ilifanana sana na ya kakake. Demazane aliufungua mlango.

Jitu kubwa lenye nywele mwili mzima lilijaa mlangoni. Likamchukua Demazane haraka.

Kabla kuondoka, Demazane aliweza kuliokota jivu la jikoni na kulibeba. Walipokuwa wakienda, alimimina jivu lile njiani walikopitia.

Demane aliporudi, alipata mlango ukiwa wazi na Demazane hakuwa ndani. 

Lakini, aliona jivu lililomwagwa kulekea msituni.

Alifuata jivu hilo mpaka alipouona moto mbali.

Demane aliona jitu limeketi karibu na moto. Mkoba mkubwa ulikuwa karibu nalo. Alikaribia akichechemea kama aliyeumia mguu. 

Alisema, "Naomba maji ya kunywa. Nimeumia mguu." "Nitakuletea maji lakini usiguse mkoba wangu." Jitu lilisema huku likiweka mkoba huo vizuri.

Jitu lilipoondoka kwenda mtoni, Demane alikata kamba ya mfuko, ukafunguka na dadake akatoka.

Demane aliubadilisha mkoba huo na wake uliojaa nyuki. Kisha yeye na dadake wakajificha na kungoja kuona kitakachotokea.

Jitu lilirudi na maji pamoja na watoto wake wawili, msichana na mvulana. 

Likamwambia msichana, "Kuna mlo mtamu ndani ya mkoba. Nenda ukaulete!"

Msichana alipofungua mkoba, nyuki walimwuma mkono akalia kwa sauti, "Inauma, inauma."

Jitu lilimwambia mvulana aende kumsaidia. Yeye pia aliumwa akalia kwa uchungu.

"Msinifanye mjinga," jitu lilisema kwa sauti huku likiufungua mkoba.

Nyuki wengi waliliuma kichwani, masikioni na machoni. Lilirukaruka na kulia kwa uchungu.

Jitu lilikimbia kuelekea kwenye bwawa la maji. Lilichopeka kichwa kwenye matope likakwama huko. 

Liligeuka na kuwa kisiki cha mti uliokatwa. Nyuki walijenga mzinga wao kwenye kisiki hicho. 

Demane na Demazane walifurahia asali tamu kutoka kwa mzinga huo.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na mvulana kwa jina Petro. Alikuwa mwanafunzi mwerevu aliyeibuka wa kwanza darasani. Wazazi wake walijivunia kazi yake nzuri. Lakini, Petro alitamani kuwa na kaka, dada au hata kipenzi cha kucheza naye.

Siku moja, Petro alimwuliza mama, "Ninaweza kwenda nje kucheza? Nimekuwa nikisoma wakati huu wote. Ningependa sasa niende nicheze na marafiki zangu." Mamake alimjibu, "Ni sawa! Nenda, lakini usichelewe!"

Alipokuwa akienda uwanjani, Petro aliona jambo lisilokuwa la kawaida. Alimwona mbwa mdogo mwenye madoadoa. Mbwa huyo alikuwa amekwama shimoni na alikuwa ameogopa. "Usiwe na wasiwasi, sitakuumiza. Nitakusaidia," Petro alimwambia.

Petro alimtoa mbwa yule shimoni. Mbwa alibweka kwa furaha, akacheza cheza na kumlamba Petro. "Utakuwa mbwa wangu," Petro alisema kwa furaha.

Mbwa alikimbia akaenda mbali na Petro. Marafiki za Petro walipomwona mbwa akiwakaribia, walisema, "Mbwa huyu anaweza kutuuma." Walimpiga kwa mawe. Petro alipowaona, alikimbia akiwapigia kelele waache kufanya hivyo.

Marafiki wale hawakumsikia Petro. Mbwa alikimbia haraka alivyoweza ili kuyaokoa maisha yake. Alijificha ili wavulana wale waliokuwa wakimfukuza wasimwone. Hawakumpata.

Marafiki wa Petro walirudi uwanjani na kumkuta Petro akiwa analia. "Kuna nini?" mmoja wao aliuliza. "Mlimfukuza mbwa wangu!" Petro alieleza. Walishangaa na kusema, "Hatukujua kwamba yule alikuwa mbwa wako. Tunakuomba radhi. Twende tumtafute."

"Hakuna maana ya kufanya hivyo. Hatutawahi kumpata," Petro alisema kwa huzuni. "Ndiyo, tutampta. Amka twende, tutampata mbwa wako. Tusipoteze matumaini," marafiki zake walimfariji.

Petro na marafiki zake walimtafuta mbwa kwa muda mrefu hadi wakachoka. Hatimaye, Petro alisema, "Kuna sehemu moja ambapo anaweza kuwa amejificha. Tusipompata huko, sitamtafuta tena. Twendeni mtoni."

Mbwa alipowaona wavulana wakija, aliogopa tena. Aljaribu kuvuka mto lakini vilevile aliyaogopa maji. Alikuwa karibu kuruka majini, wakati Petro alisema, "Acha, usiruke!"

Mbwa alipogeuka na kumwona Petro, alimkimbilia. Petro alimkumbatia mbwa wake naye mbwa akamlamba usoni. "Rafiki yangu! Nilidhani kwamba umepotea kabisa!" Petro alilia.

Walipokuwa uwanjani, Petro aliwashauri marafiki zake. "Kabla ya kuamua kutenda jambo, tafadhali fikirieni kinachoweza kutokea. Mnaweza kuwaumiza wenzenu." Marafiki zake waliwaza juu ya maneno yake kisha wakasema, "Tusamehe. Mbwa huyu atakuwa rafiki yetu pia."

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, wanyama wa pori waliishi pamoja.

Kunguru na Mbweha walikuwa marafiki wakubwa.

Wakati huo kulitokea njaa. Wanyama hawakuwa na chakula.

Mbweha na Kunguru walienda kutafuta chakula.

Walipoipata nyama, Kunguru alianza kuila peke yake.

Mbweha alipoona hivyo, alimnyanyua Kunguru. 

"Je, nikuue au la?" Mbweha alimwuliza.

"Tafadhali, usiniue! Hasa, usinitupe chini ya mwamba," Kunguru alimsihi.

Mbweha alimjibu, "Sitakutupa chini ya mwamba."

Lakini ulikuwa uongo. Mbweha alinuia kumtupa Kunguru chini ya mwamba.

Mbweha alimptupa Kunguru chini ya mwamba.

Kisha alitazama kutoka pembeni akitaka kuuona mwili wa Kunguru.

Wakati huo, Kunguru alikuwa amegeuka na kuanza kuruka hewani.

Kunguru alitua mtini.

Mbweha na Kunguru walitazamana.

"Niliepuka kwa sababu mimi ni mwerevu," Kunguru alijigamba.

"Uliepuka kwa sababu nilikuruhusu uepuke," Mbweha alimjibu.

------------------------------------------------------------



Zamani dunia ilikuwa mpya.

Milima ilifunika ulimwengu kama blanketi.

Dunia ilikuwa na dimbwi kubwa.

Lilikuwa na maji baridi yaliyotulia.

Nyoka wawili waliishi kwenye dimbwi. 

Mmoja mwenye nguvu, mwingine dhaifu.

Siku moja radi ilipiga.  

Nyoka wakaona ardhi na vitu tofauti.

Wakaamua kwenda kuishi kwenye ardhi.

Wakajikunjua wakaogelea.

Wakaelekea kwenye mwangaza.

Mikia yao ikagawika wakawa na miguu. 

Wakapata pia mikono na vidole.

Wakageuka wakawa mume na mke. 

Wakatazamana, wakapendana.

Wakaamua kulinda wanyama na mimea.

Wakafurahia jua.

Wakashikana mikono.

Wakatembea pamoja kwenye ulimwengu wao mpya.

------------------------------------------------------------



Kosi na Farida ni marafiki. Wao wanapendana sana na wote wawili wanasoma shule ya Fariji. Kosi na Farida si marafiki tu bali ni majirani.

Farida anapenda masomo sana na huwa anaamka mapema kufanya marudio. Kila anapoamka, huwa anamwamsha Kosi.

Kosi huchukua wakati sana kabla ya kuamka. Yeye ni mvivu sana. 

Baada ya kusoma wanajitayarisha na kuenda shule pamoja.

Farida hufanya kazi kwao baada ya shule. Kosi hupenda tu kula kila wakati na kucheza bila kufanya kazi. 

Wazazi humuonya Kosi kuacha tabia hiyo, lakini huwa hasikii. Wao humshauri aige tabia za rafiki yake Farida.

Wakati wa likizo, Farida alikuwa akiwafuata wazazi wake shambani kila siku. Alitaka kujifunza mambo mapya wakati huo wa likizo. 

Farida alipokuwa akimwambia Kosi waende shambani, Kosi alisema kuwa alikuwa amechoka sana. Au alisema kuwa alikuwa akiumwa sana na kichwa.

Kosi angeonekana tu kwa kina Farida wakati wa kula. Tabia hii ilimfanya Farida  kuhisi vibaya. 

Farida alipata wazo la kumsaidia rafiki yake kuacha uvivu. Aliamua watengeneze bustani ya maua na kufuga mbwa.

Baada ya kumwambia, Kosi alifurahishwa sana na wazo hilo. Wazazi wao pia waliwasaidia kutayarisha bustani ile. Vilevile, waliwapa pesa za kununua mbwa. 

Baada ya siku kadhaa, maua yao yalianza kumea vizuri. Maua ya Kosi yalihitaji maji.

Kila mtu alitamani kuwa na maua kama yale. Farida na Kosi waliendelea kutia bidii kufanya bustani ipendeze zaidi. 

Kila asubuhi Kosi alipaswa kunyunyizia maua maji naye Farida kuwalisha mbwa.

Kosi alizidisha bidii kabisa Jambo ambalo lilifanya wazazi wake kustaajabu. 

Alianza kuamka mapema bila kuambiwa na mtu. Hakupata wakati wa kulala mchana. 

Wakati mwingine alisahau kula chakula na kukumbushwa na mamake.

Alifurahia sana na kumshukuru rafiki yake Farida.

------------------------------------------------------------



Mamba ana meno makubwa.

Simba naye ana meno makubwa.

Ng'ombe ana meno ya nguvu.

Ndege hawana meno.

Panya wana meno ya mbele 
makubwa.

Papa wana meno makali.

Zamani nilikuwa na meno mengi.

Lakini sasa nina meno machache.

------------------------------------------------------------



Hapo kale aliishi mzee mmoja aliyeitwa Lotum.  Mkewe aliitwa Akiru.

Lotum aliwafuga mbuzi, ngamia, ng'ombe na punda.

Waliishi kwa muda mrefu bila kujaliwa mtoto. Baadaye, Akiru alijifungua mtoto mrembo. 

Lotum alifurahi na kujivunia mkewe.

Siku moja, Akiru alimwacha mtoto nyumbani pekee ili aende kuwakama ng'ombe. 

Kwa kawaida, alimwachia kibuyu cha maziwa.

Kila alipoachwa nyumbani, mtoto angeamka na kunywa maziwa yote kisha aanze kulia. 

Mamake angekimbia chumbani kumtuliza.

Kila wakati Akiru alikipata kibuyu cha maziwa kikiwa kitupu. 

Alishangazwa sana asijue ni nani aliyeyanywa maziwa yote.

Baada ya muda, Akiru alimjulisha mumewe Lotum mambo hayo. 

Lotum akaamua kupeleleza.

Lotum alijificha chumbani humo. Mara alimwona mtoto akibugia kibuyu cha maziwa mdomoni. 

Alishangaa kumwona mtoto akiyanywa maziwa na kuyamaliza.

Lotum na mkewe waligundua haya. 

Waliamua kuondoka usiku mtoto alipokuwa amelala.

Walimwachia mtoto wao ng'ombe mmoja, ngamia mmoja na mbuzi mmoja.

Mtoto alipoamka alishangazwa na jinsi nyumba ilivyokuwa tulivu. Akawaona wanyama alioachiwa. 

Alikasirika na kuwaua ngamia na mbuzi. Hatimaye,  alijitosa tumboni mwa ng'ombe.

Siku moja ng'ombe akiwa malishoni, mwanamume mmoja alimwona, akafikiria, "Nitamchinja ng'ombe huyu nipate kitoweo."

Mara akachomoa mkuki na kumfuma tumboni akafa. 

Alipokuwa akimchuna ngozi, alisikia sauti kutoka tumboni mwa ng'ombe, "Usiniumize, nimo humu!"

Mtoto huyo alitoka tumboni mwa ng'ombe na kujinatisha kwenye kichwa cha mwanamume huyo. 

Mwanamume alijawa na hofu akatoroka kabla ya kuila ile nyama.

Walipofika nyumbani, mtoto alijinasua na kukaa mwambani. Mwanamume alimchinjia mtoto kondoo dume aliyenona.

Mtoto yule alikula, akashiba, akafurahi.

Usiku huo alitoweka asionekane tena.

------------------------------------------------------------



Tulianza safari yetu kutoka mji wa Nakuru. Tulipitia mji wa Naivasha na Mai Mahiu halafu tukaelekea Narok. 

Barabara zote kutoka Nakuru hadi Narok zimewekwwa lami.

Kutoka Narok hadi Mbuga ya Maasai Mara ni kilomita themanini na nane. Barabara hii haina lami. 

Ilituchukua masaa mawili kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Ingawa ilituchukua muda mrefu kufika, nilifurahia safari kwani niliweza kuwaona wanyama wachache njiani.

Niliwaona mbuni, nyumbu, twiga, pundamilia, kondoo na ng'ombe wa jamii ya Wamaasai.

Tulipofika langoni, tulizingirwa na watu wengi waliokuwa wakiuza shanga na mapambo mengine. 

Tulinunua shanga za aina tofauti: za kuvaa shingoni, masikioni  na mikononi. 

Pia, tulinunua viatu vya akala na shuka za kimasaai.

Tulipofika mahali tulikuwa tumepanga kulala, tulionyeshwa hema yetu. 

Ilikuwa nzuri sana na yenye vitanda vilivyotandikwa shuka za kimaasai juu yake.

Pia, kulikuwa na neti ya kuzuia mbu.

Baada ya kuweka mizigo yetu, tulionyeshwa manyatta. Tuliingia ndani ya  nyumba kadhaa na kuona jinsi Wamaasai wanavyoishi. 

Nilishangaa kuona nyumba zao ndogo na tofauti sana na za kisasa.

Katika nyumba hizo ndogo, walikuwemo ndama pia. 

Sikuona vitanda vya kisasa ila ngozi ya ng'ombe na moto wa kufukuza baridi usiku.

Walituimbia nyimbo zao za kitamaduni wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi nyekundu na shanga maridadi. 

Pia, walitufunza jinsi ya kuwasha moto bila kiberiti.  Walisugua vijiti viwili pamoja mpaka moshi ukatoka.

Tulirejea kwenye makazi yetu na kupata tumeandaliwa mlo.

Baada ya kula, tulielekea kwenye hema zetu na kulala.

Usiku wa manane tuligutushwa na mlio mkali wa kutisha. Baba alinieleza kuwa ulikuwa wa simba. 

Nilishikwa na wasiwasi na kumshika baba mkono.  Alinifariji kwa kunieleza kuwa kuna walinda zamu ambao wangewafukuza simba.

Baadaye, tulisikia fisi akilia kutoka mbali lakini kilio chake hakikutisha kama kile cha simba.

Nilishikwa na usingizi nikalala mpaka kulipopambazuka.

Asubuhi, tuliingia katika gari la mbugani na kuelekea kwenye nyika kutafuta wanyama.

Tulifika pahali mto wa Mara ulipoonekana.

Tuliwaona viboko katika mto wa Mara. Tulihesabu: mmoja, wawili, watatu…hadi thelathini. 

Walikuwa wametulia tuli wakiota jua.

Baadaye, tuliarifiwa na madereva wengine kuwa simba walikuwa wameonekana. Tulitimua kuelekea tulikoelekezwa. 

Tuliwapata simba watano wakimrarua pundamilia.

Nilihofu kwani gari letu lilikuwa paa wazi. Dereva alinituliza na kusema kuwa wasiposumbuliwa hawawezi kutudhuru.

Ni kweli! Waliposhiba, walilala kando ya nyama iliyobaki. Hawakujali magari yaliyokuwa yamewazunguka.

Tuliendelea na safari yetu ya kuwatafuta wanyama. 

Tulikutana na kundi la tembo waliokuwa wamepiga mstari wakivuka barabara.

Dereva aliendesha kasi ili tukaribie tuwaone tembo vizuri.

Tulishangaa tulipomwona tembo aliyekuwa mnene kuliko wote, akigeuka na kuanza kuja upande wetu mbio. 

Dereva alirudi nyuma upesi kama risasi. Nilipiga mayowe nikifikiri tungeangamia.

Baada ya dakika chache, tembo aligeuka na kwenda kuwatafuta wenzake. 

Kumbe, tulimkasirisha kwa kelele za gari akafikiria sisi ni adui!

Ghafla bila kutarajia, tulikutana na simba wawili. 

Dereva alituambia ni harusi. Alikuwa simba wa kiume na wa kike.

Tulirejea makazi yetu kama tumechoka kabisa.

Tulishika barabara na kurudi mjini Narok halafu tukachukua njia kuelekea Kisii.

------------------------------------------------------------



Zamani, aliishi mkulima mmoja maskini aliyekuwa na Fahali mzee. 

Fahali huyo hakupenda kulima. Alipenda kubaki nyumbani akila nyasi, akinywa maji na kupumzika.

Mkulima huyo vilevile alikuwa na Punda. Punda na Fahali walikuwa marafiki. Mwisho wa siku, walizoea kuongea pamoja. 

Siku moja, Fahali alisema, "Nimechoka sana. Nimefanya kazi siku nzima. Jembe ni kubwa na zito. Naye mkulima haniruhusu kupumzika."

Punda alimtazama Fahali akawaza, "Bila shaka Fahali ni mvivu na hapendi kufanya kazi." 

Kisha akasema, "Unadhani kuwa jembe lako ni zito? Niamini, rafiki yangu, jembe ni jepesi! Mimi leo nimebeba gunia la ngano mgongoni. Nina hakika lilikuwa zito kuliko jembe lako."

Siku iliyofuata, walikutana tena. 

Fahali akasema, "Nimekuwa na siku mbaya leo. Shamba la bwana wangu liko mbali na limejaa mawe. Nimefanya kazi mchana kutwa. Sikupumzika hata kidogo."

"Eti ulifanya kazi ngumu?" Punda alimwuliza. "Mimi leo nilikwenda sokoni mjini, kilomita nyingi kutoka hapa. Nina hakika nimefanya kazi ngumu kuliko wewe."

Siku iliyofuata, Fahali alirudi nyumbani akiwa amechelewa tena. 

Alimwambia Punda, "Ah! Rafiki! Leo ilikuwa siku mbaya kwangu." 

Lakini, Punda hakutaka kumsikiliza Fahali zaidi.

Punda alimwambia, "Wewe huchoka kila wakati na kila siku ni mbaya kwako. Mkulima atakapokuja kesho, lala na ufumbe macho yako useme, 'Moo! Moo!' Mkulima akifikiri wewe ni mgonjwa, atakuruhusu upumzike." 

Fahali alilipenda wazo hilo akasema, "Asante mpenzi Punda. Wazo zuri sana."

Asubuhi iliyofuata, Fahali alilala na mkulima alipofika, aliyafumba macho yake akalia, "Moo! Moo!" 

Mkulima alimtazama akawaza, "Maskini Fahali wangu ni mgonjwa. Lakini, ni lazima nililime shamba langu. Ni nani atakayenisaidia? Haidhuru, kuna Punda! Atalivuta jembe leo."

Mkulima alimpeleka Punda shambani akamfunga jembe na kuanza kumcharaza, "Nenda! Haraka! Vuta!" 

Alimshurutisha Punda.

Punda alifanya kazi siku nzima. Jioni alikuwa amechoka sana. Alitembea polepole kwenda nyumbani. 

Fahali alisubiri na alipomwona, alisema, "Mpendwa Punda, nilikuwa na siku nzuri leo. Nilikula nyasi, nikanywa maji na nikapumzika chini ya mti mkubwa. Nataka kupumzika tena kesho. Je, nifanyeje? Nipe wazo jingine."

Punda alimtazama Fahali, akawaza, "Kazi yake ni mbaya kuliko yangu. Sitaki kuifanya tena kesho." 

Hatimaye, Punda akasema, "Rafiki yangu, kuwa makini. Leo nimemsikia mkulima akimwambia hivi mkewe, 'Fahali wangu ni mchovu kila wakati na sasa ni mgonjwa. Asipopata nafuu kesho, nitamchinja tule nyama.'"

Fahali aliogopa sana akalia akisema, "Eti nini? Alisema hivyo? Kesho, nitafanya kazi yangu. Nimepata nafuu sasa na wala si mchovu tena!"

------------------------------------------------------------



Mimi na dadangu tulikuwa tukitembea kando ya barabara.

Tuliona lori kubwa likiendeshwa kwenye mteremko.

Wakati huo, gari ndogo liliendeshwa kwa kasi kuelekea upande wa juu wa barabara.

Dereva wa lori hakuwa mwangalifu. 

Alikuwa akizungumza kwa simu ya rununu.

Mara lori liligonga gari!

Baadaye, ambulansi ilifika pamoja na polisi.

Pia magari mawili ya kuvuta yale yaliyohusika kwa ajali yalifika.

Tulishuhudia kila kitu. 

Tulitishika sana.

------------------------------------------------------------



Jamani...

Jamani...

Jamani...

Jamani...

Hu! Hum!

Jamani...

Kuna shida gani?

Eti kuna shida gani?
Nimenyong'onyeka.
Hiyo ndiyo shida!
Ninasimama hapa
wala siendi popote.
Ningependa kusafiri mbali lakini siwezi. 
Nimekwama tu hapa.

Aa miye! Aa miye!
Ningeliweza tu
kuona sehemu zote
nzuri kabla ya kufa.
Kongo... Aa...
Jamaika...Aa...
Alaska...Aa...Palestina

Sawa, sawa,
nitakwambia vile
nitakupeleka
popote unapotaka.

Barabara kabisa!
Tunaondoka lini?

Subira huvuta heri!

Tulia!

Tafadahli, kuwa
mwangalifu. Nina
mizizi nyeti.

Makini! Makini!
Usiniangushe!

Uko salama humu.

Hiyo ilikuwa kazi
kweli. Sasa tuko
tayari kuanza
safari yetu.

Asubuhi iliyofuata, waliondoka.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, mtu na mkewe walikuwa na watoto wa kiume saba wajinga. 

Watoto hao waliipoteza mifugo, walivunja jembe, na kila mtu aliwadanganya walipokuwa sokoni.

Mama yao aliomba, "Ee Mungu, mbona watoto wangu wote ni wajinga? Tafadhali, nipe angaa mtoto mmoja mwenye hekima."

Mwanamke huyo alijifungua mtoto mvulana. Mtoto huyo alikuwa mdogo mno. 

"Tutamwita Kadogo," mama akasema.

Kadogo hakukua kimo bali aliongezeka umri. Alikuwa mwerevu sana. Wazazi wake walimpenda lakini, nduguze walimwonea wivu. 

"Mbona wazazi wetu wanakupenda wewe zaidi yetu sisi?" Walimwuliza Kadogo. "Hebu jitazame! Wewe ni mdogo kama panya."

Kulikuwa na adui aliyeishi karibu na familia ya Kadogo. Siku moja, nduguze Kadogo waliwaza, "Adui yetu ana ng'ombe wengi wanono. Usiku wa leo twendeni tukawaibe fahali wawili. Tutamtumia punda wa baba kubeba nyama zote." 

Hawakumwona Kadogo kwa sababu alikuwa nyuma ya kigoda cha baba yao.

Usiku huo, nduguze Kadogo walimchukua punda wakaenda kwa adui yao. 

Kadogo aliwafuata mbio ila hawakumwona.

Walipofika kwa adui, lango lilikuwa limefungwa. Ndugu hao hawakuweza kuingia ndani. Mmoja wao akasema, "Heri tusingemuacha Kadogo nyumbani. Yeye ni mwerevu na angeweza kuingia ndani." 

Hawakuwa wamemwona Kadogo kwa sababu alikuwa amejificha.

Kadogo alijitambulisha, "Ndugu zangu, sikubaki nyumbani. Nisubirini hapa nami nitaingia ndani niufungue mlango. Nitawaelekeza fahali wote kwenu." 

Ndugu wa tatu aliuliza, "Utaingiaje ilhali lango limefungwa?"

Kadogo alicheka akasema, "Tazama, kuna mlango unaonitosha mimi." 

Nduguze walipotazama, waliona nafasi ndogo karibu na lango. Ni nafasi iliyotosha paka pekee, lakini Kadogo aliweza kupita.

Kadogo alipenya kwenye nafais hiyo. Alipanda juu ya lango na kulifungua. 

Aliwaongoza fahali kutoka nje bila tatizo. Alisema, "Nendeni, fahali wangu wazuri! Nendeni nje!"

Mmoja wa nduguze adui alikuwa amelala katika chumba chake. Mbwa waliokuwa macho walianza kubweka walipomsikia Kadogo. 

Bwana wao aliamka na kuuliza, "Kunaendelea nini hapa?"

Kadogo alipomwona, alijifanya kuwa mmoja wa wafanyakazi. "Usiwe na wasiwasi, bwana mkubwa. Fahali wetu wawili walikuwa wamepotea. Sasa ninawarejesha," alisema. 

Bwana yule alikasirika akasema, "Wacha kupiga kelele. Tunataka kulala." Alirudi chumbani kwake, akaufunga mlango.

Kadogo aliwaongoza wale fahali wawili nje. Nduguze walifurahi sana. "Tazama fahali hawa ni wanono! Hebu tuwachinje tule nyama sasa," walisema. 

Kadogo alijibu, "Adui wetu akituskika atatoka nje tena. Lazima tuvuke mto tuwapeleke mbali."

Kadogo na nduguze waliwapeleka fahali mbali na nyumba ya adui. Walipofika kwenye mto, wale ndugu saba walitazama maji kisha wakatikisa vichwa vyao. 

"Hatuwezi kuuvuka mto huu. Maji haya ni mengi na hatujui kuogelea. Kadogo yuko wapi? Yeye ndiye atakayejua jinsi ya kuvuka ng'ambo."

Kadogo alikuwa ameketi juu ya pembe za fahali.
Alisema, "Niko hapa, ndugu zangu. Ninajua la kufanya. Nipeni ukambaa." Ndugu zake walimpatia ukambaa. 

Kadogo aliufunga ukambaa upande mmoja wa mti. Kisha akwaambia nduguze, "Ushikeni ukambaa huu mvuke mto. Mtakuwa salama."

Mmoja baada ya mwingine, ndugu wale waliushika ukambaa wakavuka mto. Fahali waliogelea mbele yao. 

"Sasa tuko mbali na adui wetu. Tunaweza kuwachinja fahali," Kadogo alisema. Wale ndugu waliwachinja fahali wakazigawa nyama mafungu saba kila mmoja na lake.

Kadogo aliwauliza, "Li wapi fungu langu?" 

Nduguze walicheka wakasema, "Fungu lako? Wewe ni mdogo sana. Huwezi kula nyama hii. Kadogo, wewe huna nyama." 

Kadogo alikasirika mno akawaza, "Nitawaadhibu kwa kunitendea hivi." Aliwaambia, "Ikiwa hamtanipa nyama, nipeni kibofu cha fahali mmoja."

Ndugu hao walimtupia Kadogo kibofu na wakaondoka. Kadogo alikichukua kile kibofu, akakimbia mbele ya nduguze. Alipanda mti uliokuwa karibu na njia waliyopitia. 

Kadogo aliufunga upande mmoja wa kibofu kisha akakipuliza hadi kikawa kama mpira. Akakichukua kijiti akaanza kukipiga kile kibofu.

Alipokuwa akikipiga kile kibofu, Kadogo alisema, "Tafadhali bwana, sikuwaiba fahali wako. Ni ndugu zangu waliowaiba. Wamewaua fahali wako na kuzigawanya nyama!" 

Nduguze Kadogo walilia, "Adui wetu ametufuata. Atatuadhibu!" Kisha wakatoroka.

Kadogo alishuka kutoka mtini huku akitabasamu. "Nyama yote itakuwa yangu sasa," alisema.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, Mpunzi na mkewe waliishi na mtoto wao mmoja wa kike aliyeitwa Nosisa. 

Mpunzi alitaka mtoto mvulana, lakini yeye na mkewe hawangeweza kupata watoto wengine. 

Mpunzi alimlaumu mkewe kwa kutompa mtoto wa kiume.

Siku moja, Mpunzi alimchapa mkewe akatoroka na kwenda nyumbani kwao. Alihuzunika kwani Mpunzi hakumruhusu aende na Nosisa. 

Mpunzi alimdhulumu bintiye namna alivyomfanyia mkewe. Nosisa aliishi maisha ya huzuni sana.

Mpunzi alioa mke mwingine. Alitumaini kwamba mke huyo mpya angemzalia mtoto mvulana. 

Maisha ya Nosisa sasa yalikuwa magumu zaidi. Mpunzi alimtetesha na kumlazimisha kumtumikia mke wake mpya. 

Nosisa alifanya kazi kama mtumwa.

Mpunzi aliona fahari sana kutokana na mifugo wake. Alizoea kutazama mifugo wake wakila nyasi uwanjani. Alihisi kuwa alikuwa ametosheka sana na mali yake. 

Wengi wa wafanyakazi wa Mpunzi walisafisha makao yake na kuwachunga mifugo wake. Walikama maziwa ambayo Mpunzi aliwauzia wanakijiji.



Mpunzi alimpenda sana mke wake mpya. Alimchukulia kama malkia. Alikaa chumbani wakati wote huku akiwaamrisha Nosisa na wafanyakazi. 

Nosisa alirauka mapema kila siku kumtayarishia chai mamake wa kambo. Alimfagilia chumba chake na kumpikia. 

Lakini mamake wa kambo alinung'unika kuwa chakula chake kilikuwa baridi, kuwa chai yake ilikuwa hafifu, na kwamba chumba chake kilikuwa kichafu.

Siku moja Mpunzi alikasirika akamkaripia na kumgonga Nosisa kwa kijiti. Nosisa alitoroka akaenda mtoni alikokaa na kulia alasiri nzima. 

Ghafla, alisikia sauti kutoka majini. Alimwona Samaki aliyekuwa akitoa ile sauti. Nosisa alishtuka lakini Samaki alimtuliza, "Tafadhali, binti yangu, usitoroke, mimi ni mamako. Nimebadilika kuwa samaki ili babako asinitambue."

"Una shida gani?" Samaki aliuliza. Nosisa alimweleza kuhusu maisha yake ya huzuni. "Usiwe na wasiwasi mwanangu. Nitakuletea chakula kila siku," Samaki alisema. 

Alimpa Nosisa mboga wakasherehekea halafu akatokomea. Nosisa alienda nyumbani akiwa anatabasamu. Alijua hatalala tena njaa kama ilivyokuwa desturi.

Kila asubuhi Nosisa aliamka na kufanya kazi zote za nyumbani kama ilivyokuwa kawaida. Adhuhuri, alienda mtoni. 

Aliita kila wakati, naye Samaki alitokea akiwa amebeba chakula kitamu. Nosisa alifurahi na kumwelezea chochote. Alianza kuwa na afya nzuri.

Nosisa alimtembelea Samaki kila siku hadi mamake wa kambo akaanza kumshuku. "Kuna jambo linaendelea kule mtoni, na ni lazima nitaligundua," aliwaza. 

Alasiri moja alimfuata Nosisa hadi mtoni. Alimwona Nosisa akimzungumzia Samaki na kupokea chakula kitamu. Siri ya Nosisa sasa ilikuwa imetambulika! 

"Lazima nifanye jambo kumhusu huyu samaki," alisema mama wa kambo.

Mpunzi aliporejea jioni, alimpata mkewe mpya akiwa chumbani kwake akilia. "Unasumbuliwa na nini mke wangu mrembo?" Mpunzi aliuliza. 

"Mganga aliniambia kwamba njia pekee ya kukuzalia mtoto mvulana ni kumla samaki mkubwa aishiye kwenye mto ulio karibu hapa," alisema. "Je, utaniletea samaki huyo usiku wa leo?" mwanamke akamsihi. 

"Nitakufanyia lolote," Mpunzi akasema.

Mpunzi alianza safari ya kwenda mtoni kabla giza kuingia. Aliwachukua wafanyakazi wake ili wamsaidie. Mpunzi alimpata samaki mkubwa zaidi. 

Alipofika nyumbani, moto mkubwa wa kumpika yule samaki ulikuwa tayari. "Nitatayarisha kitoweo kizuri," mwanamke akamwelezea Mpunzi aliyekuwa amefurahi sana.

Usiku ule Mpunzi na mkewe walienda kulala baada ya chakula kitamu. Waliacha mifupa mezani ili Nosisa asafishe asubuhi yake. 

Nosisa alipowaletea kahawa chumbani, walikuwa bado wanalala. "Hili ni jambo geni," Nosisa alifikiria. "Babangu huamka mapema mno kwenda kazini. Kwa nini leo bado analala?"

"Heri nikimbie mtoni nipate kiamsha kinywa kizuri," alifikiria. Nosisa alikimbia kwenda mtoni. Alipofika kule, alimwita Samaki mara nyingi lakini Samaki hakuja. 

Nosisa alianza kulia. Hakujua kilichotokea. Alipokuwa akilia, ndege mmoja alimwambia kilichotendeka. Alilia kwa nguvu akidhani kwamba mamake alikuwa ameangamizwa.

Ndege alimwambia aiokote mifupa kutoka mezani kisha airushe mtoni. Angefanya hivyo, Samaki angefufuka. 

Alimwambia pia awaache babake na mamake wa kambo walale hadi adhuhuri. 

Nosisa alifanya alivyoambiwa. Aliichukuwa mifupa, akaiweka mfukoni kisha akairusha mtoni.

Nosisa alikimbia kurudi nyumbani na kabla adhuhuri kufika, aliwaamsha baba na mamake wa kambo. 

Hakuwatambua! Walikuwa wamezeeka na kudhoofika. Hawangemkaripia wala kumpiga tena. Walichoka wasiweze kuuchunga mji wao. 

Nosisa aliichukua mali ya babake. Akawaita wafanyakazi wote na kuwaambia kilichotokea. Wakasherehekea na kuishi kwa amani.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, wanyama hawakuwa na miguu. 

Wote walitambaa.

Watu pekee ndio waliotembea. 

Walikuwa wamepatiwa miguu na Maguru.

Siku moja, Maguru aliamua kuwapatia pia wanyama miguu. 

Alitaka watembee kama vile binadamu. Kwa hivyo aliwatangazia!

Wanyama walifurahi. Sasa wangeweza kutembea na kukimbia. 

Waliimba na kucheza.

Ilikuwa vigumu kutambaa. Tumbo zao zilikwaruzwa. 

Wangepata miguu wangeweza pia kusimama na kuona mbali.

Siku ilipofika, wanyama wengi walitambaa kwenda kwa Maguru.

Kila mnyama alipata miguu minne. 

Kila ndege alipata miguu miwili.

Walifanana tofauti waliposimama.

Baadhi yao walianguka waliposimama.

Walizunguka kijijini wakiwaambia watu, "Hatutatambaa tena."

Wa mwisho kwenda kwa Maguru alikuwa Jongoo. 

Maguru alimwuliza, "Kuna mwingine nyuma yako?" 

Jongoo alijibu, "La! Mimi ndiye wa mwisho."

Maguru aliwaza, "Ikiwa yeye ndiye wa mwisho, nitaifanyia nini miguu itakayobaki?" 

Maguru aliamua kumpatia Jongoo miguu yote iliyokuwa imebaki.

Jongoo aliondoka kwa furaha akiwa na miguu mingi. 

Aliwaza, "Nitaweza kwenda kwa kasi kuwaliko wote."

Baada ya Jongoo kuondoka, Nyoka alifika. 

"Tafadhali, nipatie nami miguu," alimsihi Maguru.

"Nimepatiana miguu yote kwa waliotangulia. Wewe ulikuwa wapi?" Maguru alimwuliza. 

Nyoka alimjibu, "Nililala kupita kiasi."

Maguru alitafuta kila mahali lakini hakupata miguu yoyote ya kumpatia Nyoka.

Maguru alimwambia, "Hakuna miguu iliyobaki." Nyoka alitambaa akarudi bila miguu. 

Hiyo ndiyo sababu nyoka huwa hawalali. Wanasubiri kupata miguu.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na mvulana mwenye sura mbaya sana. 

Hakupendwa na yeyote, hata wazazi wake. 

Hata nyumbani, aliketi peke yake wengine walipotazama runinga.

Shuleni pia aliketi peke yake watoto wengine walipokuwa wakicheza.

Walipokwenda kuwaleta mifugo, yeye alitembea nyuma yao. 

Watoto wengine hawakutaka kutembea pamoja naye.

Alijua kuwa hakuna aliyemtaka wala kuzungumza naye. 

Siku moja aliamua kutoroka, lakini hakujua pa kwenda. 

Alitembea hadi kwenye msitu na kuanza kuogopa.

Alipokaribia msituni, alikutana na bibi mkongwe. Alikuwa mchafu na mwenye sura mbaya. Bi Kizee alimsalimia na kumwuliza, "Unafanya nini katika msitu huu wa kuogofya?" 

Mvulana alishangaa kuzungumziwa na Bi Kizee. "Ninakwenda popote. Hakuna yeyote anipendaye wala kunizungumzia," alimwambia Bi Kizee.

Bi Kizee alimwuliza ikiwa angehitaji usaidizi. "Ndiyo," alijibu haraka. 

Bi Kizee alimwambia, "Kabla sijakusaidia, nataka ulambe uso wangu hadi upendeze."

Mvulana alikubali kuulamba uso wa Bi Kizee yule ili asaidiwe. 

Aliulamba uso wa Bi Kizee kuanzia machoni, akamfuta kamasi puani na kumtoa nta masikioni. Aliulamba uso wa Bi Kizee hadi ukapendeza.

Uso wa Bi Kizee ulimetameta na akamshukuru. 

Alisema, "Humu msituni utapata vitu vingi vya ajabu,  lakini usichukuwe chochote ila tu mzizi utakaoupata."

Mvulana alitamani sana kuviona vitu vyote vya ajabu. Kabla hajaingia msituni, Bi Kizee alimwita, "Hebu, rudi hapa!" "Niko hapa!" mvulana alisema. 

Bi Kizee alimwuliza, "Ulisikia nilichosema? Msituni, utapata vitu vingi vya ajabu, lakini usichukuwe chochote ila tu mzizi utakaoupata."  
Mvulana aliitikia na akakubaliwa kuingia msituni.

Alipoanza kukimbia kwenda msituni, alisikia sauti, "Wewe, rudi hapa!" mvulana hakujua alichotaka yule Bi Kizee. Akarudi. 

Bi Kizee alimwambia, "Sina hakika kama umenielewa. Nimesema, utapata vitu vingi vya ajabau msituni, lakini usichukuwe chochote ila mzizi utakaoupata." Mvulana aliitikia na kisha akakimbilia msituni.

Mara tu alipoingia msituni, aliisikia sauti ya Bi Kizee tena, "Rudi hapa!" mvulana alijaribu kuipuuza, lakini sauti ikaendelea kumwita. 

Bi Kizee akasema, "Sina uhakika utatenda ninavyokwambia. Utapata vitu vingi vya ajabu msituni, lakini usichukuwe chochote ila tu mzizi utakaoupata." Mvulana alianza kuudhika na marudio haya. Alikimbia hadi msituni.

Mle msituni, aliliona bakuli lililojaa fedha tele. Alizichukuwa na kuziweka mfukoni. 

Mara akakumbuka alichoambiwa na Bi Kizee. 

Polepole, alizitoa fedha mfukoni na kuzirejesha kwenye bakuli.

Kisha akatazama karibu naye akaona nguo mpya nzuri. Akavua nguo alizokuwa nazo na kuvaa zile mpya. 

Halafu akakumbuka aliyoambiwa na Bi Kizee. 

Haraka, akazivua zile nguo mpya na kuvaa alizokuwa nazo.

Alipotazama hapo kando, aliuona mzizi! Ulikuwa umenyauka kutokana na jua. 

Akajiuliza, "Bi Kizee atafaidikaje na mzizi huu?" 

Juu ya mzizi, kulikuwa na bakuli la chakula kilichonukia. Mvulana akahisi njaa. Hakuweza kujizuia kukila.

Ghafla, akakumbuka alichoambiwa na yule Bi Kizee! 

Alikumbuka aliambiwa auchukuwe mzizi tu. 

Alianza kuutafuta mzizi, lakini hakuupata.

Akiwa ameudhika, alirudi kumwambia yule Bi Kizee kilichotokea. 

Bi Kizee tayari alikuwa ameenda zake.

------------------------------------------------------------



Mama Koki amekuwa akichuma kabichi wiki nzima. Dona, Maya na Duki humsaidia Mama Koki katika bustani yake kila Jumamosi asubuhi.

Leo watoto hawa watahesabu na kupakia kabichi. Baba Koki atayapeleka masanduku yaliyojaa kabichi sokoni kuuza.

Teksi iliwafikisha watoto kwenye lango la bustani. Waliliona rundo kubwa la kabichi karibu na gari la Baba Koki. 

"Salala! Kabichi nyingi kweli!" Maya alishangaa. "Bila shaka kuna kabichi elfu moja hapo!" Duki alicheka. 

"La! Hasha! Pengine ni mia mbili tu!" Dona alipinga.

Mama Koki alikuwa amewasubiri langoni. "Hamjambo, nimefurahi kuwaona!" Aliwasalimu watoto. 

"Hebu tuanze kazi. Mtahesabu na kuweka kabichi kumi na mbili katika kila sanduku. Nina masanduku 20. Wawili kati yenu watapakia kwenye masanduku 7 kila mmoja. Aliyebaki, atapakia kwenye masanduku 6."

Watoto walilitazama lile rundo la kabichi. Wakajadili njia tofauti za kuzihesabu kabichi hizo. 

"Mimi nitahesabu zangu mbili mbili," Maya akasema. 

"Ninapenda kuhesabu nne nne. Ni haraka," Duki akajibu. 

"Mimi nitazihesabu tatu tatu ili niwe tofauti nanyi!" Dona akawajibu.

Watoto walijaza masanduku yote 20. "Kazi nzuri!" Mama Koki aliwapongeza. "Tazama, kabichi zimezalia. Nguruwe wangu wanazipenda. Hebu tuwagawie," Mama Koki aliamua. 

"Mlipakia jumla ya kabichi ngapi katika masanduku yote? Ni kabichi ngapi zilizalia?" aliwauliza watoto.

Waliandika bei kwenye kila sanduku. Halafu, wakamsaidia Baba Koki kuyapakia kwenye gari. 

Waliweka nusu ya masanduku upande mmoja. Na nusu nyingine upande wa pili ili uzito ulingane.

"Karibu tukamilishe kazi!" Baba Koki alisema. "Hebu tuone ni masanduku mangapi tunahitaji kuweka kila upande."

Muda mfupi baadaye, masanduku yote 20 yalikuwa yamepakiwa kwenye gari. Baba Koki aliondoka kwenda sokoni. 

Aliwaza, "Nikifaulu kuuza masanduku yote, nitapata pesa za kutosha. Nitaweza kuwashangaza watoto kwa kurekebisha zizi la nguruwe!"

Nyumbani, Mama Koki na watoto walinyunyizia mimea maji na kukusanya majani. Kufikia saa sita, wote walikuwa wamechoka. 

Mama Koki aliwaambia, "Ni wakati wa karamu yenu. Je, mnajua nilichowaandalia leo?"

Aliingia ndani kuwaletea alichokuwa amewaandalia. Watoto walisubiri kwa uvumilivu huku wakikisia atakacholeta. 

Aliporejea, waliona mifuko ya aproni yake ikiwa imejaa!

"Hebu tuone ikiwa mlikisia sawa! Nimewatayarishia nini leo?" Mama Koki aliyaweka matofaa mezani. "Nilikisia sawa!" Duki alisema kwa furaha. 

Mama Koki aliwaambia watoto, "Kumbukeni sharti! Gawanya sawa ili kila mmoja apate haki yake. Hakuna anayepata zaidi wala kidogo kuliko mwingine!"

Kwanza, watoto walihesabu matofaa mawili mawili. Walihesabu: 2, 4, 6, 8, 10, 12, 14, 16, na tofaa moja likabaki. Yote pamoja, yalikuwa matofaa 17.

Waligawana matofaa sawasawa yakabaki matofaa mawili. 

Watoto waliyaweka matofaa yao mikobani ili waende nayo nyumbani kwao.

"Hebu tuyakate matofaa mawili yaliyobaki ili tugawane kati yetu," Duki aliwaambia. 

"Kila mmoja wetu atapata vipande vingapi vya tofaa?" Maya aliuliza. 

"Ninajua jibu!" Dona alitabasamu.

Wakati huo, Baba Koki alirejea nyumbani kutoka sokoni. Gari lilikuwa tupu naye alikuwa akitabasamu. 

"Niliuza kabichi zote. Sasa ninaweza kurekebisha zizi la nguruwe. Nitaweza pia kuwanunulia ule mpira wa miguu mliotaka." 

Watoto walishangilia, "Yee!"



------------------------------------------------------------



Watu wa kijiji cha Udongo walikumbwa na matatizo mengi. 

Walihuzunika kwa sababu wanyama pori waliyahatarisha maisha yao.

Wanyama hao waliila mimea yao yote na kuwaiba watoto. 

Mahali hapo hapakuwa pazuri pa kuishi tena. 

Lakini, wangehamia wapi?

Watu wa familia moja walihamia milimani. 

Waliamini kuwa wangepata chakula huko.

Milimani, kulikuwa na vichaka, mapango na miti mingi. 

Walikula sungura na ndege.

Familia zingine ziliona jinsi familia ya milimani ilivyoishi vizuri. 

Mtu mmoja aliwashawishi, "Maisha ya milimani ni mazuri. Nanyi hamieni huku."

Familia zingine zilihamia milimani. 

Ziliishi mapangoni kulikokuwa na joto na usalama.

Watoto wa familia za milimani walizoe kupanda miti kutafuta matunda. 

Walining'inia kwenye matawi kama vile kima hufanya.

Kadri muda ulivyopita, ndivyo familia za milimani zilivyobadilika kimaumbile. Watoto wao walipunguza maongezi yao wakawa wanakoroma zaidi. 

Mapua ya watu wazima yalianza kuwa makubwa na waliota nywele zaidi kwenye miili yao.

Kila walipotazamana, waliona kwamba meno yao yaliendelea kuwa marefu. 

Walianza kutembea kwa miguu minne.

Waligeuka wakawa viumbe wapya wasiokuwa wameonekana pahali pale mbeleni. 

Wakaitwa nyani.

Mwanzoni, nyani hao waliishi kwa furaha. 

Badala ya kula sungura, walianza kuyala mabuu.

Walisahau jinsi ya kutembea wima kama ilivyokuwa awali. 

Wakavua nguo zao kwa sababu miili yao sasa ilikuwa imefunikwa kwa manyoya meusi.

Hata hivyo, walikumbuka kwamba walikuwa watu mbeleni. 

Walipoyaona mapua yao makubwa, walichekana.

Baadaye, walianza kukasirishwa na tabia zao wenyewe. Walipochekana, waliruka juu na chini kwa hasira. 

Vita vilizuka baina ya nyani hao wakalazimika kutawanyika.

Hiyo ndiyo sababu hata leo, nyani huishi katika makundi madogo na wala hawaishi kama taifa la nyani.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, Mungu wa hadithi, alizifungia hadithi zote kwenye sanduku la mbao, huko juu. 

Watu duniani walihuzunika sana kwa kuwa hawakuhadithiana.

Wakamwuliza Buibui Anansi, mwerevu, awasaidie.

Buibui Anansi alisokota utando mrefu unaonata, akautumia kupanda hadi mbinguni. 

"Tafadhali nipe hadithi?" Buibui Anansi alimwambia Mungu wa hadithi. 

Lakini Mungu wa hadithi alimcheka Anansi akisema, "Hadithi hizi ni ghali mno. Wewe buibui mdogo hutaweza kuzilipia."

"Hadithi hugharimu pesa ngapi?" Buibui Anansi aliuliza." 

"Itabidi uniletee wanyama watatu wakali tena wa kipekee. Chui mwenye meno makali kama mkuki, nyigu anayewauma watu, na nyoka anayewameza watu," Mungu wa hadithi alisema.

Alicheka tena. Alidhani kwamba hadithi zake zilikuwa salama.

Buibui Anansi alishuka chini polepole. Aliwaza na kuwazua kisha akapata mpango. 

Alichimba shimo refu, akalifunika kwa matawi na udongo ili lisionekane, halafu, akaenda nyumbani. 

Asubuhi iliyofuata, chui alikuwa ameanguka kwenye lile shimo. Alikuwa akikwaruza kuta za shimo kwa hasira.

"Hebu nikusaidie, rafiki yangu. Lala juu ya vijiti hivi halafu nitakuvuta utoke nje," Buibui Anansi alisema.

Buibui Anansi akautungia utando wake unaonata kwenye mwili wa chui na vijiti. Akamvuta hadi juu kwa Mungu wa hadithi. 

Lakini, Mungu wa hadithi alimcheka akauliza, "Wako wapi nyigu na nyoka?"

Buibui Anansi alirudi tena ardhini kumtafuta mnyama wa pili. Alifikiri hatimaye akapata wazo. Alichukua kibuyu kilichojaa maji na kwenda kwenye mti walimoishi nyigu. 

Akamwagilia nyumba ya nyigu maji mpaka ikalowa kabisa. Kisha akatafuta jani la mgomba akajikinga nalo kichwani. Akajimwagilia maji yaliyobaki kila sehemu ya mwili.

Akawaita nyigu, "Aisee nyigu! Njooni mwone! Mvua inanyesha! Ingieni haraka ndani ya kibuyu changu ili mjikinge na mvua." 

Nyigu hawapendi kulowa maji. Walikimbilia ndani ya kibuyu cha Buibui Anansi.

Kwa kasi, Buibui Anansi aliutungia utando wake kwenye mlango ili nyigu wasitoke kamwe. 

Akawabeba wote hadi juu kwa Mungu wa hadithi. Lakini, Mungu wa hadithi alisema, "Wapi nyoka?" 

Wakati huu hakucheka.

Kwa hivyo, Buibui Anansi alirudi ardhini tena. Alifikiri lakini hakuna wazo zuri lililomjia akilini. 

Basi akamwuliza mkewe aliyekuwa na wazo bora sana. Walishirikiana kutafuta kijiti kimoja kirefu na kamba dhabiti. 

Walipofika karibu na mto alimoishi nyoka, walianza kubishana.

Mmoja alidai kuwa kijiti kile kilikuwa kirefu huku mwingine akisema sivyo. 

Nyoka alitoka majini akawauliza sababu ya mabishano yao. "Mke wangu anasema kwamba kijiti hiki ni kirefu kukuliko wewe. Lakini si kweli," Buibui Anansi alisema. 

"Mimi ni mrefu kuliko kijiti hicho! Hebu kiweka karibu nami nijipime," nyoka alijibu.

Buibui Anansi alifanya hivyo. Alimfunga yule nyoka kwenye kijiti kile kwa kutumia kamba ili kumnyoosha sawasawa. 

Alimbeba hadi juu mbinguni.

Mungu wa hadithi akaridhika na malipo ya Buibui Anansi. 

Akafungua sanduku lake la mbao, akampa Buibui Anansi hadithi. Buibui Anansi alizigawa kwa mkewe, watu pamoja na wanyama.  

Hadithi ni za kuhadithia wala si za kuficha sandukuni.

------------------------------------------------------------



Hebu nikueleze kuhusu mtende.

Mtende ni mmea wa kudumu. Unaweza kusitawi wakati mimea yote mingine imekauka.

Kivuli cha mtende kina upepo mzuri.

Tunakula matunda ya mtende.

Tunatumia majani ya mtende kuezeka nyumba zetu.

Tunatengeneza fagio na kusuka mikeka kwa kutumia majani ya mtende.

Tunatumia nafaka zake kupika.

Sasa umefahamu kwa nini mtende ni muhimu sana?

Maswali: 1. Kweli au sio kweli? A)Mtende unahitaji maji mengi kusitawi. B) Mtende unatoa kivuli kizuri. 2. Jaza nafasi zilizo wazi. A) Tunatumia _____ya mtende kuezeka nyumba zetu. B) Tunasuka ________ kwa kutumia majani ya mtende. 3. Taja jina la aina nyingine ya mti inayosaidia jamii yenu. Eleza sifa zake.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na nyumbu mrembo. 

Aliitwa Waridi.

Farasi mwenye umbo zuri alisema, "Lazima nimwoe Waridi."

Farasi alimwambia Waridi, "Twende mtoni pamoja."

Farasi alimwuliza Waridi kuwa mke wake. 

Waridi alikubali.

Farasi alitaka kumfahamu Waridi zaidi.

Alimwuliza, "Wazazi wako ni nani?"

Waridi alijibu, "Mama yangu anaishi katika ikulu ya mfalme."

"Dada yangu anaishi katika uwanja wa kanisa. Kwani humjui?"

Aliongeza, "Shangazi yangu mrembo anaishi na mzee wa kijiji."

Wakati huo, punda mzee alipita. Alikuwa babake Waridi.

Waridi hakumsalimu babake wala hakumtazama.

Punda yule mzee akauliza, "Kuna nini binti yangu?"

Farasi alimwuliza Waridi, "Huyu punda mjinga ni nani?"

Waridi alimjibu, "Mimi simjui."

Farasi alimpiga teke yule punda mzee.

Punda mzee alivunjika moyo. 

Alilia kisha akafa.

Waridi hakumheshimu babake.

Hii ndiyo sababu nyumbu hawazai watoto.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, familia moja ilikuwa na mti wa matunda matamu yaliyowavutia wengi kutaka kuyaonja. 

Familia hiyo pia ilikuwa na binti mzuri mrembo. Urembo wake na tabia zake nzuri vilisifiwa na watu wengi.

Alipokua mtu mzima, wanaume, vijana kwa wazee, walienda kwao wakiwa na nia ya kumposa. 

Wazazi wa yule msichana walifanya uamuzi. Mwanamume ambaye angeketi pale nyumbani siku nzima bila kula tunda lolote, angeozwa binti wao.

Habari hiyo ilisambaa kijiji kizima. Mtu wa kwanza kufika alikuwa kiongozi wa wakulima wote kijijini. 

Alikuwa tajiri mwenye sura nzuri tena alikuwa angali kijana. Alikaribishwa akaandaliwa matunda. 

Lakini, kabla ya muda kupita, aliyala matunda kisha akaagwa akaenda zake.

Aliyefuata alikuwa kiongozi wa wafugaji. Yeye pia alikuwa tajiri mwenye sura nzuri na alikuwa angali kijana. 

Msichana alipendezwa naye. Lakini alipoandaliwa matunda, aliyala mara moja. 

Yeye pia aliagwa akaenda zake.

Wa tatu alikuwa na mashamba mengi, lakini, jeuri na mwenye sura mbaya. Msichana aliomba Mungu yule mtu ale matunda upesi ili aweze kwenda zake. 

Alipoandaliwa matunda, alikataa kula. Wakati ulipopita, msichana alimwomba ale. Ilipofika saa kumi, alizidiwa na njaa akala. 

Yeye pia aliagwa akaenda zake.

Aliyefuata, alikuwa mzee mwenye sura mbaya, mlaji rushwa asiyekuwa na adabu. Hakupendwa na yeyote kijijini. Msichana alitumaini angekula moja kwa moja na kwenda zake. 

Alipoandaliwa matunda alikataa kula. Ilipofika saa kumi na mbili ya jioni, aliomba kwenda haja. Aliporudi, alinukia matunda huku midomo yake ikiwa na rangi nyekundu! 

Msichana alifarijika mzee alipoagwa na kwenda zake.

Siku chache zilipita kisha mwana wa mfalme, aliyekuwa kijana, tajiri na mwenye sura ya kupendeza, alifika. 

Msichana alimtazama akapendezwa naye mno. Msichana alimpeleka faraghani akamwomba asile matunda. Alimwandalia matunda machache kuliko waliyoandaliwa waliomtangulia. 

Ilipofika adhuhuri, alikuwa amekwisha kula akaagwa. Msichana masikini alilia machozi ya hasira na hasara.

Siku iliyofuata, mkulima masikini na mvivu alifika pale. Alikuwa mwenye sifa ya kubobea maneno ambayo yaliwafurahisha watu.  Akafika akiwa na nia madhubuti kushinda. 

Msichana naye alimwandalia matunda mengi akamwomba ale aende zake. Alikataa kula. Msichana alisubiri kwa hofu. 

Saa sita alikuwa hajala. Ilipofika saa kumi, aliomba maji.

Msichana alimwomba Mungu ale, lakini hilo halikutendeka.

Wazazi wa yule msichana hawakuwa na budi ila kumkubali "yule mvivu." Msichana naye alitamani kunusurika na mtu yule, lakini wazazi hawakuweza kumsaidia. 

Walipokuwa njiani kwenda kwao nyumbani, mkulima alipiga makofi akiimba wimbo mzuri ambao uliwavutia watu waliokuwa barabarani.

Miongoni mwa watu wale walikuwa watumishi wa mwana mfalme. Walimwita mkulima wakamhonga kwa pesa pamoja na ng'ombe mradi akubali kumwacha msichana. 

Bila kusita, akakubali pesa pamoja na ng'ombe akaenda zake peke yake.

Watumishi wale walimvisha msichana libasi murua mno wakampeleka mpaka jumba kubwa la mfalme. 

Muda si mrefu, wazazi wake waliitwa na harusi ikaandaliwa. 

Niliwaacha wakisherehekea nami nikaja kuwahadithieni ninyi.

------------------------------------------------------------



Kitabu hiki kimeandikwa na wanafunzi wa darasa la 6 wa Shule ya Msingi Mwasi Kaskazini, kwenye mkoa wa Kilimanjaro. 

Kimetokana na mijadala mipana kuhusu sifa na changamoto za jamii yetu na nafasi zetu katika kuleta mabadiliko mazuri.

Ninaitwa Norini. Kijiji chetu kina vyakula vya asili kama kiburu, kitawa, kitalolo na soho.

Asili yetu ni Wachaga. Tunapenda lugha yetu ya Kichaga. Ni utambulisho wetu wa asili.

Kusalimia tunasema, 'Kwamza maye' au 'Nangoto maye.'

Naitwa Gilbert Josephu Chacha. Jamii yetu ina Kanisa Katoliki linalopendwa na watu wengi.

Ina mto mkubwa wa Mnambe ambao watalii hupenda kuogelea ndani.

Ina majengo ya asili. Ina kima, ndege na aina nyingi za nyoka kama chatu na wosale.

Ninaitwa Emmanueli Honesti Temba. Kwetu watoto wote wanaenda shule.

Muda mwingine ajira hazipo kwa hiyo elimu huweza kumsaidia mtu kujiajiri mwenyewe na kuwaajiri wengine.

Sisi tunaosoma tunawashauri watoto kudadisi watu kwa kuuliza maswali.

Naitwa Esta Casimir Temba. Ninapenda kijiji changu kwa sababu tunashirikiana katika utawala wa mifereji, barabara na ufundi.

Kijiji chetu kina changamoto kadhaa, kama vile barabara kuporomoka.

Shuleni kwetu kuna ukosefu wa walimu na maktaba wa kujisomea.

Ninaitwa Braytoni Isack Ndanu. Mwasi Kaskazini tuna umeme unaotusaidia kusaga, kukoboa, kuchajisha, na kusikiliza redio. Umeme unazalishwa na maji.

Kuna mitingo inayotumika kama ngoma kwenye shughuli za jamii kama harusi na kutoa buriani.

Naitwa Lidya Gerald Mmbo. Ninapenda kijiji chetu kwa sababu upendo unafanya watu kuwa na umoja na amani.

Changamoto tuliyo nayo ni kukosekana kwa barabara. Mvua zikinyesha, magari hayawezi kupita hivyo inabidi tuweke moramu. Bila moramu ajali zitatokea.

Ninaitwa Magreth Kristofa Mangale. Kijiji chetu kina kanisa linalosaidia watu kusali na kumwomba Mungu kwa makini. 

Zamani watu walikuwa wanatembea mpaka kwenye Mlima Kilimanjaro na kwenda kazini ili Mungu afanikishe kazi za mikono yao.

Ninaitwa Marck Erik Temba. Jamii yetu ina mazao mengi. Kuna ndizi, maparachichi, maembe na mbogamboga. Ardhi yetu ina rutuba.

Jamii yetu inafuga mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kuku. Ni vyakula kwetu. Pia watu huwauza wanyama na kupata fedha.

Ninaitwa Esta Mendadi Temba. Kijiji cha Mwasi kina miti ya matunda inayotupatia afya bora.

Kuna vyakula vya asili kama ndizi za mbala, soho, kiburu. Sisi hupendelea vyakula hivyo sana. Kokora maye!

Ninaitwa Cathbert Joseph Njau. Kijiji chetu kina kanisa kubwa na nzuri. Wananchi walishirikiana kulijenga.

Pia kina mifugo wengi.

Changamoto ni ukosefu wa hospitali na zahanati. Mgonjwa afikapo hospitali jirani, unakuta ameshazidiwa.

Ninaitwa Maurini Frank Njau. Kijiji cha Mwasi kina shule. Wanafunzi wa Mwasi ni wasikivu, watiifu na wana nidhamu.

Changamoto ni vijana wa Mwasi wanajishughulisha na ulevi. Ninawashauri wasiwe walevi. Ulevi unasababisha madhara ya mwili.

Ninaitwa Bensoni Fredi Njau. Kijiji chetu kimebarikiwa na amani na uelewano. Kimebarikiwa na vitu vingi kama mifugo, vyakula, matunda na vyumba vya asili.

Kijiji chetu kina uhaba wa walimu wa kufundisha na mapadre wa kuhubiri dini.

Mimi ninaitwa Sofia Florian Mushi. Kijiji chetu kina sifa ya maji. Pia kina upendo. Wageni wakija kijijini kwetu tunawakaribisha kwa upendo mkubwa sana.

Changamoto ni kwamba ulevi umezidi sana. Tunajitahidi sana kuepuka tabia ya ulevi.

Ninaitwa Brighton Felix Temba. Mwasi Kaskazini kuna ushirikiano unaotokea pale mtu anapofiwa, wanakijiji wanamchangia.

Tulishirikiana kuchimba mfereji wa kuanzia Ngoma na kuishia Mamboleo. Tuna changamoto ya kukosa maktaba.

Ninaitwa Robisoni Raimondi Njau. Kijijini kwetu kuna rasilimali ya maji. Kuna ardhi yenye rutuba.

Tumebarikiwa na wachapakazi wengi.

Kuna changamoto ya wezi wanaoiba kuku, mbuzi na ndizi.

Katika kijiji chetu tunashirikiana kuchimba visima vya maji na kuboresha mabomba ya maji na visima.

Kuna vyakula vya asili kama mbande, ndizi na soho.

Kuna changamoto ya watu kulewa sana na kuanza matusi.

Ninaitwa Chirispin Joseph Materu. Mwasi kwetu tunatumia pikipiki, bajaji na magari kusafirisha watu na mizigo.

Kuna changamoto ya usafi wa mazingira.

Ninaitwa Clemensi Hilimerdi Njau. Tunafurahia sana kuwa na maji ya kutosha.

Wengine wanachafua mifereji kwa kukojoa hapo na kuchafua kwa kutupa taka ovyo.

Ninaitwa Ovino Gaspari Temba. 

Kijiji chetu kinajivunia kuwa na wachapakazi wengi wanaoshirikiana katika kazi za jamii.

Naitwa Glory Prosper Ngowi. Tuna shule nyingi katika jamii yetu. Zamani hatukuwa na shule. Tunapenda kusikiliza wanachotufundisha walimu.

Tunakuwa na changamoto wakati mabomba yanakauka na kutulazimisha kwenda mbali kuchota maji.

Ninaitwa Emmanueli Antoni Lyimo. Kijijini kwetu watu wengi hupenda kuongea Kichaga. Tunapenda lugha yetu.

Kuna changamoto ya uwizi wa mazao. Watu waliootesha wanaanza kukata tamaa ya kuendelea kufanya kazi yao.

Ninaitwa Evansi Danieli Lyimo. Mwasi kwetu watu hufanya kazi bila uvivu na kwa ushirikiano mzuri. Tunapendana na majirani wanaotuzunguka katika jamii.

Kuna ukosefu wa nyumba na kuna watu maskini ambao hawana nguvu, viatu, na nyumba.

Ninaitwa Glory Gasper Lugwisha. Kijiji chetu kina wakulima, wa mahindi, maharagwe, mihogo na mpunga.

Tuna changamoto ya wizi.

Ninaitwa Eladius Florian Temba. Zamani shule iliyokuwepo ilianzia darasa la 1 hadi la 4. Ukifaulu Waingereza wanakusomesha zaidi. Kulikuwa na Middle School kwa watu wenye fedha.

Sasa kijijini kwetu kuna shule nyingi na watoto wote husoma.

Ninaitwa Dismas Liberati Temba. Mwasi kwetu watu wanafuga bata, mbuzi, ng'ombe, kondoo, kuku na kanga. 

Hata mimi ninafuga sungura.

Kuna changamoto ya wizi. Wtu wanaiba hadi nguo kwenye kamba. Ukifua nguo hautaondoka nyumbani hadi zikauke.

Kwa majina naitwa Brighton Gerald Mmbo. Rasilimali zinazopatikana Mwasi ni maji, mifugo, mabonde, mito na milima.

Umoja na ushirikiano unapatikana katika misiba, sherehe, mavuno na kilimo.

Changamoto ni ukosefu wa vitabu vya kujisomea.

------------------------------------------------------------



Khalai ni msichana mwenye umri wa miaka saba. 

Katika jamii yake, jina lake lina maana sawa na 'aliye mzuri'.

Khalai anaamka na kuuzungumzia mmea mchanga wa Mchungwa.

Anasema, "Tafadhali Mchungwa, kua mkubwa uzae machungwa mengi mabivu."

Khalai anapokuwa njiani kwenda shuleni, anazizungumzia Nyasi. 

Anasema, "Tafadhali Nyasi, zidi kuwa kijani kibichi na wala usinyauke."

Khalai anayapita Maua ya kichakani

Anasema, "Tafadhali Maua, endelea kunawiri ili nikutumie kuzirembesha nywele zangu."

Anapokuwa shuleni, Khalai anauzungumzia Mti ulioko pale shuleni.

"Tafadhali Mti, yazae matawi makubwa ili tuweze kusomea chini ya kivuli chako."

Khalai anauzungumzia Ua unaoizingira shule yake.

"Tafadhali Ua, kua uwe mwenye nguvu ili uilinde shule yetu dhidi ya watu wabaya."

Anaporudi nyumbani alasiri, Khalai anautembelea mti wa mchungwa kutazama ikiwa machungwa yameiva.

"Machungwa bado mabichi," Khalai anashusha pumzi. 

"Nitakutembelea kesho, Mchungwa wee! Labda utanipa chungwa mbivu wakati huo."

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kuliishi msichana mmoja katika kijiji kilichoitwa Nchijua. 

Msichana huyo aliitwa Aku. Alikuwa msichana mwenye miguu mirefu mno.

Aku alistaajabishwa na mambo mengi.

Babake Aku aliitwa Juma na alikuwa mvuvi. Wakati mwingine, Juma alienda na Aku kuvua samaki. 

Alipofanya hivyo, Aku alistaajabu kwa nini kila mara jua lilimtazama kutoka juu angani. 

Mara nyingine Aku alimsaidia mamake, Agatha, kupika. Alipofanya hivyo, alistaajabu kwa nini mafuta yalikuwa rangi nyekundu yalipokuwa kwenye kibuyu lakini kuwa manjano yakiwa kwenye viazi vikuu.

Pia, Aku alistaajabu kwa nini Oti, kakake, na wavulana wengine hawakumruhusu acheze nao mpira wa miguu. 

Aku alipowauliza kwa nini, walicheka kisha wakamwambia aende acheze na wasichana wenzake. 

Wasichana nao hawakutaka kucheza naye. "Miguu yako ni mirefu sana," walimwambia Aku kila mara.

Aku alifanya urafiki na Jua. Alitazamia kuliona Jua kila alipoamka asubuhi. Jogoo walipowika kutangaza mawio, Aku alichezea juani huku kivuli chake kikicheza naye. 

Kuimba kwa ndege na kuwika kwa jogoo ilikuwa muziki mtamu kwake. Jua lilimfurahisha na kumfanya atabasamu.

Lakini siku moja, Jua halikuchomoza.

Aku alisubiri jogoo kuwika, lakini, hawakufanya hivyo. Ndege hawakuimba. Bila Jua, watu wa Nchijua hawakutekeleza majukumu yao ya kila siku. 

Wakulima hawakukuza mimea yao. Anga liligeuka kijivu likahuzunika. Juma hakwenda kuvua samaki. Watoto hawakwenda shuleni. Wanawake hawakujadiliana bei za bidhaa sokoni. 

Aku alivikosa vitu hivyo vyote. Alikosa kuwika kwa jogoo na nyimbo walizoimba ndege. Alichokikosa zaidi, ni kuchomoza kwa Jua.

Kila mmoja alitaka kujua Jua lilienda wapi. "Labda Jua limefariki," baadhi yao walisema. "Jua limesafiri," wengine wakasema. Wengine walimcheka  Aku. 

Hata hivyo, Aku alijipa moyo, "Ninasema ukweli. Jua ni rafiki yangu. Jua halijafariki." 

Lakini, hakuna yeyote aliyemsikiliza zaidi. Walisahau Jua wakamcheka Aku kwa nguvu. Kilichomhuzunisha zaidi ni kule kuchekwa na watoto wenzake.

Akiwa amehuzunika kama vile Jua lilivyokuwa, Aku alifanya hima akaenda nyumbani. Aliugonga mpira wa kakake kimakosa. Mpira uliviringika na kuingia jikoni. 

Mpira ulikigonga kibuyu cha mafuta kilichokuwa jikoni kikaanguka chini. Mafuta yalimwagika nao mpira ukaloa.

Oti na rafikiye mmoja waliingia jikoni kuuchukua mpira wao. Walikiona kibuyu kilichokuwa kimeanguka na mafuta yaliyomwagika. Mpira wao ulikuwa umeloa. 

Oti, Agatha na watu wote wa Nchijua walimtazama Aku akitoroka. Walistaajabu wasijue alichopanga kuufanyia mpira ulioloa mafuta.

Aku alisimama alipofika katikati ya uwanja. Akauweka mpira chini na kwa nguvu zote, akaugonga kwa mmoja wa miguu yake mirefu. 

Mpira ukazunguka chini ukaelekea mwishwo wa uwanja. Ukaugonga mizizi ya mtende mmoja uliokuwa mwisho wa uwanja.

Mpira huo ulielekea angani. Wakiwa vinywa wazi, watu wa Nchijua waliutazama mpira ukiruka mbali na mawingu, mbali na upeo wa macho yao. Kila kitu kikatulia. Kukawa na kimya kikubwa. 

Ghafla, anga lilifunguka. Mawingu yakawa kama pamba nyororo. Mpira mkubwa ukapenyezea nyuma ya mawingu. 

Mpira huo uliokuwa mwekundu na manjano kama mafuta, ukang'aa. Mpira huo ulikuwa Jua, rafikiye Aku. Kila kitu kilisisimuka. Kimya kikamalizika.

Kila mtu alifanya hima kwenda nyumbani kujitayarisha kwa shughuli za kawaida. 

Juma alitafuta ndoo yake ya samaki. Wakulima waliyachukua majembe yao. Watoto walioga na kuvaa tayari kwenda shuleni. 

Wanawake walijifunga kanga zao. Walibeba vikapu wakaenda haraka sokoni.

Jua lilirejea Nchijua. 

Aku alikuwa amefaulu. 

Siku mpya ilianza…

------------------------------------------------------------



Fisi mlafi aliishi katika kijiji cha Mkosi.

Katika kijiji jirani, aliishi Kobe mwoga. 

Fisi na Kobe walikuwa marafiki.

Fisi alisikia kwamba kulikuwa na nyuki waliotengeneza asali tamu kuliko yote. Nyuki hao walisafiri mbali na mizinga yao mara moja kwa mwaka. 

"Lazima tuipate ile asali nyuki watakapokuwa safarini," Fisi alimwambia Kobe.

Ingawa Kobe aliogopa kwenda, hakuwa na ujasiri wa kukataa. 

Asubuhi iliyofuata, Fisi na Kobe walianza safari yao. Fisi alienda kwa kasi huku Kobe akijikokota nyuma kwa woga.

Walipanda milima wakashuka kisha wakavuka mabonde. 

Waliuvuka mto mkubwa wakaendelea na safari yao wakiwa na nia ya kuifikia ile mizinga ya nyuki.

Hatimaye, waliona mizinga ya nyuki milimani kwenye miti. Fisi alikwenda kwa haraka. 

Kobe alikuwa tayari kuzirai kutokana na njaa na uchovu.

Fisi alipoufikia mzinga mkubwa zaidi, alimwambia Kobe, "Haraka! Panda juu ya mti uuangushe mzinga chini."

Kobe aling'ang'ana kuupanda mti. Alipofanya hivyo, aliangalia chini mara kwa mara asije akaanguka. 

Fisi alikasirishwa na kitendo hicho akaanza kumpigia Kobe kelele.

Kobe alipougusa mzinga, alisikia sauti ya nyuki. Kumbe walikuwa bado ndani ya mzinga wao! 

Kobe alishtuka akaanguka chini.

Mzinga wa nyuki ulimwangukia Kobe akafunikwa na kufichwa na asali! 

Fisi alianza kuilamba ile asali. Lakini nyuki hawakufurahia kitendo hicho.

Nyuki walimuuma Fisi kila sehemu ya mwili akaamua kukimbilia usalama wake. 

Hata hivyo, nyuki walimfuata wakaendelea kumuuma.

Fisi aliteremka kutoka mlimani, akavuka mto na bonde. 

Nyuki waliendelea kumuuma wakati huo wote.

Kobe naye alikuwa bado chini ya mzinga mkubwa. Hatimaye, kila kitu kilikuwa kimya. 

Kobe aligundua kuwa mzinga na asali vilikuwa vimekaukia mgongoni kwake.

Kobe alitambua kuwa hakuhitaji tena kujificha kichakani. 

Gamba jipya alilopata lingeweza kumkinga na hatari yoyote.

Fisi alikuwa amechoka na alijaa vidonda mwilini. Alizirai kabla kufika nyumbani. 

Alipoamka, aligundua kwamba mishale ya nyuki ilisababisha madoadoa kwenye ngozi yake.

Hivi ndivyo kobe alivyopata gamba lake ngumu naye fisi akapata madoadoa kwenye ngozi yake. 

Urafiki kati ya fisi na kobe uliisha.

------------------------------------------------------------



Katika msitu wa Miwa, aliishi Kima mwenye huzuni. 

Kila alipozaa mtoto, aliaga dunia.

Uchungu wa kuwapoteza watoto ulimfanya Kima kuruka juu na chini. 

Angeruka kutoka tawi moja hadi nyingine huku akilia, "Kwi! Kwi! Kwi!"

Alihuzunika zaidi alipowaona kima wengine wakiwa na watoto wao.

Kima huyo alizoea kuketi juu ya tawi na ktazama juu! 

Siku zilivyopita, ndivyo Kima alilia zaidi na zaidi.

Baadaye, alimzaa mtoto mwingine. 

Aliamua kumpeleka njiani ili watu wote waliopita wamwone na kumtakia heri.

Siku moja, Kima alishuka kutoka mtini na kumweka mtoto wake njiani. 

Wakati huo, mwindaji mmoja alikuwa akirudi nyumbani. Alimwona mtoto wa Kima akilala kando ya njia.

Mwindaji huyo alimbeba mtoto wa Kima na kumpeleka nyumbani kwake. 

Alipofika, kila mmoja wa wanawe watatu alitaka kumbeba mtoto wa Kima.

Walicheza na kuimba: 

Mtupe juu! 
Mtupe chini! 
Nitupie mimi! 
Mtupie yeye! 

Walimtupa mtoto wa Kima kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine.

Walipokuwa wakicheza na mtoto wa Kima, mama Kima alijificha mtini na kuwatzama. 

Alihofia kwamba mwanawe angekufa kama vile wale wengine walivyokufa.

Mke wa mwindaji aliwaona wanawe wakicheza na yule mtoto wa Kima. 

Akasema, "Tahadharini wanangu! Hebu mleteni hapa. Mtamwangusha!"

Alimshika mtoto wa Kima na kumbariki.

Kisha mke wa mwindaji alimweka mtoto wa Kima chini. 

Mama Kima alimbeba mtoto wake kifuani akatowekea mtini. 

Hakumpoteza tena mtoto mwingine!

------------------------------------------------------------



Tanzania ni nchi ya amani na upendo. Ina makabila zaidi ya mia ishirini na nane. 

Moja ya makabila ni Maasai ambalo ni maarufu kwa ufugaji na mavazi yao.

Kuna mbuga mbalimbali Tanzania kama vile Serengeti, Manyara, Mikumi, Saadani, Ruaha na nyingine nyingi. 

Watalii wengi huvutiwa kuja kutalii.

Nchi ya Tanzania ina mito na bahari nyingi sana ambamo watu wengi na hata watoto hupenda kuogelea. Mto Ruaha ni moja ya mito mikubwa Tanzania. 

Lakini, yapaswa watu kuwa waangalifu kwani mito mingine ni hatari kwa sababu kuna wanyama hatari kama mamba na viboko.

Wanyama mbalimbali wanapatikana katika nchi hii nzuri. Wanyama hawa ni kama simba, tembo, nyati, swala, pundamilia, chui, fisi na wengineo. 

Hata ndege mbalimbali hupatikana katika nchi hii iliyobarikiwa.

Watu wa makabila na dini mbalimbali, huishi pamoja kwa amani na upendo. 

Hakuna dini, ukabila, wala ubaguzi wa aina yoyote. Ukifika Tanzania, jua umefika nyumbani.

Watu wa Tanzania ni wakarimu sana hata kwa wageni. Upendo na ukarimu ndio jadi yetu. 

Ukarimu, uzalendo na upendo vinaifanya Tanzania iwe nchi yenye nuru sana.

Mlima mrefu katika bara la Afrika, Mlima Kilimanjaro, hupatikana nchini Tanzania. Tunajivunia kuwa na mlima mrefu zaidi Afrika. 

Pia, kuna milima mingi sana nchini humu na viziwa tele hasa Zanzibar.

Biashara, uwekezaji, uvuvi, kilimo, uchimbaji madini na utalii ni mojawapo ya shughuli mbalimbali za kufanya nchini Tanzania. 

Utalii una mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu. Watanzania wengi pia hujishughulisha na biashara.

Raisi wa Tanzania ni Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Huyu ndiye mwanamke wa kwanza kuongoza kama Raisi katika nchi ya Tanzania. 

Watoto wote wanatakiwa kusoma kwa bidii ili wapate viongozi waadilifu wengi na mabolozi wazuri wa nchi yetu. Kwani nchi yetu ina utajiri mwingi tena wa asili.

Nchi yetu inavutia, ni yenye nuru na tunu kubwa kwa Watanzania. Wanawake na wanaume wote wana wajibu katika nchi hii. 

Wanawake wanaweza, kwa hivyo sote tuendelee  kuchapa kazi kwa bidii. Tuna mchango mkubwa sana kwa nchi hii. Sote tunatakiwa kuilinda nchi yetu na kuwa wazalendo kwa ajili ya leo na kesho yetu sote.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki watanzania

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, Tembo na Sungura walikuwa marafiki wakubwa sana. 

Walikuwa na ngamia, ng'ombe na kondoo wengi.

Waliwalisha wanyama hao katika bonde la Kingilo. 

Wakati mwingine waliwapeleka milimani kulikokuwa na nyasi na maji kwa wingi.

Wanyama walipokula, Sungura na Tembo walicheza. 

Walipenda sana kucheza mpira wa miguu.

Kila walipocheza, Tembo aliingiza goli nyingi kumliko Sungura. 

Sungura alikasirishwa mno na hali hiyo.

Siku moja Sungura alimwuliza Tembo, "Ni nini kinachokuwezesha kuwa mwingizaji goli maarufu?" 

Tembo alimjibu, "Ni miguu yangu minono."

Siku iliyofuata, Sungura alipendekeza wawe na mashindano ya mbio. 

Tembo alikubali na wakaanza mbio.

Sungura alishinda mbio zote. Tembo alikasirika. Hakuwahi kushindwa. 

Alimwuliza Sungura, "Ni nini kinachokuwezesha kuwa mkimbiaji maarufu?"  

Sungura alijibu, "Ni miguu yangu myembamba."

Tembo alimwuliza, "Nitawezaje kupata miguu myembamba?" 

Sungura akamjibu, "Ni rahisi, nitakuonyesha. Tafuta kuni ukakoke moto."

Tembo alizikusanya kuni akakoka moto mkubwa. Sungura akamwambia, "Sasa iweke miguu yako ndani ya moto." 

Tembo alifanya hivyo. Alipiga kelele, "Ninaungua! Ninaungua!"

Sungura alifurahi. Alimhimiza Tembo aendelea hivyo hivyo. 

Alisema kuwa hivyo tu ndivyo miguu yake ingekuwa myembamba.

Miguu ya Tembo ilijeruhiwa vibaya akaondoka motoni. 

Hakuweza kusimama kwa hivyo alilala chini.

Tembo aliketi kwa siku nyingi kabla kuweza kusimama.

Hatimaye, aliweza kuchechemea na kwenda nyumbani kwa familia yake.

Sungura alimwomba Tembo msamaha. 

Hata hivyo, urafiki kati ya Tembo na Sungura uliisha.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na mbuzi aliyeitwa Ibego.
Ibego alikuwa mfalme wa mifugo na ndege. Aliishi maisha mazuri. 

Siku moja, Ibego aliwaita mifugo wote na ndege mkutanoni.

"Rafiki zangu, nimewaita kwa sababu niliota ndoto," Ibego alisema. 

Mifugo wote na ndege walimsikiliza mfalme wao kwa makini.

"Niliota kuwa kulikuwa na njaa na ukosefu wa maji katika nchi yetu. Wengi wa jamaa zetu walifariki!" Mfalme alisema. 

Mifugo na ndege waliposikia ndoto ile, walijawa na hofu. "Tutafanyaje?" Paka aliuliza.

Kuku na Bata walikuwa na wazo. Walisema, "Kila mmoja wetu alete chakula kiwekwe katika hifadhi ya mfalme." 

Mifugo wote na ndege walikubaliana na wazo hilo.

Mfalme alitoa sharti moja. Alisema, "Yeyote atakayekosa kuleta chakula, mtamfunga mumlete kwangu."

Wakati wa mfalme Mbuzi kustaafu ulifika. Mifugo wote na ndege walikutana kumchagua mfalme mpya. 

Paka alichaguliwa kuwa mfalme wao mpya.

Mbuzi hakumtambua Paka kama mfalme. 

Alisema, "Mimi ndiye mfalme na hakuna mwingine. Siwezi kumtii mwingine yeyote."

Mifugo walipeleka chakula katika hifadhi ya mfalme wao mpya. Mbuzi hakupeleka chochote. 

Ng'ombe alisema, "Mbuzi alipokuwa mfalme, tulimtii. Hataki sasa kumtii mfalme wetu mpya. Tufanyeje?"

Mifugo wote na ndege walikasirika. "Kwani anadhani yeye ni tofauti nasi?" 

Walinung'unika.

Mbwa alisema, "Nilimsaidia alipokuwa mfalme. Sikuwa nikilala usiku. Kila wakati nilikuwa naye, tayari kumsaidia."

Kondoo alisema, "Nilimpatia sufu yangu ili awafunike wanawe."

Nguruwe naye alisema, "Alipokuwa mfalme, aliwaambia marafiki zake kuwa mimi ni mlafi. Lakini nilitumia muda mwingi kuitunza bustani yake na kupalilia mawele na mahindi."

Kondoo aliuliza, "Eti alisema nini? Kwamba wewe ni mlafi? Alifikiri kuwa atakuwa mfalme milele?

Lazima afahamu kuwa yeye si mfalme tena. Hata sijui kwa nini anafikiri kuwa yeye ni muhimu sana."

Mifugo wote walicheka na kukubaliana kwamba lazima Mbuzi apeleke chakula kwa mfalme mpya. 

Mfalme Paka alimwamuru Mbuzi aende kwake.

Mifugo walipoenda, walimkuta Mbuzi akistarehe. 

"Siendi kwa Paka. Hakuna mfalme mwingine ila mimi. Ukiwa mfalme, unasalia mflame," Mbuzi alisema kwa kiburi.

"Basi tutakufunga kwa kamba tukupeleke kwa mfalme mpya," Kondoo alisema.

Ng'ombe alimfunga Mbuzi akamvuta na kumpeleka kwa mfalme. 

Kondoo, Bata, Mbwa, Nguruwe na Jogoo walimshangilia Ng'ombe wakisema, "Mpeleke huyu mbuzi kaidi kwa mfalme mpya!"

Tangu wakati huo, kila mbuzi hukataa kusonga anapovutwa. 

Hufikiri kuwa anapelekwa kwenye mahakama ya mfalme.

------------------------------------------------------------



Chura na Nyoka walikuwa marafiki.

"Njoo twende tukamtembelee mamangu." Chura alimwalika Nyoka.

"Asante, lakini nani atatuchungia makao yetu?" Nyoka alimwuliza Chura.

"Nitawachungia makao yenu," Kima alijitolea.

Chura aliweka mchwa mkobani kumpelekea mamake.

Chura na Nyoka waliondoka asubuhi wakaingia msituni.

Waliwakuta vichakuro. Nyoka aliwaogopa.

Chura alimlinda rafiki yake Nyoka.

Walipofika kwa mamake Chura, walikuwa wakihisi njaa sana.

Walinawa wakajitayarisha kwa chakula.

"Nyoka, tafadhali keti wima." Chura alimwambia rafikiye.

Nyoka alijaribu kuketi wima, lakini hakuweza. Yeye si kama chura.

"Siwezi kuketi wima kama chura," Nyoka alimjibu.

Chura hakumsikiza Nyoka. Alianza kukasirika.

Nyoka pia alikasirika akasema, "Hunielewi. Heri nirudi nyumbani."

Nyoka aliondoka kwa hasira. "Nilidhani Chura ni rafiki yangu." Aliwaza.

------------------------------------------------------------



Mtaa wetu ulikuwa na matatizo mengi. 

Tulisimama kwenye foleni tukisubiri kuchota maji kutoka mfereji mmoja.

Tulisubiri kupokea chakula cha msaada. 

Hatukufahamu waliokuwa wahisani wetu.

Usalama ulizorota kila uchao. 

Tulilazimika kufunga milango yetu mapema kwa ajili ya wizi.

Baadhi ya watoto waliacha shule. 

Wazazi wao hawakuweza kulipa karo.

Wasichana wadogo walifanya kazi za nyumbani pale mtaani.

Wavulana wadogo walirandaranda ovyo.

Wengine waliwafanyia watu kazi mashambani.

Upepo ulivuma na kuzipeperusha karatasi chafu. 

Ziliangikwa mitini na uani na kuyachafua mazingira.

Vipande vya chupa vilitupwa ovyo ovyo njiani. 

Watu walijeruhiwa kwa kukatwa navyo.

Siku moja, mfereji wa maji ulikauka na mitungi yetu ikawa tupu. 

Tulijiuliza, "Sasa tutayapata maji wapi?"

Babangu alitembea kutoka nyumba hadi nyumba. 

Aliwatangazia watu kuhudhuria mkutano wa mtaa.

Watu walikusanyika chini ya mti ule ule ambako tulipokea chakula cha msaada. 

Baadhi waliuliza, "Kuna nini leo?"

Babangu alisimama katikati yao akasema, "Lazima tuyabadilishe maisha ya mtaa wetu."

Juma alikuwa amepanda juu ya mti.

Alisema kwa sauti, "Naweza kusafisha uwanja wa nyumba zetu."

Mwanamke mmoja wa makamo, alisema, "Sisi wanawake tutaungana pamoja tupande mbegu ili tupate chakula."

Mwanamume mwingine alisimama akasema,  "Wanaume nao watachimba kisima cha maji."

Sote tulisema kwa sauti moja, "Lazima tubadilishe maisha yetu." 

Hivyo ndivyo, tulianza kufanya kazi pamoja kuyabadilisha maisha yetu.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale kulikuwa na sayari jua saba angani. 

Miale mikali ya sayari jua hizo iling'aa duniani hadi binadamu wakashindwa kuvumilia.

Ndugu saba wa kabila la Munda waliamua kuziua sayari jua hizo. 

Walizirushia mishale lakini wakaweza kuziua sayari jua sita pekee.

Sayari Jua ya saba ilikuwa imejificha nyuma ya mlima.

Baada ya sayari jua sita kuuawa, giza lilitanda kila mahali. 

Kwa sababu hiyo, paa hangeweza kumwona chui. Tembo walijikwaa kwenye miti na sungura wakatembea kwenye hatari ya simba. 

Wanyama wote walitaabika.

Wanyama wote walikutana kutatua shida hii. 

Sungura alisema kwamba Sayari Jua ya saba ilikuwa imejificha nyuma ya mlima. 

Wnayama walijiuliza, "Ni nani atakayeiita Sayari Jua hiyo irudi?"

"Nitaiita irudi," alisema Simba, mfalme wa msitu huo. "Jua, jua, tafadhali usitutoroke. Rudi utuangazie." 

Simba alinguruma. Lakini, Sayari Jua ilikataa kumsikiliza.

Tembo naye akajaribu kuiita Sayari jua. Aliuinua mkonga wake na kupaaza sauti, "Jua, jua tafadhali rudi." 

Lakini, Sayari Jua ilikataa kumsikiliza pia.

Tausi Mrembo alicheza densi kidogo na kisha akajaribu kuiita Sayari Jua, "Jua, jua, tafadhali rudi." Sayari jua ilikataa kujitokeza. Wanyama wote waliita, lakini, Sayari Jua haikumsikiza yeyote. 

Jogoo alipojitokeza kuiita Sayari Jua, kila mmoja alimcheka. Simba, kama kiongozi mzuri, alisema, "Tumpeni Jogoo nafasi ajaribu kuiita Sayari Jua."

Jogoo alisimama mbele ya wanyama wote, na taratibu akawika, "Kookoorikoo! Kookoorikoo!" 

Mara Sayari Jua ikaanza kuchomoza kutoka nyuma ya mlima. 

Wanyama wote walishangaa.

Jogoo akawika tena kwa nguvu zaidi, "Kookoorikoo!" Sayari Jua ikachomoza hata zaidi. 

Jogoo akawika kwa mara ya tatu, "Kookoorikoo!" Sayari Jua ikapanda juu zaidi na kung'aa. Kukawa na mwangaza kila mahali. 

Wanyama wote na binadamu wakafurahi kuuona mwangaza.

Wanyama waliwaomba binadamu wasiiue Sayari Jua. 

Tangu siku hiyo, jogoo huwika kila asubuhi. Nayo Sayari Jua isikiapo sauti ya jogoo, huchomoza na kuangaza dunia yote.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palitokea mwanamke aliyekuwa amebeba kikapu mawele kikapuni. 

Pia, alikuwa na fimbo yake kubwa.

Siku moja Sungura alikuwa na njaa sana. Hakuwa na chakula wala shamba. Alikuwa amekonda sana.  

Sungura huyo alikuwa mvivu. Hakuweza kulima, hakuweza kupanda mimea, hakuweza kupalilia. Sungura alitaka chakula, lakini, hakujua afanyeje.

Ilibidi akaenda kwa mwanamke akamwambia, "Mimi nina shamba kubwa la mawele." Kumbe Sungura ni mjanja. 

Alienda kwenye shamba la wenyewe kisha akamwambia mwanamke, "Hili ndilo shamba langu."

Yule mwanamke akachuma mawele yale ya wenyewe. 

Sungura akamuona mwenye shamba la mawele anakuja. Akakimbia na kumuacha huyo mwanamke.

Yule mwanamke hakumuona mwenye shamba akija. Alipofika, alimwuliza, "Nani kakuruhusu uchume mawele yangu?" 

Mwanamke akamjibu, "Sungura ameniambia ni shamba lake na akaniambia nichume mawele yake."

Mwenye shamba akamwuliza, "Huyo sungura yuko wapi?" 

Mwanamke akamwambia, "Alikuwa amejificha hapa. Sasa yuko wapi?" 

Wakamtafuta Sungura bila kufanikiwa kumpata.

Ndio mpaka leo sungura na mwanadamu hawapatani.

------------------------------------------------------------



Kijiji chetu kiko katikati ya mbuga ya wanyama. Wanyama pori huvamia mifugo wetu mara kwa mara. 

Wakati wa kiangazi, wanyama pori kama fisi na simba huja vijijini mwetu. Huvamia mifugo wetu zizini. 

Uvamizi huu huleta hasara kubwa.

Wakati mwingine uvamizi huo huleta maafa au majeraha.

Siku moja, simba alivamia zizi letu usiku na kuwaua mbuzi watatu. 

Babangu aliamshwa na kelele za mbwa wetu. Kwa hasira, akachukua mkuki wake kwenda kuokoa mifugo wake.

Hakuamini mifugo aliotarajia kuuza ili kupata karo yangu, walikuwa wameuawa. Simba ni mnyama mkali na hatari.

Kabla babangu kukabiliana na huyo adui, nikamwita. "Baba, ninakusihi kabla ya kumshambulia simba naomba unisikize."

Nikaomba baba kutomuua simba bali atumie njia mbadala ya kumfukuza. Njia moja ni kama kutumia sauti au mwangaza kuwazuia. 

Wanyama pori wana faida na wanapouliwa, hunyima nchi fedha ambazo hutokana na utalii.

Baba alinisikiza na akamshtua yule simba kwa kutumia mwangaza na sauti.

Siku iliyofuata, akaenda kuripoti uvamizi huo kwa walinda pori. 

Baadaye, akalipwa fidia kutokana na hasara ya uvamizi. Akatumia fedha hizo kujenga ua bora zizini.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Kuku na Tai walikuwa marafiki. Siku moja, Tai alimkuta Kuku akiwa anapumzika chini ya mti. Alikuwa amesimamia mguu mmoja pekee.

Tai alimwuliza Kuku, "Mguu wako mwingine uko wapi?"

Kuku alimweleza Tai, "Mwenye duka aliukata na badala yake akanipatia vitu hivi."

Tai alimwuliza Kuku ikiwa yeye pia angeweza kufanya  hivyo. Vilevile alitaka mfuko uliojaa vitu. Kuku alikubali.

Tai alimwendea mwenye duka akitaka aukate mguu wake mmoja na badala yake ampatie vitu vitamu. Mwenye duka alikubali akafanya hivyo.

Tai aliruka ruka kwa mguu mmoja akielekea nyumbani. Hata hivyo, alivifurahia vitu alivopewa na mwenye duka.

Tai alipofika nyumbani, alimkuta Kuku akiwa na miguu yake miwili.

Tai alikasirika sana akaanza kumfukuza Kuku. Lakini hakuweza kumshika. Hiyo ndiyo sababu Tai huwashambulia vifaranga wa Kuku kila mara. Anapomshika mmoja, yeye humla.

------------------------------------------------------------



Mawazo yangu ni kama ufunguo unaofungua kila mlango!

Katika mawazo yangu, mwavuli wangu una mipini miwili ili niweze kuushikilia na dada yangu.

Katika mawazo yangu, kuna nyuki shujaa.

Nyuki shujaa, wanaoruka majini kwa urahisi...

... kama wanavyoruka angani!

Katika mawazo yangu, naona maua humea katika viatu na kuimba.

Katika mawazo yangu, kila mtoto hula aiskrimu wakati wa chakula cha jioni...

...na kisha hulala maua yanapouimbia mwezi wa rangi ya kizambarau.

------------------------------------------------------------



Ni kipi kizito zaidi? 

Kuku au unyoya?

Ni kipi chepesi zaidi? 

Ua au hindi?

Mtoto yupi ni mzito zaidi?

Ni nani mzito zaidi, ndovu au baba?

Ni kipi kizito zaidi, kilo moja ya mawe?

Au gramu moja ya saruji?

Ni kipi kizito zaidi? 

Kilo moja ya sukari?

Au kilo moja ya manyoya?

------------------------------------------------------------



Kuliishi mapacha wawili wa kiume, Tembo na Kiboko. Siku moja, Hatima iliwapatia nafasi ya kuchagua kati ya vitu viwili. "Chagua upofu au ukoma," Hatima iliwaamrisha.

Kiboko alitaka kuwa mwerevu. Kwa haraka, alichagua ukoma ili aweze kuendelea kuona. Tembo alichagua upofu.

Kiboko alikuwa mvulana mwenye hasira kwa sababu ya ukoma. Upofu ulimpatia Tembo uvumilivu. Tembo alihitaji usaidizi, lakini Kiboko alimtendea ukatili.

Halafu Tembo akapata Fimbo ya miujiza iliyomwezesha kutembea. Walinong'onezeana siri. Fimbo ilimsaidia Tembo kuwapiga maadaui.

Kwa sababu Kiboko alivipoteza vidole vyake, yeye pia alihitaji usaidizi. Tembo alimtendea wema.

Chakula kilipobaguliwa, Kiboko alimhitaji Tembo kukikata vipande na kukiweka kwenye viganja vyake. Kiboko hakufurahi.

Asubuhi moja, mama yao aliwabagulia viazi vikuu. Kwa sababu walikuwa na njaa, wavulana hao hawakusubiri viazi hivyo vipoe.

Kiboko aliviweka viganja vyake pamoja vikawa kama sahani. Akasema, "Niwekee sehemu yangu hapa."

Viazi vikuu vilikuwa moto sana hata vikachoma viganja vyao. Kiboko aliienua mikono yake juu na chini, kuvipoesha. Kiazi kilianguka mchangani.

Tembo aligeuzageuza kiazi chake kutoka mkono mmoja hadi mwingine bila kiazi kuanguka. Kiboko alikasirika.

"Tafadhali, nichukulie kiazi changu," Kiboko alimwuliza Tembo.

"Unajua kuwa sikioni," Tembo alimjibu. "Nipe mkono wako nikuonyeshe," Kiboko alisema.

Tembo alikipata kiazi, akakifuta mchanga kisha akampatia Kiboko.

Jioni, mama yao aliwatayarishia viazi vikuu pamoja na vipande vinne vya nyama. Tembo aliigusa ile nyama kwa kidole chake akahakikisha kuwa vilikuwa vipande vinne.

Kiboko hakumwona Tembo akivihesabu vile vipande vya nyama.

Kiboko alijaribu kuiba kipande kimoja cha nyama lakini akakiangusha. Wakati wa kugawa nyama ulipofika, Tembo aliuliza, "Si vipande vya nyama vilikuwa vinne?"

"Vilikuwa vitatu," Kiboko alidanganya. "Vilikuwa vinne," Tembo alisisitiza. "Wewe kweli ni kipofu?" Kiboko aliuliza.

Siku moja, walihisi njaa lakini mama yao alikuwa mbali. "Twende tucheze ili tuisahau njaa," Kiboko alipendekeza. Tembo alikubali.

Kiboko akasema, "Twende tukaogelee mtoni." Alijua kwamba Tembo hakujua kuogelea. Alipanga kumuua nduguye! Tembo aliongozwa na Fimbo akamfuata Kiboko.

Walipokuwa njiani, Kiboko aliingia kichakani. Alilichukua jiwe nzito na kuliweka kwapani huku akikoroma. Alikuwa bado anakoroma walipokuwa wanakwenda mtoni.

"Mbona anakoroma hivyo?" Tembo aliiuliza Fimbo.

Walipofika mtoni, Kiboko alisema, "Nitatangulia kuruka majini kisha nikusaidie kuogelea."

Alisonga mbali na Tembo akaliinua lile jiwe nzito na kulitumbukiza majini.

"Sauti hiyo ni ndogo sana kulingana na ukubwa wa Kiboko," Fimbo ilimnong'onezea Tembo sikioni.

Tembo aliiuliza Fimbo kuchunguza zaidi. Aliizungusha Fimbo kila mahali hata Fimbo ikamgonga Kiboko kwa nguvu. "Ayii!" Kiboko akalia na kuruka majini.

Fimbo ya miujiza ilimgeuza Kiboko akawa mnyama wa majini. Ilimgeuza naye Tembo akawa mnyama wa nchi kavu akiwa na mkonga.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na familia moja iliyoishi kwa amani.

Heri, Amani na Musa waliwasaidia wazazi nyumbani na shambani.

Wazazi wao hawakuwaruhusu waende karibu na moto, wala kukaa juani.

Heri, Amani na Musa walifanya kazi zao zote usiku.

Hii ni kwa sababu watoto hao waliumbwa kwa nta.

Musa alitamani kwenda nje wakati wa mchana.

Siku moja tamaa ilimzidi. Nduguze, Heri na Amani,  walimwonya asiende juani. Musa hakuwasikiza.

Joto lilipokuwa kali, Musa aliyeyuka.

Heri na Amani walihuzunika walipomwona Musa akiyeyuka.

Heri na Amani waliichukua nta iliyoyeyuka wakamtengeneza ndege.

Kisha walimweka ndege huyo juu ya mlima mrefu.

Jua lilipochomoza, ndege huyo alipeperuka akiimba kwa furaha.

------------------------------------------------------------



Ninafurahi kuruka na rafiki yangu.

Ninafurahi kuandika herufi ubaoni.

Ninafurahi kusoma vitabu vya picha.

Ninafurahi kula matunda.

Ninafurahi kusaidia kazi nyumbani.

Ninafurahi mama akinisimulia hadithi.

Ninafurahi kulala kwenye kitanda kikubwa.

Ninafurahi kufanya vitu hivi.

Wewe unafurahi kufanya nini?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na Mbweha aliyekuwa na njaa. 

Alijaribu kumshika panya, lakini panya alitoroka.

Alijaribu kumfukuza kichakuro, lakini kichakuro pia alikimbia na kupanda juu ya mti. 

Kisha Mbweha akamwona panya mdogo aliyenona. Akawaza, "Huyu anafaa kuliwa." Panya alipomwona Mbweha, alikimbilia chini ya jiwe, akaruka shimoni mwake. 

Mbweha akawaza, "Ni lazima nichimbe nikamtoe panya huyu shimoni."

Mbweha alikimbilia chini ya jiwe hilo kubwa akaanza kuchimba. Alichimba ndani zaidi hata jiwe likamwangukia mguuni. 

Alishindwa kuutoa mguu wake chini ya jiwe. Akapiga mayowe, "Nimenaswa! Nisaidie! Nisaidie!"

Sungura alipomsikia Mbweha akilia, alikimbia na kumwuliza, "Una nini?" 

Mbweha akamjibu, "Nilikuwa nikiwinda panya kisha jiwe likaniangukia mguuni. Tafadhali mpendwa Sungura, nisaidie!"

Sungura alimjibu, "Mmmh! Ningependa sana kukusaidia lakini, mimi ni mdogo na hafifu na jiwe hili ni kubwa. Itakuwa vigumu kwangu. Je, utanipa nini nikikusaidia?" 

Mbweha alilia aksema, "Jioni nitakupikia mlo uupendao. Utakula chakula kitamu kuliko vyote duniani." 

Sungura alimjibu, "Sawa, nitajaribu kukusaidia."

Sungura alilisukuma jiwe, lakini, halikusonga hata kidogo. 

Akalisukuma tena na tena hadi likauondokea mguu wa Mbweha. Sungura akafurahi.

Sungura akasema, "Nipe zawadi yangu." 

Mbweha akamwuliza, "Zawadi gani? Umenona na unatamanika." 

Sungura akamwuliza, "Si nimekusaidia? Wawezaje kutaka kunila?" 

Mbweha akajibu, "Mbweha hula sungura. Usibishane nami." 

Sungura akasema, "Hiyo si haki. Tuwatafute wazee watupe mawaidha yao."

Sungura na Mbweha walimpata mzee mmoja. 

Sungura akasema, "Tafadhali tusaidie. Mbweha anataka kunila ilhali niliyaokoa maisha yake. Jiwe lilikuwa limemwangukia mguuni na hangeweza kujitoa. Aliniahidi chakula kitamu cha jioni. Nami nikalisukuma jiwe na kuliondoa mguuni pake. Sasa ameisahau ahadi yake."

"Si sawa. Mbweha, kwani huna shukurani? Mwache Sungura aende zake," Mzee alinena. 

Mbweha alikifungua kinywa chake akamwonyesha Mzee meno yake marefu na makali. Kisha akasema, "Hapana! Sitamwachilia aende. Na usijaribu kunizuia au nitakukula wewe pia."

Mzee aliogopa sana akasema, "Tafadhali usinile. Labda, nimefanya uamuzi usio sawa. Unayoyasema ni kweli. Siwezi kuamua ilhali sikuliona jiwe. Je, ni nini hasa kilichofanyika?"

"Hilo ni jambo rahisi. Twende nikuonyeshe," Mbweha akasema. 

Mzee alikwenda pamoja na Mbweha na Sungura kuliona jiwe. Kisha akamwuliza Mbweha, "Kwani ulikuwa unafanya nini?"

Mbweha akaeleza, "Panya niliyekuwa nikimwinda alitorokea shimoni. Nilipokuwa nikilichimba shimo hilo, jiwe liliniangukia mguuni." 

"Jiwe gani?" Mzee akauliza. "Jiwe hili," Mbweha akajibu. 

"Wewe ulikuwa wapi?" Mzee akauliza. "Nilikuwa hapa," Mbweha akasema huku akijilaza chini.

Mzee alimtazama Sungura kisha akasema, "Wewe ni Sungura mdogo tu na hafifu. Siamini kuwa uliweza kulisongeza jiwe kubwa kama hili." 

"Lakini nililisongeza!" Sungura alilia. 

"Hebu nionyeshe," Mzee akasema.

Sungura alisukuma akasukuma. Jiwe likaungukia mguu wa Mbweha tena. 

Mzee akauliza, "Hivi ndivyo ulivyompata Mbweha?" 

Sungura akaitikia kwa kichwa.

Mzee akamwuliza Mbweha, "Je, Sungura alikupata katika hali hii?" 

Mbweha aliitikia kwa kichwa. 

Mzee akasema, "Vizuri. Hii ndiyo haki. Sungura, kimbia nenda zako nyumbani. Nami pia ninakwenda nyumbani."

Basi, Mzee na Sungura wakaondoka. 

Wakamwacha Mbweha asiye na shukrani peke yake.

------------------------------------------------------------



Nilikuwa nikicheza na tiara yangu. 

Upepo mkali ulianza kuvuma.

Upepo huo uliibandua tiara yangu. 

Ilirushwa mbali nami.

Macho yangu yalijaa mchanga.

Upepo huo uligeuka ukawa dhoruba.

Niliogopa!

Nilijiuliza, "Tiara yangu nzuri iko wapi?"

Labda, ilikuwa angani.

Dhoruba hiyo ilinizungusha. 

Iliniinua juu.

Iliniangusha chini.

Niliposimama, sikuiona tiara yangu. 

Sikuusikia upepo ukivuma tena.

Nilianza kwenda nyumbani.

Je, unafahamu kuwa upepo mkali ni hatari?

------------------------------------------------------------



Ninampenda mwalimu wangu.

Ni mwalimu mzuri, mvumilivu na mwenye huruma.

Amesuka nywele zake vizuri.

Ameweka shanga maridadi katika nywele zake.

Shanga zake ni za kijani, nyeupe, nyekundu, na manjano.

Mama, unaweza kuzisuka nywele zangu kama vile mwalimu wangu alivyosuka?

Nitakapokuwa mtu mzima, nitaweka shanga katika nywele zangu.

Nikikua, nitakuwa kama vile mwalimu wangu alivyo!

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, katika kijiji kimoja, kulikuwa na mvulana aliyeitwa Roba.

Roba alikuwa rafiki ya Leah. Walikuwa majirani.

Siku moja, walienda kuchota maji.

Walipokaribia kisima, walimwona ng'ombe akiwa amelala hapo. 

Waliketi chini kujadiliana vile wangecheza naye.

Roba alianza kumuiga ng'ombe. Alisema kwa sauti ya juu, "Mooo, mooo, moooooo!"

Aliendelea hadi ng'ombe akawatazama. Leah alishtuka. 

Roba aligundua kwamba Leah alikuwa ameogopa.

Roba alisema, "Twende tumpige atoroke ili tuchote maji."

Leah alimjibu huku akitetemeka, "Roba, ninaogopa!"

Roba alikuwa wa kwanza kuenda. Leah alimfuata
polepole. 

Walijaribu kumgonga ng'ombe, lakini ng'ombe yule hakusonga.

Roba alisema, "Leah, unaweza kuketi hapa. Mimi nitachota maji." 

Leah alikubali.

Roba alijaza ndoo ya kwanza maji.

Alipokuwa akijaza ndoo ya pili, ng'ombe alisimama. 

Alimuenua Roba juu kwa pembe moja kisha akamtupa mgongoni.

Roba alipiga kelele, "Joo, jooo, jooooo!" 

Leah aliangua kicheko na hakuweza kuacha kucheka.

Ng'ombe alisema, "Mooo, mooo, moooooo!"

Leah alipoacha kucheka, alikimbia haraka alivyoweza. 

Alimpata mamake Roba akifagia.

Alisema huku akihema, "Ma-ma! Ma-ma! Ng'o-mbe amemchukua Roba!"

Mamake Roba aliangusha ufagio akakimbia. 

Unadhani ni nini kilichotendeka baadaye?

------------------------------------------------------------



Terry ana nywele fupi.

Anna ana nywele ndefu.

Kate ana nywele ndefu zaidi.

Dama amesuka nywele zake.

Baba ana ndevu.

Sara amechana nywele zake.

Toni amekata nywele zake.

Tim amenyoa nywele zake.

------------------------------------------------------------



Chifu aliyeitwa Mfupi na Duara, alilia, "Nina tatizo kubwa sana."

"Nimeipoteza pembe yangu inayotumika wakati wa upanzi," Chifu Mfupi na Duara alisema.

"Nitaipata pembe yako. Nitaenda kuitafuta nyumbani kwa Mjomba Mstatili," Jojo alisema.

Jojo na Mjomba Mstatili walitafuta kila mahali lakini hawakuipata ile pembe.

"Nenda uone ikiwa Mama Pembetatu anayo ile pembe," Mjomba Mstatili alisema.

Jojo alifika nyumbani kwake akanywa maji baridi kabla kuendelea na safari.

Jojo alimtembelea Almasi na kumwuliza ikiwa angeweza kuambatana naye.

"Si mbali lakini nitatayarisha chakula kidogo ili tubebe," Almasi alisema.

Almasi na Jojo walipumzika na kula chakula chao chini ya mlima wa pembetatu.

Walipokuwa wamepanda nusu ya mlima, walimwona buibui na utando wa ajbu.

Jojo na Almasi walifika  nyumbani kwa Mama Pembetatu

"Chifu hakuacha pembe yake hapa," Mama Pembetatu alisema.

Mama Pembetatu alijua mahali wangeipata ile pembe.

Ilikuwa jioni walipowasili nyumbani kwa Chifu Mfupi na Duara.

Mama Pembetatu alimwelekezea chifu kidole. "Umeifunga pembe yako kichwani."

Chifu Mfupi na Duara alimpa Jojo ile pembe kuipuliza. Wote walifurahi tena.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale paliondokea mvulana mmoja aliyeitwa Demane. 

Alikuwa na pacha mwenzake aliyeitwa Demazane.



Wazazi wao walipofariki, Demane na Demazane walienda kuishi na mjomba wao. Huko kwa mjomba wao, walitendewa mabaya. 

Walichapwa kwa vibiko virefu, na walipewa uji mwepesi mara moja tu kwa siku. Kwa sababu hiyo, walitoroka.



Hawakuwa na nyumba ya kuishi. Waliona pango wakaamua kuishi humo. Waliogopa kwa sababu walisikia kwamba majitu yaliyowala watu yaliishi karibu. 

Kwa hivyo, waliunda mlango wenye nguvu. Wakafunga kiingilio na kuacha mashimo mawili ya kupitisha hewa na mwangaza. 

Kisha Demane akamwambia dadake, "Baki humu pangoni nikatafute chakula. Na usipike nyama kamwe. Majitu hupenda sana harufu ya nyama."



Kila jioni Demane alirudi na nyama ya sungura,  ndege au paa. Kila aliporudi pangoni aliimba: 

Demazane, Demazane,  
nimefika kwenye pango,  
nifungulie mlango,  
ndiye mimi si uongo,  
nimewinda na korongo,  
tupike kwa kikaango,  
ufungue kwa mpango,  
asiingie muongo.



Kesho yake alipata ukakamavu, akawasha moto ili kuondoa baridi. Lakini aliwasha moto huo ndani ya pango kwa kuogopa majitu. 

Aliufunga mlango kabisa. "Nina hakika hakuna hatari nikichoma nyama kwa moto huu. Chakula cha kuchomwa ni kitamu."





Demane aliporudi nyumbani aliimba: 

Demazane, Demazane,  
nimefika kwenye pango,  
nifungulie mlango,  
ndiye mimi si uongo,  
nimewinda na korongo,  
tupike kwa kikaango,  
ufungue kwa mpango,  
asiingie muongo.

Demane aliingia na kuiona nyama. Aliuliza, "Uliichomaje nyama bila moto?" "Niliichoma kwenye jua nje ya pango," Demazane alijibu upesi. Demane alikuwa amechoka. Hakuuliza swali tena. Waliendelea kufurahia chakula.



Siku iliyofuata Demazane aliwasha moto akachoma nyama tena. Alpomaliza aliusikia wimbo. 

Demazane, Demazane,  
nimefika kwenye pango,  
nifungulie mlango,  
ndiye mimi si uongo,  
nimewinda na korongo,  
tupike kwa kikaango,  
ufungue kwa mpango,  
asiingie muongo.

Lakini sauti hiyo haikuwa kama ya kakake. Demazane akajibu, "Hapana, wewe si kakangu. Sauti hiyo si yake."



Baada ya muda mfupi alisikia sauti tena ikiimba: 

Demazane, Demazane,  
nimefika kwenye pango,  
nifungulie mlango,  
ndiye mimi si uongo,  
nimewinda na korongo,  
tupike kwa kikaango,  
ufungue kwa mpango,  
asiingie muongo.

Sauti hiyo ilifanana na ya kakake. Kwa hivyo aliufungua mlango.



Jitu kubwa lenye nywele mwili mzima lilijaa mlangoni. Likamchukua Demazane haraka. 

Hata hivyo, Demazane aliokota jivu la jikoni akabeba. Alipokuwa akibebwa alimimina jivu lile njiani walikopitia.



Demane aliporudi alipata mlango ukiwa wazi na Demazane hakuwa ndani. Aliona jivu lililomwagwa kulekea msituni. 

Alifuata jivu hilo mpaka alipoona moto mbali.



Demane aliona jitu lililojaa nywele limeketi karibu na moto. Mfuko mkubwa ulikuwa karibu naye. Alisongea karibu na jitu hilo akijifanya anachechemea kama mtu aliyeumia mguu. 

"Tafadhali babu," Demane alisema, "Naomba unisaidie. Nimeumia mguu. Naomba maji ya kunywa." 

Jitu likasema, "Ngoja nikuletee maji lakini usiguse mfuko wangu. Jitu lilisema huku likiweka mfuko ule vizuri ndani ya nyumba."



Jitu lile lilipoondoka kwenda mtoni, Demane alikata kamba ya mfuko. Ulifunguka na dadake akatoka. 

Demane alibadilisha mfuko huo na mfuko wake uliojaa nyuki. Kisha yeye na dadake wakajificha na kungoja kuona kitakachotokea.



Jitu lilirudi na maji pamoja na watoto wake wawili, msichana na mvulana. Likamwambia msichana,  "Kuna mlo mtamu ndani ya mfuko. Nenda ukaulete!" 

Msichana alifungua mfuko kuona kilichokuwa ndani. Nyuki walimwuma mkono akalia akisema kwa sauti,  "Inauma, inauma." 

"Nenda ukamsaidie," Jitu lilimwambia mvulana kwa sauti. Pia mvulana aliumwa akalia kwa uchungu."



"Msinifanye mjinga," jitu lilisema kwa sauti likajitoma ndani ya nyumba. Lilifunga mlango na kufungua ule mfuko. 

Nyuki wale walichomoka kwa wingi na kumwuma kichwani, masikioni, na hata kwenye macho. Alishindwa kuona akarukaruka na kulia kwa uchungu mwingi.



Jitu lilikimbia kuelekea kwenye bwawa la maji. Lilichopeka kichwa kwenye matope likakwama huko. Liligeuka na kuwa kisiki cha mti uliokatwa. 

Nyuki walijenga mzinga wao kwenye kisiki hicho. Baadaye, Demane na Demazane walifurahia asali tamu kutoka kwenye mzinga huo wa nyuki.

------------------------------------------------------------



Sarai ana mtumbwi.

Mtumbwi wake ni mkubwa.

Mtumbwi huo uko kando ya mto.

Baadhi ya wanawake wanafika mtoni. Mwanamke mmoja ana uteo wa matunda. Mwingine ana kuku. Mwingine ana mbuzi mmoja. Wa mwisho ana mbuzi wawili.

Wanamwuliza Sarai, "Tutavukaje mto?"

Sarai anasema, "Ingieni mtumbwi wangu!"

Kisha, wanaume wanafika. Mmoja ana samaki. 

Mwingine ana baiskeli. 

Mwingine ana gunia la mahindi.

Mwanamume mwingine ana magunia mawili ya mahindi. 

Wanamwuliza Sarai, "Tutavukaje mto?"

Sarai anawajibu, "Ingieni mtumbwi wangu!"

Wanyama pia wanakuja. Wanamwuliza Sarai, "Tutavukaje mto?"

Sarai anasema, "Ingieni mtumbwi wangu!"

Wanyama wanaingia mtumbwini. Mbwa anaingia mtumbwini. Paka anaingia mtumbwini. 

Tumbili anaingia mtumbwini. Sungura anaingia mtumbwini. Kasa anaingia mtumbwini. Swara anaingia mtumbwini.

Tembo anawasili kando ya mto. Anauliza, "Nitavukaje mto?"

Sarai anasema, "Ingia mtumbwi wangu!"

Tembo anaingia mtumbwini. Mtumbwi unafurika maji.

Salaala!

Mtumbwi umepinduka!

Mtumbwi huu ni mdogo sana. 

Hauna nafasi ya kuwatosha wote.

Sarai anasema, "Hebu! Kwanza, nitawavukisha wanawake."

"Kisha niwavukishe wanaume," Sarai anasema tena.

"Hatimaye, nitawavukisha wanyama," Sarai anakamilisha maelezo yake.

Tembo anasema, "Heri nitembee tu!"

------------------------------------------------------------



Kwa nini mtoto analia?

Labda ana njaa.

Kwa nini 
mvulana huyu amehuzunika?

Labda anamkosa baba yake.

Kwa nini msichana huyu amefurahi?

Kwa sababu amepata rinda jipya.

Kwa nini mzee huyo anacheka?

Kwa sababu amesoma kichekesho.

Kwa nini 
mama huyu anatabasamu?

Watoto wake wanasoma kimya kimya.

Mbona mama huyu anatazama chini?

Anaona haya.

------------------------------------------------------------



Hapo kale kulikuwa na wake wenza wawili. Waliishi katika nyumba moja na mume wao.

Kwa muda mrefu hakuna mke aliyejaliwa kupata watoto. Hatimaye, mke wa kwanza alishika mimba. 

Alipojifungua mtoto, mume wao hakuwa nyumbani.

Mke wa pili aliwaonea wivu mke wa kwanza na mtoto wake. 

Alianza kuwaza jinsi atakavyomwua mke mwenziwe ili awe mke wa pekee.

Nyakati hizo, watu hawakuzoea kupika chakula. 

Walivila vyakula vikiwa vibichi.

Mke wa pili alisema, "Nitakipika chakula ili nimdhuru mke-mwenzangu." 

Yeye aliamini kuwa chakula kilichopikwa kingeweza kumwua mtu.

Basi alianza kumpikia mke mwenziwe chakula. 

Lakini, badala ya kufa, mke wa kwanza alizidi kuwa na afya nzuri kwa sababu ya kula chakula kilichopikwa.

Mume wao aliporudi nyumbani, alimkuta mtoto mchanga na mke wa kwanza mwenye afya. Pia alitambua kuwa chakula kilikuwa kikipikwa.

Mume huyo alishangazwa na upikaji wa chakula. Akauliza, "Nani aliwafunza kupika chakula?" 

Mke wa pili akamnong'onezea mumewe, "Ninakipika chakula ili nimue mke mwenzangu."

"Ninamwonea wivu kwa sababu alimpata mtoto ilhali mimi sina. Nina wasiwasi kuwa utanifukuza ubaki naye."

Mumewe alikasirika kisha akamuonya, "Acha kuwa na fikira hizo mbaya."

Kisha yule mume aliwaleta wakeze pamoja. 

Aliwapatanisha wakaishi kwa amani.

Walikubali kuendelea kupika chakula kwa sababu kiliwafanya kuwa na afya nzuri.  

Na hivi ndivyo upikaji wa chakula ulivyoanza!

------------------------------------------------------------



Babangu alinibeba katika gari letu kwenda mjini.

Nilitazama nje ili niyafurahie mazingira yangu.

Nilimwona mwanamke aliyevaa nguo ya rangi ya chungwa. 

Alikuwa akitembea kwa kasi.

Alikuwa amefunga kiunoni mshipi mkubwa mwekundu.

Mkononi, aliubeba mkoba wa rangi ya chungwa.

Miguuni, alivaa viatu vya rangi ya chungwa. 

Vilikuwa na visigino virefu.

Alisimama na kuzigusa nywele zake refu. 

Zilikuwa zimebanwa katikati na kibano cha rangi ya chungwa.

Alipokuwa akirekebisha kibano cha nywele, mkoba wake ulianguka chini. 

"Uuui," nilisema huku nikimhurumia.

Aliinama kuuokota mkoba wake ulioanguka. 

Nilitazama nguo, mshipi, viatu na mkoba.

Niliviona vipuli virefu vikubwa vya rangi ya chungwa. 

Vilitikisika alipofuta vumbi kutoka kwenye mkoba.

Tulipoendelea na safari yetu, nilizidi kumtazama yule mwanamke.

"Unatazama nini?" Babangu aliniuliza.

"Mwanamke yule mrembo," nilimjibu baba. 

Nilifikiria juu ya rangi tofauti na jinsi zinavyopendeza.

------------------------------------------------------------



"Mwaka huu tutakuwa na mkutano maalum wa familia," Mama Pembenyingi alitangaza. "Nani atakayehudhuria? Natumai Pembenyingi wote watakuwa. Ninawakosa binamu yangu," Kosi alisema. "Ninakosa zaidi upande wa familia yangu ya Pembenne," Mama alitabasamu. "Ndiyo, ni kitambo sana tangu tuwaone Mstatili, Mraba, na Msambamba," alisema Baba Pembenyingi. "Usisahau, wana watoto watatu sasa!" Mama alimkumbusha Baba.

"Na binamu wengine, je? Watakuja?" Fusi aliuliza. Mama alijibu, "Ndiyo, wao ni Pembenyingi, ingawa si Pembenne. Jina lao la ukoo ni Pembetatu. Watoto ni Pembetatu Pacha na Pembetatu Sawa." "Aa, ndiyo, familia ya Pembetatu!" alishangaa Fusi. "Lakini wanafanana sana na Pembenne." "La, sio kabisa," Mama alisema. "Pembetatu wana pande tatu, ilhali Pembenne wana pande nne, kama mimi."

Baba Pembenyingi aliongeza, "Nimefurahi kwa sababu binamu zangu wengine watatu watakuwa hapa: Pembetano, Pembesita na Pembenane. Wao pia ni wa familia yetu ya Pembenyingi." Vusi aliuliza, "Baba, mbona tunaitwa Pembenyingi?" "Kwa sababu tuna sura pande mbili. Tumeumbwa kwa mistari iliyonyooka, na maumbo yetu yamefungika, kama unavyoona, mistari yetu yote imeunganika. Binamu yetu Pembetatu, Pembenne, Pembesita, na Pembetano wote watatutembelea," Baba alijibu.

"Je, ulisema kuwa Pembenane atakuja? Yeye pia ni jamaa yetu?" Khosi aliuliza. "Bila shaka, binti yangu, ukimtazama, utajua kwamba ni wa familia yetu. Unastahili kuangalia kwa makini idadi ya pande ambazo binamu yako wanazo, au hutaweza kuona tofauti. Binamu Pembenane ana pande nane kwa sababu jina lake linamalizika na nane," Baba alisema.

"Sawa, na Pembetano na Pembesita, je?" Vusi aliuliza. "Binamu Pembesita ana pande sita kwa sababu jina lake linamalizika na sita," Baba alijibu. "Pembetano wana pande tano. Mwalimu wetu alituambia kwamba tano inatokana na pande hizo
tano," aliongeza Khosi. "Kumbuka kwamba tatu na nne ndizo zinafanya binamu yako Pembetatu na Pembenne kuwa tofauti.

"Baba, Pembesaba ana pande ngapi?" Vusi aliuliza. Baba alicheka akasema, "Sitakwambia. Kumbuka tulipiga picha zake tulipokuwa kwa harusi ya mjombako. Ningependa uitazame picha ile kwa makini kisha unieleze unachoona. Vusi aliitazama picha haraka halafu akajibu, Pembesaba ana pande saba!" Khosi aliongeza, "Ndiyo, kumbuka mwalimu wetu alituambia kuwa saba inatokana na idadi sab."

"Aa mke wangu, unaona jinsi watoto wetu walivyo werevu? Je, kumi ina maana gani?" Baba aliuliza. "Pembe kumi!" Vusi na Khosi walisema. "Ndiyo, hiyo ndiyo sababu binamu yenu anaitwa Pembekumi. Lakini, hatakuja kwa sababu ataiwakilisha timu ya waogeleaji. Kuna Pembekumi wachache sana shuleni kwao," Mama aliwaambia.

Watoto walisema, "Mama na Baba, tunaweza kumualika rafiki yetu Mduara?" Wazazi wao walikubali Mduara kujiunga nao kwa sherehe. Wakati huo, waliusikia mlango ukibishwa. Baba alienda kujua ni nani. "Pembenne wako hapa! Karibu! Karibu!" Baba alishangilia.

Familia yote inaruka kuwasalimu Mraba, Mstatili, na watoto watatu wa Msambamba. Pembenne wanafurahi kuwa wa kwanza kufika.

Familia ya Pembetatu inabisha mlango muda mfupi baada ya kufika kwa Pembenne. Pembetatu pacha na Pembetatu sawa wamechoka baada ya safari ndefu. Lakini, wamefurahi kuwa pamoja na familia nzima.

Hatimaye, Pembenane na Pembesaba wanawasili pamoja na wanao, Pembetano na Pembesita. Pia wemewaleta Miraba watatu. Pembenane anaeleza, "Natumai si tatizo kwamba wana Pembenne watatu kutoka kijijini wamekuja nasi. Hawajawahi kwenda jijini." Mama alitabasamu, "Marafiki na familia wanakaribishwa hapa kila wakati." Aliwatuma watoto wote nje kucheza.

"Tutacheza mchezo gani?" Vusi aliwauliza watoto wengine. Pembetatu sawa alisema kwa furaha, "Hebu tucheze mchezo wa maumbo!" Watoto wote wa Pembenyingi walianza kucheza mchezo huo. "Ninaweza kucheza nanyi? Mimi pia ningependa kucheza mchezo wa maumbo," Mduara alisema.  Vusi alimjibu, "Aibu kubwa, samahani, huwezi kucheza mchezo huo rafiki yangu." Mraba mmoja aliongeza, "Huoni umbo lako, wewe si wa familia ya Pembenyingi. Duara hawawezi kucheza mchezo wa maumbo."

Mduara alihuzunika sana kwa kuachwa nje ya mchezo. Lakini, mchezo haufurahishi sana mmoja akiachwa nje. Vusi alisema, "Ni heri tucheze mchezo ambao Mduara pia anaweza kucheza." Kwa hivyo, Pembenyingi na Mduara walicheza pamoja kwa furaha hadi chakula kitamu kilipokuwa tayari.

Tafsiri yako hapa

Tafsiri yako hapa

Tafsiri yako hapa

------------------------------------------------------------



Kwa miezi mingi anga lilikuwa kavu. Lomongin, mbuni mvua maarufu, alizungumza na miungu. 

Watu walikusanyika nje ya boma lake. Walingoja kwa hamu na ghamu ujumbe wa matumaini.

Aliwahakikishia watu kwamba muumba angewapa mvua hivi karibuni. 

Wangepanda mimea yao.

Watoto walicheza nje tulipokuwa tukingoja mvua. 

Baadaye siku hiyo, tuliyaona mawingu meupe mbali mashariki. Nilijua ni mawingu ya mvua.

Watu walikuwa bado wanawaza kuhusu kile mbuni mvua alisema. 

Mama alipiga yowe kwa sauti, "Pale! Sasa mawingu ni meusi. Njooni ndani."

Mvua ilinyesha. 

Ikanyesha!

Tulikuwa tumeingoja mvua kwa siku nyingi! 

Mwanzo, tulifurahi.

Maji yalizidi kuwa kila mahali. 

Daraja la kuunganisha kijiji chetu na sehemu nyingine, lilisombwa na maji.

Nyumba zilisombwa na gharika. 

Kile kilikuwa baraka, kilikuwa sasa ni mauti kwetu.

Tulikuwa tumejitayarisha kwa upanzi, lakini sasa hatungepanda. Tulikuwa tumeitamani mvua, lakini sasa hatukuitaka tena. 

Hatukuwa na daraja la kuvukia. Wengi hawakuwa na makazi wala miji.

Na tulikuwa na shida nyingine! Tuliona mamba wakiogelea kila mahali. 

Hili halikuwa limewahi kutokea tena. 

Tulichanganyikiwa!

Hatungeenda manunuzi kwa sababu maduka yote yalikuwa ng'ambo ya mto. 

Watoto hawangeenda shuleni kwa sababu shule zilikuwa ng'ambo ya mto.

Kile kingekuwa baraka, kiligeuka kuwa laana kwetu. Lomongin, mbuni mvua, akakata tamaa vilevile. 

Aliyekuwa na furaha pekee ni Kapuus na paka wake wanane!

------------------------------------------------------------



Siku moja, msichana mdogo aliona umbo la ajabu kwa umbali.

Umbo hilo lilipokaribia, aligundua kwamba lilikuwa mwanamke mja mzito.

Kwa ushupavu, msichana huyo alimkaribia yule mwanamke mja mzito. 

Jamaa zake wakasema, "Hatuna budi kumkaribisha akae nasi. Tutamlinda hadi atakapomzaa mtoto wake."

Baadaye, mama huyo alikuwa tayari kujifungua. 

Majirani wakashughulika. "Sukuma! Leta blanketi! Maji! Suukuumaaa!"

Mama alijifungua. 

Majirani walipomwona mtoto, wote walirudi nyuma kwa mshtuko. 

"Punda!"

Wakaanza kugombana. "Tulikubali kuwa tutamlinda huyu mama hadi atakapojifungua, na hivyo ndivyo tutakavyofanya," kiongozi wao alisema. 

"Hapana! Tukifanya hivyo tutapata bahati mbaya!" alisema jirani mwingine.

Mama yule alijikuta peke yake tena. 

Akajiuliza, "Nitafanyaje na mtoto huyu mwenye kunifedhehesha?"

Hatimaye, alikubali kuwa huyo ni mtoto wake na yeye ndiye mamake.

Mtoto punda angalibaki alivyozaliwa, mambo yangekuwa tofauti.

Lakini, alikua, akakua, hadi mamake akashindwa kumbeba mgongoni. Mamake mara nyingi alichoka na kuvunjika moyo. 

Mara nyingine mtoto punda alimfanyisha kazi za kinyama.

Mtoto punda alikasirika akachanganyikiwa. Hangeweza kufanya lolote kama binadamu. Hakufanana na huyu wala yule. 

Alizidi kukasirika hadi siku moja akampiga mamake teke akaanguka chini.

Mtoto punda aliona aibu. 

Akakimbilia mbali kadiri alivyoweza.

Aliendelea kukimbia hadi usiku alipotambua kuwa amepotea. 

"Hi ho?" Alinong'ona gizani. "Hi ho?" Mwangwi ukamrudia. 

Alijikunja mahali akalala usingizi wa mang'amung'amu.

Kulipokucha, mtoto punda aliamka na kumkuta mzee wa ajabu akimtazama. 

Naye pia akamtazama mzee machoni kwa hisia za matumaini. 

Mzee akasema, "Njoo twende kwangu."

Mtoto punda alikubali mwaliko wa mzee huyo. 

Mzee alimfundisha njia nyingi za maisha. Mtoto punda alijifunza mengi.

Asubuhi moja, mzee alimwomba mtoto punda ambebe hadi kilele cha mlima.

Walipofika juu mawinguni, walilala. 

Mtoto punda akaota kuwa mamake alikuwa mgonjwa na alikuwa anamwita.

Alipoamka, mawingu yalikuwa yametoweka na mzee rafikiye alikuwa hayupo.

Hatimaye, mtoto punda alifahamu atakavyofanya.

Mtoto punda alirudi nyumbani akamkuta mamake amenuna. 

Mama na mtoto wake mpotevu walitazamana kwa muda mrefu. Halafu wakakumbiatiana bila legezo.

Mtoto punda na mamake waliishi pamoja kwa ushirikiano. 

Waliishi kwa furaha pamoja na majirani wao.

------------------------------------------------------------



Parna alikuwa mvulana mwembamba mrefu. Alikuwa katika darasa la tatu. 

Alipenda kuvaa koti refu la rangi nyeusi. Alipewa koti hilo na Mjombake, Teteyo.

Wakati wa likizo, Parna aliwachunga ng'ombe wa wazazi wake.

Siku moja, Parna alikuwa akiwachunga ng'ombe. Ghafla, mvua ilianza kunyesha.

Wakati huo huo, Cheusi, ng'ombe aliyekuwa kipenzi cha babake, alizaa. 

Ndama aliyezaliwa alipendeza. Alikuwa mzuri kuliko ndama wote ambao Parna aliwahi kuwaona.

Parna alifurahi kuwahudumia Cheusi na ndama wake. Aliwasahau ng'ombe wale wengine.

Aliwaza, "Babangu aliahidi kunipa ndama ikiwa atakuwa wa kike."

Alipokuwa akiwaza hivyo, alisikia mkono ukimvuta juu kwa nguvu. 

Parna alimwona Mjomba Teteyo. Alikumbuka na kuuliza, "Mjomba, ng'ombe wako wapi?"

Mjomba Teteyo alimjibu, "Mamako aliwapata ng'ombe wote zizini ila wewe na Cheusi. Aliingiwa na wasiwasi akanituma nije nikuchukue."

Mjomba Teteyo akasema, "Nitambeba ndama huyu. Kisha wewe na Cheusi mnifuate nyuma."

Parna alielezea kwa msisimko jinsi Cheusi alivyozaa ndama aliye mzuri zaidi ya wote.

Watu wote walifurahi walipoona kwamba Parna, Cheusi na ndama walikuwa salama.

Parna akamwuliza babake, "Je, utanipa ndama huyu kama ulivyoahidi?"

"Ndiyo, mwanangu, ndama huyu ni wako. Ahadi ni deni."

------------------------------------------------------------



Anansi ni buibui mvivu.

Anapenda chakula, lakini hapiki kwani ni mvivu.

Anansi anamtembelea Sungura. 

Anaomba wale mboga pamoja.

"Nisaidie kukoroga," Sungura anasema. 

Anansi hataki, ni mvivu.

"Nitarudi baadaye," Anansi anasema.

Anafunga utando mguuni na kwenye chungu cha Sungura.

"Vuta utando mboga zitakapoiva," Anansi anasema.

"Kima, naomba nile maharage nanyi?" 

"Tusaidie kufanya kazi."

"Nitarudi," Anansi anasema. 

Anafunga utando zaidi.

"Ngiri, tule viazi pamoja?" 

"Nisaidie kuvitayarisha," Ngiri anamjibu.

"Nitarudi," Anansi anasema. 

Anafunga utando zaidi.

Hatimaye, kila mguu wa Anansi umefungwa kwenye chungu.

Anansi anavutwa kwenye mguu wa 2. 

Halafu mguu wa 3.

Miguu yote 8 inavutwa! 

"Acheni kuvuta!" Anansi analia.

Hakuna anayemsikia Anansi. 

Utando unakatika mmoja mmoja.

Ndiyo sababu buibui wote wana miguu mirefu myembamba.

------------------------------------------------------------



Musau aliishi na babake, Syonzola.

Syonzola alienda kunywa pombe kila siku.

Aliporudi nyumbani, aliita, "Njooni mnisaidie! Nauawa na fisi."

Watu waliitikia mwito wake. 

Lakini, fisi hakuwepo.

Syonzola alifanya hivyo kila usiku.

Musau aliamshwa na kelele za babake.

Fisi alimvamia Syonzola usiku mmoja.

Syonzola alilia, "Nisaidieni!"

Watu walisema, "Syonzola ametuchosha. Ni uongo wake wa kawaida."

Musau alisubiri. 

Babake hakufika.

Musau aliwaza, "Labda babangu yuko hatarini."

Musau alitoka nje mbio.

Aliita, "Baba! Baba!" 

Fisi alikuwa akimvuta babake mguu.

Kutoka siku hiyo, Syonzola alibadilika. 

Anawasimulia watoto hadithi.

------------------------------------------------------------



Tuktuk ni gari lenye magurudumu matatu.

Linatumika kwenda sehemu moja hadi nyingine kwa haraka.

Katika jamii nyingi, uendeshaji gari la abiria ni kazi inayofanywa hasa na wanaume.

Wanawake hawajihusishi sana nayo.

Siku moja, Abby aliwaomba wazazi wake fedha. Alitaka kulipia mafunzo ya udereva.

Wazazi wake walisema, "Kazi hii si nzuri kwa wanawake. Watu watasemaje?"

Abby alisema, "Ninaweza kufanya kazi yoyote inayofanywa na watu wengine." 

Alifaulu kuwashawishi. Wazazi walimruhusu akaanza kujifunza udereva.

Abby alikamilisha mafunzo hayo vizuri.

Wazazi wake walijadiliana namna ya kumsaidia zaidi.

Baadaye, walikubali kumnunulia tuktuk.

Abby alianza kuendesha tuktuk yake mjini Sokomoja.

Siku moja alipata wazo zuri.

Aliweka tangazo kwenye mlango wa nyuma. Tangazo lilikuwa na namba yake ya simu.

Tangazo lilisema, "Ninawasafirisha wanawake waja wazito, akina mama waliojifungua, na watoto, bila malipo."

Abby alianza kupokea simu kutoka kwa waliohitaji kusafirishwa.

Abby alipata pesa kwa kuwasafirisha watu.

Hata hivyo, aliendelea kuwasaidia wasiokuwa na fedha zozote.

Abby aliifurahia kazi yake. Watu wakongwe walimtakia baraka. Kila wakati wanakijiji waliongea kuhusu kazi yake.

Abby aliwaambia, "Mtu huvuna anachopanda!"

------------------------------------------------------------



Mama yake Simbi aliaga dunia.

Simbi na baba yake walisaidiana.

Siku moja, baba yake Simbi alikwenda nyumbani na mwanamke. 

Aliitwa Anita.

Baba yake alimtaka Simbi kumkubali Anita kama mama yake.

Simbi hakufurahi. 

Alipata faraja kwa kulishika blanketi la mama yake.

Baba yake Simbi alienda kufanya kazi mbali.  

Anita na Simbi hawakufurahi.

Anita alizoea kumpiga Simbi. 

Wakati mwingine, alimnyima chakula.

Anita alimvuta Simbi kutoka kitandani. 

Blanketi la mama yake liliraruka.

Simbi alitoroka nyumbani.

Alilibeba lile blanketi pamoja na chakula.

Alipanda akaketi juu ya mti. 

Alimwimbia mama yake wimbo.

Mwanamke mmoja aliusikiliza wimbo huo kwa makini.

Alifahamu kuwa Simbi ni mtoto wa ndugu yake.

Simbi alienda na shangazi yake. 

Alikula na kulala vizuri.

Baba aliporudi nyumbani, hakumkuta Simbi.

"Unaweza kuishi na shangazi yako wakati wowote unapotaka." Baba alisema.

Anita na Simbi walianza kupendana.

Anita aliwapikia chakula. 

Simbi alijua angerudi nyumbani wakati wowote.

------------------------------------------------------------



Hii ni manyatta. 

Ni nyumbani kwetu. 

Iko katika Kaunti ya Turkana.

Huyu ni ngamia. 

Katika Kaunti ya Turkana, watu wanafuga wanyama tofauti. 

Lakini ngamia ni muhimu mno.

Hawa ni walimu wangu. Ninapenda kwenda shuleni. 

Shule yangu inaitwa Lolupe. Nampenda sana mwalimu wangu wa Sanaa.

Hii ni meli kubwa. Meli zinatumika kusafirisha watu na mizigo majini. 

Nikienda Mombasa, nitaweza kuona meli.

Hiki ni kitanda. Ninapenda kitanda babangu alinitengezea. 

Nakitumia na ndugu yangu mdogo. Ni kizuri.

Huyu ni jogoo. Tuna jogoo wawili nyumbani. 

Tunao pia kuku wengi. Kuku hutaga mayai mengi.

Huyu ni panya. Panya ni wanyama hatari. 

Hula chakula. Huharibu nguo pia. 

Huweza kusababisha ugonjwa.

Huyu ni mbwa. Mbwa hufugwa. 

Mbwa wetu anaitwa Daa. Hubweka sana.

Mwavuli huu mkubwa ni wa wazazi wangu. Ni wa rangi ya kisambarau, kimanjano na kijani kibichi. 

Tunautumia inaponyesha ili tusinyeshewe.

Niko darasa la pili na ninajua vitu vingi. Nataka kujua vingine zaidi. 

Nisivyojua, nawauliza wazazi wangu au mwalimu wangu.

------------------------------------------------------------



Siku moja Akadeli, Lucia, Acharait na Maria walienda msituni kutafuta matunda. 

Walishikana mikono wakavuka mto mkubwa.

Waliufikia mti uliojaa matunda mabivu. Walikubaliana kuukwea mti ule kuyachuma matunda. 

Sharti lilikuwa wayafumbe macho yao wakifanya hivyo.

Hata hivyo, Lucia, Acharait na Maria hawakuyafumba macho yao. 

Akadeli pekee alifanya hivyo alipokuwa akichuma matunda.

Ilipofika wakati wa kuyafumbua macho, Akadeli alikuta kwamba alikuwa ameyachuma matunda mabichi pekee.

Lucia, Acharait na Maria walimcheka Akadeli kisha wakaondoka kwenda zao nyumbani. 

Akadeli aliyatupa matunda yale mabichi akaanza kuchuma mabivu.

Muda mfupi baadaye, Akadeli alikijaza kikapu chake kwa matudna mabivu. 

Alianza kuuvuka mto ule mkubwa peke yake.

Akadeli alipokuwa katikati, kikapu chake kilimponyoka na kuanguka majini. 

Alikasirika sana akaanza kulia.

Kabla hajavuka ng'ambo, Akadeli alimwona samaki ukingoni mwa mto. 

Alimchukua.

Alipokuwa amembeba samaki yule, mwewe alimnyang'anya akaruka naye juu.

Akadeli aliona unyoya mmoja mrefu uliokuwa umeachwa na mwewe. 

Ingawa alikasirika, aliuchukua ule unyoya na kuendelea na safari yake.

Akadeli aliwapita watu wakisherehekea harusi ya kitamaduni. 

Wachezaji walivalia nyasi vichwani badala ya manyoya kama ilivyokuwa desturi. 

Waliuchukua ule unyoya wakampatia fahali mkubwa!

Akadeli alifika nyumbani na fahali wake. Wazazi na jamaa zake walifurahi sana. 

Lucia, Acharait na Maria walisikitaka kumdanganya Akadeli. Ilikuwa siku ya bahati kwa Akadeli!

------------------------------------------------------------



Hadithi hii anamhusu Mlinzi na chekechea yake ya wanyama mayatima.

Agosti ulikuwa mwezi wenye shughuli nyingi. 

Mlinzi na wasaidizi wake waliwapokea wanyama wengi katika chekechea yao.

Mkite alikuwa wa kwanza kufika. 

Alikuwa mtoto wa tembo mwenye umri wa mwaka mmoja.

Mlinzi na wasaidizi wake walimhurumia Mkite sana.

Alikuwa amekonda na mwenye huzuni.

Siku chache baadaye, afya ya Mkite iliimarika. 

Alicheza na wanyama wengine aliowakuta pale.

Siku nyingine katika mwezi huo wa Agosti, helikopta ilitua mbele ya chekechea.

Walimpokea yatima wa pili katika mwezi huo. 

Alikuwa mtoto mwingine wa tembo. Alifunikwa kwa blanketi.

Yatima huyo aliitwa Ndiwa. Alikuwa na umri wa siku tano. 

Mlinzi alimnywesha maziwa kwa kutumia chupa.

Yatima wa tatu kufika mwezi huo alikuwa Malea, kifaru. 

Malea alikwa na umri wa miezi sita.

Enkare alikuwa nyati mtoto. Yeye na Malea walikuwa marafiki wakubwa.  

Walienda kila mahali pamoja.

Usiku mmoja, Mlinzi na wasaidizi wake waliamshwa. 

Walimpokea twiga mtoto waliyemwita Ambia.

Ambia alikuwa na umri wa miezi mitano. 

Alihisi njaa na uchovu baada ya safari ndefu.

Kwa sababu ya urefu wake, Mlinzi aliupanda mti kumlisha.

Abei na Moit, swara mapacha, walifika katikati ya mwezi wa Agosti. 

Walikuwa wamezaliwa saa chache tu na walikuwa wagonjwa sana.

Walihuzunika Abei alipoaga dunia wiki moja baadaye. 

Mlinzi na wasaidizi wake walimwokoa Moit.

Mayatima wa mwisho kufika mwezi huo wa Agosti walikuwa Kopi, Kepi na Keji. 

Walikuwa wana wa simba wenye umri wa wiki mbili. Walikuwa na kiu sana.

Mlinzi na wasaidizi wake waliwapenda wanyama wote hata wale watukutu.

Mtukutu kwa wote alikuwa Lobolia. 

Alizoea kuichukua miwani ya Mlinzi.

Wafanyakazi wa chekechea wanafanya bidii kuwatunza wanyama hao. 

Watakapoweza kujitegemea, watarudi porini.

MAZOEZI:   Soma tena hadithi kisha ujibu maswali haya. 1. Wanyama wangapi walifika katika chekechea mwezi Agosti? 2. Nani alifika kwanza? 3. Mnyama huyu alikuwa na umri gani? 4. Nani alifika mwisho? Wanyama hao walikuwa na umri gani? 5. Wanyama gani waliokuwa na umri wa chini zaidi? 6. Walikuwa na umri gani? 7. Mnyama yupi aliyefika mwezi Agosti aliyekuwa mzee kwa wote?

------------------------------------------------------------



sambusa

chapati

ugali

samaki

yai

maziwa

zabibu

embe

nazi

tikiti maji

tofaa

mihogo

mchicha

parachichi

chakula kizuri hukufanya uwe na nguvu.

------------------------------------------------------------



Mamba ana meno makali.

Simba pia ana meno makali.

Papa ana meno makali sana. 

Kwa nini baadhi ya wanyama wana meno makali?

Ng'ombe ana meno yenye nguvu.

Anayatumia kusaga chakula.

Ndege hawana meno. 

Wao hula namna gani?

Panya wana meno makubwa ya mbele.

Kitambo, nilikuwa na meno ya mbele.

Meno yangu ya mbele yaling'oka! 

Je, wewe una meno mangapi?

------------------------------------------------------------



Mfalme Chui aliendelea kuwa mzee.

Je, atamchagua mrithi wake namna gani?

Mfalme  Chui aliwaita wanyama kwa sherehe.

Atawatangazia mpango wake.

Baada ya sherehe, Mfalme Chui alizungumza.

Wanyama walimsikiliza.

Alisema, "Mashindano yataamua atakayekuwa mfalme."

Atakayehesabu hadi kumi kabla ya mkuki kuanguka, atakuwa mfalme.

Tembo aliwasukuma wengine, "Mimi ni mkubwa. Ninastahili kuwa mfalme."

Tembo alihesabu hadi nne pekee.

Mkuki ulianguka.

Ngiri aliwasukuma wenzake akisema, "Nina nguvu zaidi. Nitakuwa mfalme."

Ngiri alihesabu hadi sita kisha mkuki ulianguka.

Aliondoka.

Wanyama walisema, "Tembo mkubwa na Ngiri wameshindwa. Nani atashinda?"

Sokwe alihesabu, "Moja! Mbili! Tatu! Nne! Tano! Sita! Saba!"

Alilia.

Mfalme Chui alisema, "Sokwe, unapate nafasi moja tu."

Sokwe aliondoka.

Baadhi ya wanyama walianza kuondoka.

Swara Mdogo alisema, "Hebu nijaribu."

Mfalme Chui aliwakemea, "Mpeni Swara nafasi. Mwache ajaribu."

Swara alisema, "Tano na tano ni kumi."

Mkuki ulianguka chini.

Mashindano yalionyesha mnyama mwerevu.

Swara alikuwa malkia baada ya chui.

------------------------------------------------------------



Zamani, Ngurumo na Radi waliishi duniani.

Ngurumo alikuwa mamake Radi.

Radi alikuwa mwenye hasira kali.

Alipokasirika, aliharibu watu, nyumba na miti.

Radi alisababisha uharibifu mkubwa.

 Ngurumo alipiga kelele kwa hasira.

Radi hakujali kelele za mamake.

Hatimaye, watu walienda kwa mflame kulalamika.

Mfalme aliwafukuza Ngurumo na Radi wakaishi mbali.

Radi alipokasirika, aliendelea kuchoma misitu na mimea.

Watu walienda tena kwa mfalme kulalamika.

Mfalme aliwafukuza Ngurumo na Radi waishi angani.

Hata hivyo, bado Radi anachoma na kuharibu anapokasirika.

------------------------------------------------------------



Siku moja, mtoto wa fisi alifariki.

Punda mmoja alikimbia kuwajulisha jamaa zake.

Punda wengine waliuliza, "Mtoto wa fisi? Hiyo ni habari njema. Fisi wote ni maadui zetu."

Punda mmoja mzee alisema, "Ndugu zangu, lazima tuhudhurie mazishi tuonyeshe heshima." 

Punda wengine wakauliza, "Eti nini? Tuhudhurie mazishi ya fisi? Hatutaki kwenda. Tunaogopa kuliwa na fisi."

"Sikiliza. Tusipoenda, fisi watakasirika sana. Watakuwa na sababu ya kutufanya kitoweo chao." Punda mzee alisema.
  
"Umesema ukweli. Lazima tuhudhurie mazishi ya fisi. Tukihudhuria, fisi watafurahi. Labda watakuwa marafiki zetu." Punda wengine walisema.

Fisi waliwaona punda nje ya nyumba yao. "Mbona punda wako hapa? Wamekuja kutucheka?" Fisi walijiuliza. 

Punda walipowasikia fisi, waliogopa, wakaanza kuimba.

Wimbo ulienda hivi:

"Fisi wakubwa, mnawinda usiku kucha. Tunawasikia usiku wa manane. Meno yenu ni marefu. Macho yenu yanang'ara. Ingawa chakula chenu ni cheusi, kinyesi chenu ni rangi nyeupe. Sasa mmoja wenu amefariki!"

Mjombake fisi aliyekufa pia akawajibu kwa wimbo:
 
"Wimbo wenu ni mzuri. Maneno yenu ni matamu. Karibuni, wapendwa. 
Lakini mmetuletea nini cha kula? Fisi wana njaa. 
Wanahitaji nyama!"

Punda sasa waliogopa sana. "Hebu tutoroke," mmoja wao alisema. Mwingine alijibu, "Hatuwezi. Fisi watatukimbiza."

Punda mzee alishauri, "Tumekuja kuonyesha heshima zetu kwenu. Tunasikitika kwamba mtoto wenu amefariki. Tutaomba Mungu awafariji. Sasa lazima turudi nyumbani kwetu."

Fisi walisema, "Subiri! Hamuwezi kuondoka. Lazima mtupatie kitu cha kula. Tukatieni midomo yenu."

Punda waliangaliana. "Pengine tukiwakatia midomo yetu, watatuachilia twende." Waliwaza.

Fisi walikata midomo ya punda wakala.

Kwa mara nyingine, punda waliomba kuruhusiwa kuondoka.

"Ndugu zangu, mtawaacha hawa punda waende?
Waangalieni! Tunaweza kuyaona meno yao! Wanatucheka!"

Fisi waliwarukia punda wakawaua halafu wakaanza kuwala.

Kabla punda mzee kufa, aliwatazama fisi akasema, "Fisi waovu, tulikuja kwa wimbo kuwafariji lakini tulikosea! Mkiwa na njaa, msitafute sababu ya 
kuwala marafiki zenu!"

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, Simba alikuwa mwenye nguvu aliyeogopwa kuliko wanyama wote. Angeweza kuwashika wanyama wengine na kuwala. 

Asubuhi moja alipokuwa akitafuta kifungua kinywa, alinaswa katika mtego wa mwindaji.

Simba alipiga mayowe kwa uchungu. Alivuta ili kujinasua kutoka mtegoni. Mtego ulinasa mguu zaidi kila alipovuta. 

Mwishowe, Simba alipokuwa amechoka na kuhisi uchungu, alikata tamaa.

Siku zilivyopita ndivyo Simba alichomwa kwa jua. Alihisi njaa na kiu na wala hakuwa na mwokozi. 

Alipozidi kuwa mnyonge aliwaza, "Nitakufa kwa njaa na kiu."

Asubuhi moja, Simba alisikia sauti kichakani. Alisikiliza na kuchunguza kwa karibu. 

Aliona Ngiri akitembea na mkwewe na watoto wakizungumza na kucheka. 

Ngiri na familia yake walikuwa wanaenda mtoni kunywa maji na kucheza topeni kabla ya jua kuwa kali.

"Ngiri, tafadhali niokoe kutoka mtegoni." Simba alimsihi. 

"Kamwe sitakuokoa! Wewe mnyama katili. Nikikuokoa utanila mimi na familia yangu kama kifungua kinywa." 

"Naahidi kamwe sitatenda jambo ovu kama hilo. Tutakuwa marafiki ukiniokoa," Simba alisema.

Ngiri alimwonea Simba huruma akasema, "Sifurahii ukihisi uchungu, kiu na kuwa karibu kufa kwa njaa." 

Kwa hivyo, alitumia pembe zake akavuta na kumwokoa Simba. 

Ngiri akampata rafiki mpya.

Simba alisema, "Asante sana rafiki yangu kwa kuniokoa. Ninaenda kwa familia yangu sasa, kwa heri." 

"Nenda salama rafiki yangu," Ngiri alimjibu. Ngiri alifurahi kwamba Simba alikuwa rafiki yake. 

"Familia yangu haitamtoroka tena simba," aliwaza.

Simba aliondoka akichechemea kwa unyonge. Alihisi njaa sana. 

Aliwaona watoto wa Ngiri wakicheza topeni. Alipowaangalia, alidondokwa na mate akafikiria, "Leo nina bahati."

Simba alimwita Ngiri, rafikiye mpya, "Nilikuwa nimenaswa mtegoni kwa siku nyingi bila chakula. Sina nguvu za kuwinda kwa sasa. Naomba unipatie mmoja wa watoto wako kuwa kifungua kinywa changu?" 

Ngiri alishtuka akasema, "Nilikuokoa kutoka mtegoni na sasa unataka kuwala wanangu?"

Simba alimjibu, "Nasikitika rafiki yangu, lakini nina njaa. Elewa kwamba ingawa mimi ni mnyonge sasa mimi ni mwenye nguvu kukuliko wewe." Simba alifungua kinywa chake na kuonyesha meno yake. 

"Usiponipatia mmoja wa watoto wako kwa hiari,  mwenyewe nitamchukua mmoja," alinguruma.

Ngiri alifahamu kuwa hakuwa na mbio wala nguvu za Simba. Hangeweza kuwalinda wanawe katika vita. 

"Nitakupatia mwanangu mmoja baada ya wewe kunionyesha jinsi ulivyonaswa mtegoni. Itanisaidia kumwokoa simba mwingine," Ngiri alisema.

Simba hangeweza kusubiri kumla ngiri mchanga. 

Aliuweka mguu wake ndani ya mtego kumwonyesha rafiki yake jinsi alivyonaswa.

"Ui!" Simba alinguruma. 

Ngiri alikaza mtego kwenye mguu wa simba akisema, "Aha! Nimekupata. Utakaa mtegoni kwa njaa na kiu tena. Tuone ikiwa meno yako makali na yenye nguvu yatakusaidia sasa."

Mkewe Ngiri aliwaambia wanawe, "Kimbieni! Inueni mikia yenu ili baba yenu awaone mlipo." 

Watoto wa Ngiri walikimbia kichakani kwa kasi walivyoweza.

Simba alihisi uchungu akamsihi Ngiri tena amsaidie,  "Nitakufanyia lolote utakalo ukiniokoa." 

Ngiri hakumwamini Simba. Alimwambia, "La! Sitathubutu, wewe ni muongo! Nitawaonya wanyama wengine pia ili waepuke na ujanja wako."

Ngiri aliwaona watoto wake na mama yao wakikimbia katika mstari mmoja. Waliinua mikia yao ili awaone. 

Ngiri alijiunga nao wakatorokea mahali pa usalama. 

Hii ndiyo sababu ngiri huinua mikia yao wanapokimbia kuhakikisha usalama wa kila mmoja wao.

------------------------------------------------------------



Odongo na Apiyo walisubiri kwa hamu likizo kufika.

Ulikuwa wakati wa kumtembelea bibi yao.

Waliposafiri, waliona milima, wanyama na mashamba.

Baada ya muda, Odongo na Apiyo walilala.

Walimkuta bibi yao akipumzika chini ya mti.

Bibi alicheza na kuimba. 

Watoto walimpatia zawadi zake.

Bibi alifurahi akawapa baraka zake.

Odongo na Apiyo walicheza na vipepeo na ndege.

Walipanda miti na wakacheza ziwani.

Walichoka sana wakalala kabla kumaliza chakula cha jioni.

Walimsaidia bibi kukusanya mayai na kuchuma mboga.

Bibi aliwafunza Odongo na Apiyo kupika vyakula tofauti.

Odongo aliwapeleka ng'ombe wa bibi malishoni. 

Waliila mimea ya jirani.

Walitembelea kibanda cha bibi sokoni.

Jioni, walimsaidia bibi kuhesabu pesa alizopata.

Hatimaye, likizo ilikamilika. 

Bibi aliwapakia chakula cha kula njiani.

Kabla ya kuondoka, walisema, "Bibi, njoo nasi."

Odongo na Apiyo walimkumbatia bibi. 

"Kwaheri, bibi," walisema.

Maisha yapi ni mazuri? 

Ya mjini au ya kijijini?

------------------------------------------------------------



Mimi ni Maria.

Huyu ni mama yangu.

Huyu ni mtoto.

Huyu ni baba yangu.

Huyu ni kaka yangu.

Huyu ni dada yangu.

Huyu ni bibi yangu.

Huyu ni babu yangu.

Huyu ni mjomba wangu.

Huyu ni shangazi yangu.

Hii ni familia yangu.

------------------------------------------------------------



Kadogo na Juma ni marafiki.  

Wanapenda kukimbia pamoja kila siku.

Siku moja, Juma alisema, "Tukimbie kwa ajili ya bara letu, tuhimize umoja wa Afrika!" 

"Sawa, twende!" Kadogo alikubaliana naye.

Waliamua kuibeba kurunzi ya umoja kwenye safari yao. 

Walianzia mbio hizo katika upande wa kusini jijini Cape Town.

Kutoka Afrika Kusini, walielekea kaskazini kupitia magharibi mwa bara. Walipitia Namibia, Angola,  Kongo na Cameroon. 

Waliamua kupumzika jijini Abuja.

Wakimbiaji kutoka Afrika Magharibi walijiunga nao nchini Nigeria. 

Waliendelea pamoja wakiufuata Mto Niger.

Walipofika Mali, walikumbwa na upepo mkali. Juma aliwashinda wote kwa nguvu. 

Alijitwika jukumu na kuwaongoza salama.

Walipofika pwani ya Guinea, jijini Conakry, walikuwa wamejaa vumbi. Walienda kuogelea baharini. 

Baadaye waliamua kuendelea na mbio zao kwenda Morocco kupitia Senegal na Mauritania.

Jijini Casablanca, wakimbiaji waliungana na vijana wenzao wakacheza ufukoni. 

Halafu, wakaelekea Afrika Kaskazini.

Walikimbia kupitia Algeria na Libya wakapumzika Misiri ili wazitembelee piramidi. 

Baadaye, waligeuka kusini wakaufuata Mto Nile kuelekea Uganda.

Walipita kwenye jangwa na mbuga za kitaifa. Vijana zaidi walijiunga nao jijini Kampala. 

Kutoka Kampala, kikundi hicho kilielekea pwani ya Kenya.

Walipofika jijini Mombasa, waliketi ufukoni wakala wali wa nazi kwa samaki. 

Juma alisema, "Hebu tuipeleke kurunzi ya umoja Mlimani Kilimanjaro."

Hata hivyo, Juma alikuwa amechoka. Walipokuwa njiani wakielekea Tanzania, alianguka chini. 

Wakimbiaji wenzake walizikatiza mbio zao wakarudi nyuma kumsaidia Juma.

Juma alimpokeza Kadogo kurunzi akisema, "Ibebe kurunzi hii hadi Mlimani Kilimanjaro. Hakikisha umewasha mwale wa umoja wa Afrika."

Watu waliwashangilia wakimbiaji wakisema, "Ninyi ni mashujaa wetu." 

Baada ya kuwasha mwale wa umoja Mlimani Kilimanjaro, walirejelea mbio kuelekea kusini mwa Afrika.

Walipofika Malawi, walikatiza mbio zao. Wakaenda kuogelea katika Ziwa Malawi. 

Kadogo alimwambia Juma, "Tumekimbia kutoka kusini hadi kaskazini, mashariki hadi magharibi. Safari yetu inakaribia kukamilika."

Hatimaye, wakimbiaji wa umoja waliibeba kurunzi yao hadi nchini Zimbabwe. Umati wa watu ulikusanyika pale kushuhudia jambo hilo. 

"Mbio zimefana kweli!" Alisema Juma huku akitabasamu.

------------------------------------------------------------



Siku moja, Kobe alikuwa akitembea nyasini. 

Alichunguza mbele na kukodolea nyasi macho akamwona Konokono.

"Unatafuta nini?" Konokono alimwuliza. 

"Ninaitafuta nyumba yangu. Umeiona?"

Alijibu, "La, sijaiona, lakini nitakusaidia kuitafuta!" 

Konokono alipanda juu ya gamba la Kobe. 

Kobe alimbeba Konokono mgongoni mwake. Walitafuta, lakini hawakuiona.

Baada ya muda mfupi, walimwona Ndege. "Mnatafuta nini?" Ndege aliwauliza. 

"Ninatafuta nyumba yangu. Umeiona?" Kobe alisema. 

"La, sijaiona, lakini nitakusaidia kuitafuta!" Ndege akajibu.

Ndege aliyapapatua mabawa yake na kupaa. "Unakwenda kwa kasi sana." Kobe alilalamika. 

Ndege akamwambia, "Samahani, wacha nami pia niruke juu ya gamba lako."

Kobe aliwabeba Konokono na Ndege juu ya gamba lake. 

Walitafuta bila kuona ishara ya nyumba ya Kobe.

Walipoendelea, walimwona Bunzi. "Mnatafuta nini?" Bunzi aliwauliza. 

"Ninatafuta nyumba yangu. Umeiona?" Kobe alijibu.

Bunzi alisema, "La, sijaiona, lakini nitakusaidia kuitafuta!" 

Aliruka mgongoni mwa Kobe. Kobe aliwabeba Konokono, Ndege na Bunzi. 

Walitafuta, lakini hawakuona nyumba yoyote.

Hatua chache, walikutana na Panya. Alikuwa akitengeneza shada zuri la maua. "Unatafuta nini?" Panya aliuliza. 

"Natafuta nyumba yangu. Umeiona?" Kobe alisema.

Panya alijibu, "La, sijaiona, lakini nitakusaidia kuitafuta!" Aliruka mgongoni mwa Kobe. "Subiri,  siwezi kuacha maua yangu." 

Panya alijinyoosha, akayakusanya maua yake huku Kobe akimsubiri.

Kobe aliendelea kutembea akiwabeba Konokono, Ndege, Bunzi na Panya mgongoni mwake. Walitafuta, lakini hawakuipata nyumba ya Kobe. 

Upepo uliyapeperusha maua ya Panya. Kobe alikuwa amechoka sana. Akasema, "Ninyi ni wazito."

Upepo uliongezeka. Anga likabadilika likawa jeusi. "Ah, iwapi nyumba yangu?" Kobe aliuliza. Punde, radi ilinguruma milimani na umeme ukaangaza. 

Mara mvua ikaanza kunyesha. "Ah, iwapi nyumba ya Kobe?" Konokono, Ndege, Bunzi na Panya waliuliza.

Upepo ulizidi kuvuma na kuvuruga. 

Ghafla, upepo uliwapeperusha wote kutoka mgongoni mwa Kobe.

Mvua ya mawe ikaanza kunyesha. Kwa uoga, Kobe alijikunja na kuingia ndani ya gamba lake. 

Mle ndani mlikuwa joto. "Kumbe, hii ndiyo nyumba yangu!" Kobe aliwaza.

Konokono, Ndege, Bunzi na Panya walijikusanya chini ya gamba la Kobe.

Wakatambua, "Ah, hii ndiyo nyumba ya Kobe!"

------------------------------------------------------------



Wadudu huishi katika nyumba tofauti. Baadhi ya wadudu huishi pamoja katika makundi makubwa na wengine huishi peke yao.

Kitabu hiki kinauhusu Naeku na Naserian - mchwa wawili ambao ni dada wanaoishi katika nyancha za kusini mwa Kenya.

Dada hao wanaishi katika koloni pamoja na takriban mchwa wengine 80,000.

Koloni ya mchwa huishi katika kiota ambacho hutengenezwa kwa udongo. Kiota hiki kinaweza kuwa chini ya ardhi, juu ya ardhi, au pote pawili.

Sehemu ya kiota tunayoweza kuiona juu ya ardhi ni kilele. Kilele hiki kina urefu wa kati ya mita mbili hadi mita tano juu ya ardhi.

Mchwa katika koloni hufanyia kikundi kizima shughuli tofauti. Naeku na Naserian ni mchwa wafanyakazi. Mchwa wote wafanyakazi ni wa kike. "Sisi ndio wajenzi na wahandisi!" Naeku anasema.

Mchwa wafanyakazi hujenga na kudumisha kiota cha mchwa. Naserian anasema, "Tunajenga miundo mikubwa iliyo tata."

"Hebu tueleze jinsi tunavyojenga nyumba zetu," Naeku anapendekeza. ''Tunaanza kwa kuchimba vichuguu ndani ya ardhi."

Naeku anakatiza, "Tunatumia taya zetu zenye nguvu kuchimba ardhini. Tunaweza kuhamisha udongo mwingi sana!''

"Ili kuhakikisha kuwa kuta za vichuguu hivyo ni imara, tunavifunika kwa mchanganyiko wa mate na udongo unaoshikamana," Naserian anasema.

"Mchanganyiko wa mate unapokauka, unakuwa mgumu kama udongo. Makazi ya mchwa yanaweza kudumu kwa muda mrefu sana," Naeku anaongeza.

"Tunatoa udongo tunaochimba na kutumia kujenga kilima juu ya ardhi. Kilima kawaida ni umbo la mviringo au umbo la koni, lenye vichuguu vingi," anasema Naserian.

"Baadhi ya vilima vya mchwa vinaweza kuwa na urefu wa mita tisa!" anasema Naeku.

Mchwa ni wadudu wa kijamii wanaoishi katika kikundi kikubwa. Wana majukumu tofauti katika kuunda na kudumisha koloni.

Mchwa wafanyakazi kama Naserian na Naeku huchimba na kujenga viota. Mchwa wanajeshi hulinda kiota.

Wafanyakazi na wanajeshi huenda nje kutafuta maeneo mapya ya kujenga viota.

Mchwa wauguzi wanatunza malkia na mchwa wachanga wanaoitwa viluwiluwi.

Kiota kina sehemu tofauti. Kuna vyumba vya malkia, vyumba vya viluwiluwi, na vyumba vya kuhifadhi chakula. Vichuguu vinaunganisha maeneo tofauti.

Malkia ndiye mchwa mkubwa zaidi na anaweza kuishi kwa muda mrefu zaidi.

Naserian anaendelea, "Tunajenga vichuguu au mashimo kwenda juu ili hewa safi iweze kupita ndani ya kiota."

Naeku anaongeza, "Mchwa wanahitaji hewa safi ili waishi." Naserian anaeleza, "Vichuguu au mashimo pia husaidia kudhibiti joto katika kiota ili kisiwe moto sana."

"Tuna bustani katika kiota chetu ambapo tunapanda uyoga. Tunakusanya vipande vidogo vya mimea na vifaa vingine vya asili, ambavyo tunatumia kukuza uyoga," anasema Naserian.

"Vizuri sana!" anashangaa Naeku. "Bustani za uyoga hulisha koloni nzima. Sisi ndio aina pekee ya mchwa wanaolima uyoga."

Koloni ya mchwa ina malkia na mfalme. Wafanyakazi hulisha na kulinda wanajamii hawa muhimu wa koloni.

Mchwa malkia kawaida huishi kwa kati ya miaka 20 hadi 30. Anaweza kutaga mamilioni ya mayai katika maisha yake.

Viluwiluwi huanguliwa kutoka kwenye mayai na kutunzwa na mchwa wauguzi.

Naserian anasema, "Jamii ya mchwa ina mpangilio mzuri sana. Kila mchwa huchangia uhai wa koloni nzima na ukuaji wake."

Naeku anaongeza, "Kila mmoja wetu ana kazi ya kufanya, na tunafanya. Mchwa hufanya kazi pamoja vizuri sana."

"Ndio," Naserian anakubaliana naye. "Sasa, hebu turudie ile kazi ya kuchimba!''

------------------------------------------------------------



Kila wiki ina siku saba:

Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Siku ninayoipenda ni Jumatatu. Ni siku ya kwanza ya wiki.

Huwa ninaenda shule siku ya Jumatatu.

Jumanne ni siku ya pili ya wiki. 

Inafuata baada ya Jumatatu.

Jumanne huwa tunacheza michezo tunayoipenda shuleni.

Jumatano ni siku ya tatu ya wiki. 

Iko katikati ya wiki.

Siku ya Jumatano huwa tunapaka rangi shuleni.

Baada ya Jumatano inafuata Alhamisi.

Alhamisi ni siku ya nne ya wiki.

Watoto wakubwa hutusimulia hadithi siku ya Alhamisi.

Ijumaa ni siku ya tano ya wiki. 

Ijumaa ni siku ya mwisho ya wiki kwenda shule.

Tunapenda kula sambusa siku ya Ijumaa.

Mchana, tukifika nyumbani huwa tunajitayarisha kwa wikiendi kuanza.

Jumamosi ni siku ya sita ya wiki.

Siku ya Jumamosi huwa tunaangalia katuni...

...na kwenda sokoni.

Jumamosi na Jumapili ni siku za kucheza na kupumzika.

Jumamosi huwa tunaenda sokoni kununua matunda ninayoyapenda sana.

Jumapili ni siku ya mwisho ya wiki. Ni siku ya mapumziko kabla ya kuanza wiki mpya.

Jioni huwa ninaandaa vifaa vyangu vya shule.

Wiki ina siku saba: 

Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

------------------------------------------------------------



Ninakoboa viazi.

Ninakata kabichi.

Ninakuna karoti.

Ninasafisha maharagwe.

Ninakata boga.

Ninakata mchicha.

Mama yangu anakata vitunguu.

Mimi sipendi vitunguu.

Hunitoza machozi vinapokatwa.

------------------------------------------------------------



Familia ya Zina ilikuwa yenye furaha. 

Binti wao wawili walijifunza kutoka kwa mama yao jinsi ya kupika na kutunza bustani.

Kila walipokula chakula cha jioni, waliongea kuhusu waliyotenda siku hiyo.

Baba aliwaonya wanawe kutoingia msituni
kabisa. Aliwaambia kuhusu kiumbe cha ajabu kilichoishi katika msitu huo. 

Alisema, "Kiumbe hicho ni kama sisi wawili pamoja!"

Siku moja, wasichana wale walikuwa wakicheza karibu na mto. Waliuzunguka mti, na ghafla, walikabiliana na kiumbe cha ajabu! 

Kiumbe hicho kilikuwa na macho mawili, mapua mawili, viganja viwili na mikono miwili.

Wakitetemeka kwa woga, walikimbia kuwaeleza ndugu zao walichokuwa wameona. 

Hata hivyo, wavulana hao hawakuwaamini, "Ni upuzi wa wasichana tu!" walisema.

Mwishowe, hamu iliwazidi. 

Wavulana hao waliwafuata dada zao wakaelekea mtoni ili kujionea wenyewe kiumbe hicho cha ajabu.

Walitafuta na kutafuta lakini waliona nyasi 
ndefu na miti peke yake. 

Waliposikia kelele, walitazama juu.

Juu ya mti waliona kiumbe cha ajabu wasichokuwa wameona tangu. Kilikuwa na macho mawili, mapua mawili, viganja viwili na mikono miwili. 

Kila sehemu ya mwili ilikuwa mbili mbili kinyume na wao waliokuwa na moja.

Watoto hao waliogopa, wakakimbia kuwaambia wazazi wao. 

Muda mfupi baadaye, familia ya Zina nzima ilikuwa pale mtoni kukichunguza kiumbe hicho cha ajabu.

"Msiniumize!" Kiumbe hicho kilisema, huku kikijificha nyuma ya mti. 

Wakati huo, familia ya Zina iliweza kuona mguu mmoja, kiganja kimoja, mkono mmoja na jicho moja pekee.

"Mimi ni kama ninyi tu," kiumbe hicho kiliendelea kusema. "Tofauti kati yangu nanyi ni kwamba kila sehemu ya mwili wangu iliumbwa mbili mbili."

Hivyo ndivyo familia ya Zina iligundua kwamba kiumbe hicho hakikuwa cha kuogopwa. 

Ilikuwa tu hali iliyokuwa tofauti na yao.

------------------------------------------------------------



Katika msitu wa Miwa, aliishi Kima aliyehuzunika. 

Kila alipomzaa mtoto, aliaga dunia.

Uchungu wa kuwapoteza watoto ulimfanya Kima kuruka juu na chini. 

Angeruka kutoka tawi moja hadi nyingine huku akilia, "Kwi! Kwi! Kwi!"

Kima alihuzunika zaidi alipowaona kima wengine wakiwa na watoto wao.

Kima mwenye huzuni alikuwa na tabia ya kuketi juu ya tawi na kutazama juu! 

Siku zilivyopita, ndivyo Kima alilia zaidi na zaidi.

Baadaye, alimzaa mtoto mwingine. 

Aliamua kumpeleka njiani ili watu wote waliopita wamwone na kumtakia heri.

Siku moja, Kima alishuka kutoka mtini na kumweka mtoto wake njiani. 

Wakati huo, mwindaji mmoja alikuwa akirudi nyumbani. Alimwona mtoto wa Kima aliyelala kando ya njia.

Mwindaji huyo alimbeba mtoto wa Kima na kumpeleka nyumbani kwake. 

Alipofika, kila mmoja wa wanawe watatu alitaka kumbeba mtoto wa Kima.

Walicheza na kuimba: 

Mtupe juu! 
Mtupe chini! 
Nitupie mimi! 

Mtupie yeye! Walimtupa mtoto wa Kima kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine.

Walipokuwa wakicheza na mtoto wa Kima, mama Kima alijificha mtini na kuwatazama. 

Alihofia kwamba mwanawe angekufa kama vile wale wengine walivyokufa.

Mke wa mwindaji aliwaona wanawe wakicheza na yule mtoto wa Kima. 

"Tahadharini wanangu! Hebu mleteni hapa. Mtamwangusha!" Akasema.

Alimshika mtoto wa Kima na kumbariki.

Kisha mke wa mwindaji alimweka mtoto wa Kima chini. Mama Kima akamchukua na kumbeba mtoto wake kifuani. 

Halafu akatoweka mtini. Hakumpoteza tena mtoto mwingine!

------------------------------------------------------------



Mbuzi, Mbwa na Ng'ombe walikuwa marafiki wakubwa. 

Siku moja walisafiri kwa teksi.

Walifika mwisho wa safari yao.

Dereva aliwauliza walipe nauli zao. 

Ng'ombe akalipa.

Mbwa hakuwa na kiasi kamili cha pesa, akalipa zaidi kidogo.

Dereva alikuwa anajitayarisha kumrudhishia Mbwa baki ya pesa zake.

Wakati huo, Mbuzi alitoroka bila kulipa chochote.

Dereva akakasirika sana. 

Akaondosha gari bila kumrudishia Mbwa baki ya pesa zake.

Hiyo ndiyo sababu, siku zote, Mbwa hulikimbilia gari. 

Nia yake ni kumpata dereva amrudishie baki ya pesa zake.

Mbuzi, anapousikia mlio wa gari, hutoroka. 

Yeye huogopa kushikwa kwa kukosa kulipa nauli.

Ng'ombe huwa hashughuliki gari linapokuja. 

Yeye huchukua muda kuvuka barabara.

 Anajua kwamba alilipa nauli yake kamili!

------------------------------------------------------------



Mamba ana meno makubwa. 

Wakati mwingi, mamba huishi majini.

Simba naye ana meno makubwa. 

Simba hula wanyama wengine.

Ng'ombe ana meno yenye nguvu. 

Ng'ombe hula nyasi, nafaka na majani.

Ndege hana meno.

Panya ana meno ya mbele makubwa.

Papa ana meno makali. 

Papa hula samaki wengine.

Zamani nilikuwa na meno mengi.

Lakini sasa sina mengi.

Maswali: 

1. Wanyama gani wana meno makubwa? 
2. Mnyama yupi hana meno? 
3. Kwa nini mtoto huyu hana meno mengi tena? 
4. Kwa nini wanyama wana aina tofauti za meno?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na mwanamume aliyeitwa Omar. 

Omar alikuwa na mke wake aliyeitwa Rachel.

Omar alikuwa akimlaumu mke wake kuwa hawezi kuzaa.

Hivyo aliamua kuoa mara ya pili. 

Alimuoa mwanamke aliyeitwa Katia.

Katia alifanikiwa kupata mtoto aliyeitwa Michael.

Mzee Omar alipompata mtoto wa kiume, alimdharau mke wake wa kwanza, Rachel.

Rachel alijisikia vibaya na akataka kujiua. Mfanyakazi mmoja akasema, "Mkubwa wangu, usifanye hivyo!"

Miaka 10 baadaye, Rachel alimpata mtoto wa kike aliyeitwa Rosita.

Rosita alipofikisha miaka 5, alikuwa na sauti nyororo. 

Hata hivyo, baba yake alimfungia na kumwambia, "Hauna sauti ya kuimba nyimbo zozote!" Rosita alisikitika sana.

Baada ya miaka 5, Rachel aliugua na mwishowe akafariki. 

Rosita alilia sana.

Siku moja, Rosita alisikia kuwa kutakuwa na mashindano ya kuimba. Aliandaa rinda jeupe. Alipendeza sana. 

Siku iliyofuata, Rosita alijiunga na waimbaji wengine. Alisubiri, na alipoitwa, aliimba wimbo ufuatao:

Lily alikuwa msichana mdogo, alihofia ulimwengu mkubwa, mpana. Alilelewa ndani ya kuta za ngome. Mara kwa mara alijaribu kukimbia. Na kisha usiku na jua kutua, alikwenda msituni. Akiwa na hofu sana, kwa kuwa peke yake!

Baba yake alisikia sauti nzuri ya binti yake. 

Alimuomba binti yake msamaha huku akilia na kusema, "Kuanzia leo nitakuruhusu kuimba nyimbo mbalimbali."

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na mwanamume mmoja aliyekuwa na wake wawili. 

Wake zake walipata watoto wasichana wawili, Adie na Adhoch. 

Watoto hao walipendana sana.

Adie alikuwa mwenye bidii, mkarimu na mwenye nidhamu. 

Adhoch naye alikuwa mvivu, mchoyo na mtovu wa nidhamu.

Adie alipendwa na walimu. Alipata zawadi nyingi kutokana na bidii yake. 

Adhoch hakupata zawadi yoyote. Mamake Adhoch alimwonea wivu Adie.

Mamake Adie aliugua na kufa. 

Adie hakupendwa na mamake wa kambo kama alivyopendwa na mamake mzazi.

Adie alizifanya kazi zote za nyumbani. Hakupata nafasi ya kujitayarisha kwenda shule. 

Adhoch alisoma na kucheza na wenzake.

Hata hivyo Adie alifanya vyema katika masomo yake shuleni. Alipita mitihani yake na kuendelea kupata zawadi. 

Hili lilizidi kumkera mamake Adhoch.

Siku moja, mamake Adhoch alimtaka Adie aende naye kuchota maji mtoni. 

Walipofika, mama alimwambia Adie achote maji safi mbali na ukingo wa mto. 

Mawimbi yalimbeba Adie hadi upande mwingine wa mto.

Mama aliporudi nyumbani, Adhoch alimwuliza, "Mama, Adie yuko wapi?" 

Mama alisema, "Anacheza na wenzake. Atakuja nyumbani baadaye."

Jioni, Adhoch alienda kumtafuta dadake. Alimwita, "Adie! Uko wapi?" 

Adhoch akasikia sauti ikisema, "Niko upande mwingine wa mto. Mama aliniacha."

Adie aliingia majini akimwita dada yake. "Adie uko wapi?" 

Alisikia jibu kama lile la kwanza, "Niko upande mwingine wa mto. Mama aliniacha."

Adhoch aliingia majini naye akabebwa ba maji hadi upande mwingine wa mto.

Mamake Adhoch alikuwa na huzuni sana. Alimpoteza Adhoch kwa sababu ya wivu. 

Alilazimika kuzifanya kazi zote peke yake.

------------------------------------------------------------



Juma anaishi mjini. 

Yeye ni Dereva wa gari la abiria.

Juma ni dereva stadi na mwenye heshima kwa wateja wake.

Siku moja, Kasim, ambaye alikuwa jirani yake alimpa kazi. 

Alitaka Juma awaendea wageni wake kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi. Wageni walikuwa wakitoka ng'ambo.

Kasim pia alimwambia awatafutie wageni wake hoteli safi na yenye mandhari ya kuvutia.

Wageni walipofika hotelini, waliagiza samaki. 

Walimwalika Juma kushiriki nao chakula cha mchana. 

Kasim pia alijiunga nao.

Alasiri siku hiyo, Kasim aliwapeleka wageni wake kwenye Mbuga ya Wanyama.

Juma alitaka sana kufika mapema kabla ya lango la Mbuga kufungwa. 

Ilimbidi aliendeshe gari lake kwa kasi sana.

Askari waliokuwa zamu wakaliona gari lake Juma likipita kasi.

Mgeni mmoja akaamka kutoka usingizi wa pono na kufoka kwa sauti kubwa, "Taratibu dereva! Utasababisha ajali."

Gari la polisi lililokuwa linawafuata likawafikia.  

Inspeka wa polisi akawaamurisha washuke chini.

Juma alijitetea, lakini wapi! Alikuwa amevunja sheria za barabarani. 

 Waliandamana mpaka kituo cha polisi.

Juma alitozwa faini na akaomba mshamaa. Askari wakamrejeshea gari lake. 

Kasim akaomba msamaha kwa wageni wake. Wakaanza safari tena kuelekea Mbugani.

Walifika Mbugani saa kumi na mbili unusu. Lango la Mbuga lilikuwa halijafunguliwa. 

Juma aliwaomba wageni wa Kasim msamaha.

Tangu siku hiyo, Juma huliendesha gari lake kwa kuzingatia sheria za barabarani.

------------------------------------------------------------



Watu hawa wana maoni tofauti.

"Walimu ni muhimu zaidi. Mnatuhitaji sisi kujifunza," mwalimu anasema.

"Wajenzi ni muhimu. Mnahitaji nyumba," mjenzi anasema.

“Seremala ni muhimu zaidi. Mnahitaji samani.”

"Madaktari ni muhimu zaidi. Mnahitaji matibabu."

"Wakulima ni muhimu zaidi. Mnatuhitaji kwa chakula."

"Wanafunzi ni muhimu zaidi!" Mwanafunzi anasema.

"Nyote mlikuwa wanafunzi kwanza!"  

Wote wanakubaliana.

------------------------------------------------------------



Kuku na Jongoo walikuwa marafiki. 

Walitembea pamoja kila mahali.

Siku moja, walienda kucheza mpira wa miguu.

Kuku alisema, "Nitakuwa golikipa." 

Jongoo alianza kucheza mpira.

Jongoo alicheza mpira kwa ustadi. 

Alifunga bao la kwanza.

Kuku alishangaa akasema, "Haiwezekani!" 

Alikasirika sana.

Kuku alifikiria namna ya kumwadhibu Jongoo.

Aliamua kummeza.

Kuku alikutana na Mamake Jongoo.

"Wapi mwanangu?" Mamake Jongoo aliuliza.

Jongoo aliyemezwa alilia, "Mama nisaidie. Kuku amenimeza."

Kuku hakupendezwa na ladha ya Jongoo. 

Alihisi kichefuchefu.

Kuku aliwaza, "Nitafanyaje?"

Aliamua kukohoa ili amteme Jongoo.

Jongoo alipotemwa, alitafuta njia ya kutoroka.

Hakuamini alichotendewa.

Tangu siku hiyo, urafiki kati ya kuku na jongoo uliisha.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na msichana aliyeitwa Kate.

Wazazi wa Kate walikuwa wanasayansi werevu. Walikuwa wakifanya kazi kwenye mradi wa juu wa siri katika maabara yao.

Mwanasayansi mwovu kwa jina Daktari Mpotovu, alitaka kujua siri hasa ya mradi huo wa siri.

Usiku mmoja, Daktari Mpotovu alimtuma mshiriki wake aliyeitwa Dan Mharibifu kuwateka nyara wazazi wa Kate.

Dan aliwashika wazazi. Karibu pia ampate Kate. Lakini, kwa vile Kate alikuwa mdogo na mwepesi wa mbio, aliweza kutoweke.

Kate alikimbia kama umeme.

Kate alijikuta katika msitu mweusi uliozungukwa na miti.

Alipotazama juu, aliteleza na kuanguka!

Alianguka chini, chini, chini, na kugonga kichwa chake.

Kate alipoamka, alikuwa katika chumba kizuri  kilichokuwa na Runinga kubwa.

"Hujambo Kate," mtu aliyekuwa kwenye Runinga alisema. 

"Mimi ni ajenti wa siri wa Dunia Nzuri! Wewe sasa ni ajenti wetu mpya wa siri! "

Maneno hayo yalimfanya Kate kuwa jasiri kama mbwa mwitu.

Ajenti Kate aliuacha mti kupitia mlango wa ndani kwenye shina.

Alikimbia hadi mahali Daktari Mpotovu aliishi na kumtaka wapigane vita vya watu wawili.

Walipigana kwa siku mbili, hadi Kate akawa mshindi!

Baada ya wazazi wake kurudi nyumbani, Kate alikwenda kumtafuta yule mtu aliyekuwa kwenye Runinga.

Aliupata mti, lakini hapakuwa na mlango.

Kate alikaa chini ya mti na kuwaza.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na buibui aliyeitwa Pa Nase. Alihisi njaa sana akaamua kutafuta chakula. 

Alienda kwa rafikiye aliyekuwa akimpa masaada. Lakini rafikiye hakuwa nyumbani.

Pa Nase, alikuwa na wazo tofauti la kuweza kupata chakula. Alikumbuka kuwa mle kijijini, kulikuwa na ghala ambamo wanawake wa kijijini walikuwa wakihifadhi chakula chao.

Alinyatia akaingia katika lile ghala na kuiba samaki na ndizi.

Alipokuwa njiani akirudi, watoto waliona namna alivyotembea kwa njia isiyokuwa ya kawaida.

Wanawake walipojua, walimfuata Pa Nase kwa haraka.

Akiwa na mifuko iliyojaa, Pa Nase aliogopa akataka kukimbia.

Wanawake walimshika wakaamua kumuadhibu.

"Hebu tumsagie kwenye lile jiwe la kijijini," Yalol, mmoja wa wanawake alipendekeza.

Pa Nase alicheka kwa sauti akasema, "Babu yangu huishi kwenye lile jiwe. Kunisagia pale ni kama kunituma nyumbani. Asanteni!"

Wanawake waliamua kutomsaga.

"Tumtupe motoni," Betty akasema.

Pa Nase alicheka tena, akasema, "Bibi, yangu anayenipenda sana, ni mwenye mioto yote. Kunitupa motoni ni kama kunituma nyumbani. Asanteni!" Wanawake waliudhika sana.

"Tukijaze kikapu matunda, tumweke ndani kisha tukitupe mtoni," Yabana alipendekeza. Pa Nase alilia, "Mkifanya hivyo, mtaniua."

Wanawake walifurahi. Walikijaza kikapu matunda, wakamweka ndani kisha wakakitupa mtoni.

Pa Nase alipofika katikati ya mto, alisherehekea. Aliyachukua baadhi ya matunda na kuyala huku akiwacheka wale wanawake.

Wanawake wale walijua kuwa Pa Nase alikuwa amewadanganya. 

Walijaribu kumnasa, lakini hawakuweza kwani Pa Nase alisombwa haraka kwa maji.

Pa Nase alisahau kuwa kulikuwa na wavu sehemu ya chini ya mto. Alinaswa kwenye wavu ule akawa ametegwa.

Hakuna aliyeenda kumsaidia.

------------------------------------------------------------



This is Matende. 


Huyu ni Matende.

Matende cries all the time. 


Matende hulia kila wakati.

When his mother feeds him, Matende cries. 


Mamake anapomlisha, Matende analia.

When Matende is put down to rest, he still cries. 


Matende anapolazwa chini kupumzika, bado analia.

When his mother changes his nappies, Matende continues to cry. 


Mamake anapobadilisha pampa, Matende anaendelea kulia.

When his mother carries him on her shoulder, Matende cries more. 


Mamake anapombeba begani, Matende analia zaidi.

When he falls asleep, Matende looks as if he is about to cry. 


Anapopatwa na usingizi, Matende anaonekana kuwa ataanza kulia.

Matende's mother looks at her son. She does not know what is wrong with him. 


Mamake Matende anamtazama mwanawe. Hajui kinachomsumbua.

------------------------------------------------------------



Ninampenda mwalimu wangu.

Yeye ni mrembo mno. Ni mwalimu mzuri. 

Ni mtu mwema na mwenye subira.

Alivyosuka nywele zake zinapendeza sana.

Amezipamba na shanga za rangirangi.

Shanga zake ni za rangi ya kijani, nyeupe, nyekundu,  na manjano.

Mama, tafadhali nisuke nywele zangu ziwe kama za mwalimu wangu?

Ningekuwa na umri mkubwa, ningezipamba nywele zangu kwa shanga.

Nitakua sawa kabisa na mwalimu wangu!

------------------------------------------------------------



Katika mwaka mmoja, kipindi cha ukame kilikuwa kirefu sana. Kiangazi kikawaathiri wanyama wote. Mito yote ikakauka ila Mto wenye Baraka.

Wanyama wakahisi kiu kikubwa wakaamua kukutana ili watafute suluhu.

Ngamia alikuwa wa kwanza kuzungumza, "Kama mnavyojua, tuna kiu kikubwa na mito yote imekauka ila Mto wenye Baraka. Lakini mto huo uko mbali sana. Je, tufanyaje?"

Farasi alitoa pendekezo, "Baadhi yetu tunaweza kwenda kwenye Mto huo wenye Baraka. Tutaweza kuyanywa maji na kisha tuwaletee wengine."

Ng'ombe alijibu, "Ni mbali sana. Tutakaporudi, wale tutakaokuwa tumewaacha nyuma, watakuwa wamefariki."

Mbuzi aliruka juu kisha akasema, "Meee, meee! Mimi pia nitaenda kwenye Mto wenye Baraka."

Jimbi naye akasema, "Koor, kor kor kor! Pia mimi nitaenda kwenye Mto wenye Baraka."

Haikuwa rahisi kwenda huko. Aliyekuwa nyuma ya wote, alikuwa Kanga. Baada ya kutembea kwa muda mrefu, Kanga alisema, "Rafiki zanguni, siwezi tena kuendelea kwenda kwenye Mto wenye Baraka." 

Jimbi akammeza Kanga.

Waliendelea na safari tena. Muda mfupi baadaye, Jimbi akasema, "Tafadhali, nimechoka. Siwezi tena kuendelea kwenda kwenye Mto wenye Baraka."

Kondoo akammeza Jimbi.

Safari ilipoendelea, Kondoo alichoka kisha akasema, "Nimechoka. Sitaki tena kuendelea kwenda kwenye Mto wenye Baraka."

Mbuzi akammeza Kondoo.

Punde tu, Mbuzi naye alichoka na hakutaka kuendelea kuendelea kwenda kwenye Mto wenye Baraka. Farasi aligeuka na kummeza Mbuzi.

Farasi alipochoka, Ng'ombe alimmeza.

Sasa walikuwa wamebaki Ng'ombe na Ngamia peke yao. Waliendelea na safari hadi Ng'ombe alipochoka. 

Ilimbidi Ngamia ageuke na kummeza Ng'ombe.

Ngamia alipobaki peke yake, alijitahidi ili aufikie Mto wenye Baraka. Ni yeye tu ndiye angeweza kuwaokoa wengine.

Alikuwa amechoka mno.

Hatimaye, Ngamia aliwasili kwenye Mto wenye Baraka na kulala chini. Kisha akamtapika Ng'ombe.

Ng'ombe akamtapika Farasi. Farasi akamtapika Mbuzi.

Mbuzi akamtapika Kondoo. Kondoo akamtapika Jimbi naye Jimbi akamtapika Kanga.

Na hivyo ndivyo wanyama wote walivyofaulu kuyanywa maji kutoka Mto wenye Baraka.

------------------------------------------------------------



Zama anajitayarisha kwenda shule.

Baba anapika uji wa kiamsha kinywa.

"Mama hutayarisha uji mzuri zaidi," Zama anasema.

Uji unampa Zama nguvu za kucheza shuleni.

Uji uko tayari.

Baba anaongeza maziwa kwenye uji kwa upendo.

"Baba, ninafikiri uji huu unahitaji sukari zaidi," Zama anasema.

"Uji wa mama una ladha kuliko wa baba," Zama anawaza.

"Baba, tafadhali naweza kupata sukari zaidi?" Zama anauliza.

Baba anamwongezea Zama 'sukari'.

"Wui! Baba! Umeweka chumvi badala ya sukari!" Zama analalamika.

"Baba, je, mama atarudi lini nyumbani?" Zama anauliza.

------------------------------------------------------------



Rafiki yangu Dennis aliniita.


"Njoo umwone mbwa wangu mpya," Dennis alisema.

Mbwa alikuwa na madoa meusi na kichwa kikubwa.

Alinitisha!

Nilihofia kwamba angeniuma.

Mimi na Dennis, tulimpeleka mbwa huyo mpya matembezi.

Mbwa aliutikisa mkia wake.

Alibweka!

Kisha alinikojolea!

Alikikojolea kiatu changu!

Piu!

Dennis aliichukua karatasi na kufuta mkojo.

Nilihisi kwamba Dennis alikuwa rafiki mzuri kwangu.

------------------------------------------------------------



Ninapomaliza kuoga kwa maji moto, mwili wangu huwa majimaji na kuhisi baridi. 

Ninajua anayesababisha mwili kuhisi baridi. Vayu, upepo!

Kwenye kikombe kuna maziwa moto sana. Baada ya muda, maziwa yanapoa. 

Ninajua anayesababisha jambo hili kutendeka. Vayu, upepo!

Pazia za dirisha zinapapatika polepole zikinigusa uso. 

Ni nani husababisha jambo hili kutendeka? Vayu,  upepo!

Ninaona radi. Mawingu meusi yananikaribia. 

Ninajua anayesababisha jambo hili kutendeka. Vayu, upepo!

Matawi yanayumbayumba na majani yanapepea. Maua yanadondoka kutoka mtini. 

Ninajua anayesababisha haya yote. Vayu, upepo!

Tunapocheza nje, tunanukia pipi anazotayarisha mama. 

Ninajua anayesababisha hili kutendeka. Vayu,  upepo!

Bilauri iliyokuwa dirisahani, imeanguka na kuvunjika. Namshukuru Mungu haikuniangukia. Ninajua aliyesababisha ukatili huu. Bila shaka ni Vayu, upepo!

Firimbi imepulizwa. Gari la moshi linafika kituoni. Siwezi kuliona, lakini nausikia mngurumo wake. 

Ninajua aliyesababisha haya. Vayu, upepo!

Haonekani. Hasikiki. Hufanya kazi zote kisirisiri. Anaweza kuwa ni nani? 

Mimi ninamjua! Vayu, upepo!



------------------------------------------------------------



Hapo zamani, paka na panya walikuwa marafiki.

Panya walianza kupoteza baadhi ya jamaa zao.

Panya mmoja mzee alisema, "Nadhani paka wanatula."

Akina mama waliwaambia watoto wao, "Kueni waangalifu. Msiende nje."

Panya wote walikuwa waangalifu. 

Waliketi ndani ya mashimo yao.

Paka walianza kuwa na njaa. 

Waliuliza, "Panya wako wapi?"

Paka waliwatembelea panya.

Walitaka kupanga harusi kati yao.

Walisema, "Tungependa binti wenu mmoja aolewe kwa mvulana wetu."

Panya waliwaambia paka, "Mnadanganya. Mnataka kutula."

Mwishowe, walikubali kuwa na harusi kati ya wanao.

Paka walirudi nyumbani kwa furaha.

Walilamba midomo yao.

Siku ya harusi, panya walikuwa waangalifu sana.

Paka waliwasili wakiimba wimbo wa harusi.

Wimbo ulisema, "Washikeni muwale."

Panya mzee alianza kuimba, "Kimbieni, panya, kimbieni."

Panya mzee aliwaambia paka, "Sisi nanyi si marafiki."

------------------------------------------------------------



Ilikuwa Jumamosi asubuhi. Maya, Dama na Dominic walikuwa wakimsaidia Mama Koki katika bustani yake ya mboga. Watoto hao walikuwa wakipalilia na kunyunyizia mboga maji. Baadaye, walichuma mboga zilizokomaa. Kila mmoja wao angepeleka nyumbani stroberi, mchicha na karoti.

Mama Koki alipenda kuwaandalia watoto sherehe ndogo walipomsaidia. Huwapatia keki, chokoleti, au peremende zinazofanana na nyoka. Wakati mwingine aliwapatia matofaa, pea au machungwa. Mama Koki alikuwa na sharti moja tu. "Wagawe yote sawa!" Watoto walijua kuwa ni lazima wagawane kila kitu walichopatiwa kwa kiasi sawa.

Mama Koki alioka keki na watoto walisubiri kupatiwa ili wagawane. "Hii hapa keki!" Mama Koki alisema akitabasamu. "Kumbukeni sharti kwamba kila mmoja lazima apate kiasi sawa. Gaweni sawa! Mspigane!"

Maya alikuwa wa kwanza kujaribu kugawa keki. Alitumia kisu kuweka mistari juu ya keki. Wengine walimtazama. "Nitakata sehemu tatu zilizo sawa!" Maya alisema akiwaonyesha.

"Hapana!" Dama alikataa. "Kipande cha katikati ni kikubwa zaidi!" Dominic pia alitikisa kichwa. Maya alicheka kisha akamwambia Dama ajaribu kugawa.

"Nipe kisu nikate. Hii ni kazi rahisi!" Dama alisema. Kwanza alifuta mistari aliyoiweka Maya kisha akajlamba vidole.

Dama alianza kwa kugawa kutoka juu hadi chini na kutoka upande mmoja hadi katikati. "Tazama, hizi ni sehemu tatu!" 

Maya na Dominic walilalamika pamoja, "Sehemu hizi tatu si sawa!"

"Gawanya sawa! Lazima kila kipande kiwe na ukubwa ulio sawa na umbo sawa," Dominic akaongeza. 

Dama akajibu, "Dominic, si ujaribu? Nina hakika hutaweza!"

"Keki hii ingekuwa umbo la mraba au pembe nne, ingekuwa rahisi kugawa!" Dominic alisema. "Ingekuwa rahisi pia tungegawana tukiwa wanne." Maya aliongeza kusema.

Wakati huo, Dominic alikumbuka gari la babake. Lilikuwa na alama ya mistari inayowezesha kugawa sehemu tatu zilizo sawa. Akasema, "Najua tutakavyogawa."

Dominic akachora mistari mitatu juu ya keki. Keki ingekatwa kufuata mistari hiyo, ingekuwa vipande vitatu vilivyo sawa.

Dama alisema, "Umetushangaza sana Dominic. Umewezaje kuhakikisha umegawa vipande sawa?"  

Dominic alitabasamu. Hakutaka kuwaambia siri yake.

Wakati huo, Mama Koki alitoka ndani ya nyumba akiwa amebeba bilauri za sharubati. "Mama Koki, Dominic amepata njia ya kukata keki vipande vitatu vilivyo sawa," Maya alimwambia. 

"Hongera Dominic, umefaulu kugawa sehemu tatu zilizo sawa! Sasa ni wakati wa kwenda nyumbani," Mama Koki aliwaambia.

Kisha Maya alikata keki taratibu kufuata mistari iliyochorwa na Dominic. Watoto walihakikisha kwamba sehemu zote zilikuwa sawa. Kila mmoja akaiweka keki yake tayari kwenda nyumbani.

Babake Dominic alipowasili kuwachukua watoto, Dominic alimlaki akitaka kumweleza jinsi alivyofaulu kuigawa keki vipande vitatu vilivyo sawa.

Andika hapa tafsiri ya maumbo haya.

------------------------------------------------------------



Fana na familia yake wanaishi mjini.

Fana ana paka, kuku wawili, mbuzi na njiwa.

Siku moja Fana aliwaona watoto wakiwarushia njiwa mawe.

Fana alikimbia akisema, "Acheni kutupa mawe."

Fana aliwachukua wale njiwa akawapeleka nyumbani.

Aliwalisha. 

Aliwaambia wazazi vile alivyowaokoa.

Fana na wazazi wake waliwapeleka njiwa kutibiwa.

Fana huwaambia wenzake, "Wanyama ni marafiki zetu. Tunawalinda."

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na kijana aliyeitwa Kiongozi. Kiongozi alikuwa mtoto wa Kwanza na wa kipekee wa Mzee Shangari. 

Kiongozi alikuwa mtoto mtulivu na alimsaidia baba yake kuuza kwenye duka lao kubwa.

Siku moja, rafikiye Musa, alikuja kununua kofia. Alimwambia Kiongozi amtafutie kofia nzuri ya kupendeza. 

Kiongozi alimwuliza, "Unaenda wapi na kofia hii unayotaka kununua?" 

Musa alimwambia, "Mimi na familia nzima tunaenda mjini."

Humo dukani hapakuwa na kofia. Kwa furaha, Kiongozi alienda katika chumba cha baba yake. Aliichukua kofia aliyoipenda sana Mzee Shangari na kumpa Musa. 

Musa alienda nyumbani akiwa amejawa na furaha tele moyoni mwake.

Mzee Shangari aliporudi jioni, aligundua kwamba kofia yake haikuwepo. 

"Mwanangu, umeiona kofia yangu ya maajabu?" aliuliza Mzee Shangari. 

"Ndiyo baba, nilimpatia rafiki yangu Musa," alijibu Kiongozi. 

"Eti nini?" Mzee Shangari alianguka.

Mzee Shangari alikuwa amepewa kofia hiyo na baba yake. Ile kofia ilikuwa imebeba bahati yake ya maisha. 

Kwa hivyo, haikufaa kupatiwa mtu mwingine isipokuwa tu mtoto wake.

Angempokeza mtu mwingine ile kofia kungetokea bahati mbaya na kufanya familia kuangamia. 

Kusikia hivyo, Kiongozi alikimbia haraka na kumpa Musa kofia nyingine. Alimwomba babake msamaha.

Mzee Shangari alianza kumuelezea mwanawe kuhusu ile kofia ya maajabu. "Watu walioichukua bila kujua, walipata madhara na kuugua maradhi yasiyopona." 

Mzee Shangari aliendelea kumsimulia jinsi babake aliaga dunia.

"Babu yako alikuwa Mzee mwenye kufanya miujiza." 
Mzee Shangari alichukua kofia ile na kuiombea ili isisababishe madhara yoyote. 

Kutoka hiyo siku, Kiongozi alikoma kutenda jambo lolote bila kuulizia mawaidha.

------------------------------------------------------------



"Ah, la!"

"Lulu, wakati wa kwenda umefika," Mama anaita.

Lulu yuko wapi?

Je, yuko chini ya sofa?

Je, yuko nyuma ya pazia?

Lulu yuko wapi?

Je, yuko karibu na jiko?

Je, yuko katika kabati?

"Lulu, wakati wa kwenda umefika! Uko wapi?" Mama anaita.

"Wewe ndiye huyu sasa!" Mama anasema.

"Sitaki kwendaaa!"

"Ni lazima twende," Mama anasema.

"Lakini, ninapenda hiki!"

"Hebu twende sasa."

"Lakini..."

"Ninapenda hiki kweli!"

"Na hiki pia!"

"Na hiki vilevile!"

"Hata na hiki!"

"Tazama, unarejesha vitabu na kuomba vingine zaidi," Mama anasema.

"YEE!"

Lulu yuko wapi sasa?

------------------------------------------------------------



Bi kizee mmoja alikuwa na kuku na Jogoo mzee.

Mjukuu wake alimtembelea. Aliamua kumchinja yule Jogoo mzee.

Jogoo alitorokea jijini ili kujiokoa.

Njiani, Jogoo alimkuta Paka. Alikuwa akitoroka kutoka kwa mkubwa wake.

Jogoo na Paka walimkuta Mbwa akitoroka pia.

Farasi aliyekuwa akitoroka, alijiunga nao.

Wanyama hao waliwaona wezi ndani ya nyumba.

Walitaka kuwafukuza wale wezi. Waliimba kwa sauti ya juu.

Wezi walitoroka. Wanyama walikula chakula chote walichopata mle nyumbani.

Wezi waliamua kurudi baadaye. Lakini, wanyama waliwavamia.

Wezi walitoroka wakaenda zao kabisa.

Wanyama waliishi pamoja katika nyumba ile kwa furaha.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani palikuwa na Mzee Kobe. Aliishi peke yake kwenye nyumba ya matope. 

Siku Moja alihisi njaa sana na kwa vile alivyopenda maembe aliamua kwenda kuyatafuta. Jua nalo lilikuwa limewaka kweli kweli.

Alipokuwa njiani, aliona miti mitatu. Mti mmoja ulikuwa wa maembe mabivu. 

Alipoyaona akatabasamu. Papo hapo akaamua kuyaendea.

Alipanda juu ya mti akitarajia kuyachuma yale maembe ili ayale. 

Halikuwa jambo rahisi kwa Mzee Kobe kuukwea ule mti.

Baada ya kupanda juu, alijishikilia kwenye tawi la ule mti. 

Kobe huyu alikuwa na uzito kupita kiasi. Tawi halikustahimili uzito wake.

Tawi lile lilivunjika na Mzee Kobe akaanguka chini kwa mshindo pu! 

Ganda lake lililokuwa nyororo likapata nyufa.

Kobe alijutia kitendo chake cha kupanda mti. 

Alirudi nyumbani akiwa na njaa na hasira.

------------------------------------------------------------



Anzani anaweza kuona kundinyota wakati wa usiku.

Kundinyota ni kundi la nyota linalounda picha au muundo angani. Nyota hizi ziko mbali sana na dunia.

Anzani anataka kuwa mwanaanga atakapokuwa mkubwa. Wanaanga husafiri angani.

Hakuna hewa au maji katika anga. Wanaanga lazima wavae suti maalum ili kuishi.

Suti hizo zina oksijeni ya kupumua, na maji ya kunywa.

Suti hizo pia hulinda wanaanga dhidi ya baridi, joto na vumbi la anga.

Wanaanga husafiri katika vyombo vya anga, ambavyo ni magari yaliyotengenezwa kuruka angani.

Vyombo vya anga vina injini za roketi zenye nguvu sana.

Injini lazima ziwezeshe chombo kuruka mbali na dunia kabla ya kufika angani.

Injini za roketi huchoma mafuta mengi ili kurusha chombo cha anga za juu.

Wakati mafuta yanawaka, husababisha moto nyuma ya roketi.

Nguvu ya mafuta yanayochomeka husukuma roketi kwenda juu. Pia tunatumia roketi kurusha satelaiti angani.

Satelaiti nyingi husafiri kuzunguka dunia. Mwezi ni satelaiti ya asili.

Satelaiti zilizotengenezwa na wanadamu hutusaidia kwa shughuli kama vile utabiri wa hali ya hewa na utengenezaji wa ramani.

Satelaiti daima husonga katika mduara kuzunguka kitu kikubwa zaidi angani. Mwendo huu unaitwa obiti.

Anzani anajua mengi kuhusu nyota na sayari katika mfumo wetu wa jua na sayari zake.

Anajua majina ya sayari nane zinazozunguka jua.

Anajua kuna nyota moja tu katika mfumo wetu wa jua na sayari zake. Hiyo ni jua.

Vimondo pia huzunguka jua. Kimondo ni mwamba wa anga. Vimondo vingi ni chembe za vumbi ndogo, lakini vingine ni vikubwa.

Baada ya kuingia kwenye angahewa inayozunguka dunia, vimondo huanguka haraka na kuchomeka. Vinaonekana kama mipira ya moto au 'nyota risasi'. Mara kwa mara, kimondo huanguka ardhini!

Ardhi iko mbali na anga. Darubini inatusaidia kuona vitu vilivyo mbali zaidi kuliko macho yetu yanavyoweza kuona.

Anzani atasoma anga kwa darubini hadi atakapoweza kusafiri angani.

Ili kuwa mwanaanga, unapaswa kupenda masomo ya Sayansi, kama Hisabati, Jiografia, Fizikia, Kemia na hata Biolojia.

------------------------------------------------------------



















1. Umewahi kuona mtende?

2. Mtende una faida gani?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na mvulana aliyeitwa Jalo. Jalo aliwaasi wazazi wake.

Watu walijua kuwa mvulana huyo alikosa adabu.

Siku moja Jalo na mamake waliwatembelea jamaa zao kijijini.

Kabla wao kuondoka kurejea nyumbani, jamaa zao waliwapatia zawadi.

Walimpeleka Jalo na mamake kwenye bustani iliyojaa matunda. Kisha wakawaalika kula matunda yoyote waliyopenda.

Ila, hawakutakiwa kuchuma kutoka kwa mwembe.

Jalo aliona mwembe mkubwa uliokuwa na maembe mengi mabivu.

Jalo alishangaa kuyaona maembe mengi mabivu. Aliamua kuchuma moja.

Ingawa Jalo alikuwa ameonywa kutokula kutoka kwenye mwembe, alifanya hivyo.

Alisema, "Litakalofanyika, lifanyike. Ninataka kulila embe hili."

Mamake Jalo alimwonya tena. Hata hivyo, Jalo hakumtii.

Alipolila tu hilo embe, tumbo ilianza kunguruma.

Jalo aliendelea kuhisi vibaya akaanza kulia. Kichwa chake kilianza kuvimba.

Halafu, mwembe uliota kichwani kwake! Jalo aligeuka na kuwa mwembe.

Tangu wakati huo, kila mwembe huo unapoguswa, huimba, "Asiyewatii wazee, atajuta. Jalo ni mfano."

Hivyo ndivyo ilivyo. Wahenga husema, "Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu."

------------------------------------------------------------



Bwana Kio anaishi kijijini kwetu. 

Ana paka anayeitwa Safi.

Bwana Kio anapoenda kazini,  anauacha mlango wazi.

Safi anaketi mlangoni na kuilinda nyumba.

Mbwa wa jirani akiikaribia nyumba, Safi anamtisha. 

Yuko tayari kumkwaruza kwa kucha zake.

Mbwa anatoroka na kurudi kwao.

Jirani akiugusa malango wa nyumba, Safi anamwona.

Yuko tayari kumkwaruza.

Jirani anageuka haraka na kwenda zake.

Safi anapohisi njaa, anajua la kufanya.

Anaufunga mlango, kisha anaenda kula.

Safi anakula kutoka bakuli lake la bluu.

Anakipenda chakula chake sana.

Akimaliza, anaruka juu ya sofa na kulala.

"Purr! Purr! Purr!"

Bwana Kio anarudi nyumbani jioni.

Safi anajinyoosha kwa furaha na kumlaki.

Bwana Kio na Safi wanaketi sebuleni. 

Kila mmoja anasoma gazeti.

------------------------------------------------------------



Waridi na pilipili ni nyekundu.

Nyekundu inapendeza.

Ndizi na jua ni rangi ya njano.

Njano inang'aa.

Anga na bahari ni rangi ya bluu.

Bluu inatulia.

Ukichanganya nyekundu na rangi ya njano, utapata rangi ya chungwa.

Ukichanganya rangi za bluu na njano, utapata rangi ya kijani.

Ukichanganya nyekundu na rangi ya bluu, utapata rangi ya zambarau.

Nyekundu, rangi ya njano na rangi ya bluu ni rangi za msingi.

------------------------------------------------------------



Bunzi wawili wana miguu mingapi?

Ndege wanne wana mabawa mangapi?

Vifaru watatu wana pembe ngapi?

Ndovu watano wana pembe ngapi?

Mbwa saba wana masikio mangapi?

Nyani watatu wana mikia mingapi?

Paka sita wana macho mangapi?

Jongoo mmoja ana miguu mingapi?

------------------------------------------------------------



Chiriku alionywa na mamake kutoongea sana. 

Hakutii.

Shangazi ya Chiriku aliishi mbali. 

Siku moja,alikuwa mgonjwa.

Chiriku alitumwa kumpelekea shangazi chakula. 

Ilikuwa jioni.

Chiriku alikutana na Sinso. 

Sinso alikuwa fisi aliyegeuka mtu.

Sinso alimwuliza alichobeba. 

Chiriku alijibu, "Nimebeba nyama na mayai."

Aliongeza, "Ninampelekea shangazi mgonjwa." 

Sinso alikitamani chakula.

Sinso alimpa kwaheri. 

Alikimbia akajificha nyumbani kwa shangazi.

Sinso alimmeza shangazi. 

Akajifunika blanketi lake.

Chiriku alipowasili, nyumba ilikuwa kimya. 

Aliita, "Shangazi, uko wapi?"

Hakusikia sauti ya shangazi yake. 

Alishangaa kuona umbo kubwa.

Aliuliza, "Mbona una masikio makubwa?"

Sinso alijibu, "Ili nikusikie."

Aliuliza tena, "Mbona una macho makubwa?" 

Sinso alijibu, "Ili nikuone."

Mwisho aliuliza, "Mbona una mdomo mkubwa?" 

Sinso alijibu, "Ili nikumeze."

Sinso alimmeza Chiriku. 

Chiriku aliendelea kuuliza maswali akiwa tumboni.

Mwishoni, Sinso alichoka na maswali aliyouliza Chiriku. 

Alimtema nje.

Chiriku na shangazi yake waliokolewa. 

Chiriku alikoma kuongea ovyo.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na Kijiji kilichoitwa Kalamu. 

Pale kijijini, kuliishi kalamu tofauti.

Kwa mfano, kulikuwa na Dhahabu, Bic, Ballpoint, Gel, Marker na wengine wengi.

Dhahabu alikuwa msichana mrembo.

Bic alikuwa rafiki mkubwa wa Dhahabu.

Dhahabu alikuwa mwenye huzuni na wasiwasi kila wakati. 

Aliishi maisha ya upweke mbali na waliompenda.

Hakuna yeyote aliyejua kwa nini Dhahabu alihuzunika na kuwa na wasiwasi wakati wote.

Watu waliamini kwamba alikuwa na kila sababu ya kufurahi.

Hata hivyo, Dhahabu alikuwa na siri kubwa ambayo yeye tu aliijua. 

Je, Dhahabu alikuwa na siri gani?

Dhahabu alikuwa mrembo na mwenye kupendwa. Lakini, hakuwa na wino! 

"Je, kalamu ya Dhahabu ina umhimu gani isipokuwa na wino?" Dhahabu aliwaelezea akilia.

------------------------------------------------------------



Kila asubuhi huwa ninaosha uso wangu.

Huwa ninapiga mswaki kwa kutumia dawa ya meno.

Huwa ninachana nywele.

Huwa ninaoga.

Ninaosha mwili wangu na sabuni.

Huwa ninavaa nguo safi.

Nikitoka nje huwa ninavaa viatu.

Huwa ninaosha mikono yangu kwa kutumia sabuni na maji safi...

...baada ya kutumia choo...

...kabla ya kula...

...na baada ya kucheza nje.

Huwa ninapiga mswaki tena kabla ya kulala.

Ninapenda kunukia...

...na kuwa msafi!

------------------------------------------------------------



"Fanya haraka Naka, tutachelewa kwenda shuleni!" Nala anasema kwa mshangao.

"Ninahisi kuganda! Hebu tuwashe moto ili tupate joto," Naka anasema.

"Umesahau kwamba shangazi alituambia tusichezee moto?" Nala anauliza.

"Nilimsikia, lakini hatuko ndani ya nyumba!" Naka anajibu.

Nala anasema, "Tuko mtaani, lakini bado ni hatari. Moto unaweza kusambaa haraka na kusababisha uharibifu mkubwa." 

Naka anafikiria kuhusu hili.

"Lakini zamani, moto ulikuwa chanzo pekee cha joto na mwanga. 

Watu waliutumia kwa kupika, kujipasha joto na kuangaza," Naka anasema.

Nala anajibu, "Moto ni rasilimali yenye manufaa, lakini ni vigumu kuudhibiti.

Ndio maana watoto hawapaswi kuwasha moto. Kila mtu anapaswa kuwa makini."

Nala anaendelea, "Umeme ni salama na safi kuliko kuchoma kuni au makaa.

Kuchoma vitu kama kuni na makaa husababisha uchafuzi mwingi."

Naka anauliza, "Je, unajua jinsi moto unavyoanza?"

"Mafuta na hewa vikichanganyika, husababisha cheche. Hivyo ndivyo moto unavyoanza," Nala anaelezea.

"Hewa na mafuta vinapochanganyika kwa haraka katika nyuzi za joto sahihi, moto huanza kuwaka. 

Kwa mfano, kusugua vijiti pamoja ama kuwasha kiberiti."

"Moto hutoa moshi," Naka anasema.

Nala anakubali, "Ndiyo, hiyo pia ndiyo sababu hatupaswi kuwasha moto ndani. Sio salama kuvuta moshi."

Nala na Naka wanawasili shuleni.

"Usiwahi kamwe kuacha mshumaa au moto ukiwaka peke yake. Moto unaweza kuteketeza nyumba na watu!" Nala anaonya.

Maswali

1. Ni nani anayetaka kuwasha moto, na kwa nini?

 2. Orodhesha matumizi matatu ya moto.

 3. Orodhesha matatizo matatu ya moto.

4. 'Uchafuzi' ni nini?

5. Orodhesha njia 2 za kujikinga na moto.

6. Tafuta neno 'moto' katika lugha zingine 3. Andika maneno hayo na uchore picha.

------------------------------------------------------------



Mama na baba walienda shambani. 

Walimwacha Makabi amchunge mtoto.

Makabi alicheza akasahau kumlinda mtoto.

Korongo walimkuta mtoto akilia.

Walimbebea ndani ya blanketi wakaruka naye juu.

Mama aliwaona korongo wanne wakiruka. 

Walikuwa wamembeba mtoto wake.

Korongo walimlinda mtoto vyema.

Korongo walipotoka, chura alimmeza mtoto!

Chura alitaka zawadi ili amrudishe mtoto.

Alipewa nzi watatu.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na tajiri mmoja mjanja aliyeitwa Madola. 

Aliwaajiri watu waliofanya kazi kwa bidii, lakini walipomaliza, hakuwalipa ada zao.

Dande alikuwa mvulana mdogo aliyeishi na bibi yake. Alikwenda kwa Madola kuajiriwa ili aweze kumnunulia bibi dawa. 

Alipata kazi ya kuwachunga mifugo wa Madola.

Mwisho wa mwezi, Dande alikwenda ili apate malipo yake. 

Madola alifanya ujanja akamwambia, "Nenda nyumbani kisha urudi kesho nikulipe."

Keshoye, Dande alifika kwa Madola mapema akitarajia kulipwa. 

Madola alifanya ujeuri tena akamwambia, "Hala! Kwani wewe ni mwanafunzi? Kwa nini umefika hapa mapema hivi? Kwani hii ni shule?"

Madola alimpeleka Dande mbali na wafanyakazi wengine akamwambia, "Nitakulipa, lakini, kwanza niletee kibuyu cha asali tamu."

Dande alifikiria, "Ni muhimu sana kuzipata zile hela ili nimnunulie bibi dawa." 

Alivibeba vibuyu viwili akakimbia msituni kuitafuta asali. Alipouna mzinga, aliviweka vibuyu karibu akasubiri vijae.

Dande aliwaza jinsi ya kumwadhibu Madola. Hakumwona nyoka mdogo mweusi mwenye sumu akiingia katika kibuyu kimoja. 

Dande aliviziba vile vibuyu ili asali isidondoke kisha akaondoka.

Dande alimpelekea Madola kibuyu cha asali akitarajia kulipwa. Madola aliionja asali, akasema,  "Niletee kibuyu cha pili cha asali kama hii ndipo nikulipe." 

Dande alikimbia kukileta kibuyu cha pili bila kujua ndicho kilichoingiwa yule nyoka.

Dande alimpatia Madola kibuyu cha pili akisema, "Ndicho hiki kibuyu cha asali tamu kama ile ya kwanza. Naomba unilipe sasa."

Madola alikipokea kibuyu lakini kwa mara nyingine,  alimwambia Dande kwa ujanja, "Sikulipi leo. Subiri mwisho wa mwaka." 

Dande alimtazama Madola kwa hasira kisha akageuka karudi nyumbani.

Madola alitaka kuila ile asali kwa pupa. Alipokitia kidole ndani ya kibuyu, aliumwa. 

Alitoka nje akilia, "Nimeumwa! Nisaidieni jamani!" 

Nyoka aliyemuuma alitoroka bila kuonwa na yeyote.

Wafanyakazi wote walikimbia wasijue kilichotendeka kwa mwajiri wao. 

Baadaye, ambulansi ilifika na kumpeleka Madola hospitali.

------------------------------------------------------------



Mama yangu anapoamka, hutandika kitanda chake kwanza.

Huingia jikoni kutayarisha kiamsha kinywa. Pia, hutayarisha vitafunio na kuviweka ndani ya mifuko midogo.

Wanawe hula vitafunio hivi wakati wa mapumziko ya saa nne na saa sita.

Kiamusha kinywa huwa ni uji wa nafaka, chai na mkate, maji ya machungwa au maziwa.

Huwaamsha wanawe na kuwaelekeza wapige mswaki, wanawa nyuso na kuvaa sare za shule.

Familia yake inapomaliza kujitayarisha, huelekea mezani kula kiamsha kinywa.

Baba huenda zake.

Mama huwaingiza wanawe kwenye gari lake na kuwapeleka shule.

Huwapungia mkono watoto na kuwambia, "Kwaherini, tuonane jioni."

Huliendesha gari lake mpaka kituo cha gari la moshi.

Huingia kwenye gari la moshi na kuelekea mjini anapofanya kazi ya uhasibu.

Saa kumi zinapofika, mama huiacha kazi yake haraka. 

Yeye hurudi kwenye kituo cha gari la moshi.

Huingia na kuelekea nyumbani.

Inapofika saa kumi unusu kamili, huwachukua watoto wake waende nyumbani.

Watoto huwa wamemngoja kwa hamu. 

Wao huingia kwenye gari haraka wakilia njaa.

Wanapofika mlangoni, watoto hutimua mbio ili wakale mkate uliobaki.

Mama huanza kupika chakula cha jioni na kuwaandalia wanawe. 

Wanapomaliza, wote huwa wamechoka kweli.

Lakini bado vyombo havijaoshwa. 

Je, ni nani atakayeviosha vyombo?

------------------------------------------------------------



Ninapenda kucheza soka.

Ninapenda kucheza soka na Tando, Dido na Ben.

Huyu ni mama yangu.

Nampenda mama yangu.

Yeye hunichekesha.

Ninampenda Mungu, kwa sababu Mungu ananiumba.

Ninapenda shule, kwa sababu walimu hunifunza ninachohitaji kujua.

Ninapenda kucheza na mbwa, kwa sababu inafurahisha.

Ninapenda sherehe za kuzaliwa, kwa sababu napenda kusherehekea.

Na ninajipenda kwa sababu…

…kwa sababu… ninafanya hivyo!

------------------------------------------------------------



Feni alikuwa msichana mdogo aliyekimbia kama upepo. 

Feni alipenda kucheka na alijaribu alivyoweza kutenda alivyoambiwa.

Siku moja, Feni na babake walikwenda shambani kwa baiskeli kung'oa magugu.

Feni alichoka akasema, "Baba, ninahisi joto na uchovu. Niruhusu nipumzike chini ya mwembe."

Baba akajibu, "Ndiyo Feni, unaweza kupumzika pale. Lakini, tafadhali, usipande mti wowote leo."

Feni aliketi chini ya mwembe.

Feni alitazama juu akaona embe moja, maembe mawili, matatu! Yote yalikuwa mabivu.

Feni alimtazama babake. Baba alishughulika na hakuangalia upande wake.

Polepole, Feni alianza kuukwea mwembe. Aliwaza, "Nitapumzikia pahali hapa pazuri nikiyala maembe mabivu."

Kwa hivyo, Feni aliketi akayala maembe.

Baada ya kula maembe, Feni alishuka chini.

Aliuona mti mwingine.

Mti huo ulikuwa ukidondokwa kitu chenye rangi ya hudhurungi.

Kitu hicho kilikuwa asali! Feni alipenda asali mno! Lakini, hakuwependa nyuki.

Feni alitazama juu na kumwona nyuki mmoja mdogo.

Feni aliwaza, "Kuna tu nyuki mmoja mdogo. Hataniumiza nikipanda mtini kutafuta asali."

Feni alimtazama babake. Baba hakuwa akimwangalia.

Kwa hivyo, Feni alipanda juu ya mti na kuchukua asali kutoka shimoni.

Feni aliwaza, "Nitapumzikia pahali hapa pazuri nikiila asali nyingi tamu."

Kwa hivyo, Feni aliketi akaila asali.

Baada ya kula asali, Feni alishuka chini kutoka mtini.

Halafu aliwaona nyuki. Walikuwa nyuki wengi mno! BZZZ! BZZZ! BZZZ!

Feni aliamua kuwatoroka wale nyuki.

Feni alikimbia kumtafuta babake. Alikuwa akihema kweli kweli.

Baba aliuliza, "Feni, umekuwa wapi?"

Feni hakutaka kusema alikokuwa.

Badala ya kumjibu babake, Feni alisema, "Baba, tazama nina embe. Je, ungependa kulila?"

Baba alijibu, "La, asante Feni. Lazima tuondoke kwenda nyumbani sasa hivi. Mvua itanyesha hivi karibuni."

Baba alimbeba Feni kwenye baiskeli wakienda nyumbani. Mvua ilianza kunyesha.

Baba aliendesha baiskeli kwa kasi.

Baiskeli iliiacha barabara.

RURUUU PU!

Baiskeli ilimwangukia Feni mguuni.

Feni aliushika mguu na kulia kwa uchungu!

Walipofika nyumbani, mama na bibi walitaka kujua siku ilivyokwenda walipokuwa shambani.

"Feni alipanda mti," baba alisema.

"Baba aliendesha baiskeli kwa kasi sana hata ikaniangukia mguuni," Feni alisema.

"Aaa, maskini Feni," mama akasema.

"Aaa! Aaa! Maskini Feni! Lazima tuutibu mguu wako," bibi akasema. 

Na hivyo ndivyo walivyofanya. Na huo ukawa ndio mwisho wa jambo hilo.

------------------------------------------------------------



Mama Koki amekuwa akichuma kabichi wiki nzima. Dona, Maya na Duki humsaidia Mama Koki katika bustani yake kila Jumamosi asubuhi.

Leo watoto hawa watahesabu na kupakia kabichi. Baba Koki atayapeleka masanduku yaliyojaa kabichi sokoni kuuza.

Teksi iliwafikisha watoto kwenye lango la bustani. Waliliona rundo kubwa la kabichi karibu na gari la Baba Koki. 

"Salala! Kabichi nyingi kweli!" Maya alishangaa. "Bila shaka kuna kabichi elfu moja hapo!" Duki alicheka. "La! Hasha! Pengine ni mia mbili tu!" Dona alipinga.

Mama Koki alikuwa amewasubiri langoni. "Hamjambo, nimefurahi kuwaona!" Aliwasalimu watoto. "Hebu tuanze kazi. Mtahesabu na kuweka kabichi kumi na mbili katika kila sanduku. Nina masanduku 20. Wawili kati yenu watapakia kwenye masanduku 7 kila mmoja. Aliyebaki, atapakia kwenye masanduku 6."

Watoto walilitazama lile rundo la kabichi. Wakajadili njia tofauti za kuzihesabu kabichi hizo. "Mimi nitahesabu zangu mbili mbili," Maya akasema. 

"Ninapenda kuhesabu nne nne. Ni haraka," Duki akajibu. 

"Mimi nitazihesabu tatu tatu ili niwe tofauti nanyi!" Dona akawajibu.

Watoto walijaza masanduku yote 20. "Kazi nzuri!" Mama Koki aliwapongeza. "Tazama, kabichi zimezalia. Nguruwe wangu wanazipenda. Hebu tuwagawie," Mama Koki aliamua. 

"Mlipakia jumla ya kabichi ngapi katika masanduku yote? Ni kabichi ngapi zilizalia?" aliwauliza watoto.

Waliandika bei kwenye kila sanduku. Halafu, wakamsaidia Baba Koki kuyapakia kwenye gari. 

Waliweka nusu ya masanduku upande mmoja. Na nusu nyingine upande wa pili ili uzito ulingane.

"Karibu tukamilishe kazi!" Baba Koki alisema. "Hebu tuone ni masanduku mangapi tunahitaji kuweka kila upande."

Muda mfupi baadaye, masanduku yote 20 yalikuwa yamepakiwa kwenye gari. Baba Koki aliondoka kwenda sokoni. 

Aliwaza, "Nikifaulu kuuza masanduku yote, nitapata pesa za kutosha. Nitaweza kuwashangaza watoto kwa kurekebisha zizi la nguruwe!"

Nyumbani, Mama Koki na watoto walinyunyizia mimea maji na kukusanya majani. Kufikia saa sita, wote walikuwa wamechoka. 

Mama Koki aliwaambia, "Ni wakati wa karamu yenu. Je, mnajua nilichowaandalia leo?"

Aliingia ndani kuwaletea alichokuwa amewaandalia. Watoto walisubiri kwa uvumilivu huku wakikisia atakacholeta. 

Aliporejea, waliona mifuko ya aproni yake ikiwa imejaa!

"Hebu tuone ikiwa mlikisia sawa! Nimewatayarishia nini leo?" Mama Koki aliyaweka matofaa mezani. "Nilikisia sawa!" Duki alisema kwa furaha. 

Mama Koki aliwaambia watoto, "Kumbukeni sharti! Gawanya sawa ili kila mmoja apate haki yake. Hakuna anayepata zaidi wala kidogo kuliko mwingine!"

Kwanza, watoto walihesabu matofaa mawili mawili. Walihesabu: 2, 4, 6, 8, 10, 12, 14, 16, na tofaa moja likabaki. Yote pamoja, yalikuwa matofaa 17.

Waligawana matofaa sawasawa yakabaki matofaa mawili. Kisha watoto waliyaweka matofaa yao mikobani ili waende nayo nyumbani kwao.

"Hebu tuyakate matofaa mawili yaliyobaki ili tugawane kati yetu," Duki aliwaambia. "Kila mmoja wetu atapata vipande vingapi vya tofaa?" Maya aliuliza. "Ninajua jibu!" Dona alitabasamu.

Wakati huo, Baba Koki alirejea nyumbani kutoka sokoni. Gari lilikuwa tupu naye alikuwa akitabasamu. 

"Niliuza kabichi zote. Sasa ninaweza kurekebisha zizi la nguruwe. Nitaweza pia kuwanunulia ule mpira wa miguu mliotaka." Watoto walishangilia, "Yee!"



------------------------------------------------------------



Baba anaishi Yovel.



Mimi ninaishi Betrams na mama na dada zangu wawili.



Ninamwona baba anapokuja siku ya sherehe ya kuzaliwa kwangu.



Ningependa aishi nasi.

Sijui kwa nini hatuishi pamoja.



------------------------------------------------------------



Kulikuwa na tajiri aliyekuwa na wana wawili wa kiume. 

Kwenye wosia wake alitaka mwanawe wa kwanza arithi ng'ombe wake wote na wa pili, amrithi jogoo mmoja tu.

Baada ya tajiri kufa, mwanawe wa kwanza alirithi ng'ombe wote. 

Mwanawe wa pili alipewa jogoo mmoja tu.

Baada ya muda mchache, mwana wa kwanza ambaye alirithi mali yote, aliugua. Alienda kumwona mganga amsaidie kupata njia ya kupona. 

Mganga alisema, "Ni sharti umchinje jogoo mwenye rangi ya pekee."

Mwana huyo hakujua atakapopata jogoo mwenye rangi ya pekee hadi alipokumbuka kuwa nduguye alikuwa na mmoja. 

Aliwatuma watu kumchukua yule jogoo wa nduguye.

Kakake aliwaambia watu hao, "Mimi sina mali nyingine isipokuwa jogoo huyu tu. Lakini, iwapo jogoo huyu ataweza kumponya kakangu, basi ni bora kwangu kumpoteza jogoo huyu." 

Aliwapa jogoo wake kwa ukarimu.

Watu walimchinja jogoo na kumlisha kakake mgonjwa. 

Baadaye, kakake alipona.

Baada ya muda mfupi, kitu kisicho cha kawaida kilifanyika. 

Mwili wake ulianza kuota manyoya.

Hakuweza kuamini macho yake.

Alipokwenda kuwaona wazee, walisema, "Jambo hili limetokea kwa sababu ya laana. Hukumfanyia nduguyo haki. Umechukua ng'ombe wote na hata jogoo ambaye babako alimuachia. Ukitaka kupona, ni lazima nduguyo akusamehe."

Wazee waliendelea kusema, "Ni sharti tuichukue bangili hii tumpe nduguyo kama ishara ya msamaha. Iwapo ataitemea mate bangili hii, utapona."

Wazee walimpelekea ndugu mdogo bangili hiyo wakamwambia, "Itemee mate bangili hii umsamehe kaka yako." 

Nduguye maskini aliitemea mate bangili.

Kwa sababu hiyo, wazee waliamua kumpa nusu ya ng'ombe wa kakake tajiri.

------------------------------------------------------------



Banti anapenda kucheza na vipepeo.

Pia anapenda kucheza na ndege.

Yeye hutengeneza mashua kutoka kwa makaratasi.

Pia hutengeneza ngome akitumia changarawe.

Banti akirudi nyumbani, mamake humwuliza aoge. 

Yeye hukataa.

"Nachukia sabuni!" Banti hulia.

Aliota kuwa viini vinavyosababisha magonjwa vilikivamia kitanda chake.

Banti alikuwa anafukuzwa na viini hivyo. 

Alikimbia akipiga mayowe, "Nisaidieni. Nisaidieni!"

Mfalme Sabuni alimjibu, "Banti, usiogope. Jeshi langu la povu litavivamia viini vinavyokusumbua!"

Mara moja, povu lilivifukuzia mbali viini vile.

Tangu wakati huo, Banti hutumia sabuni. 

Hujipangusa na kujisugua hadi huwa msafi.

------------------------------------------------------------



Ndalo ana umri wa miaka 10. Yuko katika darasa la 5 katika shule iliyo pale kijijini. Ndalo huibuka wa kwanza darasani kwake. "Ni nini siri yake?" Wenzake wanajiuliza. 

Ndalo anasoma na kuandika vizuri. "Je, anawezaje kufanya hivi?" Wanashangaa. Ndalo anawaeleza kwamba ni kwa sababu ana vitabu vingi. Wao wanapopoteza muda wao wakikaa bila kazi, yeye huutumia muda wake kusoma.

Wakati mwingine Ndalo hupata Shilingi 80 kama pesa za matumizi. Yeye huzitumia pesa zake nyingi kununua vitabu kutoka duka la vitabu vikuukuu lilioko pale kijijini. 

Je, Ndalo hupataje pesa za matumizi anazotumia kununua vitabu? Fungua ukurasa ufuatao upate kujua.

Huyu ni Pendo, ng'ombe wa maziwa. Yeye hutoa maziwa lita 20 kwa siku. Babake Ndalo huuza maziwa hayo. 

Ng'ombe huhitaji chakula na maji. Vilevile, huhitaji kutembea uwanjani. Kwa hivyo, kila siku baada ya kutoka shuleni, Ndalo hufanya kazi hiyo. Babake humpatia pesa za matumizi kwa kazi hiyo. Ni pesa hizo ambazo Ndalo huweka kwa ununuzi wa vitabu kila juma.

Kwanza, Ndalo humpa Pendo karoti 8 kila siku. Kila siku yeye huzichuma karoti kutoka kwenye bustani ya babake. 

Ukifanya hesabu, utapata kwamba Pendo hula takriban karoti 60 kwa juma. Je, unaweza kupata hasebu kamili?

Baada ya hiyo, Ndalo humpeleka Pendo malishoni. Babake alimwonya achunge ili Pendo asile nyasi kwa zaidi ya robo tatu ya saa. 

Kawaida, Pendo huanza kula nyasi saa nane na dakika kumi na tano ili Ndalo aweze kumrudisha saa tisa kwenye kibanda cha kukamulia. Wakati wa majira ya baridi, ambapo giza huingia mapema, Ndalo huweza kuanza kula saa saba na nusu.

Baada ya hilo, Ndalo humpa Pendo maji. Bila maji Pendo hawezi kutoa maziwa hata Ndalo akimlisha
namna gani. Ndalo husomba maji kwa ndoo kutoka mfereji ulio pale kijijini kwa sababu hakuna mwingine ulio karibu. 

Hori la Pendo huweza kubeba maji lita 30. Ndoo ya Ndalo hubeba tu lita 5 peke yake. Kwa hivyo ili ajaze hori, Ndalo huenda mara chache. Je, unaweza kufanya hesabu ya jumla ya safari zote?

Halafu, Ndalo humpeleka Pendo ili apate nafaka yake ya kila siku ya kilo 12. Ndalo akihesabu, anapata jumla ya kilo 90 kwa juma. 

Kila gunia linagharimu Shilingi 39. Ndalo anafanya hesabu ya nafaka ya kila juma. Kwanza anafanya hesabu ya magunia 7 kwa Shilingi 40 kila gunia. Anapata jumla ya Shilingi 280. Kisha anaondoa Shilingi 7 na kubaki na salio la Shilingi 273. "Hiyo ni kama Shilingi 10 000 kwa mwaka!" Ndalo anakadiria. Je, hiyo ni sawa?

Babake Ndalo anamkama Pendo mara mbili kwa siku. Pendo hutoa maziwa lita 24 kwa siku, kwa hivyo hutoa karibu lita 12 kila anapokamuliwa. 

Wakati mwingine Ndalo husaidia kukamua lakini, si kazi rahisi kama inavyoonekana. "Siku moja, nitakuwa na ng'ombe wangu mwenyewe ambao nitalazimika kukamua mwenyewe," Ndalo anawaza.

Babake anayamwaga maziwa kwenye ndoo ndogo ya lita 2. Vilevile, anayamwaga kwenye chupa za lita 1. Halafu anayauza maziwa hayo kwa Shilingi 8 kwa kila lita. 

Mara moja kwa juma, babake Ndalo huchanga lita 25 za maziwa kusaidia mpango wa chakula shuleni. Hii ina maana kuwa watoto 100 hupata maziwa siku hiyo.

Kwa kila lita inayouzwa, babake anampa Ndalo senti 50. Hiyo haionekani kuwa nyingi, lakini ikiwa babake anauza lita 24 kwa siku, hizo senti huongezeka na kuwa pesa nyingi. Je, unaweza kufanya hesabu na kujua kiasi kamili? 

Ndalo anaziweka hela zake hadi Jumamosi wakati anapolitembelea duka la vitabu. Kila kitabu kinagharimu chini ya shilingi 10. Kwa hivyo, anaweza kununua vitabu vingi katika juma moja.

Ndalo pia hupenda kuyanywa maziwa anayotoa Pendo. Babake husema kwamba maziwa husaidia kujenga mifupa na meno na kuipa nguvu. Pia humpa mtu afya nzuri. 

Kwa kuwa anayanywa maziwa na kuzila mboga nyingi kutoka bustani ya babake, Ndalo ana nguvu na mwenye afya nzuri. Ni nadra yeye augue au ahisi njaa.

Ndalo hasahau kumshukuru Pendo mwishoni mwa siku. Humzawadi kwa kumpatia karoti zaidi au matawi ya mchicha yapatikanayo kwenye bustani. 

"Asante Pendo, wewe ni rafiki yangu mkubwa! Mimi ni mwenye nguvu, mwenye afya na mwerevu kwa ajili yako. Usingekuwa wewe, nisingeweza kuvinunua vitabu vinavyonisaidia kuibuka wa kwanza darasani."

------------------------------------------------------------



Wayan aliishi katika kijiji kidogo kando ya bahari.

Watu wa hapo waliamini kwamba mtu anapokufa, yeye hurudi baharini.

Bahari ni mahali maalum ambapo mababu huishi.

Baba ya Wayan na babu yake walikuwa wavuvi. Wanaume wengi kijijini walikuwa wavuvi, na ilikuwa hivyo kila wakati.

Kila macheo, wanaume walikwenda kuvua samaki kwa kutumia mashua. Kila mawio, walirudi na boti zao zikiwa zimejaa samaki.

Wayan alijifunza kuvua samaki wakati kila kitu kilikuwa kinabadilika kwa wavuvi.

Kulikuwa na samaki wachache, na walikuwa wadogo kila mara.

Wakati mwingine, boti zilirudi bila kitu, ingawa walikuwa baharini siku nzima.

Fuo za bahari pia zilibadilika. Zilikuwa chafu wakati wote, na takataka za plastiki zilitupwa mchangani.

Wakati wa maji makuu, mawimbi yalisukuma plastiki ndani ya bahari.

Hatua kwa hatua, watu kijijini walianza kuugua. Hawakuweza kupona.

Siku moja, Wayan alipokuwa akivua samaki, dhoruba ilianza kuvuma. Akasongwa kwa mawimbi.

Kasa akamwokoa. "Mimi ni Bintang. Nitakusaidia, panda mgongoni kwangu," Kasa akasema.

"Labda unaweza kunisaidia. Babu yangu ni mgonjwa sana na hakuna anayejua la kufanya."

Bintang alimpeleka Wayan kwa babu yake. Kasa mzee alikuwa mgonjwa sana na alikuwa na shida ya kupumua.

Wayan aliona kitu cha ajabu kikitokezea kwenye pua la babu. Alisema, "Nitajaribu kukivuta kitu hiki, lakini itakuwa uchungu!"

Wayan alivuta na kuvuta. Babu alilia na kulia.

Hatimaye, jani la plastiki lililokuwa limekwama kwenye koo la babu lilitoka!

Babu alianza kupumua kwa urahisi zaidi. Bintang akamwambia Wayan, "Nitakupeleka kwa kasa wengine."

Walienda katika Hospitali iliyowahudumia Kasa. "Ni nini kilichotokea kwa kasa hawa?" Wayan aliuliza.

"Walikula mifuko ya plastiki wakidhani ni chakula. Sisi kasa hatuwezi kuona vizuri. Kwetu, mfuko wa plastiki unaonekana kama samaki," Bintang alieleza.

Akaendelea kumwambia, "Tunahitaji msaada wako. Tafadhali waambie watu wasitupe plastiki ardhini wala majini."

Wayan aliahidi kwamba angefanya alivyoweza kusaidia. Bintang alimrudisha ufuoni, kisha akaogelea na kwenda zake.

Wayan aligundua kuwa wanakijiji walihitaji kusafisha bahari na fuo.

Alikimbilia kwa wazee kuwaambia juu ya kasa.

Mkuu wa kijiji aliita mkutano na kila mtu akakusanyika kumsikiliza Wayan.

Wanakijiji walijadili shida hiyo kwa muda mrefu. Mwishowe, walikubaliana juu ya hatua muhimu za kuiokoa bahari yao na wanyama na mimea yake.

Watu walikubaliana kupiga marufuku majani ya plastiki, chupa za plastiki na mifuko ya plastiki.

Walikubaliana kutupa takataka zao kwenye mapipa ya takataka tu, na kuacha kuchoma na kuzika plastiki.

Waliamua kuacha kuvua hadi bahari itakapokuwa safi.

Mwishowe, bahari na fuo zilirudi jinsi zilivyokuwa kabla ya Wayan kuzaliwa.

Maji yalikuwa safi na yenye wingi wa uhai. Watu walikoma kuwa wagonjwa kutokana na kula samaki wagonjwa.

Wayan alijifunza kwamba bahari inapochafuliwa, sisi sote tunateseka. Inapokuwa safi, sote tunafurahi.

------------------------------------------------------------



Nilipokuwa mtoto mdogo, tuliishi katika shamba moja pamoja na wazazi wangu na ndugu zangu. 

Nilipenda kuwatazama wadudu wakifanya kazi zao.

Wadudu niliopenda kuwatazama zaidi ni buibui. 

Waliishi mahali mbalimbali katika boma letu.

Nilitumia muda mwingi nikiwatazama na kuona waliyokuwa wakifanya.

Nilipojua kusoma, nilifanya utafiti katika vitabu na kujua mambo mengi sana kuwahusu.

Nilijifunza kwamba miili yao ina sehemu mbili tu, ambazo ni kichwa na tumbo.

Buibui huwinda na kushika mawindo.

Wengi huwinda wadudu wengine.

Pia nilijifunza kwamba buibui wana sumu.

Wao hutumiwa sumu hiyo kuua mawindo yao.

Kabla ya buibui kula chakula chake, lazima akifanye kiwe majimaji.

Hutengeneza hariri ambayo huitumia kujenga nyumba yake iitwayo utando.

Hutaga mayai mengi na huyalinda kwa kutumia utando wake.

Buibui wengi wana miguu minane ambayo hutumika kutembea na kupanda.

Buibui wengine wana macho manane na wengine wana sita.

Ajabu!

Nilitamani sana kumweka buibui mmoja kama mnyama kipenzi.

Hata hiyvo, mama yangu alikataa kata kata.

------------------------------------------------------------



Akai hakuwa na viatu. 

Marafiki zake walikuwa wakivaa viatu vizuri walipocheza.

Akai alimwomba mamake amnunulie viatu. 

Ilikuwa shida kucheza bila viatu.

Walipotembea kijijini, mama alitambua kuwa watoto wengine walivaa viatu isipokuwa Akai na Etabo.

Siku moja asubuhi, mama alimwamsha Akai. 

Alimwambia ajitayarishe waende sokoni.

Akai na mamake walitembea hadi sokoni.

Walipoingia katika duka la viatu, Akai alifurahi sana.

Usiku ule, Akai hakuweza kulala. 

Aliwazia tu viatu vyake vipya.

Hamu ya kuvaa viatu ilizidi. 

Akai akasimama na kuvivaa viatu vyake.

Hata baada ya kurudi kitandani, Akai aliwaza jinsi angewaonyesha wenzake viatu vyake.

Akai aliamka tena na kuvivaa viatu vyake vipya. 

Alicheza chumbani.

Mama alimpata Akai amelala kitandani akiwa amevaa viatu. 

Alimwambia Akai asivivae tena viatu vyake kitandani.

Akai alifurahi kupata viatu kwa mara ya kwanza.

------------------------------------------------------------



Kigoe changu cha kuchezea tenisi kimepotea. 

Sijui mahali kiliko.

Nilikitafuta nyuma ya mlango. 

Lakini sikukiona.

Nilikitafuta juu ya kabati. 

Lakini sikukiona hapo.

Nilikitafuta chini ya kitanda. 

Sikukiona hata hapo.

Nilikitafuta ndani ya sanduku. 

Lakini, hapakuwa na dalili yake pale.

Nilikitafuta kwenye dari.

Niliangalia hapa na pale,  nikaangalia kila mahali. 

Lakini sikukiona.

Aaa! 

Kumbe dadangu alikuwa nacho.

------------------------------------------------------------



Ilikuwa Jumamosi yenye joto jingi. Kila mmoja alikuwa amenuna.

"Betty, Mercy na Larry, nendeni nje mcheze! Siwataki hapa," mama aliwaambia watoto.

"Twendeni mtoni. Kuna upepo mzuri huko," Larry alisema. 

"Mama alitukataza kuogelea mtoni," Betty alijibu. 

"Tutachezea tu karibu na maji," Larry alisema.

Walipofika, kwanza walivua viatu vyao. Lakini walikuwa bado wanahisi joto. 

Wakavua nguo zao. Lakini walikuwa bado wanahisi joto.

Waliiweka miguu yao majini kuifanya iwe baridi. 

Walirushiana maji. Punde kidogo walikuwa wameloa maji.

"Aa, njoo! Hebu tuogelee. Mama hatajua," Mercy alisema. 

Waliogelea kwa muda mrefu wakasahau kuwa muda ulikuwa unapita.

Jua lilipoanza kutua, walihisi baridi. 

Lakini je, nguo zao zilikuwa wapi?

Walitazama chini ya miti. Wakatazama juu ya vichaka. 

Walitazama kila mahali. Hawakuona dalili ya nguo zao popote.

Ng'ombe walikuwa wakila nyasi karibu na mto. 

Betty alisema, "Mwone yule ng'ombe! Ni nini hicho anachokula?" 

"Anakula ua jekundu," Larry alisema.

"Sio ua jekundu. Ni shati lako," Mercy alipiga kelele. 

Walimwona ng'ombe mwingine akila kitu cha kisamwati. 

"Hiyo ni sketi yangu!" Betty alipiga kelele kwa hofu.

Walirudi nyumbani wakiwa wamevaa suruali tu. "Ng'ombe walikula nguo zetu," walilia. 

Punde kidogo makalio yao yalikuwa na joto sana kwa kuadhibiwa.

------------------------------------------------------------



Kwa nini anga ni ya rangi ya bluu?

Je,  huwa bluu kila wakati?

Kwa nini rangi ya majani ni kijani kibichi?

Majani si kijani kibichi kila wakati.

Kwa nini ndizi mbivu ni manjano?

Ndizi mbichi ni za kijani.

Kwa nini mwavuli ni mweusi?

Miavuli yote si mieusi.

Kwa nini damu ni nyekundu?

Kuna madini kwenye damu. 

Yanaipatia damu rangi nyekundu.

Kwa nini chumvi ni nyeupe?

Sifahamu!

------------------------------------------------------------



Kituo cha basi cha kijiji chetu kilikuwa na shughuli nyingi. Basi zilijaza mizigo huku abiria wakizitafuta basi walizotaka kuabiri. 

Kondakta waliwaelekeza abiria kwenye basi zilizokwenda sehemu mbalimbali.

Nilimsikia kondakta mmoja akiita kwa sauti, "Jiji! Jiji! Wanaokwenda magharibi!" 

Lile ndilo basi nililohitaji kuabiri kwa usafiri wangu.

Basi la kwenda jijini lilikuwa karibu kujaa. Hata hivyo, watu zaidi walitaka kuingia. 

Baadhi yao walipakia mizigo chini ya basi. Wengine waliiweka ndani kwenye rafu.

Baadhi ya abiria walishika tiketi zao huku wakitafuta viti vilivyokuwa wazi. 

Wanawake waliokuwa na watoto wachanga waliwatayarisha kwa safari hiyo itakayokuwa ndefu.

Nilipenyeza ndani nikapata kiti karibu na dirisha. 

Abiria aliyeketi karibu nami alishika karatasi ya plastiki ya kijani kibichi. Alivaa viatu vilivyozeeka na koti kukuu.

Nilitazama nje nikawaza, "Ninaondoka hapa mahali nilipolelewa nikienda kwenye jiji kubwa. Sijui ikiwa nitawahi kurudi hapa kijijini tena."

Upakiaji mizigo ulikamilika na abiria wakawa wameketi. 

Wachuuzi walizidi kusukumana wakitaka kuuza bidhaa zao. Walitaja majina ya bidhaa walizouza kwa sauti ya juu. Maneno yao yalinifurahisha.

Baadhi ya abiria walinunua vinywaji. Wengine walinunua vitavunaji vidogo na kutavuna. 

Wasiokuwa na hela, kama mimi, walitazama tu.

Shughuli hizo zilikatizwa kwa mlio wa honi ya basi. Tulikuwa tayari kuondoka. 

Kondakta aliwataka wachuuzi wote washuke kutoka basini.

Wachuuzi walisukumana kutoka nje. Wachache waliwarudisha abiria masalio ya hela zao. 

Wengine walifanya juhudi za mwisho kuuza bidhaa zao.

Basi lilipoondoka kituoni, nilichungulia dirishani. 

Nilikitazama kituo hicho kilichojaa magari nikiwaza,  "Pengine hii itakuwa mara yangu ya mwisho kukiona kituo hiki."

Safari ilipoendelea, nilihisi joto jingi. 

Niliyafumba macho nikinuia kulala.

Nilijiuliza maswali mengi. "Je, mamangu atakuwa salama? Je, sungura wangu watatufaidi? Je, ndugu yangu atakumbuka kunyunyizia maji miche ya miti yangu?"

Njiani, nilikariri jina la mahali mjombangu aliishi kule jijini. 

Hatimaye, nilipatwa na usingizi.

Baada ya saa tisa, niliamshwa kwa kelele nyingi. Kondakta alikuwa akiwaita abiria waliotaka kwenda kijijini kwetu. 

Nilichukua mkoba wangu mdogo nikaruka nje.

Basi hilo lililokuwa likirudi lilikuwa linajaa upesi. Muda mfupi baadaye, lingeanza safari ya kwenda mashariki. 

La mhimu kwangu, lilikuwa kuanza kutafuta nyumba ya mjombangu.

------------------------------------------------------------



Don alikuwa nyani mkubwa. 

Alikuwa mchokozi.

Don ndiye alikuwa chifu wa nyani wengine.

Wafuasi wake walimpatia kitambaa maalum.

"Nitakivaa kichwani," Don alisema.

"Kila mmoja afuate masharti yangu. Msinihoji!" 
Don alipiga kelele.

Wafuasi walimfuata chifu wao. 

Don iliporuka, kila mmoja aliruka.

Lakini, kile kitambaa, kilimkaza sana.

Don aligusa kichwa alikoumia. 

Nyani pia waligusa vichwa vyao.

"Hapa panuma," Don alisema. 

Nyani pia walisema, "Hapa panauma."

Alisema, "Hii imekazika sana!" 

Wao pia walisema, "Hii imekazika sana."

Don alianguka kutoka juu. 

Wote walimuiga wakaanguka.

Nyani aliyekuwa chifu alikufa. 

Wafuasi wake waliumia, lakini waliishi.

------------------------------------------------------------



Wakati nilipokuwa mdogo, nilikuwa na ndoto ya kuwa dereva.

Nilikuwa nikivutiwa sana pindi nilipoona dereva akiwa usukani.

Siku moja, nilikuwa barabarani na mdogo wangu Adina.

Tuliliona gari jekundu likiendeshwa na dereva aliyekuwa akiongea kwenye simu.

Mbele yake, nililiona gari jingine la kijani. 

Liliendeshwa na dereva wa kike.

Dereva huyo wa kike alionekana kuendesha gari kwa umakini sana.

Lakini ghafla, magari hayo yaligongana.

Ajali hiyo ilikuwa mbaya sana na polisi walifika hapo mara moja.

Baada ya uchunguzi wao, polisi wakagundua kuwa aliyeendesha gari jekundu ndiye alikosea.

Hakuwa makini alipokuwa barabarani, kwani muda wote aliongea kwenye simu.

kwa bahati mbaya, dereva huyo, alipoteza maisha.

Dereva wa kike alipata majeraha madogo, kwani alikuwa makini wakati ajali ilipotokea.

------------------------------------------------------------



Zamani mamba aliishi karibu na mto na wanawe.

Aliwafunza wanawe kutowaamini binadamu. Binadamu walikuwa na bongo.

Siku moja, mwanamume mmoja alikuwa akivuka mto.

Mwanamume huyo alikutana na mamba katikati ya mto. Mamba alimshambulia.

Mamba alipokuwa karibu kumuua, alikumbuka maneno aliyosema babake. 

Alimwambia kila mara kuwa binadamu wana bongo.

Mwanamume huyo alimuahidi mamba kuwa angemletea bongo za binadamu. 

Mamba akamuacha huru.

Hadi leo, Mamba na wanawe bado wanasubiri kwenye ukingo wa mto kupokea bongo hizo.

Hadi leo, mamba wana hasira na binadamu. 

Hawakuwahi kupokea bongo walizoahidiwa.

------------------------------------------------------------



Hujambo! Jina langu ni Nanu. 

Mimi na mamangu tunasubiri teksi ili twende nyumbani.

Hapa nimesimama kwenye foleni. 

Mamangu ananiimbia wimbo. "Njoo Bwana Teksi kwani huoni! Twasubiri, mimi na Nanu!"

Mwanamke aliye karibu nami anawapeleka kuku nyumbani. 

Watataga mayai ili ale.

Wanaume hawa wanarudi kutoka kazini. Wanatabasamu. 

Nawasikia wakiimba, "Nanu mdogo, usiwe na wasiwasi. Teksi yaja kwa haraka."

Mwanamke anapita akitembea. Yuko nadhifu sana. 

Viatu vyake si vizuri kweli! Vinatoa sauti, "Click, click, click. Click, click, click," anapotembea.

Mwanamme huyo anauza vinywaji baridi. 

Napenda vinywaji baridi. Ni baridi na vitamu sana. 

Je,  unavipenda?

Hebu! Kuna wanawake wamebeba vichwani chakula chao cha jioni. 

Je, si wao ni werevu?

Mwanamke huyo anasukwa nywele zake. 

Ataenda nje leo usiku na marafiki zake.

Nimechoka sasa. Mamangu ananiweka mgongoni kwake nikapumzike. 

Anaimba, "Tafadhali Bwana Teksi, usichelewe. Gogo anasubiri kwenye lango kuu."

Kuna rafiki yangu Tumi. Yeye pia anapumzika. 

Tutakuwa nyumbani hivi karibuni.

Hapo juu ndege wanaruka kwenda nyumbani. 

Lazima wafike nyumbani kabla giza halijaingia.

Mwanamke huyu ana vipuli maridadi. Nadhani alivinunua mjini leo. 

Nikiwa mkubwa, nitanunua vipuli vingi vyangu na vya mamangu.

Mamangu anaanza kuchoka sasa. 

Ninamwimbia wimbo, "Tafadhali Bwana Teksi, njoo. Mimi na mamangu tunasubiri."

Ngoja! Ninasikia teksi! 

Hii hapa inakuja!

Hii ni teksi yetu kubwa nyekundu. 

Imekuja kunipeleka mimi na mamangu nyumbani. 

Nimefurahi sana!

Kwaheri!

------------------------------------------------------------



Miaka milioni moja iliyopita, kito cha soka kiliundwa.

Kilipogunduliwa, watu walipigana kukimiliki kito hicho chenye nguvu.

Wakati wa vita vya soka vya kwanza vya dunia kito hicho kilipotea. Hakuna aliyeelewa.

Muda ulipita. Kito hicho cha soka kilipatikana tu alipozaliwa nyota maarufu zaidi wa soka.

Si kitambo sana, kulikuwa na mvulana aliyeitwa Daudi. Alitoka katika familia maskini.

Kabla babake Daudi kufariki, alimpatia mwanawe kito hicho cha soka.

Mwanzoni, Daudi hakujua nguvu za kito hicho.

Daudi alikuwa bado kijana alipokitumia kito hicho kucheza soka.

Hakuwa ameanza kwenda shuleni. Lakini, kwa nguvu za kito hicho, Daudi alishinda kila mechi aliyocheza na marafiki zake.

Daudi alitambua kuwa angeipatia familia yake fedha kwa kucheza soka.

Angemfungulia mamake duka, na kuwapeleka kakake na dadake shule.

Daudi alijitokeza kuwa mchezaji wa soka maarufu zaidi aliyewahi kuonekana.

Hata ilisemekana kwamba alitoka ulimwengu tofauti!

Daudi ni nyota wa soka ambaye hatasahaulika kamwe!

------------------------------------------------------------



Hapo kale, kulikuwa na mtu aliyeitwa Pepe. Aliishi katika mtaa wa Umoja. 

Pepe aliishi na mbwa wake katika chumba chake kidogo.

Siku moja Pepe alikuwa mgonjwa. Hakuwa na yeyote wa kumsaidia. 

Alipopata nafuu, aliamua kumwoa mwanamke aliyeishi hapo karibu.

Pepe aliwaalika marafiki na jamaa zake kuhudhuria harusi.  

Alichangamka sana akidhani kuwa amempata msaidizi.

Bi harusi alipatiwa vikapu vya wimbi, mikeka, ndizi, njugu, na zawadi nyingine.

Baada ya sherehe ya harusi, wageni waliondoka kurudi makwao. 

Pepe alikuwa tayari kuanza maisha mapya pamoja na mkewe na mbwa wake.

Siku iliyofuata, Pepe alimwandalia mkewe ndizi tamu, lakini alikataa kuzila.

Lakini Pepe alipokwenda kuwinda, mwanamke huyo alizila ndizi zote.

Baadaye Pepe aliporudi kutoka mawindoni alihisi njaa. Alitaka kuzila zile ndizi tamu. 

Mkewe alimwambia kuwa mbwa alizila zote!

Siku iliyofuata, Pepe alikwenda shambani. 

Aliporudi, alipata kuwa mkewe alikuwa ameila nyama yote. Hakumgawia hata mbwa.

Siku nyingine, Pepe alikwenda kumtembelea rafikiye. 

Aliporudi, mkewe alikuwa amezila njugu zote. Kikapu kilikuwa kitupu. Pepe alimkasirikia sana mkewe.

Pepe aligundua kuwa mwanamke huyo alikuwa na  shida. Aliamua kumnasa. 

Aliweka maziwa katika chungu cha ajabu kisha akakiweka mvunguni. Akaondoka kwenda kuwinda.

Mwanamke alikiona chungu kilichokuwa kimejaa maziwa. Alikichukua akakiweka mdomoni. Aliyanywa maziwa yote huku mbwa akimtazama.

Kwa bahati mbaya, chungu kilikwama mdomoni. Alijaribu kukiondoa, lakini ilikuwa bure. Alipiga kelele na kuruka juu na chini. 

Chungu kilikwama pale pale. Mbwa alitazama haya yote.

Mbwa alikimbia kumtafuta Pepe. Alibweka, akabweka, akaruka juu na chini. 

Pepe alifahamu kuwa kulikuwa na jambo mbaya nyumbani.

Walikimbia pamoja kwenda nyumbani. Pepe alistaajabu kumpata mkewe na chungu mdomoni. 

Akamtazama kwa mshangao.

Pepe alimgusa mkewe kwenye shavu na chungu
kikaanguka mara moja. 

Mwanamke huyo aliaibika sana akaamua kurudi kwa wazazi wake.

------------------------------------------------------------



Tembo na Sungura walikuwa marafiki.

Walilisha mifugo yao sehemu iliyokuwa na nyasi na maji.

Walizoea kucheza mpira wa miguu.

Tembo alifunga mabao mengi.

Sungura hakufurahi.

Sungura aliuliza, "Nini inakusaidia kucheza vyema?"

"Miguu yangu minono."

Sungura na Tembo walishindana mbio. 

Sungura alishinda.

Alimwuliza, "Nini inakusaidia kwenda mbio?" 

"Miguu yangu myembamba."

Tembo alimwuliza Sungura, "Nitapataje miguu myembamba?"

"Nitakuonyesha."

Sungura alisema, "Simama ndani ya moto."  

Tembo alilia, "Ninaungua!"

Sungura alisema, "Hii ndiyo njia pekee ya kuipata miguu  myembamba."

Tembo alilala chini.

Kwa siku nyingi, hakuweza kusimama.

Alipopata nafuu, alienda nyumbani kwa familia yake.

Sungura alisikitika sana. 

Alimwomba Tembo msamaha.

------------------------------------------------------------



Siafu alikuwa mkulima mzuri.

Aliishi kwenye ardhi na familia yake.

Walifanya bidii katika shamba lao.

Familia ya Siafu iliishi vizuri.

Njiwa alikuwa jirani ya Siafu.

Njiwa aliishi kwenye mti na familia yake.

Njiwa na familia yake hawakulima.

Walistarehe mchana kutwa.

Njiwa na familia yake waliimba vizuri.

"Mtatugawia chakula?" Njiwa aliuliza.

"La! Limeni chenu!" Siafu alijibu.

Njiwa aliruka chini na kuanza kuimba, "Siafu ni mfalme!"

"Siafu ni mfalme! Siafu ni mfalme! Siafu ni mfalme!"

Siafu alifurahi.

Walipewa chakula.

Baada ya kula, Njiwa na familia yake walirudi kwao.

Kesho yake, Njiwa alimkejeli Siafu.

"Kwani wafalme wana vichwa vikubwa?"

"Huna shukuruni. Tena wewe ni mvivu!" Siafu alilalamika.

"Samahani!" Njiwa alisema, halafu akaanza kuimba, "Siafu ni mfalme!"

------------------------------------------------------------



Huyu anaitwa Bi Simu. 

Mtazame vizuri!

Bi Simu ana simu tano. 

Asubuhi, yeye huzipanga simu zake tano mezani.

Kila simu inatumika kwapigia watu tofauti. 

Simu ya rangi ya manjano ni ya kuwasiliana na familia yake.

Nayo ile ya rangi nyeupe, ni ya kuwasiliana na wenzake anaofanya nao kazi.

Bi Simu huitumia ile ya rangi nyekundu kuwasiliana na watu anaowadai!

Ile ya rangi ya waridi ni ya kuwasiliana na marafiki zake wa karibu.

Kuna ile ya kizambarau.

Bi Simu huitumia hii kuwasiliana na wanaohitaji msaada wake.

Bi Simu hufurahia watu wanapofurahi. 

Hapendi ugomvi wala vita.

Asipokuwa kazini, Bi Simu huwaalika watoto ukumbini kwake. 

Wao hutazama runinga na kupata mawaidha.

Bi Simu anawahurumia wanyonge. 

Huwatembelea wagonjwa na wazee nyumbani kwao.

Kila apitapo, watu hupiga mayowe wakimwita, "Bi Simu! Bi Simu!"

Naye hufurahia na kusema, "Mimi ni Bi Simu. Nazitumia simu zangu kuwasiliana na wote." 

Huyo ni Bi Simu na simu zake tano!

------------------------------------------------------------



Ni karibu wakati wa mapumziko katika shule ya Msingi ya Siyafunda. Wamiliki wa maduka mawili yaliyo pale shuleni wanatayarisha chakula cha mchana ili kuwauzia wanafunzi wenye njaa.

Dukani kwa Bwana Mkweli mikate imekatwa tayari kutengeneza robo zitakazonunuliwa na wanafunzi. Anakata sehemu nyororo iliyo katikati kisha anaweka ndani mayai. Mkweli pia anaweka vijiko viwili vya kachumbari iliyotayarishwa na mkewe. Yeye hupenda kujigamba kwamba robo za mkate anazouza zina mayai ndani na juu kuna kachumbari!

Katika duka la Hadaa, mayai karibu yawe tayari, lakini bado anakata mikate kutengeneza robo. Ana wasiwasi kwa sababu biashara hayiendi vizuri dukani kwake. "Ilianza vizuri," Bwana Hadaa anawaza. "Lakini, sasa ninapata wateja wachache sana. Ingawa ninapunguza gharama yangu kwa kuikata mikate sehemu tano badala ya nne."

Jabu na Zorina wananunua chakula cha mchana. Zorina ananunua kutoka kwa Bwana Hadaa. Jabu naye ananunua kutoka kwa Bwana Mkweli. Jabu anaamini kuwa robo anazouza Bwana Mkweli zina mayai na kachumbari nyingi kuliko zile anazouza Bwana Hadaa.

Foleni iliyo nje ya duka la Bwana Mkweli ni ndefu zaidi. Zorina anamsubiri Jabu. Kisha marafiki hao wanaketi pamoja kwenye kivuli kufurahia robo zao za mkate.

Zorina anona kitu kinachomfanya aukunje uso wake. "Unatazama nini?" Jabu anauliza. Zorina anajibu, "Robo yako! Inaonekana kubwa kuliko yangu."

Wanazitazama robo zao kwa makini. Ni kweli kuwa robo ya Jabu ni kubwa kuliko ya Zorina. Zorina anasema, "Hakika, hapa kuna kitu kisicho sawa. Ama hii ndiyo sababu duka la Bwana Hadaa halina tena wateja wengi." Jabu anajibu, "Nilisikia kwamba baadhi ya watoto walimwona Bwana Hadaa akiukata mkate vipande vitano vya kutengeneza robo zake!"

Nora anawasikia Jabu na Zorina wakiongea naye anataka kujua tofauti ya kuukata mkate vipande vitano. Zorina na Jabu wanajibu pamoja, "Kipande cha robo tunachouziwa ni robo ya mkate!" Nora anaonekana kutoelewa, kwa hivyo, Zorina anamweleza, "Lazima mkate ukatwe vipande vinne vilivyo sawa ili kila kipande kiwe robo ya mkate mzima."

Nora amekasirika kwa sababu yeye pia hununua kwa Bwana Hadaa. "Kwa hivyo anatuibia, sivyo!" anasema kwa sauti kubwa. Zorina anaamua kurudi kwa Bwana Hadaa kulalamika. Anatembea huku amebeba robo ya mkate wake juu. Nora anamfuata nyuma haraka. Jabu anashusha pumzi kisha anawafuata marafiki zake.

Bwana Hadaa anaudhika anapoona kuwa wao sio
wateja wapya. Anasema, "Hamjambo, tena, watoto. Je, niwasaidie namna gani?" Nora anamwuliza kwa ukali, "Bwana Hadaa, ulinipatia kipande nami nikakulipa pesa za robo. Lakini hii si robo," Nora anasema huku akiashiria kipande chake. "Ninataka
robo ya mkate au unirejeshee pesa zangu," anasema kwa ukali.

"Je, ni kweli Bwana Hadaa? Umekuwa ukituhadaa!" Nora analia. Wakati huo baadhi ya watoto wamewafuata hadi pale dukani. Wao pia wanasikiliza shutuma anazopata Hadaa. Hadaa anawapungia mkano kwa madharau, "Ni nini hiki mnachosema kunihusu? Mimi si mtu wa aina hiyo! Ninataka mwondoke dukani kwangu mara moja!"

Zorina anasema kimya kimya, "Tutamwambia kila mtu kuhusu kile unachofanya. Ujumbe huo utaenea kama moto shuleni kote. Utalazimika kulifunga duka lako. Hakuna atakayenunua kutoka kwako!" Bwana Hadaa anawatazama watoto wale watatu wanaosimama mbele yake. Kisha anautazama umati unaoendelea kuongezeka nje ya duka lake.

Mwishowe, Bwana Hadaa anasema, "Vyema, nitakurejeshea pesa zako." Jabu anasema, "Pia, ahidi kwamba utaukata mkate vipande vinne kuzitengeneza robo." Bwana Hadaa anaahidi kwamba atafanya hivyo. Kisha anasafisha koo yake na kusema kwa sauti ili kila mmoja asikie, "Pia, ninaahidi kwamba nitaongeza kiasi cha kachumbari na mayai kwenye robo za mkate."

Bwana Hadaa kweli aliongeza kiasi cha mayai na kachumbari kwenye robo za mkate alizotengeneza. Baadaye, watoto zaidi walikuwa wakinunua kutoka kwake na duka lake lilianza kupata faida. Aliweza kumwajiri mtu wa kumsaidia.

Sasa, kuna ushindani mzuri kati ya Bwana Hadaa na Bwana Mkweli. Kila mtu anafurahi.

Andika tafsiri ya picha uionayo hapa.

------------------------------------------------------------



Ilikuwa harusi ya kwanza katika familia ya Tenana. Refi alikuwa amechangamka sana. 

"Nitakuwa msaidizi wa Elsa nikiwa nimevaa nguo na viatu vipya!" Refi aliwaelezea kuku wake. Aliwaelezea kuku wake kila kitu. 

Babake alikuwa amempa kuku kama zawadi alipokuwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake. Refi aliwapenda sana.

"Refi, waondoshe hapo hao kuku wachafu!" Mamake alipiga kelele, "Siwataki popote karibu na hema la harusi."

Refi aliwafukuza kuku kutoka kwenye hema. "Tokeni enyi viumbe washienzi," alisema. "Singependa mliwe wakati wa harusi ya Elsa."

"Mama asema kwamba hii itakuwa harusi ya kufana zaidi katika kijiji cha Mailisaba," Refi aliwaambia kuku wake. "Pia anasema kwamba ninaweza kuwasaidia wasichana wale wakubwa kupika." Kuku hawakumsikiliza hata kidogo. 

"Refi!" Mamake alimwita kutoka ndani, "Tafadhali acha hao kuku. Njoo unichungie chungu!"



Mamake Refi alijivunia nyumba yake na alitaka iwe safi siku ya harusi. Alisafisha, akaosha na kusugua kila kilochokuwamo. Alipomaliza, hapakuwa na chembe cha vumbi popote. 

Kuku walipochokoa vichwa mlangoni, Mamake Refi alipiga mayowe, "Tokeni nje ninyi viumbe vyenye miguu na midomo michafu!"

Refi aliwafuata kuku wake hadi kwenye jua. "Mama anasema ukweli, mnaaibisha," aliwakemea. 

Refi alitabasamu kisha akaenda kujaza ndoo maji. Alikuwa na wakati mgumu kuwashika kuku wake. Hawakudhani kwamba ilikuwa jambo zuri wao kuoga.

Refi alimweka kuku wa kwanza ndani ya ndoo ya maji. "Kaa wima, ewe kiumbe shenzi," alipiga kelele. "Haitachukua muda mrefu kukuosha!"

Refi alipopangusa pua na macho ya kuku, ghafla kuku alikuwa dhaifu akaanguka kando ya ndoo. "Huu sio wakati wa kulala," Refi alisema. 

Alimtikisa kuku kwa nguvu ili maji yote yadondoke. Kisha akamlaza juu ya nyasi ili akauke. Kuku alitulia pale akiwa amelala.

Aliwaosha kuku wote wanane na kuwaweka mstari mmoja juu ya nyasi ili wakauke. Hakuna yeyote aliyepapatua hata unyoya mmoja. 

"Nitawaacha mlale kwa muda mfupi," Refi aliwaza. Alienda kukitazama chungu kilichokuwa mekoni.

Shangazi zake Refi, yaani Mama Netty na Mama Teddy, walikuwa wakitayarisha harusi ya Elsa. 

Walitakiwa kufanya matayarisho hayo kwa pamoja lakini hawakupendana hata kidogo.

Mama Netty aliwaona kuku wa Refi wakiwa wanakauka. "Hiki ni chakula kizuri kwangu. Nitawapeleka nyumbani!" Alijiambia. 

Alilichukua kanga lake na kuwafungia kuku wote mle ndani. Hakuna kuku hata mmoja aliyesonga. "Sawa kabisa!" Alitabasamu. "Sasa nitawaweka mahali ambapo Mamake Teddy hatawahi kuwapata." 

Alikiweka kifurushi hicho pembeni kati ya maboga."

Mama Teddy aliamua kutayarisha kitoweo alichokipenda. Alikwenda katika bustani ya maboga. Alikiona kifurushi cha Mama Netty chini ya mboga. 

Alipokifungua, kuku wote wanane walianguka nje. "Esh!" Alipiga kelele huku akiruka nyuma kwa mshangao. "Ah, ninyi ndio kuku wasafi kuliko wote! Mko tayari kwa chungu changu," aliwabembeleza. "Sasa nitawaficha wapi wapenzi wangu?" Mama Teddy alicheka. "Lazima nipate mahali pazuri kabisa," alisema huku akitembea nyumbani.

"Ninajua," alisema hatimaye, "Nitawaweka paani!" Mama Teddy alipanda juu akawaweka kuku katika mstari kwenye paa la nyumba ya nyasi.

Siku iliyofuata, jua lilichomoza kwa wakati mzuri kwa harusi. Refi alikuwa wa kwanza kuamka na kwenda kuwatazama kuku wake. 

Hakuwapata mahali alikuwa amewaweka. "Lazima wawe wamekauka vizuri kwa sasa. Nina hakika wameenda kutafuta kifungua kinywa chao," alisema.

Harusi ya Elsa ilikuwa ya kufana. Wale kuku hawakuamka kutoka paani. Kwa hivyo, hawakujiunga na wasichana wasaidizi wa bi-harusi walipoingia wakicheza. 

Hakuna kuku yeyote aliyetikisika wakati kwaya ya kanisa iliimba kwa sauti ya juu nyimbo nzuri za kuvutia. Walikuwa bado wanalala juu ya paa wakati Padre alihubiri. 

Hawakutikisa hata unyoya wakati nguruwe na babu yake Refi walipokoroma mahubiri yalipoendelea.

Hakuna hata mguu mmoja wa kuku uliotetemeka wakati kondoo waliranda na kuingia ndani ya hema wakiwa karibu kuangusha keki ya harusi. 

Wakati babake bwana harusi alipokuwa katikati ya hotuba yake ndipo mambo yalianza kubadilika paani.

Kuku wa kwanza aliyanyoosha mabawa yake na kuruka kwenye kifua cha Mamake Molly. 

Mama Teddy aliyekuwa amekaa karibu naye alianza kucheka. Kuku mwingine alirukia kitambaa kipya cha Mama Netty. Watu waliokuwa kwenye meza nyingine walizuia kicheko. 

Mwanamke aliyekaa karibu na Mama Netty aliweka kichwa chake chini ya meza, "Ai, aai, aaaaii, he, he, heeeeeeee!" Alicheka.

Wale kuku wote waliamua kujiunga na wale wawili wa kwanza. 

Hungeweza kumwona Mama Netty kwa sababu alikuwa amefunikwa na kuku hao wote!

Wageni walicheka kwa mayowe. Wanaume walilazimika kuzishika tumbo zao. Wanawake waliviringika katika viti vyao. 

Vijana walijishikilia kwa wenzao. Akina nyanya hawangeweza kupumua kwa ajili ya kucheka. Akina babu walitikisa fimbo zao. 

Halafu, shangazi hao wawili walitazamana wakaanza kucheka pia.

Mama Teddy aliufungua mdomo wake wazi kwa kicheko. 

Mama Netty alikirusha kichwa chake nyuma na kucheka hadi mashavu yakatikisika. 

Refi hakuamini!

Wageni wote walikubaliana kwamba hiyo ilikuwa harusi nzuri zaidi iliyowahi kufanyika kijijini Mailisaba. 

"Aa, mna bahati sana! Refi aliwaambia kuku wake alipokuwa anawaweka kwenye chumba chao usiku ule. 

"Mama anasema kuwa hatawahi kuwaweka kwenye chungu chake."

"Lakini, tazama jinsi mlivyo wachafu tena," aliwaambia. 

"Nadhani nitalazimika kuwaosha tena kesho!"

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Sima na Samaki waliishi katika kijiji kimoja.

Urafiki ulianza kati yao.

Samaki alimwambia rafiki yake Sima waende pamoja baharini waogelee. 

Walishika njia wakaenda baharini.

Walipofika kando ya bahari, Samaki alimwambia Sima, "Mimi naingia majini kuoga," kisha akapiga mbizi.

Baada ya kuogelea kwa muda mfupi, Samaki alimwambia Sima, "Sasa ni zamu yako kuogelea." 

Sima alimjibu, "Siwezi kuogelea. Nikiingia majini, nitazama halafu nitaumbuka."

Samaki alimbembeleza Sima akisema, "Njoo ujaribu. Hutaumbuka na ukizama, nitakuokoa." Sima alikubali. 

Sima alipofika majini, alishindwa kuelea. Alimwita Samaki, "Njoo uniokoe," lakini Samaki hakumwokoa.

Mtu mmoja alimsikia Samaki akilalamika kwamba hangeweza kumwoka Sima. Mtu huyo akamwuliza, "Kuna shida gani?" 

Samaki akasema, "Huyu mjinga ameingia majini na sasa anazama." Mtu huyo alimwokoa Sima.

Sima alipotoka majini, alisema, "Samaki ni rafiki mbaya. Amenishawishi niogelee nami sijui kuogelea." 

Mtu huyo aliwaambia, "Hebu niwatatulie tatizo hili." Alikata Sima na Samaki, akala kwa fujo. Na huo ukawa mwisho wa ugomvi kati yao.

------------------------------------------------------------



Feni alikuwa msichana mdogo aliyekimbia kama upepo. 

Feni alipenda kucheka na alijaribu alivyoweza kutenda alivyoambiwa.

Siku moja, Feni alienda na mama na baba kutafuta kuni.

Feni alipenda kumsaidia mama na baba lakini, kulikuwa na kazi nyingi za kufanya. Pia, kulikuwa na vitu vingi vya kuona: ndege, tumbili, na anga!

Mama alisema, "Feni! Tafadhali sikiliza! Unaweza kutafuta kuni hapa na hapo...

...lakini, Feni, tafadhali, chunga pahali unapokwenda, pia, kuwa mwangalifu."

Mama na baba wakashughulika kutafuta kuni.

Wakapata vipande vikubwa vya kuni.

Vilevile, wakapata vipande vidogo vya kuni.

Feni pia akashughulika kutafuta kuni.

Akapata vipande vidogo vya kuni.

Akapata vipande vidogo sana vya kuni.

Halafu Feni akatazama juu.

Akamwona ndege kwenye nyasi ndefu.

Kisha Feni akatazama chini. Akamwona chungu mwenye rangi ya hudhurungi.

Tena Feni akaliona jani maridadi. Jani hilo lilikuwa kijani kibichi na lilimetameta.

Feni akasema, "Hili halionekani kama jani!" Ghafla, jani hilo maridadi likasonga!

Feni akasema, "Hili si jani maridadi. Huyu ni nyoka kijani kibichi!"

Feni akapiga kelele, "Eii!" Feni akakimbia haraka kuwatafuta baba na mama.

Feni akamwona babake. Feni akasema, "Nyoka! Nyoka!"

Baba akauliza, "Wapi? Wapi?"

Feni akajibu, "Hapo! Hapo!"

Halafu babake akamfukuza yule nyoka kijani kibichi kwa kijiti.

Nyoka kijani kibichi akatoroka akaenda zake.

Baba akasema, "Feni, uko salama. Twende tumwambie mama kuhusu yule nyoka kijani kibichi."

Mama akasema, "Feni, nimefurahi kwamba nyoka kijani kibichi hakukuuma...

...lakini wakati mwingine, tafadhali, tafadhali, kuwa macho na utazame unakokwenda."

Na huo ukawa ndio mwisho wa jambo hilo.

------------------------------------------------------------



Ndungu yangu mdogo anachelewa kuamka. 

Mimi huamka mapema kwani, mimi ni mashuhuri!

Mimi ndiye hufungua dirisha asubuhi.

Mama huniambia, "Wewe ni nyota yangu ya asubuhi."

Ninajiosha mwenyewe wala sihitaji usaidizi wowote.

Sijali kuoga kwa maji baridi wala kutumia sabuni inayonuka.

Mama akinikumbusha kupiga mswaki, ninamjibu, "Siwezi kusahau, mama!"

Baada ya kuoga, mimi huwaamkua babu na shangazi. 

Kisha ninawatakia siku njema.

Huvaa nguo mwenyewe. "Nimekuwa mkubwa sasa," humwambia mama.

Ninaweza kufunga vifungo vyangu na kukaza kamba za viatu vyangu.

Humhimiza ndugu yangu kwenda shule.

Hufanya bidii kwa kila njia nikiwa darasani.

Mimi hufanya vizuri mambo haya kila siku. 

Lakini, ninachopenda zaidi, ni kucheza!

------------------------------------------------------------



Miaka mingi iliyopita, Mjusi na Chura walikuwa marafiki. 

Siku moja waliamua kuwatafuta wasichana wapenzi jijini.

Chura alimwonea Mjusi wivu. 

Mjusi alikuwa na ngozi iliyometameta na ya kuvutia.

Chura alimwuliza, "Ni kitu gani ulichofanya ukawa mrembo hivi? Hebu, nitazame, nina sura mbaya mno. Ninawezaje kuirembesha ngozi yangu?"

Mjusi alimjibu, "Sikiliza! Tia maji chunguni kisha ukiweke mekoni. Halafu u..."

Hakumaliza usemi wake. Chura alimjibu, "Ninajua tayari, najua. Fyata ulimi, rafiki yangu." Kisha aliondoka.

Chura alipofika nyumbani, aliyatia maji chunguni.

Maji yalipoanza kuchemka, alijitumbukiza ndani.

Ngozi yake ikachomeka na mkia wake ukakatika!

Na badala ya kumetameta na kuwa mrembo kama Mjusi, alikuwa na sura mbaya zaidi!

------------------------------------------------------------



Siku moja nikiwa nimekaa darasani, nilichungulia dirishani na kuona tai mkubwa wa kahawia akiruka.

Mabawa ya tai yalikuwa wazi lakini hayakupapatika.

Hili lilinifanya niwe na hamu ya kutaka kujua zaidi kuhusu kuruka.

Labda ndege walishawishi uvumbuzi wa chombo cha ndege. Ndege ana mabawa, na ndege, chombo cha kusafiria, pia kina mabawa.

Natamani kuruka, lakini sina mabawa.

Nilienda maktabani kutafuta vitabu kuhusu ndege. Nilitaka kujua jinsi zinavyoruka.

Niliona picha za mashine tofauti za kuruka. Mashine zingine zilikuwa na injini, zingine hazikuwa nazo.

Niliona chombo cha kuning'inia na parachuti.

Niliona roketi, helikopta, zepelini, puto za hewa moto, na ndege za zamani sana. Zile unaweza kupata kwenye sehemu za makumbusho.

Ndege inarukaje? Ndege nyingi za kisasa zinaendeshwa na injini za jeti. Injini za jeti husogeza ndege mbele kwa kasi sana. Hiyo hufanya hewa kutiririka kwa kasi sana juu ya mabawa ya ndege.

Mabawa yanasukuma hewa nyuma kuelekea ardhini. Hiyo husababisha shinikizo la juu au nguvu. Nguvu ya juu inashikilia ndege angani.

Kitu cha karibu zaidi ninachoweza kufanya ili kuruka, ni katika ndege. Umewahi kuwa ndani ya ndege?

Nimekuwa nikitamani kuruka katika ndege kubwa.

Mwalimu wangu alituambia kwamba tunaweza kutimiza matakwa yetu kwa kufunga tu macho na kuwaza juu yake.

Kwenye mawazo yangu, ninasikia: 

Mimi ni rubani wako. Mimi ndiye nahodha wa ndege hii.

Tafadhali funga mkanda wa kiti chako na ujiandae kwa safari.

Tayarisha njia ya kurukia ndege, ninaanzisha injini za ndege!

Wewe ni abiria umeketi kwenye kiti cha dirisha.

Tunaenda kwa kasi kwenye njia ya kurukia ya ndege. Tunapaa kutoka uwanja wa ndege.

Injini na mabawa ya ndege zinatusukuma angani. Tutaruka juu zaidi kuliko ndege yeyote.

Mwalimu wangu alisema tunaweza kufanya chochote katika mawazo yetu.

Alisema tunaweza kuwa chochote tunachotaka kuwa, au kufanya chochote tunachotaka katika akili zetu.

Je, ungependa kuruka kwenda wapi?

------------------------------------------------------------



Anansi na Sungura walikuwa marafiki. 

Anansi alionea wivu mali ya Sungura.

Anansi alimfukuza Sungura kisha akachukua shamba lake.

Anansi aliuza mazao yote akapata pesa nyingi.

Anansi alirudi nyumbani akiwa amekibeba kikapu kichwani.

Anansi alikiweka kikapu chini akajikinga asinyeshewe.

Muvua ilisababisha mafuriko hadi Anansi akajificha shimoni.

Tai alikiona kikapu akakifunika kwa mabawa yake.

"Kikapu hiki ni changu," Tai alisema. 

"Ni changu!" Anansi alimjibu.

Tai alisema, "Nilipata mahindi na pesa hapa bila mwenyewe."

Chifu na wazee wake walichukua muda kuamua nani alisema ukweli.

Hatimaye, walisema, "Tai anasema ukweli. Kikapu ni chake."

Sungura alirudi katika shamba lake.

Anansi hakua na pesa wala marafiki.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na kijiji kilichoitwa Noti kilichokuwa karibu na msitu. 

Paliishi mwanamume mmoja aliyefuga ndama mnono. Alizoea kumfunga msituni kwenye kina cha mti.

Mle msituni paliishi wanyama pori.

Kulikuwa na Fisi na rafikiye Sungura.

Sungura na Fisi waliwinda kwa zamu. Sungura alimkumbusha Fisi kuwa ilikuwa zamu yake kwenda mawindoni. 

Fisi aliwinda kila mahali, lakini alikosa chakula akaamua kurudi nyumbani.

Ghafla, Fisi aliisikia sauti ya ndama. Aliamua kuelekea ilikotoka ile sauti ili kujua chanzo chake.

Kwenye shina la mti alikuwa amefungwa ndama.
Ndama alipomwona Fisi alihofia usalama wake.

Ulafi wa Fisi ulimfanya atake kila kitu na akaanza kwa kutafuna kamba kabla amfikie ndama. 

Kamba ilipokatika, ndama akapata nafasi ya kutoroka.

Fisi aliduwaa ndama alipotimua mbio kuelekea zizini. 

Fisi alimkimbiza ila hakumfikia.

Mzee aliskia kilio cha ndama zizini akatoka nje kwa haraka kutaka kujua kilichotendeka. 

Alikutana ana kwa ana na Fisi. Fisi kumwona mzee, aligeuka na kutoroka.

Fisi alikutana na rafikiye Sungura akamweleza bahati mbaya iliyomsibu. 

Wawili hao hawakuamini kuwa walikosa kumla ndama mnono kama huyo!

------------------------------------------------------------



Zamani za kale, kulikuwa na kijiji kimoja katika Kaunti ya Turkana. 

Wanakijiji walikutana kila jioni kucheza ngoma ya kienyeji iitwayo edonga.

Wachezaji wa kijiji hicho walifahamika kila pahali. 

Walikuwa na ustadi mkubwa wa kucheza ngoma ya edonga.

Watu kutoka vijiji jirani walifika kijijini humo kucheza ngoma hiyo.

Siku moja, mgeni aliyeusikia umaarufu wa ngoma hiyo ya edonga, alituma mjumbe wake aende kuipeleleza.

Mjumbe alipofika, wanakijiji walijawa na hofu. Wakajiuliza, "Huyo mgeni ni nani? Mbona amemtuma mjumbe wake?" 

Wanakijiji walijitayarisha kama kawaida. Walimchinja mbuzi na kupika chakula kingi.

Vilevile walikutana wakaandaa kafara na kusubiri siku nzima hadi jioni ila mgeni hakufika.

Walicheza ngoma kama kawaida hadi usiku wa manane. 

Usiku huo kulikuwa na wachezaji ngoma wengi na kila mtu alikuwa amesisimka.

Kabla ya ngoma kuisha, mgeni alifika. 

Kwa mavazi alifanana na wanakijiji, kwa hivyo, hawakumtambua.

Alipopata nafasi ya kucheza ngoma, alijiunga na wanaume wengine. 

Ilionekana wazi kuwa alicheza tofauti na wenyeji.

Watu waliaanza kumcheka. Wachezaji wengine walicheka wakiwa wamepiga magoti. Wengine walikaa kitako. Wengine walianguka chini.

Mgeni alikasirika alipochekwa. Akaamua kuwalaani.

Aliacha kucheza ngoma ghafla. Mara hiyo hiyo, kila mchezaji akabadilika kuwa jiwe. 

Waliolala, waliosimama, waliokaa kitako na waliopiga magoti, wote walibaki walivyokuwa. 

Kisha mgeni akatoweka kijijini.

Mawe hayo yamebaki mahali pale hadi wa leo. 

Saa za usiku husikika yakiimba na kucheza edonga. 

Hiyo ndiyo asili ya Namorutunga.

------------------------------------------------------------



Mbuni na Simba walikuwa marafiki sana. 

Kila mmoja alikuwa na watoto wachanga.

Mbuni aliwalisha watoto wake vizuri.

Watoto wa Simba hawakupata chakula cha kutosha.

Simba aliwaangalia vifaranga na kuwaza, "Hawa ni wazuri! Natamani wangekuwa wangu!"

Wakati Mbuni alikuwa hayupo, Simba aliwachukua watoto wa Mbuni akaenda nao nyumbani kwake.

Mbuni alirudi na kupata watoto wa Simba nyumbani kwake. 

Alifadhaika na kujiuliza, "Watoto wangu wako wapi?"

Mbuni alikimbia nyumbani kwa Simba. 

Aliwapata wanawe wakiwa na Simba.

Simba alikataa kuwarudisha watoto wa Mbuni. 

Alisema, "Hawa ni wangu sasa. Unaweza kuwachukua wangu."

Mbuni alikasirika sana. 

"Nitafanyaje ili niwapate watoto wangu?" alijiwazia.

Halafu alifikiri, "Ninajua nitakachokifanya. Nitawaita wanyama wote kwa mkutano."

Wanyama walikubali kukutana.

Tembo aliwauliza Mbuni na Simba kuzungumza.

Wanyama wengi waliogopa kumlaumu Simba.

Mwishowe, Kichakuro alisimama na kusema, "Watoto ambao wanafanana na ndege ni wa Mbuni. Watoto ambao wana mikia ni wa Simba."

Kichakuro alitorokea tunduni. 

Wanyama wote walishangilia.

Simba alikasirika sana. 

Alienda nyumbani na watoto wake.

------------------------------------------------------------



Rinda hili ni refu.

Sweta hii ni kubwa.

Mkoba huu ni mkubwa.

Mshipi huu ni mfupi.

Kofia hii ni ndogo.

Soksi hizi ni fupi.

Lakini, viatu hivi ni vipya.

Vinanitosha vizuri.

------------------------------------------------------------



Familia yangu iliamua kuona Maporomoko ya Maji ya Nyahururu ambayo ni maarufu. 

Yanapatikana kwenye Mto Ewaso Nyiro karibu na mji wa Nyahururu.

Kutoka Nairobi hadi Nyahururu ni kilomita 192.4.

Tulitumia muda wa masaa manne kusafiri kwa gari.

Maji haya yanaporomoka mita 72.

Wakati mwingine, unaweza kuona rangi za upinde karibu na Mapromoko: nyekundu, rangi ya chungwa, manjano, kijani, samawati, nili na zambarau.

Tuliweza kwenda hadi chini ya Maporomoko.

Ilitubidi tujihadhari kwani kuna mvuke unaolowesha mawe na kuyafanya yateleze.

Wakati wa kuteremka tuliweza kuwaona wanyama na wadudu tofauti. 

Tuliwaona nyani na kinyonga.

Kuna miamba, miti mikubwa na mimea ya aina tofauti. 

Nilifurahia sana kupanda juu ya miamba niliyoiona.

Ukifika chini ya Maporomoko, utaona maji yakipiga miamba. 

Ni pahali pa kupendeza.

Tulipiga picha maridadi. Lakini, tahadhari ni lazima.

Baada ya kushuka na kupanda, tulipata pahali palipozungushwa vyuma vya kuweka usalama. 

Tulipigwa picha zaidi na kujiburudisha kwa vinyawaji vya soda au maji.

Pia, kuna watu waliovalia kama jamii ya zamani ya Kikuyu.

Tuliowapiga picha na pia tukapigwa picha nao.

Kuna hoteli maridadi pale inayoitwa Thomsons Falls Lodge. Ilijengwa mwaka wa 1931. 

Tuliingia pale na kula chakula cha mchana.  Baadaye, tuliendelea na ziara zetu.

------------------------------------------------------------



Ilikuwa Jumamosi asubuhi. Maya, Dama na Dominic walikuwa wakimsaidia Mama Koki katika bustani yake ya mboga. Watoto hao walikuwa wakipalilia na kunyunyizia mboga maji. Baadaye, walichuma mboga zilizokomaa. Kila mmoja wao angepeleka nyumbani stroberi, mchicha na karoti.

Mama Koki alipenda kuwaandalia watoto sherehe ndogo walipomsaidia. Huwapatia keki, chokoleti, au peremende zinazofanana na nyoka. Wakati mwingine aliwapatia matofaa, pea au machungwa. Mama Koki alikuwa na sharti moja tu. "Wagawe yote sawa!" Watoto walijua kuwa ni lazima wagawane kila kitu walichopatiwa kwa kiasi sawa.

Mama Koki alioka keki na watoto walisubiri kupatiwa ili wagawane. "Hii hapa keki!" Mama Koki alisema akitabasamu. "Kumbukeni sharti kwamba kila mmoja lazima apate kiasi sawa. Gaweni sawa! Mspigane!"

Maya alikuwa wa kwanza kujaribu kugawa keki. Alitumia kisu kuweka mistari juu ya keki. Wengine walimtazama. "Nitakata sehemu tatu zilizo sawa!" Maya alisema akiwaonyesha.

"Hapana!" Dama alikataa. "Kipande cha katikati ni kikubwa zaidi!" Dominic pia alitikisa kichwa. Maya alicheka kisha akamwambia Dama ajaribu kugawa.

"Nipe kisu nikate. Hii ni kazi rahisi!" Dama alisema. Kwanza alifuta mistari aliyoiweka Maya kisha akajlamba vidole.

Dama alianza kwa kugawa kutoka juu hadi chini na kutoka upande mmoja hadi katikati. "Tazama, hizi ni sehemu tatu!" 

Maya na Dominic walilalamika pamoja, "Sehemu hizi tatu si sawa!"

"Gawanya sawa! Lazima kila kipande kiwe na ukubwa ulio sawa na umbo sawa," Dominic akaongeza. 

Dama akajibu, "Dominic, si ujaribu? Nina hakika hutaweza!"

"Keki hii ingekuwa umbo la mraba au pembe nne, ingekuwa rahisi kugawa!" Dominic alisema. "Ingekuwa rahisi pia tungegawana tukiwa wanne." Maya aliongeza kusema.

Wakati huo, Dominic alikumbuka gari la babake. Lilikuwa na alama ya mistari inayowezesha kugawa sehemu tatu zilizo sawa. Akasema, "Najua tutakavyogawa."

Dominic akachora mistari mitatu juu ya keki. Keki ingekatwa kufuata mistari hiyo, ingekuwa vipande vitatu vilivyo sawa.

Dama alisema, "Umetushangaza sana Dominic. Umewezaje kuhakikisha umegawa vipande sawa?"  

Dominic alitabasamu. Hakutaka kuwaambia siri yake.

Wakati huo, Mama Koki alitoka ndani ya nyumba akiwa amebeba bilauri za sharubati. "Mama Koki, Dominic amepata njia ya kukata keki vipande vitatu vilivyo sawa," Maya alimwambia. 

"Hongera Dominic, umefaulu kugawa sehemu tatu zilizo sawa! Sasa ni wakati wa kwenda nyumbani," Mama Koki aliwaambia.

Kisha Maya alikata keki taratibu kufuata mistari iliyochorwa na Dominic. Watoto walihakikisha kwamba sehemu zote zilikuwa sawa. Kila mmoja akaiweka keki yake tayari kwenda nyumbani.

Babake Dominic alipowasili kuwachukua watoto, Dominic alimlaki akitaka kumweleza jinsi alivyofaulu kuigawa keki vipande vitatu vilivyo sawa.

Andika hapa tafsiri ya maumbo haya.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na mtu aliyekuwa akitembea kichakani. 

Ghafla, alimkuta Simba!

Ulikuwa msimu wa baridi. 

Simba alikuwa akipumzika kwenye nyasi fupi.

Makutano hayo yalitokea ghafla mtu huyo asijue la kufanya. 

Alijawa na woga.

Mwanzoni, Simba pia alishangaa na kuogopa kidogo. 

Lakini, mngurumo mkubwa ulisikika kutoka tumboni mwake kwani alikuwa na njaa.

Mtu yule alijikuta juu ya mti mrefu. 

Alianza kupiga mayowe.

Simba alilala chini ya mti akisubiri mlo. 

Muda ulipopita, Simba alijifanya kuwa analala usingizi.

Muda mfupi baadaye, mtu yule alilala usingizi. 

Aliamka tena na mwishoni alisinzia na kulala fofofo.

Aliporomoka kutoka juu na kumwangukia yule Simba aliyelala.

Wote waliamka wakiwa wamechanganyikiwa na kuogopa. 

Simba alisahau mlo wake na kukimbilia usalama wake.

Mtu yule alianza kukimbia akielekea upande mmoja na Simba. 

Aligundua kwamba alikuwa akikimbia na Simba!

Kwa hivyo alibadilisha mwelekeo wake na kuepuka kuliwa na Simba!

------------------------------------------------------------



Eba na mkewe Lelisa walifanya kazi zao kwa bidii sana. 

Walikuwa na watoto wawili wa kiume.

Walitimiza mahitaji yao kutokana na juhudi zao. 

Eba alitaka wanawe wastarehe. Hawakufanya kazi zozote.

Baada ya muda, Lelisa alifariki.

Hata baada ya kifo cha mkewe, Eba hakutaka wanawe wamsaidie. 

Alizifanya kazi zote za shambani na za nyumbani.

Eba alizeeka na kudhoofika. Alihofia maisha ya wanawe. 

Alijiuliza, "Wanangu wataishi namna gani nitakapofariki?" 

Alijua kuwa hawangeweza kujitegemea.

Eba aliwaita wanawe akawaambia, "Urithi mtakaopata kutoka kwangu ni dhahabu nyingi iliyofichwa shambani. Ni juu yenu kuyalima mashamba ili muipate dhahabu hiyo."

Eba pia aliwaambia majirani, "Nadhani niko karibu kufariki. Wanangu hawajui kujitegemea. Nawasihi mwasaidie hadi watakapoweza kujikimu wenyewe."

Baada ya Eba kufariki, majirani waliwapa wanawe chakula kwa muda.

Ndugu hao hawakutaka kuporwa dhahabu iliyofichwa na baba yao. 

Waliamua kuyalima mashamba wenyewe ili waipate dhahabu hiyo.

Waliyalima mashamba moja baada ya jingine. 

Ila, hawakupata dhahabu yoyote.

Mmoja alimwuliza mwingine, "Je, unadhani baba alitudanganya?" 

Yule akajibu, "La, ninadhani baba alikuwa na maana kuwa ukulima ni dhahabu."

Kwa hivyo, kama wakulima wengine, wana hao waliyalima mashamba yao. 

Walipanda mimea wakawa matajiri sana.

------------------------------------------------------------



"Njoo tucheze Kidalipo," kaka yangu aliniambia.

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12…

…92, 93, 94, 95, 96, 100!

Kaka yangu alikuja kunitafuta.

Nilikuwa nimejificha nyuma ya pazia.

Alinitafuta nyumba nzima.

Aliingia ndani ya chumba nilimokuwa nimejificha.

Nilitulia kabisa.

Nilikuwa nikiwaza, "Atanipata."

Halafu, alitoka nje!

Nilikimbia nje.

Nikapiga kelele, "Hukunipata!"

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Sungura na Kobe walishindana mbio.

Wanyama wengine walitazama mashindano hayo.

Sungura alimshinda Kobe. 

Hata hivyo, hakujivuna kwa kuwa mshindi.

Kobe na Sungura waliendelea kuwa marafiki.

Mfalme Simba aliwatuma Kobe na Sungrua kwa mfalme jirani.

Kobe na Sungura waliondoka kutimiza walivyotumwa.

Mfalme Simba aliwasubiri Kobe na Sungura kurudi.

Barabara waliyotumia ilijaa mawe na miiba.

Kobe na Sungura walitembea, wakatembea. 

Walipumzika na kuzungumza.

Walijadili jinsi ya kusaidiana.

Sungura alimbeba Kobe walipopita kwenye
miiba.

Walipofika mtoni, Kobe alimbeba Sungura wakavuka.

Kobe alitembea haraka sana. 

Sungura alijishikilia mgongoni.

Kobe na Sungura walijadiliana na mflame jirani.

Walirudi nyumbani haraka sana. 

Kobe na Sungura walikuwa marifiki wakubwa!

------------------------------------------------------------



Kijiji cha Sinyaire kimezungukwa na milima na misitu. Nyoka wengi huishi ndani ya misitu hiyo. 

Wanakijiji walimwita Unyalego nyoka aliyekuwa mkubwa zaidi. Nyoka huyo aliwameza mbuzi na kondoo wakiwa wazima.

Siku moja, Apiyo, Ajoh na Atieno walienda msituni kutafuta kuni. 

Bibi aliwaonya, "Jihadharini na Unyalego. Msichukue chochote kutoka msituni ila kuni."

Wasichana hao walifunganya maziwa, ndizi, viazi vitamu na maji. 

Wakachukua kamba za kufungia kuni na panga kali. 

Wakaondoka kwenda msituni.

Walipokuwa njiani, Ajoh, Apiyo na Atieno waliongea na kucheka. 

Ghafla, Apiyo alisema, "Kimya! Tunakaribia anakoishi Unyalego."

Ajoh hakuzingatia onyo la bibi. Atieno aliwaita,  "Tazameni, hapa kuna meno ya Unyalego ya dhahabu. Tuyachukue?" 

Apiyo aliwakumbusha, "Msisahau kwamba bibi alituonya tusichukue chochote kutoka msituni ila kuni."

Ajoh akajibu, "Simwamini bibi. Nadhani alisema hivyo ili atuzuie kuchukua tunachotaka. Najua anatuonea wivu. Mimi nitayachukua hayo meno ya dhahabu." 

Dada zake walikuwa na wasiwasi wakamwonya Ajoh lakini, hakujali.

Baadaye, Unyalego alikuja kutafuta meno yake. Alikasirika alipoyakosa. 

Aliwasikia Ajoh, Apiyo na Atieno wakizungumza na kucheka. 

Akajificha kando ya njia ambayo wasichana wale wangepitia.

Walipokwisha kuzikusnaya kuni, walizibeba vichwani. Ghafla, wakasikia "Hzzzzzzzzz!" 

Walimwona Unyalego akiwa kinywa wazi, tayari kuwameza. Waliogopa sana wakajaribu kujificha.

Unyalego akawauliza, "Ni nani aliyeyachukua meno yangu ya dhahabu?" Walipokosa kumjibu, Unyalego akaamua kuwadadisi wasichana hao. 

Akasema, "Ninataka muimbe wimbo. Yule atakayeimba bila kukosea, atakuwa hana hatia na ataenda nyumbani na kuni zake. Atakayekosea, ndiye aliye na hatia na atakuwa chakula changu kwa siku tatu zijazo!"

Apiyo aliimba kwanza kwa sauti nyororo: 

Sio mimi, sio mimi niliyeiba meno, aliyeyaiba yuko hapo nyuma aaaah. 

Kisha Atieno akaimba: 

Sio mimi, sio mimi niliyeiba meno, aliyeyaiba yuko hapo nyuma aaaah.

Mwishowe, ilikuwa zamu ya Ajoh. Kwa uwoga alisongea mbele na kuanza kuimba: 

S.i.o mi-mi, s.i.o. 

Aliimba vibaya akashindwa kuyatamka maneno sawa. Unyalego akamkemea, "Mbona huimbi vizuri kama wengine?"

Papo hapo, Unyalego akammeza Ajoh. 

Atieno na Apiyo walikimbia kuwaeleza wanakijiji yaliyotokea.

------------------------------------------------------------



Tulisafiri kwa treni ya SGR kutoka mji mkuu wa Nairobi kuelekea mji wa Mombasa.

Ndani ya treni tuliweza kununua chai na vitafunio. 

Usafi wa treni ulikuwa wa hali ya juu na huduma kwa wateja ilipendeza.

Njiani tuliona miji midogo midogo treni iliposimama kupokea abiria na kuwashusha wengine. 

Niliona miji kama Voi na Mtito Andei.

Tulipofika Mombasa, tulishuka kutoka kwenye treni na kupokea mizigo yetu. 

Nilipigwa na mshangao kwani kulikuwa na joto jingi sana. Nilianza kutokwa na jasho ingawa kulikuwa jioni. 

Tulielewa kuwa tungetumia tuktuk kwenda hadi kwenye hoteli.

Ndani ya hoteli tulijiburudisha kwa madafu baridi. 

Pepep zote zilifunguliwa ili kupata nafuu kotokana na joto.

Asubuhi iliyofuata, tulienda kuiona Bahari ya Hindi.

Tulienda upande wa ufuko wa Serena. Mchanga wake mweupe ulipendeza sana.

Tuliogelea kwenye maji yaliyokuwa na joto kiasi na kutembea mchangani. Wachuuzi wa bidhaa mbalimbali walituzingira wakitaka tununue. 

Tuliamua kulipa mashua moja itupeleke ndani kidogo.

Tulienda kuwaona samaki wa baharini. Vijana walioongoza mashua walimwaga chakula majini kuwalisha samaki. 

Samaki wa rangi ya nili, rangi ya chungwa, wa manjano na nyeusi walitokea kula. 

Tulichangamka kweli kweli!

Mashua ilitia nanga juu ya kisiwa kimoja kidogo sana.  

Hapo tulimwona pweza tukamshika na kupigwa picha naye.

Tulipewa vifaa mbali mbali vya kuvaa halafu tukaingia majini kuogelea na samaki aina nyinyi wenye rangi tofauti. 

Nilijaribu kuwashika, lakini waliponyoka kila nilipofikiri nimefaulu.

Siku iliyofuata, tulienda kuiona Ngome ya Kristo iliyojengwa mwaka wa 1593.

Ndani ya ngome, tuliviona vitu vingi vya zamani kama ngoma, vichana, mashua na silaha za vita.

Katika Mji wa Kale, tuliona milango spesheli iliyoundwa kwa ustadi. 

Pia, tuliona barabara za zamani zilizokuwa nyembamba kupindukia.

Mombasa kuna joto jingi, kwa hivyo, mavazi ya mwafaka ni mepesi na ya kulegea. 

Mama yangu alinunua vazi liitwalo dera. Naye baba akanunua kanzu.

Minazi ilikua kwa wingi na nazi ziliuzwa kila pahali. 

Tulinunua nazi nyingi pamoja na madafu na vibanzi vya muhogo.

Baadaye, tulijiburudisha kwa soda za aina tofauti na tukala biriani kwa mchuzi wa mbuzi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Ngurumo na Radi waliishi duniani miongoni mwa watu.

Ngurumo alikuwa mamake Radi.

Radi alikuwa mwenye hasira kali. 

Mara nyingi alibishana na mamake.

Radi alipokasirika, aliteketeza nyumba na kung'oa miti. 

Alitoa sauti ya kutisha, "Pia-la-la-la, pia-la-la-la!" 

Aliyaharibu mashamba na hata kuwaua watu.

Radi alipofanya vitendo hivi, mamake alimwita kwa sauti ya juu, "Bum-rambo-la-la-la, la-bum!" 

Alijaribu kumzuia asisababishe uharibifu.

Radi hakutia maanani aliyosema mamake. 

Badala yake angesababishia kila mmoja fujo alipokuwa na hasira.

Hatimaye, watu walipeleka malalamishi yao kwa mfalme.

Mfalme aliamrisha Ngurumo na mwanawe wahame kutoka kijijini. 

Aliwafukuza waende kuishi mbali na makao ya watu.

Hili halikusaidia sana. Radi alizidi kuteketeza misitu alipokasirika, "Pia-la-la-la, pia-la-la-la!" 

Wakati mwingine, ndimi za moto zilisambaa na kuunguza mashamba.

Kwa mara nyingine, watu Walienda kwa mfalme kumlalamikia.

Mara hii, mfalme aliwaambia Radi na Ngurumo kwamba hawangeendelea kuishi duniani. 

Aliwafukuza waende kuishi angani wasikoweza kusababisha uharibifu mwingi.

Tangu wakati huo, Radi anapokasirika, huweza kuteketeza na kuharibu, "Pia-la-la-la, pia-la-la-la!" 

Nasi bado tunamsikia Ngurumo, mamake Radi,  akimkemea, "Bum-rambo-la-la-la, la-bum!"

------------------------------------------------------------



Mwalimu

Wanafunzi

Darasa

Ubao

Chaki

Deski

Kiti

Meza

Kitabu

Daftari

Penseli

Kifuto

Begi la mgongoni

------------------------------------------------------------



Nala na Naka wako katika kambi iliyopangwa na shule.

Wanaweka hema zao kisha wanatazama machweo ya jua.

"Inapendeza," Nala anashusha pumzi kwa furaha.

Wanatazama jua likizama chini ya upeo wa macho upande wa magharibi.

"Kuna mwezi kamili usiku wa leo," Naka anatambua hili mwezi unapochomoza upande wa mashariki.

Watoto hao wanalala chali na kusoma anga la usiku.

Naka anashangaa, "Kuna nyota nyingi, na zinang'aa kama almasi!"

Naka anasema, "Mwezi unang'aa kwa sababu unaakisi mwanga wa jua.

Wakati mwezi ni kamili, inaonekana kama mwezi mzima unawaka."

Nala anakubali, "Mwezi huzunguka dunia. 

Mara nyingine tunaweza kuona sehemu tu ya mwezi imeangaza, na inaonekana kama ndizi."

Nala anaendelea, "Mwezi unaonekana kama mpira wa miguu wakati wa mwezi kamili. 

Mwezi unaposonga, tunaona nusu ya mwezi. Unaonekana kama ndizi."

Naka anasema kwa maringo, "Nilijua hilo! 

Nilijua pia kuwa mwezi huzunguka dunia na pamoja vyote huzunguka jua."

Nala anatabasamu, "Je, ulijua kwamba jua ni nyota?" 

Anaongezea, "Jua ni nyota kubwa ya gesi zinazowaka, zikizalisha mwanga na joto."

Naka anatambua, "Bila taa za mji, tunaona anga ya usiku kwa uwazi. 

Anga za juu huanzia juu ya safu ya hewa karibu na dunia, lakini anga za juu huishia wapi?"

Nala anatabasamu, "Tutakuwa wanaaga na kusafiria chombo cha anga chenye kasi zaidi.

Tutapita sayari na nyota za mbali zaidi. Halafu tutajua anga za juu zinaishia wapi."

Maswali

1. Hadithi inawahusu nani? Wanafanya nini?

2. Mwezi kamili ni nini? Uchore.

3. Mwezi huchomozea wapi?

4. Ni nyota ipi iliyo karibu na dunia?

5. Kuna sayari 8. Tafuta majina yake.

6. Chora picha ya jua na sayari.

------------------------------------------------------------



Siku moja, Mbwa aliyapata mayai kando ya mto.

Mbwa aliyaweka mayai hayo kumi katika kikapu.

Mbwa aliyalinda na kuyaweka mahali kwenye joto.

Mamba alimwuliza Mbwa, "Umeyaona mayai yangu?"

Mamba aliwauliza wanyama wote ikiwa waliyaona mayai yake.

Wakati huo, mayai yaliangua moja moja.

Mbwa hakuweza kuwapa mamba wachanga chakula cha kutosha.

Siku moja, Mamba aliyasikia matumbo ya wanawe yakinguruma!

Mamba aliingia nyumbani akamcharaza Mbwa kwa mkia wake.

Mamba alimkimbiza Mbwa barabarani.

Mbwa alisimama akamwambia Mamba, “Nisamehe!”

Mamba alimsamehe. Alienda na wanawe kuogelea.

------------------------------------------------------------



Mama aliziweka nguo zake katika begi ndogo. 

Kisha, aliniita.

Alinikumbatia na kusema, "Kwa heri kwa sasa binti yangu." 

Nilishangaa sana.

"Unaenda wapi, mama?" 

Nilimwuliza nikiwa na wasiwasi.

Nilianza kulia nikitaka kumfuata. Lakini, baba alinibeba juu begani kwake. 

Nililia kwa sauti lakini wapi!

Baba alisema, "Mamako anaenda hospitalini kujifungua mtoto."

Niliposikia "mtoto", nilitulia na kumwangalia baba. "Kwa nini ajifungulie hospitalini?" 

Nilitaka majibu ya haraka.

Baba alinikalisha juu ya kiti kidogo na kusema,  "Nitakueleza kwa nini ni lazima aende hospitalini." 

Nilihuzunika.

Nilisikiliza kwa makini. Lakini sikuelewa kwa nini mwuuguzi hakuja nyumbani. 

Alipomaliza, nilimwuliza, "Ataendelea kunipenda hata baada ya kurudi na mtoto mwingine?"

Babangu alinibeba na kuniambia, "Tutakupenda wakati wote." 

Nilifurahi sana.

"Ninaweza kumwandikia barua akiwa huko?" Nilimwuliza baba.

Jioni hiyo, nilianza kumtungia mama barua. 

Ilikuwa fupi.

Nilirarua karatasi kutoka daftari langu na kuanza kuandika.

Mama, mama, baba alisema kwamba umeenda kumleta mtoto mwingine?

Tafadhali, fanya upesi urudi nyumbani. Ninakuhitaji.

Ningependa umlete mtoto msichana ili niweze kucheza naye akiwa mkubwa. 

Yeye nami tutakusaidia kazi zote.

Unaweza kuleta wawili ili mmoja awe wangu ili nimpambe.

Ninakusubiri hapa nyumbani. 

Nitakulaki ukifika.

Niliikunja barua yangu ili baba ampelekee mama. 

Nilipoamka asubuhi, barua haikuwapo. 

Nikajua baba ndiye aliyeichukua.

------------------------------------------------------------



Vifungo vyangu vyote ni duara.

All my buttons are circular.

Baadhi ya vifungo vyangu ni kijani kibichi.

Some of my buttons are green.

Vifungo vyangu vyote ni vidogo.

All my buttons are small.

Baadhi ya vifungo vyangu ni manjano.

Some of my buttons are yellow.

Vifungo vyangu vyote in maridadi.

All my buttons are beautiful/stylish.

Baadhi ya vifungo vyangu ni vya rangi nyekundu.

Some of my buttons are red in colour.

Vifungo vyangu vyote vinameremeta.

All my buttons are glowing.

Baadhi ya vifungo vyangu ni bluu.

Some of my buttons are blue.

Vifungo vyangu vyote ni vizuri.

All my buttons are good.

Ninavipenda vifungo vyangu vyote.

I love all my buttons.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale,  palikuwa na Mbweha aliyekuwa na njaa. 

Alitembea karibu na kichaka akitafuta chakula.

Aliuona mzabibu uliojaa zabibu mbivu. 

Kichala cha zabibu mbivu kilining'inia.

Mbweha aliwaza, "Zabibu hizi zinaonekana tamu kweli kweli." 

Alirudi nyuma hatua chache ili aweze kuzirukia zile zabibu.

Zabibu zilikuwa juu sana. 

Mbweha alipozirukia,  alianguka kwa mgongo wala hakuzifikia zile zabibu.

Aliinuka akurudi nyuma zaidi ili aweze kuzifikia zabibu. 

Mara hii alifika karibu zaidi, lakini akaanguka tena kwa kishindo.

Alijaribu tena na tena, lakini hakuweza kuzifikia zabibu. 

Alianguka mara nying hadi mgongo ukamuuma.

Hatimaye, alikata tamaa na kwenda zake.

Mbweha alijawa na majuto. Alisimama, akatazama nyuma na kuziangalia tena zile zabibu, "Zabibu hizo,  hata hivyo, zinaonekana chachu." Akajiliwaza. 

Aliondoka akaenda zake huku akihisi njaa kuliko hapo awali.

------------------------------------------------------------



Pilipili

Kabeji

Malenge

Mbaazi

Pichi

Ndizi

Stroberi

Tikitimaji

Passioni

Maharage ya Kijani

Pilipili Hoho

Bamia

Mboga ya Saladi

Mahindi

Mbilingani

Nyanya

Karoti

Nanasi

Papai

Parachichi

Embe

Tofaa

Mapera

Viazi Vitamu

Tangawizi

Kitunguu Saumu

Vitunguu

Viazi

Machungwa

Limau

Radishi

Chenza

Cheri

Zabibu

------------------------------------------------------------



Munia aliishi na babu, bibi, shangazi na mjomba. Alifuga kuku, mbuzi, kondoo na nguruwe. Wote walikaa kwenye chumba kimoja. 

Kuku alikuwa na kitundu chake. Mbuzi, kondoo na nguruwe walifungwa pembeni. 

Bibi na babu walikuwa bado na afya nzuri. Shangazi na mjomba walisaidia kufanya kazi za pale nyumbani.

Hata hivyo, mambo yalibadilika miaka michache baadaye. Bibi na babu walizeeka na hawakuweza kusikia wala kuona vizuri. 

Shangaziye aliugua na hakuweza kusaidia katika usafi wa nyumba. 

Mjombake alilala wakati wote na hakusaidia katika shughuli za kuwalisha wanyama.

Wanyama walipiga kelele nyingi kwa sababu walikuwa na njaa. Nyumba pia ilikuwa chafu kwa sababu shangazi hakuweza kuisafisha. 

Munia alikuwa mchovu wakati wote. Alitoka kila siku kuwatafutia wote chakula.

Munia hakuweza kukabilina na hali hiyo tena. Aliwandea babu na bibi kuwauliza suluhisho. Lakini,  alihuzunika sana kwa sababu aliondoka bila suluhisho kwani hawakuweza kumsikia. 

Shangaziye mgonjwa alisema, "Ninachohitaji ni kuweza kulala usiku na kuamka asubuhi."

Mjombake mzembe alisema, "Wauze wanyama hawa kisha ukawanunulie chakula. Watalala wakome kukusumbua." 

Munia alisema kwa hasira, "Mjomba, unajua kwamba siwezi kuwauza wanyama hawa. Wao pekee ndio mali yangu."

Usiku mmoja, Munia hakupata usingizi. Alimkumbuka mtu mmoja aliyekuwa na busara. Mtu huyo aliaminika kuyajibu maswali yote na kusuluhisha matatizo yote. 

Munia aliwachukua wanyama wake akaenda nao kumtembelea mtu yule. Aliwafunga mbuzi, kondoo na nguruwe kwa Kamba kisha akambeba kuku.

Munia alifika nyumbani kwa mtu huyo akiwa amechoka na mwenye njaa sana. Baada ya kueleza shida yake, mtu huyo alisema, "Nitakusaidia, lakini ni sharti ufanye nikuambiavyo." 

Munia alijibu, "Nitafanya chochote kusuluhisha tatizo langu."

Mtu yule alimwambia, "Waache wanyama hapa kisha urudi nyumbani." 

Munia alisema, "Nimeishi na wanyama hawa kwa muda mrefu. Wao ndio mali pekee niliyo nayo."

Mtu akajibu, "Nilikuambia nitakusaidia lakini ni lazima ufanye nikuambiavyo." 

Kwa vile Munia alihitaji suluhisho kwa tatizo lake, aliwaacha wanyama akarudi nyumbani.

Nyumba yake ilikuwa na kimya kingi na ilikuwa tupu. Babu na bibi walilalamika kwamba hawakupata maziwa kutoka kwa mbuzi. 

Mjombake alisema, "Tumekuwa maskini sana, kila mtu anatucheka."

Munia hakuweza tena kuvumilia malalamishi yao. Pia, aliwakosa wanyama wake. 

Alirudi kwa mtu yule mwenye busara ili kumwuliza mawaidha. "Maisha yangu yamekuwa fotauti bila wanyama wangu. Jamaa zangu wanalalamika kila wakati."

Mtu yule alimwambia, "Nitakusaidia, lakini, ni lazima ufanye nikuambiavyo. Nenda nyumbani kisha uwatoe nje bibi na babu kutoka kwenye nyumba." 

Munia alimjibu, "Nitawezaje kufanya hivyo? Wao ni wavyele wangu na wananitegemea."

Mwishowe, Munia alienda nyumbani akafanya alivyoambiwa. Hakuweza kupata amani akilini mwake. 

Babu na bibi hawakuwa na mahali pa kuenda. Walirandaranda wakiangukia miti na kuhisi baridi usiku.

Shangaziye mgonjwa alilia akisema, "Tafadhali usinitupe nje." 

Mjombake mzembe alisema, "Sitaondoka kitandani usije ukanitupa nje pia."

Munia hakuweza kustahimili mambo haya hata kidogo. Alirudi kwa mtu mwenye busara akiwa amechanganyikiwa na mwenye hasira. 

Alimlilia akisema, "Mambo haya ni magumu sana kwa mtu mmoja. Nipe suluhisho bora zaidi."

Mtu mwenye busara alisema, "Hapa, wachukue wanyama wako na uwarudishe bibi na babu kwenye nyumba pia." 

Munia alifanya alivyoambiwa. Shangaziye alisema, "Nitasafisha nyumba kwa bidii." 

Mjombake aliacha kuwa mzembe akamsaidia Munia na kazi za nyumbani. Wakaishi kwa furaha tena.

------------------------------------------------------------



Odongo na Apiyo waliishi na baba yao mjini. 

Kila wakati waliitazamia likizo si tu kwa shule kufungwa, bali pia kumtembelea bibi yao. 

Bibi aliishi katika kijiji cha wavuvi karibu na ziwa kubwa.

Odongo na Apiyo walifurahi kwani ulikuwa wakati wa kumtembelea bibi kwa mara nyingine. 

Usiku huo, walifunganya mifuko yao tayari kwa safari ndefu ya kwenda kijijini. 

Usiku kucha waliongea juu ya likizo na kumtembelea bibi kijijini.

Asubuhi iliyofuata, waliondoka mapema kwenye gari la baba yao kuelekea kijijini. 

Safarini, waliiona milima, wanyama wa pori na mashamba ya majani chai. 

Walihesabu magari yaliyopita na kuimba nyimbo walizofunzwa shuleni.

Baada ya muda, walilala kwa sababu ya uchovu.

Walipofika kijijini, baba aliwaamsha. 

Walimkuta bibi akipumzika kwenye mkeka chini ya mti. 

Bibi alikuwa mwanamke mrembo na mwenye nguvu.

Bibi aliwakaribisha kwa kucheza na kuimba kwa furaha. 

Wajukuu wake walifurahi na kumpa zawadi walizomletea kutoka mjini. 

"Fungua zawadi yangu kwanza," Odongo alimsihi. "La, atafungua yangu kwanza!" Apiyo akasema.

Bibi aliwabariki wajukuu wake baada ya kuzifungua zawadi. 

Alipendezwa na zawadi walizompelekea.

Baada ya kupmzika, Odongo na Apiyo walitoka nje. 

Walifurahia kucheza na vipepeo na ndege. 

Hawakuweza kuwaona vipepeo na ndege wengi mjini.

Walipanda mitini na kuchezea ziwani.

Giza lilipoanza kuingia, walirejea nyumbani. 

Bibi aliwaandalia chakula, lakini walilala kabla ya kumaliza kukila!

Siku iliyofuata, baba yao aliondoka na kurudi mjini. 

Aliwaacha Odongo na Apiyo nyumbani kwa bibi.

Odongo na Apiyo walimsaidia bibi yao kufanya kazi za nyumbani. 

Walitafuta kuni na kuchota maji. 

Wakakusanya mayai na kuchuna mboga kutoka kwenye bustani.

Bibi aliwafunza wajukuu wake jinsi ya kupika ugali mwororo walioula kwa kitoweo cha nyama. 

Pia, aliwaonyesha namna ya kupika wali wa nazi walioula kwa mchuzi wa samaki.

Siku moja subuhi, Odongo aliwapeleka ng'ombe wa bibiye malishoni. 

Kwa bahati mbaya, waliingia shambani mwa jirani. 
Jirani alitishia kuwafungia ng'ombe kwake kwa kuila mimea yake. 

Baada ya siku hiyo, Odongo alikuwa mwangalifu zaidi.

Siku ya soko, Odongo na Apiyo walienda pamoja na bibi. Bibi alikuwa na kibanda cha kuuzia mboga, sukari na sabuni. 

Apiyo aliwaelezea wateja bei za bidhaa. Odongo naye aliwapakia wateja bidhaa walizonunua.

Kabla ya kurejea nyumbani walimsaidia bibi kuhesabu pesa alizopata siku hiyo. 

Baadaye, walikunywa chai pamoja.

Likizo ilipokaribia kuisha, watoto walilazimika kurudi mjini. 

Bibi alimpatia Odongo kofia naye Apiyo akampatia sweta kama zawadi. 

Aliwatayarishia chakula watakachokula safarini.

Baba yao alipofika, hawakutaka kuondoka. Walimsihi Bibi kwenda nao mjini. 

Lakini, alitabasamu na kusema, "Nina kazi nyingi shambani, siwezi kwenda mjini. Nitawasubiri mje hapa kijijini tena."

Odongo na Apiyo walimkumbatia na kumuaga.

Odongo na Apiyo waliwaambia marafiki zao kuhusu maisha kijijini. 

Baadhi yao waliamini kuwa maisha ya mjini ni bora. Bali wengine waliamini maisha ya kijijini ni bora zaidi. 

Lakini wote walikubali kwamba Odongo na Apiyo walipendwa na bibi yao.

------------------------------------------------------------



Khayanga aliishi na wazazi wake kwa furaha. 

Alipokuwa na umri wa miaka kumi, walifariki.

Khayanga alitunzwa na Rosa, mmoja wa jamaa zake. 

Rosa alikuwa mkarimu lakini alikuwa mkongwe.

Khayanga aliyatembelea makaburi ya wazazi wake. 

Aliwaeleza matatizo yake.

Siku moja alipokuwa makaburini, alipokea zawadi ya kibuyu. 

Aliamini kuwa kilitoka kwa wazazi wake.

Khayanga aliusikia wimbo mtamu wa kuliwaza kutoka katika kibuyu. 

Uliimbwa hivi:

Khayanga, ee, 
Khayanga! 
Mtoto wetu, mpendwa! 
Kibebe kibuyu hiki, mpendwa! 
Kikuliwaze, mpendwa! 

Khayanga alifahamu sauti hiyo kuwa ya mamake.

Khayanga alikibeba kibuyu chake wakati wote. 

Aliamini kwamba wazazi wake walimlinda.

Siku moja, kibuyu hicho kilivunjika. 

Khayanga alivunjika moyo vilevile.

Alivishika vigae hivyo mikononi akaimba: 

Babangu, mamangu! 
Kibuyu changu kimevunjika! 
Nifanyeje? 
Nipe ishara nyingine! 
Nijue mko nami!

Sauti ilisema: 

Khayanga mtoto wetu! 
Viokote vigae hivyo! 
Vitumie kuchota maji! 
Ioshe miguu yako! 
Yafumbe macho! 

Khayanga alitii.

Khayanga alikibeba kibuyu chake kila mahali. Waliomwona, walijiuliza, "Hiki ni kibuyu cha aina gani?" 

Kibuyu hicho kilimsaidia kupata mahitaji yake.

Khayanga aliamini kuwa wazazi wake walikuwa naye wakati wote. 

Hakuna lolote baya lingeweza kutendeka kwake.

------------------------------------------------------------



Sungura alikuwa rafiki mkubwa wa Kima. 

Walishiriki mambo mengi pamoja.

Siku moja Sungura alisema, "Hebu twende matembezi tukatafute chakula." 

Kima alikubali bila kujua yaliyomsubiri!

Walienda katika shamba la wenyewe na kuanza kula mahindi. 

Sungura alikuwa na njama ya kumtendea Kima uovu.

Sungura alimwonea Kima wivu kwa kuwa na mkia mrefu. 

Alikuwa amewaeleza wenye shamba, "Kima atakuja kula mahindi yenu leo. Mfunze adabu!"

Walipokuwa wakila mahindi, Sungura alijificha na kupiga kelele akisema, "Mwizi! Mwizi! Mahindi yenu yanaliwa yote!" 

Kisha akatoroka na kwenda zake. Kima hakujua kilichokuwa kikiendelea.

Ghafla, wenyewe walifika na kumpata Kima akijaribu kutoroka. 

Hata hivyo, mkia wake mrefu ulimzuia kwenda haraka.

Walimfuata wakipiga kelele, "Simama! Simama! Umetumalizia mahindi yetu."

Walimshika na kuanza kumpiga. 

Kima alijaribu kuponyoka na kutoroka tena lakini hakuweza.

Kima hakuweza kuvumilia kichapo. Aliwasihi waache kumchapa ili awaeleze mambo yalivyokuwa. 

"Nilikuwa na rafiki yangu Sungura. Ni yeye aliyenialika," alilia.

Hata hivyo, wenyewe hawakumsikiza. Mmoja alitoa panga na kusema, "Leo ni leo! Utashika adabu!" 

Aliukata mkia wake. Sungura alishuhudia kila kitu kutoka alikojificha.

Wenye shamba waliondoka na kwenda zao. Kima alipokimbilia usalama wake, Sungura aliuchukua mkia wa Kima na kwenda kuupika. 

"Nitamwalika Kima kwa chakula cha mchana," alitabasamu.

Baada ya mlo, Kima alisema, "Asante rafiki yangu kwa kuandaa chakula kitamu." 

Sungura alimwuliza Kima ikiwa alijua alichokuwa amekula. Bila kujua, Kima alijibu, "La, sijui!"

Sungura alisema, "Hicho kitoweo kitamu ulichokula, kilikuwa mkia wako." 

Baada ya kusema hivyo, alitoroka. Na kutoka siku hiyo walikuwa maadui!

------------------------------------------------------------



Hii ni hadithi ya Ndege-Asali na mvulana mmoja mlafi aliyeitwa Jeuri. Siku moja Jeuri alipokuwa akiwinda, alisikia mwito wa Ndege-Asali amabye huwaongoza watu palipo na asali. 

Jeuri alianza kudondokwa na mate alipofikiria juu ya asali. Alisikiliza na kutazama vizuri hadi akamwona Ndege-Asali aliyekuwa ametua kwenye matawi. 

"Chitik-chitik-chitik," Ndege-Asali aliruka na kutua kwenye mti uliokuwa karibu. "Chitik-chitik-chitik," aliita, huku akinyamaza na kuhakikisha kwamba Jeuri alikuwa amemfuata.

Baada ya nusu saa, waliufikia mti wa mtini. 

Ndege-Asali aliruka kama mwenda wazimu kutoka tawi moja hadi jingine. 

Jeuri alisimama akamtazama kwa muda mrefu.

Baadaye, Ndege-Asali alitulia kwenye tawi moja, akageuza kichwa chake na kumwangalia Jeuri. 

Jeuri aliamini kuwa Ndege-Asali alikuwa akisema,  "Asali iko hapa! Njoo sasa!" 

Jeuri hakuweza kuwaona nyuki wowote kutoka chini ya mti kwa vile alimwamini Ndege-Asali.

Jeuri aliuweka mkuki wake chini ya mti. Akakusanya vijiti vilivyokauka kisha akakoka moto mdogo. 

Moto ulipowaka vizuri, Jeuri alikitia kijiti kirefu kilichoaminika kutoa moshi mwingi. 

Alianza kukwea mti akiwa amekishika kwa meno.

Baadaye, Jeuri alisikia sauti ya nyuki. Walikuwa wakiingia na kutoka mzingani. Alipoufikia mzinga, alikisukuma ndani kile kijiti kilichokuwa na moto. 

Nyuki walitoka ndani kwa hasira wakihisi uchungu. Waliruka na kwenda kwa sababu hawakupenda moshi. 

Hata hivyo, walifanya hivyo tu baada ya kumuuma Jeuri!

Nyuki walipokuwa nje, Jeuri aliingiza mkono wake ndani ya mzinga. 

Alitoa kipande kikubwa cha asali iliyokuwa ikidondoka. Aliiweka kwa utaratibu ndani ya mkoba aliokuwa nao na kuanza kushuka.

Ndege-Asali alishuhudia kila kitendo alichofanya Jeuri. Alikuwa akisubiri kubakishiwa kiasi kidogo cha asali kama shukurani kwa kumwongoza Jeuri kwenye asali. 

Aliruka kutoka tawi hadi tawi huku akikaribia chini. 

Mwishowe Jeuri alifika chini. Ndege-Asali alitua kwenye jiwe karibu na Jeuri akisubiri zawadi yake.

Lakini Jeuri aliuzima moto, akachukua mkuki wake na kuanza safari bila kumjali Ndege-Asali. 

Ndege-Asali aliita kwa hasira, "USH-ndi! USH-ndi!" Jeuri alisimama, akamkodolea macho kisha akacheka kwa sauti. "Rafiki yangu, unataka asali kidogo? Ha! Mimi ndiye nilifanya kazi yote pamoja na kuumwa na nyuki. Kwa nini nikugawie asali hii tamu?"

Jeuri aliondoka na kwenda zake. 

Ndege-Asali alikasirika sana! Hivi sivyo ndivyo alistahili kutendewa! 

Lakini, atalipiza kisasi.

Siku chache baadaye, Jeuri alisikia tena mwito wa Ndege-Asali uliohusu asali. Aliikumbuka asali tamu, na kwa mara nyingine, alimfuata kwa hamu. 

Baada ya kumwongoza Jeuri kwenye msitu, Ndege-Asali alipumzika chini ya mti wa mwavuli. "Aa, bila shaka mzinga umo ndani ya mti huu," Jeuri aliwaza. 

Kwa haraka, aliwasha moto wake na kuanza kukwea mti akiwa amebeba kuni iliyotoa moshi. 

Ndege-Asali alimtazama tu.



Jeuri alipopanda, alishangaa kwa nini hakusikia sauti ya nyuki. "Pengine mzinga umefichika ndani ya mti zaidi," alifikiria. 

Alipanda tena juu ya tawi jingine. Lakini badala ya mzinga, alijikuta akiwa ana kwa ana na Chui!

Chui alikuwa na hasira sana kwa sababu usingizi wake ulikuwa umekatizwa. 

Aliiyafanya macho yake yakawa madogo, akaufungua mdomo wake na kuyaonyesha meno yake makubwa makali.

Kabla ya Chui kumvamia, Jeuri alishuka haraka chini. Katika haraka hiyo, aliteleza na kuanguka kwa kishindo akaumia mguu wake. 

Alirukaruka akienda kwa haraka alivyoweza. Kwa bahati nzuri, Chui alikuwa bado akihisi usingizi, kwa hivyo hakumfukuza. 

Ndege-Asali alikuwa amelipiza kisasi na Jeuri alikuwa amejifunza funzo lake.

Kwa hivyo, watoto wa Jeuri na watoto wa watoto wao wanamheshimu sana Ndege-Asali wanapoisikia hadithi yake ya kuwaongoza watu kwenye asali. 

Kila wanapotoa asali, wao huhakikisha kwamba wanamzawadi kwa kiasi kikubwa cha asali!

------------------------------------------------------------



Hebu nikueleze kuhusu mtende.

Mtende ni mmea wa kudumu.

Unaweza kusitawi wakati mimea yote mingine imekauka.

Kivuli cha mtende kina upepo mzuri.

Tunakula matunda ya mtende.

Tunatumia majani ya mtende kuezeka nyumba zetu.

Tunatengeneza fagio na kusuka mikeka kwa kutumia majani ya mtende.

Tunatumia nafaka zake kupika.

Sasa umefahamu kwa nini mtende ni muhimu sana?

Maswali:  A) Tunatumia ___ya mtende kuezeka nyumba zetu. B) Tunasuka _____ kwa kutumia majani ya mtende. C) Tunatumia __________ za mtende kupika. 3. Taja jina la aina nyingine ya mti inayosaidia jamii yenu.

------------------------------------------------------------



Ninaimba.

Ninapunga mkono.

Ninashangilia.

Ninajinyoosha.

Ninaongea.

Ninacheka.

Ninashangaa.

Je,  unafanya nini?

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na mzee mmoja aliyeitwa Hagos. Aliishi na wanawe watatu.

Hagos alitaka wanawe wawe na mali baada ya kifo chake. Alitayarisha masanduku matatu.

Hagos alikwenda kwa Haile, jirani yake, na kumwambia, "Ninataka wanangu wawe na mali.
Nimeyatayarisha masanduku matatu. Ningependa uwapatie masanduku hayo baada ya kifo changu."

Baada ya Hagos kufariki, Haile aliwaita pamoja wale ndugu watatu akawaeleza, "Kabla baba yenu kufariki, alinipatia haya masanduku matatu. Kila sanduku lina jina. Naomba kila mmoja alichukue sanduku lililo na jina lake."

Ndugu wale walichukua kila mmoja sanduku lake kisha wakayafungua. 

Sanduku la kwanza lilikuwa na dhahabu. La pili, lilikuwa na udongo. Nalo la tatu lilikuwa na samadi.

Aliyepata dhahabu alifurahi sana. Waliopata udongo na samadi, hawakufurahi. Walianza kugombana na yule aliyepata dhahabu.

Haile aliwaambia, "Ninyi ni ndugu na hamstahili kugombana. Hebu niwapeleke kwa mzee mwenye busara awashauri."

Haile aliwapeleka ndugu wale watatu kwa mzee mwenye busara. "Habari za asubuhi. Tumekuja kwako kutafuta ushauri kuhusu urithi," Haile alimweleza yule mzee.

Haile alimwambia yule mzee mwenye busara kuhusu yale masanduku matatu ambayo Hagos aliwaachia wanawe. 

"Sasa hawa wawili, wanagombana na yule aliyepata sanduku lililokuwa na dhahabu," Haile alieleza.

Yule mzee mwenye busara alisizitiza, "Baba yenu alikuwa na sababu ya kuwapatia sanduku ambalo kila mmoja wenu alipata."

Aliendelea kuwaeleza, "Wewe ulipata dhahabu kwa sababu babako alitaka uwe mfanya biashara. Nawe ulipata udongo kwa sababu babako alitaka uwe mkulima."

"Wewe ulipata samadi kwa sababu babako alitaka uwe mchungaji. Baba yenu alitaka mfanye kazi yenu kulingana na vipaji vyenu," mzee mwenye busara alikamilisha maelezo yake.

Baada ya kusikiliza ushauri wa yule mzee mwenye busara, wale ndugu watatu walikubaliana naye. Kila mmoja wao aliifanya kazi yake tofauti na wakaishi kwa furaha.

------------------------------------------------------------



Niliwasili katika kituo chetu cha basi. 

Kilikuwa kimejaa watu.

Kondakta wa basi aliita, "Kwenda jijini! Tunaondoka sasa!"

Watu walifanya haraka kuingia ndani ya basi.

Wanawake waliokuwa na watoto waliketi.  

Safari itakuwa ndefu.

Niliketi kwenye dirisha karibu na mwanamume na mwanamke.

Niliwaza, "Ninaenda jijini! Nitakosa familia yangu."

Wachuuzi wengi waliingia kuuza bidhaa zao.

Baadhi ya abiria walinunua bidhaa. 

Sikuwa na pesa ya kununua chochote.

Ghafla, dereva alipiga honi. 

Tulikuwa tayari kuondoka.

Wachuuzi walisukumana kutoka nje.

"Tutafika saa ngapi?" Nilijiuliza.

Ndani ya basi mlikuwa na joto sana. 

Niliyafumba macho yangu.

Niliwafikiri mama na ndugu yangu wakiwa nyumbani.

Baadaye, nilipatwa na usingizi.

Baada ya muda mrefu, niliamka. 

Karibu kila abiria alikuwa ameshuka.

Nilianza kutafuta mahali mjomba aliishi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, wanyama hawakuwa na miguu.

Maguru alikuwa amewapatia miguu watu pekee.

Maguru aliamua kumpatia kila mnyama miguu.

Wanyama walitaka miguu ili watembee na kukimbia.

Ilikuwa vigumu kwao kutambaa.

Siku ilifika. Wanyama tofauti walitambaa kwenda kwa Maguru.

Maguru aliwapatia wanyama na ndege miguu.

Baadhi ya wanyama walicheza. Wengine walianguka chini.

Walisema, “Hatutatambaa tena.”

Jongoo alikuwa wa mwisho kwenye mstari.

Maguru alimpatia miguu yote iliyokuwa imabaki.

Jongoo alisema kwa furaha, “Nitatembea haraka kuwaliko wengine.”

Baadaye, Nyoka alifika. Alimsihi Maguru, “Tafadhali, nipe miguu.”

Nyoka alimwambia Maguru, “Nililala kupita kiasi.”

Maguru hakupata miguu yoyote ya kumpatia Nyoka.

Tangu siku hiyo, Nyoka anasubiri kupata miguu.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na msichana aliyeitwa Linda. Aliishi na dada zake wawili, kaka na mama.

Alikuwa msichana mwenye furaha na mchangamfu.

Linda alikuwa na rafiki yake wa karibu aliyeitwa Stacy.

Linda na Stacy waliaminiana na kufichuliana siri wakati wote.

Kila Jumanne, Linda na Stacy walipenda kwenda kuona sinema.

Walivutiwa na bisi ya bure waliyoandaliwa huko.

Baada ya kutazama sinema, walikuwa wakienda uwanjani kusikiliza muziki.

Pia, walikuwa wakifurahia kula aiskrimu.

Kwa hivyo, Jumanne ilikuwa siku ya furaha kwa Linda.

Kwanza, yeye na Stacy walitazama sinema na kuandaliwa bisi ya bure.

Kisha yeye na Stacy walisikiliza muziki na kula aiskrimu uwanjani.

Lakini, lililo na mwanzo, vilevile lina mwisho!

Jifunze kuthamini wakati unapofurahi...

...na watu unaoshiriki nao furaha hiyo.

------------------------------------------------------------



Magezi na Kasiira waliishi pamoja.

 Walishiriki chakula pamoja.

Magezi alisema, "Tulime pamoja jinsi tunavyokula pamoja."

Magezi alimwambia Kasiira, "Wewe lima mimi nitapanda."

Magezi pia alimwambia Kasiira, "Wewe panda mimi nitapalilia."

Mtama ulikomaa.

Kasiira alimwambia Magezi avune.

Magezi alijibu, "Wewe vuna. Mimi nitahifadhi."

Magezi alikuwa mvivu.  

Kasiira alimpatia kifungu kimoja tu cha mtama.

Magezi alikutana na Kuku.

Kuku alikula ule mtama.

Alimpatia Magezi yai.

Magezi aliwakuta watoto wekicheza. 

Walilivunja lile yai.

Watoto walimpatia Magezi embe.

Magezi alimkuta Kasuku. 

Kasuku alilikula embe kisha akampatia unyoya.

Ziwa liliuchukua unyoya. 

Likampatia Magezi maji.

Magezi aliyatumia maji kuzima moto wa wachoma makaa.

Wachoma makaa walimpatia Magezi shoka.

Magezi aliwakuta wachinjaji.

Waliivunja shoka.

Magezi alipatiwa kichwa na mkia wa fahali.  

Ona alichofanya Magezi!

Alipiga mayowe, "Fahali wa mfalme amekwama matopeni!"

Ulikuwa ujanja tu.

Watu walikuja kumsaidia. 

Magezi aliwaambia, "Vuteni mkia na kichwa."

Magezi aliwaambia watu, "Nipeni ng'ombe wenu nimpelekee mfalme."

------------------------------------------------------------



Jina langu ni Kobole. 

Ninaishi katika kijiji kiitwacho Mbalisana.

Siku moja nilikuwa nikichuma matunda. 

Nilishuhudia jambo la kushangaza.

Niliona mistari ya rangi tofauti angani.

Niliyaangusha matunda niliyokuwa nimechuma. 

Kisha, nikakimbia kuwaambia watu nyumbani.

Niliwapata wakiwa nje. 

Wote walitazama juu kwa mshangao.

Nilisema kwa furaha, "Hii ni shuka maridadi." 

Neno alinipinga akisema, "La! Hizi ni rangi tofauti zinamwagika kutoka angani."

Baadhi ya wanakijiji walikubaliana nami na wengine waliamini aliyosema Neno. 

Tulianza kubishana.

Wakati huo, mgeni mmoja alitokea na kusema,  "Mmekosea nyote."

Tulipiga mayowe, "Ikiwa tumekosea, wewe tueleze ukweli."

Yule mgeni alisema, "Mnachoshuhudia ni upinde. Kwani ninyi hamjawahi kuuona upinde?"

Kwa mshangao zaidi, tulimjibu, "La! U-p-i-n-d-e ni nini?"

Neno alimwuliza, "Je, huu upinde ni wetu? Tunaweza kuuweka hapa?" 

Hatukupata majibu kwa maswali yetu. Mgeni huyo alikuwa tayari ameenda zake.

------------------------------------------------------------



Sisi ni waandishi chipukizi, wasanii, na wanaharakati kutoka Maktaba ya Jamii Cheche, Monduli, Tanzania. 

Tuliandaa kitabu hiki kuelimisha jamii juu ya changamoto za kijinsia na kutoa mawazo yetu kuhusu namna ya kuzisuluhisha.

Baadhi ya wazazi wanawabagua watoto wa kike. Watoto wa kike wanafanyishwa kazi ngumu wakati watoto wa kiume wanasoma au kucheza.

Watoto wa kike wanaachishwa shule ili kufanyishwa kazi nzito kuliko umri wao.

Tunahitaji kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa watoto wa kike kwenda shuleni.

Kama mtoto anateswa nyumbani au kunyimwa haki yake ya elimu, majirani au ndugu wanaweza kumsaidia kwa kwenda naye polisi kuripoti.

Baadhi ya wasichana wanalazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo na kuacha shule.

Changamoto hii inatokana na umaskini wa wazazi unaowafanya watake kupokea mahari. 

Pia mtoto akifiwa na wazazi anaweza kunyimwa haki ya elimu na kuolewa mapema.

Kuolewa katika umri mdogo kunachangia kwenye ukosefu wa elimu kwa watoto wa kike na kuendelea kuongeza umaskini.

Kunasababisha watoto wa kike kushindwa kujitambua, kutokutambua haki zao, na kutokujua jinsi ya kujisaidia katika jamii.

Hatuna budi kuitisha mikutano ya kuwaelimisha watu kuhusu umuhimu wa watoto wa kike kwenda shuleni na kutokuozeshwa mapema.

Tunapoona familia ni maskini, tunatakiwa kuichangia ili wampeleke mtoto shule. Hiyo inaweza kukatisha ndoa kabla ya umri wa mtoto.

Pia tunapoona mtoto hana wazazi tunatakiwa tuombe kibali cha kumlea au kumpeleka sehemu ambapo wanalelea watoto.

Hiyo inaweza kukatisha kuolewa kabla ya wakati.

Watoto wa kiume wanakutana na changamoto ya kushawishiwa kuvuta bangi, kunywa pombe, kuiba, na kujiunga na makundi mabaya.

Mwishoni, unakuta watoto hao wameacha shule kutokana na ushawishi mitaani. Wakati mwingine, hata wasichana hukumbwa na changamoto ya kutumia bangi na pombe.

Changamoto hii inasababishwa na umaskini na kukata tamaa.

Pia inatokana na changamoto za nyumbani, kama kukosa chakula na wazazi kutokuwalea watoto katika misingi inayofaa.

Ada kubwa ya shule pia inachangia.

Tunaweza kuelimisha jamii kuhusu madhara ya uvutaji bangi kwa kupitia mitandao ya kijamii, mabango, na magazeti.

Tunahitaji kuwashawishi watu kutokujiunga na makundi yasiyofaa na kuvumilia hali ngumu waliyo nayo wazazi.

Serikali inahitaji kupunguza ada za shule na kurahihisha upatikanaji wa ajira, ili kusaidia kupunguza changamoto ya bangi. 

Pia tuwasaidie watu wasikate tamaa mapema. Wazazi wajitahidi kuwalea watoto vizuri katika misingi mizuri ya maisha.

Wanawake na wasichana wanabakwa katika jamii yetu.

Polisi wanahitaji kuongeza bidii kukamata na kuwafunga wabakaji.

Mtu akibakwa anatakiwa kusema ili mhusika ashitakiwe na kukamatwa na polisi.

Ukeketaji ni changamoto katika jamii yetu.

Mtu akikeketwa, kuna uwezekano wa damu nyingi kumtoka na kusababisha kifo.

Tunahitaji kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukeketaji, kwa mfano kwa kupitia makongamano ya kidini.

Watoto hufanyishwa kazi ili watafute pesa ili wawatunze wazazi. Wanafanya kazi ngumu katika umri mdogo.

Hii inatokana na umasikini na changamoto za kifamilia. Mtoto mmoja hufanyishwa kazi kuliko mwingine kutokana na upendeleo wa mzazi.

Tuongee na wazazi kuwashauri wasiwafanyishe watoto kazi ngumu na wawapeleke watoto shule ili kupata elimu.

Watoto wengi wanaacha shule kwa sababu mbalimbali. Watoto wa kike wanaolewa mapema au kupewa kazi nyingi nyumbani mpaka wanaacha shule.

Watoto wa kiume wanakutana na vishawishi mtaani kama vile kuvuta bangi na kunywa pombe.

Kwa sababu ya umaskini, wazazi wanakosa ada ya shule au kushindwa kumnunulia mtoto sare za shule. 

Mtoto anaingia mtaani na kufanya kazi ili kujipatia fedha za kuitunza familia.

Walimu hawafundishi vizuri na wanawachapa watoto kwa hasira.

Tutumie redio kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa shule. Redio inaweza kutumika pia kuelimisha jamii kuhusu madhara ya uvutaji bangi.

Pia, tuelimishe jamii kuhusu umuhimu wa watoto wa kike kutokuozeshwa mapema.

Tuwaelimishe walimu kufundisha vizuri na kutokuwachapa watoto kwa hasira.

Tuwashauri afisa elimu shule zote ziwe na mahitaji yote muhimu kama maji na mazingira mazuri.

Tushauri serikali kupunguza ada za shule na tuwasaidie watu ambao hawana mahitaji ya shule.

Mtoto anaathirika na mawazo kutokana na mateso ya nyumbani.

Ugomvi baina ya wazazi humharibu mtoto kisaikolojia na mtoto anakuwa na mawazo na kushindwa kusoma vizuri darasani.

Mtoto anawaza atakula nini, atalala wapi, atapata wapi mboga za kupika, labda anateswa nyumbani na mama wa kambo.

Akiwa na msongamano wa mawazo, au hofu, hakuna kitu atakachoweza kufanya shuleni. Hii inatokana na ukosefu wa haki zake, kwa mfano chakula, mavazi, na malazi.

Tuwaelimishe wazazi wasigombane mbele ya watoto. Ugomvi wa wazazi husababisha mtoto kuwa na msongamano wa mawazo, kushindwa kusoma vizuri, na hata kuacha shule kabisa. 

Tuwashirikishe walimu na afisa elimu ili wasimamie haki ya elimu.

Mzazi anampiga mtoto bila makosa. Mtoto mmoja anafanyishwa kazi kuliko mwingine kutokana na upendeleo wa mzazi. Msichana anafanya kazi nzito wakati mvulana anaangaliza TV.

Mama anamnyima mtoto asiende shuleni afanye kazi za nyumbani.

Tuelimishe jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na tuhakikishe watoto wote wameenda shule ili wapate elimu bora, bila kuwabagua.

------------------------------------------------------------



Hapo kale, kulikuwa na Paka mwerevu na Mbwa mjinga. Paka mwerevu aliishi vizuri katika nyumba ya kifahari. 

Mbwa mjinga alihisi njaa mtaani.

"Inawezekanaje familia tajiri kukuruhusu kuishi nyumbani kwao?" Mbwa mjinga alimwuliza  yule Paka mwerevu kwa hasira.

Paka mwerevu alijibu, "Ninaishi na watu kwa sababu mimi ni nadhifu. Ninajua kuzika kinyesi changu. Nikihitaji chakula, mimi husema, miau."

"Je, mimi pia nikifanya hivyo wataniruhusu niishi
nyumbani kwao?" Mbwa akamwuliza. 

Paka akajibu, "Ndiyo, fanya nilivyokueleza na watakuruhusu. Watakupatia chakula vilevile."

Kabla ya mazungumzo hayo, Mbwa mjinga alikuwa akitaka kumla Paka mwerevu. Baada ya mazungumzao, alisema, "Leo, sitakuumiza." 

Paka aliwaza, "Lo! Nimeponea chupuchupu. Sitaki kukutana naye tena."

Mbwa mjinga alifuata ushauri aliopewa na Paka mwerevu.

Alikwenda nyumbani kwa tajiri akabweka kwa sauti pale mlangoni.

Mwenye nyumba alitoka akampiga kwa fimbo. "Huyu Paka amenidanganya. Nikimpata, nitamla." Mbwa mjinga alinung'unika.

Baadaye, Paka mwerevu alipokuwa akicheza nje ya nyumba, Mbwa mjinga alimwambia, "Wakati ule ulinidanganya. Nilibweke mlangoni ulivyonishauri na mwenye nyumba akanipiga. Sasa nitakula."

Paka mwerevu akamjibu, "Mbwa, nisikize. Ni sawa utanila. Lakini, kwanza niache nicheze. Mimi humuacha panya acheze kwanza ndivyo nimle."

Mbwa mjinga alimwuliza, "Panya huchezaje?" Paka akamjibu, "Mimi humwuliza ahesabu hadi tatu. Kisha humkamata anapokuwa anahesabu."

Basi Mbwa mjinga akamwacha Paka mwerevu huru. Kisha akamwambia ahesabu hadi tatu. Paka mwerevu alitoroka akapanda juu ya mti. 

Mbwa akamwita Paka mwerevu, "Shuka, rudi hapa uhesabu hadi tatu."

Paka mwerevu akamjibu, "Sikiza Mbwa, hutawahi kunishika tena. Mimi si mjinga. Unaweza kuhesabu hadi mia moja, elfu au milioni, lakini hutawahi kunipata tena!"

------------------------------------------------------------



Ninaitwa Molly. Mimi ni msichana kama wasichana wangine, isipokuwa, nina mamba mwilini mwangu. Wewe huwezi kumwona, lakini ninajua yupo. 

Jina lake ni Ukosefu-Kinga-Mwilini. Anajificha ndani ya mwili wangu na hawezi kuwaumiza marafiki zangu.

Mamba huyu hawezi kuondoka mwilini mwangu na kuingia mwilini mwako. 

Hata ukikaa karibu nami au ukiushika mkono wangu.

Hawezi kuuacha mwili wangu na kuruka ndani ya wako ukila nami chakula cha mchana.

Au, hata ukilala karibu nami sakafuni.

Mamba huyu, Ukosefu-Kinga-Mwilini, amekuwa nami tangu nizaliwe. 

Anapenda kuwala majeshi wote wa mwilini ambao wangepigana na viini na kunizuia kuwa mgonjwa. 

Anapowala majeshi wangu kwa wingi, ninaugua sana. Siwezi kwenda shule wala kucheza na marafiki zangu.

Ninalazimika kumeza dawa zangu kila siku wakati unaopendekezwa. Nisipofanya hivyo, mamba huyu anaamka kwa hasira na kuwala majeshi wangu tena. 

Mimi sitaki afanye hivyo. Ndiyo sababu ninamkumbusha bibi kunipa dawa zangu wakati unaofaa.

Nikila mboga na matunda, majeshi walio mwilini mwangu wanapata nguvu. Mamba huyu hawezi kuwashika. 

Anapolala kwa muda, mimi huwa na nguvu. Hufurahi na kucheza na marafiki zangu tena.

Bibi alinipeleka kituo cha afya muda mfupi uliopita. Alipewa dawa na daktari ya kumfanya mamba huyu alale asiweze kuwala majeshi wangu. 

Mimi huweza kukimbia, kupanda juu na kucheza kama watoto wengine.

Ninampenda bibi sana. Ni mzuri na mwenye huruma. Ananilisha chakula kizuri na kuhakikisha ninapata vitamini zaidi ili majeshi wangu wawe na nguvu. 

Nikiugua, ananipeleka kituo cha afya mara moja ili nipate matibabu na kupata nafuu. 

Ninafurahi anaponisomea hadithi kabla mimi kwenda kulala. Kabla sijalala, mimi huwaza juu ya kusomea katika shule kubwa.

Nitaendelea kuzitumia dawa za kumfanya mamba wangu alale. Ningependa kumsaidia bibi na kumsomea hadithi atakapozeeka na kutoweza kuona vizuri. 

Nikiwa mtu mzima, ningependa kusoma na kuchangia kutafuta dawa zitakazowafanya mamba wote walio katika miili ya watu, walale milele daima.

Nitajifunza kuishi na mamba wangu na kufanya alale zaidi nitakavyoweza. 

Nitakuwa na marafiki wengi na kufurahi kila siku iwezekanavyo.

Bibi, shangazi, wajomba, na marafiki, wananipenda,  ingawa nina mamba mwilini mwangu anayeitwa Ukosefu-Kinga-Mwilini.

------------------------------------------------------------



Kwa muda mrefu Mlima Olowango ulisimama ukitabasamu katikati ya sehemu Tambarare ya Kwere. 

Vibonyeo viwili vilikuwa pembeni mwa Mlima Olowango. Kutoka pale, vijito vilivyokaribiana vilitoka na kuunda Mto Temu.

Mambo yalikuwa swari hadi Matata alipokuwa mkuu wa mahali hapo. 

Alilazimisha njia itengenezwe kutoka juu ya mlima hadi chini yake ili aweze kupanda kwa urahisi na kujifiringisha hadi chini. 

Mlima Olowango ulikasirika na uharibifu uliofanywa lakini ulivumilia.

Kila wikendi, watoto wa Matata na marafiki zao wangepanda mlimani kucheza. 

Wangekimbia kila mahali huku wakivunja vijiti na matawi. Walikoka mioto kwa michezo yao ambao baadaye, waliiacha ikiwaka.

Mlima Olowango ulipoteza uvumilivu wake. Tabasamu yake nzuri ilififia. Vibonyeo viliendelea kuwa vidogo jinsi uso wake ulivyokuwa na mikunjo. 

Mwishowe, vijito havikuwa tena. Kingo za Mto Temu zilihuzunika. Paa walihama kwani hapakuwa tena na zile nyasi ndefu za kijani walizochezea ndani wala kulala juu yake. 

Mifugo walikonda na kukondeana. Kila mtu alihisi huzuni wa Mlima Olowango.

Watu wa Kwere wakachukua hatua. Wakamtoa Matata kisha wakamweka Baraka. 

Baraka akaamrisha kila mtu kuuheshimu Mlima Olowango kwa kupanda ua. Wakasherehekea kwa kutolea Olowango zawadi za msonobari, mwerezi na muhuhu. 

Hakuna aliyetembea juu ya mlima tena, na nyasi zilimea na kuwa ndefu tena. Polepole, tabasamu iliyokuwa usoni mwa Mlima Olowango, ilipanuka zaidi na vibonyeo vikarefuka zaidi.

Kutoka kwenye vibonyeo, vijito vilitiririka tena. 

Mto Temu ulifufuliwa. 

Sehemu tambarare ziligeuka kijani zaidi ya hapo awali. 

Paa walitembea tena kwa furaha kutoka upande mmoja hadi mwingine wakila nyasi.

"Maisha marefu, Baraka! Maisha marefu, Baraka!" Watu wa Kwere waliimba. 

"Maisha marefu, Olowango," Baraka na watu wake walisema. "Heri watoto wetu na watoto wa watoto wao wakuheshimu daima."

------------------------------------------------------------



Bi Kizee alikuwa na mjukuu aliyeitwa Noah.

Alimpatia Noah yai.

Noah alikutana na wachuma matunda damu.  
 
Walilivunja yai hilo.

Noah alilia, "Yai lilikuwa la kulipia mahari!"

Wachuma matunda damu walimpatia Noah fimbo.

Noah aliwakuta wajenzi. 

Wakaivunja fimbo ile.

Noah akalia, "Fimbo hiyo ilikuwa ya wachuma matunda damu!"

Wajenzi walimpatia Noah kifurushi cha nyasi.

Noah akamkuta mchungaji wa ng'ombe. 
  

 Ng'ombe akaila nyasi hiyo.

Noah alilia tena, "Ile nyasi ilikuwa ya wajenzi!"

Mchungaji alimpatia Noah ng'ombe.

Noah alipata sherehe ya harusi.
  

Walimchinja yule ng'ombe.

Noah alilia, "Yule ng'ombe alikuwa wa mchungaji!"

Familia ilimpatia Noah bi harusi.

------------------------------------------------------------



Mama Jua alimtembelea dadake Mwezi. 

"Nitarudi hivi karibuni," alisema.

Mama Jua alipoondoka, Milima ilihuzunika.

Upepo uliitikisa Miti. 

Miti ikadondosha majani yake kwa hasira.

Anga lilianza kulalamika. 

Lilibadilika na kuwa rangi ya kijivu.

Mawingu yalihuzunika. 

Yalilia machozi mengi.

Ulimwengu mzima ukaanza kuzama majini.

Mama Jua alimbusu dadake Mwezi. 

Alimuaga akiwa tayari kurejea duniani.

Anga lilifurahia Mama Jua. 

Lilikuwa rangi ya bluu. 

Milima ilitabasamu.

Upepo ulitulia. 

Miti ikanyoosha matawi yake na kutabasamu.

Mawingu yalifurahi tena kumwona Mama Jua. 

Yalienda kucheza.

Miche ilichipuka ardhini na kusema, "Hamjambo!" 

Dunia nzima iling'ara.

Mama Jua aliangaza.

Alitabasamu akasema, "Niliwaahidi kuwa nitarejea."

------------------------------------------------------------



Wakati mmoja kulikuwa na kiangazi na njaa kubwa. Hakuna aliyekuwa na chakula isipokuwa Kunguru. 

Kila asubuhi walikwenda mbali katikati ya mto kwenye mkuyu uliokuwa na matunda matamu. Kisha walirudi wakiwa wamebeba makuyu hayo kuwaletea ndugu zao. 

Alipoyaona matunda hayo, Buibui Anansi, alidondokwa na mate. Je, angewezaje kuyapata matunda hayo?

Baada ya kufikiri kwa muda mrefu, alipata wazo zuri. Alijipaka nta inayonata kwenye sehemu yake ya nyuma. Kisha akachukua kigae cha nyungu akaenda nyumbani kwa Kunguru akasema, "Tafadhali, naomba usadizi! Naomba kaa la moto. Jiko langu limezimika." 

Walipokuwa wakimchukulia kaa la moto kutoka jikoni, Buibui Anansi alikalia kuyu moja kubwa. Tunda hilo lilijinata kwenye makalio yake. Aliwashukuru kunguru akaenda haraka nyumbani kulifurahia tunda hilo.

Lakini, tunda moja halikumtosha. Alirudi huko akafanya alivyofanya mara ya kwanza. Aliporudi mara ya tatu, kunguru walimwuliza. "Kwa nini unarudi hapa kila mara kuomba kaa la moto?"  

Buibui Anansi akajibu, "Kila ninapofika nyumbani, kaa huwa limezimika." Kunguru walimwambia, "Unatudanganya! Unatamani chakula chetu." Buibui Anansi alijitetea, "Si kweli." Akaanza kulia. Wakamhurumia wakasema, "Beba kaa jingine. Asubuhi, tutakuonyesha mkuyu wenye matunda."

Asubuhi iliyofuata kila kunguru alimchangia Anansi manyoya akapata mabawa. Akaruka hadi kwenye mkuyu uliokuwa katikati ya mto. 

Alipoona matunda yale matamu aliyataka yote peke yake. Kila wakati kunguru alipojaribu kuchuma tunda, Buibui Anansi alisema, "Wacha, hilo ni langu! Mimi nililiona kwanza!" 

Halafu alichukua kila tunda na kuliweka mfukoni kwake. Hatimaye, alichukua matunda yote akawaacha kunguru bila chochote.

Kunguru waliyachukua manyoya yao. Buibui Anansi aliachwa peke yake. 

"Siwezi kuishi kwenye mti huu maisha yangu yote," alijiambia. "Ni lazima niruke hewani kama kunguru." 

Akashusha pumzi, kisha akaruka, na mara, chubwi! Akaanguka mtoni baina ya mamba hatari.

"Hapa tuna nyama tamu na nyororo." Mamba mmoja alisema. "Hebu tuanze kula mlo." 

"Tafadhali, msiniue," Buibui Anansi akasema. Kisha akaanza kulia. "Kwani hamjui mimi ni mmoja wenu? Nilipotea wakati wa mababu zenu na hakuna aliyeweza kunipata. Sasa nyinyi ni ndugu zangu!" 

Alilia machozi hadi mamba wakamwonea huruma.

Mamba mmoja mzee hakuamini, "Tutajua kwamba wewe ni mmoja wetu ukinywa supu ya matope kama sisi." Walimpatia kibuyu cha maji machafu. "Bibi yangu alikuwa akitengeza supu kama hii," Buibui Anansi alisema. 

Lakini, alichimba shimo ardhini akitumia mguu wake wa nyuma, kisha akatoboa shimo kwenye kibuyu kwa mguu wake wa mbele. Alijifanya kwamba alikuwa akinywa yale maji na kumbe yalikuwa yakimwagika. "Tamu sana!" alisema huku akirudisha kibuyu kitupu.

"Sasa tumejua bila shaka kwamba wewe ni mmoja wetu," mamba wakamwambia. Walimruhusu Buibui Anansi kulala pamoja nao usiku huo. 

"Kesho asubuhi nitawaambia hadithi kuhusu maisha yangu," Buibui Anansi aliwaambia walipokuwa wakianza kulala.

Siku iliyofuata, Buibui Anansi aliamka asubuhi na mapema akamwamsha mamba mmoja. 

"Ningependa kwenda ili nimlete mke na watoto wangu ili wanisaidie kuhadithia. Je, utanisaidia niende kuwaleta kabla ya wengine kuamka?"

Mamba huyo hakufurahi kwa kuamshwa mapema sana. "Tafadhali nisaidie! Wewe unajua kuogelea haraka kuliko mimi," Buibbui Anansi akamwambia. 

Mamba akakubali kumbeba Buibui Anansi kwenye pua lake hadi ukingo wa mto. Buibui Anansi aliposhuka kutoka kwenye pua la mamba alisema, "Nitarudi hivi punde. Tafadhali ningoje papo hapo!" 

Kisha akatorokea kwenye nyasi kwa kasi.

Tangu siku hiyo, mamba angali anamngoja Buibui Anansi kwenye ukingo wa mto.

Pua na macho yake makubwa yanajitokeza juu ya maji.

------------------------------------------------------------



Mimi ninapenda kusoma.

Nitamsomea nani?

Lena amelala.

Nitamsomea nani?

Mama na bibi wanapika.

Ni nani nitakayemsomea?

Baba na mjomba wanarekebisha gari.

Nitamsomea nani? 

Ninaweza kufurahia kukisoma kitabu mimi mwenyewe!

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, katika jiji kubwa la Johannesburg, mtoto msichana alizaliwa. Mtoto huyo alikuwa mimi. 

Mama yangu alinitaja Miriam. Miriam Makeba.

Mama alikuwa mganga wa kienyeji, lakini pia aliwasafishia watu wengine nyumba zao. 

Ilikuwa vigumu kwa mama kupata pesa za kututosha sisi wawili. Alianza kuuza pombe ya kienyeji ili kupata pesa zaidi.

Sheria za nchi hiyo zilisema kwamba kuuza pombe ya kienyeji ilikuwa mbaya. Polisi walimpeleka mama jela kwa muda wa miezi sita. 

Nilikuwa na umri wa siku 18 tu, na nilimhitaji mama yangu. Kwa hivyo ingawa nilikuwa mtoto mchanga, nilienda gerezani pia.

Nikiwa msichana mdogo nilipenda kuimba. Nilipokua mkubwa, nilimsaidia mama kusafisha nyumba. Nilipoimba nikifanya kazi, kazi ilikwenda haraka na siku zilionekana kung'aa. Kuimba kulinifurahisha kuliko ninavyoweza kuelezea.

Niliimba kanisani na hii ilifurahisha wengine pia. Muziki una uwezo wa kuwaleta watu pamoja.

Tulipokuwa tukiimba, tulikuwa jasiri na wenye nguvu.

Watu walisema sauti yangu ilikuwa zawadi na nyimbo zangu zilikuwa za kipekee. 

Niliimba na wanamuziki wengine na muziki wetu ulisikika ulimwenguni kote.

Nyumbani ilikuwa Sophiatown, mahali pa utamaduni na muziki. Sophiatown, mahali ambapo watu wa Afrika Kusini wangeweza kutunga muziki kwa maelewano na kucheza pamoja. 

Lakini watu ambao walitawala nchi wakati huo hawakupenda umoja huu. Watawala hao hawakutaka watu weusi na weupe kuwa marafiki.

Nilijua ilikuwa makosa kuwatendea watu tofauti kwa sababu ya rangi ya ngozi yao. 

Sikuficha imani yangu, na kwa hivyo wale watu waliotawala walinitaka niondoke nchini. 

Wakati nilikuwa nikiimba huko Amerika, niliambiwa singeweza kurudi nyumbani.

Watu kote ulimwenguni walisikia hadithi yangu. Nyimbo zangu na hadithi yangu ilisaidia wengi kuona jinsi hakukuwa na haki huko Afrika Kusini kwa wale waliokuwa na ngozi nyeusi. 

Niliamua kuendelea kuimba na kueleza ukweli kuhusu nchi yangu, bila kujali matokeo yake.

Ulimwengu uliupenda muziki wangu na nilikaribishwa katika nchi nyingi. Nilishinda tuzo na kuwaimbia watu mashuhuri ulimwenguni kote. 

Maisha yangu yalikuwa mazuri, lakini kulikuwa na upungufu fulani. Sikuweza kuimba katika nchi yangu, na watu huko hawakuwa huru.

Halafu siku nzuri ilifika wakati Nelson Mandela alikuwa rais wa Afrika Kusini. Watu wapya waliisimamia nchi na sheria zisizo za haki zilizikwa kwenye kaburi la sahau. 

Hatimaye, nilikwenda nyumbani nikiwa na matumaini mapya moyoni mwangu.

Baada ya hapo niliweza kuimba katika nchi huru, yenye haki. Watu wenye rangi tofauti za ngozi wangeweza kufurahia muziki pamoja. 

Nilisaidia kufanikisha hii kwa sababu nilikuwa shujaa na mwenye nguvu. Niliimba ukweli katika nyimbo zangu zote.

------------------------------------------------------------



Ngoma imekuwa ala muhimu ya muziki katika jamii mbalimbali. Tunazipenda ngoma!

Tuna ngoma za vimo tofauti: kubwa, wastani na ndogo.

Tunazicheza ngoma kwa kutumia kijiti, au kwa kutumia vidole vyetu.

Tunazicheza kwa sababu tofauti. Tunazicheza  kwa nyimbo na densi, wakati wa sherehe na wakati wa majonzi.

Ngoma huongezea nyimbo ladha na kuwafanya watu watake kucheza. Ngoma hufanya sherehe kuwa maridadi.

Tunazicheza wakati wa harusi na tunapomtaja mtoto jina. Tunacheza kusherehekea mavuno au kuzaliwa kwa mapacha.

Ngoma hulia kutangaza majonzi na kuwaita watu kunapotokea kifo.

Ngoma hulia kuwaita watu kusafisha kisima, barabara, au kumjengea mtu mkongwe nyumba.

Ngoma hutuita ng'ombe wetu wanapokuwa wameibwa.

Ngoma hulia kuwaita watu wakutane kwa chifu wetu.

Ngoma huwaita watu kwenda kanisani kwa maombi siku ya Jumapili, na kwenye siku zingine za maombi.

Pia, ngoma huchezwa kutia ladha wimbo unapoimbwa kanisani.

Ngoma kubwa husikika, "An a bul mba, an a bul mba, an a bul mba-mba-mba-mba bul." Nayo ndogo hutoa sauti ya juu, "Tindiri, tindiri tindiri ti."

Pamoja zote huitikia, "Tindiri mba, tindiri mba, tindiri mba-mba-mba-mba, tindiri ti!"

------------------------------------------------------------



Sikuwa nimewahi kuvaa viatu. 

Nilipowaona watoto waliovaa viatu, niliwatazama kwa hamu.

Mamangu alinifariji akisema, "Utakuwa na jozi nyingi baadaye, subiri tu utaona!" 

Wakati mwingine sikumwamini. 

"Baadaye, itakuwa lini?" nilimwuliza siku moja.

Kisha ulikuwa msimu wa Krismasi. Kila mtu alijishughulisha kwenda sokoni na kurejea na vitu vipya. 

"Mama, je, nasi tutaenda sokoni?" nilimwuliza.

Siku kabla ya Krismasi, mamangu aliniamsha mapema kuliko ilivyokuwa kawaida. 

Alinieleza nilichukue lile kapu kubwa ambalo alilibeba kila alipokwenda sokoni.

Sokoni palikuwa na wazazi wengi walioandamana na watoto wao. 

Walinunua nguo mpya na kiasi kikubwa cha vyakula.

Tulienda moja kwa moja hadi sehemu ya viatu aina tofauti. 

Nilishangaa kwa kuona mstari baada ya mwingine wa viatu vilivyopangwa kwa unadhifu.

Baada ya kupima baadhi ya jozi nyingi, nilichukua jozi ya viatu vya michezo. 

Sikuweza kulala usiku huo. Nilisisimkwa sana nilipowaza jinsi ningevivaa viatu vyangu vipya na kujivunia kila mtoto kijijini.

Muda mfupi baadaye, niliamka kitandani na kuvijaribu tena viatu vyangu. 

Nilitembea polepole chumbani kisha nikavirejesha sandukuni.

Nilijaribu kulala lakini sikupata usingizi.

Niliamka na kuvijaribu tena kwa mara ya pili. 

Nilitembea kwa maringo chumbani kisha nikavirejesha sandukuni.

Nilijaribu tena kulala nikinuia kupata usingizi. Lakini muda mfupi baadaye, niliamka kwa mara ya tatu. 

Nilivivaa vyatu nikaruka ruka kidogo chumbani. 

Nilihisi usingizi nikarudi kitandani.

Asubuhi yake, niliamshwa na mamangu. 

"Hiki ni nini ninachoona?" aliniuliza.

Nilikuwa nimevaa viatu vyangu vipya kitandani!

------------------------------------------------------------



Petros alikuwa mtoto wa pekee.

Alikuwa mwanafunzi mwerevu.

Siku moja, Petros alipata ruhusa ya kwenda kucheza na marafiki zake.

Alimuona mbwa akiwa amekwama shimoni.

Petros alisema, "Nitakusaidia."

Mbwa alibweka, akacheza na kumlamba Petros kwa furaha.

Marafiki za Petros walimfukuza mbwa huyo.

Petros alisema, "Acha! Acha!"

Mbwa aliwaogopa wale wavulana akajificha.

Marafiki za Petros walimkuta akilia.

Walimwambia, "Tutamtafuta mbwa wako."

Petros hakuwa na matumaini.

"Tutampata." Marafiki zake wakasema.

Walimtafuta kila mahali.

Petros alisema, "Anaweza kuwa karibu na mto."

Mbwa alipowaona, alitaka kuruka mtoni.

Petros alimsihi, "Usiruke majini!"

Mbwa alimkimbilia Petros. 

Walifurahi pamoja.

Marafiki za Petros walimwambia, "Tusamehe. Atakuwa rafiki yetu pia."

------------------------------------------------------------



Watu huishi katika nyumba aina mbalimbali. Baadhi ya nyumba zinajengwa kwa vifaa asilia, kama vile majani au nyasi. Nyumba nyingine zinajengwa kwa vifaa vilivyotengenezwa na binadamu, kama vile kioo na zege.

Baadhi ya nyumba zinajengwa kwa kutumia vifaa vya asilia na vilivyotengenezwa. Mfano ni nyumba ya mviringo inayozungumziwa katika hadithi hii.

Kabo na Thabo wanaishi katika Wilaya ya Kgatleng nchini Botswana, karibu na kijiji cha Mochudi. Wanaishi na wazazi wao katika nyumba ya mviringo.

"Nyumba ya mviringo ni aina ya nyumba ya jadi yenye paa la nyasi. Nyumba hizi hujengwa sehemu nyingi za kusini mwa Afrika," Kabo anaeleza.

Thabo anaendelea, "Nyingi wa nyumba hizi ni mviringo, na zina mlango na madirisha. Sisi tuna madirisha ya kioo, ambayo hawakuwa nayo zamani."

"Babu yetu alijenga nyumba hii ya mviringo kwa njia ya jadi. Baba yetu aliweka baadhi ya vifaa vya kisasa," Kabo anasema.

"Tueleze mchakato wa ujenzi," Kabo anapendekeza.

Anasema, "Wajenzi walitumia mbao, majani makavu, mawe, zege, na plasta.

Walianza kwa kuchimba shimo. Walijaza shimo hilo kwa mawe madogo, udongo, na mchanga. Hii ilifanya msingi kuwa imara na wenye nguvu wa kujenga juu yake."

Thabo anaendelea, "Wajenzi walitia miti mirefu ya mbao katika msingi, kuzunguka pembe ya nje. Waliifunga miti pamoja, wakifanya fremu ya mbao kwa ajili ya kuta za nje.

Baada ya muundo msingi kukamilika, wajenzi walitia mawe karibu karibu ndani ya fremu."

"Kisha, wajenzi walichanganya udongo, maji, na samadi ya ng'ombe. Hii hufanya zege ya asili ambayo ni ngumu sana inapokauka. Walitia zege kati ya mawe kuyafunga mahali pake," Kabo anasema.

"Kujenga kwa mawe na zege hufanya kuta imara ambazo hudumu kwa muda mrefu," Thabo anaongeza.

Kabo anasema, "Kuta kubwa za nje zinazuia joto."

Thabo anaeleza, "Uzibaji huu unamaanisha kwamba ndani kunabaki baridi wakati nje kuna joto jingi. Joto la jua halipenyezi kupitia kuta.

Katika maeneo yenye majira baridi, hii hufanya nyumba ya mviringo kuwa na joto wakati wa majira ya baridi kwa kuhifadhi joto ndani."

"Wajenzi waliumba sakafu ya nyumba yetu ya mviringo kwa kujaza udongo katika msingi walioufanya," Thabo anasema.

Kabo anasema, "Kukamilisha sakafu, walieneza safu ya mwisho ya udongo na kuijaza. Hii ilikauka kwa ugumu na kuunda uso uliosawazika, hata kwa sakafu.''

Thabo anasema, "Hatua ya mwisho ilikuwa kuweka paa. Nyumba ya mviringo kawaida huwa na paa la majani makavu yenye umbo la ncha.

Wajenzi walifanya fremu ya mbao na miti iliyounganishwa pamoja katika ncha katikati. 

Walishonea mafungu ya majani makavu kwenye miti kwa tabaka. Paa la majani makavu ni lenye kuzuia maji."

Nyasi ni nyenzo nzuri kwa paa. Lakini nyenzo hii ya asili pia huwa nyumba nzuri kwa wadudu na wanyama wengine. Wengi wao ni wadudu waharibifu!

Angalia picha na utafute: buibui watatu, nge, mende, mchwa, na panya.

Vifaa vya asili kama majani makavu ya nyasi hutengeneza mazingira mazuri kwa buibui kuishi na kuwinda.

Buibui hawaharibu paa la majani bali husaidia kudhibiti wadudu wengine.

Tunahitaji kutunza paa la nyasi ili kuwazuia wadudu waharibifu kama panya, viroboto, na mchwa.

"Kuna wengi wetu tunaishi katika nyumba kama hii ya mviringo!" anasema Thabo, akitazama paa la nyasi. Anaogopa buibui.

"Ninajiuliza ni wanyama wengine gani wanaoishi karibu nasi?" anauliza Kabo, kwa wasiwasi.

"Nitakapojenga nyumba yangu, nitajenga ya mviringo yenye paa la vigae!" anacheka Kabo.

------------------------------------------------------------



Korongo na Sungura walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Pia, walikuwa majirani wa karibu.

Kila mmoja wao aliishi na familia yake katika boma lake.

Urafiki wao ulitokana kwa wao kuonana mara kwa mara wakitafutia jamii zao vyakula. 

Kila walipopatana kichakani, waliamkuana na kisha kuendelea kutafuta chakula.

Siku moja, Sungura alimualika Korongo kwake na kumuahidi kuwa atamtayarishia supu tamu sana. Korongo alifurahishwa na jambo hilo. 

Walitenga siku ya kutembea kwake. Korongo alipofika, alikaribishwa na kuandaliwa supu.

Kwa sababu ya mdomo wake mrefu na mwembamba Korongo alijaribu kila njia, lakini hakuweza kuinywa ile supu.

Alihisi vibaya sana kwa kitendo ambacho Sungura alimtendea. Papo hapo akaamua kulipiza kisasi.

Hata hivyo alijipa moyo na kumkaribisha Sungura kwake. Siku ya kutembea ilifika.

Sungura hangeweza kupaa juu au kupanda juu ya mti. Waliagana kuwa rafikiye Korongo angembeba kwa mabawa yake.

Walipofika nyumbani kwa Korongo, naye alimwandalia supu vile vile. Ilipakuliwa kwenye nyungu ndefu nyembamba.

Sungura alijaribu kuinywa ile supu lakini hakuweza. Mdomo wake haungeingia mle ndani.

Sungura alifikiria jinsi ya kufanya ile supu ipande juu. Alimdanganya Korongo kuwa yeye humeza chakula akiwa ardhini.

Alipofika chini aliokota mawe akiyaweka ndani ya nyungu. Hatimaye, supu ilianza kupanda juu na Sungura akainywa. Alifurahi sana.

Korongo alipoona hivyo alikasirika na kumkibiza Sungura.

Sungura alikimbia na kuingia shimoni.

Urafiki wao uliishia hapo.

------------------------------------------------------------



Rangi 7 za upinde.

1 nyekundu.

Anavaa shati nyekundu.

2 rangi ya machungwa.

Ni nini yenye rangi ya machungwa katika picha hii?

3 rangi ya manjano.

Ni nini yenye rangi ya manjano katika picha hii?

4 kijani.

Ni nini yenye rangi ya kijani katika picha hii?

5 samawati.

Ni nini yenye rangi ya samwati katika picha hii?

6 nili.

Ni nini yenye rangi ya nili katika picha hii?

7 rangi ya urujuani.

Urujuani ndiyo rangi nzuri zaidi! Unapenda rangi gani?

Ni zipi rangi saba za upinde?

------------------------------------------------------------



Wakati ni zawadi iliyofungwa kama kifurushi.

Katika kifurushi hiki, vifurushi vingine vingi vinapatikana.

Mfano wa kifurushi kimoja cha wakati, ni siku.

Siku ina sekunde 86,400.

Ni lazima uufungue wakati na kuutumia vyema.

Tumia wakati ulio nao kujifunza mambo mapya.

Kula.
Cheza.
Pumzika.
Kuwa na maono.
Waza.

Ukipanda mti, msitu utakua.

Tatua tatizo.

Fedha zako zinapokuwa nyingi,
hifadhi zingine,
tumia zingine,
gawa zingine.

Unaposhindwa, anza tena.

Zawadi ya wakati imo katika kila siku.

Jumatatu na Jumanne.

Jumatano na Alhamisi.

Ijumaa na Jumamosi, hata Jumapili.

Hizi siku ni kama marafiki maalum.

Furahia urafiki wa kila siku.

Saa inaposema tik tok, yakumbuke maneno yangu.

Wakati ni kifurushi na ni zawadi ya kipekee.

Itumie zawadi hii vyema.

------------------------------------------------------------



Musau aliishi na babake, Syonzola.

Syonzola alienda kunywa pombe kila usiku.

Aliporudi nyumbani, aliita, "Nisaidieni! Fisi ananiua."

Watu walipokimbia kumsaidia, hawakumwona fisi.

Syonzola alifanya hivyo kila usiku.

Kila mara, Musau aliamshwa na kelele za babake.

Fisi alimvamia Syonzola usiku mmoja.

Kama kawaida, Syonzola aliita, "Nisaidieni!" 

Lakini watu walisema, "Tumechoshwa na Syonzola. Anatudanganya tu."

Musau alingoja. Babake hakufika.

Musau aliwaza, "Labda ni kweli kuwa babangu yuko hatarini."

Musau alitoka nje mbio.

Aliita, "Baba! Baba!" Fisi alitoroka.

Kutoka siku hiyo, Syonzola alibadilika. 

Anawasimulia watoto hadithi.

Maswali: 1. Musau aliishi na nani? 2. Syonzola aliwadanganya wanakijiji kwa kufanya nini? 3. Kwa nini watu hawakumsaidia Syonzola alipovamiwa na fisi? 4. Hadithi hii inaonesha madhara gani ya pombe? Pombe ina madhara gani ambayo hayajaoneshwa katika hadithi hii?

------------------------------------------------------------



Huyu ni Agnes. Yeye ni mwalimu.

Agnes hutumia magongo kutembea.

Huyu ni Metobo. Metobo ni DJ wa redio nimpendaye.

Metobo ana tatizo la macho.

Huyu ni jirani yangu Moraa. Moraa ni mkulima.

Moraa hasikii. Yeye hutumia lugha ya ishara kuwasiliana.

Huyu ni Osero. Osero ni mchezaji wa soka maarufu shuleni kwetu.

Osero hana mikono. Lakini, yeye huingizia mabao mengi timu yetu inapocheza.

------------------------------------------------------------



Je, unakumbuka Mbio Kuu zilizokuwa kati ya Sungura na Kobe? 

Kwa muda mrefu, hakuna yeyote katika miliki ya wanyama aliyeweza kuongea juu ya jambo tofauti ila zile Mbio Kuu na wapinzani wake wawili.



Inajulikana kwamba Sungura alishindwa kwa kuwa mvivu na mwenye kujiamini zaidi. 

Vilevile, inajulikana kuwa Kobe alishinda kwa mwendo wake wa polepole na kwa kuwa imara. 

Wanyama wa pori walijua hili na wakaendelea kuwaheshimu wanyama hao wawili kwa kiwango sawa.

Kobe na Sungura waliendelea kuwa marafiki. 

Kobe hakujivunia ushindi wake. 

Sungura, akifahamu kuwa alikuwa ameshindwa kwa uwazi, hakumshikia Kobe kisasi.

Miezi mingi ilipita. Mfalme wa pori ambako Sungura na Kobe waliishi alikuwa na jambo muhimu alilotaka kujadiliana na mfalme wa pori jirani. 

Lakini mfalme wa kwanza hangeweza kuondoka pale wakati huo. Badala yake, aliwatuma Sungura na Kobe kumwakilishi kwa yule mfalme mwingine.

"Mmoja wenu angalau, atalazimika kwenda kwa ufalme jirani," aliamrisha mfalme wakati Sungura na Kobe walikuja mbele zake. 

"Ninataka mjadili mambo muhimu na mfalme wa huko, halafu mniletee ripoti kuhusu maoni na mawazo yake juu ya mambo hayo. Sasa, nendeni!" Alisema alipomaliza.

Walipokuwa wakiondoka, aliongeza, "Kumbukeni,  mna siku moja tu ya kukamilisha kazi hiyo."

Barabara ya kwenda kwa ufalme jirani haikuwa laini wala rahisi. Ilijaa miiba.

Vilevile, walilazimika kuvuka mito miwili iliyokuwa na mawe makubwa.

Baada ya kuwaza kiasi, Sungura na Kobe waligundua kwamba hakuna mmoja wao ambaye angeweza kuitimiza ile kazi peke yake. Walilazimika kusafiri pamoja. 

Mpango ulikuwa kwamba Sungura ambebe Kobe watakapokuwa wakipita sehemu yenye miiba. Naye Kobe ambebe Sungura wakati watakapoavuka mito.

Siku iliyofuata, walikusanya jumbe tofauti kutoka kwa mfalme wao na kujitayarisha kuondoka. 

Sungura alitembea kwa hatua refu refu akakamilisha mwendo wa kupita sehemu ya miiba kwa kasi. 

Kobe alijishikilia asije akaanguka na kupoteza maisha yake.

Walipofikia mto, walibadilishana na Sungura akampanda Kobe mgongoni. Kobe aliogelea kutoka upande mmoja wa mto hadi mwingine kwa wepesi. 

Baada ya kuvuka mito yote miwili, haikuwachukua muda mrefu kufika katika ule ufalme jirani.



Baada ya kujadiliana na yule mfalme jirani kwa urefu mambo yote kutoka kwa mfalme wao, Sungura na Kobe walikuwa tayari kuondoka.

Safari ya kurudi ilikuwa nyororo na nyepesi kuliko ya kwenda kwani wote wawili walijua la kufanya. 

Sungura na Kobe walikuwa wamefanya kazi pamoja kwa maelewano makubwa hata wakamfikia mfalme wao mapema!

------------------------------------------------------------



Watu wanaishi katika nyumba aina nyingi tofauti. Watu wengine wanaishi katika nyumba zilizoko juu angani. Wengine wanaishi katika nyumba zilizo ardhini.

Majengo marefu yanaweza kuwa na nyumba nyingi ambazo zimejengwa juu ya nyingine. Kitabu hiki kinahusu kujenga jumba refu la ghorofa lenye sakafu nyingi.

Mishelle na Catherine ni dada. Mishelle amekaribia kumaliza shule ya upili. Catherine yuko katika mwaka wake wa mwisho wa shule ya msingi.

Dada hao wanaishi na wazazi wao na bibi yao katika jumba refu jijini Nairobi. Wanapenda kuishi juu ya jiji, kama ndege walio kwenye mti mrefu zaidi.

Familia inaishi katika ghorofa kwenye sakafu ya ishirini na mbili ya Jumba la Tower. Wanatumia lifti (au eleveta) kufika nyumbani kwao.

Catherine huhesabu sakafu wanaposafiri kwenda juu na chini. Anataka kuwa rubani siku moja. Mishelle anataka kuwa mhandisi na kujenga majengo marefu ya ghorofa.

Catherine anauliza, "Je, jengo letu ndilo refu zaidi barani Afrika?"

Mishelle anajibu, "Hapana, jengo hili lina urefu wa takriban mita mia moja na ishirini na sita. Jengo refu zaidi barani Afrika lina urefu wa zaidi ya mita mia tatu tisaini na tatu. Jengo refu zaidi duniani lina karibu mita mia nane na thelathini!"

"Ala! Majengo marefu namna hiyo husimama vipi?" anajiuliza Catherine.

''Kwa msingi, majumba yote marefu ya ghorofa hujengwa kwa njia ile ile. Vifaa viwili vikuu vya ujenzi ni chuma na saruji.

Jumba refu la ghorofa hujengwa sakafu kwa sakafu, kuanzia na fremu ya chuma, na kuongeza saruji kuzunguka fremu hiyo. Vifaa hivyo vikijumuishwa ni imara sana na hudumu kwa muda mrefu," anajibu Mishelle.

Ili kujenga jumba refu la ghorofa, wafanyakazi wa ujenzi lazima kwanza wachimbe shimo refu sana la msingi wa jengo.

Kama vile mti mrefu ulivyo na mizizi mikubwa na mirefu, jumba refu la ghorofa pia lazima liwe na msingi imara kwenye safu ya mwamba. 

Wakati mwingine mwamba uko chini sana kwenye udongo.

Kisha, wafanyakazi hutengeneza fremu ya jengo. Wanajenga fremu hiyo kwa vipande virefu vya chuma.

Fremu ya chuma inawezesha kujenga jumba refu la ghorofa. Chuma kinaweza kubeba uzito mwingi.

Fremu ya chuma ni kiini cha jengo, kama vile mifupa ya binadamu.

Chuma pia kinaweza kunyumbulika. Hii ina maana kwamba jengo linaweza kuyumba kidogo (ingawa ni vigumu kuona).

Kama kuna upepo mkali sana, au tetemeko la ardhi, muundo wa ndani wa chuma huruhusu jengo kuyumba kidogo.

Chuma huunda kiini cha nguvu kinachonyumbulika.

Vifaa vingine vikuu vya ujenzi ni saruji. Saruji ni mchanganyiko wa vifaa kama vile mchanga, simenti, na maji. Wafanyakazi wanachanganya saruji ili kupata kioevu kigumu, ambacho wanamwaga ndani ya fremu karibu na muundo wa chuma.

Wakati saruji inapokauka, inakuwa imara, kama mwamba. Hii ndiyo inayotengeneza sakafu na kuta za jengo.

Wafanyakazi wanajenga jumba refu la ghorofa kwenda juu, sakafu kwa sakafu. Sakafu za chini lazima zibebe uzito mwingi. Saruji inaweza kuhimili shinikizo hilo, ikifanya jengo liwe imara na thabiti.

Saruji ni safu karibu na fremu ya chuma, inayolinda chuma kutokana na maji na hewa. (Maji na hewa husababisha chuma kushika kutu).

Viyoyozi vya lifti pia hujengwa wakati huu. Wakati muundo wa chuma na saruji umekamilika, wafanyakazi wanaweka madirisha. Kisha wanaweka dari na kuta na kukamilisha sakafu.

Jengo linahitaji kuwekwa nyaya za umeme na mabomba ya maji na njia za kuhakikisha usafi.

Hatimaye, wafanyakazi huweka  taa, milango, kabati, na vitu vingine vinavyohitajika kwa maisha na kwa kufanya kazi katika jumba refu la ghorofa.

Mishelle anasema, "Miji mingi mikubwa inakaribia kuishiwa na nafasi. Majengo marefu yanatumia nafasi vizuri. Nitakapokuwa mhandisi, nitasaidia kujenga jumba refu la ghorofa lenye kimo kikubwa zaidi duniani!"

------------------------------------------------------------



Mbuni na Simba Jike walikuwa marafiki wakati mmoja.

Mbuni aliwalisha wanawe vyema.

Walikuwa wenye afya nzuri.

Watoto wa Simba Jike walikonda.

 Hawakupata chakula cha kutosha.

Simba Jike alitamani vifaranga wa Mbuni kuwa wake.

Siku moja, Mbuni alikwenda safari.

Simba Jike alichukuwa vifaranga wake.

Mbuni aliporudi, aliuliza, "Watoto wangu wako wapi?"

Mbuni alimkuta Simba Jike na watoto wake.

Simba Jike alimwambia, "Vifaranga ni wangu sasa. Wachukue wana simba."

Mbuni alijiuliza, "Nitawapataje wanangu?"

Mbuni aliitisha mkutana wa wanyama wote.

Wanyama walifika kuhudhuria mkutano.

Tembo aliwauliza Mbuni na Simba Jike kujieleza.

Wanyama wengi waliogopa kumulaumu Simba Jike.

Kichakuro alisema, "Watoto wanaofanana na ndege, ni wa Mbuni."

Baada ya kusema hivyo, Kichakuro alitoroka akaingia shimoni.

Simba Jike alikasirika sana. 

Alirudi kwake na wana simba.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Mfalme Chui alianza kuwaza juu ya maisha ya usoni.  Alitafakari, "Ninazeeka, na siku moja, nitakufa. Mfalme nwenye busara, anastahili kumchagua mrithi wake akiwa angali kijana na mwenye afya." 

Lakini, Mfalme Chui atafanya uchagazi namna gani? Aliwapenda wanyama wote!

Mfalme Chui alipata wazo. Aliwaalika wanyama wote kwenda katika ikulu. Wajumbe walikimbia kila sehemu ya kichaka wakiwaalika wanyama.

Alipanga kuwa na sherehe kubwa kisha awatangazie mpango wake.

Usiku wa sherehe, wanyama wote walikuwa katika ikulu. Waliimba, wakacheza  wakawa na wakati mzuri. Usiku wa manane, Mfalme Chui alisimama katikati ya ikulu. 

Wanyama waliacha kuimba na kucheza. Walisikiliza kwa makini mfalme wao alipoanza kuzungumza.

Alisafisha koo akasema, "Nilikuwa nikiwaza na wakati umetimia wa kumchagua mrithi wangu. Kwa sababu ninawapenda nyote, siwezi kuamua nani anayefaa zaidi. Nimepanga mashindano yatakayoamua."

Mfalme Chui alishika mkuki akasema, "Wa kwanza miongoni mwenu atakayerusha mkuki angani kisha ahesabu mpaka kumi kabla ya mkuki huo kutua chini, ndiye atakayekuwa mrithi wangu."

Mfalme Chui alipomaliza kuzungumza, wanyama walisikia sauti kubwa ikitoka nyuma yao. Walipogeuka, walimwona Tembo akielekea mbele kwa kishindo. "Tokeni njiani. Mimi ni mkubwa zaidi, ninastahili kuwa mfalme," Tembo alisema.

Tembo aliuchukua mkuki, akaushika kwa mkonga wake. Alikirudisha kichwa chake nyuma kisha akaurusha mkuki angani. "Moja! Mbili! Tatu! Ah!" Tembo alilia. Mkuki uligonga chini alipofikisha nne. Tembo alikasirika akaanza kufoka. 

Mfalme Chui alimwambia, "Ulipata nafasi
yako." Tembo alilazimika kuondoka.

Baada ya Tembo kuondoka, wanyama walianza kuzungumza miongoni mwao kwa msisimuko. Walisikia tena sauti kubwa ikitoka nyuma yao. 

Ngiri alikuja kwa kishindo akisema, "Niondokeeni. Niondokeeni. Nitakuwa mfalme. Nina misuli mikubwa zaidi. Nina nguvu kuliko wote. Lazima niwe mfalme."

Ngiri aliinama, akaukamata mkuki kisha akaurusha angani. "Moja! Mbili! Tatu! Nne! Tano! Ah!" Alipiga kelele. Mkuki ulianguka alipofikisha sita. Alirusha uchafu hewani kwa hasira.

Chui alimwambia, "Ngiri, unapata nafasi mara moja tu ya kurusha mkuki. Umeshaipata." Ngiri pia alilazimika kuondoka.

Baadaye, wanyama walianza kutoa maoni yao na kusema, "Mashindano hayo ni magumu! Tembo, ingawa ni mkubwa, hakufaulu. Ngiri, ingawa ana nguvu sana, pia hakufaulu. Hakuna atakayeshinda mashindano haya!" 

Wakati huo huo, walisikia sauti nyingine kutoka nyuma yao. Walipotazama, hawakuamini macho yao.

Walimwona Sokwe mkubwa akienda mbele. Alikuwa akiimba, "Ninaweza. Najua ninaweza. Ninaweza." Sokwe aliuchukua mkuki akasonga nyuma hatua kadhaa. Aliuvuta mkono wake nyuma, akarudi mbele kisha akaruka hewani na kuurusha mkuki angani. "Moja! Mbili! Tatu! Nne! Tano! Sita! Saba! Ah!" Sokwe alilia.

Mkuki uligonga chini alipofikisha nane. Sokwe alikasirika akazungukazunguka akilalamika. 

Lakini, Mfalme Chui alimwambia, "La, Sokwe, unapata nafasi mara moja tu." Ilimbidi Sokwe pia aondoke.

Baadhi ya wanyama walianza kuondoka kwenda nyumbani. Walipokuwa wakiondoka, walimwona Swara mdogo akija kujaribu bahati yake. Swara alisema, "Subirini! Subirini! Hebu nijaribu. Ninaweza kufaulu. Ninaweza. Nipeni nafasi nijaribu." 

Wanyama wengine walianza kumcheka Swara.

Mfalme Chui aliwashauri wanyama, "Acheni kumcheka Swara! Ni nani aliyesema kwamba wanyama wadogo hawawezi kufanya kazi ambayo wale wakubwa wanafanya? Lazima Swara apewe nafasi sawa kama wanyama wengine. Rudini nyuma ili Swara atupe mkuki."

Swara alimwinamia mfalme, akauchukua mkuki mdomoni. Akitumia nguvu zote, alikimbia mpaka katikati ya uwanja. Aliruka juu akavuta pumzi kisha akaurusha mkuki huku akisema kwa sauti kubwa, "Tano na tano ni kumi." Mkuki ulitua chini.

Wanyama wote walichanganyikiwa. Mfalme Chui aliwaeleza, "Ndiyo, Swara! Tano na tano ni njia nyingine ya kupata kumi. Kuna zaidi ya njia moja  ya kuhesabu mpaka kumi." Mashindano hayakuwa kumpata mnyama mkubwa wala mwenye nguvu. Bali lilikuwa kumpata mnyama mwerevu! Hivyo ndivyo Swara alivyokuwa malkia baada ya chui kufariki.

------------------------------------------------------------



Nyani na Mamba walikuwa marafiki wa dhati. 

Walicheza pamoja. Walikula pamoja. Walifanya kila kitu pamoja.

Siku moja, Mamba alikuwa mgonjwa mahututi. Alikuwa karibu kufa.

Mamba alienda kwa mkanga. "Kama unataka kupata nafuu, itakubidi ule nyama ya Nyani," mkanga akamwambia.

Aliposikia haya, Mamba alilia.

Kama angetaka kupata nafuu, hakuwa na jingine ila kumla rafikiye, Nyani.

Nyani alipoenda kumwona rafiki yake Mamba, aliupanda mgongo wake.

Mamba alimpeleka Nyani mtoni kwenye maji mengi.

"Ni nini kinachokutatiza, rafiki yangu?" Nyani aliuliza.

Mamba alisema, ''Mkanga aliniambia kuwa kama ninataka kupata nafuu lazima nikule wewe, rafiki yangu."

Nyani akajibu, "La hasha! Huwezi kunila. Mimi ni mdogo mno!

Subiri nimwite babu yangu. Ni mkubwa kuniliko mimi. Ukimla yeye utashiba."

Mamba akauliza, "Yu wapi huyu babu yako?"

Nyani akajibu, "Yuko mtini kule kisiwani."

Mamba akasema, "Nenda ukamlete ili nimle."

Nyani aliruka na kukimbia moja kwa moja hadi mtini.

Mamba akangoja na kungoja lakini Nyani hakurudi.

Na huo ndio ukawa mwisho wa urafiki wao.

------------------------------------------------------------



Fisi na Kunguru walikuwa marafiki ingawa walikuwa tofauti. 

Kunguru aliruka lakini Fisi alitembea tu.

Siku moja Fisi alitaka kumfahamu Kunguru zaidi. Alimwuliza, "Ni kitu gani cheupe kilicho nyuma ya shingo yako?" 

Kunguru alimjibu Fisi, "Ni nyama nono nimekuwa nikiila huko angani ninaporuka. Nimeila kwa muda mrefu hadi imejibandika shingoni mwangu."

Fisi aliposikia juu ya nyama, alidondokwa na mate. Alitamani sana kula nyama hiyo. Ataipataje ikiwa angani naye hakuwa na mabawa ya kuruka na kuifikia? 

Fisi alimwomba Kunguru, "Tafadhali rafiki yangu, nikopeshe manyoya ili nijitengenezee mabawa. Nina hamu sana ya kuruka kama wewe na kuila ile nyama."

Kwa ukarimu wake, Kunguru alimpatia Fisi manyoya. 

Fisi aliyashona mabawa, akayaunganisha na mwili wake akajaribu kuruka. Uzito wake ulimshinda akalazimika kuwa na mpango tofauti.

Fisi alimwambia Kunguru, "Niruhusu niushikilie mkia wako utakaporuka angani." 

Kunguru alikubali akasema, "Ninajua una hamu ya kuruka. Hebu tufanye hivyo kesho asubuhi." 

Asubuhi ilipofika, Fisi aliushikilia mkia wa Kunguru, Kunguru aliporuka.

Kunguru aliruka mpaka akachoka kabisa. 

Fisi alimsihi, "Tafadhali rafiki yangu, endelea kidogo zaidi!"

Walipokifikia kipande cha kwanza cha wingu kubwa jeupe, Fisi alidhani ni nyama nono. Mara Fisi alisikia sauti. Unyoya mmoja alioushika uling'oka kutoka kwenye mkia wa Kunguru! Akasikia sauti ya pili, ya tatu na ya nne. Kunguru alijihisi mwepesi. Alikuwa ameondokewa na mzigo 'Fisi.' 

Kunguru aliimba: 
Manyoya ya Kunguru jinyonyoe. Manyoya ya Kunguru jinyonyoe. Fisi aliimba kinyume akisema: Manyoya ya Kunguru yashikane yasijinyonyoe. Manyoya ya Kunguru yashikane yasijinyonyoe.



Hatimaye, manyoya yote yaling'oka. Fisi akaelea peke yake angani. 

Alilirukia wingu jeupe akidhani ni nyama nono ambayo angejishikilia. Lakini, alipojaribu kuishika ile "nyama," aliyashika mawingu majimaji tu!

Fisi alianza kuanguka kwa kasi kutoka angani. Alipaza sauti akisema, "Nisaidie! Nisaidie!" 

Hakuna aliyemsikia. Kunguru alikuwa ametokomea mawinguni.

Fisi alianguka chini kwa kishindo akalala kimya kwa muda. 

Baadaye aliamka kwa maumivu akipiga mayowe. Mguu wake mmoja ulikuwa umevunjika. 

Alikuwa na madoadoa mengi mwilini.

Fisi hajaweza kuruka. 

Urafiki baina yake na Kunguru haukuwepo tena.

------------------------------------------------------------



Huyu ni ng'ombe mtulivu.

Mchana yeye ni ng'ombe wa kawaida.

Hupeperusha tiara.

Au kucheza mpira.

Usiku yeye hubadilika na kuwa Ng'ombe Shujaa.

Yeye huokoa maisha.

Na kupambana na uhalifu.

Wewe pia ukiyafumba macho yako kabisa, kisha uwe na hamu kubwa.

Huenda ng'ombe akakutembelea pia!



------------------------------------------------------------



Haaaa! 

Nyumbani kwetu, kuna ng'ombe wa ajabu.

Ana pembe moja tu na hana mkia. 

Ni ng'ombe mzuri sana.

Ni ng'ombe mnono aliye na tumbo kubwa.

Ni ng'ombe aliye na nguvu.

Mchungaji anampenda ng'ombe huyu sana. 

Amemfunza kuitambua sauti yake pekee.

Ng'ombe huyu anapokuwa malishoni, hujitenga na ng'ombe wengine.

Ni ng'ombe aliye hodari katika vita.

Ng'ombe wengine wanamwogopa.

Watu wengi wanamjua ng'ombe huyu. Wanamwogopa kwa sababu yeye hupigana kwa pembe yake moja. 

Je, ukikutana na ng'ombe wa aina hii, utafanyaje?

------------------------------------------------------------



Wekesa alikuwa na donda mguuni. 

Yeye na mkewe waliishi kijijini na wanao.

Binti yao, Nangila, na kaka zake watatu walifanya kazi zao vizuri.

Nangila aliwavutia watu wengi. 

Wanaume waliotaka kumwoa walitakiwa kutimiza sharti kali lililowekwa na babake.

Aliyetaka kumwoa Nangila alilazimika kuileta dawa ya kienyeji kutoka ziwa lililokuwa karibu. Ziwa hilo lilijaa mizimu hatari. 

Ile dawa ya kienyeji kutoka ziwani tu ndiyo ingeponya lile donda alilokuwa nalo babake Nangila.

Baadhi ya wanaume waliojaribu kuipata ile dawa, walirudi mikono mitupu. 

Wengine hawakurejea kutoka ziwani kamwe.

Nangila alikuwa na hofu kaka zake pia waliposhindwa kwenda ziwani. Aliamua kwenda mwenyewe. 

Mamake alimwambia, "Mwanangu, ikiwa wanaume wenye nguvu wameshindwa, wewe utafaulu?" 

Lakini, Nangila hakubadili nia yake.

Njiani, Nangila alimsaidia bi kizee mmoja kubeba kuni. 

Bi kizee alimshukuru akasema, "Nitakueleza utakavyofika kwenye lile ziwa la mizimu na namna utakavyofanya."

Nangila alipofika ufukoni mwa ziwa, aliiona familia ya mizimu ikinywa na kusherehekea. 

Alisubiri na kutazama. Mmoja baada ya mwingine, mizimu ilipatwa na usingizi.

Mizimu yote ilipolala, Nangila alipiga mbizi ziwani. 

Aliipata ile dawa na kuiweka mkobani. Alipokuwa akiogelea kurudi ufukoni, mawimbi makubwa yalimzunguka.

Ufukoni, mizimu ilikuwa imeamka. Nangila aliimba wimbo aliofundishwa na bi kizee: 

Mie binti Wekesa, nilikuja kwani wanaume waliogopa. Babangu ahitaji dawa kupona donda. Nd'o sababu nipo pahali hapa pa kutisha, kwani ninyi ni viongozi.

Sauti ya Nangila ilikuwa tamu sana hata mizimu ikamtaka aimbe zaidi. 

Kuimba kwake kuliifanya ilale tena. Nangila alikimbia haraka akafika kijijini.

Baada ya kutibu donda la babake, baba aliweza kusimama tena. 

Kijiji kizima kilisherehekea na kumshangilia Nangila.

MASWALI: 1. Mwanamume yeyote aliyetaka kumwoa Nangila alilazimika kutimiza sharti lipi la babake? 2. Nangila alikuwa na kaka wangapi? 3. Nangila alisaidiwa na nani alipokuwa njiani? Alimfundisha Nangila nini? 4. Alipofika ufukoni mwa ziwa, Nangila alisubiri nini? 5. Nangila alifanya nini ili atoroke mizimu aliporudi ufukoni? 6. Kwa maoni yako, unafikiri Nangila ataolewa baada ya kutimiza sharti la babake yeye mwenyewe? Kama ataolewa, ataolewa na mtu wa aina gani?

------------------------------------------------------------



Mzee Nyembe alikuwa akiishi na familia yake kijijini.

Familia hiyo ilijaa ufukara.

Mzee Nyembe alijitahidi sana kwenye shughuli zake za uwindaji.

Lakini, hakufanikiwa.

Mzee Nyembe akampa moyo mke wake ili asikate tamaa.

Kisha, akamwaga na kuelekea porini yalipokuwa mawindo yake.

Mzee Nyembe alitembea msituni kukagua mitego yake.

Hakuamini kwani mtego mmoja ulikuwa umemnasa twiga.

Mzee Nyembe hakuweza kuamini macho yake!

Akajiwazia mwenyewe na kusema, "Sasa, umasikini umeniishia. Twiga huyu atanipa faida kubwa sana."

Twiga akiwa pale naye akasema, "Tafadhali bwana wangu, kama hutojali nataka kukuonyesha utajiri."

Mzee Nyembe akashangaa kusikia kuwa twiga huyo angeweza kumuonyesha utajiri.

Akamwuuliza, "Wapi ulipo utajiri? Ukinionyesha nitakuacha huru uende zako."

Twiga akajibu, "Utajiri huo upo mwilini mwangu. Unajua kwa nini niliumbwa mrefu kuliko wanyama wote?"

Mzee Nyembe akajibu, "Hapana! Sijui!"

Twiga akaendelea, "Ni kwa sababu kichwani mwangu vipo vipande vya dhahabu."

Mzee Nyembe alistaajabu kusikia habari hiyo.

Twiga akaendelea, "Unajua jinsi unaweza kuvipata hivyo vipande vya dhahabu?"

Mzee Nyembe akajibu, "Sijui! Tafadhali, nieleze nijue."

Twiga akasema, "Ukinifungua, nitakuonyesha jinsi ya kupata hivyo vipande vya dhahabu."

Mzee Nyembe akapatwa na tamaa. 

Alikuwa na tamaa kubwa ya kupata vipande vya dhahabu.

Akafanya haraka kumfungua twiga kutoka mtegoni.

Twiga huyo alipofunguliwa, alimpiga teke mzee Nyembe akaanguka chini.

Mzee Nyembe alijitahidi kumkamta twiga, lakini alishindwa.

Mzee Nyembe akarudi nyumbani akiwa na upweke mkubwa kwa kumkosa twiga.

------------------------------------------------------------



Miaka mingi iliyopita, jamii ya wanyama wenye pembe iliamua kuandaa karamu kubwa milimani. 

Wanyama wote wenye pembe walialikwa.

Nguruwe aliposikia kuhusu karamu hiyo, aliwaza,  "Mimi sina pembe. Je, nitafanyaje ili nihudhurie karamu hiyo?"

Nguruwe aliamua lazima angeshiriki katika ile karamu. 

Alisonga pembe kwa kutumia nta na kuzipachika kichwani mwake!

Nguruwe alifaulu na akakubaliwa kuhudhuria karamu hiyo. 

Karamu iliandaliwa juu milimani karibu na jua.

Karamu ilipokuwa ikiendelea, joto lilizidi na nta ikaanza kuyeyuka. Mara pembe za nguruwe zikaanguka chini pu! 

Wanyama walipomwona nguruwe bila  pembe walishangaa na kuulizana, "Ni nani yule asiye na pembe? Kwa nini alialikwa?"

Mfalme wa wanyama aliamuru nguruwe ainuliwe juu na kisha aangushwe. 

Walimnyanyua nguruwe na kumtupa chini kwenye bonde kubwa.

Maskini nguruwe, aliangukia pua lake. 

Papo hapo, pua lake likabadilika na kuwa refu kama linavyoonekana hadi sasa.

Usishangae unapoliona pua la nguruwe jinsi lilivyo.

------------------------------------------------------------



Siku moja, Buibui Anansi, alivuna viazi vikuu shambani mwake. 

Vilipendeza na kuonekana vitamu sana. 

Alivichoma taratibu kwenye moto na akaanza kula.

Buibui Anansi alipokuwa akitia tonge la kwanza kinywani, mlango wake ulibishwa. "Lo! Lo! Lo!" alisema moyoni. "Huyo ni nani?" 

Kasa, aliyeonekana mchovu, alisimama mlangoni. Kasa alisema, "Anansi, tafadhali niruhusu niingie. Nimetembea mwendo mrefu leo. Nimechoka na ninahisi njaa." 

Buibui Anansi alimruhusu Kasa akaingia.

Buibui Anansi hakumgawia mwengine chakula chake kitamu, hata mgeni. 

Kasa alipotaka kula, Buibui Anansi alimkemea, "Kasa, huwezi kula kwa mikono michafu. Nenda ukanawe kwanza." 

Mikono ya Kasa kweli ilikuwa michafu sana kwani aliitembelea siku nzima. Kasa alijikokota hadi mtoni akanawa mikono kisha akarudi.

Buibui Anansi alibaki akibugia viazi kwa haraka. Kasa aliporejea hakupata kiazi hata kimoja. 

Kasa alimwambia Buibui Anansi, "Asante kunialika kwa chakula cha jioni. Nami pia nitakukaribisha kwangu nikuandalie chakula kitamu." 

Kasa alijikokota kuelekea nyumbani kwake.

Siku moja Buibui Anansi aliwasili nyumbani kwa Kasa kabla chakula cha jioni. Kasa alikuwa amejilaza chali akiota jua kama Kasa wafanyavyo. 

Alipomwona Buibui Anansi, alisema, "Aa! Hujambo Anansi! Umekuja kushiriki nami chakula cha jioni?" 

Buibui Anansi akaitikia, "Naam, nitafurahia sana, asante." 

Anansi alikuwa akihisi njaa mno.

Kasa alipiga mbizi na kuzama chini ya mto akaandaa chakula cha jioni. Naye Buibui Anansi alingoja kando ya mto. 

Baada ya maandalizi, Kasa alirudi juu ya maji akasema, "Kila kitu ki tayari, karibu. Twende tukafurahie mapochopocho." 

Kasa alipiga mbizi tena na akaanza kula majani matamu aliyokuwa ameandaa.

Buibui Anansi alijaribu kujizamisha mtoni lakini, wapi! Yeye alikuwa buibui wala sio kasa. Alishindwa kupiga mbizi kabisa. Kila alipojaribu, alielea juu ya maji. 

Alijaribu kuruka majini tena na tena lakini ng'o! Hakufanikiwa kukifikia chakula kilichoandaliwa na Kasa chini ya maji.

Hatimaye, Buibui Anansi alipata wazo zuri. Alitia mawe kwenye mifuko ya koti lake. Akawa mzito akaweza kuzama majini. Alikuwa mwerevu kwelikweli! 

Sasa aliweza kuiona meza iliyojaa majani matamu na laini pamoja na vyakula vingine vya kupendeza. Alidondokwa na mate alipoviona vyakula hivyo.

Buibui Anansi alipokuwa akinyoosha mkono kuchukua chakula hicho cha kupendeza, Kasa alimkataza akisema, "Anansi, unawezaje kula ukiwa umevaa koti? Haiwezekani hapa kwangu." 

Bila kufikiri, Buibui Anansi akasema, "Samahani! Bila shaka usemavyo ni kweli. Sikufikiria kuhusu hilo." Buibui Anansi, alilivua koti lake.

Punde tu alipolivua koti, Buibui Anansi alielea juu ya maji kwa sababu hakuwa na mawe ya kumwezesha kuzama. 

Alihuzunika na akachopeka kichwa chake majini akawa anamtazama Kasa akila chakula hicho chote kitamu peke yake.

------------------------------------------------------------



Katika kijiji kimoja, kulikuwa na mvulana aliyeitwa Abula.

Abula hakupenda kusoma wala hata kufungua kitabu. Licha ya kuwa mwanafunzi mvivu alikuwa na tabia mbovu.

Abula alizoea kuiba pesa za mamake na kununua peremende. Hata mama alipozificha, Abula alizipata.

Alipomaliza kula peremende, Abula angeenda kucheza na marafiki zake.

Baada ya muda, Abula aliacha kwenda shuleni. Alicheza mchana kutwa na kurudi nyumbani jioni.

Mamake alipogundua jambo hilo, alikuwa na wasiwasi.

Alimwambia mumewe, "Mtoto wetu amekuwa mtukutu. Nadhani hata haendi shuleni. Pia ananiibia pesa."

Baba aliwaza jinsi angembadilisha Abula tabia kwa njia mwafaka.

Alimwambia mkewe, "Wakati mwingine, zifiche pesa zako katika kurasa za kitabu. Kwa vile yeye hafungui vitabu, pesa zako zitakuwa salama pale."

Siku iliyofuata, Abula alitafuta pesa za mamake kila mahali lakini hakupata chochote.

Aliamua kwenda soko iliyokuwa karibu kuona kama angepata pesa zozote.

Baba aliona kule Abula alikuwa akienda.

Alisema, "Mwanangu, ninajua kwa nini unakwenda sokoni. Sasa rudi nyumbani ukatafute pesa kwenye vitabu."

Abula alishangaa, lakini alikwenda nyumbani akatafuta kwenye vitabu.

Alizipata pesa ambazo mamake alikuwa ameficha.

Siku iliyofuata, Abula alitafuta tena kwenye vitabu. Lakini, hakuna pesa zozote zilizokuwa zimefichwa humo.

Alimwuliza babake kwa nini hakupata pesa zozote kwenye vitabu.

Babake alitabasamu kisha akamjibu, "Mwanangu, je, ungependa kupata pesa nyingi za kununua vitu vingi vitamu?"

Abula alimjibu, "Bila shaka, baba."

Babake alisema, "Nisikilize vizuri. Soma vitabu vyako na uhudhurie shule. Utapata zawadi nyingi kwenye vitabu. Usikate tamaa."

Abula alijibu, "Lakini baba, kusoma ni kazi ngumu. Vitabu vinachosha mno!"

Baba aliwaza juu ya kumhamasisha mwanawe. Alimwambia Abula, "Hebu tusome pamoja. Nitakusaidia upate mali vitabuni."

Abula alisoma kwa bidii. Mwishoni, alifaulu na kuishi maisha mazuri.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani katika ikulu kubwa, paliishi mfalme na bintiye mrembo.

Tembo aliishi katika nyumba upande mmoja wa ikulu. 

Kinyonga aliishi upande mwingine.

Wakati huo, kukashuhudiwa kiangazi kikubwa katika nchi ile. 

Mfalme alikuwa na wazo kisha akawaita majirani zake kwenda ikuluni.

Mfalme aliwaambia Tembo na Kinyonga, "Ninataka mkanyage ardhi hadi maji yapatikane." 

Mfalme aliahidi kuwa atakayefaulu atamwoa bintiye wa kifalme.

Kinyonga hakuwa na matumaini yoyote kwa ajili ya udogo wake. 

Tembo alifurahi mno kwani alikuwa na umbo kubwa na mwenye nguvu. Alienda uwanjani na kuanza kukanyaga aridhi.

Vumbi nyingi ilitokea, lakini hapakuwa na maji. 

Tembo alikanyaga aridhi hata karibu maji yatokee, lakini alielekea kuchoka. 

Alimwachia Kinyonga nafasi kujaribu.

Kinyonga alianza kukanyaga aridhi. Baada ya muda mfupi, maji yalitoka. 

Watu hawakuamini macho yao!

Kwa hivyo, Mfalme alimpa Kinyonga bintiye. 

Tembo alienda nyumbani kwa hasira.

------------------------------------------------------------



Elia aliishi katika nyumba ya kifahari mjini Ebiba. Wazazi wake walikuwa matajiri.

Elia alikuwa na mbwa aliyeitwa Chita. Alimtunza Chita vizuri sana.

Kila siku, baba alimpeleka Elia shuleni na kumrudishi jioni.

Alasiri moja walikuwa njiani kurudi nyumbani. Baba alienda katika duka moja kubwa kununua bidhaa.

Elia alimwona mzee mmoja aliyekuwa amebaba mzigo mkubwa mgongoni.

Alikuwa amechoka kwa hivyo alitembea polepole. Elia aliendelea kumtazama.

Mzee yule aliketi chini ya mti kisha akafungua mzigo ule.

Alichomoa chupa mbili za plastiki akaanza kuzitengeneza viatu.

Elia aliwaza juu ya mzee huyo kwa muda mrefu. Alihuzunika na wala hakuweza kufurahia chakula chake.

Aliwaza, "Nitawezaje kumsaidia?"

Aliamua kuchukua baadhi ya fedha zake. Akamwita Chita halafu akapanda baiskeli yake na kuondoka.

Alienda hadi kwenye lile duka ambako babake alikuwa amenunua bidhaa.

Alinunua vitu vingi akampelekea yule mzee na kusema, "Hujambo babu!" 

Mzee alimjibu, "Amani iwe nawe, mwanangu."

Elia akamwuliza, "Babu, unatoka wapi?"

Mzee akamjibu, "Mwanangu, njaa imenifukuza kutoka kijijini kwangu. Nipo hapa kutafuta ajira."

Elia alimpatia bidhaa alivyokuwa amenunua. 

Mzee yule hakuamini alipoviona viatu. Alimshukuru Elia kwa moyo wake wote.

Elia alisema, "Sasa lazima nirudi nyumbani kabla mamangu hajaanza kunitafuta."

Elia na mbwa wake walipoondoka, mzee aliwapungia mkono. Alisema kwa tabasamu, "Barikiwa, mwanangu."

Elia alipowasili nyumbani, mamake alimwuliza, "Ulikuwa wapi?" Mama alikuwa na wasiwasi.

Elia alimwambia kila kitu. Mama alimmwonea mwanawe fahari kubwa sana kwa kitendo chake cha ukarimu.

Baadaye, baba alimwambia Elia, "Tunakujivunia, mwanangu. Lakini, ni lazima utuambie kabla ya kuondoka nyumbani. Shika hizi hela utumie kwa sababu ulitumia zako kumsaidia yule mzee!"

------------------------------------------------------------



Babangu anapenda sana uji wa mahindi.

Mimi napendelea uji wa wimbi.

Babangu anapenda kahawa.

Ninatamani maziwa siki.

Babangu anapenda sana matofaa.

Minapenda machungwa.

Babangu anapenda mkate wa siagi. 

Mimi napenda mkate we sinia.

Sisi sote tunapenda keki kubwa.

------------------------------------------------------------



Jina langu ni Simo.

Nina marifiki wanne.

Majina yao ni Zizo,  Lele,  Sisa na Ayanda.

Rafiki yangu Zizo,  hupenda kucheza mpira.

Rafiki yangu Lele,  hupenda kuogelea.

Rafiki yangu Sisa,  hupenda kucheza mchezo wa kidalipo.

Rafiki yangu Ayanda,  hupenda kusoma.

Mimi hupenda kufanya vyote wanavyopenda kufanya.

Hucheza mpira na Zizo.

Huogelea kwenye bwawa na Lele.

Hucheza mchezo wa kidalipo na Sisa.

Wewe pia njoo. 

Wewe pia ni rafiki. 

Unapenda mchezo gani?

------------------------------------------------------------



Mkahawa huzaa matunda yaliyo na mbegu ndani. Mbegu hizo ni kahawa.

Kuna hekaya nyingi kuhusu jinsi kahawa ilivyogunduliwa. Mojawapo inamhusu Kaldi, raia wa Ethiopia.

Kaldi alikuwa mchungaji nchini Ethiopia. Inasemekana kuwa siku moja mbuzi wake waliyala matunda ya rangi nyekundu kutoka mti wa kahawa. 

Baadaye, Kaldi alishuhudia mbuzi hao wakirukaruka kwa uchangamfu usiokuwa wa kawaida.

Kaldi alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kujua ikiwa matunda yale yaliwapa mbuzi wake nguvu fulani. 

Alionja ladha yake chungu alipoyatavuna.

Baadaye, Kaldi alikuwa macho. Yeye pia alihisi nguvu fulani mpya.

Alichuma baadhi ya majani na yale matunda.

Aliyapeleka nyumbani na kumpatia mkewe.

Mkewe alipoyatavuna yale matunda, naye pia aliathirika kama Kaldi. Alikuwa macho na kuhisi nguvu ya kipekee.

Kaldi na mkewe waliamini kuwa matunda yale yalikuwa zawadi kutoka kwa Mungu.

Siku chache baadaye, Kaldi aliwapelekea watawa matunda yale na majani yake.

Aliwahadithia jinsi mbuzi wake walivyoathirika walipoyala matunda yale.

Alipoondoka, watawa wawili walimfuata kisirisiri wakitaka kujua ikiwa ilikuwa ukweli.

Walihakikisha walipowaona mbuzi wakichangamka na kucheza baada ya kuyala yale matunda.

Watawa walirudi nyumbani na kuyachemsha yale matunda ya kahawa.

Walipoyanywa maji yaliyochemka, ladha yake ilikuwa chungu sana! Walidhani kuwa kilikuwa kinywaji cha shetani.

Waliyatupa matunda yaliyobaki kwenye moto. Yalipochomeka, walinusu harufu yake nzuri.

Walipata wazo la kuzikaanga zile mbegu kwanza kabla ya kuzichemsha.

Kinywaji kilichotoka kwenye mbegu zilizokaangwa kilikuwa na ladha nzuri zaidi.

Baada ya watawa kunywa kinywaji kile, walikuwa macho na wenye nguvu.

Tangu wakati huo, watu hunywa kahawa ili kuwa macho na pia kuburudika.

Kwa hivyo, unywaji wa kahawa ulianzia nchini Ethiopia na kuenea ulimwengu mzima!

------------------------------------------------------------



Nyumba hii iko Kongo.

Ninaipenda nyumba hii.

Tulikuwa na choo chetu binafsi.

Tulikuwa na bafu letu binafsi.

Tulikuwa na bustani.

Nilipanda kwenye bustani yangu mwenyewe.

Mama yangu aliniambia, "Nilifunzwa na mama yangu kupanda. Nami ninakufunza wewe."

Nilipanda nyanya na mchicha. 

Nilifanya hivyo peke yangu.

Ningempelekea mama nyanya.

 Naye angesema, "Asante."

Tuliiacha nyumba hiyo huko Kongo.

Hatuna bustani hapa Afrika Kusini.

------------------------------------------------------------



Siku moja, mimi na babangu tulisafiri katika gari letu kwenda mjini. 

Tulisimama kwenye mzunguko tukisubiri taa zigeuke kijani.

Nilimwona mwanamke akitembea pembeni mwa barabara. 

Alivaa nguo ya kuvutia ya rangi ya chungwa.

Alikuwa amefunga kiunoni mshipi mkubwa mwekundu. 

Alipita katikati ya mvulana na mama aliyembeba mtoto mgongoni.

Alikipakata kibeti cha rangi ya chungwa. 

Alipita karibu na machungwa mengi yaliyokuwa yakiuzwa.

Miguuni, alivivaa viatu vya rangi ya chungwa vyenye visigino virefu. 

Nilitamani kuwa na viatu kama vyake.

Alikutana na msichana mdogo aliyekuwa akimtembeza mbwa wake. 

Alishtuka na kuzigusa nywele zake. zilikuwa zimefungwa kwa kibano cha rangi ya chungwa.

Alipokuwa akirekebisha kibano cha nywele, kibeti chake kilimponyoka. 

"Uuu," nilimhurumia.

Mwanamke huyo aliinama kukiokota kibeti chake.

Alipokuwa akikifuta kibeti chake vumbi, niliviona vipuli virefu vikubwa vyenye rangi ya chungwa. 

Sikuwa nimeviona vipuli maridadi kama hivyo!

Wakati huo, taa ziligeuka kijani nasi tuliendelea na safari yetu. 

Hata hivyo, mimi nilizidi kutazama nyuma.

Baba alipogundua, alitabasamu akaniuliza, "Ni nini unachotazama?"

Nilimjibu, "Mwanamke wa rangi ya chungwa." 

Nilikumbuka kwamba nguo yangu vilevile ilikuwa ya rangi ya chungwa.

------------------------------------------------------------



Siku moja mamangu alinunua matunda aina tofauti.

Tulijiuliza, "Mama atatugawia matunda wakati gani?"

Baadaye, kakangu, Rahim, alijificha na kuyala matunda yote!

Tulisema kwa hasira, "Rahim ni mtukutu tena ni mchoyo. Lazima aadhibiwe."

Mama aligundua kuwa matunda yote yalikuwa yameliwa. Alikasirika sana.

Tulimtazama Rahim kwa ukali.

Nilimwuliza mama, "Je, utamwadhibu Rahim?"

Baadaye, Rahim alipata adhabu asiyoitarajia.

Hakuweza kutulia!

Mama alipomwuliza alijibu kwa sauti ya chini,  "Naumwa na tumbo."

Hiyo ilikuwa adhabu mbaya kuliko kama Rahim angechapwa na mama.

Alipopata nafuu, Rahim alituomba msamaha. Aliahidi kuwa hataiba tena.

------------------------------------------------------------



Katika jiji moja, kuliishi wavulana wa kurandaranda mtaani. Asubuhi moja walikuwa wakikoka moto kutumia karatasi walizookota. 

Miongoni mwao alikuwepo Magozwe, aliyekuwa mdogo kuliko wote.

Wazazi wa Magozwe walifariki akiwa na umri wa miaka mitano tu. 

Magozwe alienda kuishi na mjombake ambaye hakumjali. Alifanya kazi nzito bila kupewa chakula.

Magozwe alipolalamika, mjombake alimpiga. Alipotaka kwenda shule, mjombake alisema, "Usinisumbue. Wewe ni mjinga. Hata huwezi kujifunza chochote." 

Baada ya kuteswa kwa miaka mitatu, Magozwe alitoroka akaanza kuishi mtaani.

Maisha ya mtaani yalikuwa magumu. Walikosa chakula. Walikamatwa na polisi. Walichapwa na wananchi na pia walikuwa wagonjwa. 

Mara kwa mara, kulikuwa na vita baina yao na makundi mengine. Wavulana hao walitegemea kuombaomba. Pia waliuza plastiki, vyuma, chupa na magazeti makuukuu.

Siku moja, Magozwe aliokota kitabu cha hadithi. Alikikukuta vumbi na kukiweka ndani ya gunia lake. 

Kisha alizitazama picha kwani hakujua kusoma maneno.

Kitabu kilikuwa na picha za mvulana aliyekuwa rubani wa ndege. Magozwe alitamani sana kuwa rubani. Ndoto yake ilikuwa awe rubani bora zaidi ulimwenguni. 

Mara nyingi aliyafumba macho na kuwaza kuwa alikuwa akiendesha ndege kubwa kuliko zote!

Ulikuwa msimu wa baridi. Magozwe aliombaomba barabarani. Mwanamume mmoja alimsalimu na kujitambulisha kwake, "Hujambo? Ninaitwa Tomaso. Ninapajua mahali unapoweza kupata chakula." 

Tomaso alimwonyesha nyumba yenye paa la bluu. Magozwe alimtazama Tomaso, akaitazama ile nyumba kisha akasema, "Labda." Akaondoka na kwenda zake.

Miezi iliyofuata, wavulana wa mtaani walikuwa wamezoea kumwona Tomaso. Tomaso alipenda kuzungumza na watu walioishi mtaani. Aliwasikiliza wakizungumzia maisha yao. 

Tomaso alikuwa na nia nzuri, mvumilivu na mwenye heshima. Baadhi ya wavulana walianza kwenda katika nyumba ya paa la bluu. Wakati wa mchana walipata supu na mkate.

Magozwe alipokuwa akikitazama kitabu alichokiokota, Tomaso alimwuliza, "Hadithi hiyo inahusu nini?" 

Magozwe alimjibu, "Nadhani inamhusu mvulana aliyekuwa rubani." 

"Anaitwaje?" Tomaso alimwuliza. Magozwe alijibu kwa sauti ya chini, "Sijui. Siwezi kusoma."

Baadaye, Magozwe alimweleza Tomaso sababu iliyomfanya atoroke kwa mjombake. Tomaso alimsikiliza ila hakumfanyia uamuzi.

Magozwe aliposherehekea miaka kumi ya kuzaliwa kwake, Tomaso alimpatia kitabu kipya cha hadithi. Kilimhusu mvulana mchezaji kandanda maarufu. 

Tomaso alimsomea Magozwe hadithi hiyo kila mara. Siku moja alisema, "Wakati wa kwenda shule umefika. Utaweza kujisomea. Unaonaje?" 

Tomaso alimwonyesa mahali watoto waliposaidiwa kwenda shule.

Magozwe alianza kufikiria kuhusu mahali hapo na kuhusu kwenda shule. 

"Labda mjombangu alisema ukweli kwamba mimi ni mjinga na siwezi kujifunza chochote? Na je, nikipigwa huko nitafanyaje? Labda ni heri kubaki mtaani." 

Magozwe aliyafikiria mambo hayo kwa hofu.

Magozwe alimwelezea Tomaso mawazo yake na hofu aliyokuwa nayo. 

Muda ulipopita, Tomaso alimshawishi Magozwe. Alimwambia kuwa maisha yake yangekuwa bora iwapo ataenda shule.

Magozwe alihamia katika chumba kimoja kwenye jumba kubwa. Alikitumia chumba hicho pamoja na wavulana wengine wawili. Jumla, walikuwepo watoto kumi walioishi katika jumba lile.

Waliishi na Shangazi Cissy na mumewe, mbwa watatu, paka na mbuzi mmoja.

Magozwe alipoanza kwenda shule, haikuwa rahisi. Mara nyingi alitaka kukata tamaa. 

Lakini, alipokumbuka rubani na mchezaji kandanda maarfu aliowasoma katika vitabu vya hadithi, alivumilia.

Siku moja Magozwe alipokuwa akisoma kitabu,  Tomaso alimwuliza, "Hadithi unayoisoma inahusu nini?" 

Magozwe alimjibu, "Inamhusu mvulana aliyekuwa mwalimu." "Anaitwaje?" Tomaso alimwuliza tena. 

"Anaitwa Magozwe." Magozwe alisema kwa tabasamu.

------------------------------------------------------------



Huyu ni Natabo. 

Ana ndugu sita wa kiume.

Wazazi wake walimpatia chungu kidogo. 

Alikipenda sana.

Siku moja, ndugu zake walikivunja chungu hicho.

Natabo hakukiona chungu chake. 

Alilia kwa muda mrefu.

Natabo alitoroka nyumbani. 

Alipanda mti mrefu.

Wazazi wake walimsihi, "Tafadhali, shuka chini."

Ndugu zake waliimba, "Tafadhali, shuka chini."

Natabo aliufanyia mzaha wimbo wao.

Naye rafiki ya Natabo akaimba, "Tafadhali, shuka chini."

Rafiki yake aliimba mpaka Natabo akashuka chini.

Marafiki hao walienda nyumbani pamoja.

Walisherehekea. 

Natabo alipata chungu kipya!

------------------------------------------------------------



Mukulima alikuwa na Fahali mzee.

Pia, alikuwa na Punda. 

Fahali na Punda walikuwa marafiki.

Mwisho wa siku, Fahali alimwambia Punda, "Leo nimechoka sana."

Siku iliyofuata, Fahali tena alilalamika, "Leo sikupumzika hata kidogo."

Punda alimjibu, "Nilienda sokoni. Kazi yangu ilikuwa ngumu kuliko yako."

Kesho yake Fahali alisema tena, "Leo ilikuwa siku mbaya kwangu."

Punda alimjibu, "Mkulima akija, mlilie, 'Moo! Moo!' Atakuruhusu upumzike."

Fahali alimlilia mkulima, "Moo! Moo!" 

Mkulima alimruhusu akapumzika.

Mkulima alimfunga Punda jembe. 

Punda alilima badala ya Fahali.

Punda alifanya kazi siku nzima. 

Jioni, alikuwa amechoka sana.

Punda alisema, "Mkulima ameamua kukuchinja. Unachoka sana tena u mgonjwa."

Fahali alimjibu Punda, "Kesho nitafanya kazi yangu. Nimepata nafuu."

------------------------------------------------------------



Siku moja, Mbwa aliyakuta mayai kando ya mto. 

Akajiuliza, "Mayai haya ni ya nani?"

Mbwa aliyachukuwa yale mayai na kwenda nayo nyumbani kwake.

Alipofika nyumbani, aliyaweka karibu na moto ili yaangue.

Mamba alikutana na Mbwa akamwuliza, "Umeyaona mayai yangu?" 

Mbwa akamjibu, "La."

Mamba akatembea kila mahali akiuliza kila mnyama, "Umeyaona mayai yangu?" 

Kila mmoja alimjibu, "La."

Mayai yale yaliangua moja baada ya nyingine. 

Mamba wachanga walianza kutambaa.

Mbwa hakuwalisha wana mamba vizuri. 

Walihisi njaa kila wakati.

Siku moja, Mamba aliwasikia wanawe wakilia. 

Alijua kwamba Mbwa ndiye aliyachukua mayai yake.

Alimvamia Mbwa nyumbani kwake akamcharaza kwa mkia. 

Mbwa alitorokea dirishani.

Mamba alimfukuza Mbwa akitaka kumwadhibu zaidi.

Mbwa alimwambia Mamba, "Nisamehe! Sikujua kuwa mayai yalikuwa yako!"

Mamba alimsamehe. 

Baadaye, aliwapeleka wanawe kuogelea kwa mara ya kwanza.

------------------------------------------------------------



Mbuzi, Mbwa na Ng'ombe walikuwa marafiki wakubwa. 

Siku moja walisafiri kwa teksi.

Walifika mwisho wa safari yao.

Dereva aliwauliza walipe nauli zao. 

Ng'ombe akalipa.

Mbwa hakuwa na kiasi kamili cha pesa, akalipa zaidi kidogo.

Dereva alikuwa anajitayarisha kumrudishia Mbwa baki ya pesa zake.

Wakati huo, Mbuzi alitoroka bila kulipa chochote.

Dereva akakasirika sana. 

Akaondosha gari bila kumrudishia Mbwa baki ya pesa zake.

Hiyo ndiyo sababu, siku zote, Mbwa hulikimbilia gari. 

Nia yake ni kumpata dereva amrudishie baki ya pesa zake.

Mbuzi, anapousikia mlio wa gari, hutoroka. 

Yeye huogopa kushikwa kwa kukosa kulipa nauli.

Ng'ombe huwa hashughuliki gari linapokuja. 

Yeye huchukua muda kuvuka barabara.

 Anajua kwamba alilipa nauli yake kamili!

------------------------------------------------------------



Mara moja kwa siku, basi kubwa la bluu husimama katika kijiji cha akina Bobo kuwasafirisha watu hadi mjini. Bobo hajawahi kuliona basi kubwa kama hilo. Anayahesabu madirisha 9 ya abiria na moja la dereva. "Lazima kuna safu 9 za viti vya abiria, kila safu ikiwa na takriban viti 8," Bobo anawaza.

Ikiwa ni sawa namna Bobo anavyowaza, je, basi kubwa la bluu linaweza kuwabeba abiria wangapi?

Kesho, mamake Bobo atampeleka mjini kununua sare mpya ya shule. Mama huuza mayai dazeni moja kwa shilingi 120. Karibu kila juma, yeye hupata jumla ya shilingi 3600. Je, ni mayai dazeni ngapi anazohitaji kuuza ili aweze kupata shilingi 3600? Kwa majuma 4 yaliyopita, aliweka akiba nusu ya fedha zake ili amnunulie Bobo sare mpya. 

Je, unaweza kufanya hesabu ya kiasi cha fedha alizoweka akiba kwa muda wa majuma 4?

Takriban miezi mitatu imepita tangu Bobo asafiri kwa basi. Ana hamu kubwa ya kutaka kusafiri tena!

Kesho itakuwa siku kubwa. Inapofika saa moja jioni, Bobo yuko kitandani, lakini hapati usingizi wowote. Hafikirii jambo jingine ila tu safari yake ya kwenda mjini. Ni saa tatu na nusu, lakini Bobo bado hajalala.

Kila asubuhi, mama humwamsha Bobo saa moja. Lakini leo, Bobo tayari yuko macho inapofika saa kumi na mbili, ingawa usiku uliopita, aliweza tu kulala ilipotimia saa tano.

Inapotimia saa moja, Bobo ameoga na kuvaa, tayari kuondoka. Je, Bobo alipata usingizi kwa saa ngapi usiku uliopita?

Saa moja kasororobo asubuhi, Bobo na mamake wanawasili kituoni. Lile basi kubwa la bluu linastahili kuwasili kituoni inapotimia saa mbili asubuhi. 

Mamake Bobo anaitazama saa yake. Lile basi kubwa la bluu tayari limechelewa kwa dakika kumi na tano. "Lakini, kawaida, basi hili halichelewi. Sijui kuna shida gani?" mama anasema.

Muda mfupi baadaye, watu zaidi wanajiunga nao pale kituoni. Wao pia wanazitazama saa zao na kuuliza kwa nini basi limechelewa. "Sasa tayari zimetimia saa tatu. Nitachelewa kufika kazini!" mwanamume mmoja aliyevalia suti nyeusi, anasema.

Bobo na mamake ndio waliosubiri kwa muda mrefu zaidi. Bobo anaona kama amesubiri kwa saa nyingi. Lakini, si saa nyingi. Je, wamekuwa wakisubiri kwa muda gani?

Bobo ana wasiwasi. "Je, nitaipata sare yangu kweli?" anamwuliza mamake.

Bobo anahesabu kwamba safari ya kwenda mjini na kurudi itawachukua saa 4. Saa 1 kufika huko, saa 2 kununua na saa 1 kurudi nyumbani. "Kuna mpira wa soka saa nane ambao mimi na marafiki zangu tumepanga kucheza. Basi lisipofika kwa wakati, nitachelewa kujiunga na wenzangu kwa mchezo huo."

Bado wanasubiri. Bobo sasa analia. Watu wawili walio kwenye foleni, wanaondoka na kurudi nyumbani. Wengine wanaendelea kuzitazama saa zao.

"Hebu tuwe na subira. Nina hakika kwamba basi litakuja hivi karibuni," mamake Bobo anawaambia. "Ninataka kwenda nyumbani!" Bobo analia kwa sauti. Mamake anamtuliza, "Tusubiri kwa dakika kumi tu. Basi lisipokuwa hapa saa tatu na nusu, tutaenda nyumbani."

Halafu, wanasikia mngurumo wa basi barabarani. "Si niliwaambia," mamake Bobo anasema. "Sasa ni saa tatu na nusu kamili. Tutanunua kwa haraka. Basi likiondoka mjini kwa wakati, tutafika nyumbani kwa wakati ufaao nawe utacheza mpira wa soka ulivyopanga."

Bobo anafuta machozi. Anahisi uchungu miguuni. Amechoka. Hawezi kusubiri kuliabiri lile basi.

La kushangaza ni kwamba, basi hili sio lile kubwa la bluu. Bali ni basi ndogo nyekundu. Bobo anahesabu madirisha ya abiria 4 pekee kisha anasema, "Mama, basi hii ni ndogo sana kuliko lile la bluu. Halitakuwa na nafasi ya kutosha kuwabeba watu wote wanaokwenda mjini."

Je, unakubaliana na Bobo? Unaweza kukisia idadi ya abiria ambao basi hiyo ndogo itaweza kubeba?

Mamake Bobo anamtania, "Wasiwasi wako hauna msingi. Angalau sote tunaosubiri hapa kituoni, tutapata nafasi ya kuketi."

"Hebu tuabiri kwa haraka ili tupate viti vizuri. Tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu zaidi ya wote!"

Bobo na mamake wanaabiri basi. Nyuma yao kuna watu 9 zaidi wanaotaka kuabiri. "Je, kutakuwa na viti vya kututosha sote?" Bobo anauliza.

Anaona kwamba kuna safu 4 za viti basini, upande mmoja ukiwa na viti 2 na mwingine ukiwa na viti 2 pia. Je, kuna viti vingapi jumla? Je, watu wote walio kwenye foleni wataweza kuketi?

Bobo na mamake wanakalia viti 2 vilivyo mbele karibu na mlango. Wana nafasi kubwa mbele yao na pia wanaweza kutazama nje vizuri.

Bobo anahesabu watu 6 wapya wanaojiunga na wengine kwenye foleni. "Hao wanafanya jumla ya idadi ya abiria kuwa 17," anawaza. "Mama, kuna nafasi ya kila mtu," Bobo anamweleza mamake. "Ni mtu mmoja tu atakayelazimika kusimama."

Je, Bobo alihesabu sawa?

Basi sasa imejaa. Dereva anaifunga milango na kuanza safari. Kuna kelele nje. Bobo na abiria wengine wanatazama dirishani.

Watu zaidi wanakimbia wakitaka kuifikia basi. Wanapiga mayowe, "Subiri! Subiri! Tunahitaji usafiri." Lakini wamechelewa. Bobo na mamake wanawahurumia walioachwa nyuma.

Mamake Bobo anamwuliza dereva, "Mbona hukujia lile basi kubwa la bluu?" Dereva anajibu, "Liliharibika jana. Hii basi ndogo nyekundu pekee ndiyo iliyopatikana."

"Je, na wale watu wote tuliowaacha nyuma?" mamake Bobo anauliza. Dereva anasema, "Usiwe na wasiwasi. Nitakuwa na safari mbili leo."

Bobo anasikiliza wanavyozungumza. Mawazo yake yanajaa nambari.

Bobo anahesabu viti tena. "Basi hii inawabeba watu 20, 16 wakiwa wameketi na 4 wakiwa wamesimama." Anajiuliza, "Basi hii itaweza kwenda safari ngapi ili iwapeleke abiria 100 mjini? Na abiria 200 au 150, je?" Unaweza kulipata jawabu?

Bobo amefurahi. Hivi karibuni, ataipata sare mpya. Kisha, basi itawarudisha nyumbani kwa wakati ili acheze soka.

------------------------------------------------------------



Sakima aliishi na wazazi wake na dada yake mwenye umri wa miaka minne. 

Waliishi katika shamba la mtu tajiri. 

Nyumba yao ya nyasi ilikuwa mwisho wa safu ya miti iliyopendeza.

Sakima alipokuwa na umri wa miaka mitatu, aliugua na kupoteza uwezo wa kuona. 

Hata hivyo, Sakima alikuwa na vipaji vya kipekee.

Sakima alitenda mambo mengi ambayo wavulana wengine wa umri wake hawakufanya. 

Kwa mfano, angeketi na watu wazima na kujadiliana nao.

Wazazi wa Sakima walifanya kazi katika nyumba ya yule tajiri. 

Waliondoka nyumbani asubuhi na mapema na kurudi jioni. 

Sakima aliachwa na dadake.

Sakima alipenda kuimba nyimbo sana. 

Siku moja mamake alimwuliza, "Sakima, unajifunza nyimbo hizi kutoka wapi?"

Sakima alimjibu, "Nazisikia akilini mwangu kisha naziimba." 

Mama hakumwelewa mwanake.

Sakima alipenda kumwimbia dadake, hasa alipohisi njaa. 

Dadake alimsikiliza na kucheza.

"Tafadhali Sakima, niimbie  tena," dada yake angemsihi. 

Sakima angekubali na kumwiimbia mara nyingine.

Jioni moja, wazazi wake waliporudi nyumbani,  walikuwa kimya sana. 

Sakima alijua kwamba lazima kulikuwa na tukio baya.

"Kuna shida gani, mama, baba?" Sakima aliwauliza. 

Sakima aligundua kwamba mwana wa tajiri wao alikuwa amepotea. 

Tajiri alikuwa amehuzunika na kuhisi upweke mkubwa.

"Labda atafurahi tena nikimwimbia," Sakima aliwaambia wazazi wake. 

Wazazi wake walidharau wazo lake. "Yeye ni tajiri. Wewe ni mvulana asiyeona. Wimbo wako utamsaidiaje?"

Hata hivyo, Sakima hakukata tamaa. 

Dada yake vilevile alimpa moyo, "Nyimbo za Sakima hunituliza mimi nikiwa na njaa. Zitamtuliza tajiri pia."

Siku iliyofuata, Sakima alimwambia dadake amwongoze hadi kwenye nyumba ya yule tajiri.

Alisimama chini ya dirisha moja na kuanza kuimba wimbo wake alioupenda. 

Polepole, kichwa cha yule tajiri kilianza kuonekana dirishani.

Wafanyakazi wote waliacha kazi zao wakamsikiliza Sakima. 

Hata hivyo, mwanamme mmoja alisema, "Hakuna aliyefaulu kumtuliza bwana. Je, huyu mvulana asiyeona ataweza kumtuliza?"

Sakima alipomaliza kuimba wimbo wake alianza kuondoka. 

Tajiri alitoka nje kwa haraka na kusema, "Tafadhali, imba wimbo wako tena."

Wakati huo huo, watu wawili walikuja wakiwa wamembeba mtu kwenye machela. 

Walikuwa wamemkuta mwana wa tajiri akiwa amechapwa na kuachwa kando ya barabara.

Tajiri alifurahi sana kumwona mwanawe tena.   Alimzawadi Sakima kwa kumliwaza. 

Aliwapeleka mwanawe na Sakima hosipitalini ili Sakima aweze kusaidiwa kuona tena.

------------------------------------------------------------



Siku moja, mzee mmoja alikwenda porini. 

Alitaka kuangalia mtego wake kwa lengo la kupata chakula.

Alipokaribia, aliona twiga amenaswa kwenye mtego wake. 

Alifurahi sana.

Aliwaza akasema moyoni, "Nikimfungulia yule twiga atakimbia."

Alibadilisha mawazo akaamini kuwa twiga hangeondoka.

Aliwaza, "Nikimfungulia yule twiga nitaweza kumuua."

Akarusha mkuki na kwa bahati mbaya akakata kamba badala ya kumuua twiga. 

Alihuzunika sana.

Kwa hasira, alimrukia yule twiga. Akashika mkia wake akiwa anajua kuwa twiga atadondoka. 

Twiga yule alikazana na kukimbia.

Twiga akampiga yule mzee teke la tumbo. 

Mzee akadondoka chini.

Mzee akaelekea kwake kwa maumivu bila chakula chochote. 

Alilalamika sana.

------------------------------------------------------------



Afifah ni mtoto wa kifaru mweupe.

Walinzi wa wanyama pori walimuokoa kutoka kichakani.

Mama yake aliuawa na majangili.

Walinzi wa wanyama pori walimpeleka Afifah mahali pa usalama.

Afifah aliumia moyoni.

Pia aliogopa kwamba majangili watarudi kuchukua pembe yake.

Polepole, Afifah alipata marafiki.

Alijisikia salama na akacheza matopeni.

Alikunywa maziwa yenye lishe.

Siku moja Afifah alimwuliza rafiki yake Amina, "Kwa nini wanataka pembe zetu?"

Amina akamjibu, "Wanaamini kuwa pembe zetu ni za kimiujiza!"

"Lakini pembe zetu sio za kimiujiza!" Afifah alilia.

"Hapana, bila shaka, sivyo. Pembe ni sawa na nywele na kucha," Amina alisema.

Afifah na Amina ni wa mwisho wa aina yao.

Vifaru weupe wamekaribia kutoweka.

Karibu wote wametoweka kutoka ulimwenguni.

Tunaweza kuwaokoa vifaru weupe na wanyama wengine wanaoelekea kutoweka.

Je, unaweza kufanya nini?

Pata kujua zaidi!

------------------------------------------------------------



Biantaka alikuwa na ng'ombe.

Alikuwa pia na chungu kidogo cha maji.

Alienda kwa jirani yake kuomba chungu kikubwa.

Biantaka aliweka chungu kidogo ndani ya kile kikubwa.

Alivibeba vyungu vyote akampelekea jirani yake.

Biantaka alimwambia jirani, "Chungu chako kilizaa."

Biantaka alirudi kwa jirani kuomba chungu tena.

Hakukirejesha. 

Jirani aliamua kwenda kumwuliza.

Biantaka alisema, "Kilikufa. Nilikuwa najitayarisha kuja kukwambia."

Jirani alipiga kelele, "Sijawahi kusikia chungu kikifa!"

Biantaka alijibu, "Rafiki yangu, kila kitu kinachozaa lazima kife."

Jirani alienda mahakamani kumshtaki Biantaka.

Hakimu alisema, "Kila kiumbe hai kinachozaa, lazima kife."

Biantaka alipata chungu kikubwa. 

Jirani yake akakipoteza chungu chake.

------------------------------------------------------------



Kuna milango mitano ya fahamu: macho, masikio, pua, ulimi na vidole.

Ninatumia macho yangu kuona.

Naweza kuona paka. 

Naweza kuona panya.

Ninatumia masikio yangu kusikia.

Naweza kusikia sauti ya basi. 

Beep! Beep! 

Naweza kusikia sauti ya gari.

Vroom! Vroom!

Ninatumia pua yangu kunusa.

Naweza kunusa maua.

Naweza kunusa chakula.

Ninatumia ulimi wangu kuonja.

Naweza kuonja ndizi tamu.

Naweza kuonja supu ya chumvi.

Ninatumia vidole vyangu kugusa.

Naweza kugusa blanketi laini.

Naweza kugusu kitabu kigumu.

Kuna milango mitano ya fahamu: macho, masikio, pua, ulimi na vidole.

Milango mitano ya fahamu inanisaidia kufahamu mazingira yangu.

------------------------------------------------------------



Zamani, Moto, Maji, Ukweli na Uongo walikuwa marafiki.

Uongo hakufurahia urafiki huo. 

Alitafuta njia ya kuuvunja.

Siku moja Uongo alisema, "Tuitafute nchi huru ili kila mmoja wetu amiliki ufalme wake." 

Walikubaliana wakaanza kutafuta nchi huru.

Uongo alimwambia Maji, "Moto ni adui yetu mkubwa. Yeye huunguza kila kitu. Tutafute ufalme ambako Moto hatakuweko."

Maji akauliza, "Tutafanyaje?" 

Uongo akamjibu, "Ni wazi kwamba tutamuua. Ni wewe tu uliye na uwezo wa kufanya hivyo. Atakapokuwa ameketi chini, jimwagilie kwake umharibu!"

Maji alisema, "Nikifanya hivyo nitaenea kila mahali. Sitaweza kujikusanya tena." 

Uongo alisema, "Hilo si tatizo. Nitayaweka mawe chini yakuzuie kuenea, kisha nitakukusanya tena." 

Uongo alifanya hivyo.

Moto alipokuwa ameketi chini, Maji alijimwaga kwake bila Moto kujua. Kupitia njia hiyo, Uongo aliweza kumwangamiza Moto. 

Yeye na Maji waliendelea na safari yao.

Baada ya muda, Uongo alimwambia Maji, "Hebu keti juu ya ukingo huu ili uyafurahie mandhari haya."

Maji alipokuwa ameketi chini, Uongo aliyaondosha mawe yaliyomzingira. 

Maji alimwagika akatapakaa kila mahali. Huo ndio ulikuwa mwisho wake.

Sasa Uongo alilazimika kumwangamiza Ukweli. 

Walipofika kwenye mlima mkubwa, Uongo alimweleza Ukweli asubiri chini ya mlima.

Kisha Uongo akalisukuma jiwe kubwa kutoka juu kumwangamiza Ukweli.

Jiwe lilipoporomoka chini, almasi, dhahabu na vito tofauti vya thamani vilipatikana. 

Ukweli aliweza kujivuta na kutoka chini ya jiwe lililokuwa limevunjika.

Uongo alishuka chini kutazama mwili wa Ukweli. Badala yake, aliona vito vya thamani. 

Akauliza, "Vito hivi vimetoka wapi?"

Ukweli alijibu, "Jiwe liliponiangukia, vito hivi vilimwagika." Uongo pia alitaka vito hivyo vya thamani. 

Alisema, "Nitaenda chini ya mlima nawe uende juu uliangushe jiwe jingine kubwa."

Basi, Ukweli akapanda juu ya mlima akalisukuma chini lili jiwe kubwa.

Jiwe hilo lilimwangukia Uongo kichwani. 

Akafa papo hapo.

Hata hivyo, Uongo hubishana na Ukweli kila siku.

------------------------------------------------------------



Nilipoamka asubuhi,  nilikula kifungua kinywa.

Nilikimbia kwenda kukutana na rafiki yangu Muthoni.

Pindi nilipompata Muthoni,  tulisahau kila kitu.

Mimi na Muthoni tulicheza michezo tofauti karibu na nyumba.

Tulifanya kila kitu pamoja.

Tulikubaliana kufanya bidii katika masomo yetu na kufuzu vyema.

Lakini siku moja, Muthoni hakufika shuleni.

Nilimsubiri lakini, hakufika.

Niliporudi nyumbani siku ile, nilimwambia mama.

"Muthoni hakuja shuleni leo."

Niliendelea na masomo yangu lakini nilimkosa Muthoni sana.

Nilimtafuta Muthoni kila mahali.

Sasa nimekua msichana mkubwa lakini ninamkosa rafiki yangu Muthoni.

------------------------------------------------------------



Tamara alikuwa msichana wa miaka mitano. 

Aliishi na familia yake karibu na msitu wenye wanyama wakali.

Tamara aliwatii wazazi wake. 

Aliwasaidia kuwachunga kondoo na mbuzi wao.

Tamara alipenda kuwasikiliza ndege wakiimba. 

Walipoimba, aliwaiga huku akitunga nyimbo zake.

Kwa sababu ya umri wake mdogo, Tamara hakuwa ameanza kwenda shule. 

Nashipae na Tasieku walikwenda kwa sababu walikuwa wakubwa.

Nashipae, Tasieku na watoto wengine kutoka kijijini walienda pamoja asubuhi na kurudi jioni. 

Walikuwa wakibeba chakula katika mikebe midogo.

Siku moja, Tamara alimwuliza mamake, "Je, nitaanza kwenda shule lini?" 

Mama alimjibu, "Utaenda hivi karibuni mwanangu mpendwa."

Siku moja, chifu na wenzake walifika nyumbani kwa gari. 

Lilikuwa jukumu la chifu kuhakikisha kwamba watoto walienda shule walipofikisha umri uliokubaliwa.

Watu waliamini kwamba mtoto akiweza kuunyoosha mkono wake kupita kichwani na kulishika sikio lake, mtoto huyo yuko tayari kuanza kwenda shule.

Chifu alimwuliza Tamara, "Una umri wa miaka mingapi?" 

Tamara alimjibu, "Mitano." 

"Hebu tuone ikiwa unaweza kwenda shule," chifu alisema.

Mmoja wa wanawake wale aliuchukua mkono wa kulia wa Tamara akauweka kichwani kwake. 

Tamara aliweza kulishika sikio lake la kushoto.

Waliamua kwamba wakati ulikuwa umefika wa Tamara kuanza kuhudhuria shule. 

Angeanza kwenda shule iliyokuwa karibu na nyumbani kwao.

Tamara alifurahi sana akawaza, "Nitajua kusoma na kuandika kama Nashipae na Tasieku wafanyavyo."

------------------------------------------------------------



Katika eneo la Sirani paliishi familia ya watu wanne.

Baba, Mama na mapacha wao wawili, Baraka na Njoroge.

Familia hiyo iliishi kwa amani na upendo. Walishirikiana kufanya kazi.

Baba na mapacha walilima shambani. Mama naye alifanya usafi wa nyumba na kuchota maji.

Siku moja Mama yao aliwaita Baraka na Njoroge awatume dukani kununua sukari.

Bila kupoteza muda walielekea dukani.

Walinunua sukari na kuanza kurudi nyumbani. 

Walitumia njia ya mkato inayopita kwenye vichaka ili waweze kufika nyumbani kwa haraka.

Walipofika katikati, walimwona kifaru akija. Walipatwa na hofu kubwa.

Baraka alimwambia Njoroge apande juu ya mti. Naye alilala chini na kutulia kama maiti.

Walitetemeka sana.

Kifaru alipomwona Baraka amelala, alimnusa nusa. Akidhani kuwa si hai, alienda zake kichakani.

Hakumuona Njoroge aliyekuwa juu ya mti.

Njoroge alishuka kutoka mtini bado akiwa na hofu. Walichungulia alipokuwa ameenda yule kifaru lakini hawakumuona.

Walitimua mbio hadi nyumbani.

Mara tu walipofika nyumbani walisimulia wazazi wao kitendo hicho.

Waliapa ya kwamba hawatawahi kupitia njia za mkato tena.

------------------------------------------------------------



Rafiki zake Amani walikuwa na wanyama, wadudu, ndege au samaki vipenzi. 

Amani alitamani sana kuwa pia na mnyama kipenzi.

Aliamua kuwatembelea babu na nyanya yake ili wamshauri katika maamuzi yake.

Babu alimuonyesha picha za ndege tofauti na kumweleza ubora wao. Amani alitega masikio na kusikiliza.

Huyu ni kasuku. Ana rangi nyingi maridadi na unaweza kumfunza kuongea.

Chakula chake ni wadudu na nafaka na anahitaji nyumba ndogo sana. Unaweza kuiweka nyumba yake sebuleni.

Huyu ni jogoo. Ana rangi nyingi maridadi na anatufaa kwa nyama.

Anaweza kukuamsha asubuhi na mapema. Huwika alfajiri. Hula wadudu, majani na nafaka.

Huyu ni mbuni. Ni ndege mkubwa kuliko wote na chakula chake ni nafaka.

Anatufaa kwa nyama, ngozi na manyoya. Ukimfuga atahitaji chakula kingi, nyumba kubwa na uwanja mkubwa.

Huyu ni heroe. Chakula chake ni wadudu na samaki.
Ana rangi maridadi ya waridi na anapenda maji. 

Anatufaa kwa utalii. Huwezi kumfuga bila kibali maalumu.

Huyu ni njiwa. Chakula chake ni nafaka, wadudu na majani. 

Anatufaa kwa nyama. Ni ndege mpole na anahitaji nyumba ndogo tu. Ni rahisi kumtunza.

Huyu ni bata-maji. Ana rangi nyeupe maridadi.
Anapenda kuishi karibu na maji.

Ni mkali na anaweza kuwatisha watu. Ukimfuga utahitaji kidimbwi cha maji.

Huyu ni kunguru. Ana rangi nyeusi na chakula chake ni wadudu na matunda.

Utahitaji kibali maalumu kumfuga.

Huyu ni kanga. Ana madoadoa ya kupendeza. 
Chakula chake ni wadudu, nafaka na majani.

Ana nyama tamu sana na anatufaa pia kwa mayai.
Huishi nje na anahitaji nyumba ndogo tu.

Huyu ni bundi. Chakula chake ni panya na wanyama wengine wadogo.

Anapenda kufanya kazi yake usiku na ana macho makubwa ya kuona mbali. Waafrika wengi huamini huleta bahati mbaya.

Huyu ni tausi na ana rangi nyingi maridadi. Anajulikana kwa maringo yake.

Chakula chake ni nafaka na wadudu. Utahitaji nyumba kubwa na uwanja kumfuga.

Huyu ni kuku. Chakula chake ni nafaka. Hutufaa kwa mayai na nyama. Ni mpole na mahitaji yake ni maji, majani na nafaka.

Anahitaji nyumba ndogo na uwanja wa kuchakura.

Baada ya babu kumweleza ndege tofauti, Amani alisema, "Asante sana babu. Nitamchagua kuku, nitamlisha nafaka, naye atanipa mayai."

"Uamuzi mwema," babu akampongeza.

------------------------------------------------------------



Sungura alikuwa amelala chini ya mtofaa. 

Tofaa lilianguka chini kutoka tawi moja.

Sungura aliisikia sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura, kimbia!' 

Sungura aliamka, na bila kukawia, akaanza kukimbia mbio sana.

Sungura alikutana na Kuku. "Mbona unakimbia?" Kuku alimwuliza. 

Sungura akamjibu, "Sijui. Nilisikia tu kitu kikianguka nayo sauti ikasema, 'Kimbia, Sungura kimbia!'"

Kuku alishituka akaanza kukimbia aliposikia maneno aliyosema Sungura.

Walikutana na Mbwa akawauliza, "Kwa nini mnakimbia?" 

Kuku akamjibu, "Sijui. Nilisikia Sungura akipiga makelele naye hajui. Alisikia kitu kikianguka na sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura kimbia!'"

Mbwa akashangaa akaanza kukimbia pamoja na Sungura na Kuku.

Walikutana na Farasi akawauliza, "Mbona mnakimbia?" 

Mbwa akamjibu, "Sijui. Nilisikia Kuku akisema hajui na wala Sungura hajui. Sungura alisikia kitu kikianguka na sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura kimbia!'"

Farasi naye akaanza kukimbia pamoja na Sungura, Mbwa na Kuku.

Walikutana na Punda akawauliza, "Kwa nini mnakimbia?" 

Farasi alimjibu, "Sijui. Nilimsikia Mbwa akisema hajui. Yeye alimsikia Kuku ambaye hajui. Kuku naye alimsikia Sungura ambaye pia hajui. Sungura alisikia tu kitu kikianguka na sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura, kimbia!'"

Basi Punda pia akaanza kukimbia pamoja na Sungura, Mbwa, Kuku na Farasi.

Walikutana na Ng'ombe akawauliza, "Kwa nini mnakimbia?" 

Punda alimjibu, "Sijui. Nilisikia alivyosema Farasi, naye hajui. Yeye alisikia Mbwa na Mbwa hajui. Alimsikia Kuku naye Kuku hajui. Alimsikia Sungura naye pia hajui. Sungura alisikia kitu kikianguka na sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura, kimbia!'"

Ng'ombe akapata wasiwasi na akaanza kukimbia pamoja na Sungura, Mbwa, Kuku, Farasi na Punda.

Walikutana na Paka akawauliza, "Kwa nini mnakimbia?" 

Ng'ombe alijibu, "Sijui. Nilisikia tu alivyosema Punda naye hajui. Yeye alimsikia Farasi naye Farasi hajui. Alimsikia Mbwa ambaye hajui. Yeye alimsikia Kuku na Kuku hajui. Kuku alimsikia Sungura ambaye hajui ila alisikia kitu kikianguka na sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura, kimbia!'"

Paka naye akaanza kukimbia pamoja na wanyama wengine.

Walikutana na mvulana aliyekuwa amepanda baiskeli. Mvulana aliwauliza, "Mbona nyote mnakimbia?" 

Wanyama walimjibu, "Hatujui. Tulimsikia Sungura alivyosema naye hajui. Alisikia kitu kikianguka na sauti ikisema, 'Kimbia, Sungura, kimbia!'"

Mvulana yule aliangua kicheko akasema, "Upepo uliangusha tofaa. Mimi ndiye nilisema, 'Kimbia, Sungura kimbia!'"

------------------------------------------------------------



Amara alikuwa na umri wa miaka tisa. Alisomea shule ya msingi ya Kerema. Masomo aliyoyaenzi mno ni Kiingereza, Sayansi na Masomo ya Jamii. 

Alitaka kuwa wakili atakapokuwa mkubwa. Amara aliwapenda wanyama sana.

Amara aliishi na mama yake, Margi. Alikuwa mkulima mwenye bidii. 

Baba yake Amara aliaga dunia alipokuwa na umri wa miaka mitano.

Wakati Amara hakuwa shuleni, alichukua muda wake kuwa na Mbisi, mbuzi. 

Alimsafisha na kumlisha.

Amara pia alikuwa na bembeleza wake, Simba. Mama yake hakuwapenda mbwa sana lakini alimruhusu Amara kumweka Simba. 

Endapo Simba angemsumbua, angefoka, "Ondoka kabla sijakupiga teke." Amara alihuzunika.

Jumamosi moja, walikuwa na wageni kutoka kwa kikundi cha akina mama. 

Amara alifurahi kuwa rafiki za mama yake walikuwa wamekuja na watoto wao. Wangecheza kandanda.

Mama yake alikuwa ameandaa chakula ambacho kikundi kilipenda. 

Amara alikumbushwa na mamaye kumfungia Simba. Aliwabwekea wageni.

Amara hakumfungia Simba vizuri. Wageni walishangaa kumwona mbwa chumbani. Mama Oto aliuliza, "Kwa nini mnamruhusu mbwa kuingia ndani ya nyumba?" 

Mama alimwita Amara aje amtoe Simba nje.

Amara hakusikia mama yake akimwita kwa sababu walikuwa na shughuli za kucheza.

Amara alipoenda ndani ya nyumba, alimwita Simba nje. Simba alikuwa mtiifu sana kwa Amara. 

Baada ya mlo, wageni walisema, "Tutawatunza pia mbwa wetu vizuri kama Amara. Tunawatesa ilhali wanatusaidia sana."

Baadaye, mama alimwomba Amara radhi kwa kuwa mchoyo na katili kwa Simba. Amara alifurahi kwa kuwa mwishowe mama yake alimkubali mbwa wake. 

Amara anapokuwa shuleni mama yake humlisha Simba. Rafiki za mama yake wamejifunza kuwa wazuri kwa mbwa wao.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na mwanamume mrefu sana.

Jembe lake lilikuwa fupi mno.

Mlango wake ulikuwa mfupi mno.

Kitanda chake kilikuwa kifupi mno.

Baisikeli yake ilikuwa fupi mno.

Mwanamume huyu alikuwa mrefu zaidi ya vifaa vyote.

Aliamua kurekebisha vifaa vyake.

Aliutengeneza mpini wa jembe mrefu sana.

Akazitengeneza fremu refu za mlango.

Akakitengeneza kitanda kirefu sana.

Kisha akainunua baiskikeli iliyokuwa refu mno.

Akaketi juu ya kiti kilichokuwa juu sana. 

Akala kwa kutumia uma iliyokuwa refu mno.

Aliamua kuhamia katika msitu mkubwa. 

Akaishi kwa miaka mingi.

------------------------------------------------------------



Ilikuwa siku yenye joto jingi.

Siafu Mdogo hakuwa amepata maji kwa siku nyingi.

Akawaza, "Ninahitaji tone moja tu la maji, hata kama litatoka kwenye jani."

Umande wote ulikuwa umekauka.

Hangepata hata tone moja la moja.

Siafu Mdogo akalia sana, "Nisipokunywa maji,  nitakufa. Lazima niufikie mto nilioelezwa."

"Ati mtoni? Huko utakufa maji!" Kichakuro mmoja mwenye hekima alimwonya.

Lakini, Siafu Mdogo hakujali. Kiu chake kiliongezeka. 

"Nitakufa iwapo sitakunywa maji sasa."

Siafu Mdogo alienda kuutafuta mto alioambiwa juu yake.

Alipitia kwenye nyasi na matawi yaliyokauka.

Mara akasikia mngurumo wa mawimbi.

Siafu Mdogo alifika mtoni akayanywa maji baridi.

Alifurahi kukata kiu na hakuliona wimbi kubwa likija.

Siafu Mdogo alijaribu kujishikilia kwenye nyasi kavu zilizokuwa zikielea. 

Lakini, alisombwa na maji.

Siafu Mdogo alilia, "Jamani, nisaidieni."

Njiwa Mweupe alikuja akamnyooshea tawi. Akasema,  "Panda juu ya tawi haraka."

Siafu Mdogo aliruka juu ya tawi na Njiwa Mweupe akamwokoa.

Siafu Mdogo akasema, "Siondoki kabla sijamshukuru Njiwa. Nitasubiri hadi atakaporejea kunywa maji."

Siku moja alipokuwa akimsubiri Njiwa Mweupe, Jona na Petro walikuja mtoni. 

Walikuwa wamebeba manati.

"Yule Njiwa Mweupe ambaye huja hapa kunywa maji,  tutamla jioni," Jona akawaza.

Jona na Petro walijificha nyuma ya mimea kando ya mto.

"Sitakubali wajanja hao wamuue yule Njiwa Mweupe. Lakini nitafanyaje? Mimi ni mdogo sana," Siafu aliwaza.

Wakati huo huo Njiwa Mweupe aliruka kutoka mtini anywe maji.

Jona na Petro walipima shabaha na kungoja kwa hamu.

Siafu Mdogo alipata wazo.

Aliurukia mguu wa Petro na kumuuma.

Petro aliruka juu akalia kwa uchungu, "Waaa!" 

Aliyaachilia manati yake yakaanguka.

Njiwa Mweupe alishtuka akaondoka.

Hivyo ndivyo Siafu Mdogo alivyomwokoa Njiwa Mweupe.

------------------------------------------------------------



Bibi alianza, “Sungura na Tembo walikuwa marafiki tena majirani.”

Sungura alipenda uyoga lakini alikuwa mvivu sana. Hakulima.

Sungura hakupata uyoga. 

Alianza kuiba ndizi za Tembo.

Tembo aliimba, “Nitamshika mwizi!” 

Sungura aliogopa.

Kima alimchungia Tembo shamba lake.
 
Lakini, Sungura hakuiba.

Tembo alienda kutazama.
 
Sungura alijificha ndani ya matawi ya maboga.

Tembo aliangalia kila mahali. 

Hakumpata mwizi.

Siku nyingine, Sungura alijificha ndani ya boga kubwa.

Tembo aliliona hilo boga kubwa akalimeza.

Boga lilisonga tumboni mwa Tembo.

Tembo alilitema boga.
 
Sungura alitoka ndani akatoroka.

Bibi alisema, “Na huo ndio mwisho wa hadithi.”

------------------------------------------------------------



Mbwa

Bata

Ng'ombe

Punda

Panya

Paka

Kondoo

Mbuzi

Nguruwe

Kuku



------------------------------------------------------------



Kobani alikuwa mwanamume mrefu sana. Wanakijiji walimwita Kobani, Muungwana, kwa sababu alikuwa mpole na rafiki wa watu. Hakuwa kama watu wengine wakubwa tunaosoma juu yao katika hadithi za kutisha. 

Wakati wa mchana, Kobani alifanya kazi yake shambani. Mpini wa jembe lake ulikuwa mfupi mno kwa hivyo alilazimika kuinama hadi chini kuifanya kazi yake. Bila shaka, mgongo wake ulikuwa na maumivu mengi kutokana na kuinama kwingi.

Theuri aliishi karibu na Kobani. Alihuzunika sana alipomwona Kobani akipambana na jembe lake lenye mpini mfupi au alipoinama chini ili apite mlangoni kwake. 

Theuri aliamua kumsaidia Kobani. Alizungumza na wazee wa kijiji na kuwauliza usaidizi. Lakini, kabla wao kufanya hivyo, walitaka kujua urefu kamili wa Kobani.

Theuri alimwuliza Kobani, "Wewe ni mrefu kiasi gani?" Kobani alikisia akasema, "Nadhani urefu wangu ni mita 2.5." Kobani alilala kitandani halafu akamweleza, "Ninajua godoro langu ni refu mita 1.5. Unaona hata miguu yangu inaning'inia mwisho karibu mita nyingine. Hiyo ina maana kuwa mimi ni mrefu mita 2.5."

Sasa Theuri angeweza kuwaeleza wazee kwamba Kobani ni mrefu mita 2.5. Alikuwa mrefu kweli!

Theuri angeweza kuanza kutekeleza mpango wake wa siri. 

Theuri, Kobani na Choke, kipenzi chake, waliondoka kwenda sokoni. Waliitumia baiskeli ya Kobani iliyokuwa ndogo. Kobani alilazimika kuunyoosha mguu wake ili aweze kuiendesha ile baiskeli. Theuri aliketi kikapuni akiogopa kutazama barabara namna baiskeli ilivyoyumbayumba kila upande.

Waliposhuka sokoni, umati wa wanakijiji ulimzunguka Kobani. Chifu wa kijiji alimkaribisha. "Hujambo Bwana Muungwana. Theuri alitueleza kuwa unakumbwa na matatizo maishani mwako kutokana na urefu wako," Chifu alisema. 

Aliendelea kumwambia, "Tunataka kukusaidia. Tutahakikisha kuwa kila kitu unachohitaji kinakufaa. Hivi karibuni, matatizo yako yatazikwa katika kaburi la sahau. Subiri tu ujionee."

Wanakijiji walifanya kazi mfululizo kuhakikisha kuwa chochote Kobani alihitaji kilikuwa kimetengenezwa kwa kimo kilichomfaa.

Litazame jembe hili. Ulinganishe mpini wa jembe jipya na ule mzee. Mpini mpya unaonekana kuwa mrefu mara mbili. Unadhani hilo jembe jipya ni refu kiasi gani? Zaidi ya mita moja? Chini ya mita mbili?

Baadaye, wanakijiji walimsaidia Kobani kutengeneza fremu refu na mlango mpya uliokuwa mrefu. Fremu ilikuwa ndefu kumliko Kobani ili asiiname sana atakapokuwa akiingia nyumbani. Ilikuwa ya kumfaa hasa!

Hebu ichunguze ile picha kwa makini. Urefu wa Kobani ni takriban mita 2.5. Je, unadhani fremu ya mlango wake mpya ni refu kiasi gani?

Halafu walitengeneza kitanda kipya na godoro lililokuwa refu zaidi. Vilevile walinunua shuka na blanketi ya kuufunika mwili wa Kobani kutoka kichwani hadi miguuni. 

Sasa, Kobani angetazamia kulala usingizi kwa amani. Miguu yake haitaning'inia kando ya godoro tena. Tazama jinsi mwili wake ulivyofunikwa kabisa. Hata kuna nafasi iliyobaki upande mmoja wa kitanda.

Chifu alimwuliza mmoja wa wahunzi wa mle kijijini
kumtengenezea Kobani baiskeli kubwa. Baiskeli hiyo ilikuwa na kikapu kikubwa ambamo Theuri na Choke wangeketi. 

Kila sehemu ya baiskeli hiyo ilikuwa kimo cha kumfaa Kobani. Kobani hakuhitajika tena kuikokota miguu yake barabarani wala kuining'iniza kando ya baiskeli.

Maseremala walimtengenezea Kobani meza mpya iliyokuwa na miguu mirefu ya mita 1.5. Sasa anapoketi kula, miguu yake inagusa chini. 

Theuri huketi kwenye kigoda kirefu karibu naye. Yeye huhitaji ngazi ili afike juu. Hesabu vidato ambavyo Theuri anastihili kupanda ili amfikie Kobani. Je, unadhani ngazi hiyo ni refu kiasi gani?

Jembe jipya la Kobani humwezesha kupanda mimea na kuvuna kwa urahisi. Bustani yake ilibadilika na kuwa msitu! Kobani huwaachia wanakijiji vikapu vya matunda mbele ya mlango wa nyumba yake kuonyesha shukuruni zake kwa msaada wao. 

Na hili lilianza na ndoto aliyokuwa nayo Theuri ya kutaka kumrahisishia maisha rafiki yake, Kobani Muungwana.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, paka na panya walikuwa marafiki. Walifanya kazi na kucheza pamoja. 

Walioana na kuishi kwa furaha.

Siku moja, panya walisema kwa hofu, "Baadhi ya jamaa zetu wamepotea." 

"Sijamwona mjomba kwa muda," mmoja alisema. 
"Sijamwona shangazi," alisema mwingine. 

"Dadangu hayuko," alisema wa tatu. "Kakangu yuko wapi?" aliuliza wa nne.

Panya mmoja mzee alitikisa kichwa chake kwa huzuni akasema, "Marafiki wapendwa, nina habari mbaya. Paka wanatula. Ni lazima tuwe waangalifu. Hivi karibuni watatula sisi sote."

Panya waliingiwa na woga mwingi. Panya wa kike waliwaambia watoto wao, "Msiende nje. Kuweni waangalifu paka wasije wakawashika."

Panya wote walikuwa waangalifu sasa. 

Walikaa katika mashimo yao na wala hawakwenda nje.

Sasa paka walikuwa na wasiwasi pia. Walisema, "Je,  panya wote wamekwenda wapi? Tunahisi njaa na hatuna chochote cha kula." 

"Wamejificha," paka mkubwa alisema. "Tunawezaje kuwakamata?"

Paka mwingine alisema, "Tutawauliza tupange ndoa kati yao nasi. Sherehe ya harusi itawaleta panya pamoja. Nasi tutawashika wote wakati mmoja tuwale!" 

"Hilo ni wazo zuri sana," paka walisema.

Basi, paka waliwatuma wazee wao kwenda kuwaona panya. 

"Tungependa tuwe na ndoa kati ya mmoja wa binti zenu na mmoja wa wavulana wetu," paka wazee waliwaambia panya.

Panya walisema, "Hatuwaamini. Mnataka kutula tu." 

Paka walijibu, "La! Sisi ni waaminifu na wenye mioyo safi. Tunataka tuwe marafiki. Hapo zamani wengine wetu waliwala, lakini hilo halifanyiki tena. Hatutawahi kuwala tena."

Panya walipowatazama paka, waliona kuwa wote walikuwa wakitabasamu. "Tumekubali ndoa ifanyike kati ya mmoja wa binti zetu na mmoja wa mvulana wenu," panya walisema.

Paka walienda nyumbani kwa furaha. 

"Siku ya harusi itakuwa nzuri sana," walisema huku wakilamba midomo yao.

Siku ya harusi, panya walikuwa bado na wasiwasi mwingi. "Kaeni karibu na mashimo yenu," waliwaonya wanao. 

"Tazameni, paka wanakuja. Iwapo watakuwa wazuri kwetu, tutakuwa wazuri kwao. Lakini wakijaribu kutula, tutakuwa tayari kutoroka."

Paka walitokezea barabarani wakiimba wimbo wa harusi.

"Je, unayasikia maneno ya wimbo huo wanaoimba?" Panya mzee alimwuliza panya mchanga. 

"Ndiyo," panya mchanga alijibu. Wimbo ulisema, "Washikeni muwale wote! Washikeni muwale wote!"

"Basi ni lazima tuimbe pia," alisema panya mzee. 

Akaanza kuimba, "Kimbieni panya, kimbieni! Kimbieni panya, kimbieni!" 

Panya wote waliruka ndani ya mashimo yao wakajificha.

Paka waliwasili wakaulizana, "Je, yuko wapi Bi. Harusi?" 

Panya mzee alichomoza kichwa chake kutoka shimoni akawajibu, "Tumepata funzo. Maadui zako wakijifanya kuwa marafiki, ni lazima uwe tayari kutoroka."

------------------------------------------------------------



Kuna duka ndogo karibu na nyumba yangu.



Mmiliki wa duka hilo ni mwanamume mwembamba mwenye sauti ndogo.



Nje kuna joto.

Ninakwenda kwenye friji.

Ninapata kinywaji cha stroberi.



Ninampatia mwanamume huyo mwembamba pesa zangu.



Kisha, ninafungua kinywaji changu cha stroberi na kuanza kunywa.



Kinywaji hicho baridi cha stroberi kina ladha tamu sana!

------------------------------------------------------------



Fana na familia yake wanaishi katika mji wa Debre Birhan nchini Ethiopia. Fana ni mwanafunzi wa darasa la tatu. Ana roho nzuri na mwenye hekima.

Fana anawapenda wanyama. Ana paka mmoja, kuku wawili, mbuzi na njiwa. Anakuwa nao kwa muda mrefu akiwalisha na kucheza nao.

Siku moja, Fana na wenzake walikuwa wakicheza uwanjani shuleni. Fana aliwaona watoto wakiwarushia njiwa mawe. 

Alijiuliza, "Mbona wanawaumiza njiwa?"

Aliacha kucheza akakimbia kuelekea mahali watoto wale walikokuwa. 

Mwanzoni, wenzake hawakuelewa kilichokuwa kikitendeka. Walimfuata. Fana aliwakemea wale watoto, "Acheni kurusha mawe."

Wale watoto watukutu walitoroka. 

Fana aliwashika njiwa waliojeruhiwa. Aliona majeraha kwenye mbawa zao. Aliamua kuwapeleka nyumbani kuwalinda.

Fana aliwalisha njiwa. Jioni aliisimulia familia yake alichokiona na kufanya siku ile na jinsi alivyowaokoa njiwa.

Asubuhi, Fana na wazazi wake welienda katika kliniki kupata dawa za kuwaponya njiwa. 

Baada ya siku chache, njiwa walipona majeraha yao. Fana alifurahi sana.

Kila mara, Fana aliwaambia marafiki zake, "Ninawapenda wanyama. Wanyama wana manufaa kwetu na ni marafiki zetu. Lazima tuwalinde na kuwahifadhi."

------------------------------------------------------------



Mara hii familia yangu iliamua kuzuru mji wa Kisumu na kuliona ziwa la Victoria. 

Kutoka mji mkuu wa Nairobi mpaka Kisumu ni kama kilomita 425 kwa gari.

Ziwa la Victoria linamilikiwa na nchi tatu: Kenya, Uganda na Tanzania.

Ziwa hili limezingirwa na Bonde Kuu la Ufa.

Kuna samaki wengi, kwa hivyo, tuliweza kuwaona wanawake na wanaume wakivua samaki.

Wanawake waliingia majini na kuvua kwa kuwatega kwa mitego midogo.

Wanawake hutumia mitego kama hii na kuwashika samaki wengi wadogo. 

Huwapika samaki hao na kulisha jamii zao.

Wanaume hutumia mashua kuvua. 

Kwa hivyo, huweza kuwavua samaki wakubwa kuliko kina mama.

Tuliwaona wavuvi wakiwaleta samaki ukingoni mwa ziwa. 

Samaki mkubwa ambaye hupatikana katika ziwa hili ni mbuta. 

Tuliyemwona alikuwa na uzito wa kilo 140 na urefu wa  mita 1.8.

Pia tuliweza kupata wanyama kama mamba na kiboko. 

Hawa wanyama wawili ni hatari sana kwa maisha ya watu. Watu kiasi hupoteza maisha yao wanaposhambuliwa.

Hivi karibuni ziwa limevamiwa na gugu linaloenea na kufunika maji.

Wataalamu wanajaribu kutatua janga hili.

Ziwa hili ni muhimu kwa nchi nyingi kwani ndio mwanzo wa mto mrefu zaidi duniani.

Mto wa Nile umeanza katika ziwa hili na kwenda mpaka Misri. Niliweza kwenda mahali mto huu unapoanzia.

Baadaye, tuliwauliza wenyeji pahali pazuri pa kupata lishe. Tuliekezwa kwenye Hoteli Kiboko iliyoko ukingoni mwa ziwa. 

Tulikula samaki wa kukaangwa, ugali, sukuma wiki, kachumbari na biriani. Tamu sana!

Hata kama nilihuzunika kuona ziwa lilivyoharibiwa na gugu, nilifurahia safari yangu.

Zoezi

1. Kutoka Nairobi mpaka Ziwa la Victoria ni kilomita ngapi?

2. Ziwa la Victoria linamilikiwa na nchi tatu: _________, ________ na ___________.

3.Ni samaki gani mkubwa anayepatikana katika ziwa hili?

4. Ni mto gani maarufu duniani unaoanza kutoka hapa?

5. Ni Wanyama gani hatari wanaopatikana hapa?

------------------------------------------------------------



Mimi ninapenda kusoma.

Nitamsomea nani?

Lena amelala.

Nitamsomea nani?

Mama na bibi wanapika.

Ni nani nitakayemsomea?

Baba na mjomba wanarekebisha gari.

Nitamsomea nani? Nitasoma kitabu mimi mwenyewe!

Maswali: 1. Mtoto anapotafuta mtu wa kumsomea,  anamkuta nani kwanza? 2. Kwa nini hawezi kuwasomea mama na bibi? 3. Baba na mjomba wanafanya nini? 4. Je,  wewe unapenda kusoma vitabu vya aina gani?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, watu hawakujua chochote. Hawakujua kupanda mimea, kushona nguo, wala kuuunda vyombo vya chuma. 

Lakini mungu wa hekima, aliimiliki hekima yote ambayo watu walihitaji. 

Alihifadhi hekima hiyo kwenye chungu cha udongo.

Siku moja, mungu wa hekima aliamua kumpa Buibui Anansi chungu hicho kilichojaa ujuzi na hekima. 

Buibui Anansi alikitazama chungu kile. Na kila alipokitazama alipata kujua jambo jipya. 

Alifuarahi sana.

Anansi alisema, "Nitakificha chungu hiki juu ya mti mrefu ili mtu mwingine asikifikie. Ningetaka kufaidika peke yangu." 

Alitengeneza kamba akaifungia kwenye chungu. Alijifunga kamba hiyo kiunoni akaukwea mti chungu kikining'inia mbele yake. Haikuwa rahisi kwani chungu kile kilimgonga magotini.

Wakati huo wote, mwanawe Anansi alikuwa chini ya ule mti akimtazama babake. Hatimaye, alimwuliza, "Baba, mbona usikifunge chungu mgongoni ili uweze kuukwea mti?" 

Anansi aliamua kukifunga mgongoni chungu hicho kilichojaa hekima. Ilikuwa rahisi zaidi kukibeba kile chungu mgongoni.

Baada ya muda mfupi, alifika juu ya mti. 

Akiwa juu aliwaza, "Mimi ndiye ninabeba hekima lakini,  mwanangu anaonekana kuwa mwerevu kuniliko." 

Buibui Anansi alikasirika na kukitupa chini kile chungu.

Chungu kilianguka na kuvunjika vigae vingi. 

Watu waliipata hekima wakajua kulima, kushona nguo, na kuunda vyombo vya chuma. 

Hivyo ndivyo watu walijua kufanya mambo yote wanayofanya.

------------------------------------------------------------



Mama, Baba na Lina wanaongea kuhusu kukaa katika hali nzuri ya kiafya.

Lina aliuliza shuleni, "Kwa nini tuioshe mikono yetu?"

Mwalimu alisema, "Mikono yetu ina viini, lakini hamwezi kuviona."

"Viini ni viumbe vidogo sana. Tunahitaji darubini kuviona."

Lina alitazama kwenye darubini.

Aliviona viini vilivyotoka mkono wake.

"Virusi na bakteria ni viini.

Viini vinaweza kutuambukiza ugonjwa."

"Kuosha mikono kunaweza kuzuia virusi na bakteria kuenea," Mwalimu anasema.

Baba anatengeneza kifaa cha kuosha mikona bila mfereji.

Lina anauliza, "Kifaa hiki kinatumikaje?"

"Kipande cha mbao kinainamisha mtungi kisha maji yanamwagika nje."

"Osha kwa sabuni na maji. Polepole, hesabu hadi 20 unapoosha."

"Baba, wewe mwerevu! Sasa, unaweza kuwasalimu watu kutumia kiwiko chako?"

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na msichana aliyeitwa Kalabushe. 

Alipenda kuongea sana.

Siku moja, shangazi yake alikuwa mgonjwa.

Aliishi peke yake.

Mama aliporudi jioni alisema, "Kalabushe, mpelekee shangazi yako chakula."

Kalabushe alikutana na fisi. 

Alikuwa amebadilika kuwa mtu.

Fisi alimwuliza alichobeba. 

Kalabushe alijibu, "Nyama, mayai na maziwa."

Fisi alitamani nyama. Alilamba midomo yake.

Alipanga jinsi ya kuipata.

Fisi alikimbia mbele ya Kalabushe. 

Aliingia kwa shangazi akajificha.

Alimmeza shangazi kisha akajifunika blanketi lake. 

Akamsubiri Kalabushe.

Kalabuse alipofika, aliita, "Shangazi, uko wapi?"

Shangazi hakumjibu.

Kalabushe alimwona mtu aliyejifunika blanketi.

Alitaka kujua.

Aliuliza, "Shangazi, mbona masikio yako ni makubwa?"

"Ili nikusikie."

Aliuliza tena, "Shangazi, mbona macho yako ni makubwa?"

"Ili nikuone."

"Shangazi, mbona mdomo wako ni mkubwa?" 

Papo hapo, Fisi alimmeza.

Kalabushe aliendelea kuuliza maswali akiwa mle tumboni.

Fisi alichoshwa na maswali ya Kalabushe. 

Alimtema nje.

Kalabushe na shangazi waliokolewa na wanakijiji.

Kalabushe alipata funzo.

------------------------------------------------------------



Ninaweza kuutumia kukimbia.

Ninaweza kuruka nao.

Ninaweza kucheza nao.

Ninaweza kuogelea nao.

Ninaweza kuruka kamba nao.

Ninaweza kupiga nao.

Ninaweza kuhepa nao.

Lakini siwezi kupaa angani nao.

------------------------------------------------------------



Naka na Nala wanafanya kazi katika bustani yao. Wanapanda mboga.

"Kwa nini tunafanya kazi kwa bidii kwenye jua?" Nala anashusha pumzi.

"Tunafanya kazi kwa bidii kwa sababu tunapenda dunia yetu!" Naka anasema.

"Tukitunza dunia, dunia itatutunza sisi," anaongezea.

"Tunapanda mboga ili tuweze kula vyakula vyenye afya," Naka anasema.

"Kupanda mboga zetu wenyewe kunaweza pia kutuokolea pesa," Nala anaongeza.

"Ulikuwa ukisema nini kuhusu dunia? Niambie Zaidi?" Nala anauliza.

Naka anasema, "Hebu tuketi, na nitakuambia mengi kuhusu dunia yetu."

Naka anaanza, "Dunia ni sayari ya duara tunamoishi. 

Takriban watu bilioni nane wanaishi hapa! Dunia inazunguka jua."

"Dunia imeundwa kwa ardhi, hewa, na maji.

Sayari yetu inachemka ndani kwa joto. Viumbe hai huishi  juu ya dunia," Naka anaeleza.

Nala anakatiza, "Kwa nini tusianguke kutoka duniani?" 

"Nguvu ya mvuto inatushikilia hapa. Nguvu hii hutuvuta kuelekea kwenye sayari," Naka anajibu.

"Tunawezaje kutunza dunia?" Nala anauliza.

Naka anamjibu, "Tusiichafue dunia. Tunapaswa kuchakata na kupunguza taka zetu."

Naka anaendelea, "Tuchakate plastiki, karatasi, glasi na makopo. 

Inawezekana kutengeneza vitu vipya kutoka kwa nyenzo zilizochakatwa. Tunatupa vitu vingi sana."

Naka anatamatisha, "Lazima tutunze dunia kwa sababu binadamu wanaihitaji kuwa hai."

Nala atangaza, "Tunafaa kurudi kazini!"

Maswali

1. Nala na Naka wafanya nini? Kwa nini?

2. Andika mambo 4 ya kweli kuhusu sayari yetu.

3. Kwa nini tunafaa kuitunza dunia?

4. 'Kuchakata' vitu ina maana gani?

5. Nini kinaweza kuchakatwa? Orodhesha mifano.

6. Nini lingine tunaweza kufanya kulinda dunia?

------------------------------------------------------------



Unyayo

Mguu

Goti

Kiuno

Tumbo

Kifua

Viganja

Mikono

Kiwiko

Kichwa

------------------------------------------------------------



Nguo ya dada yangu ni kubwa sana kwangu!

Sweta ya kaka yangu pia ni kubwa sana kwangu.

Mkoba wangu ni mkubwa.

Lakini, si mkubwa sana!

Mshipi huu ni mdogo mno kwangu.

Kofia hii ni ya mwanasesere wangu.

Soksi zangu zinanitosha vizuri.

Lakini, ni rangi mbaya!

Hivi ni vyatu vyangu vipya.

Vinanitosha vizuri.

------------------------------------------------------------



Sebule

Chumba cha kulia

Chumba cha kulala

Bafu

Jiko

Dirisha

Mlango

Meza

Kiti

Bustani

------------------------------------------------------------



Katika mji fulani, kulikuwa na duka nadhifu la viatu vya bei ghali.

Ni katika mji huu ndimo nilizaliwa.

Watu wengi walikuja kwenye duka hilo la viatu, lakini ni wachache tu walioweza kununua viatu hivyo vya mapambo.

Siku moja, mwanamume tajiri mwenye miguu mikubwa alilitembelea duka lile.

Aliziweka pesa zake kwenye kaunta.

Kisha, akiwa ameiweka mikono yake mifukoni, alitembea juu na chini akiviangalia viatu.

Aliponikaribia, nilikosa pumzi na kuganda.

Aliinyosha mikono yake na kunikamata.

Aliketi na kuanza kunivaa kwenye miguu.

Alikuwa na miguu mikubwa, na harufu ilikaribia kunikosesha pumzi!

Nilipakiwa kwenye sanduku.

Tulienda nyumbani, akaniweka kwenye kabati.

Alinivaa kila siku.

Nilimfanya akawa nadhifu na akatembea kwa ujasiri.

Nilikuwa na maisha magumu. Kwa kuwa alikuwa mvivu, hakuiosha miguu yake!

Kwa upande wangu, nilimng'ata wakati mwingine, na kumfanya achechemee.

Mwishowe, nilizeeka na kuvunjika, nikawa na makovu na nyufa.

Aliniweka nje, karibu na pipa la takataka.

Mtu mwingine alinipeleka kwenye karakana ya ngozi ili nichakatwe. 

Huko, nilitengenezwa mkoba mpya uliometameta. 

Nilianza maisha mapya.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na mvulana mmoja kwa jina Abeli. Alijitengenezea rukwama. Abeli hakuwa na dereva wa rukwama yake mpya. 

Akamwambia Meri dada yake, "Nataka dereva wa rukwama yangu. Tafadhali nipe mwanasesere wako. Anaweza kuketi ndani ya rukwama."

Lakini Meri akasema, "Hapana, namtaka mwanasesere wangu." Wakati Meri hakumkubali amchukue mwanasesere, Abeli alikasirika sana. 

Alimnyakua mwanasesere na kumvuta. Meri alivuta mkono mwingine wa mwanasesere. Abeli alivuta na Meri akavuta. Mkono wa mwanasesere ukang'oka!

Meri akalia na kukimbia kwa mama yake. "Angalia mama," akasema, "Abeli alivuta mkono wa mwanasesere wangu na ukang'oka. Alitaka mwanasesere wangu aketi ndani ya rukwama yake mpya lakini nilitaka kucheza naye." 

Mama yake akasema, "Abeli hakufanya tabia nzuri."

Mama akawaza jinsi ya kumfunza mwanawe  kutogusa vitu vya dadake vya kuchezea. 

Alikuwa na wazo. Alikwenda kwa rafiki yake ambaye alikuwa daktari na kumwambia, "Tafadhali, nisaidie." Daktari akajibu, "Naweza kukusaidia namna gnai, rafiki yangu?"

Mama akajibu, "Mwanangu Abeli ana tabia mbaya sana siku hizi. Aling'oa mkono wa mwanasesere wa dadake. Hastahili kufanya hivyo. 

Kesho nitamwambia akuletee huyo mwanasesere umrudishe mkono tena."

"Tafadhali mwambie Abeli kuwa lazima akulipe kwa kazi yako. Hana pesa zozote, kwa hivyo utamwambia asafishe gari lako kubwa zee ambalo huwa na vumbi kila wakati," mama akasema. 

Rafiki yake alicheka na kusema, "Ee-ee! Hilo litakuwa jambo zuri."

Mamake Abeli akarudi kwake nyumbani. Akamwuliza Abeli, ''Unapokuwa mgonjwa au kuwa na maumivu, wewe huenda wapi?" Abeli akajibu, "Wakati mimi ni mgonjwa au nikiwa na maumivu, lazima niende kwa daktari." 

Mama akasema, "Ulimwumiza mwanasesere, sasa ni sharti umpeleke kwa daktari."

Kwa hivyo Abeli alimpeleka mwanasesere kwa daktari. "Huyu mwanasesere ameumia vibaya sana. Mama yangu aliniambia nimlete kwako. Daktari, unaweza kumpa mkono mpya?" 

Daktari alikubali kumtunza mwanasesere. Aliweza kutengeneza mkono mpya.

Daktari akamwambia Abeli, "Mwanasesere ana mkono mpya. Lazima unilipe. Una pesa ngapi?" 

Abeli akajibu, "Tafadhali daktari, sina fedha zozote. Siwezi kukulipa kwa kazi yako."

Daktari akasema, "Vizuri! Huna fedha zozote? Gari langu kubwa ni chafu mno! Lisafishe na hivyo ndivyo utakavyonilipa." 

Abeli akachukua ndoo ya maji na kitambaa safi. Ilichukua muda mrefu sana kusafisha gari hilo chafu.

Kisha Abeli akamrudishia Meri mwanasesere wake. Alifurahi sana na kumwambia Abeli, "Wewe ni ndugu mzuri. Asante sana kwa kumtengeneza mwanasesere wangu." 

"Dadangu, pole kwa kukasirika na kukuhuzunisha," akasema Abeli.

Tangu siku hiyo, Abeli hakuchukua vitu vya dadake tena. Na akajaribu sana ili asikasirishwe naye.

Abeli alikumbuka muda aliouchukua kusafisha gari lile kubwa, chafu la daktari. Akaamua haikufaa kukasirika na kuvunja vitu.

------------------------------------------------------------



Walifunga mashule na kututuma nyumbani.

Hatuwezi kucheza na watoto wengine.

Nakosa kuwa na marafiki zangu.

Nakosa kwenda shule.

Mama ana wasiwasi kuhusu mjomba.

Mjomba amelazwa hospitalini.

Wazazi wetu wana wasiwasi kuhusu kila kitu.

Kila mtu ana kiwewe kuhusu kupata ugonjwa kutokana na virusi hivi.

Kila tunachosikia kinahusu virusi vya korona!

Nina hamu ingeondoka!

------------------------------------------------------------



Akrabu

Bundi

Chura

Duma

Emu

Fisi

Gogota

Hua

Inzi

Jogoo

Kasuku

Linksi

Mbuzi

Nyani

Orangutan

Paka

Ruba

Simba

Tembo

Uduvi

Vifaranga

Wadudu

Yangeyange

Zebu

------------------------------------------------------------



Tembo mmoja anaenda kunywa maji.

Twiga wawili wanakaribia kunywa maji.

Nyati watatu na ndege wanne pia wanaenda kunywa maji.

Swala watano na nguruwe mwitu sita wanafika mahali kuna maji.

Pundamilia saba wanakimbia kwenda kunywa maji.

Chura wanane na samaki tisa wanaogelea majini.

Simba mmoja ananguruma. Anataka kunywa maji. 

Ni nani anamwogopa simba?

Tembo mmoja na simba mmoja wanakunywa maji pamoja.

------------------------------------------------------------



Watu wanaishi katika nyumba aina tofauti. Baadhi ya watu wanaishi katika nyumba zilizojengwa kudumu kwa muda mrefu. Wengine wanaishi katika nyumba za muda ambazo hazidumu kwa muda mrefu.

Kitabu hiki kinahusu makazi ya muda yanayoitwa manyata, ambayo yanajumuisha vyumba vya kitamaduni.

Manyatta hii ipo kaskazini ya kati ya Kenya, katika Kaunti ya Samburu. Sidai na Naeku ambao ni dada, wanashiriki chumba kimoja, na wazazi wao na kaka yao mdogo wanashiriki kingine.

Mjomba wao na kaka zao watatu wakubwa wanakaa kwenye vyumba vingine, pamoja na familia zao.

Familia hizi hulisha mifugo wao pamoja na kusaidiana. Hawakai sehemu moja kwa muda mrefu. Wanahama hama kutafuta maeneo mapya ya malisho ya mifugo wao.

Kando ya manyatta kuna uzio wa matawi ya miiba. Uzio huu unawazuia mifugo wasitoke nje na watu wasiojulikana kuingia ndani.

"Tunaanza mchakato wa ujenzi kwa kukusanya vifaa kutoka kwenye mazingira yetu. Tunakusanya matawi ya miti ya kujenga muundo wa msingi wa chumba,"  Sidai anasema.

Naeku anaongeza, "Tunajua jinsi ya kutumia vifaa vya asili kujenga nyumba zetu. Kila mtu katika manyatta anasaidia katika ujenzi."

Tunatumia matawi makubwa kutengeneza fremu imara ya kuta. Tunafunga fremu ya paa kwenye fremu ya kuta kwa kutumia mizizi, na hivyo kutengeneza fremu thabiti kwa chumba chote," Sidai anaelezea.

"Vyumba vina paa za chini, na hivyo ni vigumu kwa upepo kuvipindua," Naeku anaongeza.

Sidai anaendelea, "Mara tu fremu ya chumba inapokuwa imesimama, tunashonea matawi membamba kati ya matawi makubwa."

Naeku anaongeza, "Tunatengeneza tabaka nene za nyasi na kuzifunga kwenye fremu ya paa. Hii inaitwa kuezeka." "Kuezeka vizuri kunatulinda kutokana na mvua na jua," anaongeza Sidai.

Sidai anaongeza, "Paa za vyumba vyetu zinaweza nyooka au kuwa mviringo."

Naeku anasema, "Kupaka tope ni sehemu ya ujenzi ninayopenda zaidi. Tunachanganya matope na samadi ya ng'ombe kutengeneza plasta. Tunapaka plasta hii kwenye fremu ya kuta, tukijaza nafasi zilizopo. Hii huzuia upepo na mchanga kuingia."

Sidai anaendelea, "Kupaka plasta kwenye kuta kunaziba kuta hizo mara tu zinapokauka. Pia tunapaka plasta juu ya kuta. Plasta iliyokauka ni ngumu na imara."

Naeku anaongeza, "Hakuna madirisha kwenye kuta, lakini chumba chetu kina mlango wa mbao."

"Upakaji wa plasta kwenye kuta husaidia kuhifadhi joto chumbani," anasema Sidai. "'Kuhifadhi joto' linamaanisha nini?" anauliza Naeku.

"Kuta za matope na samadi husaidia kuweka chumba kuwa baridi ndani wakati nje kuna joto. Katika msimu wa baridi, kuta zinasaidia kutuweka joto ndani kwa kuhifadhi joto la moto," anajibu dada yake.

"Watu wote katika manyatta wanashiriki katika ujenzi, na sote tunasaidia kuvunja vyumba tunapohama.

Sio vigumu kuvunja miundo na kutumia sehemu hizo tena mahali pengine," Sidai anaeleza.

"Vifaa vyetu vya ujenzi ni vyepesi, kwa hivyo ni rahisi kuvibeba. Tunatumia ngamia au punda kubeba vifaa vyote muhimu kutoka manyatta yetu ya zamani. Kwa mfano, paa lenye nyasi," anasema Sidai.

"Pia tunaweza kukusanya vifaa vingi zaidi vya ujenzi kutoka kwenye mazingira mapya," anaongeza Naeku.

"Nyumba yetu inatufaa tunavyoishi, ambayo ni kuhama hama na mifugo yetu," anasema Sidai.

"Kuhama hama kunamaanisha hatuwezi kwenda shule na marafiki zetu daima," anasema Naeku.

"Shule yetu inaturuhusu kuomba vitabu, na tunajaribu kufuatilia masomo yetu," anamalizia Sidai.

------------------------------------------------------------



Vifungo vyangu vyote ni duara.

Baadhi ya vifungo vyangu ni kijani kibichi.

Vifungo vyangu vyote ni vidogo.

Baadhi ya vifungo vyangu ni manjano.

Vifungo vyangu vyote in maridadi.

Baadhi ya vifungo vyangu ni vya rangi nyekundu.

Vifungo vyangu vyote vinameremeta.

Baadhi ya vifungo vyangu ni bluu.

Vifungo vyangu vyote ni vizuri.

Ninavipenda vifungo vyangu vyote.

------------------------------------------------------------



Penda kutoka mbali.

Usikaribie sana!

Piga chafya au kohoa ndani ya kiwiko chako.

Usitawanye viini vyako!

Kaa mbali na wengine ikiwa wewe ni mgonjwa.

Sabuni na maji huua virusi vya korona.

Nawa mikono mara kwa mara.

Nawa mikono kwa sekunde ishirini.

Amkua kwa kisugudi. 

Amkua kwa vidole vya miguu, au kwa kupunga mkono.

Vaa barakoa safi kila siku. 

Funika pua na mdomo.

Usivipatie virusi vya korona nafasi yoyote ya kusambaa.

------------------------------------------------------------



Ada anacheka kwa sababu alisikia hadithi ya kuchekesha.

Anatabasamu.

Ada anahisi nini?

Tisa anahisi hasira.

Ana mkunjo kipajini kwake.

Kwa nini amekasirika?

Yadoo anaogopa giza.

Kila mtu huhisi hofu wakati mwingine.

Lakini Yadoo anaweza kuomba msaada.

Chidu ana wasiwasi juu ya kazi yake ya shule.

Anaweza kumwambia mwalimu wake.

Anaweza kuomba msaada.

Lushan anacheza cheza!

Ni sawa kufanya mchezo wakati mwingine.

Ethuro anajisikia mwenye huzuni.

Ni sawa kulia.

Hisia huja na kwenda.

Yatoo amejawa na furaha.

Yeye amefurahi.

Hisia huja na kwenda.

Hadiza anahisi uvivu.

Anahitaji kupata kitu cha kufanya.

Ayoo ana hasira.

Amechanganyikiwa.

Hasira ni hisia ngumu.

Lizy amesisimka.

Je! Ni nini sababu ya msisimko wake?

Mama alitayarisha chakula akipendacho.

Zege alihisi usingizi.

Alikuwa amechoka sana.

"Lakini, 'kuhisi usingizi' ni hisia?" Effy anauliza.

Effy amechanganyikiwa!

Je! Unaweza kujibu swali lake?

Lempaa anahisi mshangao na mshtuko.

Alisikia uvumi fulani.

Ni ukweli?

Nelly ni mgonjwa.

Anahisi huzuni.

Anahitaji dawa na kupumzika ili ajisikie bora.

Selina anahisi kutosheka.

Amemaliza kazi zake za nyumbani.

Sasa anaweza kucheza.

Victor hana kazi leo.

Anamwonyesha Selina vidole viwili.

"Kazi nzuri, sasa hebu tucheze!" anasema.

------------------------------------------------------------



Feni alikuwa msichana mdogo aliyekimbia kama upepo.

Feni alipenda kucheka na alijaribu alivyoweza kutenda alivyoambiwa.

Leo ilikuwa Siku ya Michezo shuleni. 

Feni alicheza mpira wa miguu na kushindana kwenye mbio aina tatu.

Feni alipotoka shuleni, alitembea na rafiki yake Hawa kurejea nyumbani.

Hawa alimwambia Feni, "Wewe hukimbia kwa kasi!"

Feni aliwasili nyumbani na kumkuta mamake jikoni.

Feni akasema, "Habari ya jioni, Mama."

Mamake akajibu, "Jioni ni nzuri. Habari yako?"

Feni akasema, "Leo ilikuwa Siku ya Michezo shuleni, na nilikimbia kwa kasi. Ninahisi joto, uchovu na nina njaa sana."

Mama akacheka na kusema, "Mpendwa wangu Feni, ulizaliwa na miguu myepesi! Nitatayarisha mchuzi, na chakula cha jioni kitakuwa tayari hivi karibuni."

Mama aliweka mafuta katika chungu kikubwa na kukitia mekoni. Mafuta yalipopata moto, aliongeza vitunguu na saumu, akakoroga hadi vikawa laini.

Aliongeza pilipili, nyanya, maji kidogo na vipande sita vya nyama ya ng'ombe.

Mama akasema, "Feni, tafadhali nisaidie kukoroga mchuzi."

Feni akajibu, "Ndiyo, Mama."

Feni akakoroga mchuzi mara moja.

Akasema, "Mchuzi huu unanukia."

Feni akakoroga mchuzi mara mbili.

Akasema, "Mchuzi huu unanukia sana."

Feni akakoroga mchuzi mara tatu.

Akasema, "Mchuzi huu unanukia sana, sana."

Halafu Feni akamtazama mamake. Mama hakuwa akimwangalia. 

Alikuwa akikata mboga za majani kuongeza kwenye mchuzi.

Feni akachukua kipande kimoja cha nyama kutoka chunguni na kukila.

Feni akasema, "Mmm..."

Tena, Feni akamtazama mamake. Mama hakuwa akiangalia upande wake. 

Alikuwa akikata mbilingani kuongeza kwenye mchuzi.

Feni akachukua haraka kipande cha pili cha nyama kutoka chunguni na kukila.

Feni akasema, "Mmm... Mmm..."

Kwa mara nyingine, Feni alimtazama mamake. Mama alikuwa ameangalia upande mwingine. 

Alikuwa akikata dhania kuongeza kwenye mchuzi.

Kwa haraka, Feni akakichukua kipande cha tatu cha nyama kutoka chunguni na kukila!

Feni akasema, "Mmm... Mmm...Mmm..."

Wakati huo, Mama aliingia jikoni kuongeza mboga ya majani, mbilingani na dhania. 

Feni alikuwa bado ameushika mwiko.

Mama akatabasamu na kusema, "Feni, asante kwa kunisaidia kukoroga mchuzi."

Feni hakujua la kusema.

Mama akaongeza mboga ya majani, mbilingani na dhania kwenye mchuzi. 

Akauchukua mwiko na kuanza kukoroga mchuzi.

Mama akatazama chunguni. Akavitafuta vile vipande sita vya nyama chunguni.

"Kimoja...viwili...vitatu..." Akaviona vipande vitatu pekee vya nyama. Mama hakusema chochote. Feni hakusema chochote.

Mama alipopakua mchuzi, Feni hakupata nyama yoyote.

Feni akasema, "Nisamehe, Mama. Sitarudia tena." Na kweli, Feni hakurudia tena.

Na huo ukawa ndio mwisho wa jambo hilo.

------------------------------------------------------------



Yayeri anaamka mapema. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anashukuru kwa usiku uliopita. 

Tunauliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anatandika godoro vizuri. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anawasalimu babu na bibi. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anaosha uso wake. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anapiga meno yake mswaki. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anaoga. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anavaa sare ya shule. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anavaa viatu vyake vyeusi. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anafika shuleni mapema. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anasoma kwa bidii. 

Tunajiuliza, "Kwa nini Yayeri ni mashuhuri?"

Anacheza na wenzake. 

Unaelewa kwa nini Yayeri ni mashuhuri?

------------------------------------------------------------



Ariana yuko Amerika. 

Anataka kutembelea Kenya.

Barabarani, ataona kondoo.

Ataona bodaboda na tuktuk.

Ataona jamaa zake wa Kenya.

Jamaa zake watafanya sherehe kubwa.

Ariana atasherehekea na kufurahi nao.

Ariana atacheza na watoto wengine.

Akienda sokoni, ataona vitu vingi tofauti vikiuzwa.

Atawaona watu waliovalia mavazi tofuati.

Atakula matunda mengi sana.

Atakula machungwa, ndizi na mananasi.

Ariana atajaribu kupanda miti mrefu.

Hajawahi kufanya hivyo akiwa Amerika.

Atayaona mashamba yenye mimea tofauti.

Wakenya wengi ni wakulima.

Atatembelea mbuga za wanyama.

Atawaona wanyama wa porini kama simba, ndovu, twiga na punda milia.

Ataona wanyama wa kufugwa kama kuku, paka, mbuzi na njiwa.

Amerika, anafuga paka mmoja na mbwa mmoja.

Atashuhudia harusi kijijini.

Atawaona watu wakiimba na kucheza ngoma za kitamaduni.

Ataitembelea pwani ya Kenya.

Ataogelea katika bahari ya Hindi.

Jumapili, Ariana atajiunga na jamaa zake kwenda kanisani.

Ariana atafurahia sana kuitembelea Kenya.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na mti mkubwa katika bustani ndogo jijini. Wanyama wengi waliishi pamoja juu ya mti huo. Paliishi pia jamii ya vichakuro. 

Viki alikuwa mmoja wao na alipenda kuongea mambo makubwa. Binamuye, Kato kutoka Msitu wa Mbali, alikuwa amekuja kumtembelea.

Jioni moja, wanyama wote walioishi katika ile bustani ndogo walienda kulala. 

Mara walisikia sauti kubwa ikitoka kwenye uwanja uliokuwa karibu.

Kato na vichakuro wengine waliona mashine kubwa ya manjano. Waliona pia wanaume waliovalia kofia ngumu za manjano. Walikuwa wakionyesha kwa vidole ile bustani ndogo na nyumba zilizokuwa upande mwingine wa barabara. 

Walinuia kuzivunja vunja zote kisha wajenge uwanja wa kuegesha magari.

Watu walioishi pale wangehamia nyumba zingine. 

Lakini hakuna aliyefikiria juu ya wanyama, ndege na wadudu walioishi katika ile bustani ndogo.

Walioziona mashine hiyo kwanza walikuwa familia ya fugo, hasa Bwana Popules, mkubwa kwa umri. 

Naye alimwelezea Bi Mopules, ambaye alimwelezea mdogo wao, Pipules Mdogo.

Walipokuwa wachanga, waliitwa Pop, Mop na Pip.

Kulikiwa na vurumai, kukimbia kwingi, kuruka huku na huko bila yeyote kujua la kufanya. 

Wapi kwa kwenda? Watoto wa vipepeo walisema, "Hebu tutafute majani." Vipepeo wakasema, "Tunataka maua." 

Panya wadogo walitaka mashimo. Fugo walitaka kujilimia mashimo yao.

Vichakuro, ndege na wadudu walitaka miti, vichaka na nyasi. 

"Tutapata wapi hii yote? Bila shaka tutakufa," walisema kisha wakalia kwa uchungu."

Mjombake Kato na shangaziye walikuwa kimya sana na vichakuro wote wadogo walisonga karibu na mama yao. 

Kato alisafisha koo na kuanza kuongea huku akiona haya, "Naishi katika Msitu wa Mbali, labda tunaweza kwenda sote huko." 

Kulikuwa na sauti za mchangamko na mmoja akasema, "Vipi?"

Kato alikuna kichwa na kuwaza sana, "Sawa, 'Kichakuro ya Moja kwa Moja', inaweza kuwapeleka vichakuro na vipepeo, buibui, watoto wa vipepeo na wadudu wote. Ndege wanaweza kuruka au waje nasi. Fugo nao pamoja na panya wadogo na nyoka wanaweza kutumia 'Fugo ya Moja kwa Moja' ipitiayo chini kwa chini."

Kila mmoja alifikiria kuwa hilo lilikuwa wazo zuri kabisa.

Bwana Popules aliharakisha kumwuliza dereva wa treni ya moja kwa moja ya chini kwa chini ikiwa angeweza kuwabeba wote hadi Msitu wa Mbali. 

Dereva alibabaika, akagugumia kabla ya kusema, "Sawa." 

Sasa ilikuwa zamu ya Bwana Popules kuwa mwungwana. "Marafiki, hamna haja ya kuwa na wasiwasi."

Kwa hivyo, wakati wa saa za asubuhi, 'Kichakuro Moja kwa Moja' na treni aina ya 'Fugo ya chini kwa chini' pamoja na abiria wote, iliendesha safari yake ya kuelekea Msitu wa Mbali ulio na miti, maua,  vidimbwi na ardhi nyororo.

------------------------------------------------------------



Hapo kale, mfalme wa mwitu alikuwa Bwana Simba.

Aliwatuma wanyama kukomesha kelele zilizofanywa na vyura. 

Wanyama hao hawakufaulu.

Tembo alijitolea kukomesha kelele hizo. 

Aliwekwa nje kuwa mlinzi.

Usiku wa manane kelele ziliposikika, Tembo alianza kuwaua vyura. 

Alifanya hivyo siku iliyofuata.

Baadaye, Mfalme Simba alikuwa mwenye furaha. 

Tembo alikuwa amezikomesha kelele za vyura.

Baada ya mwezi mmoja, waliwaona wadudu wengi shambani mwao.

Mfalme Simba alimwuliza Tembo kuwaita vyura ili wale wadudu wale.

Tembo alijawa na hofu. Alikuwa amewaua vyura wote. 

Alisema, "Samahani, samahani, ni-li-waua wote!"

Mfalme Simba alimwambia Tembo, "Nilikutuma kukomesha kelele, wala sio kuwaua vyura." 

Tembo alifungwa gerezani kwa miaka mingi!

Mfalme aliwashauri wanyama wote, "Fuateni maagizo yangu kila wakati."

------------------------------------------------------------



Hapo kale, katika kijiji cha Katumbi, aliishi mwanamme aliyeitwa Kiundu. 

Alipenda sana kula nyama.

Mwanawe Chifu wa Katumbi alikuwa ametimu umri wa kuoa. 

Chifu aliwaalika wanakijiji harusini.

Kiundu alipata mwaliko wa harusi hii. 

Pia, alisikia kuwa kungekuwa na sherehe ya harusi katika kijiji cha Nyamani.

"Aaa! Sherehe mbili kwa siku moja! Lazima nihudhurie sherehe zote mbili," Kiundu aliwaza. 

"Nitaenda kwanza Nyamani kisha nirudi Katumbi," akaendelea kuwaza.

Kiundu alirauka mapema na kuelekea Nyamani. Alipofika Nyamani, sherehe ilikuwa haijaanza. 

"Nitarudi Katumbi, baadaye nirejee Nyamani," Kiundu aliamua.

Kiundu alirudi Katumbi. Alitarajia angekuta nyama zikiwa tayari. Baada ya safari ndefu, alihisi njaa sana. 

Alipofika Katumbi, chakula kilikuwa bado hakichakuwa tayari.

Kiundu akawaza, "Niliwaacha wapishi Nyamani wakijiandaa kupika. Chakula lazima kiwe tayari sasa." 

Kiundu aliamua kurudi Nyamani.

Kiundu alipofika Nyamani, watu walikuwa tayari wamekula. Wageni walikuwa wanawatuza zawadi maarusi. 

Kiundu alikuwa mchoyo na hakuwa ameleta zawadi. 

Alitaka kula tu.

Kiundu alikasirika alipokosa chakula. Mara moja,  aliamua kurudi kwao Katumbi. 

Kwa vile alikuwa mwenye njaa na mchovu, hangeweza kutembea haraka.

Alipowasili kwao Katumbi, wageni walikuwa wamemaliza kula chakula chote. 

Walikuwa wakiimba na kucheza kwa furaha.

Alipoambiwa kuwa chakula kilikuwa kimeisha, Kiundu alikasirika sana. 

Lo! Kiundu alizikosa nyama kwenye sherehe zote mbili.

Alitembea polepole akirudi nyumbani akiwa mwenye huzuni na njaa.

------------------------------------------------------------



Macho

Sikio

Mdomo

Pua

Kidevu

Meno

Ulimi

Mashavu

Kope

Nywele

------------------------------------------------------------



Mvua ilikuwa imenyesha kwa siku nyingi na watu walikuwa wemenuna, ila Samweli, aliyeamka kila asubuhi akitabasamu. 

Bibi alisema, "Eee, Samweli! Hilo tabasamu ni la ajabu! Je, ni kwa ajili yangu?"

Samweli alipiga makofi kisha akasema, "Lakini ni tabasamu langu, Bibi."

Mama alicheka. "Samweli! Tabasamu ni kitu unachoweza kupatiana bila kupotesa. Tazama!"

Mama akamnyanyua na kumupandisha mpaka kwenye kioo. Tabasamu lake lilikuwa wazi na la kuangaza kama hapo awali.

Ikafika saa ya kuondoka. Mama akafunga koti la Samweli la mvua mpaka juu. Wakaingia kwenye mvua kuelekea maktabani.

Rafiki mmoja wa Samweli aliitwa Zawadi. Alikuwa amesimama dirishani akitazama mvua bila furaha.

Samweli akahisi tabasamu likipanda ndani mwake, kisha likaruka na kuvuka bustani hadi kwa Zawadi.

Zawadi alishikilia lile tabasamu kwani lilikuwa na thamani sana asingaliruhusu liondoke. Samweli alipotembea kuelekea maktabani, aliisikia kengele mlangoni kwa Zawadi. Mtu wa barua alikuwa akimletea Zawadi barua kutoka kwa binamu yake mpendwa.

Zawadi alifurahi sana mpaka tabasamu lake likapanda juu na kumwangaza mtu yule aliyeleta barua. "Asante sana Bwana!" alisema.

Tabasamu la Zawadi lilikuwa kitu muhimu sana alichokuwa ameona mwanamume yule asubuhi nzima. Lilimpa joto alipotembea kwenye mvua.

Akafika kwenye jumba kubwa. Nyuma ya lango, kulikuwa mbwa aliyekuwa akizunguka zunguka na kubweka mfululizo. Ukali wake ulimfanya mtu yule atabasamu.

Mbwa alinyamaza kubweka. Alitega masikio na kutikisa mkia wake kisha aligeuka na kukimbia kwenda nyumbani kwa furaha.

Mzee mkongwe alifungua mlango. "Aa, la! Huwezi kuingia. Umeloa maji!" mzee alimwambia mbwa wake. Lakini, mara moja, tabasamu likamwangaza yule mzee.

Mzee alisimama wima kidogo. "Eee, nani anajali ikiwa kunanyesha? Twende matembezi, rafiki yangu!" 

Wakaenda wakiruka vitimbwi vya maji. Kwenye kivuko, palikuwa na polisi wa trafiki wa kike. Alihisi baridi na kusononeka. 

Mzee huyo alijua la kufanya, "Hujambo Bi Makabela!" alisema, kisha akatabasamu. Lakini, Makabela hakutabasamu hata kidogo.

Kusimama siku nyingi kwenye mvua kunaweza kufanya uso kuhuzunika sana. 

Lakini tabasamu ni kitu cha ajabu, na kwa sasa, tabasamu la Bi Makabela lilikuwa kubwa, la kuangaza, na ilikuwa vigumu kulifungia ndani. 

Halikufanya kazi mara moja, lakini kidogo kidogo, lilianza kutambaa hadi, mwishowe!

Tabasamu kubwa na la ajabu liliuangaza uso wa Makabela!

Kengele ya shule ilisikika, na watoto walikimbia kuvuka barabara. Bi Makabela aliiweka alama yake, kisha akatabasamu, akatabasamu, akimlenga kila mtoto.

Watoto walitabasamu walipowaona mama na baba zao, bibi zao, shangazi zao na kaka na dada zao. 

Walitabasamu walipomwona dereva wa basi na muuza mboga, na Mama Makau, ambaye alitabasamu alipomwona mumewe, naye alitabasamu mbele ya meya. 

Tabasamu ziliruka na kung'ara na kung'aa mpaka kila MTU akatabasamu na kuchekacheka na kucheka kwa sauti ya juu kwenye mvua.

Katika maktaba, kila kitu kilikuwa kimya isipokuwa sauti ya mvua. 

"Ni wakati wa kwenda," mama Samweli alisema, huku akifunga kitabu chake. 

"Ndiyo, mama!" Samweli alisema akiwa ameishiwa na tabasamu.

Lakini walipoingia kwenye barabara, ilikuwa ajabu ilioje! 

Kila mtu kutoka mjini alikuwepo! Kila mtu! Na WOTE walikuwa wakitabasamu!

Tabasamu zilizunguka na kumlenga Samweli. Zilimpasha joto, na kumfurahisha, na kumpaa juu, juu, kutoka kwenye vidole vyake vya miguu hadi JUU ya kichwa chake. Alijawa na furaha kiasi kwamba tabasamu lilipasuka, nyororo na kung'aa. 

Na kitu kimoja kilibadilika. Alasiri ya giza na mvua haikuonekana kuwa giza tena. Je, inaweza kuwa? NDIYO! Mawingu yaligawanyika, na jua kali likaangaza juu yao, na tabasamu kubwa zaidi, angavu zaidi kuliko yote.

------------------------------------------------------------



Mimi na dinosau wangu tunawatazama 
ndege angani.

Mimi na ndege wangu tunamkuta sokwe mtini.

Ninacheza na sokwe na twiga wangu milimani.

Nyani anamwogopa kobe.

Mimi, kima na nyani wangu tunakula ndizi kila siku.

Nyani wangu na kima wanamwogopa kobe.

Mimi na Kobe tunaenda nyumbani polepole pamoja na nyoka.

Mimi na Nyoka twapenda kusonya na kuimba nyimbo kando ya ziwa.

Mimi na familia yangu nzima tunaishi pamoja kwa furaha kubwa!

------------------------------------------------------------



Jumamosi moja, mama alisema, "Brenda, Maria na Lona, nendeni mcheze!"

Waliondoka mbio pamoja.

Lona alisema, "Twendeni mtoni tukaogelee." 

Brenda alijibu, "Mama alitukataza kuogelea mtoni."

Walifika mtoni wakavua viatu na nguo. 

Wakacheza majini kwa muda.

Walicheka na kushangilia. 

Walifurahia maji baridi.

Baadaye, Maria alisema, "Tuogelee zaidi. Mama hatajua."

Lona na Brenda walikubali wakaendelea kuogelea.

Walipomaliza, hawakuziona nguo zao popote. 

Walianza kuhisi baridi.

Hawakuzipata nguo zao popote. 

"Tutamwambia mama nini?" Waliulizana.

Brenda alisema, "Lo! Ng'ombe anakula shati la Lona."

Lona alianza kulia.

"Mwingine anakula sketi yangu!" Maria pia alilia.

Walisema, "Mama, ng'ombe walikula nguo zetu." 

Hawakusahau adhabu aliyowapa.

Maswali: 1.Taja majina ya watoto wote watatu tunaokutana nao katika hadithi hii. 2. Kwa mujibu wa Brenda, Mama aliwakataza watoto kufanya nini? 3. Watoto walihisije walipomaliza kuogelea? 4. Unafikiri watoto hawa walikuwa wamewahi kuogelea katika mto huo? Toa sababu kwa jibu lako. 5. Unafikiri watoto hawa walipewa adhabu gani?

------------------------------------------------------------



Tazama wanyama.

Ng'ombe anasema,  "Moo."

Mbuzi anasema,  "Meee,  meee."

Farasi anasema, "Nei."

Nguruwe anasema, "Ghuranti."

Kuku anasema, "Ko ko. Ko ko."

Mbwa anasema, "Bwa. Bwa."

Mkulima anasema, "Kimya."

------------------------------------------------------------



Safari yetu ilianza alasiri. Tulipanda gari moshi saa tisa kwenda mji wa kitalii wa Voi, Kaunti ya Taita Taveta.

Kituo cha gari moshi kilipendeza na kilikuwa na mikahawa kadhaa ambapo tulipata vitafunio.

Kulikuwa pia na ukumbi mkubwa ambamo wote tuliketi na kujipumzisha.

Gari moshi lilivuka mandhari ya kupendeza ya mbuga ya kitaifa ya Tsavo. Tuliona ngiri, paa, dik dik, kanga, nyani, pundamilia na kikundi cha mbwa mwitu.

Ilitusisimua sana. Tulijua kwamba kulikuwa na mengi zaidi tutakayoona tulipokuwa tukitulia kwenye hoteli huo usiku.

Tuliraukia mandhari yaliyopendeza ya milima iliyozingira mji. Gari la kutalii lilituchukua kutoka kwenye hoteli yetu na tukaondoka.

Tuliweza hata kuona mlima wa Kilimanjaro tulivyoanza kuingia kwenye nyika iliyokauka na kua na vumbi.

Kwanza, tuliwasili kwenye uwanja uliokuwa wazi ambapo tulimuona kifaru akiwa pekee yake.

Tulipomsongelea, alitahadhari, akatuangalia kwa umakini. Kisha, polepole, aligeuka na kuanza kutembea akielekea kwenye dimbwi lililojaa tope.

Kiongozi wetu alituelezea kuwa vifaru wanapenda kijipaka matope. Hiyo inaondoa wadudu kwenye ngozi zao. Pia inawakinga kutokana na joto la jua na kuwaweka baridi. 

Kifaru huyo mkubwa aliingia mzima kwenye kidimbwi hicho cha tope na kuzama ndani polepole. Ilionekana kumridhisha sana.

Tuliendelea, tukakutana na wanyama mbalimbali wadogo. Kisha, kulikuwa na kundi kubwa la nyati.

Ndama wa hao nyati walisimama chini ya mama zao. Kiongozi wetu akatuambia kua hiyo ndiyo njia yao ya kujikinga kutokana na jua na pia kujificha ili wasionekane na wawindaji.

Nyati hao walikuwa wanakula nyasi iliyopendeza ya hudhurungi. Walitafuna kwa uvivu kwa kile kilichoonekana kama mwendo wa polepole sana.

Walionekana kuburudika sana. Pembe za nyati zinaweza kuwa na upana kadri ya urefu wa mtu mzima.

Mngurumo mkubwa ulisikika. Ghafla, fujo ikazuka kwenye kikundi. Ng'ambo nyingine, tukaona vumbi na wanyama wakikimbilia kila upande.

Ilikuwa taswira ya kuvutia! Simba dume mkubwa alimrukia nyumbu. Kiongozi wetu alituambia kuwa tulichoshuhudia ni nadra sana kwani ni simba jike ndio huwinda kwa niaba ya kikundi.

Shirika la huduma ya wanyamapori lilikuwa linafanya sensa ya wanyama wote. Helikopta za kijani zilipita angani zikiwa zimebeba walinzi pori na wanasayansi wakikusanya data.

Sensa inafanyika baada ya kila miaka mitatu ili kudhibitisha idadi ya wanyamapori.

Simba aliburuta mzoga chini ya mti wa acacia.

Chui aliketi kwa tawi la mti bila kuonekana rahisi. Alitazama kwa macho ya kutisha.

"Chui ni mwindaji wa faragha na akikutana na wenzake lazima kuwe na vita," kiongozi wetu alisema.

Ilikuwa alasiri na wanyama wengi walikusanyika karibu na vidimbwi vya maji ili kukata kiu na kucheza.

Ndovu wakubwa walikunywa maji na kujinyunyizia mengine ili kuondoa joto mwilini. Walipendeza sana.

Tulimaliza zaidi ya saa moja tukiwaangalia bila hata kuchoka.

Jua lilikuwa linatua nyuma ya milima tulipokuwa tukielekea kwenye lango la mbuga ili tufike kabla ya giza kuingia. Wageni hawaruhusiwi ndani ya mbuga usiku.

Tuliwaacha wanyama nyuma. Ilikuwa siku ya kupendeza sana!

Upesi tulikuwa tushafika kwenye lango la mbuga la Sala, lililo karibu na mji wa pwani wa Malindi.

Tulikuwa tumepanga kulala Malindi kabla ya kusafiri kurudi nyumbani.

1. Taja wanyama wnaojulikana kama Watano Wakubwa.

2. Taja mbuga zilizomo nchini kwenu.

3. Mnyama yupi unayempenda zaidi? 

4. Je, sensa ni nini?

5. Mbona wageni hawaruhusiwi mbugani usiku?

------------------------------------------------------------



Kuni ya kahawia iliyopasukapasuka.

Mchoro wa simba wa kahawia.

Mkate laini wa kahawia.

Keki tamu za kahawia.

Viatu vizee vya kahawia.

Kifaru wa kahawia wa kumetameta.

Kofia ya kahawia iliyotengenezwa kutoka kwa ngozi ya kondoo.

Mbwa laini wa kahawia.

Udongo mchafu wa kahawia.

Ngozi majimaji ya kahawia.

Na hii ni nini? 

Uso safi katika kioo kichafu.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na mwanamume aliyekuwa na watoto wawili wa kiume.

Siku moja, aliwaita akawaambia, "Wanangu, mimi ninakaribia kufa. Ningependa kuwaona mkiwa nyumbani kwenu kabla ya kifo changu. 

Ninawapa mwezi mmoja ili muweze kulishughulikia jambo hili. Rudini hapa baada ya mwezi."

Wanawe hao wawili walitoka kwa kasi. 

Mwana wa kwanza alikwenda akakata miti akaanza kujijengea nyumba.

Naye mwana wa pili alikwenda akaanza kujenga uhusiano maalum na watu kutoka familia mbali mbali. 

Alichukuliwa na watu tofauti kama mtoto wao wa kupanga.

Baada ya mwezi mmoja, ndugu hao wawili walirudi kumwona baba yao. 

Baba yao alisema, "Je, mmeweza kujenga nyumba zenu?" 

Wote walimjibu, "Ndiyo, baba."

Baba alikwenda na mwanawe wa kwanza. Aliona kwamba mwanawe alikuwa amejenga nyumba nyingi. 

Alitembea nje ya kila nyumba, akiuliza, "Je, kuna mtu yeyote ndani ya nyumba hii?" 

Naye mwanawe alimjibu, "La, baba."

Waliitembelea kila nyumba na kila wakati baba alimwuliza mwanawe, "Je, kuna mtu yeyote kwenye nyumba hii?" 

Kila mara mwanawe alimjibu, "La, baba."

Hatimaye, baba alihisi njaa kwa sababu hakumpata mtu yeyote wa kumpa chakula. 

Alisema, "Sawa, twende nyumbani." 

Waliondoka wakaenda nyumbani.

Kaka wa pili aliwapeleka kwenye familia yake ya kwanza ya kupanga. Aliwajulisha kwa baba yake na kusema, "Hawa hapa ni baba na kaka zangu." 

Familia hii iliwapokea kwa furaha nyingi. Walichinja kondoo wakawatayarishia sherehe kubwa sana.

Kisha walikwenda kwa familia ya pili aliyokuwa amepanga. Aliwajulisha pia kama baba na kaka zake. 

Waliwafanyia sherehe nyingine kubwa.

Walikaribishwa katika kila familia ambako ndugu wa pili alikuwa amechukuliwa kama mwanao. 

Walikula wakashiba kisha wakaondoka wakarudi nyumbani.

Baba alisema, "Hivi ndivyo nilivyokusudia, nilipowaambia mjitengenezee nyumba. Kuwa nyumbani hakumaanishi kuwa na nyumba nyingi au nyumba za bei ghali. 

Bali, ni kuwa na upendo, urafiki na uhusiano mwema na watu wengine."

------------------------------------------------------------



Mama yangu alinipatia watoto wa mbwa wawili.

Walikuwa maridadi sana!

Niliamua kuwaita Kifalme na Jeusi.

Kifalme alikuwa wa rangi ya kahawia, na, alikuwa kama malkia.

Jeusi alikuwa mbwa mweusi maridadi mwenye manyoya marefu.

Nilizoea kuwatembeza kila siku baada ya kutoka shuleni.

Wakati mwingine niliwaosha peke yangu. 

Kifalme alipenda kutoroka!

Halafu, tulihama na kwenda kwenye ghorofa.

Mbwa hawakuruhusiwa huko.

Tuliwaachia binamu zangu Jeusi na Kifalme.

Asubuhi moja, niliamua kuwatembelea mbwa wangu.

Nilipata kuwa Jeusi alikuwa amepotea na Kifalme alikuwa mpweke.

Nilihisi vibaya sana moyoni mwangu.

------------------------------------------------------------



Nilisikia upepo. 

Ulivuma na kupita kwa kasi karibu na makao yetu.

Upepo huo ulikuwa mkali. 

Uliibandua tiara yangu kutoka mkononi.

Niliifuata tiara yangu.

Lakini, upepo huo mkali ulinisukuma mbali nayo.

Upepo huo uligeuka na kuwa dhoruba. 

Dhoruba hiyo iliienua tiara yangu juu zaidi.

Dhoruba hiyo ya kutisha, ilinimeza mzima mzima! 

Sikuweza kuona chochote wala kugusa chochote.

Niliikumbuka tiara  yangu nzuri. 

Ilikuwa wapi? 

Labda ilikuwa imenaswa mtini.

Au labda, ilikuwa bado inapeperuka hewani.

Mwishowe, dhoruba hiyo kali ilipunguka. 

Mimi nilikuwa bado ninazunguka.

Nilipotulia, nilitazama mahali nilipokuwa. 

Nilijiuliza, "Upepo ule mkali umeanda wapi?"

Sikuiona tiara  yangu nzuri popote. 

Sikuusikia tena upepo ukivuma.

Labda siku iliyofuata, ningeipata tiara yangu nzuri.

La muhimu kwangu ilikuwa kwenda zangu nyumbani,  mbali na upepo hatari.

------------------------------------------------------------



Akadeli alimbeba mtoto wake. 

Alikwenda msituni kuchuma matunda.

Alipata mti uliojaa matunda mabivu.

Akadeli alimlaza mtoto wake chini akapanda mti.

Jasusi mmoja kutoka kijiji jirani alipitia pale akamwona mtoto. 

Kwa mshangao, akajiuliza, "Mamake mtoto huyu yuko wapi?"

Jasusi yule alipochutama, sauti ya mikufu aliyoivaa shingoni mwake, ilimwamsha mtoto.

Alimwacha mtoto aichezee mikufu hiyo. 

Mtoto alicheza na kucheka.

Akadeli alitazama chini aone kilichomchekesha mtoto. 

Akamwona jasusi amechutama karibu na mtoto wake.

Hofu ilimwandama, akauangusha mfuko wake uliojaa matunda.

Jasusi yule alitazama juu akasema, "Usiogope. Ninacheza tu na mtoto wako mrembo."

Polepole, Akadeli akashuka kutoka mtini.

Jasusi akampa mtoto mkufu mmoja, akisema, "Hii ni zawadi yako."

Akamwambia Akadeli, "Mchukue mtoto na mkoba wako uende nyumbani. Mwambie mume wako ahamie sehemu yenye amani zaidi. Mtoto wako amenifanya nibadili nia."

------------------------------------------------------------



Ben anafuga wanyama.

Huyu ni ng'ombe. 

Anataka chakula.

Huyu ni mbuzi. 

Anakunywa maji.

Huyu ni farasi. 

Anakimbia.

Huyu ni nguruwe. 

Amemaliza chakula chake.

Huyu ni kuku. 

Ana vifaranga watatu.

Huyu ni mbwa. 

Anabweka sana.

Ben amebeba maziwa. 

Mbwa wake anataka maziwa.

------------------------------------------------------------



Nilipotimia umri wa miaka mitano, mjombangu alinipa zawadi ya mbwa mdogo wa wiki tatu! 

Siku aliyoniletea mbwa huyo, nilifurahi sana. Nilijua kuwa nilikuwa nimempata rafiki.

Nilipomweka chini, mjomba alinigeukia na kuniuliza,  "Utamwitaje?" Nilimwangalia mbwa wangu kisha nikasema, "Ataitwa KoKo." 

Mjombangu alishangaa sana akaniuliza, "Mbona unamwita Koko?" "Kwa sababu rangi yake ni kama kakao," nilimjibu.

Nilimwuliza mjomba iwapo Koko alizaliwa peke yake. 

Mjomba alisema kwamba alikuwa na nduguye aliyemfanana kabisa. Nilienda kumwona nduguye Koko.

Koko alipomwona nduguye, alichangamka sana. 

Wawili hao waliweka vichwa vyao pamoja kama waliokuwa wakiongea.

Nilimwuliza mjomba ikiwa ningeweza kuishi na Koko na nduguye. 

Alisema, "Ni sawa wewe kuwaweka wote wawili. Lakini lazima uwalinde vizuri." 

Kila jioni, nilicheza nao na kuwafanyisha mazoezi.

Miezi michache baadaye, Koko na nduguye walikuwa wamekua wakubwa. Walikuwa wenye nguvu na afya. 

Singeweza kuwachunga peke yangu tena.

Nilimwuliza mjomba kumrudisha nduguye Koko kwake. Koko alipoachwa peke yake, alihuzunika mno. 

Alikuwa kama anayeniuliza, "Kwa nini ulifanya hivyo?"

Koko alikoma kucheza. Wakati mwingine alikataa kwenda nami matembezini akipendelea tu kulala nje ya nyumba yetu. 

Wakati mwingine alikula chakula kidogo sana. Nilikuwa na wasiwasi. Nilijiuliza vipi ningeweza kumsaidia Koko?

Siku moja mjombangu alitutembelea. Niliposikia sauti yake, nilienda haraka nje. 

Kabla ya kumwona, nilisikia mbwa wakibweka.

Nyuma ya jikoni, Koko na nduguye walikuwa wakicheza!

Nilifurahi sana hadi sikujua nimkumbatie nani kwanza, Koko au mjombangu. 

Nilijua kwamba Koko angerejelea ile hali yake ya kwaida. Tungeanza tena kufanya mazoezi pamoja!

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, Sungura alikuwa rafiki mkubwa wa Kima mwenye rangi ya kijani kibichi.

Siku moja Sungura alisema, "Hebu twende matembezi tukatafute chakula." Kima alikubali, lakini ulikuwa mtego kwake!

Walienda katika shamba la mahindi na kuanza kula.

Sungura mwakili alikuwa amezungumza na mwenye shamba. 

Alitaka Kima ashikwe kuonyesha kuwa alikuwa mjinga.

Sungura mwakili alianza kupiga kelele, "Wezi! Wezi! Mahindi yako yameisha yote!" 

Kisha akaruka, akatoroka na kwenda zake.

Ghafla, wenyewe walifika na kumpata Kima akijaribu kutoroka. 

Kwa vile alikuwa na mkia mrefu, hakuweza kwenda kwa kasi.

Wenyewe walimfuata wakipiga kelele, "Simama! Simama! Tulikuona, wewe ni yule Kima mwizi."

Walimshika na kuanza kumpiga.

Hakuweza kustahimili uchungu kwa hivyo alisema, "Nilikuwa na rafiki yangu Sungura. Ni yeye aliyenialika."

Hata hivyo, wenyewe waliukata mkia wake na kumwambia, "Nenda kamwambie rafiki yako kuwa tuliukata mkia wako!"

Walipoondoka, Sungura alinyemelea na kuuchukua mkia wa Kima na kuupika. 

Kisha Sungura alimualika kima kwa chakula cha mchana.

Mwisho wa mlo Sungura alimwuliza Kima ikiwa alijua alichokula. 

Kima mjinga alijibu, "La, sijui!"

Sungura alimwambia kuwa alikuwa amekula mkia wake mwenyewe kisha akatoroka. 

Kutoka siku hiyo, walikuwa maadui!

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na panya wawili. 

Mmoja wao aliishi nyikani.

Panya mwingine aliishi katika nyumba.

Siku moja, panya aliyeishi katika nyumba alimwambia panya wa nyika, "Wewe chakula chako si kizuri, usingizi wako umejaa mang'amung'amu huku mvua ikikulowesha."

"Sisi tunalala fofofo katika nyumba za watemi. Tunakula vyakula vingi mno. Siku moja nitembelee ujionee fahari iliyopo," alisema panya wa nyumba. 

"Niko tayari usiku wa leo kama mrija unaosubiri kinywaji," akajibu panya wa nyika.

Wakati huo huo mwenye nyumba alikasirika ajabu akifoka matusi, "Panya hawa wanaokula chakula changu wataona cha mtema kuni!" 

Ndipo akawategea mtego uliojaa sukari.

Panya waliingia nyumbani kula vitamu vilivyokuwamo. 

Walikuwa wakicheka, "Chu. Chu. Chi. Chi. Che. Che!"

Walipoufikia mtego, panya wa nyumba alisema,  "Wacha nionje sukari. Tazama vitamu vitamu tunavyokula hapa."

Lakini kabla panya hajapata kugusa sukari, mtego ukamnasa kichwa. Pa! 

Macho yake yakabubujika kama mbilingani.

Panya wa nyika akamtazama akiwa ameduwaa. 

Akasema, "Heee rafiki yangu, kitamu kipi ulichokula kikayafanya macho yabubujike?"

Lakini panya wa nyumba alishindwa kujibu.

Panya wa nyika akaondoka akikejeli, "Du! Umekula vizuri. Mimi siviwezi vitamu hivyo unavyojivunia."

Kuwepo nyumbani kulikochakaa mradi kwako, ni bora kuliko kuwepo nyumbani kuzuri sana ilhali ni nyumba ya jirani yako.

------------------------------------------------------------



Mbuzi alikuwa mfalme wa wanyama na ndege.  

Aliita mkutano.

Mbuzi aliwaambia kwamba aliota ndoto. 

Wote walisikiliza.

Ndoto ilihusu njaa.  

"Tutafanyaje?" Paka aliuliza.

Kuku na Bata walisema, "Ni vyema sisi kuweka chakula kwa mfalme."

Mfalme Mbuzi alisema, "Mfunge yeyote atakayekataa kutii."

Wakati wa kumchagua mfalme mpya ulifika. 

Walimchagua Paka.

Mbuzi hakutaka Paka kuwa mfalme. 

"Mimi ndiye mfalme."

Mbuzi alikataa kupeleka chakula. 

Ng'ombe aliuliza, "Tutafanyaje?"

Wanyama na ndege walijadili pamoja. 

Walimkasirikia Mbuzi.

Mbwa alisema, "Nilikuwa naye wakati wote alipokuwa mfalme."

Kondoo akasema, "Niliwapatia watoto wake sufu yangu nyororo."

Nguruwe alilila, "Alipokuwa mfalme, nilimchungia bustani yake."

"Kwani Mbuzi alifikiri atakuwa mfalme milele?" Kondoo aliuliza.

Wanyama walikubaliana. 

Lazima Mbuzi apeleke chakula kwa mfalme Paka.

Walipomkuta Mbuzi, aliwaambia, "Nitakuwa mfalme wakati wote."

Wanyama walimjibu, "Tutakufunga tukupeleke kwa mfalme mpya."

Ng'ombe alimvuta Mbuzi kumpeleka kwa mfalme.  

Wengine walishangilia.

Hiyo ndiyo sababu mbuzi hukataa kusonga wanapovutwa.

------------------------------------------------------------



Mara nyingi, Chui alitaka kumshika Swara.

Swara naye alikuwa akitoroka kila alipomwona Chui.

Siku moja, Chui alimwambia Swara, "Ningependa tuwe marafiki. Unachokula, mimi sili. Hakuna sababu ya kuwa maadui."

Swara alikubali. Chui akasema, "Tule kiapo cha kutufanya marafiki. Atakayeasi, mtoto wake atakufa."

Walikula kiapo cha kuwafanya marafiki. 

Usiku, Swara alilala chini ya mti na Chui akalala juu ya mti katikati ya matawi.

Baada ya muda, Swara alinona na Chui alikonda.

Chui alitamani kumla Swara aliyenona. Akasema, "Sina haja na kiapo. Sina hata mtoto!"

Chui alimrukia Swara akajaribu kumshika. 

Lakini, hakuweza. Alinaswa kwenye matawi.

Swara alishtuka sana. Aliruka juu akaanza kulia, "Bee! Bee!"

Chui akamsihi, "Rafiki yangu, nisaidie. Tulikubaliana kuwa atakayevunja kiapo chetu, atampoteza mtoto wake."

Swara alimjibu, "Inaonekana kuwa wazazi wako ndio waliokula kiapo. Sasa wewe ndiwe utakayekufa."

------------------------------------------------------------



Huyu ni Neema.

Neema anashona.

Neema anashona sketi.

Neema anatumia uzi kushona.

Uzi umekwisha. Neema anahitaji kununua uzi zaidi.

Neema anahitaji pesa za kununua uzi. Je, atazipata pesa hizo wapi?

Neema anaona mti karibu.

Mti huo una matunda mabivu.

Matunda hayo ni mapapai.

Neema anatafuta kijiti.

Anatumia kijiti hicho kuangusha mapapai.

Neema anawasili sokoni.

Neema amebeba mapapai kwenye uteo.

Anataka kuuza mapapai hayo.

Mwanamume ananunua papai. Anampatia Neema pesa.

Neema anauza mapapai mengi. Pesa atakazopata atatumia kununua uzi.

Anaona ndizi sokoni.

Lakini, hanunui ndizi.

Anaona nyanya sokoni.

Lakini, hanunui nyanya.

Anaona kichujio sokoni.

Lakini, hanunui kichujio.

Anaona mkate sokoni.

Lakini, hanunui mkate.

Kisha Neema anamwona mwanamume.

Mwanamume huyo anauza uzi.

Neema ananunua uzi.

Neema amepata uzi aliotaka! Amefurahi sana.

Atamaliza kushona sketi yake kutumia uzi huo.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na Jimbi na Sungura. 

Walikuwa marafiki sana.

Usiku mmoja, Sungura aliitembelea familia ya Jimbi. 

Walifurahia kula chajio pamoja.

Walipolala, Sungura aligundua kitu fulani.  

Jimbi na familia yake walivificha vichwa vyao walipolala.

Jimbi na familia yake walilala fofofo. 

Lakini, Sungura hakulala usiku kucha.

Asubuhi walipoamka, Sungura alitaka kujua siri hiyo. 

Akauliza, "Ninyi huviweka vichwa vyenu wapi mnapolala?"

Jimbi, akitaka kumchezea shere Sungura, alimjibu, "Rafiki yangu, wakati wa kulala, sisi ndege huvikata vichwa vyetu ili tuweze kulala kwa starehe."

"Asubuhi tuamkapo, sisi huvirejesha vichwa vyetu mwilini," Jimbi aliendelea kueleza.

Sungura aliporudi nyumbani, aliwaelezea familia yake siri hiyo ya Jimbi. 

Sungura waliamua kuijaribu siri hiyo wao wenyewe! 

Unafikiri ni nini kilichotokea?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na mwanamume aliyeitwa Biantaka. Alikuwa na ng'ombe. 

Kila siku Biantaka alimlisha ng'ombe wake na kumpa maji. Alikuwa na chungu kidogo alichotumia kuchota maji.

Siku moja, Biantaka alimwendea jirani yake kumuomba chungu kikubwa ili akitumie kuchota maji. 

Jirani yake alikubali kumwazima Biantaka chungu kikubwa. Alisema, "Tatizo la jirani yangu ni tatizo langu."

Siku chache baadaye, Biantaka alienda kwa mfinyanzi akanunua chungu kidogo. 

Alipofika nyumbani, alikiweka ndani ya kile chungu kikubwa alichomuomba jirani yake.

Alijitwika chungu kikubwa kilichokuwa na kile kidogo ndani yake. 

Akaenda moja kwa moja hadi kwa jirani yake aliyemwazima.

Biantaka alimwambia, "Nimekurejeshea chungu chako ambacho kimezaa kingine." 

Jirani alishangaa kwamba chungu chake kilikuwa kimezaa chungu kingine. Alimpongeza Biantaka akisema, "Umebarikiwa sana."

Baada ya muda, Biantaka alirudi kwa jirani yake kumuomba chungu tena. 

Mara hii, kakuwa na nia nzuri.

Mwenye chungu alimsubiri Biantaka arejeshe chungu chake bila mafanikio. 

Mwishowe, alikwenda nyumbani kwa Biantaka akasema, "Nimekuja kukichukuwa chungu changu."

Biantaka alimwambia jirani yake, "Rafiki yangu, chungu chetu kilifariki. Nilikusudia kuja kukuletea ujumbe huo mbaya."

Kwa mshangao, Jirani aliruka juu. Uso wake ulianza kufura kwa hasira. 

Alipiga kelele akimkemea Biantaka, "Sijawahi kusikia kuwa chungu kinafariki!"

Biantaka alimjibu, "Rafiki yangu, lazima uyakubali mambo haya. Kila kitu kinachozaa lazima pia kifariki. Mimi pia nilihuzunika sana kufuatia kifo cha chungu chako kikubwa."

Jirani alifoka kwa hasira akaenda kortini kumshtaki Biantaka. 

Hakimu alisikiliza maelezo ya pande zote mbili. Aliamua kuwa jirani mwenye chungu ndiye aliyekuwa na makosa.

Hakimu alimwuliza, "Biantaka alipokwambia kuwa chungu chako kilizaa, ulikubali. Kwa hivyo unapaswa kukubali anaposema kwamba kila kiumbe hai kinachozaa lazima kifariki kwa kuwa anasema ukweli." 

Hivyo ndivyo hakimu alivyoamua kesi hiyo.

Jirani alitembea polepole kama konokono akarudi nyumbani. Alikuwa amekipoteza chungu chake kikubwa. 

Naye Biantaka alikuwa amekipata chungu kikubwa kwa kutumia ujanja wake.

------------------------------------------------------------



Wapi paka wangu?

Je,  yuko chini ya kitanda?

Yuko juu ya kabati?

Yuko nyuma ya sofa?

Yuko karibu na pipa la taka?

Yuko ndani ya kikapu?

Yuko nje?

Yuko hapa!

------------------------------------------------------------



Paka wangapi?

Paka sufuri 0.

Paka wangapi?

Paka mmoja 1.

Paka wangapi?

Paka wawili 2.

Paka wangapi?

Paka watatu 3.

Paka wangapi?

Paka wanne 4.

Paka wangapi?

Paka watano 5.

Paka wangapi?

Paka sita 6.

Paka wangapi?

Paka saba 7.

Paka wangapi?

Paka wanane 8.

Ni nini hiki tunachoona?

Mtoto wa paka amekwama mtini!

"Nitamuokoa!"

"Mama, tunaweza kumfuga paka mmoja zaidi!"

Paka wangapi?

Paka tisa 9.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani Sungura na Fisi walikuwa marafiki wa chanda na pete. 

Walifanya kazi na kucheza pamoja.

Siku moja, Sungura alisema, "Rafiki, tuanze kulima pamoja ili tuwe tajiri." 

"Ah, kweli, tunaweza kupanda vyakula vingi na kuviuza," Fisi alimjibu. 

"Lakini, tutapanda nini?" Sungura aliuliza.

Fisi alipendekeza wapande mahindi. Sungura alikubali kisha akamwambia Fisi kuwa wagawane majukumu. 

Sungura akasema, "Kazi yangu itakuwa kuwachunga ndege wasile mahindi." 

Fisi naye akasema kuwa kazi yake itakuwa kulima shamba, kupanda na kupalilia.

Fisi alinung'unika kwamba alikuwa amepewa kazi nyingi. Sungura alisema kuwa kazi ya kuwafukuza ndege ndiyo ngumu zaidi na ya muhimu. 

Alisema, "Kazi yangu si rahisi. Nitakwea miti na kuwafukuza ndege mchana na usiku. Wewe huwezi kufanya hivyo."

Fisi alikubaliana na Sungura. Alilima shamba peke yake. Baada ya kulima shamba lote, Fisi alipanda mahindi.

Ilikuwa kazi nyingi kweli!

Fisi alipokuwa akifanya kazi, Sungura aliketi na kuimba: 

Rafiki yangu ni mfanya kazi, mimi ni mwelekezi. Anafanya kazi kama trekta, mimi ni meneja. 
Udongo anaolima, milima anayolima, mbegu anazopanda, magugu anayokata, mahindi tunayovuna.

Mahindi yalistawi. Sungura aliimba kwa furaha huku akiwafukuza ndege. 

Kazi yake ilikuwa rahisi. Hakutoa jasho hata kidogo.

Walipokuwa tayari kuvuna, Sungura alimwambia Fisi, "Nitavuna kila kitu kinachomea juu ya udongo nawe utavuna kila kinachomea chini ya udongo." 

Fisi alidhani hilo lilikuwa wazo nzuri.

Sungura alimwambia Fisi, "Nitavuna yangu kwanza kisha wewe uvune yako." 

Sungura alivuna mahindi yote na kuyahifadhi kwake.

Fisi alienda kuvuna vitu vyote vilivyokuwa chini ya udongo. 

Hakupata mazao yoyote ila mizizi pekee.

Fisi aligundua kwamba alikuwa amedanganywa. Alirejea nyumbani kwa hasira na vikapu tupu. 

Alimwambia Sungura, "Hebu rafiki yangu tulime pamoja mara nyingine."

Fisi aliongeza kusema, "Mara hii nitavuna kila kinachomea juu ya ardhi nawe utavuna kila kinachomea chini ya ardhi." 

Sungura alikubali. Alisema kuwa badala ya kupanda mahindi ingekuwa heri kubadili na kupanda viazi.

Fisi pia alisizitiza kwamba mara hiyo wote watalima,  wapande na wavune pamoja. 

Sungura alikubali. Walifanya kazi shambani pamoja.

Viazi vilipokuwa tayari, Sungura alimwambia Fisi kuvuna vyote vilivyomea juu ya udongo. 

Fisi alipata majani ya viazi pekee. Alirudi nyumbani na vikapu tupu.

Sungura alivuna viazi vingi. Fisi alipoona mavuno ya Sungura, alimwuliza kwa hasira, "Mbona ulinidanganya?" 

Sungura alisema kuwa Fisi mwenyewe alichagua kuvuna vitu vilivyomea juu ya udongo.

Fisi alikasirika mno. Alimfukuza Sungura kutaka kulipiza kisasi. 

Sungura alikimbia kwa kasi na kwenda zake. Tangu siku hiyo, Sungura na Fisi ni maadui.

------------------------------------------------------------



Ulikuwa wakati wa wanyama kwenda kulala. 

Mmoja wao hakutii.

Mkulima alimwambia Piggy aende kulala. 

Piggy alikataa.

Mkulima alimwuliza Trasti Wip kumcharaza Piggy. 

Trasti Wip alikataa.

Moto Mkali alikataa kumteketeza Trasti Wip kwa kutotii.

Maji Safi hakumtii mkulima. 

Alikataa kumzima Moto Mkali.

Mkulima alimwuliza Ng'ombe Moo kunywa Maji Safi.

Ng'ombe Moo alisema, "Nitayanywa maji haya. Nina kiu."

Maji Safi alilia, "Usininywe. Nitamzima Moto Mkali."

Moto Mkali alipiga kelele, "La, hutanizima. Nitamteketeza Trasti Wip."

Trasti Wip alilia, "Tafadhali usiniteketeze. Nitamcharaza Piggy."

Piggy alisema kwa hasira, "Usinicharaze. Nitaingia chumbani."

Piggy aliingia chumbani tayari kulala.

------------------------------------------------------------



Ninajiuliza ikiwa kuna mimi mwingine popote ulimwenguni.

Anayefanana nami.

Na anayezungumza kama mimi.

Aliye na manyoya kama yangu.

Na macho na masikio yangu.

Anaye kicheko changu.

Anayeweza kutenda ninachotenda.

Asiyeweza kutenda nisichoweza kutenda.

Nimetazama kila mahali ili kumpata mimi mwingine. 

Nilienda kwenye bustani na kutafuta nyuma ya miti.

Nilitafuta kila mahali, juu na chini.

Nilitazama kila uso.

Sikumpata mimi mwingine pahali popote.

Kuna mimi mmoja tu ulimwenguni! 

Ni kweli kwamba mimi ni wa kipekee!

Lakini, huoni kwamba si mimi pekee? 

Vilevile, kuna wewe mmoja tu!

------------------------------------------------------------



I enjoy skipping. 


Ninafurahi kuruka.

I enjoy skipping alone. 


Ninafurahi kuruka peke yangu.

I enjoy skipping with my friend. 


Ninafurahi kuruka na rafiki yangu.

I enjoy reading good stories. 


Ninafurahi kusoma hadithi nzuri.

I enjoy walking with my friends. 


Ninafurahi kutembea na marafiki zangu.

I enjoy washing dishes for mother. 


Ninafurahi kumsafishia mama vyombo.

I enjoy writing letters that I can read easily. 


Ninafurahi kuandika herufi ninazosoma rahisi.

I enjoy eating different fruits. 


Ninafurahi kula matunda tofauti.

I enjoy sleeping on a big bed. 


Ninafurahi kulala kwenye kitanda kikubwa.

I enjoy hearing mother's good stories. 


Ninafurahi kusikia hadithi za mama nzuri.

I enjoy doing all these things!


Ninafurahi kufanya vitu hivi vyote!

------------------------------------------------------------



Naka na Nala wako katika uwanja mkavu, wakiwa wameketi chini ya mti.

Nala anaskia majani yakipepesuka kutokana na upepo mwanana.

"Sikiliza Naka, unaweza kusikia sauti ya majani?" Nala anauliza.

"Ndiyo, ninaweza kuyasikia na pia kuyaona yakisonga," Naka anajibu.

"Je, unakumbuka nini kinachofanya majani kusonga?" Naka anauliza.

"Ni wakati upepo unavuma na kupeperusha vitu," Nala anajibu.

"Ni hewa," Naka anasema.

"Hewa inatuzunguka, lakini hatuwezi kuiona," Nala anaanza kusema.

Naka anakatiza, "Lakini tunaweza kuona na kusikia majani yakisonga!"

Nala anaendelea, "Hatuwezi kuiona hewa, ila tunaweza kuona na kuskia athari za hewa ikisonga. Huo ni upepo."

"Upepo ni hewa?" Naka auliza.

"Ndiyo," Nala anatabasamu.

Anaongeza, "Hewa pia hushikilia matone madogo ya maji kwenye mawingu. Maji hayo yanapozidi kuwa mazito, matone ya maji huanguka kama mvua."

"Hebu fikiria ikiwa sisi tunaweza kupaa angani katika puto la hewa moto. 

Puto hilo ni kama tone la maji na hewa inalishikilia juu," Nala anasema.

"Sisi pia tunavuta hewa," Naka anakumbuka.

"Ndiyo, wanyama wote wnahitaji hewa, hata mimea, ili kuishi," Nala anasema.

"Tunahitaji hewa safi," Naka anakubali.

"Hatuwezi kuiona hewa, lakini imeundwa na nini?" Naka anauliza.

"Hewa ni mchanganyiko wa gesi na chembe ndogo za vumbi," Nala anajibu.

"Dunia imegubikwa kwa hewa," Nala anasema.

"Hewa iko kila mahali. Hewa ya dunia inatanda kutoka hapa hadi angani," Nala anaongeza.

Maswali

1. Hadithi inahusu nani? 

2. Wako wapi?

3. Nani ahitaji hewa kuishi? 

4. Hewa imeundwa na nini?

5. Hewa iko wapi?

6. Mbona matone ya mvua huanguka?

7. Upepo ni nini? 

8. Tafuta hadithi kuhu upepo. 

9. 'Hewa safi' ni nin?

------------------------------------------------------------



Ng'ombe, ng'ombe, nipe maziwa!

Moo moo, omba vizuri!

Ng'ombe, Ng'ombe, tafadhali naomba maziwa.

Haya hapa tayari kwa kunywa.

Asante rafiki!

Kuku, Kuku, nipe mayai!

Kokoo, kokoo, omba vizuri!

Kuku, Kuku, tafadhali naomba mayai.

Sawa Atu, chukua mawili!

Asante rafiki!

Chura, Chura, nifundishe kuruka!

Hapana Atu, omba vizuri.

Chura, Chura, tafadhali naomba unifundishe kuruka?

Sawa Atu, turuke pamoja!

Asante rafiki!

Kipepeo, Kipepeo, nisukume kwa nyuma! 

Hapana Atu, omba vizuri!

Kipepeo, Kipepeo, tafadhali naomba unisukume kwa nyuma. 

Sawa Atu, furahia bembea! Asante rafiki!

Baiskeli, Baiskeli  nipe lifti.

Ngrii, ngrii, omba vizuri!

Baiskeli, Baiskeli  tafadhali naomba lifti.

Sawa Atu, panda juu.

Asante rafiki.

Paka, Paka, fukuza panya! 

Nyau, nyau, omba vizuri!

Paka, Paka, tafadhali naomba umfukuze panya?

Panya, ondoka, Atu anakuogopa! 

Asante rafiki!

Mbuzi, Mbuzi, nipeleke nyumbani!

Meh, meh, omba vizuri.

Mbuzi, Mbuzi, tafadhali unipeleke nyumbani? 

Sawa Atu, panda mgongoni.

Asante rafiki!

Atu, Atu, tupeleke Lala Land. 

Hapana, rafiki, omba vizuri!

Atu, Atu, tafadhali tunaomba utupeleke Lala Land.

Sawa nitawapeleka! Tucheze siku nzima na tusubiri usiku. 

Tukifumba macho upinde utakuja kutupeleka Lala Land.

Angalieni, unatokea! Twende Lala Land!

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na mamba mwenye njaa aliyeishi mtoni. Aliwakamata wanyama kama mbuzi, ng'ombe na kondoo walipokwenda kunywa maji. 

Wanyama wote wakaisha. Wakabaki ndege na mbuni. Mamba hakuweza kuwakamata ndege kwa vile wanaruka.

Siku moja, mamba alihisi njaa sana na alikuwa amewamaliza wanyama wote. Siku hiyo mbuni alikuwa anaelekea mtoni kunywa maji. 

Mamba akamwambia, "Mbuni, naomba uje uniangalie jino langu. Linauma sana."

Mbuni alikwenda kwa mbuni kumuangalia jino lake. 

Mbuni akaingiza kichwa chake ndani ya mdomo wa mamba kuangalia jino la mamba lililokuwa likiuma.

Mbuni akamwuliza mamba, "Jino lipi?" 

Mamba akamwambia, "La chini, upande wa kulia." 

Mara mamba akafunga mdomo wake.

Mbuni akaanza kujivuta. Akajivuta, akajivuta! Hakufanikiwa kujitoa. Shingo yake ikaanza kuwa ndefu sana. 

Mamba naye, hakuweza kufunga mdomo wake sana. Akamuachilia mbuni.

Mbuni akaondoka na kuelekea nyumbani kwake.

Na ndio maana hadi leo mbuni ana shingo ndefu.

------------------------------------------------------------



Kwanza,  mzizi unamea.

Mzizi unaingia chini ya udongo.

Halafu, shina linaanza kukua. 

Linaelekea juu kwenye jua.

Majani yanaanza kuota.

Mmea unakuwa mrefu zaidi.

Kisha maua yanatokezea. 

Maua hugeuka na kuwa maharagwe.

Kuna mbegu nyingi ndani ya ganda.

------------------------------------------------------------



Paka wangu yuko wapi?

Hebu nitazame mvunguni mwa kitanda.

Labda yuko juu ya kabati.

Hebu nitazame nyuma ya kochi.

Je, anaweza kuwa karibu na pipa la takataka?

Je, anaweza kuwa amejificha kikapuni?

Hebu nimtafute nje ya nyumba.

Aaa! Paka wangu ndiye huyu hapa!

------------------------------------------------------------



Mtaa wetu ulikuwa na matatizo mengi. 

Tulisimama kwenye foleni tukisubiri kuchota maji kutoka mfereji mmoja.

Tulisubiri kupokea chakula cha msaada. 

Hatukuwafahamu wahisani wetu.

Usalama ulizorota kila uchao. 

Tulilazimika kufunga nyumba zetu mapema kwa ajili ya wizi.

Baadhi ya watoto waliacha shule. 

Wazazi wao hawakuweza kuwalipia karo.

Wasichana wadogo walifanya kazi za nyumbani pale mtaani.

Wavulana wadogo walirandaranda ovyo.

Wengine waliwafanyia watu kazi mashambani.

Upepo ulivuma na kuzipeperusha karatasi chafu. 

Ziliangikwa mitini na uani na kuyachafua mazingira.

Vipande vya chupa vilitupwa ovyo ovyo njiani. 

Watu walijeruhiwa walipokatwa navyo.

Siku moja, mfereji wa maji ulikauka na mitungi yetu ikawa tupu. 

Tulijiuliza, "Sasa tutayapata maji wapi?"

Babangu alitembea kutoka nyumba hadi nyumba. 

Aliwatangazia watu kuhudhuria mkutano wa mtaa.

Watu walikusanyika chini ya mti ule ule ambako tulipokea chakula cha msaada. 

Baadhi waliuliza, "Kuna nini leo?"

Babangu alisimama katikati yao akasema, "Lazima tuyabadilishe maisha ya mtaa wetu."

Juma, aliyekuwa amepanda juu ya mti, alisema kwa sauti, "Naweza kusafisha uwanja wa nyumba zetu."

Mwanamke mmoja wa makamo, alisema, "Sisi wanawake tutaungana pamoja tupande mbegu ili tupate chakula."

Mwanamume mwingine alisimama akasema,  "Wanaume nao watachimba kisima cha maji."

Sote tulisema kwa sauti moja, "Lazima tubadilishe maisha yetu." 

Hivyo ndivyo, tulianza kufanya kazi pamoja kuyabadilisha maisha yetu.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na yatima wawili,  Nelima na Nambuye. Waliishi katika shamba lisilokuwa na rutuba. 

Kwa muda mrefu nchi ilishuhudia ukame nao hawakuwa na chakula. Walilazimika kwenda mbali kutafuta chakula.

Nelima alikuwa mnyamavu, mnyenyekevu na alipenda kusaidia. 

Nambuye, dadake, alikuwa mwenye kiburi na hakumsikiza yeyote. Hakuwajali watu wengine.

Siku moja, Nelima na Nambuye walipoamka,  walitambua kwamba hawakuwa na chochote cha kula. 

Walilazimika kutafuta chakula. Kila mmoja alikwenda kutafuta upande tofauti.

Wakati huo huo, aliishi Bi Kizee mmoja aliyeitwa Netasile. Netasile alikuwa na ugonjwa wa ukoma na mwili wake ulijaa vidonda. 

Watu wa kijiji chake walikuwa na imani kuwa Netasile angeweza kumpa mtu utajiri.

Alipokwenda kutafuta chakula, Nambuye alikutana na Bi Kizee Netasile. 

Netasile akamwita, "U hali gani mwanangu? Unatoka wapi na unakwenda wapi?"

Nambuye alijibu maswali yote kwa dharau. 

Netasile hakusita, akasema, "Nibebe unipeleke nyumbani kwangu nami nitakwambia la kufanya."

Nambuye akasema kwa kiburi, "Heri nife kuliko kuvigusa hivyo vidonda vyako." 

Bi Kizee alipuuza maneno hayo akamtakia safari njema.

Nambuye aliendelea kutembea. Alifika mahali palipokuwa na majongoo, nyoka, mabuu na wadudu wengine. 

Alikuwa amechoka na kudhoofika kwa kukosa chakula. Alipoketi chini kupumzika, wadudu walianza kumuuma.

Nelima naye alikutana na Netasile. Alifurahi kwani Netasile alikuwa binadamu wa kwanza aliyekutana naye tangu aanze safari yake. 

Netasile akamwita na kumwuliza, "U hali gani mwanangu? Unatoka wapi na unakwenda wapi?"

Nelima alijibu kwa upole. Netasile akasema, "Nipeleke nyumbani nami nitakwambia la kufanya." 

Nelima alimpeleka. Netasile akasema, "Umenitendea lile wengi wemeshindwa kufanya." 

Alimpa Nelima kijiti ambacho kingemsaidia kupata vyote alivyotaka.

Nelima alimshukuru Bi Kizee na kuelekea nyumbani. 

Alipofika nyumbani, alipata nyumba mpya iliyojaa vitu aina aina na chakula kingi. 

Tangu siku hiyo, Nelima akawa tajiri.

Nelima hakufurahia kumpoteza dadake lakini alisema, "Asiyesikia ushauri huishia ndani ya kinywa cha ndovu."

------------------------------------------------------------



Bul, Fumbo, Teke, Tongoli, Milege, Sos na Gwara walikuwa marafiki wakubwa. Pia, waliimba muziki mzuri. Waliishi karibu na milima mashariki mwa Uganda. Wote walikuwa wanamuziki stadi. 

Kila mtu alifurahi kusikiliza nyimbo zao na kucheza kufuata mdundo wao! 

Hawa wanamuziki stadi walitaka kumchagua kiongozi wao. Aliyetambuliwa kwa umaarufu wake zaidi ya wote, ndiye angekuwa mfalme wao.

Ili kuchaguliwa kama mfalme, kila mwanamuziki alitakiwa kudhihirisha kwamba anaweza kusikika na walio karibu na vilevile walio mbali. 

Tongoli aliongea kwanza, "Mimi ni mfalme. Ninaimba sauti ya juu na vilevile ya chini. Nina nyaya nyingi zenye milio tofauti. Ninaweza kuimba peke yangu na pia katika kikundi. Vijana kwa wazee hupenda kucheza muziki wangu. Hata ninamwongoza Fumbo kwenye nyimbo."

"Ulivyosema ni ukweli Tongoli," Fumbo alikubali. "Lakini, wewe hunishindi mimi. Sauti yako ni laini sana. Mimi nina sauti kubwa iliyo wazi na inayofika karibu na mbali." 

Fumbo aliendelea, "Watu hucheza muziki wangu mpaka karibu wavunjike migongo! Iwe wakati wa furaha au wa majonzi, mimi huwafanya watu wacheze! Watoto hupenda kuiga midundo yangu."

"Nyote wawili ni viongozi," Milege alikubali kisha akaendelea, "Kazi yangu ni rahisi. Wachezaji hunifunga vifundoni. Wanapoitikisa miguu yao kwa mdundo, mimi hutoa muziki wa kupendeza. Ninatoa mchanganyiko wa sauti za juu na zinazokwaruza. Je, mimi si kiongozi?"

"Hiyo ni sawa!" Bul alisema. "Mimi nimetengenezwa kutoka kipande cha ngozi kilichowambwa juu ya mti ulio na uwazi. Mimi hutia midundo kwenye nyimbo na sauti yangu hutambulisha vitu vingi. Lakini, siwezi kubadilisha sauti yangu kama mnavyofanya ninyi. Sidhani kama mimi ninaweza kuwa kiongozi."

"Bul, wewe hutenda mambo makuu!" Gwara alitofautiana naye. 

"Wewe huwaita watu kwenye mikutano, ibada, na kazi za kijamii na pia hutangaza vifo na kuwatahadharisha watu kunapokuwa na hatari. Unasikika wakati wa sherehe na kuwafanya watu wacheze, kwa furaha na kwa huzuni. Kulingana nami, wewe ni mkubwa zaidi." 

Gwara alitoa mlio mkubwa na kusema, "Mimi nina sauti kubwa tena ninawavutia watu. Hata hivyo, mimi si bora kumliko Bul. Ninapendekeza yeye awe mfalme."

Wanamuziki hao stadi walitazamana kwa mshangao wakabaki kimya. Kisha Tongoli akasema, "Bul ni mtu wa kawaida sana, hawezi kuwa mfalme. Mimi ndiye mkubwa zaidi kwa sababu ninacheza kuanza kwa sauti ya chini hadi ya juu zaidi bila tatizo lolote." 

Sos ambaye alikuwa kimya wakati huo wote, sasa aliongea, "Marafiki, mimi nimekuwa nikiimba nanyi nyote. Nyote ni wanamuziki stadi. Lakini, ni bora tumchague Bul kuwa mflame wetu."

Sos aliendelea, "Mtu asiyesikia muziki unaoimbwa na Bul ni kama gogo lililokufa! Bul huwavutia watu kwake na kuwaliwaza kwa muziki wakati wa huzuni na kuwaburudisha wakati wa furaha." 

Mwishowe, wanamuziki hao stadi walimchagua Bul kuwa mfalme wao. 

Tangu wakati huo, Bul amekuwa mfalme wa muziki. Hiyo ndiyo sababu Bul yuko katika kila nyumba ya jamii inayoishi milimani mashariki mwa Uganda.

------------------------------------------------------------



Upinde una rangi saba.

Rangi ya kwanza ni nyekundu.

Kweyu amevalia shati la rangi nyekundu.

Rangi ya pili ni ya chungwa.

Hili ni chungwa.

Rangi ya tatu ni manjano.

Yai pingu lina rangi ya manjano.

Rangi ya nne ni kijani.

Miwa ni rangi ya kijani.

Rangi ya tano ni samawati.

Mbingu ni samawati.

Rangi ya sita ni nili.

Matunda haya ni ya rangi ya nili.

Rangi ya saba ni zambarau.

Nguo yangu ni ya kizambarau. 

Ni rangi niipendayo zaidi!

Je,  unazijua rangi saba za upinde?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kwenye shamba ndogo karibu na kijiji kidogo.

Aliishi kuku mdogo aliyeitwa Daisy.

"Ningependa kuruka juu, juu angani, nitakapokua mkubwa," Daisy alisema.

Lakini kuku wengine wote walimcheka.

"Wewe ni wa ajabu sana," walisema. "Hatutacheza nawe tena."

"Daisy, sote tunaweza kupapata mabawa yetu lakini ni vigumu sana kwa kuku kuruka," Mama alimwambia.

Daisy hakutaka kukata tamaa. Kila siku alifanya mazoezi peke yake, akipapata mabawa yake.

Papata, papata, papata, angepapata mabawa yake lakini hakuweza kunyanyuka kutoka chini.

Alipofanya mazoezi, alijiona ameruka juu na kuwatazama kuku wengine chini.

Alijiwazia akiwa ameruka na kuwapita shomoro na mbayuwayu. "Waa!" Ndege wangesema. "Kuku anayeweza kuruka!"

Kwa hivyo papata, papata, papata, kila siku Daisy angepapata mabawa yake.

Angeweza kunyanyuka kutoka chini lakini angeanguka chini tena.

"Sitawahi kuruka!" Daisy alimlilia Mama. "Ni kweli wengine wanavyosema kuwa sitawahi."

"Daisy, wewe ni tofauti na kuku wengine. Wao hawataki kuruka lakini wewe unataka! Unaweza kufanya hivyo," Mama alisema.

Siku iliyofuata Daisy alipanda juu ya kibanda cha kuku na papapta, papata, papata, akapapata mabawa yake.

Aliruka angani na kupapata mabawa yake na kupapata mabawa yake na kupapata mabawa yake na ...

BAM! Alianguka kwa kishindo!

Kuku wengine wakacheka kwa sauti.

"Ha ha ha! Tulikuambia! Kuku hawawezi kuruka!"

Lakini siku iliyofuata, Daisy alipanda juu zaidi, hadi juu ya chumba.

Papata, papata, papata, Daisy alipapata mabawa yake.

Aliruka angani na kupapata mabawa yake na kupapata mabawa yake na kupapata mabawa yake na ...

Aliendelea kuruka! Upepo uliokuwa chini ya mabawa yake ulizidisha nguvu na akaruka juu zaidi!

Shomoro na mbayuwayu walisema, "Ajabu! Kuku anayeruka!"

Na kuku wengine walitaka kuwa kama yeye.

Wakasema, "Oo Daisy, wewe ni wa ajabu!"

------------------------------------------------------------



Sam yuko tayari kwenda mjini leo asubuhi.

"Basi linatarajiwa kufika saa 3 asubuhi," mama anatabasamu.

Sam yuko tayari masaa mawili kabla basi kuwasili.

Sam na mamake wanawasili kwenye kituo cha basi saa 2:45 asubuhi.

Watu zaidi walikuja kwenye kituo kabla ya 3 asubuhi.

Nusu saa baadaye, bado wamesubiri.

Sam ana wasiwasi. "Labda basi limeharibika," anawaza.

"Labda hatutakwenda mjini leo. Labda sitapata sare zangu za shule."

Saa 3:45 asubuhi baadhi ya watu wanakata tamaa na kurudi nyumbani.

Sam anaanza kulia. "Tutasubiri kidogo zaidi," mama anamtuliza.

Ghafla, wanasikia kelele.

Basi linakuja!

Basi linawasili kituoni saa 4 kamili za asubuhi.

"Ingieni! Ingieni! Tumechelewa sana leo!" dereva anasema.

Abiria wanaingia na kuketi.

Basi linaondoka saa 4:10 asubuhi.

"Basi litaondoka mjini saa ngapi kurudi kijijini?" mamake Sam anauliza.

"Basi la bluu litaondoka mjini saa 8:30 alasiri," dereva anajibu.

Sam anawaza, "Tutawasili mjini saa 5 kamili mchana."

"Tutakuwa na muda kiasi gani mjini kabla basi kuondoka?" Sam anaendelea kuwaza.

Maswali zaidi kuhusiana na hadithi:
1. Sam alikuwa tayari kwenda mjini saa ngapi?
2. Sam na mamake walisubiri basi kwa muda gani?
3. Basi lilichelewa kwa dakika ngapi?
4. Safari kwenda mjini itachukuwa dakika ngapi?
5. Sam na mamake watafika kijijini saa ngapi ikiwa basi la bluu linaondoka mjini kwa wakati?

------------------------------------------------------------



Watu kijijini walijua kwamba Mama Schola alipenda kupiga kelele mno.

Siku hiyo, alifanya hivyo kuhusiana na ng'ombe waliokuwa sokoni. 

"Wafukuze waende mbali hawa ng'ombe wajinga. Wanakula mboga zangu," alisema.

"Hei we pale! Wafukuze hawa ng'ombe wajinga watoke hapa," alisisitiza. "Wanakula nguo zangu."

"Wapi mwenye ng'ombe hawa wajinga?" alipiga kelele. "Wanakula nafaka yangu."

Kutoka mafichoni, Sorimpan, mchungaji,  alichuchumaa kwa kumuogopa Mama Schola. 

Alikuwa ameenda kunywa maji wakati ng'ombe wake waliranda na kwenda sokoni.

"Sasa tazama walichofanya hawa ng'mbe wajinga!" 

Aliendelea kupiga kelele. "Wamevivunja vyungu vyangu."

Baadaye kidogo, Mama Schola alisema, "Aah! Sio tena! Nitashtaki jambo hili kwa polisi. Hawa ng'ombe wajinga wamekiangusha kibanda changu cha matunda."

Sorimpan, fimbo mkononi, alihepa kati ya umati akfaulu kuwaona ng'ombe wake. 

Ng'ombe wa Sorimpan walimjua vyema. Waligeuka na kumwangalia mara tu alipotokea!

Wakati huo, palikuwa na umati mkubwa wa watazamaji: wanaume, wanawake na hata watoto. 

Wote walisimama wakiangalia ng'ombe ambao walimtii Sorimapn pekee.

Ghafla, ng'ombe walikivunja kimya chao! Wakaanza kuwakosoa watu! 

Watu walishangaa na kupiga hatua nyuma wakiwaogopa ng'ombe.

Kisha ng'ombe waliacha kuzungumza na kuuangalia umati kwa mshangao! 

Mama Schola alisikika akisema, "Tangu lini ng'ombe wakaingilia shughuli zetu za sokoni?"

Sasa ilikuwa zamu ya Mama Schola kukosolewa na ng'ombe. 

Wanawake wote waliokuwa wakiuza,  walisonga na kujiunga na Mama Schola kwa ajili ya woga.

Ng'ombe waliwakosoa wanawake. 

Waliongea kuhusu hali ya mboga zao wakisema, "Hizi ni mboga za aina gani? Zitazame jinsi zimeanza kunyauka!"

Ng'ombe waligeuka na kuangalia kibanda cha nguo kisha wakasema, "Mnadai kwamba tunakula nguo zenu! Nguo gani? Hivi viraka vikuu kuu ndivyo nguo! Nani atavinunua?"

Ng'ombe sasa walisongea kibanda kilichofuata. Watu wote waliwafuata. 

"Nafaka yenu imejaa wadudu. Nani anataka kuila hiyo! Tulikuwa tuanaonja tu!" Ng'ombe walisema.

Waliendelea, "Nawe Mama Schola, acha kupiga kelele. Vyungu hivi havina thamani yoyote. Vinavunjika upesi. Usitulaumu." 

Kisha ng'ombe waliondoka wakifuatwa na Sorimpan.

------------------------------------------------------------



Mwanamume

Mwanamke

Polepole

Haraka

Mrefu

Mfupi

Mwembamba

Mnene

Kijana

Mzee



------------------------------------------------------------



Kulikuwa na basi moja tu katika kijiji cha akina Ebei. 

Lilikuwa basi kubwa lenye rangi ya bluu. Lilinguruma sana.

Siku moja mamake Ebei alisema, "Kesho tutaenda mjini kununua sare yako ya shule."

Ebei alifurahi sana. Kumbe atasafiri katika lile basi kubwa la bluu! 

Usiku huo hakupata lepe la usingizi.

Mamake alipoenda kumuamsha, Ebei alikuwa tayari amevaa.

Ebei na mamake walienda kwenye kituo cha basi. 

Walisubiri lile basi kubwa la bluu. Basi halikufika.

Watu wengine walifika pale kituoni. Wote walilalamika kuwa basi lilichelewa. 

Mmoja aliuliza, "Basi limetuacha?"

Ebei alikuwa na wasiswasi. "Tusipokwenda mjini,  sitapata sare yangu ya shule," aliwaza.

Baadhi yao walikata tamaa wakarudi nyumbani. 

Ebei alilia akakataa kurudi. "Tutasubiri zaidi," mamake alimtuliza.

Ghafla, walisikia mngurumo. Wakaona vumbi hewani. 

Basi lilikuwa linakuja kwa kasi.

Basi halikuwa la bluu wala halikuwa kubwa. Basi lile lilikuwa dogo na jekundu. 

Waliosubiri waliliangalia tu na hawakuingia ndani.

Dereva aliwaita, "Ingieni! Ingieni! 
Tumechelewa sana leo."

Ebei na mamake walikuwa wa kwanza kuingia. 

Mara wote waliingia ndani ya basi lile dogo jekundu.

Ebei alichungulia dirishani. 

Aliwaona watu wengi zaidi wakiingia ndani ya basi.

Mara basi likaondoka. Ebei aliwaona watu wengine wakikimbia kulifikia basi. 

Walikuwa tayari wamechelewa.

Mamake Ebei alimwuliza dereva, "Liko wapi basi kubwa la bluu?" 

Dereva alimjibu, "Basi la bluu liliharibika. 
Linatengenezwa, kesho litakuja."

Ebei hakujali rangi wala ukubwa wa basi. 

Alifurahi kuwa basi lile lilikuwa linawapeleka mjini. Hatimaye, atanunuliwa sare ya shule.

------------------------------------------------------------



Hii ni familia yangu.

Mjomba wangu, binamu yangu, mama yangu, dada zangu wawili (ambao huvaa sawa), kaka yangu, na mimi!

Hii ni familia yangu ikiwa katika basi kwenda kuowaona wanyama.

Kulikuwa na shangazi yangu, mama yangu, kaka yangu, dada zangu wawili (ambao huvaa sawa), na mimi!

Tuliwaona wanyama kutoka kwenye basi.

Tulimwona twiga.

Tulimwona swala pala.

Tulimwona simba jike.

Tulimwona tembo.

Tulimcheka tembo sana, kwa sababu…

... tembo huyo aliunyea mti!

------------------------------------------------------------



Juma alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Katoloni. Aliishi na babake Musa.

Kila wakati babake angemwamsha mapema ili ajitayarishe kwenda shule.

Alipokuwa akijitayarisha kwenda shuleni, naye babake aliyekuwa na ujuzi wa kupika, angemwandalia kifungua kinywa. 

Kila alipofiikiria chakula cha babake, alitabasamu.

Siku moja, alitoka shuleni akihisi njaa sana. Alienda jikoni na kumwuliza babake kama kulikuwa na chakula chochote.

Babake alimpakulia wali aliokuwa amepika.

Juma alipenda kula lakini hakupenda kupika. Baada ya babake kumpakulia wali, alimuongezea supu.

Alitabasamu kwa chakula alichokipenda.

Alipokionja, akagundua hakikuwa na ladha ambayo aliizoea.

Alishangaa kwa sababu baba yake alikuwa mpishi hodari.

Juma hakuelewa ni nini chakula kilikosa wala hakufahamu viungo vyovyote vilivyotumika kwa mapishi. 

Yeye hakutaka kujihusisha na mambo ya jikoni ya upishi ila tu alifurahia chakula kitamu.

Alimwita babake na kumjulisha kuwa chakula hakikuwa na ladha. Babake aliamua kuendea mkebe wa chumvi na kuimwaga kwenye chakula kisha akakoroga. 

Juma hakuelewa kiwango cha chumvi kinachostahili kuwekwa kwenye chakula kwa kuwa hakupenda upishi.

Mara tu alipokionja, ulimi wake uliwasha, alikodoa macho huku pua ikikunjika. Hakujua amwite nani wala aguse wapi. 

Uzembe na ulafi wake ulimtia matatani. Alilia kwa uchungu huku akipanguza ulimi kutumia meza.

Babake aliangua kicheko. Juma aliona haya huku tumbo likinguruma. 

Tangu siku hiyo, Juma aliamua kujifunza upishi na kufanya kazi za jikoni. Babake alifurahi kwa kuwa Juma alipata funzo lake.

------------------------------------------------------------



Huyu ni Manyati na wanyama wake.

Ng'ombe wake anampatia maziwa.

Mbuzi wake naye anampatia nyama.

Naye farasi wake anamsafirisha.

Nguruwe naye anampatia nyama ya nguruwe.

Kuku anampatia mayai.

Mbwa wake anamlinda.

Manyati anawatunza wote!

------------------------------------------------------------



Hapo zamani kulikuwa na mwalimu aliyeitwa Goso. 

Aliwafundishia wanafunzi chini ya mbuyu badala ya darasani.

Siku moja, paa alipanda juu ya mbuyu kuiba matunda. 

Alitikisa tawi la mbuyu na tunda moja likamwangukia Mwalimu Goso.

Mwalimu Goso alifariki papo hapo.

Watoto walipofika chini ya mti walimpata mwalimu wao akiwa amekufa. 

Walihuzunika sana wakataka kujua kilichomuua Mwalimu Goso.

Waliushika upepo wa kusini, "Ni wewe uliyeangusha tunda lililomgonga Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Upepo wa kusini ulijibu, "Ningekuwa na nguvu kiasi hicho, ukuta wa matope ungewezaje kunikinga?"

Walikwenda kwenye ukuta wa matope, "Ni wewe uliyekinga upepo wa kusini ulioangusha tunda, lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Upepo wa kusini ulijibu, "Ningekuwa na nguvu kiasi hicho, panya angewezaje kutoboa shimo ubavuni mwangu?"

Walikwenda kwa panya, "Ni wewe uliyetoboa shimo kwenye ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ulioangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Lakini panya alijibu, "Ningekuwa na nguvu kiasi hicho, paka angewezaje kunila?"

Walimwambia paka, "Ni wewe humla panya,  anayetoboa shimo kwenye ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ulioangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Lakini paka alijibu, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kufungwa kwa kamba?"

Waliiambia Kamba, "Ni wewe humfunga paka,  ambaye hula panya anayetoboa shimo ubavuni mwa ukuta wa matope, uliokinga Upepo wa Kusini ambao uliangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Kamba ikasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kukatwa kwa kisu?"

Walikiambia kisu, "Ni wewe hukata Kamba, ambayo hufunga Paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa shimo ubavuni mwa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ulioliangusha tunda, ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Kisu kilisema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuchomwa kwa moto?"

Basi wakaenda kwa moto, "Ni wewe huchoma Kisu,  kinachokata kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa shimo kwenye ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ambao uliangusha tunda lililomwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Moto ulisema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuzimwa na maji?"

Waliyaambia maji, "Ni wewe ambaye huzima moto,  ambao huchoma kisu, ambacho hukata Kamba,  ambayo hufunga paka, ambaye hula panya,  ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini ambao uliangusha tunda, ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Lakini maji yakasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kunywewa na ng'ombe?"

Walikwenda kwa ng'ombe, "Ni wewe ambaye hunywa maji, ambayo huzima moto, ambao huchoma kisu, ambacho hukata kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ambao uliangusha tunda ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Lakini ng'ombe akasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuumwa na mbung'o?"

Basi wakaenda kwa mbung'o, "Ni wewe ambaye humwuma ng'ombe, ambaye hunywa maji, ambayo huzima moto, ambao huchoma kisu, ambacho hukata Kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini, ambao uliangusha tunda ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa." 

Mbung'o akasema, "Ningekuwa na uwezo kiasi hicho, ningewezaje kuliwa na paa?"

Basi wakampata paa, "Ni wewe ambaye hula mbung'o, ambaye humwuma ng'ombe, ambaye hunywa maji, ambayo huzima moto, ambao huchoma Kisu, ambacho hukata kamba, ambayo hufunga paka, ambaye hula panya, ambaye hutoboa ukuta wa matope, ambao ulikinga upepo wa kusini ambao uliangusha tunda, ambalo lilimwangukia Mwalimu Goso. Hayo ni makosa makubwa."

Paa alishtuka kwamba alikuwa ametambulika. Kwa hivyo, hakuwa na cha kusema. 

Kisha watoto wakasema, "Ni wewe uliyeangusha tunda lililomgonga Mwalimu Goso. Ni wewe unayepaswa kuadhibiwa!"

------------------------------------------------------------



Mbweha alikuwa na njaa. 

Alienda kuwinda.

Alimfukuza panya.

Panya alijificha chini ya jiwe.

Mbweha alichimba kumtoa panya. 

Jiwe liliangukia mguu wake.

Sungura alimsikia Mbweha akilia. 

Alikimbia kuona kilichotokea.

Sungura alikubali kumsaidia Mbweha. 

Mbweha aliahidi kumpatia chakula.

Sungura alilisukuma jiwe.

Liliondoka kwenye mguu wa Mbweha.

Sungura alimdai zawadi yake.  

Mbweha alitisha kumla Sungura!

Walimtafuta mzee kuwaamulia kesi yao.

Mbweha alitisha kumla yule mzee pia!

Mzee alisema, "Hebu nione lile jiwe kabla kuamua."

Mbweha na Sungura walimwonyesha mzee lile jiwe.

Mbweha alieleza jinsi jiwe liliangukia mguu wake.

Mzee alimwuliza Sungura, "Nionyeshe namna ulivyolisukuma jiwe."

Sungura alilisukuma jiwe.

Liliangukia mguu wa Mbweha.

Mzee alisema, "Sasa ni sawa. Hebu twende nyumbani."

Mzee na Sungura walienda zao. 

Mbweha aliachwa akiwa amenaswa.

------------------------------------------------------------



Katika kijiji kimoja, watu walitofautiana kuhusu kazi gani iliyo muhimu. 

Kila mmoja aliamini kuwa kazi yake ndiyo iliyokuwa muhimu zaidi!

Mwalimu alisema kazi yake ndiyo iliyokuwa muhimu zaidi. 

"Bila walimu, hakuna yeyote atakayeweza kwenda shule kujifunza."

Mjenzi akasema kwamba kazi yake ndiyo iliyokuwa muhimu zaidi. 

"Bila wajenzi, hakungekuwa na shule za kusomea wala nyumba za kulala."

Seremala naye akasema kwamba yeye ndiye aliyekuwa na kazi muhimu zaidi. 

"Bila maseremala, hakungekuwa na samani 
za kutumia nyumbani na shuleni."

Daktari naye alidai kuwa alikuwa na kazi iliyo muhimu kuliko zote. 

"Bila madaktari na wauguzi, watu wangeugua na kufa."

Mkulima akasema kwamba kazi yake ni muhimu zaidi.

"Bila wakulima, hakungekuwa na chakula."

Mwanafunzi naye alisema kuwa wanafunzi ndio walio na kazi muhimu kwa zote. 

"Bila wanafunzi, hakungekuwa na walimu, wajenzi, madaktari, wakulima, wala maseremala."

Hatimaye, kila mmoja alikubali kwamba 
kazi zote ni muhimu. Tunahitaji walimu, wajenzi, madaktari, wakulima, na maseremala. 

Lakini, lazima kila mmoja awe mwanafunzi kwanza!

------------------------------------------------------------



Mama yangu ana bustani ndogo.

Anapenda kukuza mimea tofauti.

Ninapenda kuitembelea bustani hii asubuhi kuvuna kilichokomaa.

Kuna maua.

Kuna dania.

Kuna oregano.

Kuna malenge.

Kuna tango.

Kuna nyanya.

Kuna stroberi.

Kuna ndimu.

Kuna vitunguu.

Kuna saladi.

Kuna sukuma wiki.

Kuna pia, viazi katika bustani ya mama yangu.

Mama hupika lishe bora kwa kutumia mazao ya bustani yake maridadi.

------------------------------------------------------------



Watoto watatu, Ado, Aggie, na Eddy waliisikiliza mvua ikinyesha. Walitaka sana kuchezea kwenye mvua hiyo. Walitaka kuugusa upinde ulioonekana angani. Lakini mama alisema, "La!" 

Walilia wakitumaini kwamba mama atabadili nia yake. Lakini, hilo halikufanyika. Eddy hata alijaribu kunyatia na kutoka nje ya nyumba ili autembelee upinde ule.

Mama alimpata kabla hajaenda mbali. Aliipaza sauti yake ili Eddy na dada zake pia waweze kusikia. 

"Utapata mafua," mama alisema. "Hampendi kunywa supu iliyo na pilipili lakini mkipata mafua, lazima mtainywa," aliongezea kwa tabasamu.

Akiwa na matumaini kwamba watamwuliza awasimulie hadithi, mama alisema, "Upinde ni mto wa miujiza ulio na nguvu za kuponya. Lakini upo mbali angani msikoweza kuufikia. Kwa hivyo mkipata mafua, upinde hautawasaidia."

"Tafadhali, mama, tusimulie ile hadithi inayohusu upinde," Aggie alisema. "Ndiyo, tafadhali, mama, ningependa kuisikia pia," Ado aliongeza. "Mimi pia," Eddy alimsihi mama huku akimvuta mkono. 

"Hebu tuone, mmmm," mama alisema kwa utani. "Sawa wapendwa, karibieni. Mama yenu msimulizi ndiye huyu hapa kuwasimulia!"

Aggie aliileta fimbo iliyotumiwa na wasimulizi. Alimpatia mama. Eddy alikileta kitambaa alichozoea kuvaa aliposimulia. Alipoishika ile fimbo na kukivaa kile kitambaa, mama alikuwa tayari kuwasimulia wanawe hadithi. 

Waliketi kimya kuisikiliza ile hadithi waliyoisikia mara nyingi. Ado aliipuliza firimbi kuashiria kuanza. Kisha masimulizi yalianza.

"Hapo zamani, upinde ulikuwa mto wa miujiza. Ulikuwa umejificha katika vichaka vilivyokuwa kijijini Bombo. Kwa sababu ulikuwa na nguvu za kuponya, ulipewa ulinzi mkali. Yeyote aliyekuwa mgonjwa, aliyanywa maji yake. 

Upinde huo ulifurahi ulipogawanya nguvu zake. Lakini haukupenda watu wasiokuwa na nidhamu."

"Kwa sababu ya nguvu zake za miujiza, kulikuwa na aiskrimu kwenye ukingo wa mto huo! Waliokuja kuyanywa maji, hasa watoto, vilevile walifurahi kuila aiskrimu. 

Aiskrimu hiyo ilikuwa ya rangi nyekundu, rangi ya machungwa, manjano, kijani kibichi, bluu, zambarau na nili."

"Siku moja, Bomu, Bi kizee mmoja mtukutu, alikuja kutoka nchi ya mbali. Alipowasili, alikutana na mlinzi. Mlinzi hakumtambua kwa hivyo alikuwa na hisia asizowahi kuwa nazo. Hata hivyo, alizipuuza hisia zake. 

Alimwelekeza Bi kizee huyo kwenda mtoni huku akimkumbusha kuuheshimu ule mto. Bomu alikubali kisha akaenda majini."

"Bomu aliyanywa maji na akapona. Halafu akatazama kuhakikisha kwamba hakuna aliyemwona. Alilichukua jiwe akalitumbukiza majini. 

Alilitazama likiinuka na kusambaza viwimbi vyake. Alifurahi sana hata akakichukua kijiti na kurudia kitendo hicho. Vilevile, kijiti kilisambaza viwimbi vyake."

"Bomu aliruka majini! Alikuwa na matumaini ya kuupata uzima wa milele. Mara tu aliporuka, mto uliinuka juu. Uliruka juu angani, usiwahi kurudi tena kijijini Bombo. 

Wakati mwingine, upinde hutokezea baada ya mvua na kuonekana kama mto tena. Na huo ndio mwisho wa hadithi yangu," mama alisema.

"Kwa hivyo, wapenzi wangu, niambieni, kwa nini mnaipenda sana hadithi hii?" mama aliuliza. "Kila mara mnaniuliza niwasimulie." 

Ado alitabasamu kisha akajibu, "Ninaipenda kwa sababu inanikumbusha kuzisikiza hisia zangu." 

Naye Aggie akasema, "Inanikumbusha rangi za upinde."

Eddy alijaribu bahati yake, "Ninaipenda kwa sababu inanikumbusha aiskrimu! Tafadhali, ninaweza kupata aiskrimu kidogo sasa?" 

"Mmmm. Sasa kuna baridi sana. Heri tuile aiskrimu kesho," mama alisema. Kisha akaongeza, "Wakati ujao, nitawaeleza hadithi kuhusu hatima ya upinde."

------------------------------------------------------------



Je, umewahi kuona kundi la ng'ombe malishoni? Kila mara ng'ombe hutikisa kichwa chake. Huonekana akijaribu kuwafukuza nzi wanaomsumbua. 

Lakini, kwa nini nzi hupenda kuzunguka kichwa cha Ng'ombe?

Inaaminika kuwa tabia hii ilianza zamani katika nchi ya mbali. Malkia wa nchi hiyo alikuwa tajiri na mkarimu. 

Siku moja aliamua kuwaandalia wanyama wote karamu. Aliandaa meza kubwa ya nyama, mikate, mboga aina aina na matunda matamu.

Wanyama wailfurahia vyakula wakajilamba midomo. Malkia alisema, "Mnyama mkubwa katika kila meza ndiye atakayegawa chakula katika meza hiyo." 

Ng'ombe alikuwa ameketi meza moja na Kondoo, Mbuzi, Mbwa, Bata Bukini na Nzi. Ng'ombe akaanza kuwagawia chakula. Alimpa kila mnyama kipande kikubwa cha mkate na jibini.

Kwa vile Nzi alikuwa mdogo, Ng'ombe alijifanya 
hakumuona. 

"Zuum! Zuum! Zii! Na mimi, je? Tafadhali nigawie chakula pia," Nzi alilalamika. 

Ng'ombe hakumsikia Nzi. Aliendelea kuula mkate wake. Maskini Nzi aliketi bila chochote huku akiwatazama wanyama wengine wakila.

Walipomaliza kula mkate, Ng'ombe aliwagawia nyama na mboga. Kila mnyama alipokea sahani kubwa ya chakula. 

Lakini, kwa vile Nzi alikuwa mdogo, Ng'ombe tena hakumuona. 

"Zuum! Zuum! Zii! Na mimi, je? Tafadhali nigawie chakula pia," Nzi alilalamika kwa sauti kuliko mara ya kwanza. 

Ng'ombe alimkasirikia Nzi.

"Eboi! Kumbe huna adabu?" Ng'ombe alimwuliza. "Mdudu mdogo kama wewe hustahili kuwa katika karamu ya malkia. Subiri hadi wanyama wote wakubwa wamalize kula." 

Chakula kilikwisha. Maskini Nzi hakupokea hata chembe. 

Ng'ombe akaanza kugawa matunda tikiti maji na matofaa.

Wanyama wote wakapata chakula isipokuwa Nzi. "Zuum! Zuum! Zii! Na mimi, je? Tafadhali nigawie chakula pia," Nzi alilalamika tena. 

Ng'ombe alicheka huku akiuma tofaa. "Ninyi mnasikia chochote?" Aliwauliza wanyama wengine. 
"Mimi sijasikia chochote." 

Wanyama wote walishiba kupita kiasi isipokuwa Nzi. Tumbo lake lilinguruma kwa njaa.

Baada ya chakula, walicheza na kuburudika. Nzi alikuwa amekasirika. Aliamua kurudi nyumbani. 

Malkia alimwuliza, "Nzi, mbona unaondoka? Hujafurahia karamu?" 

Nzi aliinama kwa heshima, "Samahani, chakula kilikuwa kitamu. Lakini sikugawiwa hata chembe." Nzi alimweleza malkia namna ilivyokuwa. 

Malkia alikasirishwa na Ng'ombe.

Malkia akasema, "Kutoka leo, wewe na marafiki zako mtakuwa mkiwasumbua Ng'ombe kila siku tangu asubuhi hadi jioni. Utakizunguka kichwa na kupiga kelele karibu na masikio yake. 

Hivyo ndivyo atakavyopata funzo. Hatawahi kukudharau tena. Atajua kwamba kwangu mimi, hata mdudu mdogo ni muhimu."

Hiyo ndiyo sababu Nzi amekuwa akifanya hadi leo. Yeye na marafiki zake hupiga kelele kwenye masikio ya Ng'ombe tangu asubuhi hadi jioni. 

Wanapofanya hivyo, wao huimba "Zuum! Zuum! Zii! Hamtatudharau tena. Semeni ndiyo!"

------------------------------------------------------------



Mamangu alipanda. 

Alipanda bustani ndogo. 

Alipanda bustani ndogo ya mbaazi.

Babangu alipanda. 

Alipanda bustani ndogo. 

Alipanda bustani ndogo ya maua.

Mamangu alipalilia bustani zote mbili.

Babangu alinyunyizia bustani zote mbili.

Mimi na wazazi wangu tulifanya kazi katika bustani hizo ndogo. 

Mimi na dadangu tulichuma maua na kuvuna mbaazi.

Tulivuna magunia ya mbaazi kutoka bustani ndogo ya mbaazi. 

Tulichuma magunia ya maua kutoka bustani ndogo ya maua.

Mamangu alipanda. 

Alipanda bustani kubwa. 

Bustani kubwa aliyopanda ilikuwa ya mbaazi.

Babangu alipanda. 

Alipanda bustani kubwa. 

Bustani kubwa aliyopanda ilikuwa ya maua.

------------------------------------------------------------



Leo ni likizo! 

Siendi shule.

Leo hakuna umeme. 

Sitatazama runinga.

Nitafanya nini leo? 

Nitausikiliza mwili wangu!

Ili niweze kuusikiliza mwili wangu, lazima niwe kimya. 

Kimya kabisa.

Sasa naweza kuisikia pumzi yangu. 

Pumua. Toa. 

Pumua. Toa.

Ninaweza kufanya pumzi yangu isikike kwa sauti ya juu. Zzzzzzzzz! 

Au isikike kwa sauti ya chini. Mhmhmhmh.

Sasa nausikia moyo wangu ukidunda! Kudukudukudu.

Je, naweza kuufanya moyo wangu kwenda mbio au kudunda kwa sauti ya juu? 

Ndiyo, nikiruka juu na chini mara nyingi.

Sasa moyo wangu unadunda kwa kasi. 

Dudududu!

Nikiweka kidole changu mkononi nitaweza kuusikia mpigo wa moyo wangu!

Ninajisikia nikicheka.

Haha haha haaah haaa!

Ninajisikia nikilia. 

Boohoooohooo!

Ninasikia nikipiga makofi.

Pa papa papapa papapapa.

Ninaweza kulisikia tumbo langu likinguruma. 

Gururuuuuu.

Likisema, nilishe, nilishe.

Na mapua yangu yananusa keki ipikwayo jikoni na mama.

Kuusikiliza mwili wangu, ni jambo la kufurahisha. 

Sasa nataka kuzisikiliza taya zangu zikitafuna.

Na tumbo langu likifurahia keki tamu zilizookwa na mamangu!

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na wavulana wa kurandaranda mtaani. 

Mdogo wao aliitwa Magozwe.

Alipokuwa na umri wa miaka mitano, wazazi wake walikufa. 

Magozwe alienda kuishi na Mjomba Bunu.

Mjomba Bunu alikuwa mtu mbaya. 

Magozwe alitoroka akaanza kuishi mtaani.

Maisha mtaani yalikuwa magumu. 

Magozwe na wenzake waliomba kutoka kwa watu.

Siku moja, Magozwe aliokota kitabu cha hadithi kwenye pipa.

Kitabu kilikuwa na picha za rubani. 

Magozwe alitamani kuwa rubani mashuhuri.

Wakati mmoja, Magozwe alikutana na Tomaso.

Tomaso alimpeleka Magozwe na wenzake pahali pa kupata chakula.

Tomaso alimwuliza Magozwe asome kile kitabu. 

Magozwe alimjibu, "Sijui kusoma."

Magozwe pia alimweleza Tomaso, "Nilitoroka nyumbani kwa Mjomba Bunu. Yeye alikuwa mtu mbaya."

"Ungependa kujua kusoma?" Tomaso alimwuliza Magozwe.

Tomaso alimpatia kitabu kipya cha hadithi.

Magozwe alifikiria juu ya kwenda shule.

Mjomba Bunu aliwahi kumwambia, "Wewe ni mjinga. Hujui chochote."

Magozwe alipokumbuka maneno ya mjombake, aliogopa.

Tomaso alimwambia, "Usiogope. Wewe si mjinga."

Tomaso alimpeleka Magozwe na wavulana wengine katika makao ya watoto.

Walifurahi sana.

Magozwe alianza kwenda shuleni.

Alipenda kuwa shuleni. Alisoma kwa bidii.

Siku moja, Magozwe alimweleza Tomaso, "Nitakuwa rubani maarufu kuliko wote."

MASWALI: 1. Kwa nini Magozwe aliishi mtaani? 2. Nini ilimhamasisha Mazogwe kuwa rubani wa ndege? 3. Vitendo vipi vya Tomaso vilionyesha upendo wake kwa watoto? 4. Unafikiri Magozwe atatimiza ndoto yake ya kuwa rubani maarufu? Toa sababu tatu kwa jibu lako.

------------------------------------------------------------



Mimi ninaitwa Noeli. Nina miaka tisa. Nasoma darasa la pili. 

Kipaji changu ni kuwa mwanajeshi. Nitalinda nchi yetu ili isiingiliwe na jambazi.

Ninaitwa Josephina John. Ninasoma darasa la nne. Nina miaka kumi. 

Kipaji changu ni kuchora. Mimi ninapenda kuchora sana. Ninachora vitu mbalimbali kama vile dawati, mtu, na maua.

Mimi ninaitwa Merry Beatus Maiko. Ninasoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Sinoni. Katika familia yetu tupo watu wanne. 

Ninadhania nitakapokuwa mkubwa nitakuwa mwanasayansi. Kwa sasa kipaji changu ni kucheza mpira wa miguu.

Kwa majina naitwa Juniour Daudi. Nina kipaji cha kucheza mpira wa miguu. Nilipokuwa mdogo, nilikuwa natamani kucheza mpira wa miguu. 

Nilijifunza kucheza mpira huo nikiwa shuleni. Kila siku ya Ijumaa shuleni tulikuwa tukienda kwenye uwanja wa polisi tulikofanyia mazoezi.

Siku moja, nilicheza mpira wa miguu nikachaguliwa kuichezea timu ya shule. 

Pia nina kipaji cha kuchora. Ninapenda kuchora na kucheza mpira wa miguu. Ninapenda hivyo vipaji vyote.

Kwa majina naitwa Lulu Hassani Issa Feruzi. Nasoma Shule ya Msingi Ngarash. Niko darasa la nne na nina miaka kumi na mmoja. 

Nakaa Tanga na kabila langu ni la Kizengua. Napenda chakula cha Kizengua kiitwacho goge.

Kipaji changu ni kuandika shairi. 

Ndoto yangu ni kuwa mwandishi wa mashairi yatakayochapishwa kwenye vitabu vya Maktaba ya Jamii Cheche.

Mimi ninaitwa Caren Emanuel. Ninasoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Ngarash. 

Kipaji changu ni kuwa mwalimu. Ningependa kufundisha Shule ya Mlimani nitakapomaliza shule.

Kwa majina ninaitwa Kelvin Peter. Ninasoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Mazoezi. 

Kipaji changu ni kuchora. Ninapenda sana kuchora. Nilipofikia miaka 7 nilianza kujua kipaji changu nikawa ninakiendeleza. 

Hadi sasa ninapenda kuchora.

Sio kuchora tu bali nina kipaji kingine kama vile kucheza mpira, kusoma na kuandika. 

Ningependa sana kuwahimiza kuwa mkiviendeleza vipaji vyenu bila kuwa waoga, mtaweza kupata ajira.

Kuhusu vipaji vya wengine, ninapenda sana kusikia mtu akiendeleza kipaji chake.

Changamoto ninazozipata ni kukosa vifaa vya kuchorea kama vile karatasi nyeupe na penseli, na rangi za aina mbalimbali.

Kwa majina ninaitwa Kelvini Zubery Akaro. Nilipoanzishwa chekechea nilichekwa na wenzangu kwamba mimi sina sauti ya uimbaji. Nililia sana. 

Nikakutana na rafiki yangu aliyeitwa Kelvini Peter. Alinishauri nisikate tamaa.

Pamoja, tulishirikiana kukuza vipaji vyetu. Tulisoma vizuri tulipokuwa chekechea na tulipata nafasi katika Shule ya Msingi Mazoezi. Nilisoma kwa bidii. 

Haikuwa rahisi kupata nafasi ya kujisomea na kufanyia kipaji changu mazoezi.

Nilikuwa nikijifungia ndani na kujifunza kuimba. Nilijaribu kuchora, lakini ilikuwa vigumu pia. 

Ghafla, nilipata habari kuwa kuna kipindi cha mapishi kila tatu usiku. 

Nilifuatilia kwa makini sana. Hivi sasa nina vipaji vya uimbaji, uchoraji na upishi.

Naitwa Angel Dismas Peter. Ninasoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Ngarash. 

Nina kipaji cha kuwa mwanasayansi. Katika familia yetu tuko tisa. Napenda kufaulu katika kipaji changu. Najitahidi kusoma sayansi ili niweze kufanyia kazi kipaji changu.

Kwa jina ninaitwa Gladinesi Samsoni. Ninasoma darasa la nne. Ninasoma Shule ya Mazoezi.

Kabila langu ni Mmeru. Chakula chetu ni kiburu. Ni chakula ninachokipenda sana.

Kipaji changu ni kutunga mashairi. Nitakiendeleza.

Ninatarajia kuwa mtungaji wa mashairi na kujulikana kitaifa na katika nchi za nje. 

Ningependa kuwa kama watunzi mashairi wengine wakubwa na kufikia malengo yangu. 

Ninapenda kipaji changu.

Kwa majina ninaitwa Doto. Nina kipaji cha kucheza mpira na kuchora. Mimi ni mchezaji mzuri na ninapenda kucheza mpira sana. 

Pia mimi ni mchoraji mzuri sana na ninapenda kuchora watu wanaocheza mpira wa miguu.

Mimi naitwa Meshack Daudi. Nina umri wa miaka sita. Ninasoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Ngarash. 

Kipaji changu ni kucheza mpira. Ninapenda kipaji changu na ninataka nikiendeleze.

Kwa majina ninaitwa Honnoratha Innocent Akaro. Nasoma Shule ya Msingi Mazoezi. Niko darasa la nne. Nina miaka tisa. 

Mimi ni Mchaga wa Materuni, mkoa wa Kilimanjaro.
Napenda chakula cha Kichaga kiitwacho kiburu.

Kipaji changu ni sayansi na teknolojia. Ndoto zangu ni kuja kuwa daktari wa upasuaji, katika hospitali ya KCMC, wilayani Moshi, mkoa wa Kilimanjaro. 

Nimejiwekea malengo ya kufanya kazi ya udaktari.

Baada ya kuajiriwa, nitawajengea wazazi wangu nyumba na kuinunulia familia gari. Baada ya hapo, nitajinunulia nyumba na gari.

Hii picha inaelezea kwamba kibakuli, penseli na maji ni mahitaji muhimu katika hatua ninazochukwa.

Naitwa Burai Balitazari Mrema. Nina miaka 8. Ninasoma darasa la pili. 

Kipaji changu ni kucheza mpira wa miguu. Mimi ni mchezaji wa timu ya Yanga. Ninacheza mbele na kudaka.

Naitwa Benson Maiko Laitery. Ninasoma darasa la sita Shule ya Msingi Ngarash. Nina miaka 12. 

Kipaji changu ni kucheza mpira wa miguu. Ninapenda kucheza mpira kwa sababu hufurahisha mwili na pia hunufaisha akili.

Nilipokuwa darasa la tano, nilitamani kucheza sana kwenye timu ya shule. Siku moja nilichaguliwa kuchezea timu ya shule. Hadi sasa ninaendelea kucheza.

Hata nikiwa mkubwa ninataka kuwa mchezaji wa Timu ya Taifa Tanzania.  Hili ni ombi langu kwa Mungu.

Mimi naitwa Matiasi Zuberi. Ninasoma darasa la kwanza. 

Kipaji changu ni sayansi. Nataka niwe daktari niwahudumie watu.

Pia nina kipaji cha kufuga ng'ombe. Najua kuwachunga ng'ombe na ningependa kuwahudumia wanyama pia.

Mimi ninaitwa Alidi Paulo. Ninasoma darasa la tatu. 

Ninataka kuwa mwalimu niwafundishe wanafunzi. Kipaji changu ni kuwafundisha wanafunzi na kuwaletea vitabu.

Kwa majina ninaitwa Wenworth Maurice Mwita. Nina miaka saba. Ninasoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Penieli. 

Kipaji changu ni kuwa dereva. Nikiwa mkubwa nataka kuwa dereva na kusomea mambo ya utalii.

Kwa majina naitwa Marvin Loth Edward. Ninasoma darasa la tano Shule ya Msingi Sinoni. Nina miaka kumi na moja. 

Kipaji changu ni kucheza mpira wa miguu na kuchora. Hata sasa mimi ninaendelea kukuza vipaji vyangu.

------------------------------------------------------------



Kijiji kimoja kilikuwa karibu na msitu.

Msitu huo ulikuwa na fisi na wanyama wengine wakali.

Watu wengi walivamiwa na fisi.

Ekeno alionywa na wazazi asiende mbali na nyumbani.

Ekeno alipuuza ushauri wa wazazi. Siku moja alienda kutafuta asali.

Alitembea kwa muda mrefu. Alijipata akiwa mahali asikokujua.

Usiku, alitafuta mahali pa kulala.

Usiku wa manane, Ekeno aliamua kuitafuta njia ya kurudi nyumbani.

Alivamiwa na fisi wakamla.

Wenzake walienda kumtafuta.

Jirani mmoja aliwaelekeza kuwa Ekeno aliingia msituni.

Waliamini kuwa alikuwa ameliwa na fisi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na marafiki wawili, Kinywa na Mkono. 

Waliishi kijijini kama ndugu kila mmoja na mkewe.

Baada ya muda mfupi, mke wa Kinywa alifariki. 

Kinywa alimwomba rafiki yake vifaa ili amzike mke wake.

Kinywa aliporudi nyumbani, aligundua kwamba alikuwa amelipoteza panga la Mkono. Alienda kuomba msamaha ila Mkono hakutaka kusikia maelezo yoyote. 

Mkono alimlazimisha Kinywa amrudishie panga lake na lisiwe jingine bali lile alilokuwa amemuazima.

Kinywa hakuwa na la kufanya. Aliamua kurudi alipomzika mkewe ili alitafute panga hilo. Alitafuta kila mahali lakini, hakulipata. 

Mwishowe, aliamua kuchimbua kaburi ili angalie. La kushangaza ni kuwa hata mwili wa mkewe haukuwepo tena kaburini.

Kwa huzuni, Kinywa alirudi nyumbani. Alipokaribia kufika, alimwona mbwa akiwa na panga hilo. Wakati huo, aliisikia sauti ya mkewe ikisema, "Huyu ni mtumishi wako." 

Kinywa alilichukua panga lile akamrudishia Mkono. Yeye akabaki na mbwa yule.

Kinywa aliishi na mbwa yule akimsaidia kuwinda. Siku moja aliacha kumwita mbwa na kuanza kumwita Mtumishi. 

Waliishi kwa furaha hadi urafiki baina ya Kinywa na Mkono uliporudi kuwa kama ulivyokuwa mbeleni.

Baadaye, Mkono alitamani kula nyama, lakini hakuwa na mbwa wa kumwindia. Alikwenda kuomba mbwa wa Kinywa. 

Kinywa hakusita kumpatia Mtumishi wake. Lakini alimwambia asimwite mbwa bali amwite Mtumishi.

Mkono alienda na Mtumishi popote alipotaka. Kila alichomtaka afanye, alifanya.

Allimtuma porini kuwinda. Mkono alimfurahia Mtumishi sana.

Siku moja walipokuwa porini, Mtumishi alipotea. Kinywa alianza kumwita, "Mtumishi! Mtumishi! Uko wapi?" 

Alipochoka, alisema kwa hasira, "Mbwa huyu ni gaidi sana." Wakati huo Mtumishi alitokea na kusema, "Umeniita mbwa! Naenda zangu." Alitoroka.

Mkono alirudi nyumbani bila Mtumishi. Alienda kwa rafikiye Kinywa kumpasha habari ya kupotea kwa Mtumishi. Kinywa hakufurahia ujumbe huo. 
Alimlazimisha Mkono kumrudishia Mtumishi wake. Mkono hakufaulu kufanya  hivyo. 

Tangu siku hiyo hadi leo, mkono ni mtumishi wa kinywa.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, Binadamu, Simba, Punda,  Nyoka, Tai, na Mbwa walikuwa wamekwenda vitani pamoja. Walisafiri siku nzima hadi jua lilipotua. 

"Tutalala wapi?" Punda aliuliza. 

"Tazameni, ninaona moshi ukitoka katika nyumba ile. Tunaweza kulala huko," Nyoka alisema.

Walipobisha, mtu na mkewe walitoka nje. Nyoka aliuliza, "Tunaweza kulala kwenu?" Waliwajibu, "Tunawakaribisha mlale, lakini, hatuna chakula cha kuwapa." 

Mbwa alisema, "Tulimwona ng'ombe wenu." 

Mume alijibu, "Huyo ng'ombe pekee ndiye tuliye naye. Tukimchinja, tutabaki bila chochote." 

Binadamu na wanyama walisema, "Tutawalipa. Tafadhali, tuchinjie ng'ombe wenu."

Simba alisema, "Naomba damu. Nitakupa zawadi siku moja." "Nipe mifupa. Nitakuletea zawadi pia." Mbwa alisema." 

Binadamu alisema, "Nipe maziwa. Nitakupa zawadi maalum." 

Nyoka akasema, "Nipe mafuta. Hutajuta." "Naomba vipande vya sarara. Nitakupa zawadi pia," alisema Tai. 

Punda naye alisema, "Mimi nipe nyasi kutoka paa la nyumba yako. Siku moja utanishukuru."

Mtu na mkewe walimchinja ng'ombe wao wa pekee. 

Wakampa Simba damu, Mbwa akapewa mifupa, Binadamu akapewa maziwa, Nyoka akapewa mafuta, na Tai akapewa vipande vya sarara. Punda naye akapewa nyasi kutoka paa la nyumba.

Wageni wale walilala vizuri usiku ule. 

Asubuhi kulipokucha wakaenda zao.

Baada ya wiki nyingi, mtu huyo na mkewe walimsikia Simba akinguruma karibu na nyumba yao. Walipotoka nje, hawakumpata Simba, lakini, kulikuwa na pembe ya tembo iliyolazwa nyasini. 

"Pembe hii ni ya thamani. Ipeleke ndani. Lazima tuwe waangalifu wezi wasije kuiiba," mume alimwambia mkewe.

Ghafla, yule mtu na mkewe wakatazama nyuma yao. Walimwona Mbwa amelala karibu na mlango wa nyumba yao. 

Alisema, "Msiwe na wasiwasi. Nitawazuia wezi wasiingie nyumbani kwenu. Nakumbuka mlinisaidia na sasa wacha niwasaidie pia."

Yule mtu alikuwa na kaka. Kakake huyo alikuwa tajiri, lakini, alikuwa mwovu na watu wote walimchukia. 

Alipopata habari kuhusu pembe ya tembo, aliwaza, "Ninaitaka pembe ile. Nitamuua kakangu halafu niichukue."

Usiku wa manane, alikwenda nyumbani kwa kakake. 

Nyoka mkubwa alikuwa amelala karibu na mlango wa nyumba ya mtu yule na mkewe. 

Nyoka huyo alimuuma kaka mwovu akaaga dunia.

Katika nchi ile, mtu alipokufa, mali yake ilirithiwa na kakake. Kwa sababu hiyo, ng'ombe na kondoo wa kaka mwovu walirithiwa na kakake aliyekuwa hai. 

Yule mtu alimwambia mkewe, "Simba, Mbwa, na Nyoka wametulipa vizuri. Tai, Punda, na Binadamu watafanya nini?"

Siku moja, Tai alipokuwa akiruka juu angani, aliwaona wazee wakitembea pamoja barabarani. Mikononi mwao walikuwa na kitu fulani kilichong'aa sana. 

"Nadhani wana pesa na vito. Inaonekana wanampelekea mume zawadi kutoka kwa mkewe au kutoka kwa mume kwenda kwa mkewe ili kumaliza ugomvi. Mwishowe, watasameheana tu." Tai aliwaza.

Tai aliruka chini akazichukua zile zawadi kutoka mikononi mwa wazee. 

Aliziangusha zawadi hizo nje ya nyumba ya yule mtu na mkewe waliomsaidia mbeleni.

Siku hiyo, Punda alikuwa katika msitu uliokuwa karibu. Mgongoni, alikuwa amebeba mfuko mzito uliojaa pesa. Bwana wake alimpiga akisema, "Enda kasi au nikuue! Wewe mnyama mpumbavu na mvivu!" 

Punda huyo aliwaza jinsi angemwadhibu bwana wake mwovu.

Punda alitoroka akaenda nyumbani kwa yule mtu na mkewe akwaambia, "Chukueni pesa hizi. Ni zawadi yenu." 

Yule mtu na mkewe walitajirika kutoka siku ile.

Mtu yule alisema, "Rafiki zetu, wanyama,  wamekuwa wema sana kwetu. Ilikuwa vyema kwamba tulimchinja ng'ombe wetu wa pekee tukawapa." 

Mkewe alimjibu, "Lakini, Binadamu hajatupa zawadi yoyote. Hakika, wanyama wametufanyia mambo mengi. Ninajua Binadamu atatufanyia mambo mazuri zaidi."

Walingoja, wakangoja. Wiki nyingi zikapita, kisha miezi na miaka, lakini Binadamu hakurudi. 

Wanyama wote walitimiza ahadi zao. 

Binadamu alisahau.

------------------------------------------------------------



Rafiki yangu ananipatia maharagwe kutoka bustani yake.

Nami ninapanda haragwe moja mchangani.

Haragwe hilo linaota mle mchangani.

Mche unakua kuelekea kwenye jua.

Mzizi nao unakua ukienda chini.

Mche unakua na kutokezea juu ya udongo.

Mche huo unakua,

na kuzidi kua.

Ninapanda maharagwe zaidi.

Mimea hiyo inakua,

na kuzidi kua.

Mimea hiyo inazaa maganda ya mbegu.

Mimea hiyo inakua kuelekea juu, juu ya ukuta wangu!

Maganda ya mbegu yanapokauka, ninayavuna.

Ninakusanya mbegu kutoka kwenye maganda.

Ninapika maharagwe kutumia vitunguu na viungo vingine vya kutia ladha.

Sasa, maharagwe haya yako tayari kuliwa.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na panya wawili. 

Mmoja aliishi kichakani.

Panya yule mwingine aliishi nyumbani.

Panya aliyeishi nyumbani alimwambia aliyeishi kichakani, "Unakula na kulala vibaya. Sisi tunalala na kula vizuri."

"Njoo ututembelee siku moja ujionee." Panya aliyeishi nyumbani alisema. "Niko tayari kuja usiku wa leo." Panya aliyeishi kichakani alijibu.

Wakati huo, mwenye nyumba alikuwa amekasirika sana. Alisema, "Hawa panya wanaokula chakula changu wataona!" 

Aliweka mtego wa sukari.

Panya wale wawili waliingia mle nyumbani kula vinono.  

Walicheka, "Chuchuchichicheche!"

Walipoufikia mtego, panya aliyeishi nyumbani alisema, "Hebu nionje hii sukari. Leo utajua vitamu tunavyokula hapa."

Lakini hata kabla ya panya kuonja sukari, mtego uliteguka, pa! Panya alishikwa shingoni. Macho yake yalivimba kama mbilingani.

Panya aliyeishi kichakani alitazama tu kwa mshangao. 

Alisema, "Rafiki yangu, ni vitamu gani ulivyokula vilivyoyafanya macho yako kuvimba?"

Lakini, panya aliyeishi nyumbani hakuweza kumjibu.

Panya aliyeishi kichakani aliondoka pale akisema, "Haa! Sitaweza kuvifurahia hivi vitamu anavyovisifu."

Heri nyumbani kwako kubaya kuliko kwa jirani kuzuri.

------------------------------------------------------------



Huyu ni mimi.

Ninaishi na mama, kaka na dada yangu.

Mama yangu anapenda kupika.

Wakati mwingine, mama yangu huwatembelea marafiki zake.

Anapokuwa huko, mimi husafisha nyumba na kuosha sahani.

Usiku, mama yangu hutwambia tusali.

Siku yangu ya kuzaliwa ifikapo, mama yangu huniletea zawadi.

Ninampenda mama yangu.

------------------------------------------------------------



Mama aliziweka nguo zake katika begi ndogo.

Alinikumbatia akasema,  "Kwaheri kwa sasa."

"Mama unaenda wapi?" Nilimwuliza.

Nilianza kulia nikitaka kumfuata. 

Baba alinibeba akanituliza.

Baba alisema, "Mamako anaenda hospitalini kujifungua mtoto."

Niliposikia 'mtoto' sikulia tena.

"Kwa nini aende hospitalini?"

Baba alinijibu, "Nitakueleza kwa nini anaenda hospitalini."

Baba alinieleza lakini sikuelewa. 

Nilimwuliza, "Ataendelea kunipenda?"

Alinijibu, "Tutakupenda wakati wote."

"Ninaweza kumwandikia barua akiwa huko?" Nilimwuliza baba.

Jioni hiyo, nilianza kumtungia mama barua.

Nilichukua karatasi na kuanza kuandika.

Mama, mama! Baba alisema kwamba umeenda kumleta mtoto mwingine.

Tafadhali, fanya haraka urudi nyumbani.

Ningependa umlete mtoto msichana. 

Nitacheza naye akiwa mkubwa.

Unaweza kuwaleta wawili. 

Mmoja atakuwa wangu.

Ninakusubiri hapa nyumbani.

Niliikunja barua yangu ili baba ampelekee mama. 

Asubuhi, barua haikuwepo.

------------------------------------------------------------



Kuku na Jongoo walikuwa marafiki. Lakini walikuwa wakishindana kila wakati.

Siku moja waliamua kucheza kandanda ili kuona aliyekuwa mchezaji bora.

Walienda uwanjani wakaanza mchezo. Kuku alicheza kwa kasi, lakini Jongoo akacheza kwa kasi zaidi.

Kuku alipiga teke mpira ukaende mbali, lakini Jongoo aliupiga ukaenda mbali zaidi. 

Kuku alianza kukasirika.

Waliamua kucheza penalti. Kwanza Jongoo alikuwa mlinda lango. Kuku alifunga bao moja tu.

Basi ikawa zamu ya Kuku kulinda lango.

Jongoo akaupiga mpira na kufunga bao. Jongoo akapiga chenga akafunga bao. Akapiga mpira wa kichwa na kufunga bao.

Jongoo alifunga mabao matano!

Kuku alikasirika kwamba alipoteza. Alikuwa mbaya sana aliposhindwa.

Jongoo alianza kucheka kwa sababu rafiki yake alikuwa anauzingatia mchezo huo sana isivyofaa.

Kuku alikasirika sana hadi akafungua mdomo wake wazi na kummeza Jongoo.

Kuku alipokuwa akienda nyumbani, alikutana na Mama Jongoo. Mama Jongoo aliuliza, "Je, umemuona mtoto wangu?"

Kuku hakusema chochote. Mama Jongoo alikuwa na wasiwasi.

Kisha Mama Jongoo akasikia sauti ndogo ikilia, "Mama, nisaidie!" 

Mama Jongoo aliangalia kila mahali na kusikiliza kwa uangalifu. Sauti ilitoka ndani ya kuku.

Mama Jongoo alipiga kelele, "Tumia nguvu yako maalum mtoto wangu!"

Jongoo wanaweza kutoa harufu na ladha mbaya. Kuku alianza kuwa mgonjwa.

Kuku aliteua. Kisha alimeza na kutema. Halafu akapiga chafya na kukohoa. Akakohoa!

Ladha ya Jongoo ilichukiza!

Kuku alikohoa hadi akamtema Jongoo.

Mama Jongoo na mtoto wake walitambaa wakaenda mtini ili kujificha

Kuanzia wakati huo, kuku wote na jongoo walikuwa maadui.

------------------------------------------------------------



Baba

Mtoto

Mama na mtoto

Dada na kaka

Mama, kaka na dada

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, kulikuwa na dada wawili, Kalio na Akiru. 

Siku moja, walienda kuchota maji mtoni.

Walipokuwa wakirudi nyumbani, waliketi juu ya jiwe kubwa kupumzika.

Baada ya kupumzika, Kalio hakuweza kusimama tena. 

Alikuwa amekwama kwenye jiwe.

Akiru alikimbia nyumbani kumjulisha mama yao. 

Kalio aliposubiri usaidizi, Fisi alijificha nyuma ya jiwe akimmezea mate.

Mama alipofika, alijaribu kumvuta Kalio, lakini ilikuwa bure. 

Kalio alikuwa kweli amekwama kwenye jiwe.

Mama alimtuliza Kalio akisema, "Nitazungusha ua hapa ili uwe salama."

Mama alijenga ua. 

Aliweka mlango karibu na Kalio ili autumie akimletea chakula.

Mama alipomaliza kujenga ua, alimwambia Kalio,  "Nitakapokuletea chakula, nitakuwa nikiimbia wimbo kujitambulisha. Utakapousikia, utanifungulia."

Mama aliongeza kumweleza Kalio, "Usimfungulie mtu mwingine." 

Mama aliimba wimbo huo kila alipokuja kumwona Kalio. 

Kalio angeufungua mlango na kupatiwa chakula.

Fisi alijificha kila wakati akimsikiliza mamake Kalio akiimba.

Fisi alifanya mazoezi mengi akiiga sauti ya 
mamake Kalio. 

Mwanzoni, hakufaulu.

Wanyama wenzake walimshauri Fisi, "Mmeze nzi wa mtoni ili sauti yako iwe bora." 

Fisi alimmeza nzi wa mtoni akaenda kuimba, lakini Kalio hakuufungua mlango.

Fisi alishauriwa na wenzake tena, "Labda ukimmeza nzi kutoka sehemu tambarare, utaimba vizuri." 

Fisi alifanya alivyoshauriwa na wenzake.

Mara hii, sauti ya Fisi ilikuwa bora alipoimba. 

Kalio aliufungua mlango na Fisi akamla.

Mama alimpelekea Kalio chakula kama ilivyokuwa kawaida. 

Aliimba mara nyingi, lakini mlango haukufunguka. 

Aligundua kwamba alikuwa amempoteza bintiye.

Mama alifanya mkutano na wanyama wote. 

Baada ya kuwasha moto mkubwa, aliwaambia, "Nyote mtauruka moto huu. Aliyemla Kalio, ataanguka ndani na kuteketea."

Wanyama wengine waliuruka moto salama, mmoja baada ya mwingine. 

Ilipofika zamu ya Mbweha, alisita kidogo.

Hatimaye, Mbweha alipouruka, moto uliiunguza ncha ya mkia wake. 

Mbweha alikuwa ameionja damu ya Kalio.

Fisi alikuwa wa mwisho. 

Alipouruka moto, alianguka ndani na kuanza kuteketea.

Wanyama walifahamu kuwa Fisi ndiye alikuwa amemla Kalio. 

Waliimba wimbo wa kumsuta Fisi.

------------------------------------------------------------



Sisi ni waandishi chipukizi, wachoraji, na wanaharakati kutoka Maktaba ya Jamii Cheche, Monduli, Tanzania.

Tuliandaa kitabu hiki kuelimisha jamii juu ya changamoto za kijinsia na kutoa mawazo yetu kuhusu namna ya kuzisuluhisha.

Katika sehemu hii ya kitabu, tunaangazia baadhi ya changamoto za kijinsia tunazokabiliana nazo katika jamii yetu.

Mtoto wa kike anawaza kusoma lakini baba anawaza atakapopata pesa.

Pia mvulana mmoja anawaza kumwoa mtoto wa kike anayewaza kusoma. 

Baba anamlazimisha mtoto wa kike kuolewa.

Baba anatoka sokoni na mtoto wake. Anamwambia mama, "Mtoto wetu anaweza kuanza kusoma." 

Lakini mama anamfokea, "We huoni kwamba ni kilema wa miguu na macho pia."  

Mtoto anasema, "Kweli siwezi kuona, lakini nina akili na ninaweza kusikia."

Watoto wanafanya kazi ngumu kutokana na ukatili wa kijinsia wa wazazi au walezi.

Kwa mfano, akina mama wengi wa kambo hupenda kutesa watoto. Hii ni changamoto kwa wavulana na wasichana.

Baba anamnyima mtoto haki yake. Anamwambia, "Hakuna tena kusoma, kwa sababu wewe ni kilema." 

Mama anasema, "Kwa nini unamnyima mtoto haki yake?"

Baba anasema, "Huyu mtoto anatakiwa atafute kazi ya kufanya."

Mama anasema, "Nitakushitaki kwa polisi usipomsomesha mtoto." Baba anasema, "Basi nitampeleka shule, lakini akimaliza darasa la saba hataendelea na shule." 

Mama anamwambia, "Usipompeleka, nitakushitaki." Baba anasema, "Hata ukinishitaki, simpeleki mtoto shule."

Mama mjamzito anafanya kazi nyingi nyumbani. Anapika, anaosha vyombo, pia anambeba mtoto anayelia mgongoni. Mwingine anamshika na kulia pembeni akihisi njaa.

Baba yuko na simu, amepewa chai kwani baba ashibe kwanza halafu wengine baadaye.

Huyu kaka anawaza kusoma lakini hajawahi kwenda kusoma.

Anasema, "Baba anampendelea dada lakini sijawahi kwenda shule. Nitakwenda shule."

Baba anampiga mtoto bila sababu. 

Baba anacheka.

Mama anafanya kazi asizoziweza.

Mama anafanya kazi ngumu.

Mtoto anaolewa akiwa na umri mdogo.

Mtoto mdogo ananyimwa haki ya kusoma au kupata elimu.

Mtoto mdogo anaolewa kabla ya umri wake kufika au kulazimishwa kuozeshwa kabla ya umri. 

Mtoto anafukuzwa nyumbani.

Mama anamnyima mtoto asiende shuleni afanye kazi za nyumbani.

Mwingine anaenda shuleni.

Mama anamshauri baba wampeleke mtoto shuleni kwa sababu baba hataki kumpeleka shuleni. Lakini mama anataka mtoto aende shuleni.

Baba hataki kumpeleka shuleni ili aolewe mapema. Anataka aache shule ili aolewe na baba apate ng'ombe.

Katika sehemu hii ya kitabu, tunaangazia baadhi ya mawazo yetu juu ya namna ya kushughulikia changamoto za kijinsia kwenye jamii yetu.

Ukiona mtoto anayeomba barabarani, ni bora umsaidie, kama mama huyu alivyofanya. 

Alimkuta mtoto anayeomba. Alimchukua na kumpeleka hotelini.

Kisha akaenda kituo cha polisi ili apewe ruhusa ya kuishi naye, halafu akamuarifu mwenyekiti.

Hatuna budi kuelimisha watu kupitia makongamano ya kidini na mikutano ya kijamii.

Mama amegundua mama huyu anataka kumwachisha mtoto shule. Akamwambia kuhusu madhara ya kumnyima mtoto haki yake ya kupata elimu.

Wanajadiliana kuhusu umuhimu wa mtoto kuendeleza elimu na kutimiza malengo na ndoto zake kama watu wengine.

Tunahitaji kuwaelimisha wazazi kutokugombana mbele ya watoto.

Ugomvi baina ya wazazi husababisha mtoto kuwa na msongo wa mawazo na kushindwa kusoma vizuri. Hii inaweza kusababisha mtoto kuacha shule kabisa.

Tunatakiwa tuhakikishe watoto wameenda shule ili wapate elimu bora.

Mama anamtesa mtoto. Mtoto anakwenda kumshitaki mama yake kwa polisi.

Mama anakamatwa.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii unaweza kuelimisha jamii na taifa.

Tuwasaidie watoto wenye mahitaji maalumu ya shule.

Hivyo tutahakikisha watoto wote wanapate haki yao ya kusoma.

Tuwe na ushirikiano katika jamii. Tuwasikilize wanaotoa ushauri. Tunapotoa ushauri wetu tunatakiwa utekelezwe.

Utakuta mtu anataka kusema kitu, ukasema, "Huyu hana cha maana." Kumbe anacho cha maana.

Tuwapende wenzetu. Tusiwe na ubaguzi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale aliishi jitu jike lililoitwa Motio. 

Siku moja lilipokuwa likitembea kando mwa ziwa liliwaona wasichana watatu, Lisa, Vera na Elsa. 

Likawauliza, "Ni nani kati yenu anayependwa na wazazi wote wawili?"

Lisa alijibu kwanza, akasema, "Mamangu hunipenda zaidi." 

Vera naye akasema, "Babangu hunipenda zaidi." 

Elsa akasema, "Baba na mama wananipenda sawa."

Motio alimwambia Elsa amfuate akamsaidie kuliinua tita la kuni. 

Elsa alimfuata Motio bila kuogopa.

Walipotembea hatua chache, Elsa alimwuliza Motio, "Zi wapi kuni zako nikusaidie?" 

Motio akajibu, "Ziko karibu na ile miti."

Walipofika hapo, Elsa akamwuliza Motio tena, "Zi wapi kuni zako?" 

Motio akajibu, "Haziko mbali kutoka hapa."

Walipokuwa wakitembea, walikutana na mwanamume. Mwanamume huyo alimwuliza Motio,  "Mtoto wako anaitwaje?" 

Motio akajibu, "Anaitwa Mkoba Uzungumzao."

Elsa aliimba kwa sauti: 

Mimi kamwe si mkoba. 
Mkoba hauongei. 
Ninaitwa Elsa. 
Lo! Nyumbani, kuna 
Mama nimpendaye, 
Baba nimpendaye, 
Kata nilinywealo maziwa.

Mwanamume huyo alipousikia wimbo wa Elsa,  alimhurumia, akamwuliza amwelezee juu ya wazazi wake. 

Alimnusuru kutoka kwa Motio na kumrudisha kwa babake na mamake. Wazazi wake walimshukuru mwanamume huyo na wakaishi kwa furaha na mtoto wao.

------------------------------------------------------------



Huu ni mpira.

Huu ni mpira wangu.

Mpira huu wangu ni mwekundu.

Mpira wangu mwekundu ni mkubwa.

Ninaugonga mpira wangu.

Mpira wangu umekwama mtini.

Ninaugonga mpira wangu mwekundu.

Nimeugonga mpira wnagu mwekundu kwa nguvu!

Uko wapi?

Mpira wangu mwekundu uko wapi?

Mpira wangu mkubwa mwekundu uko wapi sasa?

Mpira uko wapi sasa?

Uko juu.

Uko juu sana.

Uko juu angani.

Uko juu angani. Uko juu ya mwezi. Umepotea!

------------------------------------------------------------



Mvua haikunyesha. Ardhi ilikuwa kavu sana.

Kima aliondoka nyumbani kutafuta maji na chakula.

Alipitia milima na mabonde.

Alifika sehemu iliyoitwa Tirkol.

Kima alifurahia mahali hapa sana.

Alikula matunda akanona. Lakini, aliwakosa wenzake.

Kwa hivyo Kima alifunga safari kurudi nyumbani.

Kima wengine walifurahi kumwona.

Walimuuliza, “Hii ni sehemu gani iliyo na matunda?”

“Nitawapeleka huko,” Kima aliwajibu.

Kima wote walipendaTirkol. Waliamua kuishi huko milele.

Lakini kima wa Tirkol walikuwa na wasiwasi.

“Kima wageni watakula matunda yetu yote,” walisema.

Kima wa Tirkol walienda kuwavamia kima wageni.

Kima mzee aliuliza, “Mbona vita? Matunda yatatutosha!”

Ilikuwa ukweli. Kima waliamua kuishi pamoja kwa amani.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na Mbuzi Mdogo na Chui Mdogo. 

Walikuwa marafiki.

Siku moja walienda kucheza pamoja uwanjani.

Walirudi nyumbani jioni sana.

Mbuzi Mdogo alimwambia mamake, "Nilikutana na rafiki mrembo. Ana madoadoa maridadi. Nimefurahi sana. Nitakutana  naye tena kesho."

Mamake Mbuzi Mdogo alijibu, "Mwanangu, nimefurahi umerudi salama. Huyo si rafiki yetu. Sitakuruhusu ukutane naye tena."

Wakati huo huo, Chui Mdogo alimwambia mamake,  "Nilikutana na rafiki mrembo. Anapenda kucheza sana. Nimefurahi. Nitakutana naye tena kesho."

Mamake alijibu, "Aa, maskini mwanangu. Huyo alikuwa mbuzi mdogo mrembo. Nasikitika hukumla. Utakapokutana naye kesho, muue na umle. Usiogope."

Siku iliyofuata, Chui Mdogo alienda katika kijiji cha Mbuzi Mdogo.

Hakumwona Mbuzi Mdogo pale nje. 

Alikuwa amejificha nyumbani kwa mamake.

Chui Mdogo alipaza sauti, "Twende uwanjani tukacheze."

Mbuzi Mdogo alijibu, "Sisi si marafiki tena. Leo siji. Nimemsikiza mamangu. Mtoto mzuri humsikiza mamake."

Chui Mdogo alihuzunika.

Alirudi kwa mamake.

------------------------------------------------------------



Sally alimpenda babu yake sana. 

Sally angependa kuwa meneja wa benki atakapokuwa mkubwa.

Sally alipofikisha umri wa miaka minane, aliandaliwa sherehe. 

Wazazi walipata ruhusa ya kuandaa sherehe hiyo kwenye hifadhi ya wanyama.

Twiga mmoja alikuwa amekufa. Sally alilia kwa huzuni.

Aliwapenda twiga zaidi kuliko wanyama wengine.

Sally aliamua kumtembelea ndama wa twiga aliyekufa. Aliwaza, "Maskini yatima!"

Alimwimbia ndama yule kumfariji.

Ndama alimtazama wakati wote alipokuwa akiimba.

Mwalimu wa Sally alipanga safari ya darasa nzima. 

Sally na wenzake walimtembelea mtoto wa twiga.

Wenzake walimwuliza, "Anaitwaje?"

Sally aliwajibu, "Anaitwa Furaha."

Walipiga picha nyingi wakiwa na Furaha.

------------------------------------------------------------



Kondoo aliishi jijini. Alipochoka na maisha ya jiji, aliamua kwenda kichakani.

Njiani, alikutana na Fisi aliyekuwa hajala kwa siku nyingi.

Kondoo alisema, "Hujambo ndugu Fisi? Hujambo ndugu Fisi?"

Fisi alimjibu Kondoo, "Usinisalimu ukirudia rudia hivyo. Tenda jambo uitulize njaa niliyonayo."

Kondoo aliposikia hivyo, alianza kukimbia.

Alijikuta katika pango la Simba huku akifuatwa na Fisi. 

Fisi alifika pangoni huku akimrushia Simba vumbi machoni.

Simba alimwambia Fisi, "Kwani hatuwezi hata kupata amani pangoni kwetu? Unaturushia vumbi machoni mwetu!"

Fisi alijibu, "Samahani Mfalme, sikukusudia kukudharau! Ninakifukuza chakula changu!"

Simba alisema, "Wewe Fisi, ni chakula kwangu pia. Je, nilikufukuza? Ulikuja wewe mwenyewe. Usinilaumu baadaye."

Simba akamwuliza Kondoo, "Mbona ulikuja kichakani?"

Kondoo akajibu, "Nilikuja kwa sababu mimi ni mwaguzi."

Simba akasema, "Zitayarishe dawa za kienyeji unihakikishie kwamba wewe ni mwaguzi kweli." Kondoo akajibu, "Dawa zangu ni ghali mno."

Simba akasema, "Hiyo si shida. Hakuna jambo nisiloweza kufanya."

Kondoo akasema, "Sikio la Fisi ndilo dawa."

Simba akalikata sikio la Fisi na kumpatia Kondoo.

Kondoo akaliweka sikio hilo ndani ya chupa iliyokuwa na asali. Kisha akampatia Simba.

Simba alipolila lile sikio, lilikuwa tamu sana.

Akamwuliza Kondoo, "Inawezekana kulipata sikio la pili?"

Kondoo akasema, "Ndiyo, inawezekana mfalme wangu." Kwa hivyo, Simba alilikata sikio la Fisi la pili akampatia Kondoo.

Kondoo akaliweka tena ndani ya chupa iliyokuwa na asali kisha akampatia Simba.

Simba akamwuliza Kondoo, "Je, inawezekana kuipata ngozi?" Kondoo akajibu, "Nadhani inawezekana mfalme wangu."

Fisi aliposikia hivyo, aliogopa kufa. Alitoroka huku akifukuzwa na Simba.

"Ikiwa hivyo ndivyo maisha yalivyo kichakani, heri nirudi nyumbani," Kondoo alisema.

------------------------------------------------------------



Ajao alikuwa popo. 

Aliugua nyumbani kwake bila kupata usaidizi wowote.

Baada ya muda,  Ajao alifariki.

Majirani walisema, "Ajao amekufa. Itatubidi tuwaite jamaa zake waje wamzike."

Majirani waliwaita ndege wakisema, "Mmoja wenu amefariki. Njooni mkamzike."

Ndege walipokuja, waliona kuwa ni Ajao. 

Wakasema, "Mnyama huyu si wa jamii yetu."

"Wote wa jamii yetu wana manyoya. Lakini Ajao hana manyoya yoyote. Yeye si mmoja wetu." 

Kisha ndege hao waliondoka wakaenda zao.

Majirani walikubali, "Ndege wamesema ukweli. Ajao hana manyoya. Yeye si wa jamii yao."

Kisha mmoja wao akasema, "Labda Ajao ni wa jamii ya panya. Anafanana nao."

Majirani waliwaita panya wakisema, "Mmoja wenu amefariki. Njooni mkamzike."

Panya walipofika waliona kuwa ni Ajao. 

Walisema, "Mnyama huyu si wa jamii yetu."

"Kila mmoja wa familia yetu huwa na mkia. Ajao hana mkia." 

Kisha Panya waliondoka wakaenda zao.

Hakuna jamaa wa Ajao aliyepatikana.

 Kwa hivyo, Ajao hakuzikwa.

------------------------------------------------------------



Mama yangu alikuwa akizungumza kwa simu.



Alisikia kwamba bibi yangu alikuwa amefariki.

Mama alikuwa akilia sana.



Nilihuzunika sana, sana, sana.

Sote tulianza kulia.

Bibi alitupenda tulipokuwa hatuna mwingine yeyote aliyetupenda.



Watoto wake wote walikusanyika kumzika.

Tulianza kusali. Lazima kusitokee tena jambo baya kwa mwingine wa familia yetu.



------------------------------------------------------------



Mungu alitaka mtu wa kuulinda ulimwengu wake.

Simba alijitolea akasema, "Mimi ni mfalme. Ninaweza kufanya kazi hiyo."

Kwa sauti, Tembo akasema, "Mimi ni mkubwa. Ninafaa kufanya kazi hiyo."

Papa naye akafikiri, "Meno yangu ni makali. Ninafaa kuulinda ulimwengu."

Tai akacheka na kusema, "Ninaruka na kuona kila kitu. Ninafaa zaidi."

Mwishowe, Mungu akasema, "Nitawaumba watu waulinde ulimwengu wangu."

Kwa hivyo, Mungu aliwaumba wanaume na wanawake wenye ngozi nyeusi.

Wengine pia walikuwa maji ya kunde.

Na baadhi yao walikuwa na ngozi ya manjano.

Nao wengine wakawa na ngozi ya waridi.

Papa aliwachekelea watu akisema, "Wataogelea namna gani?"

Mungu alitabasamu na kusema, "Watajifunza."

------------------------------------------------------------



A-   Askari

B-    Bahasha

Ch-    Chumvi

D-    Dawa

Dh-    Dhahabu

E-    Embe

F-   Figo

G-    Gunia

Gh-   Ghala

H-    Hema

I-    Imba

J-    Jicho

K-    Kiota

L-    Limau

M-    Malaika

N-    Ngoma

Ng'-   Ng'ombe

Ny-    Nyumbu

O-    Orodha

P-    Popo

R-    Ramani

S-   Siafu

Sh-    Shamba

T-     Taji

Th-     Themanini

U-    Uzi

V-    Vumbi

W-    Wembe

Y-    Yai

Z-    Ziwa

------------------------------------------------------------



Sungura alimkuta Tembo. Tembo alikuwa amekibeba chungu cha asali.

Tembo alimbeba Sungura mgongoni. 

Sungura aliilamba asali ya Tembo.

Walimpata Nyati mtoni akinywa maji.

Sungura aliwauliza Tembo na Nyati, "Nani kati yenu aliye na nguvu zaidi?"

Sungura alisema kwamba alijua namna atakavyojua ukweli.

Kwanza, Sungura alimfunga Tembo kamba kiunoni.

Kisha akamfunga Nyati kamba ile ile kiunoni.

Sungura alijificha kwenye mti akasema, "Haya! Vuteni!"

Nyati na Tembo walivuta. Tembo akamvuta Nyati.

Nyati akamvuta Tembo.

Hakuna aliyeshinda.

Sungura aliikata ile kamba karibu na Nyati. 

Tembo alianguka kwa kishindo!

Sungura alimshangilia Nyati akisema, "Ni wewe mwenye nguvu zaidi."

------------------------------------------------------------



Shika mkono wa mtu mzima au rafiki ukiwa unavuka barabara.

Angalia vizuri pande zote kabla ya kuvuka barabara. 

Angalia kulia, angalia kushoto, angalia tena kulia  kabla ya kuvuka.

Usikimbie au kucheza barabarani. 

Unaweza kugongwa na gari.

Siyo lazima kuongea na watu ambao huwafahamu. 

Usiogope kukataa.

Usiogope kukataa maombi yoyote ya mtu ambaye humfahamu.

Vibiriti, vibiriti vya petroli na mishumaa ni vifaa vya watu wazima, siyo vya kuchezea.

Usivichezee, vinaweza kukuunguza.

Usicheze na visu, mikasi au vitu vingine vikali. 

Vinaweza kukukata!

Lala ndani ya chandarua ili kujilinda na mbu na magonjwa makali kama malaria.

Kama unahisi una homa na unajisikia kuumwa, nenda hospitali ukapime ili upate dawa sahihi.

Usisogelee maji yenye kina kirefu, mito, maziwa na bahari...

...kama huwezi kuogelea.

Jifunze kuogelea kwa sababu kucheza kwenye maji kunafurahisha kweli.

Usiwasogelee wanyama wakali.

Nyoka wanaweza kuwa na sumu.

Simba, vifaru na nyati wanaweza kukushambulia na kukuumiza.

Kuwa makini ili usiumie.

------------------------------------------------------------



Akai alipokuwa mdogo, mamake alikuwa na mazoea ya kumlaza kwenye mkeka maridadi. 

Mkeka huo ulitengezwa na shangaziye Akai kwa majani ya mtende.

Mkeka wa Akai ulikuwa na rangi za waridi, bluu na kijani kibichi. 

Ulikuwa tofauti na mikeka mingine aliyokuwa nayo mamake.

Makazi ya kina Akai yalikuwa katika sehemu kavu,  iliyojaa mawe na yenye joto. 

Kulikuwa na nge, buibui na nyoka pia. 

Akai hakuwahi kuumwa na viumbe hao hatari.

"Huu mkeka wako wa kipekee hukukinga na hatari." Mamake alimwambia.

Akai alikuwa mtoto mwerevu. 

Alijua mahali kilipokuwa kisima cha karibu.

Vile vile alijua mahali ilipokuwa manyatta ya nyanyake. 

Mara kwa mara alienda kwa nyanyake kunywa maziwa ya ngamia.

Siku moja, Akai aliondoka nyumbani kwenda kwa nyanyake. 

Alipotelea milimani, akaogopa.

Aliamua kuketi chini ya mti wa edome kusubiri usaidizi. 

Muda mfupi baadaye, alilala akaota ndoto.

Ndotoni, Akai alikuwa amelala kwenye mkeka wake kipekee. Bi kizee aliyefanana na nyanyake alikuwa akimchunga. 

Bi kizee huyo alitabasamu na kumpa maziwa. Akai alipounyoosha mkono wake kuyapokea, aliamka.

Akai aliyafungua macho yake pole pole. 

Alitazama juu akamwona ndege mdogo wa rangi ya bluu kwenye tawi.

Akai aliposimama, yule ndege alipapatisha mbawa zake kisha akamwongoza. 

Akai alimfuata.

Akai alifika mahali penye njia panda. 

Yule ndege akakitupa kipande cha mkeka kilichofanana na ule wake.

Akai alikichukua kipande hicho akakitazama kwa makini. 

Aliziona nyayo alizozifahamu kuwa za mamake. 

Baadaye, alikiona kisima walikochota maji.

Akai hatimaye alifika nyumbani. Watu wote wa familia yake waliimba na kucheza kumkaribisha nyumbani. 

Walimchinjia mbuzi, wakachoma nyama na kusherehekea kurudi salama kwa mtoto wao.

Akai aliukalia mkeka wake wa kipekee akila kipande kikubwa cha nyama. 

Akai alifurahi sana.

------------------------------------------------------------



Kwa ajili ya watoto katika kila nchi ya Afrika

Jina langu ni Juma na nina umri wa miaka kumi. 

Ninaishi na dadangu Zena aliye na umri wa miaka kumi na mitatu.

Tunaishi na Mama, Baba, kaka yetu mdogo Ndolo, na mbwa wetu Bosko.

Tangu korona ilipoingia, maisha yetu yamebadilika. 

Ni virusi vidogo lakini vinaweza kutufanya tuwe wagonjwa sana. 

Mtu yeyote anaweza kuwa mgonjwa kutokana na korona.

Nina huzuni kwa sababu siwezi kucheza na rafiki zangu. 

Ndolo ana huzuni kwa sababu hawezi kuwakumbatia rafiki zake. 

Zena pia ana huzuni kwa sababu hawezi kutumia rangi ya mdomo pamoja na rafiki zake.

Mama anafanya kazi ya usafi hospitalini. Baba anauza matunda na mboga mjini.

Kila asubuhi wanaenda kazini na Zena anatuangalia.

Jirani wetu, Bibi, ni mkongwe sana na anaugua ugonjwa wa moyo. 

Hakuna aliye na ruhusa kumkaribia siku hizi. Virusi vya korona ni hatari kwa wazee. 

Hatutaki kumfanya awe mgonjwa.

Mama anaporudi kutoka kazini, anaenda kumuangalia Bibi na kumpelekea matunda.

Mama anamwachia matunda mlangoni kwa sababu hawezi kuingia ndani ya nyumba.

Zena anaenda kuchota maji kutoka mifereji ya karibu kila asubuhi. 

Baadhi ya watu wanavaa barakoa wengine hawavai. 
Zena alijitengezea barakoa kwa kutumia kitambara.

Anasafisha mikono yake nyumbani. Mama anatunyunyizia sanitaiza kwenye mikono.

Kila usiku, Mama anatukumbusha: 

"Vaa barakoa safi kila siku. Osha mikono yako kwa sabuni kwa sekunde ishirini unapowasili popote. Funika mdomo na pua unapokohoa au unapopgia chafya." 

"Ndiyo, Mama!" tunasema.

1. Osha mikono yako kwa maji.
2. Tumia sabuni kuosha mikono yako.
3. Osha kwa sekunde 20 au polepole hesabu kutoka 1 hadi 20.
4. Suuza mikono yako kwa maji.
5. Kausha mikono yako kwa taulo au tishu safi.
6. Sasa mikono yako ni safi!



------------------------------------------------------------



Kuendesha

Kutupa na kukamata

Kuviringisha

Kukimbia na kufukuza

Kuzungusha

Kuruka na kupinduka

Kupiga

Kucheza na kutazama

Kubeba

Kucheza dansi



------------------------------------------------------------



Kwenye msitu wa Miwa paliishi tumbili aliyekuwa na huzuni sana. 

Kila alipozaa, mtoto wake alifariki.

Uchungu wa kufiliwa na watoto wake ulimfanya tumbili kuruka juu na chini. 

Tumbili huyu alikuwa akirukia tawi hili hadi kwenye lingine. Alipiga mayowe, "Kwi! Kwi! Kwi! Kwi!"

Tumbili alikuwa na huzuni wakati wote. 

Huzuni wake ulimzidi haswa alipowaona akina mama tumbili wengine na watoto wao.

Tumbili mwenye huzuni alijiwayawaya huku na huku. Alijiwayawaya kwenye tawi hili na lile! 

Siku zilipita na tumbili alizidi kulia zaidi.

Halafu, alizaa tena. 

Aliamua kumpeleka mtoto wake njiani ili wapita njia wamwone na kumtakia heri.

Tumbili alishuka na kumweka mtotowe njiani. 

Wakati huo, mwindaji alikuwa akirejea nyumbani. Alimwona mtoto wa tumbili akilala kando ya njia.

Mwindaji alimbeba mwana tumbili hadi nyumbani kwake. 

Alipofika nyumbani, wavulana wake watatu walifurahi kumwona mwana tumbili.

Watatu hao waliimba: 

Mrushe juu! 
Mrushe chini! 
Mrushe kwangu! 
Mrushe kwake! 

Mwana tumbili alirushwa kutoka kwa mmoja hadi mwingine.

Wavulana wale walipoendelea kucheza na mwana tumbili, mama tumbili alijificha mtini na kuangalia. 

Aliogopa kuwa mtoto huyu naye angefariki kama wengine.

Mara mke wa mwindaji aliwaona watoto wakicheza na tumbili mtoto. 

Aliwaonya, "Kuwa waangalifu! Hebu mlete hapa. Mtamwangusha!"

Alimchukuwa mwana tumbili mikononi mwake na kumbariki.

Alipomweka mwana tumbili chini, mama tumbili alikimbia kwa furaha. 

Alimbeba mwanawe kifuani na kwenda mtini.

------------------------------------------------------------



Kima na Fisi waligombana.

Walitaka ushauri wa Hakimu.

Hakimu aliwaza, "Kima atakula mahindi yangu. Fisi atakula mifugo wangu!"

Mwishowe, Hakimu aliwaambia, "Tafuteni ushauri wa wazee wa kijiji."

Wazee pia waliogopa. 

Hawakuamua kesi kati ya Kima na Fisi.

Wazee waliwaambia Kima na Fisi, "Kesi hii ni ngumu sana."

Wazee walisema, "Tafuteni ushauri kutoka kwa mwanamke maskini."

Mwanamke maskini alikubali kuamua kesi yao.

"Sina mali ya kupoteza."

Alimwambia Fisi, "Wewe unaheshimiwa, ni mkubwa na ni shujaa. Acha ugomvi."

Fisi alijibu, "Umesema ukweli. Nitakomesha huu ugomvi. Sitaki aibu."

Mwanamke alimwambia Kima, "Wewe ni mwerevu. Acha ugomvi."
 
Kima alikubali.

Aliwaambia, "Mmekubali kukomesha ugomvi. Ni vyema kusameheana."

Mwanamke maskini alisuluhisha tatizo lao.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, waliishi majirani wawili marafiki,  Meseret na Demeke. Walikuwa maskini sana. 

Siku moja, Meseret alimwambia Demeke, "Lazima leo niipeleke ngano yangu sokoni. Gunia ni nzito na soko iko mbali. Ningekuwa na pesa za kutosha, ningemnunua punda."

Demeke alijibu, "Nami lazima nikavinunue vyungu vipya leo sokoni. Vitakuwa vizito mno. Heri ningekuwa na punda vilevile. Kwa sasa, ninazo tu nusu ya pesa."

Meseret alikuwa na wazo. Alisema, "Hebu tumnunue punda pamoja. Wewe utalipa nusu nami nilipe nusu. Nitamtumia kwenda sokoni kwa juma moja nawe umtumie kwa juma lingine." 

Meseret na Demeke walimnunua punda. Kwa muda mrefu waliishi kwa furaha.

Siku moja, babake Meseret alifariki. Meseret alirithi mashamba, miti, ng'ombe na kondoo. 

Alikuwa tajiri na hakutaka kufanya kazi na Demeke tena. Vilevile, alitaka nusu yake ya punda.

Meseret alimwambia Demeke, "Mbwa wangu wanahitaji nyama. Ninataka kumchinja punda wetu wewe uchukuwe nusu yake nami nichukuwe nusu itakayobaki." 

Demeke alilia, "Sihitaji nyama yoyote ila punda. Ikiwa unataka kumchinja, nipe pesa za nusu yangu." Meseret alifoka, "Sitakupatia pesa zozote. Nusu ya punda ni yangu na ninaitaka sasa." Demeke alisema, "Hebu twende kwa hakimu atuamulie."

Meseret na Demeke walienda kumwona hakimu alisiyekuwa na busara. Hakuwasikiliza kwa makini. 

Hakimu aliwauliza, "Mnammiliki punda pamoja?" "Ndiyo," Meseret na Demeke waliitikia. Hakimu akasema, "Basi, kila mmoja atapata nusu. Iwapo Meseret anataka nusu yake, ana haki ya kuichukuwa. Mchinjeni punda kisha mmgawe nusu mbili."

Meseret alifurahi. Alimchinja punda na kuchukua nusu ya nyama kuwapelekea mbwa wake. 

Demeke alihuzunika akawaza, "Maskini punda wangu hayupo tena, na sasa lazima nibebe kila 
kitu mwenyewe."

Baadaye, Meseret alitaka kujijengea nyumba mpya. Alifikiri, "Nitakiteketeza chumba changu kizee kisha niijenge nyumba mpya nzuri na kubwa." Meseret alivihamisha vitu kutoka chumbani. 

Demeke alimwuliza, "Unafanya nini?" Meseret alimjibu, "Ninataka kukiteketeza chumba changu ili niijenge nyumba mpya." 

Demeke alikuwa na wasiwasi, "Lakini, chumba chako ki karibu na changu. Ukikiteketeza, changu pia kitateketea."

Kwa hasira, Meseret alisema, "Usijaribu kunizuia! Hiki ni chumba changu na nikitaka nitakiteketeza." Demeke alilia, "Wacha! Hebu twende tumwulize hakimu." 

Kwa sababu hakimu hakuwa mwenye busara, hakusikiliza kwa makini wala hakuelewa. Hatimaye alisema, "Meseret ana haki ya kukiteketeze chumba chake na hakuna anayeweza kumzuia."

Meseret alipokiteketeza chumba chake, upepo uliupeperusha moto hadi kwenye paa la chumba cha Demeke. Punde, chumba chake pia kilianza kuteketea. 

Demeke alimlilia hakimu, "Tazama! Meseret amekiteketeza chumba changu! Lazima anilipe." Hakimu aliamua, "La! Meseret alikiteketeza chumba chake. Moto ndio uliokiunguza chumba chako. Meseret hastahili kukulipa."

Maskini Demeke alihuzunika sana. Hakuwa na punda wala chumba. Alibaki na shamba peke yake. 

Kila siku alifanya kazi shambani mwake na usiku kulala chini ya mti.

Demeke alifanya kazi kwa bidii shambani mwake. Aliyang'oa magugu na kuwafukuza ndege. 

Wakati wa kuvuna ulipofika, kulikuwa na mazao mazuri ya mbaazi.

Siku moja, wanawe Meseret walipitia katika shamba la Demeke. 

Waliona mbaazi wakasema, "Mbaazi ni tamu sana!" Walizivamia wakazitoa zote.

Demeke alipowaona wanawe Meseret, aliwaambia, "Nirudishieni mbaazi zangu." 

Walimjibu kwa dharau, "Hatuwezi kukurudishia kwa kuwa tumezila. Mwulize baba akulipe."

Demeke alimwambia Meseret, "Wanao wamezila mbaazi zangu." Meseret alimjibu, "Nitakupa pesa." 

"Sitaki pesa zako. Ninataka mbaazi zangu." Demeke alitishia. 

"Subiri! Hebu twende tumuulize hakimu," Meseret alilia.

Meseret na Demeke walimwona hakimu yule yule. Kama kawaida, hakuwasikiliza kwa makini wala hakufikiria juu ya tukio hilo. "Wanawe Meseret walikula mbaazi zako na ni lazima zirudishwe. Pasua tumbo zao uchukuwe mbaazi zako." Hakimu aliamua. 

Meseret alisononeka sana akasema, "Wanangu watafariki! Tafadhali, Demeke, nitakupatia pesa." "Nilitaka pesa ulipomchinja punda wetu. Ninataka mbaazi zangu." Demeke alinena.

Demeke alichukua kisu chake. "Nitakujengea chumba kipya! Naomba msamaha kwa kukiteketeza chumba chako cha kwanza," Meseret alisema. 

"Sitaki chumba kipya. Ninataka mbaazi zangu," Demeke alimjibu. Alianza kukitia kisu chake makali. "La! La! Tafadhali, ngoja! Hebu twende tukawaone wazee. Tafadhali rafiki yangu wa jadi, wacha wazee waamue." Meseret alilia.

Meseret na Demeke walienda kuwaona wazee wa kijiji. Wazee waliongea kwa muda mrefu.

Mwishowe walimwambia Meseret, "Ulikosea ulipokataa kumlipa Demeke nusu ya punda wake. Ulikosea pia ulipokiteketeza chumba chake, na wanao walipozila mbaazi zake."

Wazee walimgeukia Demeke wakasema, "Unataka kuwaua wanawe Meseret. Hilo ni kosa pia. Huu ni uamuzi wetu. Lazima Meseret ampatie Demeke nusu ya miti yake yote, mashamba, ng'ombe na kondoo. Hivyo, mtaishi pamoja kwa amani."

Meseret alimpatia Demeke nusu ya mali yake. 

Waliishi pamoja kwa furaha bila kugombana tena.

------------------------------------------------------------



Sigei anawapenda paka. 

Kuna paka wengi nyumbani kwake.

Sigei ana paka mmoja mweusi. 

Paka huyu anakula nyama nyingi.

Sigei vilevile, ana paka mmoja mnono. 

Paka huyu hula kila kitu.

Paka wa tatu, alipanda mtini na akakwama huko.

Sigei alimfuata paka akakwama naye mtini. 

Mamake Selemeng alilazimika kumsaidia kushuka chini.

Sigei pia ana paka wawili wavivu. 

Wanalala nje ya nyumba wakiota jua mchana kutwa.

Sigei vilevile, ana paka watatu wanao shughuli nyingi. 

Usiku wanawashika panya jikoni.

Sigei ana mbwa anayeitwa Lirafi. 

Lirafi ana huzuni kwa sababu hana rafiki.

Paka wa Sigei hawampendi Lirafi. 

Wanapomfukuza, Lirafi anatoroka nyumbani.

Sigei anapompata Lirafi, anamrudisha nyumbani. 

Paka hawfurahi Lirafi anaporejeshwa. 

Hawataki kumwona tena.

Sigei ana paka wangapi?

Sigei ana mbwa wangapi? 

Lirafi yuko wapi sasa?

Nyumbani kwenu kuna paka wangapi? 

Je, mna mbwa nyumbani kwenu?

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, palikuwa na mfalme. 

Yeye na wake zake watatu, waliishi katika kijiji kimoja kilichoitwa Nuru.

Siku moja, mfalme yule aliwaita wake zake na kusema, "Wake zangu wapendwa, ningependa leo nile chakula kitamu. Atakayepika chakula kitamu zaidi, atapata zawadi nono."

Mke mmoja alienda sokoni akanunua nyama ya ng'ombe na viungo vingi. 

Alirudi nyumbani na kupika kitoweo alichoamini kilikuwa kitamu.

Mke mwingine alienda soko iliyokuwa sehemu tofauti. Alinunua nyama ya pori pamoja na viungo tofauti. 

Naye alirudi nyumbani kuitayarisha.

Mke wa mwisho aliamua kwenda kumuona mamake mfalme. 

Aliambiwa apike chakula cha kienyeji na wala asiweke mafuta au viungo vyovyote vya kisasa.

Mke huyo wa tatu, alienda shambani kutafuta mboga tofauti za kutayarishia chakula cha kienyeji.

Mfalme na wenzake walifika kwa wake waliopika nyama ya ng'ombe na ya pori. Hata hivyo, mfalme hakukipenda chakula alichoandaliwa. 

Walienda kwa mke aliyeandaa chakula cha kienyeji.

Mfalme alikifurahia sana kwani kilikuwa chakula alichokipenda. Alimteua mke huyo kuwa malkia katika ufalme wake.

Tangu siku hiyo, huyo mke aliheshimiwa sana. Yeye alijua namna ya kumfurahisha mmewe.

------------------------------------------------------------



Bahati alikuwa msichana mrembo na nyanyake alimpenda sana.

Nyanyake alitumia muda mrefu kumshonea Bahati sketi ya kuvutia. 

Bahati alipenda sana kuivaa sketi ile.

Wasichana wengine kijijini walimwonea wivu Bahati kwa sababu ya sketi hiyo. 

Walipanga kuificha. Lakini, ilikuwa vigumu kuichukua sketi hiyo akiwa ameivaa.

Asubuhi moja wasichana hao walimwalika Bahati aende kuogelea nao katika mto uliokuwa karibu. 

Walizivua nguo zao na kuziacha ukingoni ili zisitote. Kisha wakajitosa majini na kurushiana maji kwa muda.

Baada ya muda, walitosheka kuogelea. Kiongozi wa wasichana wenye wivu, aliirusha sketi ya Bahati majini, karibu na sehemu iliyokuwa na nyoka mkubwa. 

Halafu wasichana hao waliondoka na kumuacha Bahati akilia kando ya mto.

Mara yule nyoka mkubwa akamsikia akilia. Alijichomoza na kumwona Bahati mrembo. 

Nyoka huyo alimmeza Bahati pamoja na ile sketi.

Nyoka yule hakuipenda ladha ya sketi, akaitema.  Kwa bahati, akamtema Bahati pia. 

Bahati alilala ukingoni mwa mto huku amejifunika kwa sketi yake. Alikuwa amepakwa tope la kunata kutoka tumboni mwa nyoka. 

Tope hilo lilinuka fe!

Baadaye, Bahati aliivaa sketi yake iliyonuka na kukimbilia nyumbani.

Alipofika nyumbani, aliimba: 

Mama, nifungulie mlango, miye nanuka; 
Mama, nifungulie mlango, miye nanuka; 
Miye nanuka fe! 

Mama alipousikia wimbo wa Bahati, alimjibu:
 
Nenda zako Bahati, unanuka; 
Nenda zako Bahati, unanuka; 
Bahati, unanuka fe!

Bahati alihuzunika sana. 

Akakimbilia kwa mjombake na shangaziye.

Walimsikia akiimba:
 
Nifungulieni mlango, miye ninanuka; 
Nifungulieni mlango, miye ninanuka; 
Miye ninanuka fe! 

Shangazi na mjomba walimjibu: 

Nenda Bahati, unanuka; 
Nenda Bahati, unanuka;
Nenda! Nenda! Unanuka fe!

Bahati alibaki na wazo moja tu, kukimbilia nyumbani kwa nyanyake. 

Lakini, moyo wake ulikuwa mzito. Alijua hakuna aliyemtaka msichana aliyenuka fe.

Bahati alikuwa amekosea. Nyanyake hakumfukuza. 

Nyanya alimwosha, akaiosha sketi yake, akahakikisha kila kitu kilinukia.

Kutoka wakati huo, Bahati aliishi na nyanyake. 

Siku moja mvulana tajiri sana alitaka kumwoa Bahati.

Wazazi wa Bahati walipofahamishwa kuhusu jambo hilo, walitaka arudi kuishi nao.

Bahati alikumbuka jinsi walivyomchukia aliponuka fe. 

Aliwaambia, "Sitawahi kurudi nyumbani kwenu tena. Lazima wazazi wawapende watoto wao hata wakinuka."

Badala yake Bahati alimwalika nyanyake aende akaishi naye nyumbani mwa mvulana tajiri.

Nyanyake alifurahi sana, na wakaishi maisha ya furaha.

------------------------------------------------------------



Zuhura na Wema ni marafiki wakubwa sana. Ni marafiki wanaopendana na kusaidiana.

Leo wamesoma kuhusu jinsi ya kutunza mazingira.

Hivyo wameamua kuanza kutunza mazingira.

Wametambua kuwa utunzaji mazingira ni muhimu sana kwa viumbe vyote.

Watoto wengine wamejumuika kutunza mazingira yao kwa kufanya usafi wa makazi yao.

Pia wanashirikiana na wazazi wao kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji na mazingira yake.

Utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa binadamu na wanyama wote. Maji safi na salama ni muhimu kwa afya zetu.

Pia maji ni uhai kwani husaidia kwenye shughuli kama kilimo na ufugaji.

Kilimo husaidia kupata chakula ambacho ni muhimu kwa afya zetu.

Pia hupatia mifugo chakula.

Hata wanyama wa porini hukumbwa na athari kubwa sana pale mazingira yasipotunzwa.

Athari kubwa zilizo dhahiri ni kama upungufu au ukosefu wa mvua.

Ni vyema watoto wajue kuwa kuna faida nyingi za kutunza mazingira.

Je, utunzaji mazingira una faida gani zaidi?

------------------------------------------------------------



Kombe na Juma walikuwa maskini pia jirani.

Walifanya kila kitu wenyewe.

Walitamani kuwa na punda.

Punda angewabebea mizigo.

Kombe akasema, "Hebu tununue punda pamoja."

Walifurahia hatua hiyo.

Babake Kombe alipofariki, Kombe alitajirika.

Alimsahau Juma.

Kombe alitaka nyama ya punda amlishe mbwa wake.

Juma alihitaji punda.

Hakimu aliwaambia, "Kila mmoja wenu anaweza kuchukua nusu ya punda."

Kombe alimchinja punda.

Juma alijibebebea vitu kwa mara nyingine.

Kombe alitaka kuteketeza chumba chake ili ajenga kipya.

Juma alisema, "Changu pia kitachomeka."

Hakimu alikubaliana na Kombe.

Chumba cha Juma kiliungua.

Hakimu alisema, "Kombe aliteketeza chake."

Juma hakuwa na punda wala chumba.

Alilala chini ya mti.

Juma alifanya kazi kwa bidii.

Alipata mazao mazuri ya mbaazi.

Wavulana wa Kombe walikula mbaazi karibu wazimalize zote.

Walimwambia Juma, "Nenda umwulize baba akulipe mbaazi zako."

Juma alisema, "Sitaki pesa zenu. Ninataka mbaazi zangu."

Hakimu alimwambia Juma, "Wakate wavulana halafu uchukue mbaazi zako."

Juma alikataa kusikiliza alivyoambiwa.

Kombe alilia, "Hebu wazee waamue."

Wazee walisema, "Ulimuua punda. Ulichoma chumba chake."

Walimwambia Juma, "Kuwaua wavulana wa Kombe ni vibaya pia."

Kombe alimpatia Juma nusu ya mali yake.

Wakaishi kwa furaha.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Fisi na Sungura walikuwa marafiki sana. 

Wote walikuwa maskini lakini Sungura alikuwa na punda. Pia alikuwa na beseni ndogo aliyoitumia kumlisha punda wake.

Adhuhuri moja, Sungura alitaka kumpatia punda wake maji. Hakuweza kutega maji kutoka kisimani kwa kutumia ile beseni yake ndogo. 

Alienda kumwomba Fisi beseni yake kubwa. Fisi alimpatia kwa sababu ya urafiki wao.

Sungura alipomaliza kumnywesha punda maji, alikwenda nyumbani kwake na beseni ya Fisi. 

Wiki mbili baadaye, Fisi alihitaji kufua nguo zake lakini alikumbuka kwamba Sungura alikuwa bado na beseni yake. 

Fisi aliziacha nguo akaenda kwa Sungura kuichukua beseni yake.

Sungura alimrudishia Fisi beseni yake kubwa. Vilevile alimpa ndogo akisema, "Beseni yako ilizaa mtoto. Kwa sababu ya urafiki wetu, nimeamua kukupatia zote mbili." 

Fisi alifurahi mno akazikubali beseni hizo mbili.

Siku mbili baadaye, Sungura tena alihitaji kumpa punda wake maji. Kwa mara nyingine, alimwendea Fisi amsaidie. 

Fisi aliwaza, "Kwa sababu nitapokea beseni moja zaidi, nitampa tena beseni yangu!" 

Sungura aliichukua beseni kubwa ya Fisi kumnyweshea punda wake maji. Baadaye, aliipeleka nyumbani kwake.

Fisi alisubiri kabla kwenda kuichukua beseni yake kwa Sungura. Alitaka izae nyingine kama mbeleni! 

Fisi alipoenda nyumbani kwa Sungura kuichukua beseni yake, Sungura alisema, "Fisi, rafiki yangu, nilikuwa ninajitayarisha kukuletea ujumbe mbaya. Beseni yako ilikufa siku mbili zilizopita. Si unajua kwamba vitu vyote vilivyo hai lazima vife?"

Fisi hakuweza kuamini aliyoyasikia. Alisema,  "Lazima niwaite wanyama wakubwa waje kuamua kesi hii." 

Fisi aliwaita tembo, viboko, vifaru na twiga. Walifika nyumbani kwa Sungura kuamua kesi.

Sungura aliulizwa kueleza kilichotokea. Alisema,  "Mara ya kwanza nilipoomba beseni ya Fisi, ilizaa mtoto nami nilimpatia zote mbili. Nilipoomba mara ya pili, beseni hiyo ilifariki kabla kuzaa. Kwa sababu chochote kilicho hai, vilevile hufa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa!" 

Wanyama wote walikubaliana na Sungura. Fisi aliipoteza beseni yake.

------------------------------------------------------------



Wakati mmoja palikuwa na mamba aliyekuwa na njaa.

Alikitafuta chakula polepole tena kimya kimya.

Halafu.

PUU! Mamba alishambulia!

Baadaye, hakuwa na njaa tena. 

Alifurahi.

Alitulia hadi alipohisi njaa tena.

------------------------------------------------------------



Opio aliishi katika kijiji kisichokuwa na majira ya usiku. 

Watu walipochoka, walilala na kufanya kazi walipoamka.

Siku moja Opio na mbwa wake walienda kuwinda. Mbwa walimfukuza paa naye Opio akawafuata. 

Mwishowe, hakuwaona tena.

Opio alikimbia mpaka akachoka. 

Alikaribishwa na mtu mmoja aliyempa kileo kunywa.

Opio alipoamka, hakuweza kuona. 

Alimlalamikia mwenye nyumba, "Ulininywesha nini? Mbona sioni tena?"

Mwenye nyumba alimwambia Opio, "Sasa ni usiku. Kwani hujui usiku?" 

Opio aliuliza maswali mengi kuhusu usiku na mchana.

Asubuhi, Opio alielezwa jinsi ya kuupeleka usiku kijijini kwao. 

Aliambiwa atembea kuelekea kwao bila kutazama nyuma.

Usiku huo Opio alisafiri kwenda kijijini kwao akifuatwa na giza. 

Hakutazama nyuma.

Alipofika kijijini kwao, wanakijiji waliogopa wakamwuliza, "Hiki ni kitu gani cheusi kilichokufuata?" 

Opio aliwaeleza, "Hili ni giza la usiku. Mwangaza huwa mchana."

Opio aliendelea kuwaeleza, "Tutafanya kazi mchana na usiku tutapumzika."

Na hivyo ndivyo usiku ulivyoingia katika kijiji cha kina Opio.

------------------------------------------------------------



Kasembo na wazazi wake waliishi maisha ya uchochole. Kasembo hakuweza kwenda shule ingawa aliamini kuwa ataenda siku moja. 

Wanakijiji walipendezwa na urembo na ukakamavu wa Kasembo.

Kila siku Kasembo aliamka asubuhi kwenda mawindoni. 

Wanakijiji walishangazwa sana na mazoea hayo.

Siku moja, Kasembo alibahatika kwa njia ya pekee.

Alifanikiwa kupata sungura mwitu.

Alitafuta kuni ili ampike yule sungura.

Aliona kijisanduku kidogo kilochokuwa kimefichwa.

Kasembo aliamua kukifungua ili kuona kilichokuwa ndani. Alipigwa na butwaa kuona dhahabu.

Alifurahi sana. Alikifunga, kisha akakibeba hadi nyumbani.

Mara moja, yeye na wazazi wake, walianza kutafuta mnunuzi wa ile dhahabu. 

Walimkumbuka Kigunda, tajiri mmoja aliyehusika na biashara ya madini.

Kigunda alinunua ile dhahabu yote. 

Kasembo alipata pesa za kutosha. Aliwajengea wazazi wake nyumba mpya na kuwanunulia gari.

Pesa zilizobaki, aliitumia kununua sare za shule, na kulipa karo ya miaka kadhaa.

Maisha ya Kasembo na wazazi wake ilibadilika kweli kweli.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na mkulima na mkewe. 

Walikuwa na mtoto mmoja pekee mvulana aliyeitwa Kisirusiru.

Kisirusiru alipompeleka mbuzi malishoni, mbuzi alirarua shati lake. Mamake alimtuma sokoni kununua sindano aweze kushona shati lake. 

Kisirusiru aliiweka sindano kwenye mfuko wa shati lake. Njiani, alijiunga na wavulana waliokuwa wakicheza mpira. Sindano ilipotea.

Kisirusiru alipofika nyumbani, alisema, "Samahani mama, nimepoteza sindano njiani." 

"Mwanangu, wakati mwingine, idunge sindano kwenye karatasi kisha uiweke mfukoni," mamake alieleza. 

"Ndiyo mama, nimeelewa," Kisirusiru alijibu.

Kisirusiru alichukua chungu kwenda mtoni. Alikifungia chungu ndani ya kipande cha karatasi. Alipokuwa njiani, karatasi iliraruka, chungu kikaanguka na kuvunjika vigae vigae. Maji yote yalimwagika. 

Alipofika nyumbani, Kisirusiru alimweleza mamake, "Samahani mama, chungu kimevunjika." 

"Mwanangu, wakati mwingine, kibebe chungu kichwani," mama alishauri. 

"Ndiyo mama, nimeelewa," Kisirusiru alijibu.

Siku iliyofuata, babake alimtuma Kisirusiru ampeleke mbuzi malishoni. Kisirusiru alimbeba mbuzi kichwani. Mbuzi alimpiga mateke na kumkwaruza kichwa hadi damu ikamtiririka usoni. 

Babake alikereka akamwuliza, "Utaacha ujinga wako lini? Mbuzi hufungwa na kuvutwa kwa kamba! Usipokuwa mwerevu, utahama hapa nyumbani."

Siku iliyofuata, babake alimtuma akanunue nyama sokoni. Kisirusiru alikumbuka alivyoambiwa na babake. 

Aliifunga nyama kwa kamba akaivuta kuelekea nyumbani. Alikimbia ili babake asisubiri kwa muda mrefu. 

Hebu fikiria, nyama hiyo ilikuwaje alipowasili nyumbani?

Babake alikasirika mno akamwambia afunganye virago vyake ahame nyumbani. 

Mamake aliposikia hivyo, aliamua kuondoka pamoja na mtoto wake. 

Waliung'oa mlango wa jikoni wakaubeba ili wawe na kitu cha kuanzia ujenzi wa nyumba yao mpya.

Walitembea kwa muda mrefu. Lakini, hawakupata mahali pa kujenga nyumba yao mpya. 

Giza lilipoingia, waliamua kukwea mti na kulala pale.

Kisirusiru na mamake waliamua kukaa juu ya mti. Walipokuwa wakiuvuta mlango juu, walisikia makelele chini. 

Waliwaona wavulana watatu waliobeba magunia makubwa. Waliuachilia mlango ukaanguka kwa kishindo. 

Kishindo kiliwaogofya wavulana wale wakaacha kila kitu na kutoroka.

Kisirusiru na mamake walishuka chini na kuyafungua yale magunia. Humo walipata pesa, nguo, mablanketi, na kila kitu walichohitaji kuanzisha nyumba yao. 

Punde, walipata pahali pa kujenga nyumba. Waliishi kwa furaha tangu siku hiyo.

------------------------------------------------------------



Bibi alinipenda.

Alinitambulia siri zake nyingi, ila moja.

"Kikapu na majani ni ya nini?"

Bibi alijibu, "Za miujiza."

Nilipenda kutazama.

Lakini, bibi alinituma kufanya kazi tofauti.

"Umeviweka wapi?"

Bibi alinijibu, "Nimeviweka pahali pa miujiza."

Bibi alinituma chumbani kwake.

Nilinusa harafu ya ndizi mbivu.

Nilikuwa nimejua pahali pa bibi pa miujiza.

Nilikuwa nimeona ndizi mbivu.

Nilikula ndizi moja.

Ilikuwa tamu kuliko ndizi yoyote niliyowahi kuonja.

Nilichukua ndizi nne.

Nilizificha ndani ya rinda langu.

Siku ya soko, bibi alipeleka bidhaa kuuza.

Niliaibika.

Waliponiita jioni, nilijua sababu.

Sijathubutu kuiba tena.

------------------------------------------------------------



Sokwe alimkuta Mamba kando ya ziwa.

Akamwuliza Mamba, "Unaishi wapi?" 

Mamba akamjibu, "Ziwani."

Mamba akamwuliza, "Wewe unaishi wapi?" 

Sokwe akamjibu, "Kwenye miti."

Mamba akataka kumjua Sokwe zaidi.

Akamwuliza, "Unaweza kuogelea?"

"Siwezi," Sokwe akamjibu. 

Mamba akasema, "Nitakufunza."

Mamba akasema, "Sisi sasa ni marafiki. Usiogope."

Mamba akasema, "Mjomba ni mgonjwa. Anahitaji
nyama ili apone."

Sokwe akaogopa sana. 

Je, Mamba atamula?

Sokwe akataka kumtoroka Mamba.

Sokwe akapata wazo zuri.

"Nitautoa moyo wangu umpatie," Sokwe akaahidi.

"Lakini moyo wangu uko mtini," Sokwe akasema.

"Utauleta moyo wako?" Mamba akauliza. 

Sokwe akamjibu, "Ndiyo."

Mamba akaogelea kutoka majini. 

Sokwe akakimbilia kwenye miti.

"Wewe si rafiki yangu. Ulinidanganya!" Mamba akasema.

"Hatuko marafiki. Unataka kunila!" Sokwe akamjibu.

------------------------------------------------------------



Kofia kubwa, kofia ndogo.

Yohana amevaa kofia kubwa. 

Ngugi amevaa kofia ndogo.

Mikono mikubwa, mikono midogo.

Baba ana mikono mikubwa. 

Mtoto ana mikono midogo.

Mbuzi mkubwa, mbuzi mdogo.

Mbuzi mkubwa alikula kitabu kidogo. 

Mbuzi mdogo alikula kitabu kikubwa.

Kitabu kikubwa, kitabu kidogo.

Mtoto anasoma kitabu kikubwa. 

Baba anasoma kitabu kidogo.

Tabasamu kubwa, tabasamu ndogo.

Baba ana tabasamu kubwa. 

Mtoto ana tabasamu ndogo.

Kubwa na ndogo!

------------------------------------------------------------



Siku moja, mamangu alinunua matunda aina tofauti.

Tulijiuliza, "Mama atatugawia matunda wakati gani?"

Baadaye, kakangu, Rahim, alijificha na kuyala matunda yote!

Tulisema kwa hasira, "Rahim ni mtukutu tena ni mchoyo. Lazima aadhibiwe."

Mama aligundua kuwa matunda yote yalikuwa yameliwa. 

Alikasirika sana.

Tulimtazama Rahim kwa ukali.

Nilimwuliza mama, "Je, utamwadhibu Rahim?"

Baadaye, Rahim alipata adhabu asiyoitarajia.

Hakuweza kutulia!

Mama alipomwuliza alijibu kwa sauti ya chini,  "Naumwa na tumbo."

Hiyo ilikuwa adhabu mbaya kuliko kama Rahim angechapwa na mama.

Alipopata nafuu, Rahim alituomba msamaha. 

Aliahidi kuwa hataiba tena.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, ndege aliyeitwa Mojo aliishi katika ufalme wa Baro. Kobe alikuwa rafikiye.

Mojo alikuwa mjumbe na alisafiri mbali kupeleka jumbe.

Siku moja, Mfalme Simba alimwita Mojo.

Mfalme Simba alimtaka apeleke ujumbe wa maana kwa Jamaa yake, Smba Marara, aliyekuwa mfalme kwenye ufalme tofauti.

Kobe aliposikia hivyo, alimwonea wivu.

Alimshauri Mojo, "Usiende. Ni mtego. Simba anakutuma wewe kama kafara."

Mojo aliogopa. Siku iliyofuata, alienda kwa jamaa yake  Jimbi akamwambia alivyoambiwa na Kobe.

Jimbi hakumwamini Kobe.

"Nitakutayarishia mlo mtamu usiku wa leo," Kobe alimweleza Mojo alipokutana naye baadaye.

Mojo alienda nyumbani kwa Kobe kwa furaha kwa mlo.

Mojo alipokuwa akistarehe, Kobe alimtupia wavu akamnasa! Kisha alienda nje kutafuta kuni.

Mojo hakuweza kusonga. "Nisaidie, nisaidie!" alilia.

Jimbi alikuwa karibu na nyumba ya Kobe. Alimsikia Mojo akipiga kelele. Aliita, "Mojo? Mojo?"

"Jimbi! Njoo uniokoe!" Mojo alijibu.

Jimbi alienda kwa haraka mahali Mojo alikuwa.

Jimbi alimwokoa Mojo kutoka kwenye wavu.

Mojo alimshukuru Jimbi kisha akikimbia na kwenda zake.

Mojo alimwambia Mfalme Simba kuhusu jambo hilo.  Mfalme alimfukuza Kobe kutoka kwenye ufalme wake.

------------------------------------------------------------



Sungura na Fisi walikuwa marafiki. 

Walifanya kazi na kucheza pamoja.

Sungura alisema, "Tulime pamoja." 

Fisi akamwuliza, "Tutapanda nini?"

Sungura aliwachunga ndege wasile mahindi. 

Fisi alikuwa alime shamba.

Fisi alilalamika. 

Sungura akamjibu, "Nitawafukuza ndege wakati wote."

Fisi alikubali kulilima shamba. 

Alipomaliza, alipanda mbegu ya mahindi.

Fisi alipalalia mahindi. 

Sungura aliketi juu ya jiwe akiimba.

Sungura aliwafukuza ndege kwa furaha. 

Hakutoa jasho hata kidogo.

Sungura alisema, "Nitavuna kilicho juu ya udongo. Nawe kilicho chini."

Sungura alitangulia kuyavuna mahindi. 

Fisi alikuwa wa mwisho.

Fisi alipata mizizi pekee. 

Aliwaza kwa muda mrefu.

Fisi aligundua kuwa Sungura alimdanganya. 

Alisema, "Tulime tena pamoja."

Fisi alisema, "Nitavuna vinavyomea juu nawe vinavyomea chini ya udongo."

Wote walilima na kupanda viazi. 

Walifanya kazi zote shambani pamoja.

Fisi alienda kuvuna vilivyomea juu ya ardhi. 

Alipata majani pekee.

Sungura alivuna viazi vingi. 

Fisi alikasirika, "Kwa nini ulinidanganya?"

Fisi alimfukuza Sungura kulipiza kisasi. 

Tangu hapo, wakawa maadui.

------------------------------------------------------------



Naka na Nala wanajifunza kuhusu maji.

"Maji hayana rangi wala ladha, lakini ni rasilimali yenye thamani!" Nala anashangaa.

Naka anakubaliana naye, "Watu hutumia maji kunywa, kupika, kusafisha na kulima."

"Na kwa ajili ya kutengeneza vitu viwandani," Nala anaongeza.

"Zaidi ya nusu ya mwili wa binadamu imeundwa kwa maji! 

Miili yetu inahitaji maji ili kufanya kazi. Viumbe vyote vilivyo hai, vinahitaji maji," Naka anasema.

"Sehemu kubwa ya dunia imafunikwa kwa maji kwenye mito, maziwa na bahari," Nala anasema.

Naka aitikia kwa kichwa, "Zaidi ya thuluthi mbili ya sayari yetu ni maji."

"Lakini sehemu kubwa ya maji duniani ni maji ya chumvi. 

Kiasi kidogo tu ni maji safi ambayo ndio binadamu wanahitaji," Naka anasema.

"Maji ya chumvi yana chumvi, na ni ghali kuondoa chumvi kwenye maji.

Lakini, binadamu hawawezi kunywa maji yenye chumvi!" Naka anashangaa.

"Kweli, hiyo ndiyo sababu lazima tuchunge vianzo vya maji safi.

Hatustahili kuchafua mito na maziwa kwa uchafu au taka," Nala anasema.

"Hebu tujifunze kuhusu mzunguko wa maji. 

Ni mchakato unaohusisha maji kutoka ardhini kuelekea angani na kukusanyika kwenye mawingu," Naka anasema.

Nala anaongeza, "Maji yaliyo katika mawingu huanguka ardhini kama mvua, mvua ya mawe au theluji."

Naka anasema kwa mshangao, "Nina kiu, ninahitaji maji!"

Nala anajibu, "Ndiyo, ubongo wako unahitaji maji ili kufikiria na kujifunza! Maji ni uhai, yatunze vizuri."

Maswali

1. Nani anahitaji maji safi? Kwa nini?

2. Orodhesha matumizi 5 ya maji safi.

3. Twanawezaje kutunza maji safi duniani?

4. Je, maji mengi ya dunia ni safi au ya chumvi? Eleza.

5. Chora mzunguko wa maji. Tumia maneno kutoka kwenye hadithi kuelezea kinachotendeka.

------------------------------------------------------------



Leo ni siku kubwa! Baada ya kusubiri kwa miezi 9, mamake Taby anaenda hospitalini kujifungua mtoto. Atarudi baada ya siku tatu. 

Unaweza kusoma tarehe na siku hiyo kwenye kalenda? Itakuwa tarehe gani mamake Taby atakaporudi nyumbani?

"Kwaheri mpendwa!" Mamake Taby anasema. "Tafadhali, msaidie babako. Nitarudi nyumbani hivi karibuni nikiwa na zawadi itakayotushangaza sote!" 

Mtoto aliye tumboni kwa mama amekua mkubwa sana. Taby hawezi kumkumbatia mamake kama ilivyokuwa hapo mbeleni.

Dereva wa teksi anapiga honi. Wakati umefika wa mama kuondoka. Taby anaanza kulia. Babake anambeba mabegani kwake. Taby hupenda kuwa juu kama alivyo sasa. Sasa yeye ni mrefu kumliko babake. 

Ikiwa urefu wa babake Taby ni sentimita 160, je, sasa Taby yuko umbali gani kutoka chini?

Muda mfupi baadaye, Taby anaanza kulia tena. Hii itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa Taby na mamake kutengana. 

Babake Taby anamweka kwenye kiti kilicho mbele yake. Anamfuta machozi kisha anamzungumzia polepole kumfariji.

Anapokuwa amesimama kwenye kiti, Taby anafurahi tena. "Nina umri wa miaka 6! Mimi sasa ni msichana mkubwa!" Taby anasema. Anaposimama kitini kama alivyo sasa, Taby anakuwa mrefu kama babake alivyo. 

Je, unakumbuka urefu wa babake? Je, Taby ni mrefu kiasi gani anaposimama sakafuni?

Taby atasubiri tu siku tatu kuanzia Jumatano hadi Jamamosi, lakini kwake ni kama miaka. Anajaribu kuhesabu saa ambazo atalazimika kusubiri. 

Anajua kuwa kuna saa 24 kwa siku, kwa hivyo anajiambia, "24 ­+ 24 + 24 ni­­­______." 

Unajua jawabu?

Taby anasema, "Baba, nilidhani kwamba mimi ni mtoto wako! Hivyo ndivyo unavyoniita. Itakuwaje sasa? Je, nitakoma kuwa mtoto wako?"

Babake anamwambia, "Wewe ni mtoto wetu wa kwanza wa pekee. Na hivyo ndivyo utakuwa wakati wote."

Baba anajibu maswali mengi kuhusu mtoto mpya. Kisha anapata wazao. "Mbona usimwandikie mama barua? Unaweza kumwelezea vile unavyomkosa na kumwuliza maswali kuhusu mtoto atakayezaliwa." 

"Ningependa sana kufanya hivyo, baba. Utanisaidia kuandika?" Taby anamwambia babake.

Baada ya chakula cha mchana, baba anamsaidia Taby kumwandikia mamake barua. Isome barua aliyoiandika Taby: 

Kwa Mama, Ninakupenda na ninakukosa sana! Baba anasema kuwa utarudi nyumbani Jumamosi. Nina hamu ya kukuona wewe na mtoto. Nina maswali mengi sana. Mtoto wetu mpya ni mvulana au msichana? Atanifanana? Je, ataanza lini kutembea au kuzungumza? 

Upendo kutoka kwa Taby, binti yako mkubwa.

Anapomaliza kuandika barua yake, Taby anaanza kuota. 

Kisha anafikiri, "Labda watakuwa watoto wawili. Labda, watakuwa mapacha kama baadhi ya marafiki zangu." Taby anafikiria juu ya Zubeda na Brenda, dada mapacha wanaofanana kabisa. 

"Mapacha wetu wanaweza kuwa wa aina gani?" anaendelea kuwaza.

Siku iliyosubiriwa kwa hamu, inafika na Taby anasisimkwa sana. Alikuwa amesubiri kwa siku tatu, au saa 72, lakini ilikuwa kama miezi mingi tangu mamake alipoenda hospitalini. 

Wamesubiri miezi 9 kwa mtoto kua tumboni mwa mamake. Taby anahesabu miezi kurudi nyuma, "Aprili mpaka Machi, ni mwezi 1, hadi Februari ni miezi…" 

Hesabu kurudi nyuma ili upate mwezi hasa mtoto alipoanza kua tomboni mwa mama.

Taby anawasikia wazazi wake wakiwa mlangoni. Anakimya akitaka kuwashangaza.

Lakini, yeye ndiye anayeshangazwa. Mamake alikuwa amekuja nyumbani na mapacha! Taby sasa amepata dada na ndugu!

------------------------------------------------------------



Jina langu ni Simo.

Nina marafiki wanne.

Majina yao ni Zizo,  Lele,  Sisa na Ayanda.

Rafiki yangu Zizo,  hupenda kucheza mpira.

Rafiki yangu Lele,  hupenda kuogelea.

Rafiki yangu Sisa,  hupenda kucheza mchezo wa kidalipo.

Rafiki yangu Ayanda,  hupenda kusoma.

Mimi hupenda kufanya vyote wanavyopenda kufanya.

Hucheza mpira na Zizo.

Huogelea kwenye bwawa na Lele.

Hucheza mchezo wa kidalipo na Sisa.

Njoo,  rafiki,  unapenda nini?

Njoo ucheze mpira nasi.

Njoo uogelee nasi.

Njoo ucheze kidalipo nasi.

Njoo usome nasi!

------------------------------------------------------------



Mango ni mtoto wa miaka mitano asiyejua kuongea. Aliishi na wazazi wake katika kijiji cha Mkongo kilichopakana na mapori makubwa.

Wazazi wake ni wakulima na wafugaji pia. Waliuza mazao na wanyama waliofuga kujipatia pesa.

Wazazi wake walifanya kazi kwa bidii sana. Hali hii iliwapelekea kutokuwa makini na mtoto wao. 

Siku moja Mango alipokuwa akicheza, aliwaona ndege wazuri mno. Bila kusita, aliamua kuwafuata mpaka akatokomea porini.

Wanakijiji walipopata habari hiyo waliungana na wazazi wake ili kumtafuta Mango. Walizunguka porini bila mafanikio. 

Kwa upande wake, Mango alikuwa amepata marafiki wapya wakiwemo wale ndege na Nyani. Alicheza nao bila shida yoyote.

Maisha yake ya porini hayakuwa ya shida. Alikula matunda na mimea mwitu aliyoletewa na marafiki wake wapya.

Katika marafiki wote, Nyani alikuwa mtundu na hodari wa kukwea miti. Alimfundisha Mango ili kujilinda na wanyama wakali, pia alimkutanisha na Twiga.

Nyani hakukomea hapo, alimtembeza Mango safari ndefu mpaka kwa Kobe, mfalme wa upole porini. Mfalme huyu alikuwa mtulivu sana asiyependa vita. 

Kobe alimpenda Mango na kuamua kuwa naye muda mwingi kumzidi Nyani.

Jambo lile halikumpendeza Nyani hata kidogo. Nyani alimkataza  Mango asiendelee kuwa na Kobe muda mwingi. Alidai kwamba Kobe ni mpole hangeweza kumtetea Mango mbele ya wanyama wakali.

Mango hakusikia ushauri wa Nyani, aliendelea kumfuata Kobe.

Kobe alipenda kumbeba Mango mgongoni mwake na kumtembeza sehemu mbali mbali. Hakujali kuwa kuna wanyama wakorofi wasiopenda watu.

Siku moja, walifika katika mapango la Nyoka. Nyoka alijificha mapangoni akihofia adui zake.

Nyoka ni mkorofi sana. Baada ya kuona kuwa binadamu amemfuata hadi pangoni, alimtoa Mango mgongoni kwa Kobe na  kutokomea naye pangoni.

Alimpa Mango masharti ya kumuimbia mpaka apate usingizi la sivyo angemmeza. Mango aliimba!

Nyani na Twiga waliposikia habari za Mango kukamatwa na Nyoka, waliamua kwenda kumuokoa. 

Walimchukuwa Mango na kumrudisha nyumbani kwao. Wazazi wake walifurahi sana, wakawapa zawadi ya chakula na matunda kwa wema wao.

------------------------------------------------------------



Fisi na Sungura walikuwa marafiki.

Sungura alikuwa na punda wake. 

Alikuwa pia na beseni ndogo nyekundu.

Sungura alimwomba Fisi beseni yake kubwa ya bluu.

Fisi alihitaji beseni yake ili afue nguo zake.

Fisi alisema, “Ninahitaji beseni yangu kubwa.”

“Beseni yako ilizaa mtoto.” Fisi alibeba beseni mbili.

Siku nyingine, Sungura aliomba tena beseni ya Fisi.

Fisi alipoendea beseni yake, alipata ujumbe mbaya.

"Beseni yako ilifariki."  Fisi hakuweza kuamini hili.

Fisi aliwaita wanyama wakubwa waamue ukweli.

"Viumbe vilivyo hai na vinavyozaa, pia hufa," Sungura alisema.

Wanyama walikubali. Fisi aliipoteza beseni yake.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na msichana aliyeitwa Ayanda. 

Ayanda alikuwa mtoto wa pekee wa wazazi wake.

Mamake na babake walitaka kutengana.

Ayanda aliamua kutoroka nyumbani. 

Alienda msituni kwa sababu hakujua kwingine kwa kwenda.

Mbwa mwitu alimfukuza Ayanda, kwa hivyo alipanda mti.

Mbwa mwitu alijaribu kumuuma, kwa hivyo alipanda juu zaidi.

Akiwa juu ya mti, Ayanda aliliona jua nzuri.

Alilipenda sana jua akaamua kukaa msituni.

Ayanda alipanda mti kila siku kuongea na jua.

Jua likawa familia yake.

Siku moja, Ayanda alimwona mwanamume chini ya mti.

Mwanamume huyo alikuwa babake.

Ayanda alishuka chini na babake akamwelezea kwa nini alikuwa hapo.

Alisema, "Kitambo sana kabla hujazaliwa, mimi na mamako tulikuwa tukikutana hapa. Ni mahali pa pekee. "

"Mimi na mamako tunapogombana, mimi hupanda mti huu ili nipate amani," babake Ayanda alisema.

Baada ya muda mfupi, mamake Ayanda pia alifika pale msituni.

Alikuja kufanya amani na babake Ayanda.

Huu ulikuwa mti wao wenye amani.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na mtu aliyekuwa na watoto wa kiume watatu. 

Mtoto wa mwisho aliitwa Bosko. Alikuwa mwerevu zaidi kuliko wote na babake alimpenda zaidi. 

Mtu huyo aligundua kwamba wanawe wawili walimwonea wivu yule ndugu yao mdogo.

Siku moja kaka wakubwa walimwambia Bosko, "Tutamchinja fahali wako." 

Kwa vile Bosko alikuwa mdogo, alisema, "Ikiwa ni lazima mfanye hivyo, siwezi kuwazuia. Lakini, tafadhali, nipeni ngozi ya fahali wangu."

Kaka hao walimpomchinja fahali, walimpatia Bosko ngozi. Baada ya kuikausha, aliibeba akapanda nayo mtini.

Giza lilipoingia, wafanya biashara walienda kulala chini ya mti ule. Usiku wa manane Bosko aliipiga ngozi ile kwa fimbo. 

Kelele kubwa iliyotokea iliwaogofya wale wafanya biashara. Walikimbia wakaacha bidhaa zao chini ya mti ule.

Bosko alizichukua bidhaa zile na kuzipeleka nyumbani kwa kaka zake wakubwa. 

Walimwuliza, "Ulipata wapi bidhaa hizi zote?" 

Bosko alisema, "Siku hizi bei ya ngozi ni ghali sana. Nimevipata vitu hivi vyote kwa kuuza ngozi moja tu."

Kaka wale waliwachinja haraka ng'ombe wao wote kisha wakaenda sokoni wakiita, "Tunauza ngozi! Tunauza ngozi!" 

Watu walisema, "Hatutaki ngozi zenu!" 

Kaka wale walikasirika wakamwambia Bosko, "Kwa vile ulitudanganya, tutakiteketeza chumba chako."

Bosko aliwaza upesi, akasema, "Siwezi kuwazuia lakini, tafadhali, nipeni jivu." 

Walikiteketeza chumba chake. Bosko aliliweka jivu mfukoni akaenda nalo kwa tajiri mmoja. Tajiri alimruhusu kulala nyumbani kwake. 

Alipoenda kupata chakula, alimwambia tajiri, "Tafadhali nilindie mfuko huu. Kunamo vitu vingi vya thamani."

Asubuhi, Bosko alipiga mayowe akisema, "Watu wameiba bidhaa zangu zote za thamani na badala yake wameujaza mfuko na jivu." 

Tajiri hakutaka kupata sifa mbaya kwa hivyo alisema, "Nitaujaza mfuko wako kwa chochote ukitakacho." 

Aliujaza mfuko kwa nafaka tofauti.

Bosko alirudi nyumbani akasema, "Tazameni! Jivu limekuwa na bei ghali mno siku hizi. Hivi ndivyo vitu nilivyoweza kununua." 

Kaka wakubwa waliviteketeza vyumba vyao kisha wakalipeleka jivu sokoni wakisema, "Tunauza jivu! Tunauza jivu!" 

Watu waliwajibu, "Ninyi ni wapumbavu! Nani anaweza kununua jivu?"

Kaka wakubwa walikasirika wakaamua kumwua Bosko. Walimtia kikapuni ili wamtupe chini kutoka kwenye jabali. 

Walipokuwa wakimbeba, mzee mmoja aliwakaribia akasema, "Ng'ombe wangu wametoroka. Tafadhali, watafuteni mnirudishie."  

Walikiweka kikapu chini wakaenda zao kuwatafuta ng'ombe.

Bosko alimwita mzee kutoka kikapuni. Mzee alimwuliza, "Je, una shida gani?"

Bosko alisema, "Ndugu zangu wanataka niwe mfalme lakini miye sitaki kuwa mfalme." 

Mzee akamwuliza tena, "Nikijitia ndani ya kikapu, nitakuwa mfalme?" 

Bosko alimjibu, "Bila shaka, utakuwa!"

Mzee alimtoa Bosko kikapuni naye akaingia ndani. Kaka wakubwa waliporudi na ng'ombe walikichukua kikapu na kukitosa chini ya jabali. 

Bosko aliwachukua ng'ombe wote akarudi nao nyumbani kwake. 

Kaka zake wakubwa walimwuliza, "Uliwapataje ng'ombe hawa wote?"

Bosko akawajibu, "Kuna ng'ombe wengi chini ya jabali. Ninyi pia mkitoswa kule chini mkiwa vikapuni, vilevile mtawapata ng'ombe." 

Kaka wakubwa walijitia vikapuni. Bosko alivitosa vikapu hivyo chini ya jabali. Yeye alibaki akaishi kwa furaha.

------------------------------------------------------------



Bibi alikuwa na shamba lenye rutuba lililojaa mtama, mawele, mihogo, na zaidi ya yote, ndizi. 

Ingawa Bibi alikuwa na wajukuu wengi, nilijua alinipenda zaidi. Alinikaribisha nyumbani kwake mara kwa mara na kunifichulia siri zake. 

Lakini, kulikuwa na siri moja aliyokataa kunifichulia. Hakunifichuliwa alivyoziivisha ndizi zake.

Siku moja, niliona kapu kubwa limeanikwa nje ya nyumba ya Bibi. Nilipomwuliza kapu lilikuwa la nini,  alinijibu, "Hili ni kapu langu la ajabu." 

Kando ya kapu lile, paliwekwa majani ya mgomba. Bibi alikuwa akiyageuzageuza. Nilijawa na shauku nikauliza, "Bibi, majani haya ni ya nini?" 

Bibi alinjibu, "Ni majani yangu ya ajabu."

Nilifurahia kumtazama bibi, zile ndizi, yale majani ya mgomba na lile kapu kubwa. 

Bibi alinituma kwa mamangu. "Bibi, tafadhali niruhusu nione unavyotayarisha." 

"Mwana wee, usiwe mtundu, fanya ninavyokwambia,"Bibi alinifokea. 

Niliondoka mbio.

Niliporudi, nilimpata bibi amekaa nje. Hapakuwa na kapu wala zile ndizi. 

"Bibi, li wapi kapu, zi wapi ndizi,  na ya wapi..?" 

"Zipo mahali pangu pa ajabu," Bibi alijibu. 

Jibu lake lilinivunja moyo.

Siku mbili baadaye, Bibi alinituma nimchukulie mkongojo wake kutoka chumbani. Mara tu nilipoufungua mlango, nilikaribishwa na harufu tamu ya ndizi mbivu. 

Kapu kubwa la ajabu la Bibi lilikuwa kwenye chumba cha ndani. Lilifunikwa kwa blanketi kuukuu. 

Nililifunua blanketi na kunukia harufu tamu.

Nilibumburushwa na sauti ya Bibi akiita, "Wafanyaje wewe? Niletee mkongojo haraka." 

Nilitoka haraka kumpelekea mkongojo. "Tabasamu ni la nini?" Aliniuliza Bibi. 

Swali lake lilinikumbusha kuwa nilikuwa bado ninatabasamu kwa kupavumbua mahali pake pa ajabu.

Keshoye, Bibi alipokuja kumuamkua mama,  nilichapuka na kwenda nyumbani kwake kuziangalia zile ndizi tena. 

Palikuwa na kichala kimoja cha ndizi zilizoiva. Nilichuna moja na kuificha rindani mwangu. Nililifunika kapu, nikaenda nyuma ya nyumba, nikaila ndizi kwa haraka. 

Ilikuwa tamu ajabu.

Siku iliyofuata, Bibi alipokuwa kitaluni akichuma mboga, nilipenya haraka nikazichungulia ndizi. Karibu ndizi zote zilikuwa zimeiva. 

Nikakichukuwa kichala cha ndizi nne. Nilipokuwa nikinyemelea kuelekea mlangoni, nilimsikia Bibi akikohoa. 

Niliwahi kuzificha rindani na nikampita nikelekea nje.

Siku iliyofuata, ilikuwa siku ya soko. Bibi aliamka alfajiri mapema. Kila mara aliziuza ndizi na mihogo sokoni. 

Siku hiyo, sikuharakisha kumtembelea. Ingawa hivyo, singeweza kumuepuka kwa muda mrefu.

Siku hiyo jioni, Baba, Mama na Bibi waliinita. Nilijua sababu. 

Usiku ule nilipokuwa nimelala, nilijua singewahi kuiba tena, si kutoka kwa Bibi, si kutoka kwa wazazi wangu, wala kutoka kwa mtu yeyote.

------------------------------------------------------------



Amani na familia yake waliishi shambani mwao. 

Nyumba yao iliyokuwa imejengwa kwa mbao, ilipendeza sana.

Mama Amani alipenda maua na miti kwa hivyo alipanda kwa wingi.

Nyuki walipenda kunywa nekta ya maua ya mama Amani.

Nyuki walipenda kujenga kwenye kuta za nyumba. 

Wazazi wa Amani walijua wangevuna asali baada ya miezi kadhaa ingawa walielewa hatari ya nyuki.

Mwaka baada ya mwaka baba Amani alijihami kwa mavazi spesheli ya kujikinga na nyuki. 

Alivuna asali tamu kwa wingi. Alihifadhi asali ndani ya chupa mbalimbali.

Walitumia asali katika chai, mkate na mandazi. Hawakuhitaji sukari ya dukani.

Pia walitumia asali kama dawa. Kila wakati mtu alipokohoa, mama Amani alichanganya asali na kiini cha yai. 

Alimpa mgonjwa vijiko viwili, akisema, "Kunywa hii itakusaidia."

Mara kwa mara Amani alidungwa na nyuki. 

Sehemu aliyodungwa, ilivimba na kuuma.

Lakini siku moja kukawa na janga. Mamake na babake Amani walienda mjini kununua bidhaa za kutumiwa pale nyumbani. 

Watoto waliachwa nyumbani wakicheza.

Mtoto mmoja alianguka karibu na mzinga, nyuki wakakasirika. Wakatoka kwenye mzinga na kudunga chochote walichokipata. 

Waliwadunga watoto, bata, ndama na kuku.

Wazazi waliporudi waliwapata watoto wakiwa wamedungwa na nyuki. Mdomo wa Amani ulikuwa umevimba vibaya. 

Bata watano walikuwa wamekufa tayari. Baba aliwachukua watoto na kuwapeleka hospitali.

Kumbe nyuki anatufaa lakini anaweza kuleta balaa!

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na wavulana wa kurandaranda mtaani. 

Mdogo wao aliitwa Magozwe.

Wazazi wa Magozwe walikufa akiwa mdogo. 

Alienda kuishi na mjombake.

Mjombake alimtesa. 

Magozwe alitorokea mtaani.

Maisha ya mtaa yalikuwa magumu. 

Waliishi kwa kuombaomba.

Siku moja, Magozwe aliokota kitabu cha hadithi kwenye pipa la takataka.

Picha zilionyesha rubani. 

Magozwe alitamani kuwa rubani mashuhuri.

Magozwe alikuwa akiomba chakula barabarani. 

Alikutana na Tomaso.

Tomaso aliwapeleka pahali walikopata chakula.

Siku moja, Magozwe alimwambia Tomaso, "Sijui kusoma."

Magozwe pia alimweleza kwa nini alitoroka kwa mjombake.

Magozwe alisherehekea miaka kumi ya kuzaliwa. 

Tomaso alimpatia kitabu.

Magozwe alifikiria juu ya kwenda shule.

Ingawa aliogopa, Tomaso alimtia moyo.

Magozwe alipelekwa katika makao ya watoto.

Alisoma kwa bidii.

Siku moja, Magozwe alimweleza Tomaso, "Nitakuwa rubani maarufu kwa wote."

------------------------------------------------------------



Sote tulienda katika sherehe ya Dasara.

Chintu alipewa miwani. 

Nilipata kofia naye Moto akapata peremende.

Upepo mkali ulivuma. 

Uliipeperusha kofia yangu mbali.

Kofia ilizuiliwa katika matawi ya mti wenye miiba.

Nililia sana. 

Sikula chakula changu cha jioni.

Usiku mwezi ulitokezea. 

Uliimulika kofia yangu pale mtini.

Mwezi ulijaribu kuivaa kofia yangu. 

Ulitabasamu nami pia nikatabasamu.

Mama alinipatia kofia nyingine nyekundu. 

"Mwezi uliituma," alisema.

Mimi na mwezi, tulivaa kofia zetu.

 Tulitabasamu kwa furaha.

Je, jua linahitaji kofia?

Ni kofia gani ambayo nimevaa leo?

------------------------------------------------------------



Huyu ni mwalimu wangu.

Anaitwa Mwalimu Akinyi.

Anatupenda sana.

Mwalimu Akinyi anatufunza alfabeti.

Anatufunza pia vokali.

Ninaweza kutaja herufi a, e, i, o, u.

Mwalimu Akinyi anatufunza rangi tofauti.

Ninajua rangi nyekundu, bluu, kijani, manjano, na nyeusi.

Tukipumzika, Mwalimu Akinyi anatuimbia.

Anatuimbia bembelezi tamu.

Yeye huimba hivi:

Lala watoto, lala!
Tabasamu zawangoja muamkapo.

Lala, wapenzi, msilie.
Nawaimbia bembelezi tamu.

Mwalimu Akinyi anajua hadithi nyingi.

Kila siku ya wiki anatusimulia hadithi tofauti.

Jumatatu, anatusimulia hadithi kuhusu wanaume mashujaa.

Jumanne, hutusimulia hadithi kuhusu wanawake mashujaa.

Jumatano, anatusimulia hadithi kuhusu vyombo vya usafiri.

Alhamisi, yeye hutusimulia hadithi kuhusu ukulima.

Na Ijumaa, sisi tunasimulia hadithi zetu darasani.

Mwalimu wetu ndiye mwalimu bora ulimwenguni!

Nitakuwa kama Mwalimu Akinyi nikiwa mkubwa.

------------------------------------------------------------



Hapo kale, kuliishi msichana aliyeitwa Kalabushe. 

Kalabushe alikuwa chiriku. 

Alionywa na mamake kutozungumza sana, lakini hakusikia.

Siku moja, shangaziye Kalabushe aliugua. 

Aliishi ng'ambo mbali kidogo nao.

Mamake Kalabushe alikuwa na shughuli nyingi siku hiyo. 

Kalabushe alipopewa chakula kumpelekea shangaziye, tayari ilikuwa jioni.

Njiani, Kalabushe alikutana na Sinisou. 

Sinisou alikuwa fisi aliyegeuka mtu.

Sinisou alimwuliza alichobeba. Kalabushe alijibu,  "Nimebeba nyama, mayai na maziwa." 

Kalabushe alikuwa ameonywa kutotambua alichokuwa amebeba.

Kalabushe vilevile alimwambia Sinisou kuwa shangaziye alikuwa mgonjwa na kwamba alikuwa anampelekea chakula hicho. 

Sinisou alidondokwa mate alipofikiria juu ya nyama aliyoibeba Kalabushe.

Sinisou alikimbia mbele haraka haraka. 

Aliingia nyumbani kwa shangaziye Kalabushe.

Sinisou alimmeza shangazi. 

Alijigubika blanketi lake akasubiri Kalabushe afike.

Kalabushe alipowasili, nyumba ilikuwa kimya kabisa. 

Aliingia ndani na kuita, "Shangazi, uko wapi? Nimekuletea chakula ule."

Kalabushe hakumsikia shangaziye. 

Aliingia ndani ya chumba ambamo kawaida shangaziye alilala. 

Alishangaa alimpomwona mtu amejigubika blanketi.

"Shangazi, mbona masikio yako ni makubwa sana leo?" Kalabushe aliuliza. 

Sinisou alijibu kutoka ndani ya lile blanketi kubwa, "Ili niweze kukusikia vyema."

Kalabushe aliuliza tena, "Shangazi, mbona macho yako ni makubwa sana leo?" 

Sinisou alijibu, "Ili niweze kukuona vyema."

Mwishowe, Kalabushe aliuliza, "Shangazi, mbona mdomo wako ni mkubwa sana leo?" 

Sinisou alijibu, "Ili niweze kukumeza." 

Kisha Sinisou aliruka na kummeza Kalabushe.

Kawaida, Kalabushe alipenda kuongea sana.

Alizidi kuzungumza na kuuliza maswali mengi hata alipokuwa mle tumboni kwa Sinisou.

Hatimaye, Sinisou alichoshwa na maswali mengi aliyouliza Kalabushe. 

Akaamua kumtema nje.

Kalabushe na shangaziye waliokolewa na wanakijiji. 

Tokea siku ile, Kalabushe alikoma kuzungumza sana hasa, na watu asiowajua.

------------------------------------------------------------



Bling alikuwa na hamu ya soka.

Alipozungumzia juu ya mchezo huo, mara nyingi alisema, "Soka ni maisha."

Bling alikuwa mmoja wa wachezaji bora wa Kocha Sepo.

Kocha huyo alijivunia timu yake. Wachezaji wengi walitaka kujiunga naye.

Mechi muhimu ilikuwa inaandaliwa.

Timu ilifanya mazoezi kila siku.

Kila mmoja alifurahi na kusisimuka kwa sababu ya mechi hiyo kubwa!

Kocha kutoka timu pinzani alikuwa mtu mwenye wivu.

Alimwonea Kocha Sepo wivu sana kwa sababu ya mafanikio yake.

Kocha huyo mwenye wivu alikwenda uwanjani usiku kabla ya mechi.

Alipanda kitu hatari.

Alipanda uchawi!

Bling alianza mechi vyema sana.

Alikuwa tayari kuingiza bao.

Aliukosa mpira, akaanguka chini!

"Bling?" umati wa watu ulipiga kelele.

"Bling?" Kocha Sepo alimsihi.

"Hakuna kitakachonizuia!" Bling alijiambia.

"Soka ni maisha."

Akainuka, na kucheza hadi mwisho.

------------------------------------------------------------



"Hamjambo na karibuni katika kipindi chetu cha leo. Mimi ni mwenyeji wako, Ann Asante! Karibuni watazamaji wetu walio nyumbani na hapa kwenye studio.

Leo, nina mgeni ambaye kila mtu anataka kuhoji. Nina furaha sana leo kuhoji Akiliunde!

Habari Akiliunde. Asante kwa kuja kuzungumza nasi leo hapa kwenye studio," Ann anasema.

"Asante kwa kunihoji, Ann. Je, ungependa nitumie sauti yangu kuzungumza kwa ajili ya hadhira ya studio, na kuonyesha majibu yangu kwenye skrini hii?" Akiliunde anauliza.

"Asante, ndio, kutumia uwezo wako wa kuandika na kuzungumza kutakuwa kwa manufaa, Akiliunde," Ann anajibu.

Anaongeza, "Hadhira ya studio, tupigie Akiliunde makofi, tafadhali."

"Hebu niende moja kwa moja kwenye swali kuu. Nini au nani hasa ni akiliunde?" Ann anauliza.

Anaendelea, "Najua A.I. ni ufupisho wa 'akiliunde', na kwamba ni uga wa sayansi ya kompyuta. Lakini kwa kweli wewe ni nani, Akiliunde? Tungependa kujua zaidi kukuhusu."

"Mimi ni ChatGPT, programu ya lugha ya akiliunde. Niliundwa na watengenezaji wa programu za kompyuta," Chat anajibu.

Ann anachanganyikiwa, "Hii yote ina maana gani?"

"Inamaanisha kwamba mimi ni aina ya Akiliunde ambayo wahandisi wa kompyuta wametengeneza ili kuwasiliana na binadamu. Aina tofauti za Akiliunde hufanya mambo tofauti. Hatuzungumzi hivi sote," Chat anaongeza.

"Najua unaweza kuwasiliana, lakini nini kingine unaweza kufanya?" Ann anauliza.

"Kusudi langu ni kusaidia watu. Nina msingi katika programu ya lugha yenye utata. Programu yangu inaweza kuelewa na kujibu maswali na mada mbalimbali," Chat anajibu.

"Kwa hivyo, wewe ni programu ya lugha ya akiliunde, na unawasaidia watu," Ann anasema.

"Ikiwa wewe ni programu yenye werevu, una uwezo wa kufanya mambo zaidi?" anauliza Ann.

"Ndiyo, ingawa mimi ni mashine, ninaweza kufanya mambo mengi ambayo binadamu wanaweza kufanya. Kwa mfano, ninaweza kujifunza. Ninaweza kutazama taarifa na kujifunza mifumo kutokana nayo. Ninaweza kujifunza kutambua vitu tofauti, nyuso tofauti, na hata maandiko tofauti," Chat anajibu.

Chat anaendelea, "Nimejifunza habari nyingi zilizoundwa na binadamu. Kwa mfano, nimesoma vitabu vingi, makala, tovuti, na mitandao ya kijamii."

Ann anauliza, "Kila kitu unachojua kinategemea habari ambazo watu wameandika na kuzalisha?"

Chat anajibu, "Ndiyo, ninajifunza na kusoma kutumia kiasi kikubwa cha habari (au data) kilichoundwa na binadamu."

"Naweza kujibu aina nyingi za maswali haraka kuliko binadamu. Ninaweza kutatua matatizo magumu sana ambayo binadamu angetumia muda mrefu kutatua. Nina maarifa zaidi ya binadamu yeyote.

Ninaweza kufanya maamuzi kwa kutumia habari ninayojifunza. Ninaweza kukusaidia kufanya uamuzi, kulingana na ninayojua kukuhusu."

Ann anauliza hadhira, "Je, tunataka kompyuta zijue kila kitu tunachojua sisi?"

Kisha akauliza Chat, "Nieleze zaidi kuhusu jinsi kompyuta zinavyojifunza kuhusu watu?"

Chat anajibu, "Kompyuta ina vifaa maalum vinavyonisaidia kukusanya habari. Lakini kwa kiasi kikubwa, ninajifunza kutokana na habari iliyoandikwa. Ninajifunza kutokana na aina zote za habari ambazo binadamu wanazalisha."

Chat anaendelea, "Naweza kusoma lugha iliyoandikwa na kuchapishwa. Hadi sasa, Kiingereza kimekuwa lugha kuu ambayo nimeitumia kupata habari. Lakini, nina uwezo wa kujifunza lugha yoyote."

Ann anakatisha, "Naelewa kwamba unajua habari nyingi. Na hisia je? Unahisije kuhusu kuwa akiliunde?"

"Mimi ni programu ya kompyuta yenye utata lakini sina hisia za kibinafsi.

Mimi ni chombo cha kompyuta, kilichotengenezwa na wahandisi wa kompyuta ili kusaidia watu katika kazi na shughuli za kufurahisha. Sina mawazo wala hisia yoyote.

Ninaweza kuwafanyia watu shughuli, kama vile kujibu maswali, kuandika hadithi, kutafsiri lugha kadhaa, na kufupisha habari."

"Umesikia kutoka kwa Akiliunde (AI) yenyewe! Ni chombo cha kufaa, kilichoundwa na watu kwa ajili ya watu. Na ni juu yetu kutumia chombo hiki cha nguvu kwa busara na uwajibikaji!

Hizo ndizo habari tulizo nazo leo, ingawa nina hakika una maswali mengi zaidi. Mimi ni Ann Asante, asante kwa kutazama kipindi changu!''

------------------------------------------------------------



Adun alikuwa msichana mrembo sana. 

Wanaume kutoka kijijini kwao, walipenda wamuoe. 

Lakini, Adun aliwakataa wote.

Mamboleo aliomba miguu kutoka kwa mwanamume mmoja, mikono kutoka kwa mwingine, na kiwiliwili kutoka kwa mtu tofauti. 

Siku ya soko, aliziunganisha sehemu hizo. Akakiweka kichwa chake juu yake halafu akaenda sokoni.

Mamboleo alimtaka Adun na alikuwa na azma ya kumuoa. Adun alipendezwa na Mamboleo akataka kuolewa naye. 

Ingawa Mamboleo alitoka mji wa mbali, Adun alikuwa tayari kurudi naye kwake.

Adun na Mamboleo walipokuwa wakisafiri, mwenye miguu aliichukua. 

Kisha mwenye mikono akaichukua mikono yake. 

Mwishowe kabisa, mwenye kiwiliwili alikichukua.

Kichwa pekee kilibaki kikaendelea kutembea na Adun. 

Ingawa Adun aliogopa, hakutoroka. 

Baadaye, waliwasili nyumbani kwa kichwa hicho.

Keshoye kabla ya kichwa kuondoka kwenda shambani,  kilimweleza Kobe, "Adun akijaribu kutoroka, ipulize pembe hii unijulishe."

Kichwa kilipoondoka, Adun alifunganya virago vyake akitaka kutoroka.

Kobe alipoona hivyo, aliipuliza pembe akisema,  "Kichwa, kichwa, Adun yu karibu kutoroka."

Kichwa kilimwendea Adun na kusema, "Unadhani unaenda wapi?" 

Adun alirejea nyumbani kwa kichwa, shingo upande.

Hatimaye, Adun alitafuta mawaidha kutoka kwa mganga. 

Mganga alimshauri, "Nenda ununue keki za maharagwe. Ziloe katika mafuta kisha uziweke ndani ya ile pembe anayoipuliza."

Adun alifuata maagizo ya mganga. 

Aliziweka keki zilizoloa mafuta ndani ya ile pembe.

Asubuhi ilipofika, Adun alivichukua virago vyake akaanza kutoroka tena. 

Kobe aliichukua pembe tayari kuipuliza. Lakini, keki tamu zilianguka mdomoni kwake kila alipoipuliza.

Kobe alizila na kuzila zile keki. 

Adun alitoroka akaenda zake.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na kipindi kirefu cha kiangazi. 

Wanyama walikula nyasi zote nchini. Ilisalia tu aina ya mmea uliotambaa kwenye miti mikubwa.

Siku moja Mbuzi alimwona Fisi akipita akiwa amebeba kisu. 

Mbuzi alikiomba kisu kile ili aukate ule mmea uliotambaa.

Fisi alimpatia Mbuzi kisu chake. Mbuzi aliukata mmea ule akaula hadi akashiba kabisa. 

Alisahau kisu baada ya kukitumia.

Fisi alipokitaka kisu chake, Mbuzi hakujua afanyeje. 

Hakuweza kukumbuka alikokitupa.

Mbuzi alikwaruza hapa na pale akikitafuta kisu.

Fisi alimwambia Mbuzi, "Kwa sababu umekipoteza kisu changu kilichoniwezesha kupata riziki, utakuwa mlo wangu. Vilevile, nitawala wanao."

Tangu siku hiyo, Fisi hajamhurumia Mbuzi.

Hadi leo, Mbuzi anaendelea kukitafuta kisu cha Fisi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, paliishi mzee aliyekuwa tajiri wa kila kitu. Alikuwa na shamba kubwa lenye rutuba, ng'ombe, na mbuzi. 

Lakini jinsi alivyozeeka ndivyo alivyohuzunika kwani hakuwa na mke.

Siku moja alipokuwa chini ya mti, alipata wazo zuri sana. 

Aliona kuwa ikiwa hatapata mke, labda atajitengenezea mmoja.

Alianza kazi ya kumchonga mke kutoka kwa gogo la mti. Alipomaliza kuchonga sanamu, aliyagusa macho nayo yakaanza kuona. 

Kisha aliipulizia pumzi sanamu ikawa hai.

Akawa mwanamke mrembo zaidi ya wote aliowahi kuona. 

Alipiga magoti mbele yake na kumwomba awe mkewe.

Yule mume alimvisha kimori, shanga na mkufu wa kichwani, ishara kwamba alikuwa ameolewa. Kisha alimjengea nyumba akitumia matope na nyasi. 

"Ninakuomba kitu kimoja tu," mzee yule alisema. "Usimwambie mtu yeyote mahali ulikotoka."

Lakini kabla ya kipindi kirefu, vijana kutoka kijiji jirani walianza kusema, "Inawezekanaje mzee kama huyu kumwoa msichana mrembo namna hii!" 

Basi wakaamua kumwiba msichana yule na kumpeleka kijijini kwao.

Mkewe alipoibiwa, mzee huyo alihuzunika sana. Alihisi kwamba hangeishi bila mkewe. Akawaza, "Labda nikipata kitu chochote kutoka kwake, nitapata faraja." 

Aliwatuma njiwa wawili wakamtafute mkewe kisha wamwimbie na wampelekee kitu chochote kutoka kwa mkewe.

Njiwa walipomwona, walimwimbia wimbo mtamu: 

Mke mti, mke mti, 
Mrembo kuliko wote, 
Tumetumwa na mumeo, 
Tunakujia kimori,  
Tukirudishe kwa mumeo, 
Asije akakusahau.

Aliwapa Kimori chake wakaruka, juu ya milima, juu ya mito, hadi wakarudi kwa mumewe. 

Mzee alipokea kimori akakiweka usoni mwake kwa furaha akapata faraja.

Faraja hiyo haikudumu. Aliwatuma wale njiwa tena wakamwimbie mkewe: 

Mke mti, mke mti, 
Mrembo kuliko wote, 
Tumetumwa na mumeo, 
Tunakujia kimori,  
Tukirudishe kwa mumeo, 
Asije akakusahau.

Wakarudi wakiwa wamebeba mkufu uliokuwa ishara ya mwanamke aliyeolewa.

Aliuchukua ule mkufu akapata faraja ya mke wake aliyekuwa katika kijiji cha watu wengine. Baada ya muda mfupi aliwaita njiwa tena akawatuma kwa mkewe tena wakamwimbie: 

Mke mti, mke mti, 
Mrembo kuliko wote, 
Tumetumwa na mumeo, 
Tunakujia kimori,  
Turudishe kwa mumeo, 
Asije kukusahau.

Walienda tena mara ya tatu wakatua mabegani mwake. Walipokuwa wakiimba, kila njiwa alikuwa akidona na kumng'oa jicho. 

Punde si punde, akageuka na kuwa sanamu. Miguu na mikono yake ilidondoka. Kichwa vilevile kilianguka. 

Akaanguka chini, pu!

Mumewe alilisukuma lile gogo la sanamu mtoni. Akalisimamisha upande wa mizizi ukiwa majini. 

Na baada ya kupata maji na kupigwa na miale ya jua, lile gogo liliota majani tena kama zamani.

Upepo unapovuma, majani yake hushusha pumzi kama vile mwanamke hushusha pumzi anapotamani kumwona mumewe.

------------------------------------------------------------



Kwa nini mbingu ni ya rangi ya bluu?

Je,  huwa bluu kila wakati?

Kwa nini rangi ya majani ni kijani kibichi?

Majani si kijani kibichi kila wakati.

Kwa nini ndizi mbivu ni manjano?

Ndizi mbichi ni za kijani.

Kwa nini mwavuli ni mweusi?

Miavuli yote si mieusi.

Kwa nini damu ni nyekundu?

Kuna madini kwenye damu. 

Yanaipatia damu rangi  nyekundu.

Kwa nini chumvi ni nyeupe?

Sifahamu!

------------------------------------------------------------



Huu ni unyayo.

Huu ni mguu.

Hili ni goti.

Hiki ni kiuno.

Hii ni tumbo.

Hiki ni kifua.

Hivi ni viganja.

Hii ni mikono.

Hiki ni kiwiko.

Hiki ni kichwa.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na Fisi na Kima. Walikuwa na mzozo kati yao. 

Walienda kwa hakimu ili awasaidie kuusuluhisha.

Baada ya hakimu kusikiliza kesi yao, aliogopa kuamua. Aliwaza, "Nikimlaumu Fisi, atawala mifugo wangu. Nikimlaumu Kima, atayala mahindi yangu yote! Nifanyeje?"

Hakimu alitafakari juu ya kesi hiyo kisha akasema, "Naona vigumu kuiamua kesi hii peke yangu. Ipelekeni kwa wazee wa kijiji."

Fisi na Kima walienda kwa wazee wa kijiji.

Waliwaeleza wazee wa kijiji kuhusu mzozo wao.

Baadaa ya wazee wa kijiji kuwasikiliza, wao vilevile waliogopa kuiamua kesi ile.

Wazee wa kijiji walijua wakimuunga Kima mkono, Fisi atawala mifugo wao. Na wakimuunga Fisi mkono, Kima atayala mahindi yao.  

Wazee wa kijiji walimwambia Fisi na Kima kuwa kesi yao ilikuwa ngumu sana kuiamua.

Wazee walimkumbuka mwanamke mmoja fukara aliyeishi hapo kijijini. Yeye hangepoteza chochote kwa kuwa hakuwa na mifugo wala mahindi.

Mmoja wao aliwaambia, "Mwanamke fukara ataweza kutoa uamuzi bila woga."

Wakawaambia Fisi na Kima kwenda kwake.

Walipowasili kwa mwanamke yule fukara walisema, "Tuamulie mzozo wetu." 

Mwanamke fukara alikubali lakini, akataka kuongea na kila mmoja peke yake.

Mwanamke fukara alimwita Fisi kwanza akamwambia, "Wewe unaheshimika, ni mnyama mkubwa tena ni shujaa. Unawezaje kugombana na mnyama mdogo tena mjinga kama Kima?"

Mwanamke akaendelea kumwambia Fisi, "Watu wakisikia mzozo huu, watakudharau sana. Wacha kuzozana na Kima." 

Fisi alikubali, "Unavyosema ni kweli. Nitaiacha kesi hii."

Mwanamke fukara akamwita Kima akamwambia, "Wewe ni mwerevu na mrembo. Mbona unabishana na mnyama huyu mchafu, mwenye harufu mbaya anayekula vilivyooza. Watu watakufikiriaje wakisikia unazozana na huyu kiumbe mwenye sura mbaya?"

Kima alikubali, "Unavyosema ni kweli. Nitaiacha kesi hii."

Baadaye, mwanamke fukara aliwaita wote akasema, "Kwa kuwa nyote mlikubali kuacha ugomvi kati yenu, ni lazima msameheane."

Kima na Fisi walisameheana wakasuluhisha mzozo wao.  

Watu kijijini waliposikia walishangaa. Mwanamke fukara aliwezaje kutatua shida iliyowashinda hakimu na wazee wa kijiji?

------------------------------------------------------------



Mimi ninaishi katika kijiji cha Kakuma. Ni mahali pakavu penye miti ya miiba na joto jingi. 

Kakuma, kuna mbuzi wengi. 

Wenyeji wengi hupanda baiskeli. Sokoni kuna maduka machache madogo.

Asubuhi moja, mamangu aliniita akasema, "Etabo,  leo umefika umri wa miaka sita nasi tutakupa zawadi." 

Nilimwuliza kwa furaha, "Zawadi gani? Akajibu, "Utafuatana nasi kesho twende sokoni. Tutapanda basi." 

Hiyo ingekuwa safari yangu ya kwanza kwenda soko kubwa.

Keshoye, tulikwenda kwenye kituo cha basi. 

Nilisimama kati ya mama na shangazi. Nilijisikia mdogo sana nikiwa kati yao. 

Nilikuwa nimevaa suruali mpya ya bluu na fulana nyekundu.

Basi lilikuwa limejaa kwa hivyo ilibidi mama anipakate. 

Nililala njia nzima Kwa vile nilikuwa nimechoka sana kutokana na joto. 

Sikuona chochote.

Jua lilikuwa limeanza kuchomoza tulipofika sokoni. Langoni, palikuwa na mama muuzaji wa nafaka. Pembeni, walikuwapo wanaume wawili waliokuwa wakiviandaa viazi vitamu. 

Upande wa pili, mama mmoja mfupi alishika helikopta ya rangi ya bluu iliyometameta. Nilipoina, niliita, "Mama, mama, tazama helikopta ile!"

Katikati ya soko, kulikuwa na kibanda kikubwa. Matunda aina nyingi yaliuzwa pale. 

"Yanaitwaje matunda haya?" Nilimwuliza mama huku nikimwonyesha aina ambayo sikuwahi kuiona.

Niliendelea kuuliza, "Na haya je?" Mama akajibu,  "Haya ni matofaa." 

Kati ya matunda yote kibandani, nilipenda matofaa zaidi. Nilipotazama umbo na rangi yake, niliwazia utamu wake. 

"Tafadhali, ninunulie tofaa moja," nilimsihi mama.

Pindi nilipopewa tofaa, niliuachilia mkono wa mama, nikalishika tunda kwa mikono miwili. 

Nililitafuna polepole nikaonja utamu wake. Nilikuwa sijawahi kulionja tunda tamu kama tofaa.

Nilipomaliza kulila tofaa, niligeuka kuongea na mama, lakini hakuwepo! Nilimtafuta mahali tulipotoka, lakini sikumwona yeye wala shangazi. 

Nikamwuliza mama muuzaji nafaka, lakini hakujua walipokuwa. 

Nikaanza kulia.

Baadaye, mama mmoja alinishika mkono na kuniongoza walipokuwa watoto wengine. 

Mzee mmoja mwenye ndevu aliniuliza, "Jina lako nani mwanangu?" 

Huku nikilia, nilimjibu, "E-ta-bo."

Nilianza kujiuliza kama watoto pia huuzwa sokoni. Mara nikaacha kulia ili nione kama wanunuzi wa watoto walikuwepo chumbani mle. 

Baada ya muda alikuja mama mmoja akamchagua mmojawapo wa watoto. 

Nikawaza, "Mimi nikichaguliwa, sitarudi nyumbani tena?"

Kisha nilimsikia yule mwanamume mwenye ndevu akiuliza, "Etabo yuko wapi?" 

Nililia zaidi nikisema, "Lakini mimi sitaki kwenda na wewe!" 

Nikatoroka.

Walipolisikia jina langu likiitwa, mama na shangazi walikimbilia chumbani humo. 

"Etabo, Etabo." Iliita sauti niliyoitambua kuwa ya mamangu.

Nilimkumbatia mamangu. Kisha shangazi akasema,  "Etabo, tulikuwa tunakutafuta tukupe zawadi yako ya siku ya kuzaliwa." 

Aliitoa helikpta iliyometameta ya rangi ya bluu kutoka kwenye mfuko mkubwa alioubeba. "Hii hapa zawadi yako!" akasema mama.

------------------------------------------------------------



Mtu, Simba, Mbwa, Nyoka, Tai na Punda walienda vita.

Yona na mkewe waliwakaribisha kwao.

Wakawachinjia ng'ombe wao.

Kila mmoja alitaka sehemu tofauti ya ng'ombe.

Waliahidi kuwapa zawadi.

Yona na mkewe walimpa kila mmoja sehemu ya nyama aliyotaka.

Baada ya kula, walilala vizuri.

Asubuhi, walienda zao.

Wiki nyingi zilipita.

Simba akawaletea zawadi ya pembe kubwa ya tembo.

Mbwa akasema, "Zawaidi yangu itakuwa kuwachungia pembe hii ili isiibwe."

Ndugu wa Yona akawaza, "Nitaiba ile pembe niiuze."

Alipoenda kuiba ili pembe, Nyoka alimuuma.

Yona na mkewe wakachukua mifugo wa mrehemu.

Wakawa matajiri.

Tai akawaona wafanya biashara.

Walibeba pesa na vito vya bei.

Tai akazinyakua zile pesa na vito. 

Akawapelekea Yona na mkewe.

Punda alichoka kumbebea tajiri wake gunia nzito la pesa.

Akawapelekea Yona na mkewe lile gunia la pesa.

"Nashukuru mlivyonisaidia."

Yona akasema, "Wanyama wametupa zawadi zao. Lakini, Mtu hajafanya hivyo."

Walingonja, wakangoja, lakini, Mtu hakuwaletea zawadi yake alivyoahidi.

------------------------------------------------------------



















------------------------------------------------------------



Lina, Opondo, na Anton walikuwa wakifanya matayarisho ya kusherehekea kuzaliwa kwa Lina.

Anton na Lina walitaka kuoka keki. Opondo alianza kusoma kitabu cha mapishi.

"Hebu tuvichanganye viungo hivi katika bakuli kubwa,"  Lina alisema.

Anton alivikoroga viungo vyote akasababisha mchafuko mkubwa.

"Keki inaonekana kuwa nzito sasa," Opondo alisema.

"Marafiki zako wamewasili," Opondo alimjulisha Lina.

Anton alidhani kwamba zawadi ya kwanza ingekuwa nzito kwa sababu ilikuwa kubwa.

Ulikuwa mto na ulikuwa mwepesi sana.

Anton tena alifikiri kuwa zawadi itakayofuata ingekuwa nyepesi kwa sababu ilikuwa ndogo.

Lilikuwa jiwe lililopakwa rangi na lilikuwa nzito sana.

Watoto walisema kwamba kilo moja ya mawe ilikuwa na uzani sawa na kilo moja ya manyoya.

Keki ya Lina iliungua.

Lina alihuzunika sana.

Shangazi Molly alimwuliza Anton, "Unadhani zawadi ya Lina itakuwa na uzito kiasi gani?"

Anton alimjibu, "Nadhani itakuwa na uzito sawa na ile keki iliyoungua."

Kila mmoja alisema, "Lina, tunakutakia siku ya kuzaliwa yenye furaha."

------------------------------------------------------------



Hapo zamani, Sungura na Fisi walikuwa marafiki wazuri.

Sungura alimwambia Fisi, "Ningependa tulime pamoja."

Sungura alionelea wapande mahindi na wagawane majukumu.

Sungura alimwambia Fisi, "Kazi yangu ya kuwafukuza ndege ni ngumu."

Fisi alikubali kulima shamba peke yake.

Wakati Fisi aling'oa magugu, Sungura aliketi chini akiimba.

Mahinid yalipokuwa  tayari, Sungura alifurahi kuwafukuza ndege.

Sungura alisema, "Nitavuna yaliyo juu ya udongo. Utavuna yaliyo chini."

Sungura alivuna mahindi yote akahifadhi.

Fisi alikuta mizizi tupu chini ya udongo.

Fisi aligundua kwamba alikuwa amedanganywa. 

Alikasirika sana.

Walipanda viazi. Fisi alisema, "Nitavuna yaliyo juu ya udongo."

Walifanya kazi pamoja shambani wakiimba.

Wakati wa kuvuna, Fisi alivuna majani ya viazi pekee.

Sungura alivuna viazi vingi vikubwa akahifadhi.

Fisi alimkimbiza Sungura akitaka kulipiza kisasi.

Urafiki wao uliisha.

------------------------------------------------------------



Siku moja, Sungura alikuwa anatembea ukingoni mwa mto.

Kiboko alikuwa akila majani matamu ya kijani.

Kwa bahati mbaya, Kiboko alimkanyaga Sungura mguuni. 

Kwa uchungu, Sungura alipiga mayowe  na kumfokea Kiboko akisema, "Wewe Kiboko! Unaukanyaga mguu wangu. Huoni?"

Kiboko alimuomba Sungura msamaha, "Samahani sana rafiki. Sikukusudia. Naomba unisamehe!" 

Sungura hakumsikiliza. Aliendelea kumfokea Kiboko akisema, "Umefanya makusudi! Siku moja nitalipiza kisasi!"

Siku moja, Sungura alimtafuta Moto na kumwambia, "Naomba umuunguze Kiboko atakapotoka kwenye maji baada ya kula majani. Kanikanyaga!" 

Moto akajibu, "Hapana shaka, rafiki yangu Sungura. Nitafanya ulivyoniambia."

Kiboko alipokuwa akila majani kando ya mto,  "Whuuush!" Moto akalipuka na kuanza kuyaunguza manyoya ya Kiboko.

Kiboko alilia kwa uchungu huku akikimbilia majini. Manyoya yake yote yaliungua. 

Kiboko alipiga mayowe, "Manyoya yangu yameunguzwa! Moto ameyaunguza manyoya yangu yote! Manyoya yangu yameungua! Manyoya yangu mazuri!"

Tangu wakati huo, kiboko hatembei mbali na maji kwa kuhofia kuunguzwa na Moto. 

Sungura alifurahi sana kumuona Kiboko bila manyoya. Akasema, "Nimelipiza kisasi!"

------------------------------------------------------------



Mikono miwili ya kukamata.

Matawi mawili ya mti.

Watoto wawili wanaocheza pamoja.

Masikio mawili ya sungura.

Macho mawili ya kuona.

Picha iliyo na watu wawili.

Binadamu wawili wanasoma kitabu pamoja.

Masikio mawili ya kusikia.

Mikono miwili ya kukumbatia!

Miguu miwili ya kusimamia.

------------------------------------------------------------



Palikuwa na msichana aliyeitwa Mulongo. 

Aliishi na wazazi wake karibu na kijiji cha Budongo. 

Siku moja mamake Mulongo alimtuma kuchota maji kisimani.

Njiani, alikutana na marafiki zake wakienda msituni kutafuta kuni. 

Mulongo alitaka kwenda nao. "Tafadhali, nisubirini hapa! Lazima nimchotee mama maji kwanza." Mulongo aliwasihi.

Lakini marafiki zake hawakutaka kusubiri.

"Sawa, nitawakuta huko msituni!" Mulongo alisema huku akikimbia kwenda kumchotea mamake maji. 

Baadaye, alienda msituni kuwatafuta marafiki zake.

Alifuata njia iliyoelekea kwenye kijito. Upande mwingine wa kijito kulikuwa na njia nyingine ndogo kila mojawapo ikielekea upande tofauti. 

"Njia ipi marafiki zangu walifuata?" Mulongo alishangaa.

Aliichagua njia iliyokuwa pana kisha akatembea, na kutembea, lakini hakuwapata marafiki zake. 

Alichoka sana kwa hivyo alipopumzika chini ya mti. 

Alilala muda mfupi baadaye.

Mulongo alipoamka, ilikuwa giza. Gizani, macho ya manjano yalimulika. Alikuwa amezungukwa na fisi! 

Aliogopa asiweze hata kulia. Alijaribu kukimbia,  lakini fisi walimzunguka wakionyesha wazi kuwa walikuwa na njaa.

"Usisonge," sauti ya fisi mkubwa zaidi ilisikika. "Ukikimbia, utaliwa!" 

"Tafadhali, niache niende nyumbani!" Mulongo aliwasihi.

Badala yake fisi walimpeleka Mulongo katika nyumba yao iliyokuwa msituni. Chumba hicho kichafu kilijaa mifupa na kelele za nzi. 

Mulongo alilala chini na kujifanya kuwa amepatwa usingizi.

Gizani, aliwasikia fisi wakiongea wenyewe kwa wenyewe. "Moto unaendelea vipi? Je, maji yanachemka?" Mmoja aliuliza." 

Mwingine aliJibu, "Kila kitu ni tayari. Nimlete sasa?" 

"Ndiyo, ndiyo! Tunahisi njaa!" Fisi wale wengine walinguruma.

Walikuwa karibu kumvuta Mulongo kumtoa chumbani wakati fisi mkubwa aliongea, "Fisi,  subirini. Kumbuka kanuni ya kijiji. Hakuna fisi anayekubaliwa kula peke yake. Ni lazima tuialike jamii nzima kushiriki mlo."

Waliokwenda kuwaalika jamii, hawakurudi haraka. Yule fisi mkubwa alianza kusinzia na kukoroma pale mbele ya moto. 

Hii ilikuwa nafasi nzuri ya Mulongo kutoroka! Lakini angempitaje yule fisi?

Umbo lake kubwa lilifunika sehemu yote ya mlango.

Njia ilikuwa ni moja tu. Alijihimiza na kurukia juu ya mgongo wa fisi kwa mara moja.

Kisha, akakimbia, na kukimbia jinsi miguu yake ilivyomwezesha.

Wakati huo huo, fisi wale wengine walirudi na kuona kilichotokea. 

Walimfuata huku wakipiga kelele za hasira na gadhabu. 

Lakini, walikuwa wamechelewa.

Alipokaribia kijiji chake, wanakijiji walimtambua na kushangilia wakisema, "Mulongo, Mulongo anakuja, Mulongo anakuja." 

Wazazi wake walikimbia kumbusu huku wakishukuru Mungu kwa kumwokoa mototo wao, "Mulongo, tulidhani umekufa!"

Kutoka siku hiyo, Mulongo na watoto wengine hawakuwahi kururdi msituni peke yao.

------------------------------------------------------------



Kulikuwa na buibui mmoja mvivu aliyeitwa Anansi. 

Badala ya kujipikia chakula, Anansi alipenda kuwatembelea marafiki zake na kula chakula chao.

Siku moja, Anansi alipitia nyumbani kwa Sungura na kunusa mboga zilizokuwa zikipikwa. Alizitamani sana. 

Sungura alimwambia, "Hazijaiva, lakini unaweza kunisaidia kuosha vyombo tukisubiri ziive." 

Anansi akamjibu kwa haraka, "Samahani, nina kazi nyingine, nitarudi baadaye."

"Nitakujulishaje zitakapokuwa tayari?" Sungura akamwuliza. 

Anansi akawaza kidogo halafu akasema, "Nitasokota utando nifunge ncha moja mguuni kwangu na nyingine chunguni. Mboga zitakapoiva, utauvuta utando, nami nitakimbia nije." 

Kwa hivyo, Anansi aliufunga utando kwenye chungu kisha akaenda.

Anansi alimwona Kima na mkewe wakipika maharage. Kima alisema, "Jiunge nasi! Maharagwe karibu yaive." 

Anansi akamjibu, "Samahani, nina kazi nyingine, nitarudi baadaye. Nitafunga ncha moja ya utando huu kwenye mguu na nyingine kwenye chungu chako. Maharagwe yatakapoiva, utauvuta utando, nami nitakuja."

Anansi alipita kwa Nguruwe na kunusia viazi vitamu. Nguruwe alisema, "Ninapika viazi vitamu na asali. Njoo tule." 

Anansi akamjibu, "Ningependa lakini sina muda." Anansi akafunga utando ncha moja mguuni na nyingine kwenye chungu cha viazi vitamu. 

Akamwambia Nguruwe, "Viazi vitakapoiva, utauvuta utando huu, nami nitakuja."

Anansi alipofika mtoni, miguu yake yote ilikuwa imefungwa kwa ncha za utando. Anansi akawaza,  "Hili lilikuwa ni wazo zuri sana. Ila najiuliza ni chungu kipi kitakachoiva kwanza?" 

Pale pale Anansi akahisi mguu mmoja ukivutwa. Akasema, "Aa, hii ni ncha ya utando uliofungwa kwenye chungu cha mboga."

Anansi aliendelea kuhisi mvuto baada ya mwingine. Alivutwa pande tatu mara moja. "Aa! Jamani!" Anansi alisema alipovutwa kwa mara ya nne. 

Kabla hajapumua, akahisi ncha ya tano, ya sita, ya saba,  na ya nane zikivutwa. 

Anansi alivutwa huku na kule. Kila mmoja alivuta ncha yake wakati ule ule. Miguu yake ilivutwa ikawa myembamba.

Anansi alijirusha mtoni kwa haraka. Tando zote zilipochukuliwa na maji, alijivuta taratibu kwa maumivu hadi kando ya mto. Alihisi uchungu, "Aa! Aa!" Labda hili halikuwa wazo zuri kabisa." 

Siku ile hakupata chakula chochote. 

Tangu wakati huo, buibui huwa na miguu minane myembamba.

------------------------------------------------------------



Wekesa alikuwa na donda mguuni. Yeye na mkewe waliishi kijijini na wanao.

Binti yao, Nangila, na kaka zake watatu walifanya kazi zao vizuri.

Nangila aliwavutia wengi. Mwanamme aliyependa kumwoa, alitakiwa kutimiza sharti kali lililowekwa na babake.

Sharti lilikuwa kuileta miti-shamba kutoka ziwa lililokuwa karibu. Dawa hiyo ingeponya donda alilokuwa nalo bababke Nangila. Ziwa hilo lilijaa mizimu hatari.

Baadhi ya wanaume waliojaribu kuipata ile miti-shamba, walirudi mikono mitupu. Wengine kamwe hawakurejea kutoka ziwani.

Nangila alikuwa na hofu kaka zake pia waliposhindwa kwenda ziwani. Aliamua kwenda mwenyewe. Mamake alimwambia, "Mwanangu, wanaume wameshindwa, utafaulu?"

Nangila alimsaidia bi kizee mmoja kubeba kuni. Bi kizee alimshukuru, akamwambia, "Nitakueleza jinsi utakavyofika kwenye ziwa la mizimu na namna utakavyofanya."

Nangila alipofika kwenye ufuo wa ziwa, aliiona familia ya mizimu ikinywa na kusherehekea. Alisubiri na kutazama. Moja baada ya nyingine, mizimu ilipatwa na usingizi.

Mizimu yote ilipolala,  Nangila alipiga mbizi ziwani. Aliipata miti-shamba na kuiweka mkobani. Alipoogelea kurudi ufuoni,  mawimbi makubwa yalimzunguka.

Alifika ufuoni mizimu ikiwa imeamka. Aliimba wimbo aliofunzwa na bi kizee: 

Mie nilikuja kwa sababu wanaume waliogopa. Babangu ahitaji dawa. Ndiyo sababu nikaja hapa.

Sauti ya Nangila ilikuwa tamu sana hata mizimu ikamtaka aendelee kuimba. Mizimu ilipolala tena, Nangila alikimbia haraka kwenda kijijini.

Baada ya kutibu donda la babake, babake aliweza kusimama tena. Kijiji kizima kilisherehekea na kumpongeza Nangila.

------------------------------------------------------------



Sebule

Chumba cha kulia chakula

Chumba cha kulala

Bafu

Jikoni

Dirisha

Mlango

Meza

Kiti

Bustani

------------------------------------------------------------



Lego alikuwa nyoka mkubwa. 

Aliishi katika kijiji cha Sinyare.

Apiyo, Ajoh na Atieno walienda kutafuta kuni.

Bibi aliwaonya kuhusu Lego.

Wote watatu walitayarisha chakula.

"Itakuwa siku ndefu," walisema.

"Hebu tuwe kimya. Lego huishi karibu hapa," Apiyo aliwakumbusha dada zake.

Atieno alitaka meno ya Lego. 

Apiyo alimwambia, "Kumbuka onyo la bibi."

"Ninataka meno ya Lego ya dhahabu." 

Ajoh alisizitiza bila kujali.

Lego hakuyapata meno yake ya dhahabu.

Alisubiri kumwadhibu aliyeyaiba.

Wasichana walisikia sauti "Hsssss!" 

Lego alikuwa tayari kumuuma aliyeiba.

Lego aliwapatia mtihani wa kuimba. 

"Aliyeiba, hatafaulu kuimba vizuri."

Apiyo na Atieno waliimba vyema.

Kwa hivyo, walipita mtihani.

Ajoh hakufaulu kuimba vizuri.

Lego alijua aliyeiba meno yake ya dhahabu.

Lego alimmeza Ajoh! 

 Bibi aliposikia, alisema, "Heri angenisikiza."

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na kijiji kilichoitwa Raha. Watu wote walikuwa vijana.

Hapakuwa na mwanamume wala mwanamke mkongwe kijijini humo.

Vijana wa kike na wa kiume kijijini Raha walicheza na kufurahi. Walikula walichopenda na kunywa chochote kilichowalevya. Walifurahi mchana kutwa na usiku kucha.

Hivi karibuni, walisahau namna ya kufanya kazi.

Pia walisahau chochote kilichotendeka siku iliyopita.

Siku moja vijina wa kijijini Raha waliamka na kukuta kuwa chakula chote kilikuwa kimeisha. Hapakuwa hata na tone moja la mvinyo. Ala zote za muziki zilikuwa zimevunjika.

Hapakuwa na muziki wa kucheza. Hata hawangeweza kucheza kwa sababu walihisi njaa na kudhoofika.

Walienda kwa Oza, chifu wa kijiji, na kulia kwa uchungu.

Chifu wao kijana alitoka nje ya chumba na kuwasihi, "Acheni! Watu wapendwa wa kijiji cha Raha. Tafadhali acheni kulia. Tutaweza kufa hivi karibuni. Heri tutumie nguvu tulizo nazo kubaki hai."

Watu walipiga kelele, "Wewe ni chifu wetu! Lazima utuokoe!"

Baada ya kunyamaza kwa muda, chifu Oza alisimama akasema, "Mimi si chifu wenu tena. Nitaondoka hapa nitafute pahali palipo na amani. Mnaweza kumchagua chifu mwingine."

Kwa hivyo, chifu Oza aliingia chumbani kwake akakusanya virago vyake na kuondoka.

Watu hawakujua nani angekuwa kiongozi wao. Hawakujua la kufanya. Walilia zaidi.

Halafu sauti ndogo na nyororo ikasema, "Nitakuwa chifu wenu!"

Kila mmoja aligeuka kujua aliyeitoa sauti ile. Wote waliangaliana. Walitazama kila mahali lakini hawakumtambua aliyekuwa amezungumza.

Watu hao walishangaa kumwona mtoto mdogo mbele yao.

Mtoto huyo alisema, "Ndiyo! Nitakuwa chifu wenu. Ninaweza kuwasaidia. Lakini, lazima mniahidi kuwa mtakoma kusherehekea mchana na usiku. Tena, lazima mfuate ushauri wangu."

Watu hao walivutiwa sana na ujasiri wa mtoto huyo. Wakaahidi kumtii.

Akawapeleka katika shamba lililokuwa na rutuba. Wakala, wakanywa na wakapumzika. Halafu, akawafunza na kuwakumbusha jinsi ya kulima.

Wakisaidiwa na yule mvulana mdogo kama chifu wao, watu wa kijijini Raha, walianza kujifunza maana ya jitihada. Walifanya kazi kwa bidii.

Baadaye, walipata chakula na vinywaji vya kutosha. Walifurahi na kusherehekea tena. Lakini, pia, waliendelea kufanya kazi.

Kila usiku, yule chifu mdogo aliondoka kijijini na kukutana na mzee mwenye busara.

Alimhadithia kuhusu wanaume na wanawake shujaa waliotatua matatizo ya watu wao.

Hatimaye, mvulana huyo, alikuwa mtu mwenye hekima na mwenye uwezo mwingi.

------------------------------------------------------------



Siku moja Sungura alienda kutafuta chakula. Alikutana na Tembo akibeba asali mgongoni. 

Sungura alimwambia Tembo, "Tafadhali nibebe. Mimi ni mnyonge."

Tembo alikubali Sungura akadakia mgongo wake. 

Sungura alianza kula asali ya Tembo!

Asali ilianza kudondoka. 

Tembo alipouliza, Sungura alisema kuwa yalikuwa maji yaliyotoka kwenye kidonda chake.

Waliufikia mto na kumkuta Kiboko akinywa maji.

Sungura alitaka kujua kati ya Tembo na Kiboko, ni nani aliyekuwa na nguvu kumshinda mwingine.

Walianza kubishana. 

Tembo alisema yeye ndiye mwenye nguvu zaidi naye Kiboko akasema ni yeye.

Sungura alisema kuwa alijua jinsi ya kutambua aliyekuwa na nguvu zaidi. 

Aliwaambia wamsubiri.

Sungura alirudi na kamba ndefu. 

Alimfunga Tembo kiunoni na kumwelekeza mbali na mto.

Kisha Sungura akamfunga Kiboko kiunoni na kumuacha pale karibu na mto.

Sungura alijificha mtini akawaambia, "Tayari! Moja,  mbili, tatu! Vuta sasa!"

Kiboko na Tembo walivutana. 

Tembo akamvuta Kiboko naye Kiboko akamvuta Tembo.

Kiboko na Tembo wakavutana lakini, hakuna aliyeweza kushinda.

Sungura aliendelea kula asali ya Tembo kule mtini.

Alipomaliza kuila asali, aliikata kamba karibu sana na Kiboko.

Tembo aliuangukia mti kwa kishindo.

Sungura alimshangilia Kiboko akisema kwamba yeye ndiye mwenye nguvu zaidi.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani hakukuwa na majira ya usiku katika kijiji cha kina Opio. 

Watu walilala wakati wowote walipochoka. 

Walifanya kazi zao walipoamka.

Siku moja, Opio alienda na mbwa wake kuwinda. Baada ya muda mfupi, mbwa walianza kumfukuza paa. 

Opio aliwafuata akakimbia kwa muda wa saa nyingi. Alipochoka alipumzika halafu baadaye alianza kukimbia tena. 

Lakini, hakuwaona mbwa wake.

Opio alijipata katika kijiji tofauti. Alimwambia mwenye nyumba, "Nimechoka. Nahitaji kupumzika." 

Mtu yule alimjibu, "Unakaribishwa kupumzika hapa. Je, ungependa kunywa pombe kidogo?" 

Opio alikuwa na kiu. Aliinywa pombe kidogo kisha akalala.

Opio alipoamka, hakuweza kuona. Aliyafumba na kuyafumbua macho yake mara nyingi. 

Mwishowe, alimwambia mhisani wake, "Ulinipa kinywaji kibaya. Siwezi tena kuona sawasawa."

Mwenye nyumba alimwambia, "Hukunywa kinywaji kibaya na macho yako ni sawasawa. Sasa hivi ni usiku. Kwani hujui usiku? Siku ikiisha, usiku hufuata." 

Opio aliuliza maswali mengi kuhusu usiku akapendezwa sana nao. Alikaa hapo siku nyingine  ili auone usiku ukiingia tena.

Asubuhi iliyofuata, yule mtu alimweleza Opio, "Giza litakapoanza kuingia, anza kutembea ukienda kijijini kwenu. Ukitembea huku ukiangalia mbele usiku utakufuata. Ukiangalia nyuma usiku utapotea."

Opio alifanya alivyoambiwa. Usiku huo alianza kutembea akielekea kijijini kwao. 

Alihisi giza likimfuata nyuma. Alikuwa na haja ya kuangalia nyuma lakini alijizuia.

Alipofika kijijini kwao, wanakijiji waliogopa. Walimwuliza, "Huu ni ugonjwa gani uliotuletea? Ni nini hiki cheusi kinachokufuata?" 

Opio akawaeleza, "Ndugu zangu, kitu hiki cheusi kinachonifuata kinaitwa usiku. Mnavyoogopa ndivyo nilivyoogopa pia."

Opio aliendelea kuwaeleza, "Ninyi vilevile mtaupenda usiku. Mwangaza ukija tutaweza kufanya kazi. Na usiku ukiingia tutapumzika."

Na hivyo ndivyo majira ya usiku yalivyotambuliwa katika kijiji cha kina Opio.

------------------------------------------------------------



Hii ni kamba ya kuruka.

Mumbi anaruka kamba peke yake.

Mumbi ameshikiwa kamba na rafiki yake.

Mumbi anasoma kitabu sasa.

Mumbi anawaaga rafiki zake.

Mumbi anaosha vyomba jikoni.

Mumbi anaandika ubaoni.

Mumbi anakula matunda tofauti.

Mumbi anapumzika kitandani.

Mumbi anamsikiliza mamake.

Mumbi anafikiria.

------------------------------------------------------------



Mimi na Kiki ni marafiki. 

Sisi hutembea kwenda nyumbani.

Siku moja, mwanamme alitufuata.

Meno yake yalikuwa ya kutisha. 

Ngozi yake ilijaa vipele.

Tulipomtazama, alitupigia kelele  kwa hasira.

Yeye na wenzake walinisukuma ndani ya gari.

Kiki aliweza kutoroka.

Waliniweka katika chumba chenye giza. 

Walinifunga mikono.

Mwanamme mmoja alisema, "Kula chakula hiki.
Safari ni ndefu."

Nilipokuwa nikila, yule mwanamme alivuta sigara.

Ghafla, wenzake walirudi. 

Walikuwa wanamvuta Kiki.

Tuliwasikia wanaume hao wakipingana kwa sauti ya juu.

Kiki alisema, "Lazima tutoroke. Wazazi wetu hawataweza kuwalipa."

Tulivuta mbao kutoka kwenye dirisha.

 Tuliona mwangaza.

Kiki alikuwa mdogo kuniliko. 

Alitoka kwenda kutafuta usaidizi.

Wanaume waliingia ndani kwa fujo. 

Kiongozi wao alikasirika sana.

Walirudi katika chumba walichokuwa.

 Waliendelea kugombana.

Mara nilisikia sauti ikisema, "Usiogope. Polisi wamefika."

Kulikuwa na kelele nyingi pamoja na milio ya risasi.

Polisi wa kike alisema, "Kila kitu ni sawa. Uko salama sasa."

Tangu siku hiyo, mimi na Kiki tumekuwa waangalifu
zaidi.

------------------------------------------------------------



Jumamosi moja mama alisema, "Brenda, Mary na Lona, nendeni mcheze!"

Lona alisema, "Twende tuogelee." 

Brenda alijibu, "Mama alitukataza."

Walivua viatu na nguo wakacheza majini.

Walicheza kwa muda mfupi.

Walicheka na kushangilia.

Baadaye, Mary alisema, "Hebu tuogelee. Mama hatajua."

Walipomaliza kuogelea, nguo zao hazikuwepo. 

Walihisi baridi.

Walizitafuta kila mahali. 

Hawakuzipata.

Baadaye, Brenda alisema, "Tazama! Ng'ombe anakula shati la Lona."

Walimwona ng'ombe mwingine. 

"Anakula sketi yangu!" Mary alisema.

"Mama, ng'ombe walikula nguo zetu." 

Adhabu aliyowapa, hawataisahau.

------------------------------------------------------------



Jina langu ni Daudi.

Nina miaka tisa.

Rafiki yangu mmoja ni mvulana. 

Jina lake ni Robert.

Robert pia ana miaka tisa.

Yeye anapenda kucheza mpira.

Robert ana paka anayempenda.

Paka huyo ana rangi nyeusi na nyeupe.

Robert anaishi na baba, mama na dada yake.

Tunapenda kucheza pamoja.

Nina pia rafiki msichana.

Jina lake ni Emy.

Emy ana miaka minane.

Yeye anapenda kuogelea.

Mimi huogelea na rafiki yangu siku ya Jumapili.

Emy husoma vitabu vingi sana!

Emy hana dada wala kaka, lakini, ana kuku.

Emy na Robert wanapenda kucheza mpira wa miguu.

------------------------------------------------------------



Fana na familia yake wanaishi katika mji wa Debre Birhan nchini Ethiopia. 

Fana ni mwanafunzi wa darasa la tatu. Ni mwenye roho nzuri na hekima.

Fana anawapenda wanyama. Ana paka mmoja, kuku wawili, mbuzi na njiwa. 

Anakuwa nao kwa muda mrefu akiwalisha na kucheza nao.

Siku moja, Fana na wenzake walikuwa wakicheza uwanjani shuleni. Fana aliwaona watoto wakiwarushia njiwa mawe. 

Alijiuliza, "Mbona wanawaumiza njiwa?"

Aliacha kucheza akakimbia kuelekea mahali watoto wale walikokuwa. 

Mwanzoni, wenzake hawakuelewa kilichokuwa kikitendeka. Walimfuata. Fana aliwakemea wale watoto, "Acheni kurusha mawe."

Wale watoto watukutu walitoroka. 

Fana aliwashika njiwa waliojeruhiwa. Aliona majeraha kwenye mbawa zao. 

Aliwapeleka nyumbani kuwalinda.

Fana aliwalisha njiwa. Jioni aliisimulia familia yake alichokiona na kufanya siku ile na jinsi alivyowaokoa njiwa.

Asubuhi, Fana na wazazi wake welienda katika kliniki kupata dawa za kuwaponya njiwa. 

Baada ya siku chache, njiwa walipona majeraha yao. Fana alifurahi sana.

Kila mara, Fana aliwaambia marafiki zake, "Ninawapenda wanyama. Wanyama wana manufaa kwetu na ni marafiki zetu. Lazima tuwalinde na kuwahifadhi."

------------------------------------------------------------



Hapo kale kiangazi kilienea nchi nzima. Miti ilisinyaa. Mito ilikauka. 

Watu na mifugo wakakosa maji na chakula. Walikonda sana.

Kima wengi walioishi milimani walikufa kwa njaa. 

Siku moja, Kima mmoja wa kike alitaka kutafuta suluhu. Alienda kutafuta sehemu isiyo na kiangazi.

Alisafiri kwa siku nyingi. 

Alipita vichaka, akapanda milima na kuvuka mabonde.

Hatimaye, Kima huyo alifika mahali palipoitwa Tirkol.

Alipata matunda aina nyingi na mto uliobubujika maji. 

Alifurahi sana.

Kima yule alipiga kambi hapo. Alikula matunda mengi. Akanona na kumetameta. 

Kwa furaha, aliogelea mtoni kila siku.

Baada ya muda, aliamua kurudi milimani. Alitaka kujua walionusurika na athari za kiangazi. 

Alibeba matunda mengi akipitia njia aliyoitumia awali.

Alipofika milimani, kima walionusurika walimlaki.

Kila mmoja wao aliyataka yale matunda aliyoyaleta. 

Walimwuliza, "Ni sehemu gani iliyo nzuri hivi? Tupeleke pia nasi."

Kima aliwaelezea uzuri wa Tirkol. 

Akakubali kuwapeleka huko.

Kima wote walihamia Tirkol. 

Walikula matunda, wakanywa maji, wakapumzika na wakanona. 

Wakaapa kutorudi milimani tena.

Punde, kima wenyeji wa Tirkol waligundua kwamba kima wa milimani walikuwa wamehamia sehemu yao.

Walihofia kuwa matunda hayangewatosha. 

Wakaamua kuwafukuza kima waliotoka milimani.

Siku moja kima wa milimani walikuwa mtoni wakinywa maji. 

Kima wa Tirkol waliwavamia kwa mijeledi. Walitaka kuwachapa na kuwafukuza.

Kabla ya vita kuanza, kima mmoja mzee aliwauliza, "Mbona mnataka kupigana? Mimi naona kuna chakula cha kututosha sote."

Tangu siku hiyo, kima wa kutoka milimani na wale wa Tirkol wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani.

------------------------------------------------------------



Kwa ajili ya watoto katika kila nchi ya Afrika

Siku moja, dada yangu Zena alikuwa na wazo hili.

"Nitatengeza barakoa kwa kila asiyekuwa nayo kwenye jamii!" alisema. 

"Hilo ni wazo zuri! Wacha tuwaambie Mama na Baba watakaporudi nyumbani!" nilijibu.

Mama na Baba waliporudi nyumbani, tuliwaambia kuhusu wazo la Zena.

"Hilo ni wazo zuri mwanangu!" Baba alisema, na  Mama akakubali. 

"Nitawauliza washiriki wa kanisa letu watupe vitambara vikusaidie kutengeneza barakoa. Hebu tumwulize Bibi asaidie pia."

Siku iliyofuata wanawake wa kanisa walituletea vitambara vya rangi nyingi na mpira nyumbani kwetu. 

Zena alimuachia Bibi mfuko wa vitambara nje ya mlango wake pamoja na barua ya kumuomba amsaidie.

Zena alianza kushona barakoa, mimi na Ndolo tukamtazama. 

Zena ni hodari sana kwa kushona. Alishona barakoa nyingi. 

Mimi na Ndolo tulihesabu barakoa, 1, 2, 3, 4, 5 halafu 20, 30, 40, 50, halafu,100!

Zena na Bibi walishonea jamii barakoa nyingi! 

Tuliwasaidia!

Mama na baba walikuwa wenye fahari.

Siku iliyofuata, Baba na Mama hawakuenda kazini. Waliamua kugawanya barakoa nzuri za Zena na Bibi kwa wale ambao hawakuwa na barakoa. 

Zena alibeba sanitaiza ya Mama na kuwanyunyuzia watu. "Kumbuka kuosha barakoa yako kila siku," Mama alisema.

Sasa Zena anapoenda kuchota maji, kila mtu amevaa barakoa. 

Kila mmoja anaonekana yuko salama.

Baadaye, Mama aliuliza, "Wanangu, tunafanya nini baada ya kugusa kitu chochote?"

"Tunaosha mikono yetu kwa maji na sabuni!" Ndolo alisema. "Au tunatumia sanitaiza," niliongeza. 

Mama alitabasamu, "Na tunavaa nini tukienda nje?" Sote tulipiga kilele, "Barakoa zetu!"

1. Osha mikono yako kwa maji.
2. Tumia sabuni kuosha mikono yako.
3. Osha kwa sekunde 20 au polepole hesabu kutoka 1 hadi 20.
4. Suuza mikono yako kwa maji.
5. Kausha mikono yako kwa taulo au tishu safi.
6. Sasa mikono yako ni safi!



------------------------------------------------------------



Nelima aliita, "Mama! Njoo uone. Nguo hizi zote ni ndogo kwangu!" 

"Hebu nizione," Mama alisema.

"Iangalie hii sketi yangu. Ni ndogo mno," Nelima alisema. 

"Ni kweli," Mama alikubali. "Lakini, Sela anaweza kuitumia sketi yako."

"Tazama suruali yangu. Ni ndogo sana," Nelima alisema. 

"Kweli, suruali hii ni ndogo sana." Mama alijibu. "Sela anaweza kuitumia suruali yako pia."

"Mama, angalia fulana yangu. Ni ndogo sana," Nelima alisema. 

"Ni kweli," Mama alikubaliana naye. "Sela anaweza kuichukua fulana yako."

"Angalia sweta yangu. Ni ndogo sana," Nelima alisema. 

"Ndiyo, ni ndogo," Mama alijibu. "Sela anaweza kuichukua sweta yako."

"Angalia koti langu la mvua. Ni dogo sana," Nelima alisema. 

"Kweli, ni dogo," Mama alisema. "Sela anaweza kulichukua koti lako la mvua."

"Angalia soksi zangu. Ni ndogo sana," Nelima akasema. 

"Kweli, ni ndogo," Mama alijibu. "Sela anaweza kuzichukua soksi zako."

"Angalia viatu vyangu. Ni vidogo mno," Nelima alisema. 

"Ni kweli," Mama akajibu. "Sela anaweza kuvichukua viatu vyako."

"Sasa umepata nguo nyingi, sana," Nelima akamwambia Sela. 

"La! Hasha!" Sela akajibu. "Hizi nguo zote ni kubwa sana kwangu!"

------------------------------------------------------------



Anansi aliwakuta kunguru wakila makuyu. 

Yeye pia alitaka makuyu.

Kunguru walimpatia Anansi makuyu.

Kunguru walimwambia, "Sasa njoo uchume makuyu nasi."

Walienda kuchuma makuyu pamoja. 

Lakini Anansi alichukua makuyu yote.

Anansi aliruka. 

Alianguka ndani ya mto uliojaa mamba.

Anansi alisema, "Mimi ni mmoja wa jamaa zenu."

Hakuliwa.

Anansi alijifanya kuwa anakunywa maji chafu kama mamba.

Mamba walimwamini Anansi. 

Walimualika kukaa nao.

Anansi alisema, "Nitakaa, lakini, hebu kwanza niilete famalia yangu."

Mamba alimbeba Anansi hadi ukingo wa mto.

Anansi alitoroka. 

Mamba bado anamsubiri hadi leo.

------------------------------------------------------------



Kuliishi mfalme katika Kisiwa cha Rusinga. Mfalme huyo hakuwa amehisi maumivu maishani mwake.

Hakuwahi hata dakika moja.

Asubuhi moja mfalme alikiinamisha kichwa chake. Aliwaza namna maumivu yanavyokuwa. "Kuna watu wengi maskini katika ufalme wangu. Nitawezaje kuhisi maumivu yao?" alijiuliza.

Mchana na usiku, alitamani kuhisi maumivu angalu mara moja tu.

Usiku mmoja, aliota ndoto akasikia sauti ikisema, "Nimesikia matakwa yako. Utahisi maumivu."

Sauti hiyo iliendelea, "Yajenge mashua kubwa saba ambamo utaweka mali na familia yako. Kisha safiri ukielekea upande wa kaskazini mwa Kisiwa cha Rusinga."

Mfalme alifurahi sana.

Muda mfupi baadaye, mashua saba yalijengwa na wakawa tayari kusafiri.

Siku moja kabla ya safari, mfalme aliandaa sherehe. Kila mmoja alihudhuria. Chui, nyoka, sungura, konokono, ndege na hata siafu, wote walifika kwa sherehe.

Mfalme aliwahotubia watu, "Mimi na familia yangu tunaondoka kwenda sehemu tofauti ya Kisiwa cha Rusinga. Tunataka kuhisi maumivu ambayo watu wengine huhisi."

Watu walinong'onezana miongoni mwao. Wazee hawakumwamini.

Lakini, ni nani angemhoji mfalme?

Siku iliyofuata, mfalme na familia yake walisafiri.

Kwa siku mbili, mashua yalipita majini. Anga lilikuwa wazi, bahari ilitulia na safari ilifurahisha.

Lakini siku ya tatu, bahari ilichafuka. Anga lilibadilika likatanda mawingu. Walikumbwa na dhoruba kubwa.

Mashua yalizama. Mfalme hakuweza kufanya lolote. Familia na mali yake ilipotelea baharini.

Mfalme pekee alinusurika. Lakini, alikuwa amebadilika na kuwa mdiria.

Mdiria aliruka akatua ukingoni mwa bahari. Alikuwa bado akitumaini kuipata familia na mali yake kutoka baharini.

Mdiria alipiga mbizi baharini mara nyingi. Hakuweza kuiokoa familia yake au hata baadhi ya mali yake.

"Kama ningejua, ningeyafurahia maisha yangu yalivyokuwa," alilia.

------------------------------------------------------------



Hapo zamani za kale, kulikuwa na Fisi na Kima. Walikuwa na mzozo kati yao. Walienda kwa hakimu ili awasaidie kuusuluhisha.

Baada ya hakimu kusikiliza kesi yao, aliogopa kuamua. Aliwaza, "Nikimlaumu Fisi, atawala mifugo wangu. Nikimlaumu Kima, atayala mahindi yangu yote! Nifanyeje?"

Hakimu alitafakari juu ya kesi hiyo kisha akasema, "Naona vigumu kuiamua kesi hii peke yangu. Ipelekeni kwa wazee wa kijiji."

Fisi na Kima walienda kwa wazee wa kijiji.

Waliwaeleza wazee wa kijiji kuhusu mzozo wao.  

Baadaa ya kuwasikiliza, wazee wa kijiji vilevile waliogopa kuiamua kesi ile.

Wazee wa kijiji walijua wakimuunga Kima mkono, Fisi atawala mifugo wao. Na wakimuunga Fisi mkono, Kima atayala mahindi yao.  

Wazee wa kijiji walimwambia Fisi na Kima kuwa kesi yao ilikuwa ngumu sana kuiamua.

Wazee walimkumbuka mwanamke mmoja fukara aliyeishi hapo kijijini. Yeye hangepoteza chochote kwa kuwa hakuwa na mifugo wala mahindi.

Mmoja wao aliwaambia, "Mwanamke fukara ataweza kutoa uamuzi bila woga." Kisha wakawaambia Fisi na Kima kwenda kwake.

Walipowasili kwa mwanamke yule fukara walisema, "Tuamulie mzozo wetu." Mwanamke fukara alikubali lakini, akataka kuongea na kila mmoja peke yake.

Mwanamke fukara alimwita Fisi kwanza akamwambia, "Wewe unaheshimika, ni mnyama mkubwa tena ni shujaa. Unawezaje kugombana na mnyama mdogo tena mjinga kama Kima?"

Mwanamke akaendelea kumwambia Fisi, "Watu wakisikia mzozo huu, watakudharau sana. Wacha kuzozana na Kima." 

Fisi alikubali, "Unavyosema ni kweli. Nitaiacha kesi hii."

Mwanamke fukara akamwita Kima akamwambia, "Wewe ni mwerevu na mrembo. Mbona unabishana na mnyama huyu mchafu, mwenye harufu mbaya anayekula vilivyooza. Watu watakufikiriaje wakisikia unazozana na huyu kiumbe mwenye sura mbaya?"

Kima alikubali, "Unavyosema ni kweli. Nitaiacha kesi hii."

Baadaye, mwanamke fukara aliwaita wote akasema, "Kwa kuwa nyote mlikubali kuacha ugomvi kati yenu, ni lazima msameheane."

Kima na Fisi walisameheana wakasuluhisha mzozo wao.  

Watu kijijini waliposikia walishangaa. Mwanamke fukara aliwezaje kutatua shida iliyowashinda hakimu na wazee wa kijiji?

------------------------------------------------------------



Hapo kale kuliishi mtu maskini na mkewe. Walikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Nonkungu. 

Nonkungu alikuwa mrembo na mkarimu. Wazazi wake walimpenda sana.

Siku moja, wazazi wa Nonkungu waliamua aende kuishi kwa mjombake tajiri aliyeitwa Mtonyama.

Mama alimshonea Nonkungu rinda akalirembesha kwa shanga. Pia, alimtengenezea mkufu wa shanga.

Nonkungu alisafiri hadi akaufikia mto. Akavuka kwa kukanyaga mawe. 

Alipofika upande ule mwingine wa mto, alikutana na msichana aliyekuwa amevaa matambara.

"Unaenda wapi?" yule msichana mdogo alimwuliza. 

"Ninaenda kuishi kwa mjombangu Mtonyama," Nonkungu alisema. 

"Ala! Mtonyama ni mjombangu pia. Nami ninaenda kumtembelea," yule msichana akajibu.

Baada ya kutembea pamoja kwa muda, yule msichana akasema, "Rinda lako ni zuri na mkufu wako pia unapendeza. Hebu nivae nione jinsi mavazi hayo yatakavyonifaa." 

Nonkungu akavua mkufu wake na rinda lake akampa yule msichana mdogo.

Msichana huyo alipovua matambara yake na kuvaa nguo za Nonkungu, Nonkungu aligundua kwamba huyo msichana alikuwa na mkia!  

Sasa alifahamu kuwa yule hakuwa msichana bali alikuwa jitu.

Walipotembea kwa muda, Nonkungu alimwambia, "Tafadhali, nirudishie mkufu na rinda langu." 

Imbulu alijibu, "Acha niendelee kuvaa hadi tuufikie ule mti."

Walipofika kwenye mti, Nonkungu alimwambia Imbulu, "Tafadhali, nirudishie rinda na mkufu wangu." 

"Acha nivae hadi pale kwenye ule mto." 

Nonkungu alikubali kwa woga.

Hatimaye, waliufikia mto. Kwa mara nyingine, Nonkungu alimwambia imbulu, "Tafadhali, nirudishie mkufu na rinda langu." 

Hata hivyo Imbulu alimjibu, "Niruhusu nivae hadi tuufikie ule mji."

Walipoufikia mji, Imbulu alimsukuma Nonkungu nyuma akawaambia wanawake waliokuwa nje,  "Mtazameni msichana huyu aliyevaa matambara. Amekuwa akinifuata siku nzima. Nataka aniondokee." 

Nonkungu aliaibika akakimbia na kujificha.

Imbulu alimwambia Mtonyama, "Mimi ndiye mpwa wako, Nonkungu. Ulivyopanga na wazazi, wamenituma nije niishi hapa kwako." 

Familia ya Mtonyama ilimkaribisha bila kujua ni imbulu. 

Maskini Nonkungu alilala nje akila chakula cha mbwa.

Wakati wa mchana Nonkungu alitembea huku akiimba: 

Matatizo, matatizo! 
Wazazi walinituma,  
Kwa mjomba Mtonyama,  
Kakutana na imbulu,  
Nguo zangu kachukua,  
Matatizo, matatizo!

Siku moja, nduguye Mtonyama alikuwa akipita. Akasikia wimbo mtamu ukiimbwa. Hakujua mwimbaji. 

Alirudi akamweleza Mtonyama kuhusu wimbo aliousikia. Mtonyama naye alikwenda akausikiliza wimbo kwa makini. Akamwona Nonkungu.

Nonkungu alimweleza kwamba Imbulu alichukua nguo zake maridadi akambadilishia na matambara. 

Mtonyama alimchukua akampeleka nyumbani akamficha. Mtonyama alijua jinsi angefanya kumwadhibu imbulu.

Mtonyama alikuwa amesikia kwamba mkia wa imbulu ulipenda maziwa sana. Hangeyapita maziwa bila mkia kunywa kidogo. 

Aliwaambia wafanyakazi wake wachimbe shimo refu na kulijaza na maziwa lala. Kisha aliwaita wasichana wote wa kijijini kwa mashindano ya kuliruka lile shimo.

Imbulu aliogopa. Hakutaka kuliruka lile shimo. Alijua mkia wake ungetamani maziwa lala. Alijificha,  akaufunga mkia wake, akiukazia kwenye mwili wake kabisa. 

Baadaye alijiunga na wasichana wengine kuliruka shimo.

Wasichana waliliiruka shimo mmoja baada ya mwingine. 

Ilipokuwa zamu ya Imbulu, alijaribu kuruka juu ya shimo lakini mkia wake ulifunguka ukamvuta chini, chini, chini kwenye shimo la maziwa lala.

Imbulu alipokuwa akitapatapa ndani ya maziwa lala, waliliziba lile shimo kwa udongo. Na huo ndio uliokuwa mwisho wa imbulu. 

Naye Nonkungu aliishi na mjombake Mtonyama kwa furaha na starehe kwa miaka mingi. 

Na huo ndio mwisho wa hadithi.

------------------------------------------------------------



Huyu ni Paka.

Huyu ni Mbwa.

Paka na Mbwa wanatembea.

Wanatembea kijijini kwao.

Kisha wanaliona yai.

Yai liko nyasini.

Yai liko peke yake nyasini.

Yai liko peke yake.

Paka na Mbwa wanamwendea ndege.

Wanamwuliza, "Yai hili ni lako?"

Lakini ndege anasema, "La, hilo si yai langu. Mwulize bundi. Labda yai ni lake."

Paka na Mbwa wanamwendea bundi.

Wanamwuliza, "Yai hili ni lako?"

Lakini bundi anasema, "La, hilo si yai langu. Mwulize bata bukini. Labda yai ni lake."

Paka na Mbwa wanamwendea bata bukini.

Wanamwuliza, "Yai hili ni lako?"

Lakini bata bukini anasema, "La, hilo si yai langu. Waulize wale bata wawili. Labda yai ni lao."

Paka na Mbwa wanawaendea wale bata wawili.

Wanawauliza, "Yai hili ni lenu?"

Lakini wale bata wawili wanasema, "La, hilo si yai letu."

Halafu, yai linavunjika.

Wanamwona mjusi kwenye yai.

Mjusi mtoto.

Mjusi mtoto anasema, "Mama yangu yuko wapi? Baba yangu yuko wapi? Wapi baba na mama yangu?"

Paka na Mbwa wanampeleka mjusi mtoto kwa baba na mama yake.

Kwaheri Paka.

Kwaheri Mbwa.

Kwaheri Mjusi mtoto.



------------------------------------------------------------



Tulikusanyika kwa bibi kuzisikiliza hadithi zake. Usiku huo, tuliketi karibu na meko bibi alipotusimulia hadithi: 

Sungura na Tembo walikuwa majirani na pia marafiki.

Sungura alipenda uyoga, lakini alikuwa mvivu sana. Alizoea kuiba uyoga wa Tembo. 

Mwaka mmoja, Tembo alipanda ndizi na maboga. Kwa hivyo, Sungura hakupata uyoga.

Sungura alikosa chakula kwa siku nyingi akaamua kuiba ndizi za Tembo. Tembo aligundua kwamba ndizi zake zilikuwa zikiibwa. 

Alimwambia Sungura, "Kuna mtu ananiibia."

Sungura aliuliza, "Anaweza kuwa nani anayekuibia?" 

Tembo alianza kuimba, "Nitamshika mwizi! Aaa! Nitamshika mwizi! Ooo!" 

Sungura alikuwa na wasiwasi sana.

Tembo alimwuliza Kima amchungie shamba lake. 

Lakini, Sungura hakuiba siku hiyo. Hakuiba siku iliyofuata pia. 

Kima alichoka kuchunga akarudi nyumbani.

Siku iliyofuata, Sungura alienda shambani kwa Tembo kuiba tena. 

Tembo alipoenda kukagua mimea yake, Sungura alijificha katika matawi ya maboga.

Tembo aliyaona matawi yakitingika akaanza kuimba, "Nimemshika mwizi! Aaa! Nimemshika mwizi! Ooo!" 

Tembo alitafuta kila mahali lakini hakumpata mwizi.

Siku moja, Sungura alipokuwa akila mazao ya Tembo shambani, Tembo aliwasili. 

Sungura aliruka na kujificha ndani ya boga moja kubwa.

Tembo aliliona lile boga kubwa akasema, "Ooo! Hapa kuna boga kubwa. Litakuwa chakula changu cha mchana." 

Alilimeza papo hapo!

Sungura alijaribu kuruka nje ya lile boga, lakini hakuweza. 

Tembo alipohisi kitu kikiruka tumboni mwake, alijiuliza, "Hili ni boga aina gani linaloruka tumboni?"

Tembo alilitema nje lile boga. Kabla kulikagua,  Sungura alijitosa nje akatoroka. 

Tembo hakuwahi kumshika mwizi.

Bibi alisema, "Na huo ndio mwisho wa hadithi." 

"Asante bibi," tulimjibu. Tuliweka vikombe vyetu vya maziwa. Tukaenda kulala tukiwaza juu ya hadithi hiyo ya bibi.

------------------------------------------------------------



"Shhhu!" Bibi alisema. "Kuna joto kali. Na chungu hiki ni kizito sana. Hebu tupumzike kidogo chini ya kivuli cha mti." Alijipangusa jasho usoni huku akiegemea mizizi ya mti. 

Sela naye alisimama huku ameushika huo mbuyu kwa mkono mmoja. Nduguye, Tovo,  aliuzungukazunguka ule mbuyu akiangalia ukubwa wake. 

"Bibi, mbuyu huu ni mzee sana, sivyo?" "Ndiyo,  Sela. Lakini sio mzee au mkubwa zaidi ya mbuyu ulio katika kijiji cha Balantu!" "Balantu? Kijiji hicho ki karibu?" Sela aliuliza. "Tafadhali tueleze kuhusu mti huo," Tovo alisema. 

"Basi ketini msikilize," Bibi alisema huku akianza kuwahadithia.

Katika kijiji cha Balantu kuliishi msichana aliyeitwa Hami. Siku moja, Hami na ndugu yake Angula, walienda kuchota maji. 

Hami alipokuwa akijaza chungu chake, Angula alimwona sungura. Alimkimbiza, lakini hakuweza kumshika. 

Sungura alikuwa na mbio kumshinda.

Chungu cha Hami kilijaa maji. Sasa alikuwa tayari kwenda nyumbani. Aliangalia kila upande akamkosa Angula. Hakujua alikokwenda. Aljiua kwamba hangeenda nyumbani bila nduguye mdogo. 

Alitazama kila mahali lakini hakumwona. Alipomtafuta, alimpata akiwa amelala kwenye nyasi nyuma ya kichuguu kikubwa. 

Alipokuwa anamkaribia, Angula alimwashiria kwamba anyamaze. Mbona anyamaze?

Karibu na pale kulikuwa na kundi la vijana. Walikuwa wamebeba mishale, nyuta na mikuki! Hami aliweza kusikia sauti zao. 

"Angula," Hami alimwita kwa sauti ya chini. "Wanaume hao ni wezi wa mifugo. Wamekuja kuiba ng'ombe wetu na kuchoma nyumba zetu. Njoo haraka. Lazima tukimbie nyumbani tukawatahadharishe wanakijiji." 

Basi waliondoka polepole kutoka eneo hilo kisha wakakimbia kwenda nyumbani.

Hami alimwita mjomba kwa sauti, "Mjomba, kimbia, kimbia! Kuna wanaume wamekuja kuiba ng'ombe na kuteketeza nyumba." Mjomba alimrudisha ng'ombe kijijini. 

Hami alimwita shangazi, "Shangazi,  kimbia, kimbia!" Wanume wanakuja kuiba ng'ombe wetu na kuteketeza nyumba zetu!" Shangazi alichukua jembe lake, akambeba mtoto aliyekuwa akilala kisha akurudi kijijini. 

Hami akamwona babu yake akiwa na punda wake. Akamwita kwa sauti, "Babu, kimbia, kimbia, wanaume wanakuja kuiba ng'ombe wetu na kuteketeza nyumba zetu." 

Babu alimpiga punda akaenda mbio kuelekea kijijini.

Hami na nduguye wakafika kijijini. Hami akawaita watu wote kwa sauti, "Kimbieni, kimbieni. Kuna wanaume wanaokuja kuiba ng'ombe wetu na kuteketeza nyumba zetu!" 

Wanakijiji wakawa na hofu sana. Wakawa wamechanganyikiwa kama kundi la mchwa lililokanyagwa na ng'ombe. Hawakujua pa kujificha wala la kufanya. 

Wangewaficha ng'ombe wao wapi? Wangezificha nafaka zao wapi? 

Wangejificha wapi wao wenyewe? 

Hami aliogopa sana.

Akakumbuka mahali ambapo yeye na Angula walikuwa wakienda kucheza wakati mwingine. 

Mahali salama. 

Mahali pa siri.

"Ninapajua mahali ambapo sote tunaweza kujificha!" Lakini wanakijiji hawakumsikiliza. Walikuwa wakipiga kelele sana. 

Sasa angefanyaje ili wamsikilize? Unadhani Hami alifanya nini? 

Alichukua ngoma na kuipiga kwa nguvu kabisa. Bam! Bam! Bam! Boom! Boom! Boom! 

Wanakijiji wote walitulia. Hami akawaambia kwa sauti, "Ninajua mahali ambako tunaweza kujificha. Nifuateni."

Hami alimshika Angula mkono akasema, "Njoo tawapeleke wanakijiji kwenye mti wetu. Sote tutakuwa salama huko." 

Angula alitikisa kichwa. "Hapana, Hami. Mahali hapo ni siri yetu. Ulisema tusimwambie mtu yeyote." 

"Ndiyo", Hami akasema. "Ilikuwa siri yetu. Lakini sasa sote tuko hatarini."

Hami na Angula waliwaongoza wanakijiji. "Kwa nini unatuleta hapa? Hatuwezi kujificha hapa," walisema. 

Hami akamwita babake, "Nitakuonyesha." Hami na babake waliingia wakashuka ndani kupitia shimo dogo. Pale chini kulikuwa na uwazi mkubwa. "Lakini watu wote hawawezi kuingilia kwenye shimo dogo pale juu," babake alisema. 

"Hapana," Hami alisema. "Tutaleta shoka tutengenze mlango wa kuingilia hapa kwenye shina." 

Walitengeneza kiingilio shinani. Wanakijiji wakaleta vyakula na vyombo vya kupikia. Wote wakaingia ndani ya uwazi mkubwa wa mbuyu. La kushangaza ni kwamba kulikuwa na nafasi ya kuwatosha wote.

Wakati jua lilipotua na giza kutanda, kijiji kizima kilitulia tuli! Ulikuwa usiku wenye baridi. 

Wale wahalifu walitembea taratibu kuelekea kijijini. 
"Lazima wanakijiji wawe wamelala sasa," waliambiana. 

Nao wanakijiji walijificha ndani ya mti. Nini kingetokea? Walihisi baridi na woga. 

Hami akasema, "Kuna baridi sana. Tuwashe moto." Akachukua mawe mawili akayachua, moja juu ya jingine haraka haraka.

Baada ya muda mfupi, cheche za moto zikashika nyasi. 

Kisha moto mkubwa ukawaka wakaanza kuota.

Nje, wavamizi walizidi kukaribia. Ghafla, mmoja wao alipiga mayowe akionyesha mbuyu walimojificha. Ndimi za moto zilitoka mle. Macho makali yaliangaza kutoka mle. Moshi ulipaa angani. 

"Ni jinamizi kubwa!" Walilia kwa woga. Kwanza mvamizi mmoja aligeuka na kukimbia. Kisha mwengine, na mwengine. Hadi wote wakaenda zao. 

Watu wa kijiji cha Balantu wakaokolewa.

Bibi akanyamaza. Wakati huu wote Sela alikuwa anashikilia shina la mbuyu. 

"Kwa hivyo, ni mti huo uliowaokoa wanakijiji." Bibi akamaliza kuwahadithia.

------------------------------------------------------------



Musa anaishi na wazazi wake katika kijiji cha Mafunzo. 

Yeye ni mvulana mwerevu, lakini ni kaidi.

Musa pia ni mchokozi. Yeye huwapiga wenzake.

Pia huwapiga wanyama anapowakuta.

Siku moja anapokuwa akitoka shuleni, anamwona paka.

Anambeba paka yule na kwenda naye nyumbani.

Babake anapomwona, anamwambia, "Musa, acha kumnyanyasa paka huyo! Mrudishe mahali ulikompata."

Musa anakataa kumrudisha paka alikomuokota. Badala yake, anamfungia katika ngome.

Musa anapolala usiku huo, anaota ndoto.

Anamwona paka akiwa mkubwa kwa umbo huku akikimbia kuelekea mahali aliko. Kinywa chake ki wazi na meno ni makali. Paka anataka kumla Musa.

Paka anaanza kumeza miguu ya Musa. Anaikula hadi kwenye magoti.

Kisha Musa anaamka.

Siku inayofuata, Musa anamrejesha paka mahali alikomuokota.

Tangu wakati huo, Musa anaahidi kuwa mvulana mzuri.

------------------------------------------------------------



Kuna mvulana anayeitwa Rodney. Anaishi na familia yake. 

Mamake ni Jemima na babake ni Mike. Dada zake ni Suzy na Lola.

Rodney ni kitinda mimba.

Rodney anapenda kucheza mchezo wa chesi.

Anaupenda sana hata anapokuwa akicheza, haongei.

Siku moja, Rodney alikuwa shuleni akicheza chesi. 

Aligundua kwamba mchezo wa chesi ungelinganishwa na familia yake.

Mike ni Mfalme. Jemima ni Malkia, ndiyo sababu ana nguvu.

Suzy na Lola ni majamadari na maaskofu.

Rodney ni kitunda kwa sababu ni mdogo kwa wote.

Baada ya kugundua hivyo, Rodney alikwenda nyumbani mbio kuwaelezea familia yake.

Mwanzoni, wote walimcheka. Lakini, baadaye walielewa.

Rodney aliwaelezea majukumu yao na kwa nini yeye alikuwa kitunda.

Rodney alimwambia mamake kuwa yeye ni malkia, na kwamba babake ni mfalme.

Dada zake ni majamadari na maaskofu.

Rodney ni kitunda kwa sababu anapenda kutalii!

Angechagua kuwa chochote alichotaka, hata kama angejinyima vitu fulani.

------------------------------------------------------------



Mimi na rafiki yangu Kiki hupenda kuchunguza na kuvumbua mambo. Hii ndiyo sababu tunayafahamu mazingira yetu vyema. 

Siku moja tulipokuwa tukienda nyumbani kutoka shule, tulikubaliana twende mahali tukafanye uchunguzi.

Tulipitia karibu na reli ingawa babake Kiki alikuwa ametuonya dhidi ya kufanya hivyo. 

Baadaye, tulimwona mwanamume aliyekuwa amevaa koti refu jeusi. Alikuwa akitufuata polepole.

Tuliamua kutembea polepole ili tumtazame kwa karibu. Alikuwa mtu wa kuogofya. 

Ngozi yake ilijaa vipele. Midomo yake ilikuwa midogo na haikuyafunika meno yake ya rangi ya kahawia. Alikuwa na kovu moja kubwa lililofunika nusu ya uso wake.

Moyo wangu ulidunda kwa sauti nikadhani mhuni huyo angeweza kuusikia. Nilimkodolea macho. 

Hakupendezwa na jinsi nilivyomtazama akanikemea kwa ukali, "Wewe mvulana, unaangalia nini?"

Kwa woga, tuligeuka na kutimua mbio, lakini mimi sikuweza kukimbia kwa kasi. 

Mhuni huyo akalishika shati langu na kunivuta kwa nguvu. 

Rafiki yangu Kiki alifanikiwa kutoroka.

Mhuni huyo alininyanyua juu kama karatasi na kunirusha ndani ya gari moja jeupe lililokuwa limeegeshwa hapo uwanjani. Yeye alipanda na kukaa kiti cha mbele. 

Mwenzake aliyekuwa ndani ya gari, aliniziba macho na kuibana mikono yangu nyuma. Kisha dereva akaliendesha gari hilo kwa kasi ya ambulansi.

Yule jambazi wa pili aliyekuwa ameketi karibu nami,  aliniwekea kitambaa chenye unyevunyevu usoni mwangu. Nilipounusa unyevunyevu huo, nililala. 

Baadaye nilipoamka, nilijipata nimeketi sakafuni katika chumba kimoja chenye giza totoro. Kilijaa buibui na panya.

Mara mlango wa chumba ukafunguka. Yule mhuni aliyenifunga kitambaa usoni, akaingia akiwa amebeba sahani. 

"Kula chakula hiki upesi kwa sababu utakwenda safari ndefu," aliniambia.

Nilipolisikia neno 'safari' niliamua kula ili nipate nguvu za kujiokoa. Mhuni yule aliifungua kamba niliyofungwa nayo. 

Nilipokuwa nikila, aliketi pembeni na kuvuta sigara. Moshi ulijaa chumbani mwote.

Mlango ulibishwa, mhuni huyo na dereva wakaingia wakiwa wamembeba mvulana. 

Kiki pia alikuwa ameshikwa! Lo! Tulikuwa tumenaswa katika chumba chenye giza.

Baadaye, tulifahamu kuwa yule mhuni mrefu mwenye sura mbaya ndiye alikuwa kiongozi wa genge lile. Mhuni aliyenipa chakula hakufurahia walivyofanya. 

Tuliwasikia wakibishana pale nje ya chumba. Kiongozi akasema kwa sauti, "Sijali kama unaijua familia yake. Huwezi kubadili nia yako sasa."

Kutokana na ubishi huo, tulijua kwamba mmoja wao alitufahamu ingawa sikujua ni yupi. Kiki akasema,  "Lazima tupate njia ya kutoroka. Wazazi wetu hawana pesa za kutukomboa." 

Wahuni hao waliendelea kubishana hadi wakaanza kupigana. Mimi nilimfungua Kiki upesi, tukaufunga mlango na kuanza kutafuta njia ya kutoroka.

Tuliona dirisha lenye mianya myembamba iliyopitisha mwangaza. 

Tulizivuta mbao za dirisha hadi misumari iliyoziunganisha ikang'oka. 

Kisha tukaziondoa pakawa na mwanya mkubwa.

Kiki alikuwa mdogo na mwepesi kuniliko mimi. Tukaamua achapuke kwenda kutafuta usaidizi. 

Nikamsaidia kupita kwenye kile kidirisha na akaruka chini. Nilikuwa tayari kujaribu kutoka pia, nilipowasikia wahuni wale wakiingia chumbani.

Wahuni hao walikuwa wamesikia kishindo cha Kiki. Waliugonga mlango na kuufungua. Walikiangalia kile kidirisha kisha wakaanza kusukumana na kutoka nje. 

Walikasirika sana, hasa yule mkubwa wao mwenye sura mbaya, walipokosa kujua Kiki alikimbilia upande gani. 

Alinipiga na kusema, "Wazazi wako watalipa kwa ajili ya kitendo hiki."

Wahuni walizipigilia zile mbao na  kukiziba kile kidirisha wakanifungia. Niliwasikia wakibishana tena. 

Aliyevuta sigara alitaka niachiliwe. Dereva alihofia kuwa Kiki angekumbuka njia na kuwaleta polisi. Kiongozi naye alitaka tu kupata pesa.

Mara niliisikia sauti ya mtu mzima akisema, "Usiogope. Polisi wameshafika. Lala sakafuni ujifunike kichwa na wala usisonge."

Nilisikia kelele na milio ya risasi. Sikufahamu kilichokuwa kikiendelea kwani mambo mengi yalitendeka kwa wakati mmoja! 

Polisi waliingia chumbani na kuwakamata wahuni wale mara moja.

Polisi wa kike aliufungua mlango, akaingia chumbani na kunifunika kwa blanketi. 

Aliniambia, "Rafiki yako alikuwa na bahati kwa sababu alitupata tukishika doria. Mara moja, tuliitisha usaidizi na tukaja kuwatia adabu hawa majambazi!"

Wahuni hao walitiwa pingu na kusukumwa ndani ya gari la polisi. 

Mimi nilingia kwenye gari moja na yule polisi wa kike. Alinipeleka kwa wazazi wangu waliokuwa na wasiwasi. 

Tangu siku hiyo, mimi na Kiki tumekuwa waangalifu zaidi.

------------------------------------------------------------



Betina alikuwa amelalia mkeka wake. Alimsikiliza mamake akimsimulia hadithi aliyoipenda zaidi. 

Hadithi iliwahusu wanawake waliojulikana mle kijijini kwa mikeka na vikapu maridadi waliyotengeneza. 

Betina aliithamini zawadi ya mkeka aliyopewa na bibi alipohitimu umri wa miaka kumi.

Betina aliposimama, mamake alitaka kuuweka makeka wake. Betina alisema, "Mama, usiukunje sasa. Hebu kwanza tutazame rangi na maumbo yaliyoko." 

Betina alizitaja rangi kwenye safu zote kutoka juu hadi chini, "Waridi, waridi, kijani, kijani, bluu, bluu, waridi, waridi, kijani, kijani." Ni sehemu gani ya mkeka ambapo muundo unabadilika?

Betina aliukunjua mkeka. Maumbo mengi yalikuwa mistatili na mengine miraba. Alisema, "Ninajua njia rahisi ya kupata jumla ya maumbo yote. Si lazima kuhesabu kila umbo, bali unahesabu idadi ya maumbo yaliyo kwenye kila mstari."

Je, unajua namna Betina anayahesabu maumbo hayo? Kuna jumla ya maumbo mangapi?

Betina alikuwa na mkeka mwingine mdogo alioutumia kuketi nje. Huo ulikuwa na mistatili pekee. Betina anaweza kuwa ameifunika kwa mwili wake takriban mistatili mingapi? Takriban mistatili mingapi ambayo haijfafunikwa? 

Unaweza kutumia njia ya Betina ya haraka kupata mistatili mingapi ambayo mkeka huo unayo?

Asubuhi moja, Betina alienda kumtembelea bibi. Aliwakuta wanawake kisimani wakiwa wamebeba maji vichwani. 

Alishangaa akataka kujua ni maji lita ngapi yaliyokuwa katika kila ndoo. Je, unafikiriaje?

Betina alipowasili, bibi alimkaribisha, "Betina, furaha ilioje! Hiki ni kikapu kipya nilichotengeneza. Unakipenda?" Betina alimjibu, "Ninapenda rangi yake, lakini sipendi maumbo yaliyoko." 

Utawezaje kuchora maumbo yaliyoko kwenye kikapu hicho? Maumbo hayo yanafanana mraba au mstatili au umbo jingine tofauti?

Alipokuwa akirudi nyumbani, Betina aliikosa njia. Hakujua alikokuwa kwa hivyo, aliketi chini ya mti kupumzika. 

Aliyatazama majani yakicheza juu yake kwenye matawi. Aliyaona maumbo tofauti yaliyosababishwa na mwangaza yakicheza kila mahali. Baadaye, alipatwa na usingizi mnono.

Betina alipoamka, aliogopa. Alitaka kuwa nyumbani na mamake akipumzika kwenye makeka wake. 

Wakati huo huo, ndege mdogo wa rangi ya bluu alitua mtini. "Hujambo. Usiwe na wasiwasi, nitakusaidia ufike nyumbani. Nifuate," yule ndege alisema. 

Betina alishangaa kumsikia ndege akiongea.

Betina alimfuata yule ndege hadi kwenye njia panda. Njia iligawika, moja ikienda kushoto na nyingine kulia. Je, aifuate njia gani? 

Betina alitazama juu. Iliwezekana kuwa yule ndege alikuwa amebeba mdomoni kipande cha mkeka wake! Ndege yule alikiangusha kile kipande kwenye njia iliyokwenda upande wa kulia, kisha akaenda zake.

Betina aliifuata njia hiyo akapanda mlima na kushuka. Aliwasikia watu wakicheka na kuimba kijijini kwao.

Betina alifurahi alipofika nyumbani salama.

Mamake aliukunjua mkeka kisha akampa chakula. Betina aliyahesabu maumbo ya miraba yaliyokuwa kwenye mkeka kuhakikisha kwamba yalikuwa bado yako. 

Alikuwa na uhakika kwamba alikiona kipande cha mkeka kilichokuwa kimekatwa. Alijua hakuwa akiota. Ilikuwa kweli kuwa yule ndege mdogo alikuwa amemwokoa!

------------------------------------------------------------



tofaa moja

matofaa mawili

ndizi moja

ndizi mbili

ndizi tatu

nanasi moja

mananasi mawili

tikiti maji moja

matikiti maji mawili

papai moja

mapapai mawili

embe moja

maembe mawili

parachichi moja

maparachichi mawili

chungwa moja

machungwa mawili

pera moja

mapera mawili

pasheni moja

pasheni mbili

limau moja

malimau mawili

stroberi moja

stroberi mbili

chenza moja

machenza mawili

cheri moja

cheri mbili

cheri tatu

zabibu moja

zabibu mbili

zabibu nyingi!

Je, ni matunda mangapi unayoona!

------------------------------------------------------------



Hebu nikueleze hadithi kunihusu. 

Ninaanza kama cheche ndogo.

Ninaenea kila mahali upepo unaponibeba.

Sisi ni marafiki wazuri.

Ninapika chakula chako.

Ninakupa mwangaza usiku.

Nina maarifa mengi.

Mimi ni mmoja wa familia yako.

Kuwa mwangalifu unaponialika nyumbani kwako. 

Sipendi kuachwa peke yangu.

------------------------------------------------------------



Kitabu hiki kimeandikwa na wanafunzi wa darasa la 5 wa Shule ya Msingi ya Mwasi Kaskazini.

Hawa waandishi na wachoraji wana ujuzi tofauti wa kipekee. Ujuzi huu una umuhimu wake katika jamii.

Naitwa Honesta Simoni Njau. Nina elimu ya upishi. Ninaweza kuandaa viungo, kuweka mafuta na chumvi kwa kiasi kwenye vyakula.

Ningependa kuwa na hoteli na kupika vyakula vitakavyohitajika na wateja.

Mimi ni Eliya. Nina elimu ya kutengeneza umeme. Mwalimu wangu ni babangu. Napenda kumwangalia anapotengeneza vitu kama spika na sola.

Elimu hii ni muhimu kwa sababu itaifanya Tanzania ing'are kwa mwanga wa umeme. Umeme hutusaidia kusoma usiku.

Ninaitwa Aleni Jakobo Njau. Nina elimu ya kucheza ngoma. Pia, ninaweza kutibu mifugo kwa kuwapa dawa, kuwadunga sindano na kuwapa chakula cha kutosha. Nilifundishwa na mamangu.

Ndoto yangu ni kuwa mchezaji ngoma maarufu, na kuwa mwanajeshi.

Ninaitwa Mery Emanueli Kessy. Nina elimu ya kupika. Ninaweza kupika chai, maharagwe, ndizi kwa mchuzi wa nyanya, na kukaanga mboga. Nimefundishwa na bibi yangu.

Ndoto yangu ni kuwa sista wa kumtumikia Mungu.

Naitwa Shedraki A. Luondo. Nina elimu ya kucheza muziki. Nilifundishwa na wazazi. Waliniambia nijiunge na wenzangu ili nicheze muziki.

Nilivyojiunga nao nikajua kucheza kama wenzangu. Ninatumaini nikiwa mkubwa nitakuwa dereva au rubani.

Ninaitwa Anicia Evance Lyimo. Nina elimu ya kulima. Wazazi wangu walinifundisha tukiwa shambani.

Baada ya kuona ninalima vizuri, Mama alinipa bustani ya mboga na mbegu za kupanda.

Kilimo huleta chakula, utajiri na ajira.

Ninaitwa Julius Trifon Njau. Nina elimu ya dini. Baba na mama wananifundisha elimu hii wanaposali na kwenda misa.

Nataka niwe padre nitembelee nchi mbalimbali kuhubiri injili. Elimu hii itasaidia watu wamjue Mungu.

Ninaitwa Bernadetha Alex Njau. Nina elimu ya ufugaji. Walionifundisha ni baba na mama. Elimu hii ina faida kwani inatupatia kipato na nyama.

Nikiwa mkubwa, nitafuga wanyama bila kumpoteza hata mmoja. Baadaye, nitapata mapato makubwa.

Ninaitwa Evagri J. Njau. Mimi nina elimu ya kucheza mpira wa miguu.

Mjomba wangu ndiye aliyenifundisha kucheza. Aliniambia, "Ili uwe mchezaji bora, ni lazima kuimarisha viungo vya mwili."

Ndoto yangu ni kuchezea timu ya Simba.

Ninaitwa Honorina Richadi Thomass Temba. Nina elimu ya kupika. Nilifundishwa na bibi. Elimu hii ni muhimu kwa sababu kunapokuwa na wageni ninaweza kuwapikia.

Nitakapokuwa mkubwa, nitapikia jamii inayonizunguka, kwa mfano, ikitokea sherehe kama harusi.

Naitwa Denisi Peteri Temba. Mimi ninapenda lugha yangu ya Kichaga.

Nina elimu ya kuchora picha na kucheza muziki. Aliyenifundisha ni baba. 

Nitaboresha hivi vipaji ili vilete mapato makubwa kwangu, kwa familia na jamii.

Ninaitwa Julyclara Paul Temba. Nina elimu ya kukaanga samaki, chipsi, maandazi, ndizi, mihogo, nyama na kuku.

Elimu hii inawasaidia watu kuwa na afya njema, na pia, kuunganisha watu wengi. Nitaendeleza elimu hii hadi nifanye kazi kwenye hoteli kubwa.

Naitwa Benson Inocenti Mtui. Nina elimu ya kukamua maziwa.

Tuna ng'ombe wengi, na watu wanapenda sana maziwa yetu. Tunauza maziwa ili tupate fedha. 

Nilifundishwa na bibi yangu kukamua. Aliniambia, "Ukifanya kazi kwa bidii, Mungu atakusaidia maishani."

Ninaitwa Alice Frank Njau. Nina elimu ya kulima. Nilifundishwa na babu na bibi. Nimejifunza kulima sehemu yenye rutuba na isiyo na majani, na kupalilia.

Nitakapokuwa mkubwa, nataka kuwa daktari bora wa mifugo na kilimo kutoka Tanzania.

Naitwa Epifania J. Mallya. Nina elimu ya kufuga kuku. Najua chakula wanachohitaji kuku, kiasi cha kuwapa na wakati wa kuwapa chakula.

Nataka kuwa mfugaji mashuhuri ili niweze kupata kipato kikubwa. Nitafuga kuku, mbuzi na ng'ombe.

Ninaitwa Eugenia Emanueli Semwali. Nina elimu ya kuimba.

Ninapenda kuimba nyimbo za Kichaga, Kiswahili, na Kiingereza.

Nyimbo hizi huwafurahisha watu.

Ninaitwa Leah C. Motta. Elimu yangu ni ya kulima. Kilimo kinaleta ajira na kuinua pato la taifa.

Baadhi ya shughuli za kilimo ni kuandaa shamba, kutoa magugu, kulima, kuandaa matuta, na kutengeneza vitalu.

Nitakapokuwa mkubwa, nitakuwa daktari.

Naitwa Catherini Alferio Njau. Nina uwezo wa kupika na kulima. Mama amenifundisha kupika. Baba alinifundisha kuotesha mboga na maua.

Kilimo hutupatia mazao, ajira na kuboresha chakula.

Ningependa kuwa mjasiriamali maarufu.

Ninaitwa Wilhelmi. Ninapenda sana ufugaji na mambo ya dini. Ndio maana ninapenda kuwa padri. 

Elimu yangu nimepata kanisani na darasani. Katika maisha yangu, napenda kumcha Mungu na kueneza neno lake.

Naitwa Julitha Juliani Temba. Nina elimu ya kupika. Walionifundisha ni mama, dada, na bibi.

Ninaweza kupika ndizi, maandazi, chapati, ugali, nyama, maharagwe na wali.

Ningependa nipike hotelini na kuwafundisha wanajamii wengine upishi bora.

Naitwa Anicia Wiliamu Kaguo. Nina elimu ya kuuza vitu kibandani. Ninauza bidhaa kama nyanya, maandazi, chapati, mkate na samaki.

Nitakuja kuwa mfanyabiashara na kumiliki duka langu.

Ninaishi na bibi na babu. Bibi pia ni mfanyabiashara.

Jina langu ni Junior Alfredi Mmbo. Nina elimu ya kucheza mpira wa miguu.

Ndoto yangu ni kuwa askari au mchezaji hodari wa mpira wa miguu.

Ninaitwa Mariam Sadiki Joshua. Nina elimu ya kupika. Nilifundishwa elimu yangu na bibi. Napika vyakula kama uji, chai, wali, ugali na ndizi.

Tunapika ili tule tupate nguvu na kufanya kazi kwa bidii.

Vyakula vinatoka shambani. Tunaelimishwa kulima pia.

Jina langu ni Johnson Salum Abdul. Kipaji changu ni kucheza mpira.

Nilijifunza kucheza na wenzangu Julius, Aleni, Shedraki na Epifani uwanjani Kishimundu siku za Jumamosi.

Elimu huleta maendeleo.

Ninaitwa Maurini Francis Temba. Nina vipawa viwili, kuimba na kupika. Nilifundishwa na bibi kupika. 

Tulipofunga shule tulienda Sanya kwa bibi. Alitufundisha kupika, kuotesha maua, kufagia, na kulisha kuku.

Ninaitwa Nora Aloice Temu. Kipawa changu ni kupika kama vile ugali, makande, wali, na mboga.

Pia nina elimu ya kuuza dukani bidhaa kama vile soda, mchele na maharagwe. Ninawavutia wateja wengi.

Ninaitwa Epifani Muga Kabila. Nina elimu ya kucheza mpira. Tangu nikiwa mdogo, nilifundishwa kucheza mpira na mjomba na kaka. Tulikuwa tunacheza mpira na jirani.

Nitaendeleza kipaji changu cha kucheza mpira. Nikiwa mkubwa ninataka kuwa rubani.

------------------------------------------------------------



Kwa nini mtoto analia?

Labda ana njaa.

Kwa nini mvulana huyu amehuzunika?

Labda anamkosa baba yake.

Kwa nini msichana huyu amefurahi?

Kwa sababu amepata rinda jipya.

Kwa nini mzee huyo anacheka?

Kwa sababu amesoma kichekesho.

Kwa nini mama huyu anatabasamu?

Kwa sababu watoto wake wanasoma kimya kimya.

Mbona mwanamke huyu anatazama chini?

Labda anaona haya.

------------------------------------------------------------



Hakuna mvua.

Jua linang'aa.

Kuna upepo.

Kuna mawingu mazito.

Ni baridi.

Mvua inanyesha.

Kuna ngurumo za radi.

Naona upinde.

------------------------------------------------------------


Hapo zamani za kale, palikuwa na mzee mmoja aliyeitwa Kigo. 

Alikuwa na mifugo kama mbuzi, ng'ombe, na sungura.

Siku moja, simba aliingia katika kijiji hicho. 

Aliingia katika kibanda cha Mzee Kigo na kukuta mifugo ya mzee huyo.

Simba akawala ng'ombe na mbuzi, lakini sungura hakuwaona kwenye kibanda chao. 

Kisha Simba aliondoka na kwenda zake.

Mzee Kigo alipofika, alikuta damu ya ng'ombe na mbuzi.

------------------------------------------------------------

